“Jaa” ni nini katika biblia?
Jaa ni mahali ambapo uchafu unalundikwa, na uchafu huo unaweza kuwa ni kinyesi cha wanyama (yaani mbolea), au uchafu unaotokana na shughuli za kibinadamu (matakataka). Hivyo Jaa ni kama kifupi cha jalala tu.
Katika biblia tunaona neno hili likitumika..
Zaburi 133: 7 “Humwinua mnyonge kutoka mavumbini, Na kumpandisha maskini kutoka jaani”.
Maana yake Bwana anaweza kumpandisha mtu kutoka majalalani na kumpandisha juu.
Ezra 6: 11 “Pia nimetoa amri kwamba, mtu awaye yote atakayelibadili neno hili, boriti na itolewe katika nyumba yake, akainuliwe na kutungikwa juu yake; tena nyumba yake ikafanywe jaa kwa ajili ya neno hili”.
Isaya 25: 10 “Kwa maana mkono wa Bwana utatulia katika mlima huu, na Moabu atakanyagwa chini huko aliko, kama vile majani makavu yakanyagwavyo katika MAJI YA JAA”
Pia unaweza kusoma Danieli 2:5, Danieli 3:39, Maombolezo 4:5 na 1Samweli 2:8.
Katika Agano jipya neno hili limetumika mara moja tu, na Bwana Yesu Kristo katika kitabu cha Luka..
Tusome..
Luka 14:34 “Chumvi ni kitu chema; lakini chumvi ikiwa imeharibika, itiwe nini ikolee?
35 Haiifai nchi WALA JAA; watu huitupa nje. Mwenye masikio ya kusikilia, na asikie”
Kinyesi cha wanyama kikizidi kuharibika kinafaa katika mbolea, watu wanakikusanya na kukifunya mbolea baadaye, hali kadhalika takatata nyingine zote zinavyozidi kuharibika huwa hazikosi matumizi, zinaweza hata kutumika katika kuzalishe gasi ya asili, ambayo itatumika kama nishati..
Lakini chumvi ni kitu cha ajabu, ikishaharibika huwezi kuitumia kwa matumizi yoyote yale, huwezi kuitumia kwenye chakula, wala huwezi kuitumia kama mbolea, wala huwezi kuilundika pamoja na kutengeneza jalala na kuzalisha gesi, …Kwaufupi inakuwa kama mchanga tu..
Sasa Bwana Yesu alitufananisha sisi, tuliompokea yeye na chumvi..
Mathayo 5:13 “Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu.
14 Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima”.
Umeona? Bwana anatuonya, tujihadhari tunavyoenenda katika hii dunia, matendo yetu yasije yakatuharibia sifa zetu moja kwa moja, hata tusifae tena mbele za Mungu na wanadamu.
Kwa urefu juu ya somo hili la chumvi fungua hapa >> NYINYI NI CHUMVI
Je umempokea Yesu?..Kama bado, Kristo yupo mlangoni kurudi kulinyakua kanisa lake, biblia inasema atakuja kama mwivi usiku wa manane, maana yake ni hii, wakati watu na ulimwengu unahisi bado sana, kumbe huo ndio wakati wa kurudi Kristo kulichukua kanisa lake,
Swali ni je!..Bwana Yesu akija leo, una uhakika wa kwenda naye mawinguni?. Kama huna uhakika basi huo ni uthibitisho kwamba hutaenda naye atakapokuja. Hivyo tubu leo kwa dhati na amua kuanza maisha mapya na Kristo, naye atakupokea na kukupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
About the author