Category Archive Home

Uchaji ni nini kama tunavyosoma katika 1Timotheo 2:10?

Tusome..

1Timotheo 2:10 “bali kwa matendo mema, kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa Mungu”

Uchaji ni kitendo cha “kumcha Mungu”. Ni sawa na neno “Ulaji wa chakula” ni neno linalotokana na kitendo cha “kula chakla” Na vivyo hivyo uchaji, ni kitecho cha kumcha Mungu.

Lakini tukirudi kwenye mstari huo, tukianzia juu kidogo kina jambo lingine la kujifunza..Tusome,

1Timotheo 2.9 “Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani;

10  bali kwa matendo mema, kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa Mungu”

Mstari huo unawahusu wanawake, yaani vigezo vya wanawake wanaoukiri Uchaji wa Mungu, kwamba wanapaswa wawe watu wa kujisitiri, maana yake ni kuwa mwanamke ambaye hajisitiri, haijalishi anafanya kazi gani ya kanisa, au anamwimbia Mungu..Bado Hamchi Mungu..Huyo ni wa kidunia, ni mfano wa Yezebeli.

Kumbuka hili binti wa Mungu, Mwanamke hapaswi kuvaa hereni, mikufu, hapaswi kuvaa suruali (iwe pana au nyembamba), hapaswi kuchonga nyusi, hapaswi kusuka rasta, hapaswi kupaka rangi kucha, wala kupaka rangi mdomoni na mambo mengine yanayofanana na hayo. Na sababu pekee ni kwamba Miili yetu ni hekalu la Roho Mtakatifu, na sisi sio mali yetu wenyewe, ni mali ya mwingine hivyo hatuna uhuru asilimia zote wa kufanya yale tunayotaka.

Kadhalika mwanamke asiye na adabu na moyo wa kiasi, huyo pia Hamchi Mungu haijalishi anahudhuria kanisani mara ngapi, au anaimba kwaya. Huyo ni wa shetani.

Hivyo mwanamke/mama/dada kama huukiri Uchaji wa Mungu kwa kufanya hayo yaliyoorodheshwa hapo juu. Huu ni wakati wako wa kukata shauri la kuokoka. Kwasababu bado ulikuwa hujaokoka kama ulikuwa unavaa vimini. Basi tubu leo na kumpokea Yesu, na ukabatizwe ufanyike kiumbe kipya, na Roho Mtakatifu atakuja juu yako kukutengeneza kama anavyotaka Mungu.

Marana atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

Mlango uitwao “Mzuri” Unaozungumziwa katika Matendo 3:2 ndio upi?

UFUNUO: Mlango wa 1

NITAONGEZAJE NGUVU ZANGU ZA ROHONI?

OLE WAO WANAOJITAHIDI KUMFICHA BWANA MASHAURI YAO.

USHIRIKINA NA MADHARA YAKE.

Je tunapaswa tushiriki Meza ya Bwana mara ngapi?

MAMBO 5 AMBAYO KILA MKRISTO ANAPASWA KUFAHAMU.

Rudi Nyumbani:

Print this post

MWANZO WA INJILI YA YESU KRISTO.

Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo. Karibu katika kujifunza maneno yale yale ya uzima ambayo yalikuwepo tangu zamani, ukweli pekee uliodumu na utakaodumu duniani kwa wakati wote.

Leo tutajifunza jambo moja katika kitabu cha Marko.. Tukisoma pale mwanzoni Inasema..

Marko 1:1 “Mwanzo wa Injili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu.

2 Kama ilivyoandikwa katika nabii Isaya, Tazama, namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso wako, Atakayeitengeneza njia yako”.

Kama tunavyoona hapo kitabu hichi cha Marko, kimeanza na utambulisho wake, ambao ni “mwanzo wa injili ya Yesu Kristo”, tofauti na kitabu kama cha Yohana, ambacho chenyewe kinaanza kwa utambulisho wa “Hapo mwanzo kulikuwa na Neno, naye Neno alikuwa kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.”.. Sasa ni vizuri tukazingatia sana tambulisho hizi za mwanzoni mwa Vitabu, kwani hiyo itatusaidia kujua maudhui ya injili nzima inaegemea wapi.

Na ndio maana ukisoma kitabu cha Yohana chote, utaona, hakijajikita katika kueleza mizunguko ya Yesu na kazi alizozifanya sana..Bali kilikuwa kimejikita kwa sehemu kubwa kumshuhudia Yesu kama Nuru ya ulimwengu. Ni kitabu kinachomzungumzia Bwana Yesu kama Neno la kweli, la Mungu kwa namna ya kipekee sana, kiasi kwamba ukikisoma katika utulivu chini ya uongozo wa Roho Mtakatifu, utajikuta unampenda Bwana zaidi na imani yako kuimarika sana.

Sasa tukirudi kwenye kitabu cha Marko nacho kinaanza kwa namna yake, kinasema “Mwanzo wa Injili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu.”..Hii ikiwa na maana kuwa  kitabu hiki kimeegemea sana katika kuizungumzia injili yake. Sasa ni lazima tujue injili hiyo ilikuwa ni ya namna gani, na alihubiri nini..Ili na sisi tujifunze misingi ya injili ya kweli inavyopaswa iwe.

Hivyo ukiendelea mbele kidogo kwenye mstari wa 14 tutaona ni nini Yesu alianza kukihubiri katika huduma yake, Tusome;

Marko 1:14 “Hata baada ya Yohana kutiwa gerezani, Yesu akaenda Galilaya, akiihubiri Habari Njema ya Mungu,

15 akisema, WAKATI UMETIMIA, na UFALME WA MUNGU UMEKARIBIA; TUBUNI, na KUIAMINI INJILI”.

Umeona, injili yake iliegemea katika  vipengele hivyo vinne.

  1. WAKATI UMETIMIA; Hii ikiwa na maana wakati wa mataifa kuokolewa umetima. Wakati uliokuwa unasubiriwa ndio umefika. Wakati wa wokovu kupatikana bure kwa kila kiumbe duniani haijalishi atakuwa ni muafrika, mzungu, mpagani, muabudu miungu. Na sisi pia tunapaswa kuhubiri kwetu tuhubiri kutimia kwa wakati huu. Ni wakati ambao mlango umefunguliwa kwa watu wote. Hivyo kila mmoja ni wajibu wake kuhakikisha neema hiyo haimpiti.
  2. UFALME WA MUNGU UMEKARIBIA: Kwamba mwisho wa kila kitu umekaribia; Dunia haitakuwa na wakati mrefu kabla ya mambo yote kuisha, Na utawala mpya wa Mungu kuanza..dalili zote zinaonyesha. Hivyo watu waelekeze macho yako sana mbinguni, kuliko kwenye mambo ya ulimwengu huu.
  3. TUBUNI: Sasa kwa kuwa wakati umetia, na ufalme wa mbinguni umekaribia sana, kilichobakia kwa mtu ni kutubu dhambi zake. Kukubali kuoshwa dhambi zake, kukubali kumgeukia muumba wake, katika wakati mchache aliobakiwa nao.
  4. NA KUIAMINI INJILI: Maana yake ni kuamini maneno yote ya uzima na kuyaishi. Kuyasikiliza mafundisho yote ya Yesu Kristo. Katika hali ya utakatifu.

Hivyo ni vipengele mama, vya injili. ili injili ikamilike ni lazima vipengele hivyo viwepo. Huko ndiko kulikuwa kuhubiri kwa Bwana wetu Yesu, na kwa namna hiyo Mungu alimthibitisha kuwa ndiye mwana wake wa pekee.

Hivyo na sisi tuende katika nyayo hizo hizo. Vilevile tujue kuwa hizi ni nyakati za mwisho Jiulize! Wewe kama wewe Je! upo ndani ya wokovu kisawasawa?. Embu chunguza maisha yako, uangalie umesimama wapi. Saa ya wokovu ni sasa na sio kesho…

Ukiwa unaichezea hii neema, ujue haitadumu siku zote juu ya maisha yako. Kuna wakati itaondoka, na ndio maana ikaitwa neema, maana yake ni kama offer tu, ambayo hukustahili wala hatukustahili, na siku zote offer huwa haidumu wakati wote, kuna kipindi itaondolewa, vivyo hivyo na neema itaondoka tu wakati Fulani ukitimia juu yako, kama hutaiamini injili, unyakuo utapita na wale wote ambao hawajampokea Yesu watabaki hapa duniani. Kama Mungu aliiondoa kwa Israeli wateule wake Israeli na kutupa sisi. Hatashindiwa kutuondolea na sisi na kuwapa wengine.

Warumi 11:17 “Lakini iwapo matawi mengine yamekatwa, na wewe mzeituni mwitu ulipandikizwa kati yao, ukawa mshirika wa shina la mzeituni na unono wake,

18 usijisifu juu ya matawi yale; au ikiwa wajisifu, si wewe ulichukuaye shina, bali ni shina likuchukualo wewe.

19 Basi utasema, Matawi yale yalikatwa kusudi ili nipandikizwe mimi.

20 Vema. Yalikatwa kwa kutokuamini kwao, na wewe wasimama kwa imani yako. Usijivune, bali uogope.

21 Kwa maana ikiwa Mungu hakuyaachia matawi ya asili, wala hatakuachia wewe”.

Hivyo tubu, ukabatizwe kama bado hujabatizwa katika ubatizo sahihi. Na Mungu atakupa Roho wake Mtakatifu.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

JE UDHAIFU WANGU UNAWEZA KUZUIA INJILI?

IVUMBUE INJILI YA KRISTO KUTOKA KATIKA KILA JAMBO.

HATARI YA KUHUBIRI INJILI TOFAUTI NA ILIYOANDIKWA KWENYE BIBLIA.

KUTOKUIHUBIRI INJILI,KUNA MADHARA GANI?

Naomba kujua nini maana ya kuteguka uvungu wa paja?

Rudi Nyumbani:

Print this post

Duara ya Ahazi ni ipi? Na je! Kivuli cha Hezekia kilirudije nyuma?

Zamani walikuwa hawana saa za mshale, au za kukonyeza kama tulizonazo sasa hivi ili kutambua majira ya siku, badala yake walitumia  njia nyingine mbalimbali zilizowasaidia kutambua saa za mchana, na njia kuu ilikuwa ni ya kukitazama kivule cha jua

Sehemu nyingine walituma kifaa kidogo maalumu ambacho kiliwekwa mahali pa wazi, ambapo jua litaweza kukipiga pande zote . Tazama picha..

duara ya muda

Sehemu nyingine zilitumika ngazi,ambazo zilijengwa pande zote, mashariki na magharibi, mwa eneo hilo la wazi, na pale jua lilipochomoza upande wa mashariki, kivuli kilichusha kwenye ngazi, na pale lilipozama upande wa magharibi kivuli kilinyanyuka, Hivyo kwa kutazama zile ngazi waliweza kutambua saa za asubuhi, mchana na jioni.. (Tazama picha juu kabisa mwanzoni mwa somo hili),.

Hivyo inawezekana duara la Ahazi lilikuwa ni la namna hii, japo biblia haijaeleza kwa marefu lakini tunaona, Hezekia, baada kuugua sana, na kuwa hatarini kufa, alimwomba Mungu kwa kumlilia amponye ugonjwa wake. Ndipo Mungu akamsikia na kumwambia kuwa atamponya, Lakini yeye akaomba Mungu ampe ishara kuwa jambo hilo litatendeka, ndipo akapewa nafasi ya kufanya uchaguzi wa upande wa kivuli hicho kitakapoangukia ndani ya   hilo duara la Ahazi baba yake Hezekia (ambaye alilijenga kwa ajili ya shughuli hiyo ya kutambua majira),..akaulizwa je! kiendelee mbele au kirudi nyuma.

Kwa kawaida jua linapokaribia kuzama, kivuli huwa kinakwenda mbele, hivyo Hezekia akaambiwa achugue je kivuli kizidi kwenda mbele zaidi, yaani akiwa na maana kama muda ule, kivuli kilikuwa kinaonyesha ni saa 8 mchana, basi kisogee mpaka kwenye saa 12 jioni.. Au achague kirudi nyuma, mpaka kwenye saa 1 asubuhi haijalishi kuwa muda huo utakuwa ni saa 8 mchana.

Ndipo Hezekia akachagua kirudishwe nyuma, kinyume cha asili, kwani kwenda mbele linaweza likawa ni jambo la kawaida..lakini kurudi nyuma inahitaji muujiza.

2Wafalme 20:8 “Hezekia akamwambia Isaya, Je! Kutakuwa na ishara gani ya kwamba Bwana ataniponya, nami siku ya tatu nitapanda nyumbani kwa Bwana.

9 Isaya akamwambia, Jambo hili litakuwa ishara kwako, itokayo kwa Bwana, ya kwamba Bwana atalifanya neno hilo alilolinena; je! Kivuli kiendelee madaraja kumi, au kirudi nyuma madaraja kumi?

10 Hezekia akajibu, Ni jambo jepesi kivuli kuendelea madaraja kumi; la, hicho kivuli na kirudi nyuma madaraja kumi.

11 Isaya nabii akamlilia Bwana; akakirudisha nyuma kile kivuli madaraja kumi, ambayo kilikuwa kimeshuka katika madaraja ya Ahazi”.

Isaya 38:7 “Jambo hili liwe ishara kwako, itokayo kwa Bwana, ya kuwa Bwana atalitimiza jambo hili alilolisema;

8 Tazama, nitakirudisha nyuma kivuli madaraja kumi, ambayo kilishuka juu ya duara ya Ahazi kwa sababu ya jua. Basi jua likarudi madaraja kumi katika hiyo duara, ambayo limekwisha kushuka”.

Tunajifunza nini?

Mungu huwa anaweza rudisha majira na nyakati, haijalishi kitakuwa kimechelewa kiasi gani, kwasababu hakuna jambo lolote linaloshindikana kwake. Aliweza kulisimamisha jua wakati wa Yoshua, jambo ambalo hata sasa linaweza kuonekana kama ni hadithi za kutunga lakini liliwezekana, aliweza kuurudisha ujana wa Ibrahimu na Sara, aliweza kuwapa uzao wakina Elizabeti na Zekaria. Hatashindwa kufanya muujiza na kwako, hata kama mambo yataonekana leo hii hayawezekani tena muda umekwenda,. Mungu anataka sisi tumwamini yeye, bila kuangalia hali zetu. Ndipo afanye.

Hivyo habari hiyo ni ya kututia moyo, tusichoke kumtumainia Mungu na kumwamini yeye, kwasababu hakuna linaloshindikana kwake.

Yeremia 32:27 “Tazama, mimi ni Bwana, Mungu wa wote wenye mwili; je! Kuna neno gumu lo lote nisiloliweza”?

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

Makanwa ni nini katika biblia? (Danieli 6:22)

SIFONGO NA SIKI NI NINI?

Shekina ni nini? Na Je! Utukufu wa shekina unamaana gani?

Jaa ni nini katika biblia?

KIFO CHA MTAKATIFU PERPETUA NA FELISTA.

Rudi Nyumbani:

Print this post

Makanwa ni nini katika biblia? (Danieli 6:22)

Neno hilo tunaweza kulisoma katika kifungu hichi;

Danieli 6:22 “Mungu wangu amemtuma malaika wake, naye ameyafumba makanwa ya simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi nalionekana kuwa sina hatia; tena, mbele yako, Ee mfalme, sikukosa neno”.

Makanwa kwa jina lingine ni midomo.

Katika habari hiyo tunaona, baada ya Danieli kushitakiwa kwa makosa ambayo hakustahili kutokana na uaminifu wake kwa Mfalme Dario, walimkamata na kumtupa katika tundu la Simba. Simba wale walikuwa ni simba wenye njaa sana, ambao waliweza wakakaa wiki kadhaa, au hata mwezi bila kuona chakula chochote, na hata chakula kikiletwa  kilikuwa ni kidogo sana cha kuweza kuwatosheleza simba wote waliokuwa katika shimo lile, kwani chakula chao kilikuwa ni  wanadamu na si wanyama, hivyo ilikuwa mpaka aonekane mwanadamu muovu, ndipo simba hao wapate chakula.

Walifanya hivyo ili kuhakikisha kuwa mtu yeyote atakayetupwa huko ataliwa bila kubakishwa kitu chochote, mpaka mifupa yao kusagwa sagwa. Na ndicho walichomfanyia Danieli wakitazamia kuwa atakapotupwa, mara moja wale simba watamrukia, na kumpasua pasua angali akiwa bado juu, lakini tunaona Mungu alimtuma malaika wake na kuwafumba MAKANWA yao, (yaani midomo yao) wale simba.,..

Badala yake wao walipotupwa, biblia inatuambia simba wale walipokea angali wakiwa bado juu,(Danieli 6:24)

Je! Tunapata somo gani katika jambo hilo?

Mungu akifumba kinywa cha mlaji, hata kama ana njaa nyingi kwako, hawezi kula kilicho cha kwako..

Walaji sio simba tu, Mungu analo jeshi lingine la walaji, ambalo amelifananisha  ni tununu, nzige , parare na madumadu.. (Soma Yoeli 1:4) . Hawa wanaweza kuwa ni taifa, au jamii ya watu, au viongozi n.k. ambao Mungu anaweza kuwatumia kufunua makanwa yao kwako, wakakuharibu  kote kote bila kukuachia kitu, kama wewe si mtu wa haki, au ni mtenda dhambi. Utaona Mungu aliyaruhusu mataifa mbalimbali yaipige Israeli, na mengine kuwachukua utumwani kwa makosa yao tu ya kumwasi Mungu, ikapelekea makanwa ya wanadamu na mataifa kufunuliwa juu yao.

Na pia biblia inatuonyesha yapo mapepo ambayo yataachiliwa katika siku za mwisho yaliyofananishwa na nzige. Na hiyo itakuwa baada ya unyakuo kupita, na kazi yao itakuwa ni kuwauma wanadamu wote  ambao watakuwa hawana muhuri wa Mungu, juu ya vipaji vya nyuso zao.(Ufunuo 7:3). Kwa maelezo marefu juu ya habari hiyo fungua hapa>>> JINA LAKE KWA KIEBRANIA NI ABADONI,

Hata sasa, ibilisi anafunua makanwa yake na kuwameza , na kuwatafuna watu wengi pasipo wao kujua, biblia inasema….

1Petro 5:8 “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze”.

Lakini walio na muhuri wa Mungu (yaani Roho Mtakatifu) kama vile Danieli, Mungu anawaepusha nao. Swali ni je wewe nawe umetiwa muhuri huu wa Mungu?(Waefeso 4:30). Kumbuka  Roho Mtakatifu hawezi kuja juu ya mtu ikiwa mtu huyo, hajatubu dhambi zake kwa kumaanisha kabisa kuziacha, na kubatizwa.

Hivyo ikiwa leo hii utapenda kumkaribisha Yesu ndani ya maisha yako au kubatizwa, basi fungua hapa kwa ajili ya kupata maelekezo ya sala ya Toba.>>>  SALA YA TOBA

Ubarikiwe.Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

DANIELI: Mlango wa 1

OLE WAKO KORAZINI NA BETHSAIDA.

UTAWALA WA MIAKA 1000.

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 10 (Kitabu cha Zaburi).

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita..

Rudi Nyumbani:

Print this post

OLE WAKO KORAZINI NA BETHSAIDA.

Korazini na Bethsaida ilikuwa ni miji iliyokuwepo kandokando ya bahari ya Galilaya.. Sasa Bahari ya Galalilaya, iliitwa hivyo bahari lakini kiuhalisia sio bahari bali ni ziwa, kwasababu bahari ni lazima iwe na maji ya chumvi, lakini Hili la Galilaya lilikuwa na maji yasiyo chumvi (yaani maji barini), hivyo lilikuwa ni ziwa mfano wa Ziwa Victoria, isipokuwa halikuwa kubwa kama ziwa Victoria, Ziwa hilo la Galilaya mpaka leo lipo huko kaskazini mwa Israeli.

Sasa kando ya hilo ziwa la Galilaya (au Bahari ya Galilaya) kulikuwepo na miji maarufu mitatu, ambayo ni Korazini, Bethsaida na Kapernaumu. Miji hiyo kwamfano mrahisi tuseme Mji wa Mwanza, Mara na Kagera, iliyoizunguka ziwa Victoria, na ndio hivyo hivyo miji hiyo mitatu ilikuwa imeizunguka hiyo bahari ya Galilaya.

Sasa kipindi ambacho Bwana Yesu yupo duniani, sehemu za kwanza kwanza kabisa kuhubiri injili zilikuwa ni katika hiyo miji mitatu kwasababu haikuwa mbali sana na mji wa Nazareti aliokulia Bwana Yesu. Hivyo miji hii mitatu ilipata neema isiyokuwa ya kawaida kuona miujiza mikubwa. Tofauti na miji mingine yoyote ya Israeli kama Yerusalemu na Bethania au Samaria. Hivyo kwa miujiza iliyoiona ilitegemewa iwe ndio miji ya kwanza kutubu na kumkubali Mwokozi, lakini ilikuwa kinyume chake…Ndipo Bwana Yesu akaiambia siku moja maneno haya…

Mathayo 11:20  “Ndipo akaanza kuikemea miji ile ambamo ndani yake ilifanyika miujiza yake iliyo mingi, kwa sababu haikutubu.

21  Ole wako, Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu zamani kwa kuvaa magunia na majivu.

22  Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi Tiro na Sidoni kustahimili adhabu zao siku ya hukumu kuliko ninyi.

23  Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa mpaka mbinguni? Utashushwa mpaka kuzimu; kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika katika Sodoma, ungalikuwapo mji huo hata leo.

24  Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma kustahimili adhabu yake siku ya hukumu kuliko wewe”.

Maandiko hayo yanatuonyesha kuwa japokuwa watu wa Sodoma na Gomora walihukumiwa kwa adhabu ya moto, na kuchomeka kikatili, kutokana na dhambi zao, lakini kumbe bado haitoshi, wataendelea tena kuadhibiwa baadaye.

Hiyo inaogopesha sana, kama uliwahi kuona picha za ajali ya watu walioungua kwa moto, huwezi kufikiri kwamba watu kama hao wanaweza tena kwenda kuadhibiwa huko wanakokwenda…Lakini biblia inatufundisha kuwa watenda dhambi hata wakifa hapa kwa kuadhibiwa na Mungu, huko wanakokwenda watakutana na adhabu iliyo kubwa kuliko hiyo walioadhibiwa hapa..Ndicho Bwana Yesu alichokisema hapo kwenye huo mstari wa 24.

“Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma kustahimili adhabu yake siku ya hukumu kuliko wewe”.

Maana yake watu wa Sodoma, wataendelea kuadhibiwa..na sasa wapo kuzimu wanateseka, na siku ile ya Mwisho katika hukumu ya kiti cheupe cha enzi cha mwanakondoo, watahukumiwa na kutupwa kwenye ziwa la moto lenye mateso mara nyingi zaidi.

Lakini, Bwana Yesu anazidi kusema… “itakuwa heri kwa watu wa Sodoma kustahimili adhabu siku ile kuliko wewe”. Yaani hiyo miji ambayo ilihubiriwa na kuona miujiza mingi lakini haikutubu.

Hiyo inatupa picha nyingine kuwa, katika ziwa la moto, viwango vya kuadhibiwa vitatofautiana…wapo watakaoteseka sana kuliko wengine… Shetani hawezi kuteswa sawa na mzinzi, wala nabii wa uongo hawezi kuteswa sawa na kahaba..viwango vitatofautiana.

Lakini hapo Bwana anasema adhabu ya wale ambao hawatatubu, baada ya kuona miujiza mingi ya ki-Mungu ikitendeka..hao Bwana anasema dhambi yao ni kubwa kuliko ya watu wa Sodoma na Gomora, hivyo watahukumiwa zaidi kuliko watu wa Sodoma na Gomora,.

Hii ni tafakari fupi tu ya leo, ambayo ningependa tuitafakari pamoja leo. Na kujua kuwa miujiza Roho Mtakatifu anayoifanya kwenye maisha yetu, tunayoina kila mahali, sio kwa lengo la kutuburudisha, bali ni kwa lengo la kulihakikisha Neno lake kuwa ni kweli. Hivyo ni wajibu wetu kutubu na kujitakasa sana. Na kama bado Yesu yupo nje ya maisha yetu, huu ndio wakati wa kumkaribisha ili tusiangukie mikononi mwa hukumu ya Mungu.

Kwasababu ni dhahiri kuwa sisi tunaoishi sasa tunaona miujiza mikubwa ya Bwana Yesu kuliko wale watu wa kanisa la kwanza, Mpaka tunaizoelea. Kristo atusaidie tuchue hatua sahihi.

Bwana atubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312 / 0693036618.

Jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

MADHARA YA KUTAFUTA ISHARA.

CHUKI ULIZO NAZO KWA MAADUI ZAKO, SIZO ALIZONAZO MUNGU JUU YAO.

Yuko azuiaye sasa hata atakapoondolewa! ni nani huyo?

Nguo za magunia katika biblia ni zipi?

Wevi na wanyanga’anyi waliomtangulia Yesu walikuwa ni wapi?

Rudi Nyumbani:

Print this post

Mungu anaposema “nitaliweka jina langu” ana maana gani?

SWALI: Kwanini kila mahali Mungu anasema, “mahali Fulani nitaliweka jina langu au nimeliweka jina langu”, Je ana maana gani kusema hivyo, ni kwamba lile jina lake la YEHOVA, anakuwa analiweka ndani ya  sehemu hizo au?


JIBU: Mahali popote Mungu anaposema nitaliweka jina langu, anamaanisha kuwa sehemu hiyo, au kitu hicho amekichagua, au amekiweka wakfu kitumiwe kwa ajili ya aidha kumtangaza yeye , au kuwambudu, au kumfanyia ibada, n.k. hakuna cha zaida.

Hivyo sehemu yoyote au kitu chochote, au mtu yoyote aliyewekwa wakfu na Mungu (au ametiwa mafuta ya utumishi), basi ujue  kuwa tayari mtu huyo au kitu hicho Mungu kashakiwekea jina lake ndani yake. Na mtu huyo, au kitu hicho kinapaswa kichukuliwe kwa umakini sana, kwasababu kikighafilikishwa, aidha na mtu mwenyewe, au mtu mwingine ni rahisi kupata adhabu kali sana kutoka kwa Mungu.

* Kwa mfano katika biblia utaona Mungu aliweka jina lake ndani ya malaika wake kwa kusudi la kuwahudumia wana wa Israeli, na hichi ndicho alichowaambia wakiwa kule jangwani;

Kutoka 23:20 “Tazama, mimi namtuma malaika aende mbele yako, ili akulinde njiani na kukupeleka mpaka mahali pale nilipokutengezea.

21 Jitunzeni mbele yake, mwisikize sauti yake; wala msimtie kasirani; maana, hatawasamehe makosa yenu; KWA KUWA JINA LANGU LIMO NDANI YAKE”.

* Utaona tena Mungu aliliweka jina lake pia juu ya wana wote wa Israeli,. Yaani waisraeli wote walikuwa ni  wakfu kwa Mungu kati ya mataifa yote ulimwenguni. Hivyo mtu yeyote au taifa lolote ambalo liliwakosesha, au kuwafadhaisha, lilishiriki adhabu kali kutoka kwa Mungu.

Hesabu 6:27 “Ndivyo watakavyoweka jina langu juu ya wana wa Israeli; nami nitawabarikia”.

Mtu yeyote aliyeilaani Israeli, Mungu alimlaani, na yeyote aliyeibariki Mungu alimbariki, kwasababu Mungu aliliweka jina lake juu yao. Hata sasa Baraka hizi na laana zinaendelea kwa yeyote atakayeitakia heri au shari Israeli.

* Utaona tena Mungu aliliweka jina lake, katika lile Hekalu lililojengwa na Mfalme Sulemani pale Yerusalemu.

2Wafalme 21:4 “Akazijenga madhabahu ndani ya nyumba ya Bwana, napo ndipo alipopanena Bwana, Katika Yerusalemu nitaliweka jina langu”.

Hivyo, wote ambao walikuwa wanalinajisi hekalu la Mungu, mauti au adhabu kali walikumbana navyo.

Lakini wakati mwingine Mungu aliahirisha hasira yake juu ya wana wa Israeli, sio kwasababu walimpendeza sana, hapana lakini ni kwasababu tu alishaliweka jina lake ndani yao. Soma vifungu hivi, utaliona hilo, Ezekieli 36:21, Isaya 48:9-12, Ezekieli 20:9-10,

Vivyo hivyo na katika agano jipya, Mungu ameweka jina lake katika vitu kikuu viwili.

Cha kwanza ni Kanisa lake; Palipo na Kanisa hai la Kristo ujue jina la Mungu lipo mahali hapo. Lile ni hekalu la Mungu. Ambapo Mungu amepaweka pawe wafku kwa ajili ya ibada, sala na dua, na shukrani, sasa ikitokea mtu analinajisi kanisa la Kristo, kwa namna yoyote ile, ajue kuwa anashindana na mkono wa Mungu wenyewe, na bila shaka yoyote, atakuwa matatizoni.

Pili, ni Mungu analiweka jina lake ndani ya mwaminio. Yaani ndani mtu aliyeokoka. Mtu aliyeokoka, moja kwa moja anapokea kibali cha Mungu kuja ndani yake, kwa yule Roho Mtakatifu anayeachiliwa juu yake. Hivyo mtu wa namna hiyo anakuwa ni wakfu kwa Mungu, chombo kiteule cha Mungu. Na mtu yeyote akitajiribu kumfadhaisha, atakuwa anajitafutia madhara mwenyewe kutoka kwa Mungu. Kwasababu tayari Mungu alishaliweka jina lake ndani yake.

Na mtu anaokoka, kwanza kwa kutubu, kwa kumaanisha kabisa kuziacha dhambi zake, na pili, kwa kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi, na kwa jina la Yesu Kristo sawasawa na Matendo 2:38

Akishakamilisha hayo, Roho Mtakatifu atakuja juu yake, na kuanzia huo wakati, jina la Mungu litakuwa limeshawekwa ndani yake. Na yeye atakuwa mtiwa mafuta wa Bwana.

Je, na wewe upo tayari leo kuokoka? Kama jibu ni ndio basi fungua hapa, kwa ajili ya kupata maelekezo ya namna ya kutubu. >>>> SALA YA TOBA

Bwana akakubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312 / 0693036618.

Jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

Hayawani ni nini katika biblia?

Je ni wanyang’anyi wawili waliomtukana Bwana Yesu au mmoja?

Shekina ni nini? Na Je! Utukufu wa shekina unamaana gani?

Baadhi ya watu  na misemo ambayo haipo katika biblia.

JINA LA MUNGU NI LIPI?

Rudi Nyumbani:

Print this post

Hayawani ni nini katika biblia?

Mwanzo 3:14 “Bwana Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako”

Hayawani ni wanyama wa mwituni, ambao sio wa kufugwa…Wanyama wa kufungwa ni kama Kondoo, Mbuzi, Ng’ombe, Ngamia, punda n.k. Hawa wameumbwa mahususi kuishi na wanadamu, na kunyenyekea chini ya mikono ya wanadamu. Lakini wanyama wengine wote ambao kamwe hawewezi kujinyenyekeza chini ya uongozo wa wanadamu, na hivyo hawaishi na wanadamu bali mwituni kama simba, chui, nyati, fisi, mbwa-mwitu n.k Hao ndio wanaoitwa hayawani, ni wanyama wasiofugika.

Kwamfano Swala ni kama mbuzi tu, lakini huwezi kumfuga, kwanza akikuona atakimbia…kadhalika Nyati, ni kama ng’ombe tu, lakini huwezi kumfuga na kumtumikisha kama ng’ombe akikuona atatatufa kukudhuru, badala ya kukutii. Kama biblia inavyosema..

Ayubu 39: 9 “Je! Nyati atakubali kukutumikia? Au atakaa katika zizi lako?

10 Je! Waweza kumfunga nyati kwa kamba matutani? Au, yeye atayalima mabonde nyuma yako?

11 Je! Utamtumaini kwa sababu ana nguvu nyingi? Au, utamwachia yeye kazi yako?

12 Je! Utamtumaini kwamba ataileta mbegu yako nyumbani. Na kukusanya nafaka ya kiwanja chako cha kupuria?”.

Baadhi ya mistari katika biblia inayozungumzia juu ya hayawani ni pamoja Mwanzo 3:14, Mwanzo 31:39, Ayubu 35:11, Zaburi 50:10, Isaya 13:21, Isaya 23:13 n.k.

Lakini pia biblia imewafananisha Maadui wa Injili kama Hayawani wa mwituni. Maadui wa Injili ni pamoja na manabii wote wa uongo na waalimu wote wa uongo, ni pamoja na watu wote wanaoipinga injili ya msalaba. Wale Bwana Yesu aliosema katika Mathayo  7:15.

Mathayo  7:15 “Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali”.

Hivyo manabii wote wa uongo ni hayawani ambao kazi yao kubwa ni kuingia katikati ya kundi la kulidhuru, hawa hawafugiki chini ya zizi la Mchungaji mkuu Yesu Kristo, ni wanyama wa mwituni katika roho, sio miongoni mwa kondoo wake.

1Wakorintho 15: 32 “Ikiwa, kwa jinsi ya kibinadamu, nalipigana na hayawani wakali kule Efeso….”.

Hali kadhalika, mtu yeyote ambaye kwa nje anaonekana ni mkristo, lakini kwa siri ni mtu anayefanya uchafu, biblia inasema huyo naye ni hayawani..

Tito 1:12  “Mtu wa kwao, nabii wao wenyewe, amesema, Wakrete ni waongo siku zote, HAYAWANİ WABAYA, walafi wavivu”.

Hivyo tujitahiti tusiwe wanyama wasiofugiga (hayawani) bali tuwe miongoni mwa kondoo wa Yesu. Na pia tujihadhari na hayawani wote wanaojigueza na kuwa mfano mfano wa kondoo wa Yesu, biblia imesema tutawatambua kwa Matunda yao.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312 / 0693036618.

Jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

TABIA YAKO NI YA MNYAMA GANI?

CHAPA YA MNYAMA

Roho za Wanyama zinakwenda wapi baada ya kifo? Je! Watafufuliwa?

FAHAMU MAJIRA ULIYOPO NA NINI UNAPASWA UWE NACHO.

KWANINI AWE PUNDA NA SI MNYAMA MWINGINE?

Rudi Nyumbani:

Print this post

Je ni wanyang’anyi wawili waliomtukana Bwana Yesu au mmoja?

SWALI: Kitabu cha Mathayo 27:44 na Marko 15:32b inazungumzia wale wanyang’anyi walioteswa pamoja na Yesu kuwa wote wawili walimtukana Yesu pia, ila tukisoma Luka 23:39 inasema ni mmoja ndiye alimtukana sasa kwanini inakuwa hivyo naomba unisaidie nielewe?.

JIBU: Tuvipitie vifungu vyenyewe;

Mathayo 27:44 “Pia wale wanyang’anyi waliosulibiwa pamoja naye walimshutumu vile vile.

Marko 15:32 Kristo, mfalme wa Israeli, na ashuke sasa msalabani tupate kuona na kuamini. Hata wale waliosulibiwa pamoja naye wakamfyolea.

Luka 23:39 “Na mmoja wa wale wahalifu waliotungikwa alimtukana, akisema, Je! Wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi.

40 Lakini yule wa pili akamjibu akamkemea, akisema, Wewe humwogopi hata Mungu, nawe u katika hukumu iyo hiyo?

41 Nayo ni haki kwetu sisi, kwa kuwa tunapokea malipo tuliyostahili kwa matendo yetu; bali huyu hakutenda lo lote lisilofaa.

42 Kisha akasema, Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako.

43 Yesu akamwambia, Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi”.

JIBU: Ukisoma juu juu ni rahisi kusema maandiko yanajichanganya, lakini hakuna kinachojichanganya isipokuwa ni sisi wenyewe tunakosa shabaha ya kuyaelewa maandiko.

Habari hii inafanana na ile, ya wale watu wawili ambao Yesu alikutana nao kule makaburini wenye pepo, ukisoma pale utaona injili moja inaonyesha Bwana alikutana na vichaa wawili, wakati injili nyingine inaonyesha alikutana ni kichaa mmoja, Sasa habari hizo sio kwamba zinajichanganya, hivyo Ili kupata ufafanuzi wake basi fungua hapa >>> Wenye pepo

Sasa tukirudi kwenye habari hiyo tunaona Injili ya Mathayo na Marko inaonyesha kuwa wale wahalifu wawili walimdhihaki  Bwana Yesu akiwa pale msalabani, bila upingamizi wowote . Lakini Injili ya Luka inaonyesha mmoja ndiye aliyemtukana lakini yule mwingine alimwomba rehema.

Kabla hatujalijibu swali, Tukumbuke kuwa Bwana Yesu alikuwa pale msalabani kwa muda mrefu sana usiopungua masaa 6, na wakati huo wote, wale wahalifu waliosulibiwa naye walikuwa wanautazama mwitikio wake, alipokuwa katika hali kama ya kwao, ni wazi kuwa  mwanzoni wote walidhani Yesu ni kama mmojawapo wa wahalifu wenzao, na hiyo haikuwa shida wote kutoa kauli za kudhihaki na kukebehi na ndio maana injili ya Mathayo na Marko zinaonyesha kuwa wote walimkebehi..

Lakini ni wazi kuwa baadaye kidogo yule mmoja alitubu, akageuka, na hiyo ni  pengine baada ya kuona utofauti wa Yesu na matendo aliyokuwa anayaonyesha  pale msalabani, alipoona aliposhutumiwa hakurudisha majibu, alipoona anawaombea msamaha, akisema Baba wasamehe kwa kuwa hawajui watendalo, pengine hilo lilimgusa sana, alipoona upendo wake wa kipekee, japokuwa alikuwa matesoni..Hilo ndilo lililomfanya yule muhalifu mmoja ageuze mtazamo wake na kujua kabisa Kristo hakuwa na kosa lolote..

Na zaidi ya yote  alipoona mpaka giza limeingia mchana kweupe, jambo ambalo si la kawaida.. Alitubu saa ile ile na mpaka kumwambia yule wenzake sisi ni kweli tumekosea, lakini huyu hakufanya kosa lolote linalomstahili yeye kuuawa. Ee Yesu unikumbuke katika ufalme wako.

Ni kitu gani tunajifunza?

Hiyo inatuonyesha uvumilivu wa Mungu jinsi ulivyo kwa wenye dhambi. Hata wewe mwenye dhambi Inawezekana  umekuwa ukimdhihaki Mungu mara nyingi, ukizipuuzia njia zake na kuziona ni za watu waliorukwa na akili mara nyingi, hata umefikia hatua ya kuutukana wokovu waziwazi na Mungu mwenyewe., lakini bado Mungu anakupa nafasi ya kutubu leo. Lakini nafasi hiyo haitadumu milele. Kumbuka wahalifu wale wote walikufa baada ya muda mfupi, lakini mpaka sasa tunaongea mmoja yupo peponi mwingine yupo motoni.

Yule aliye motoni alipuuzia wokovu mpaka dakika ya mwisho hakujua kuwa hana muda mrefu wa kuishi. Swali ni Je! Wewe pia unatambua muda uliobakiwa nao hapa duniani? Kama hufahamu ni kwanini basi bado upo kwenye dhambi? Hivyo tubu leo Yesu akuokoe akuoshe dhambi zako, ufanyike mtoto wake kweli kweli. Hizi ni nyakati za mwisho. Majira haya ni ya kumalizia. Hivyo usiruhusu, dhambi iendelee kuwa sehemu ya maisha yako.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312 / 0693036618.

Jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

Je! ile habari ya watu wawili wenye pepo inajichanganya?

Wevi na wanyanga’anyi waliomtangulia Yesu walikuwa ni wapi?

TAZAMA, NASIMAMA MLANGONI.

USIIGEUZE NYUMBA YA MUNGU KUWA PANGO LA WANYANG’ANYI.

UFUNUO: Mlango wa 11

Rudi Nyumbani:

Print this post

Shekina ni nini? Na Je! Utukufu wa shekina unamaana gani?

Shekina au Shekhinah / schechinah, Ni neno la kiyahudi linalomaanisha, “kutua” au “kuweka makao” au “makazi” ya uwepo wa Mungu duniani. Hivyo utukufu wa Shekina maana yake ni kujifunua kwa uwepo wa Mungu kwa dhahiri duniani, ambapo kuonekana kwake kunaweza kuchukua mfumo wa vitu mbalimbali vya asili , kama vile moto, wingu,moshi,mwanga, kijiti kinachoteketea n.k.,..

Neno hili huwezi kulikuta kwenye biblia, lakini maudhui yake ipo ndani ya biblia. Ni neno lililoanzishwa,  na waalimu wa kiyahudi , (Marabi) , na yalionekana  kwenye fasihi zao na maandishi yao ya kale, kipindi cha pale katikati kutoka agano la kale kuelekea agano jipya..

  • Mara ya kwanza utukufu wa Shekina kuonekana ilikuwa ni siku ile wana wa Israeli walipokuwa wanatoka Misri, kuelekea Jangwani walipokuwa pale Sukothi, siku hiyo ndio ilikuwa mara yao ya kwanza kuuona uwepo wa  Mungu dhahiri katika wingu na nguzo ya moto,

Kutoka 13:20 “Nao wakasafiri kutoka Sukothi, wakapiga kambi Ethamu, kwenye mpaka wa ile jangwa.

21 Bwana naye akawatangulia mchana ndani ya wingu mfano wa nguzo, ili awaongoze njia; na usiku, ndani ya moto mfano wa nguzo, ili kuwapa nuru; wapate kusafiri mchana na usiku;

22 ile nguzo ya wingu haikuondoka mchana, wala ile nguzo ya moto haikuondoka usiku, mbele ya hao watu”.

  • Ulikuja kuonekana tena ndani ya hema ya kukutania, kule jangwani;  Soma (Walawi 16:2, 1Wafalme 8:10-11)
  • Ulikuja kuonekana tena Hekaluni, kipindi kile ambacho Sulemani analiweka wakfu hekalu la Bwana (1Wafalme 8:10-11)
  • Ulionekana tena siku ile Mungu alipomthibitishia Ibrahimu agano lake alipokuwa amelala, na moto ukashuja juu ya madhabahu,aliyokuwa ameitengeneza, Mwanzo 15:17
  • Ulionekana pia kwa Ayubu wakati ule Mungu alipomtokea katika upepo wa kisulisuli na kuzungumza naye dhahiri (Ayubu 38-42)
  • Katika agano jipya tunaona ulionekana kwa Paulo siku ile alipokuwa anatoka Yerusalemu na kuelekea Dameski ili kuliharibu kanisa la Mungu, ndipo utukufu wa Mungu ukamtokea katika mwanga mkali na Kristo kuongea naye.. Matendo 9:3
  • Na utaonekana pia katika ile Yerusalemu mpya ambayo  tunayoingojea huko mbeleni (Ufunuo 21:23-)

Nakadhalika, na Kadhalika..

JE! NA SISI TUNAWEZA KUKUTANA NA UTUKUFU WA SHEKINA?

Pamoja na kwamba Mungu alijifunua dhahiri katika vitu vingi vya asili, kwa watu wachache, lakini kuna wakati ambao aliuweka mahususi kwa ajili ya kujifunua kwa watu wote, katika viwango vya juu kabisa vya utukufu wake ambao havijawahi kutokea hapa duniani.. Utukufu ambao ni zaidi ya wingu, au nguzo ya moto, au moshi, au tufani..na huo sio mwingine zaidi ya mwili wa Mwanadamu, ulioitwa YESU KRISTO. Biblia inatuambia kabisa kuwa Yesu alikuwa ni Mungu mwenyewe aliyechukua umbo la kibinadamu na kuishi na sisi (1Timotheo 3:16)

Na yeye ndiye utukufu pekee wa Mungu ambao  alishawahi kufunua hapa duniani tangu dunia iumbwe..

Yohana 1:14 “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli”.

Soma tena..

Wakolosai 2:9 “Maana katika yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili”.

Hivyo kwa kifupi tunaweza kusema utukufu wa shekina tulionao sasa ni YESU KRISTO. Na kila mmoja wetu ameweza kumwona Mungu zaidi hata ya wale waliotokewa katika nguzo ya moto, ikiwa tu atakubali kuingia katika neema yake..

Swali ni Je! Utukufu huo umefunuliwa ndani yako? Je Umempokea Yesu katika maisha yako?. Kumbuka hakuna njia yoyote utakayoweza kumfikia Mungu, au hata kumjua Mungu isipokuwa kwa njia ya Yesu Kristo. Jiulize, ulimwengu umekuahidia nini tangu umeanza kuutumikia? Ukweli ni kwamba haujakupa ahadi yoyote, ya kuendelea kuishi, Lakini Kristo anakuahidia uzima wa milele baada ya kufa, kwanini usichague uzima, na mengine mengi?

Kama upo tayari leo hii kuyakabidhi maisha yako kwa Yesu, ili utukufu huu halisi wa Shekina ukujue juu yako, basi huo ni uamuzi wa busara sana kwako. Ikiwa jibu ni ndio, basi fungua hapa kwa ajili ya kuongozwa sala ya Toba na kupokea maagizo mengine.>>>  SALA YA TOBA

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312/ +255 693036618.

Jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

JINA LA MUNGU NI LIPI?

VIGEZO VYA KUWA KARIBU NA YESU KRISTO KATIKA ULIMWENGU UJAO.

LIPO LA KUJIFUNZA KWA WALE MASHUJAA 37 WA DAUDI.

TUMEPEWA AMRI YA KUKANYAGA NGE NA NYOKA.

CHUKIZO LA UHARIBIFU

MZAZI, JALI MAISHA YA KIROHO YA MTOTO WAKO.

Rudi Nyumbani:

Print this post

LIPO LA KUJIFUNZA KWA WALE MASHUJAA 37 WA DAUDI.

Kama vile Daudi alivyokuwa shujaa, vivyo hivyo yeye naye alikuwa na mashujaa wake wengine 37 waliokuwa chini yake wakimzunguka wakati wote,walipokuwa vitani kushindana na maadui zao .

Kwa ufupi mashujaa hao waligawanyika katika makundi makuu matatu (3), Kundi la kwanza lilikuwa na mashujaa watatu wa juu, kundi la pili lilikuwa na mashujaa wawili, na kundi la tatu lilikuwa na mashujaa wengine thelathini na mbili.

Hilo kundi la kwanza la juu lenye mashujaa watatu,.mtu wa kwanza aliitwa Yashobeamu Mhakmoni, mwingine ni Eleazari na wa mwisho ni Shama.. Hawa walikuwa mashujaa kweli kweli, na kundi la chini yake kidogo alikuwepo mtu mmoja aliyeitwa Abishai na mwingine ni Benaya, hawa nao walikuwa ni mashujaa sana, halafu lile kundi la mwisho, ndio alikuwepo Uria Mhiti, na wengine, yule ambaye Daudi alimtamani mke wake, hivyo akamweka kwenye vita vikali ili auwe kisha amchukue mke wake.. Huyu alikuwa mmojawapo wa wale wengine..

Sasa embu tuwatazame baadhi ya matendo ya mashujaa hawa kwa ufupi mambo waliyoyafanya, kisha mwishoni tutapata somo la kujifunza..

1) Yashobeamu Mhakmoni:

Huyu ndio Yule shujaa wa juu zaidi ya wote, katika vita alifanikiwa kuwaua wanajeshi 800 kwa mkuki wake mmoja, Jaribu kutengeneza picha mtu mmoja anaua watu 800, huyo ni shujaa kweli kweli mfano wa Samsoni,(2Samweli 23:8)

2) Eleazari, mwana wa Dodai.

Huyu naye alifanya mambo ya kustaajabisha, walipokuwa wamekusanyika ili kupigana na wafilisti kule kondeni, Israeli wote wakakimbia akabaki yeye peke yake na Daudi tu, lakini alinyanyuka na kuwapiga wafilisti, wengi kiasi kwamba hadi mkono wake ukachoka kuua, hata alipojaribu kuuachia upanga mkono wake bado umeshikamana na upanga, tu, (1Nyakati 11:12)

2Samweli 23:9 Na baada yake kulikuwa na Eleazari, mwana wa Dodai, Mwahohi, mmojawapo wa wale mashujaa watatu waliokuwa pamoja na Daudi; walipowatukana Wafilisti waliokuwa wamekusanyika huko ili kupigana, na watu wa Israeli walikuwa wamekwenda zao;

10 huyo aliinuka, akawapiga Wafilisti hata mkono wake ukachoka, na mkono wake ukaambatana na upanga; naye Bwana akafanya wokovu mkuu siku ile; nao watu wakarudi nyuma yake ili kuteka nyara tu.

3) Shama, mwana wa Agee.

Huyu naye alikuwa kwenye mashamba ya midengu pamoja na waisraeli wengine, lakini wafilisti walipotokea wakakimbia, akabaki yeye tu peke yake kondeni, akapigana na wafilisti wengi sana akawaua yeye peke yake, hivyo akafanikiwa kulilinda lile shamba la midengu lisichukuliwe na wafilisti.(2Samweli 23:11-12)

  1. Mwingine aliitwa Abishai, nduguye Yoabu,

Aliwaua kwa wakati mmoja watu 300 kwa mkuki wake,(2Samweli 23:18)

II. Benaya, mwana wa Yehoyada:

Aliwaua majitu mawili wa Kimoabu, pia alimuua simba katikati ya pango, vilevile alimuua Mmisri ambaye alikuwa mrefu sana mfano wa Goliathi, kwa kutumia silaha ya adui yake.

2Samweli 23:20…..”aliwaua simba wakali wawili wa Moabu, pia akashuka akamwua simba katikati ya shimo wakati wa theruji.

21 huyo naye akamwua Mmisri, mtu mrefu; naye huyo Mmisri alikuwa na mkuki mkononi; lakini yeye alimshukia na gongo, akamnyakulia Mmisri mkuki mkononi mwake, akamwua kwa mkuki wake mwenyewe”.

III. Mwingine ni Elhanani ambaye alimwangusha Goliathi, mfano wa yule aliyeangushwa na Daudi.

2Samweli 21:19 “Kulikuwa na vita tena na Wafilisti huko Gobu; na Elhanani, mwana wa Yairi, Mbethlehemi, alimwua Goliathi, Mgiti, ambaye mti wa mkuki wake ulikuwa kama mti wa mfumaji.

20 Kulikuwa na vita tena huko Gathi; ambako kulikuwa na mtu mrefu sana, mwenye vidole sita katika kila mkono, na vidole sita katika kila mguu, jumla yake ishirini na vinne; yeye naye alizaliwa kwa Mrefai.

21 Naye huyo alipowatukana Israeli, ndipo Yonathani, mwana wa Shama, nduguye Daudi, akamwua.

22 Hao wanne walizaliwa kwake huyo Mrefai wa Gathi; wakaanguka kwa mkono wa Daudi, na kwa mikono ya watumishi wake.

IV. Na mashujaa wengine ambao walifanya matendo ya kishujaa unaweza kuwasoma katika..2Samweli 23:14-17..

Lakini tunavyousoma ushujaa wao watu hawa, tunaweza kujiuliza Daudi aliwatolea wapi? Je aliwaiba katikati ya jeshi la Sauli?, au alienda kuwatafuta miongoni mwa watu waliokuwa na nguvu sana Israeli? Jibu ni la!

Mashujaa hawa 37, Daudi aliokuwa nao, hakuwatoa katikati ya kambi za kivita, bali walikuwa ni watu wa kawaida sana wasiokuwa na uelekeo wowote wa ki maisha, watu hohe-hahe tu, watu waliokuwa katika umaskini, wenye dhiki nyingi, wenye madeni, watu dhaifu, watu wasio na raha moyoni, ndio waliokusanyika wakawa pamoja na Daudi, na kati ya hao ndio likanyanyuka wimbi kubwa la mashujaa namna ile ambao waliogopeka na majeshi makubwa yaliyokuwepo wakati ule.

1Samweli 22:1 “Basi Daudi akaondoka huko, akakimbilia pango la Adulamu; na ndugu zake na watu wote wa mbari ya baba yake waliposikia habari hiyo, wakamwendea huko.

2 Na kila mtu aliyekuwa katika hali ya dhiki, na kila mtu aliyekuwa na deni, na watu wote wenye uchungu mioyoni mwao, wakakusanyika kwake; naye akawa jemadari wao; nao waliokuwa pamoja naye walipata kama watu mia nne”.

Sasa Daudi ni mfano wa Kristo, hata sasa Bwana anao mashujaa wake wa Injili, na bado anaendelea kuwatafuta, lakini maandiko yanatuambia mashujaa hao hawatafuti katikati ya watu wenye vyeo, watu matajiri, watu wenye ujuzi mwingi, badala yake anawatafuta katikati ya watu wasiokuwa na uelekeo wowote, watu wa kawaida sana…

1Wakoritho 1:26 “Maana, ndugu zangu, angalieni mwito wenu, ya kwamba si wengi wenye hekima ya mwilini, si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa;

27 bali Mungu aliyachagua mambo mapumbavu ya dunia awaaibishe wenye hekima; tena Mungu alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu;

28 tena Mungu alivichagua vitu vinyonge vya dunia na vilivyodharauliwa, naam, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko;

29 mwenye mwili awaye yote asije akajisifu mbele za Mungu”.

Unaona, hivyo ndugu.. Mimi na wewe tunayo nafasi sana kubwa ya kuwa mashujaa wa Kristo ikiwa tu tutakubali kuambatana naye, hilo tu, umaskini wako sio kigezo, madeni yako sio sababu, dhiki zako sio sababu za wewe kutokuwa shujaa wa Bwana. Usije ukasema ooh! Mimi nilikuwa sina pesa ndio maana nikashindwa kukutumikia..Siku ile mashujaa kama hao watatuhukumu.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312 / 0693036618.

Jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

Rudi Nyumbani:

Print this post