MBINGU MPYA NA NCHI MPYA. (Sehemu ya 1)

MBINGU MPYA NA NCHI MPYA. (Sehemu ya 1)

Nakusalimu katika jina kuu sana lipitalo majina yote la Bwana wetu Yesu Kristo, Nakukaribisha katika kujifunza maneno ya uzima.  Na leo tutajifunza juu ya mbingu mpya na nchi mpya.

Hili ni moja ya maswali yanayoulizwa na watu wengi, Je! Hiyo mbingu mpya na Nchi mpya inayozungumziwa katika maandiko itakuwa wapi? Je ni mbinguni au duniani?. Na Je! Itakuwa ni hii hii dunia yetu au italetwa dunia nyingine na Mungu?. Ili kufahamu fuatana nami mpaka mwisho wa makala hizi.

Historia ya mbingu na nchi:

Sasa kabla hatujaenda kutazama juu ya mbingu mpya na nchi mpya, ni vizuri tukafahamu historia ya “mbingu na nchi” ilianzia wapi. Tukisoma kile kitabu cha Mwanzo, biblia inasema

Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi ..(Mwanzo 1:1)

Inaposema “mbingu” inamaanisha anga lote, yaani sayari, na nyota na magimba yote yanayoonekana juu. Na “Nchi” inamaanisha hii dunia yetu tunayoishi sisi wanadamu na viumbe vyote.

Sasa Mungu alipoiumba, ilikuwa ni kamilifu sana, yenye kupendeza, lakini baada ya muda Fulani kupita,ambao biblia haijaeleza ni kipindi cha muda gani, ilikuja kuharibiwa na kuwa UKIWA.  Ikiwa na maana hakukuwa na kiumbe chochote kinachoishi, au uhai wowote unaoendelea, ikabakia kuwa kama mojawapo ya sayari nyingine, isipokuwa tu, hii yetu ilisalia na maji.

Mwanzo 1:2 “Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji”.

Najua pengine unaweza ukawa na swali, Je! Umejuaje, kuwa dunia yetu, hapo mwanzo ilikuwa ni nzuri na kamilifu kabla ya Mungu kuanza kutuumba sisi. Jibu ni kuwa maandiko yanatuambia Mungu hajawahi kuiumba nchi na kuiacha katika hali ya ukiwa. Soma.

Isaya 45:18 “Maana Bwana, aliyeziumba mbingu, asema hivi; Yeye ni Mungu; ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya; ndiye aliyeifanya imara; HAKUIUMBA UKIWA, aliiumba ili ikaliwe na watu; Mimi ni Bwana, wala hapana mwingine”.

Unaona hapo? Anasema, hakuiumba ukiwa, ikiwa na maana kuwa Mungu haachi kazi nusu nusu anaumba kikamilifu. Hivyo hiyo inatuonyesha kuwa kabla ya sisi wanadamu kuumbwa, Mungu alikuwa tayari kashaiumba dunia kamilifu na yenye uhai ndani yake, Lakini kukatokea jambo Fulani la uharibifu, ikapelekea Mungu kuiharibu dunia ile, Na hatuwezi kushangaa jambo kama hilo kusababishwa na shetani, na mapepo yake, kwasababu hao ndio waliokuwepo kabla ya sisi wanadamu kuumbwa. Lakini siri hiyo Mungu kaificha ni yeye mwenyewe ndiye anayejua yaliyokuwa yanaendelea huko nyuma.

Sasa wakati ulipofika wa sisi kuumbwa Mungu akaanza kuikarabati dunia tena. ndipo hapo  tunaona akasema na iwe mwanga ikawa mwanga, n.k. Mpaka ikiwa sehemu nzuri sana tena ya kutuvutia, lakini tunajua maisha yalipokuja kuendelea mbele Adamu akaasi, dhambi ikaingia, baadaye hali ikaendelea kuwa mbaya kupitiliza, hadi Mungu akaghahiri kuwaumba wanadamu, baadaye akasema nitawaangamiza wanadamu wote, watoke katika uso wa nchi.

Ndipo hapo akaleta kitu kinachoitwa gharika duniani, akaigharikisha dunia nzima. Akasalia Nuhu tu, na familia yake, jumla watu 8, dunia ikabakia ukiwa kama ilivyokuwa pale mwanzo.

Isaya 24:1 “Tazama, Bwana ameifanya dunia kuwa tupu, aifanya ukiwa, aipindua, na kuwatawanya wakaao ndani yake”.

Hivyo, dunia ya wakati ule ilipogharikishwa, haikukarabatiwa tena na Mungu kama alivyofanya pale mwanzo, badala yake aliyakausha maji tu, lakini uzuri mwingi wa mbingu na nchi ulipotea, jua likawa kali kuliko pale mwanzo, kwasababu maji yaliyokuwa juu ya anga yalipunguzwa, umri wa watu kuishi ukapungua sana, kutoka miaka elfu hadi miaka 120, Kama Mungu alivyosema.

Basi, baada ya hapo maisha yakaendelea tena kama kawaida, watu wakaongezeka , wakaijaza dunia, maasi yakarudi na kuongeza, tena hata zaidi ya kipindi kile cha Nuhu, Mungu akaanza kuwaonya wanadamu kwa vinywa vya manabii wake, akawaambia huu ulimwengu utakwenda kuangamizwa , kama ilivyokuwa kipindi kile cha gharika, lakini kuangamziwa kwake hakutakuwa kwa maji tena, bali kwa moto, ili kuifanya kuwa UKIWA tena.

Unaweza kusoma hilo katika vifungu hivyo katika mistari hii;

Isaya 13:9 “Tazama, siku ya Bwana inakuja, siku kali, ya hasira na ghadhabu kuu, ILI IIFANYE NCHI KUWA UKIWA, na kuwaharibu watu wake, wenye dhambi, wasikae ndani yake.

10 Maana nyota za mbinguni na matangamano havitatoa nuru yake; jua litatiwa giza wakati wa kucha kwake, na mwezi utaacha nuru yake isiangaze.

11 Nami nitaadhibu ulimwengu kwa sababu ya ubaya wake, na wenye dhambi kwa sababu ya hatia yao; nami nitaikomesha fahari yao wenye kiburi; nami nitayaangusha chini majivuno yao walio wakali;

12 nitafanya wanadamu kuadimika kuliko dhahabu safi, na watu kuliko dhahabu ya Ofiri.

13 Kwa hiyo nitazitetemesha mbingu, na dunia itatikiswa itoke katika mahali pake, kwa sababu ya ghadhabu ya Bwana wa majeshi, na kwa sababu ya siku ya hasira yake kali”.

Soma pia,

2Petro 3:6 “kwa hayo dunia ile ya wakati ule iligharikishwa na maji, ikaangamia.

7 Lakini MBINGU ZA SASA NA NCHI zimewekwa akiba kwa moto, kwa neno lilo hilo, zikilindwa hata siku ya hukumu, na ya kuangamia kwao wanadamu wasiomcha Mungu”.

Unaona? Zoezi lile lile la Mungu kuiharibu nchi, linaendelea, lilianza kabla ya sisi kuumbwa, likatokea tena wakati wa Nuhu, na litamalizia, na wakati wetu sisi tunaoishi. Kwahiyo kinachongojewa sasa ni Mungu kuwanyakua tu watakatifu wake, baada ya hapo, kitakachofuata ni uharibifu mkubwa sana wa huu ulimwengu.Ambao utakuwa ni wa kutisha sana, kwasababu, dunia itatikiswa kwa namna ambayo haijawahi kutokea, jua litatiwa giza, visiwa vitahama, waovu wote watakufa, watakaosalia watakawa ni wachache sana pengine watu 10 tu, katika dunia nzima, kwasababu moto usiokuwa wa kawaida utaipika hii dunia tena, ili kuifanya kuwa ukiwa kama pale mwanzo.

Ufunuo 16:17 “Na huyo wa saba akakimimina kitasa chake juu ya anga. Sauti kuu ikatoka katika hekalu, katika kile kiti cha enzi, ikisema, Imekwisha kuwa.

18 Pakawa na umeme na sauti na radi; na palikuwa na tetemeko la nchi kubwa, ambalo tangu wanadamu kuwako juu ya nchi hapakuwa namna ile, jinsi lilivyokuwa kubwa tetemeko hilo. Hii ndio siku ya kiama inayofamika na wengi.

19 Na mji ule mkuu ukagawanyikana mafungu matatu, na miji ya mataifa ikaanguka; na Babeli ule mkuu ukakumbukwa mbele za Mungu, kupewa kikombe cha mvinyo ya ghadhabu ya hasira yake.

20 Kila kisiwa kikakimbia, wala milima haikuonekana tena.

21 Na mvua ya mawe kubwa sana, ya mawe mazito kama talanta, ikashuka kutoka mbinguni juu ya wanadamu. Wanadamu wakamtukana Mungu kwa sababu ya lile pigo la mvua ya mawe; kwa maana pigo lake ni kubwa mno”.

Huu wakati unatisha sana, hatuwezi kueleza mambo yote, lakini kama utataka somo linalohusiana na hii siku ya Bwana itakavyokuwa basi bofya link hii>>>> https://wingulamashahidi.org/2018/07/17/siku-ya-bwana-inayotisha-yaja/

Msingi huu utatusaidia kufahamu agenda ya Mungu juu ya hii dunia yetu, na mpaka mwisho wake utakavyokuja kuwa.

Mpaka hapo tunaweza kuendelea  katika sehemu ya pili ya mbingu mpya na nchi mpya.. Hivyo kwa mwendelezo unaweza kubofya chini>>

MBINGU MPYA NA NCHI MPYA. (Sehemu ya 2)

MBINGU MPYA NA NCHI MPYA. (Sehemu ya 3)

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

MAPIGO YA VITASA SABA, NA SIKU YA BWANA.

KRISIMASI (CHRISTMAS) NI NINI? JE IPO KATIKA BIBLIA?

Je! tunapaswa kukiamini Kitabu cha Henoko?

UFUNUO: Mlango wa 18

Rudi nyumbani

Print this post

WEKA KUMBUKUMBU YA MAMBO BWANA ANAYOKUFANYIA KWASABABU YATAKUFAA MBELENI.

Jina la Bwana wetu Yesu, libarikiwe.

Kuna umuhimu mkubwa sana wa kuweka kumbukumbu za mambo Bwana anayoyafanya katika maisha yako, kwasababu aidha zitakusaidia wewe mbeleni au zitawasaidia wengine. Kila tendo la kimiujiza Bwana analokufanyia liandike chini. Kwasababu zitakuja nyakati ambazo utaishiwa nguvu, na kama utakuwa huna kumbukumbu yoyote kichwani kwako itakuwa ni ngumu kushinda majaribu hayo..

Nguvu ya Daudi kumshinda Goliathi, si upako aliokuwa nao, wala si maono aliyoona wala ndoto aliyoota, bali ni uwezo wa kukumbuka mambo Mungu aliyomtendea wakati alipokutana na simba na dubu, walipokuwa wanavizia kondoo, Bwana alivyomsaidia akawaua, na alipoliweka hilo moyoni, ulipokuja wakati wa jaribu kubwa kama hilo la Goliathi, aliweza kukumbuka jinsi Bwana alivyomsaidia kuwaua wale hayawani wakali, na akamchukulia Goliathi kuwa naye pia atamwua kama alivyowaua wale wanyama.

1 Samweli 17:32 “Daudi akamwambia Sauli, Asizimie moyo mtu ye yote kwa ajili ya huyu; mimi mtumishi wako nitakwenda kupigana na Mfilisti huyu.

33 Sauli akamwambia Daudi, Huwezi wewe kumwendea Mfilisti huyu upigane naye; maana wewe u kijana tu; na huyu ni mtu wa vita tangu ujana wake.

34 Daudi akamwambia Sauli, Mtumishi wako alikuwa akichunga kondoo za baba yake, na alipokuwa akija simba, au dubu, akamkamata mwana-kondoo wa lile kundi,

35 mimi hutoka nikamfuata, nikampiga, nikampokonya kinywani mwake; na akinirukia, humshika ndevu zake, nikampiga, nikamwua.

36 Mtumishi wako alimwua simba na dubu pia; na huyu Mfilisti asiyetahiriwa atakuwa kama mmoja wao, kwa sababu amewatukana majeshi ya Mungu aliye hai.

37 Daudi akasema, Bwana aliyeniokoa na makucha ya simba, na makucha ya dubu, ataniokoa na mkono wa Mfilisti huyu. Sauli akamwambia Daudi, Enenda, na Bwana atakuwa pamoja nawe”

Umeona hapo?..Daudi alitumia tu USHUHUDA wa Dubu na Simba, kumwangusha Goliathi. Lakini hebu fikiri angekuwa ni mtu wa kusahau, matendo makuu ya Mungu, angepata wapi ujasiri wa kumsogelea Goliathi?.

Kwahiyo tunachoweza kujifunza ni kuwa Ushuhuda wa Daudi kuwaua Dubu na Simba, ulikuwa ni wa muhimu sana kwa nyakati zijazo.

Kadhalika yapo mambo mengi ya kimiujiza ujiza yanayoendelea kila siku katika maisha yetu, ambayo Bwana anayafanya, hatuna budi kuyahifadhi hayo, aidha kwa maandishi, au kama tunakumbukumbu nzuri basi tuyahifadhi mioyoni mwetu yasiweze kupotea.

Hebu tuangalie mfano mwingine wa mtu aliyetunza mambo makuu Mungu aliyoyafanya mbele ya macho yake, ambapo yakaja kuwa ya maana sana siku za mbeleni.

Na mtu huyo si mwingine zaidi ya Mariamu, mama yake YESU.

Asilimia kubwa ya habari tunazozisoma za kuzaliwa kwa Bwana Yesu, na matukio yaliyokuwa yanaendelea wakati wa kuzaliwa kwake, ni kutokana na Mariamu kuwasimulia watu, hakuna mwingine aliyekuwa na taarifa za kutosha kuhusu kuzaliwa kwa Yesu zaidi ya mama yake Mariamu.

Kwamfano habari za wale wachungaji makondeni tunazozisoma, Waandishi kama wakina Luka, Mathayo na Yohana hawakufunuliwa, bali walizipata kutoka kwa Mariamu, mama yake, kwani walikwenda kumuuliza ni nini kilikuwa kinaendelea wakati wa kuzaliwa kwake..Na Mariamu akawaeleza na ndio wakaandika habari hizo.. Hawakufunuliwa habari hizo na Roho Mtakatifu, wala hawakuona maono, hapana!, bali walihadithiwa na wakina Mariamu..

Luka mwenyewe anashuhudia hayo…

Luka 1:1 “Kwa kuwa watu wengi wametia mikono kutunga kwa taratibu habari za mambo yale yaliyotimizwa katikati yetu,

2  KAMA WALIVYOTUHADITHIA WALE WALIOKUWA MASHAHIDI WENYE KUYAONA, na watumishi wa lile neno tokea mwanzo,

3  nimeona vema mimi nami, kwa kuwa nimejitafutia usahihi wa mambo hayo yote tangu mwanzo, kukuandikia kwa taratibu, Theofilo mtukufu,”.

Umeona hapo?. Luka anasema “kama walivyotuhadithia”.. Maana yake ulipofika wakati wa kwenda kuandika habari za Bwana kiusahihi, waliwatafuta wakina Mariamu, na wengine wachache waliokuwepo wakati wa kuzaliwa kwake, wawasimulie yaliyokuwa yanajiri..

Sasa hebu tuchunguze zile habari za wachungaji makondeni Mwandishi Luka alizitolea wapi!..

Luka 2:8  “Na katika nchi ile ile walikuwako wachungaji wakikaa makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu usiku.

9  Malaika wa Bwana akawatokea ghafula, utukufu wa Bwana ukawang’aria pande zote, wakaingiwa na hofu kuu.

10  Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote;

11  maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana.

12  Na hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelala katika hori ya kulia ng’ombe.

13  Mara walikuwapo pamoja na huyo malaika, wingi wa jeshi la mbinguni, wakimsifu Mungu, na kusema,

14  Atukuzwe Mungu juu mbinguni, Na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.

15  Ikawa, malaika hao walipoondoka kwenda zao mbinguni, wale wachungaji waliambiana, Haya, na twendeni mpaka Bethlehemu, tukalione hilo lililofanyika, alilotujulisha Bwana.

16  Wakaenda kwa haraka wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelala horini.

17  Walipomwona wakatoa habari waliyoambiwa juu ya huyo mtoto.

18  wote waliosikia wakastaajabu kwa hayo waliyoambiwa na wachungaji.

19  LAKINI MARIAMU AKAYAWEKA MANENO HAYO YOTE, AKIYAFIKIRI MOYONI MWAKE.

20  Wale wachungaji wakarudi, huku wanamtukuza Mungu na kumsifu kwa mambo yote waliyosikia na kuyaona, kama walivyoambiwa”

Umeona hapo?, Mariamu aliyaweka hayo yote moyoni!, hakuyapuuzia tu na kuyaacha yapite!, bali aliyatunza, kwasababu alijua siku moja yatakuja kuwafaa wengine huko mbeleni, ambao ndio wakina Luka pamoja na sisi.

Kadhalika tuchunguze sehemu nyingine tena Mariamu, aliyoweka kumbukumbu ya maisha ya Mwokozi Yesu..

Luka 2:48 Na walipomwona walishangaa, na mama yake akamwambia, Mwanangu, mbona umetutenda hivi? Tazama, baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni.

49  Akawaambia, Kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu?

50  Nao hawakuelewa na neno hilo alilowaambia.

51  Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii; NA MAMAYE ALIYAWEKA HAYO YOTE MOYONI MWAKE.

52  Naye Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu”

Umeona na hapo?..Kama Mariamu asingeyaweka moyoni leo hii tusingejua kama Bwana alikuwa ni mtii kwa Mungu na kwa wanadamu. Na sio tu hayo bali na mengine yote tunayoyasoma yanayomhusu Bwana, ni kutokana na mtu, au watu Fulani kutunza kumbukumbu hizo.

Jambo ambalo limekuja kuwa Baraka kwetu sisi, watu wa vizazi vya baadaye..

Kadhalika na sisi hatuna budi kujifunza katika hayo, tutunze kumbukumbu za yote Bwana anayoyafanya kwetu, au kwa watoto wetu, au kwa jamii yetu, ili kumbukumbu hizo ziweze kuja kutusaidia katika nyakati za baadaye za majaribu, na ziweze pia kusaidia vizazi vingine vijavyo kama vitakuwepo.

Mithali 13:22 “Mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi; Na mali ya mkosaji huwa akiba kwa mwenye haki”.

Bwana atubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Pia kama utapenda uwe unafikiwa na masomo ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP basi bofya hapa ujiunge moja kwa moja  >>>> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

MAMA, TAZAMA, MWANAO.

Na ulimi laini huvunja mfupa.(Mithali 25:15)

SIKU YA HOFU YANGU NITAKUTUMAINI WEWE.

Hanithi ni nini katika biblia? (kumbukumbu 23:17)

Hapana hata mmoja aliyethubutu kuambatana nao;

HUYU MELKIZEDEKI NI NANI?

Rudi nyumbani

Print this post

KWANINI MITUME WAMUULIZE BWANA FARAGHANI?

Yapo mambo mengi ambayo, mitume waliyasikia yakizungumzwa na Bwana, na wakati huo huo wakamuuliza maana yake na wakapewa majibu yake,. Lakini yapo majira ambayo walipoyasikia maneno ya Bwana, hawakuwa na haraka ya kuuliza maswali yao muda huo huo, Bali walimtafuta Bwana faraghani(yaani akiwa peke yake) katika utulivu, ndipo wakawasilisha maswali yao.

Unaweza kujiuliza ni kwanini iwe faragha? Ni kwasababu, walihitaji umakini sana wa kupokea majibu ya maswali yao yaliyowasumbua vichwa.. Na leo tutaona baadhi ya maswali hayo, ambayo na sisi kama wakristo, tunahitaji sana faragha na Bwana ili tuweze kuyaelewa majibu yake, vinginevyo hatutakaa tuelewe kama tutakuwa ni watu wa kuchukulia tu kila kitu juu juu.

Maswali yenyewe tunayasoma katika kile kitabu cha Mathayo 24 Tusome;

Mathayo 24:1 “Yesu akaenda zake, akatoka hekaluni; wanafunzi wake wakamwendea ili kumwonyesha majengo ya hekalu.

2 Naye akajibu akawaambia, Hamyaoni haya yote? Amin, nawaambieni, Halitasalia hapa jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa.

3 Hata alipokuwa ameketi katika mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamwendea kwa faragha, wakisema, Tuambie, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini dalili ya kuja kwako, na ya mwisho wa dunia”?

Kama unavyoweza kusoma  hapo kwenye huo  mstari wa tatu, biblia inasema walimfuata Bwana kwa faragha, wakiwa wenyewe, muda ambao hakuna masumbufu ya makutano, au ndugu au shughuli yoyote ile.

Wakati ambao mazingira ni tulivu kuna shwari kuu, na Bwana hayupo katika shughuli yoyote ya kihuduma, ndipo kwa pamoja wakamfuata, wakamuuliza hayo maswali makuu matatu yanayohusiana na mwisho wa dunia.

Sasa yafuatilie kwa makini maswali haya, kwasababu kumbuka iliwagharimu mitume “faragha”, kuyaelewa majibu yake. Na ndio maana hawakuyumbishwa na mafundisho ya uongo, yanayohusiana na siku za mwisho, kama ilivyo leo wakristo wengi wanavyoyumbishwa na vitu ambavyo hata havipo katika maandiko, hiyo yote ni kwasababu hatutaki kuwa katika utulivu rohoni kusikia Kristo anasema nini katika Neno lake.

Maswali yenyewe yalikuwa ni haya;

1)Mambo hayo yatakuwa lini?

2) Nayo ni nini dalili ya kuja kwako

3) na ya mwisho wa dunia

1) Tukianzana na swali la kwanza, Mambo hayo yatakuwa lini?

Swali hilo lililenga moja kwa moja, juu ya siku, tarehe, na mwaka, wanafunzi walikuwa wanataka kujua ni “LINI” atarudi, ni lini atakuja kulichukua kanisa lake, tarehe ngapi, mwaka gani na mwezi gani. Ndipo Bwana Yesu akawajibu moja kwa moja swali lao katika ule mstari wa 36-44 na kuwaambia..

Mathayo 24:36 “Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake.

37 Kwa maana kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.

38 Kwa kuwa kama vile siku zile zilizokuwa kabla ya Gharika watu walivyokuwa wakila, na kunywa, wakioa na kuolewa, hata siku ile aliyoingia Nuhu katika safina,

39 wasitambue, hata Gharika ikaja, ikawachukua wote, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.

40 Wakati ule watu wawili watakuwako kondeni; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa;

41 wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa.

42 Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu.

43 Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa.

44 Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja”.

Unaona hapo? Aliwaeleza wazi kuwa siku hiyo atakayorudi hakuna aijuaye, ni siri ya Mungu, lakini hakuwaacha tu hivyo hivyo hewani waishie kujua hivyo, bali aliendelea kuwaeleza mwonekano wa siku hiyo jinsi utakavyokuwa, kwamba wasidhani siku hiyo kutakuwa na mabadiliko yoyote ya kimwonekano duniani, hapana, itakuwa ni siku kama siku nyingine, watu watakuwa wakila na kunywa, wakipanda na kuvuna, wakiwekeza, uchumi wa taifa ukiimarika, wakioa na kuolewa, kama ilivyokuwa siku za Nuhu na Lutu, lakini ghafla tu, kufumba na kufumbua, Yesu amerudi ameshachukua watakatifu wake amekwenda nao mbinguni.

Kama tu ilivyo leo ndugu yangu,Kristo akirudi leo, huwezi amini, kwasababu, ungetazamia labda, uone ishara Fulani kubwa mbinguni, au watu wengi wakienda kanisani?,Lakini hamna, itakuwa siku kama ya leo, ambayo unaona serikali ikiweka mipango yake, na wanadamu wakijishughulisha na kazi zao za kila siku, ndio hapo wengine watakuwa shambani, wengine vitandani kama alivyosema. Ni siku ya kitofauti sana ambayo Itakuwa nje kabisa na matazamio ya watu wengi.

2) Swali la pili lilikuwa ni nini dalili ya kuja kwako;

Walitamani kufahamu sasa, dalili zitakazoonyesha yupo karibuni kufika. Hapo ndipo utaona akieleza dalili hizo kuanzia mstari ule wa 4-28, kwamba kutatokea manabii wa uongo, matetemeko ya nchi, vita, magonjwa(Corona), kuchipuka kwa Israeli, kuongezeka kwa maasi, akawaambia mkiyaona hayo yote basi mjue nipo mlangoni kurudi.

Mambo ambayo sisi tunaoishi sasa hivi tumeshayashuhudia yote, na wala hakuna hata moja ambalo halijatimia. Hivyo, hiyo ni kutuonyesha kuwa siku yoyote, tutamwona Kristo. Kama vile wanavyosema dalili ya mvua ni mawingu, nasi dalili zote zimeshatimia hakuna asiyejua ni paraparanda tu kulia.

3) Na swali la tatu na la mwisho, lilikuwa ni kuhusiana na mwisho wa dunia.

Walitamani kujua pia, mwisho wa dunia utakuwaje, tukiachia mbali siku ya kurudi kwake, kiama kitakuwaje? Je! Kutakuwa ni gharika kama ilivyokuwa kwa Nuhu, au ulimwengu utaendelea kudumu hivyo hivyo mpaka milele. Lakini tunasoma Bwana Yesu aliwajibu swali hilo katika mistari hii;

“29 Lakini mara, baada ya dhiki ya siku zile, jua litatiwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake, na nyota zitaanguka mbinguni, na nguvu za mbinguni zitatikisika;

30 ndipo itakapoonekana ishara yake Mwana wa Adamu mbinguni; ndipo mataifa yote ya ulimwengu watakapoomboleza, nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi.”

Siku hii ni mbaya sana, kwasababu jua litakuwa giza, na mwezi kuwa mwekundu, kutakuwa na tetemeko kubwa la ardhi, ambalo litapelekea mpaka visiwa kuhama, hadi watu watatamani milima iwaangukie,wafe, ili tu waikwepe  hiyo ghadhabu ya Mungu.

Siku ya kiama inatisha ndugu yangu. Mpaka Mungu mwenyewe anauliza kwanini mwaitamani siku hiyo? Ni siku mbaya sana ambayo haijawahi kutokea katika historia ya dunia.

Itoshe tu kusema hayo, lakini mambo haya unapaswa uyajue, kuwa siku isiyokuwa na dalili Kristo anarudi, swali ni je! Umejiwekaje ndugu?  Je! Bado upo nje ya Kristo? Kama sivyo basi tubu leo umepokee Kristo, ayabadilishe maisha yako, kisha uwe tayari kubatizwa kwa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako. Ikiwa upo tayari leo kutubu, basi wasiliana nasi kwa namba zetu hizi 0693036618, tuombe pamoja, na vilevile ikiwa unahitaji ubatizo basi fanya hivyo hivyo tutakusaidia.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Mafundisho

MUUNGANO WA DINI NA MADHEHEBU YOTE, UMEKARIBIA.

DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 10 (Kitabu cha Zaburi).

Nini maana ya “Roho za manabii huwatii manabii?

Rudi nyumbani

Print this post

Je ni lazima kupitia mafundisho ya muda mrefu kabla ya kubatizwa?

Jibu: Ubatizo ni tendo linalopaswa lifanyike, haraka sana baada ya mtu kuamini. Tunaposema kuamini tunamaanisha  kumwamini Bwana Yesu kuwa ndiye mkombozi wa ulimwengu, na kumkiri kwa kinywa na kisha kuungama dhambi zote mbele zake.

Hivyo mtu anapoamini tu namna hiyo, hapaswi kwenda kupitia mafunzo Fulani ya ubatizo, la!.. Bali moja kwa moja anapaswa akabatizwe, ikiwezekana siku hiyo hiyo alipoamini, ndivyo maandiko yanavyosema..

Sasa Ili kulithibitisha hilo tunaweza kujifunza mifano kadha katika biblia…

Mfano wa kwanza ni kuhusu habari ya Yule Mkushi-Towashi aliyekutana na Filipo. Maandiko yanasema Mkushi Yule alipoamini, saa ile ile baada ya kuamini alibatizwa..

Matendo 8:34  “Yule towashi akamjibu Filipo, akasema, Nakuomba, nabii huyu; asema maneno haya kwa habari ya nani; ni habari zake mwenyewe au za mtu mwingine?

35  Filipo akafunua kinywa chake, naye, akianza kwa andiko lilo hilo, akamhubiri habari njema za Yesu. 36  Wakawa wakiendelea njiani, wakafika mahali penye maji; yule towashi akasema, Tazama, maji haya; ni nini kinachonizuia nisibatizwe?

37  Filipo akasema, Ukiamini kwa moyo wako wote, inawezekana. Akajibu, akanena, Naamini ya kwamba Yesu Kristo ndiye Mwana wa Mungu.]

38  Akaamuru lile gari lisimame; wakatelemka wote wawili majini, Filipo na yule towashi; naye akambatiza”.

Umeona hapo?.. Filipo hakumwambia huyu Mkushi, asubiri apitia mafunzo Fulani kwanza ya ubatizo, ya wiki kadhaa, au miezi kadhaa, ndipo akidhi vigezo vya kubatizwa!.. La! Hakumwambia hayo hata kidogo.. Bali alimbatiza pale pale alipoona kuwa tayari kushamwamini Bwana, na yeye mwenyewe yupo tayari..

Mfano wa pili ambao unaweza kuzidi kututhibitishia, ni ule unaomhusu Kornelio na familia yake. Kwani Kornelio aliyekuwa akida wa jeshi la kirumi, aliposikia tu habari za Yesu na kuamini, zilizohubiriwa na Mtume Petro aliamini, na Roho Mtakatifu aliwashukia na baada ya hapo wakabatizwa siku ile ile.. hawakungoja siku nyingine, wala Petro hakuwaambia wakae kwanza chini ya mafundisho ndipo wabatizwe!.. bali tunaona ni siku ile ile walibatizwa..

Matendo 10:44 “ Petro alipokuwa akisema maneno hayo Roho Mtakatifu akawashukia wote waliolisikia lile neno.

45  Na wale waliotahiriwa, walioamini, wakashangaa, watu wote waliokuja pamoja na Petro, kwa sababu Mataifa nao wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu.

46  Kwa maana waliwasikia wakisema kwa lugha, na kumwadhimisha Mungu. Ndipo Petro akajibu,

47  Ni nani awezaye kuzuia maji, hawa wasibatizwe, watu waliopokea Roho Mtakatifu vile vile kama sisi?

48  Akaamuru wabatizwe kwa Jina lake Yesu Kristo. Ndipo wakamsihi azidi kukaa siku kadha wa kadha”.

Sehemu nyingine ya mwisho katika biblia inayoweza kututhibitishia kuwa ubatizo unapaswa ufanyike punde tu mtu anapoamini ni katika habari za Yule Askari wa gereza aliyewekwa kuwalinda Paulo na Sila.

Maandiko yanatuambia, mara baada ya Yule askari kuona ishara ile kubwa ya nchi kutetemeka na milango kufunguka, alitaka kujiua, lakini Mungu alimwepusha na hilo na kinyume chake akamwamini Yesu usiku ule ule, na katika usiku ule ule alioamini, alikwenda kubatizwa yeye na familia yake yote!, wala Paulo hakusubiri kupambazuke ndipo akambatize!, bali usiku ule ule alikwenda kuwabatiza.

Matendo 16:25 “Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza.

26  Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote vikalegezwa.

27  Yule mlinzi wa gereza akaamka, naye alipoona ya kuwa milango ya gereza imefunguka, alifuta upanga, akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wamekimbia.

28  Ila Paulo akapaza sauti yake kwa nguvu, akisema, Usijidhuru, kwa maana sisi sote tupo hapa.

29  Akataka taa ziletwe, akarukia ndani, akitetemeka kwa hofu, akawaangukia Paulo na Sila;

30  kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate kuokoka?

31  Wakamwambia, Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako.

32  Wakamwambia neno la Bwana, yeye na watu wote waliomo nyumbani mwake.

33  Akawakaribisha saa ile ile ya usiku, akawaosha mapigo yao, KISHA AKABATIZWA, YEYE NA WATU WAKE WOTE WAKATI UO HUO.

34  Akawaleta juu nyumbani kwake, akawaandalia chakula, akafurahi sana, yeye na nyumba yake yote, maana amekwisha kumwamini Mungu”

Hapo katika mstari wa 33, maandiko yanasema “KISHA AKABATIZWA, YEYE NA WATU WAKE WOTE WAKATI UO HUO”.. Na sio kesho yake, au asubuhi yake!, bali “wakati huo huo” baada ya kuamini tu!.

Na kama biblia ndio mwongozo wetu na Taa yetu, basi hatuna budi na sisi kufanya kama Mitume walivyofanya.. kwamba mtu anapoamini, hapo hapo anapaswa akabatizwe!, na hapaswi kungojeshwa sana!.

Kadhalika na sisi tulioamini ambao bado hatujabatizwa!.. Ni lazima tuutafute ubatizo haraka sana kwasababu ni tendo la muhimu sana, na lenye madhara makubwa katika ufalme wa giza, ndio maana shetani hataki watu wabatizwe haraka pale tu baada ya kuamini, kwasababu anajua mtu akishabatizwa bali uhalali wa kummiliki Yule mtu unakuwa unapotea.. na yeye, shetani hawezi kuwa tayari kuona anampoteza mtu kirahisi hivyo.

Swali ni je umebatizwa baada tu ya wewe kuamini?.. kumbuka siku zote ubatizo sahihi ni ule wa maji tele, na kwa jina la Yesu Kristo kulingana na maandiko (Matendo 2:38), na si wa kunyunyiziwa, na vile vile watoto wadogo!, hawabatizwi kwasababu bado hata hawajajitambua na hawajaamua kumpokea Yesu na kutubu!.

Hivyo kama bado hujabatizwa!, ni vyema ukatafuta kubatizwa haraka iwezekanavyo, popote pale unapoweza kuupata!, au kama hujui mahali utakapoweza kuupata ubatizo sahihi kwa haraka, basi unaweza kuwasiliana nasi kwa namba hizi 0693036618/0789001312.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

TOFAUTISHA KATI YA MAFUNDISHO YA YESU, NA YA WAANDISHI.

Nini maana ya kuabudu malaika? (Wakolosai 2:18)

KUJIFUNUA KWA YESU KWA PILI.

saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada

Mlima wa Mizeituni  unaumuhimu gani kwetu?

Nini maana ya “Roho za manabii huwatii manabii?

Rudi nyumbani

Print this post

Nini maana ya “Heri kuchagua jina jema kuliko mali nyingi”?

SWALI: Biblia inamaanisha nini inaposema “Heri kuchagua jina jema kuliko mali nyingi”?


JIBU: Tusome

Mithali 22:1 “Heri kuchagua jina jema kuliko mali nyingi; Na neema kuliko fedha na dhahabu”.

Inaposema kuchagua jina jema, inamaanisha Sifa njema, kwamfano labda kwenye jamii utasikia watu wanasema mtu Fulani ni mkarimu, au fulani ana upendo, au yule ana utu, hilo tayari ni jina jema, ambalo limezalika kutokana na tabia zake nzuri, Lakini ukisikia wanasema mtu yule ni muhuni, au kibaka, au tapeli, au fisadi, au jambazi, tayari hilo ni jina baya, ambalo halijazuka hivi hivi tu, bali limeonekana katika maisha ya yule mtu.

Sasa tukirudi katika mstari huo , hapo haimaanishi mtu kuwa na mali nyingi ni vibaya.. Hapana, bali anamaanisha kuchagua mali, Zaidi ya sifa njema hiyo ndio mbaya sana.

Kwamfano, utakuta mtu anachagua kufanya kazi ya bar/ casino, kisa tu inamlipa pesa nyingine kuliko zile nyingine za kawaida. Jiulize, mtu kama huyu atatafsiriwaje katika jamii, kama sio barmaid, au kahaba? Hiyo yote ni kwasababu kachagua pesa Zaidi ya jina zuri.

Au mkristo unapoacha kumwimbia Mungu wake, unakwenda moja kwa moja kuimba jimbo za kidunia, kisa tu atapata pesa za haraka. Hajui kuwa jina lake linabadilika kutoka katika kuwa mtumishi hadi muhuni.

Au kanisa la Kristo, linaposhiriki katika kampeni za kisiasa kisa tu limeahidiwa donge nono kutoka kwa wanasiasa. Jiulize ni nini kinajengeka katika macho ya jamii? Si wataliita chama cha kisiasa na sio kanisa tena sivyo? Japo ni kweli watapata pesa lakini tayari jina lao limeshabadilika. Hakuna mtu atakayewaamini.

Vivyo hivyo na sisi katika mambo yetu ya maisha ya kila siku, Ni heri tuchague jina jema, kwamfano sio kila huduma tutoze watu pesa, tukifanya hivyo hatuwezi kuitwa wakarimu, hatuwezi kuitwa wenye utu, au wenye upendo.

Tumuige Bwana wetu Yesu Kristo ambaye alitafuta, heshima, na jina jema katika huu ulimwengu Zaidi ya kitu kingine chochote.

Luka 2:52 “Naye Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu”.

Jina jema linatupa kibali kikubwa sana cha kukaribiwa au kutumiwa na Mungu, Mfano, Kornerio alitokewa na Mungu mpaka kupewa neema ya wokovu kutokana na sifa yake nzuri katika jamii.

Warumi 10:22 “Wakasema, Kornelio akida, mtu mwenye haki, mchaji wa Mungu, aliye na sifa njema kwa taifa lote la Wayahudi, alionywa na malaika mtakatifu kutuma watu kwako, uende nyumbani kwake, apate kusikiliza maneno kwako”

Na wengine wengi utawasoma katika biblia kama vile Anania (Matendo 22:12) na Stefano, (Matendo 6:3-5) wote hawa kutokana na sifa zao nzuri, Mungu aliwatumia sana. Vivyo hivyo na sisi tuthamini jina jema, kuliko mali, au mambo ya huu ulimwengu yanayopita.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

IFAHAMU HUZUNI NA FURAHA YA MALAIKA.

Pesa za bindoni ni nini?(Marko 6:8)

Maswali na Majibu

Nini maana ya Mungu amemfanya mwanadamu mnyofu?

Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa watoto wake wote.

Rudi nyumbani

Print this post

Biblia inamaanisha nini inaposema “Mwenye haki huufikiri uhai wa mnyama wake”?

 Mithali 12:10 “Mwenye haki huufikiri uhai wa mnyama wake; Bali huruma za mtu mwovu ni ukatili”.


JIBU: Hapa ni Mungu alikuwa anaonyesha tabia za mtu mwenye haki jinsi zilivyo kwamba huruma zake haziishi tu kwa wanadamu wenzake, bali pia zitadhihirika mpaka na kwa wanyama.

Kama vile Mungu sasa anavyowajali wanyama wake, kiasi kwamba hakuna hata mmoja anayekufa bila ya yeye kujua, na vivyo hivyo na sisi tunapaswa tuwe na tabia hizo, alisema ..

Mathayo 10:29 “Je! Mashomoro wawili hawauzwi kwa senti moja? Wala hata mmoja haanguki chini asipojua Baba yenu;”

Sehemu nyingine Bwana Yesu alisema maneno haya;

Luka 14:5 Akawaambia, Ni nani miongoni mwenu, ikiwa ng’ombe wake au punda wake ametumbukia kisimani, asiyemwopoa mara hiyo siku ya sabato?

 Akimaanisha kuwa, kumbe watu wengi walikuwa wanainajisi sabato pasipo wao kujua na Mungu asiwahesabie makosa, kwa tendo tu hilo la kuwaokoa wanyama wao.

Utaona pia sehemu nyingine, Balaamu Yule nabii wa uongo alipompigia Yule punda wake, mara tatu, Mungu alichukizwa sana na kitendo kile.. Na ndio maana swali la kwanza aliloulizwa na Yule malaika ni kwanini amempiga Yule punda kiasi kile? (Hesabu 22:32)

 Kuonyesha kuwa Mungu hapendezwi na kitendo cha utesaji wanyama.

Hivyo na sisi pia kama tulikuwa na tabia za kuwatesa wanyama, au kutoijali mifugo yetu, kiasi kwamba ukimkuta mbwa unamsindikiza na mawe,tuache hizo tabia, kama wanaishi na sisi pasipo madhara yoyote, hakuna sababu ya kuwapiga piga ovyo, au kuwafuga na kutowahudumia.

Kwasababu kitendo cha kuwatendea mema, biblia inasema kinaongeza pia siku za kuishi duniani soma,

Kumbukumbu 22:6 “Kiota cha ndege kikitukia kuwa mbele yako njiani, katika mti wo wote, au chini, chenye makinda au mayai, naye koo ameatamia juu ya makinda, au juu ya mayai, usimtwae yule koo pamoja na makinda;

7 sharti umwache yule koo aende zake, lakini makinda waweza kuyatwaa uwe nayo; ili upate kufanikiwa, ufanye siku zako kuwa nyingi”.

Hiyo ndio maana ya huo mstari ..Mithali 12:10 “Mwenye haki huufikiri uhai wa mnyama wake; Bali huruma za mtu mwovu ni ukatili”.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa watoto wake wote.

HAKUNA MTU ANIONDOLEAYE, BALI MIMI NAUTOA MWENYEWE

WALA MSIUANGALIE MWILI, HATA KUWASHA TAMAA ZAKE.

SINA PESA SASA, YESU ATANISAIDIA NINI?

Rudi nyumbani

Print this post

Kwanini Paulo, alihukumu wakati hukumu hairuhusiwi?

SWALI: Tukisoma katika Kitabu cha 1 Wakorintho Sura ile ya Tano, Tunaona Mtume Paulo Akizungumzia Habari Ya kutengwa Kwa Watu wenye kulichafua kanisa la Mungu,… sasa tukija katika Mstari wa 3, alisema hivi..

“ Kwa maana kweli, nisipokuwapo kwa mwili, lakini nikiwapo kwa roho, mimi mwenyewe nimekwisha KUMHUKUMU yeye aliyetenda jambo hilo, kana kwamba nikiwapo”.

Swali langu ni hili, Katika Huo mstari wa Tatu, naona Mtume Paulo anasema kwamba, mtu wa namna ile, Yaani aliye mzinzi, mlevi N.K.. yeye Amekwisha Kumuhukumu,… Sasa na Tukisoma katika kitabu cha Mathayo, 7:1, Bwana Yesu alituonya Kwamba tusihukumu, kwa maana tukihukumu mtu nasi tutahukimiwa….Sasa hapa imekaaje kaaje?


JIBU: Hukumu Mtume Paulo aliyomaanisha hapo si kuhukumu ile inayozungumziwa katika Mathayo 7..Kwamba msihukumu msije mkahukumiwa,.. Ile inayozungumziwa inakuja pale mtu anapotoa maneno yanatoa hatma ya maisha ya mtu mwingine, kana kwamba ni Mungu , kwamfano,kumwambia mwenzako wewe ni wa motoni tu, hata iweje huwezi kuokoka.  Hapo umeshahukumu. Au unapowaona wenye dhambi, kama vile mashoga, na unaanza kusema wale makafiri Mungu hawezi kuwakubali milele, dhambi zao hazifutiki,..Hapo tayari umeshahukumu.

Lakini mtume alichokimaanisha hapo sio hicho, bali alimaanisha hukumu ya ADHABU. Yaani kuadhibiwa kwa huyo mtu.

Na jambo kama hilo Mungu ameliruhusu wakati mwingine katika kanisa kufanyika.. Kwamfano katika habari hiyo ukiendelea kusoma mistari inayofuata utaona, mtume Paulo alisikia wakorintho wamejihusisha na zinaa mbaya, iliyokithiri ambayo haipo hata kwa watu wenye dhambi, yaani mtu anazini na mama yake halafu bado yupo katika kanisa. Sasa kwa kosa kama hilo Paulo akawaambia wakorintho, hata kabla hajafika tayari ameshamuhukumia adhabu mtu kama huyo. Na adhabu yenyewe ni kumkabidhisha shetani amuue, mwili aungamie ili roho ipone siku ile ya hukumu.

Hata sasa, matendo kama haya, yanaendelea katika kanisa la Kristo, leo hii limekuwa ni jambo la kawaida kusikia wachungaji wanazini na washirika wao, wengine wanavuka mipaka hadi na watoto wadogo, utasikia askofu anazini na muumini pamoja na mama yake, jambo ambalo huwezi kuliona hata kwa watu wenye dhambi. Na wenyewe wanaona ni sawa kwasababu hakuna mtu wa kuwakabidhisha kwa shetani.

Paulo anasema, ni heri ukabidhiwe kwa shetani uuawe, walau hasira ya Mungu utapoa juu yako, na siku  ile ya hukumu unusurike, kuliko kuendelea kuishi, katika hali hiyo hiyo mpaka kufa kwako, kwani adhabu yako itakuwa kubwa sana siku ile.

Luka 12:47 “Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana”.

Hivyo hiyo inatukumbusha  tuwe makini sana, katika ukristo wetu, vilevile  na katika wito wetu.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Nini maana ya msiwe waalimu wengi (Yakobo 1:3)?

Tofauti ya kazi ya Damu ya Yesu na Jina la Yesu ni ipi?

Tofauti kati ya mtume na mwanafunzi ni ipi kibiblia?

TABIA YA WAZI INAYOWATOFAUTISHA MANABII WA UONGO NA WALE WA UKWELI.

Mungu anaposema “nitaliweka jina langu” ana maana gani?

Rudi nyumbani

Print this post

Je mbinguni itakuwa ni kuimba tu wakati wote?.

Jibu: Hakuna andiko lolote katika biblia linalosema mbinguni ni mahali pa kuimba tu wakati wote!. Bwana Yesu alisema anakwenda kutuandalia makao..

Yohana 14:1 “Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi.

2  Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali.

3  Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo”.

Umeona hapo anasema anaenda kutuandalia Makao, maana yake makazi..Na tena anasema yapo makao Mengi! (Si machache)…Na sehemu yoyote yenye makao/ makazi maana yake kuna shughuli nyingi, sio kuimba tu!. Kwa ufupi mbinguni itakuwa ni sehemu yenye upeo mkubwa kuliko duniani, vinginevyo basi duniani pangekuwa bora kuliko mbinguni.

Kama duniani tu! Vipo vitu vingi ambavyo vinavyowapa wanadamu raha, (ambavyo kimojawapo ndio hiyo kuimba) basi mbinguni hapawezi kuwa panyonge kuliko duniani, maana yake kule ni mara elfu elfu ya hapa.. zitakuwepo shughuli nyingi, na mambo mengi yatakayotupa raha na furaha, na sio kuimba tu!..kuimba itakuwa ni sehemu ya vitu hivyo!..Ndio maana mpaka sasa Bwana anatuandalia makao hayo, tukifika huko tutamfurahia Mungu katika viwango ambavyo hatujawahi kumfurahia.

Hivyo kwa hitimisho ni kwamba mbinguni hapatakuwa ni mahali pa kuimba tu usiku na mchana, bali kutakuwepo na mambo mengine mengi, ambayo biblia inasema jicho halijawahi kuona wala sikio kusikia.

1Wakorintho 2:9 “ lakini, kama ilivyoandikwa, Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, (Wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu,) Mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao”

Kwahiyo hatuna budi kutafuta kuingia mbinguni kwa gharama zozote zile, ili tusiyakose hayo mambo mazuri tuliyoahidiwa na Baba. Na lango la kuingia mbinguni ni moja tu!, nalo ni YESU KRISTO, alisema..

Yohana 14:5 “Tomaso akamwambia, Bwana, sisi hatujui uendako; nasi twaijuaje njia?

6  Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi”

Kwa kumwamini Yesu, na kuungama dhambi zetu zote, na kubatizwa katika ubatizo sahihi, na kupokea Roho Mtakatifu, hapo tayari tutakuwa tumeshaanza safari ya kwenda mbinguni. Tutakuwa tumeshaiona njia.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

YANAYOENDELEA SASA KATIKA MADHABAHU YA MUNGU ROHONI.

TABIA ZITAKAZOMTAMBULISHA MPINGA-KRISTO AJAYE.

BASI TUENDELEE KUMJUA MUNGU,NAYE ATATUJILIA KAMA MVUA YA VULI.

Jiepushe na tamaa ya Mali/kupenda fedha.

Rudi nyumbani

Print this post

Je! Watu ambao hawajawahi kusikia injili kabisa siku ya mwisho watahukumiwa?

JIBU: Kumbuka Mungu ameiandika injili yake katika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza ni katika kitabu, na sehemu ya pili ni katika moyo wa mwanadamu.

Watu wengi tunadhani, ni mpaka tusikie ndio tutahukumiwa hapana, hiyo ni sehemu ya kwanza, lakini kuna sheria ambayo Mungu tayari kashiweka katika moyo wa kila mwanadamu ajapo hapa duniani, ambayo hiyo inathibitishwa na kutetewa na “dhamiri na mawazo” ya mtu mwenyewe.

Biblia inasema..

Warumi 2:14 “Kwa maana watu wa Mataifa wasio na sheria wafanyapo kwa tabia zao yaliyo ndani ya torati, hao wasio na sheria wamekuwa sheria kwa nafsi zao wenyewe.

15 Hao waionyesha KAZI YA TORATI ILIYOANDIKWA MIOYONI MWAO, dhamiri yao ikiwashuhudia, na mawazo yao, yenyewe kwa yenyewe, yakiwashitaki au kuwatetea;”

Umeona? Ikiwa na maana kuwa, hata ukienda katika jamii za watu ambao wamejitenga kabisa huko maporini, hawajui chochote kinachoendelea ulimwenguni, kazi yao ni kuwinda na kukusanya tu..bado utawakuta na tabia ambazo zinaendana kabisa na sheria za Mungu, kana kwamba wanaijui torati. Kwamfano utakuta wanapinga vitendo vya uuaji, wizi, au uzinzi n.k.

Mambo kama hayo, hawakuyasoma kwanza kwenye biblia, bali tayari yalishaandikwa mioyoni mwao kana kwamba walikuwa wanaijua biblia. Na ndio katika hayo Mungu atawahukumu. Kwasababu kama tulivyosoma hapo, kwamba kama mtu atafanya yaliyo ndani ya sheria, hata kama hajaisikia, basi tayari anaitenda sheria hiyo ndani ya moyo wake.

Lakini wakati wasasa tunaoishi, injili ya Kristo imeshasambaa ulimwenguni kote, Tumesikia, na bado mioyo yetu inatushuhudia. Haijalishi utaiamini, au huiamini,  Hivyo tujue kuwa tusipoitii hatutakuwa na udhuru siku ile ya hukumu.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

JE! WATOTO WACHANGA WANAWEZA KUHUKUMIWA NA KUTUPWA MOTONI.

KUJIFUNUA KWA YESU KWA PILI.

HUTATAMBUA LOLOTE, SIKU YA UNYAKUO IKIFIKA.

NI LIPI KATI YA MAKUNDI HAYA, WEWE UPO?

Rudi nyumbani

Print this post

WAPENZI, MSIIAMINI KILA ROHO.

Wakati tunaoishi ni wakati ambao kuna machafuko mkubwa sana ya rohoni kuliko hata nyakati nyingine zilizowahi kupita huko nyuma,. Na muasisi wa hayo  ni shetani kwasababu anajua katika agano letu jipya kiini cha Kanisa ni ROHO MTAKATIFU. Hivyo anajua akiruhusu Roho wa Mungu peke yake alitawale kanisa, atawakosa watu wengi sana.

Hivyo tangu ule wakati wa mitume, alibadilisha mbinu zake za kivita, akitaka kulishambulia kanisa, haji tena mwilini, bali, ni anakuja na roho za udanganyifu zinazofanana sana na Roho Mtakatifu wa kweli kumbe sio.

Hivyo kuanzia ule wakati alianza kutoa matoleo mengi sana ya roho hizo. Mpaka sasa matoleo aliyonayo ni ya hali ya juu sana, kiasi kwamba usipokuwa makini utaweza ukavamiwa na roho za udanganyifu ukadhani ni Roho Mtakatifu kumbe ni uongo. Tupo katika wakati ambao si wa kiziamini kila roho zinazohubiriwa na watu.

Na ndio maana mitume walituonya na kusema..

1 Yohana 4:1 “Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani”.

Sasa ili tuwe salama ni vizuri tukajua tabia za kweli za  Roho Mtakatifu zipoje, ili tuwe na amani na tulichokipokea.

  1. Tabia ya kwanza ni kuwa Atakufanya uwe Mtakatifu: 

Kama jina lake lilivyo, “Roho Mtakatifu”, ndicho anachokifanya ndani ya mtu pale anapokuja juu yake rasmi, Atamfanya awe mtakatifu. Kama alivyosema katika 1Wakorintho 3:16, kuwa miili yetu ni lazima iwe mitakatifu kwasababu huyo Roho anayekaa ndani yetu ni Mtakatifu. Hivyo Ni lazima ahakikishe kuwa yale matunda yote ya roho yapo ndani yako sawasawa (Wagalatia 5:22-23)

Hivyo ukiona umepokea Roho, ambayo ndani yako haikupi kiu ya kuwa mtakatifu, yaani kuacha anasa, kuacha uvaaji mbovu, kuacha, miziki ya kidunia, kuacha vimini, na milegezo, kuwa na upendo, na kiasi, basi ujue hiyo sio Roho ya Mungu, haijalishi utanena kwa lugha muda mrefu kiasi gani.. Kimbia hapo, haraka sana.

2) Atakuongoza katika kuijua kweli yote(Yohana 16:13): 

Kazi nyingine ya Roho wa kweli wa Mungu, ni kuwa hatakuacha katika hali hiyo hiyo,ya ujinga wa kiroho uliokuwa nao sikuzote, ni lazima akupigishe hatua za kiufahamu mpaka kufikia kusimama imara katika maandiko. Lakini ukiona umeokoka na miaka nenda rudi, hujui chochote kuhusiana na Neno la Mungu, wewe unachojua ni habari za wachawi na mapepo, ujue kuwa Huyo sio Roho Mtakatifu uliyempokea bali ni roho nyingine ya adui ipo ndani yako.

3) Atamshuhudia Kristo ndani yako : 

Roho Mtakatifu kazi yake ni kutoa ushuhuda wa Kristo katikati ya kanisa lake, na sio wa mwanadamu yoyote. Ikiwa na maana kiini cha kanisa ulilopo, au huduma, unayoitumikia msingi wa hapo ni lazima awe Bwana Yesu Kristo. Na sio mwanadamu Fulani, au mtakatifu Fulani. Ukiona Kristo hapewi kipaumbele chochote, au anachukuliwa kama mtu wa ziada tu, ujue roho ya mpingakristo ipo hapo.

1Yohana 4:2 “Katika hili mwamjua Roho wa Mungu; kila roho ikiriyo kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili yatokana na Mungu.

3 Na kila roho isiyomkiri Yesu haitokani na Mungu. Na hii ndiyo roho ya mpinga Kristo ambayo mmesikia kwamba yaja; na sasa imekwisha kuwako duniani”.

4) Ataweka karama au huduma ndani yako (1Wakorintho 12):

Karama hiyo/ huduma hiyo Roho Mtakatifu anaiweka kwa lengo la kulijenga kanisa la Mungu. Haiwezekani, ukawa umeokoka muda mrefu na miaka mingi, na umesema umepokea Roho Mtakatifu lakini kazi yako katika ufalme wa mbinguni haionekani. Wakati mojawapo ya kazi ya Roho Mtakatifu ni kuweka vipawa ndani yetu.

Hivyo kama hutakuwa mchungaji, au nabii, au mwinjilisti, au shemasi, au mwenye karama ya lugha, n.k basi utakuwa ni nyingine yenye faida katika kanisa kama kukirimu, kuimba, kufadhili n.k. Lakini haiwezekani kiungo kikawa hakina kazi kabisa katika mwili wa Kristo, kama mshirika anayekuja na kuondoka, miaka yote, ukiona hivyo ujue kuwa Roho uliyempokea si wa Mungu, bali ni wa adui.

5) Atachochea kuomba ndani yako. (Warumi 8:26)

Maandiko yanasema Roho Mtakatifu anaugua ndani yetu, kwa namna isiyoweza kutamkwa. Ikiwa na maana Mkristo wa kweli aliyepokea Roho, hataona amani kukaa wiki, miezi, miaka bila kuomba. Ile furaha ya wokovu itaondoka tu ndani yake, Hivyo atalazimika, kuwa mwombaji mzuri, kuhudhuria mikesha, na kufunga wakati mwingine.

Lakini ukiona unayo amani, kukaa mwezi mzima bila kuomba, na ndani yako husikii chochote, au mzigo wowote, hapo umepokea Roho nyingine ya adui. Jitathimini tena.

Tabia hizi tano (5), ukiziona ndani yako. Basi ujue Roho uliyempokea ni kweli Roho Mtakatifu, uwe na amani. Lakini kama hivyo vyote havipo ndani yako, Roho uliyepokea ni ya adui ibilisi. Unachopaswa ufanye ni umaanishe kuokoka katika maisha yako.

Maana yake, utubu dhambi zako kweli kweli, kisha ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO (Matendo 2:38). Kisha baada ya hapo, Roho wa kweli ataingia ndani yako, kuanza kukupigisha hizo hatua.

Kumbuka hizi ni siku za mwisho, na tumeaswa sana tuzijaribu hizo roho, usiridhike, na tabia mojawapo tu, jiulize je! Zote hizo zinaonekana ndani yako?

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

TUJIFUNZE JAMBO KWA WANAWAKE HAWA WAWILI.

Tofauti ya kazi ya Damu ya Yesu na Jina la Yesu ni ipi?

Kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?

AHADI YA ROHO ILIYOSALIA SASA KWA KIPINDI CHETU.

Rudi nyumbani

Print this post