Category Archive Uncategorized @sw-tz

Hapo ndipo, atakapompa Mungu Baba ufalme wake.

SWALI: Kulingana na Danieli 7:14 inatabiri kuwa Ufalme wa Bwana Yesu utakuwa ni wa milele, Lakini tukirudi katika 1Wakorintho 15:24 anasema mwishoni atampa Baba yake ufalme wake,

Je hapo inamaana gani , Bwana Yesu ataurejesha ufalme kwa Baba yake au?


JIBU: Tusome vifungu vyote..

Danieli 7:13 “Nikaona katika njozi za usiku, na tazama, mmoja aliye mfano wa mwanadamu akaja pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribia huyo mzee wa siku, wakamleta karibu naye.

14 Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa”.

Pia..

1Wakoritho 15:24 “Hapo ndipo mwisho, atakapompa Mungu Baba ufalme wake; atakapobatilisha utawala wote, na mamlaka yote, na nguvu.

25 Maana sharti amiliki yeye, hata awaweke maadui wake wote chini ya miguu yake.

26 Adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mauti”.

Ni vema tukumbuke kuwa Mungu na Yesu, sio watu wawili tofauti, wenye falme mbili tofauti.. Hapana, “SIRI ya uungu” ni kubwa sana, kama vile mtume Paulo alivyoandika katika 1Timotheo 3:16, Ikiwa na maana mtu usipofumbuliwa macho na kuielewa sehemu ya siri hii, anaweza kudhani Bwana Yesu na Baba yake, ni watu wawili tofauti kabisa…

Ukweli ni kwamba, ufalme Yesu, ndio ufalme wa Baba yake, na Ufalme wa Baba yake ndio ufalme wa Yesu, hivyo akimrudishia Baba ufalme, hakufanyi badiliko lolote, kwasababu yeye na Baba ni kitu kimoja. Ni kama anavyopenda tu yeye mwenyewe atawalie katika ofisi ipi!! Je ya Baba au ya Mwana.. hivyo tu..

Kwahiyo Ufalme huo, kwasasa unatawala rohoni, lakini utadhihirika rasmi, tunapoingia katika ule utawala wa miaka1000, ambapo Mungu (Ndani ya Kristo), atatawala kwa miaka hiyo elfu mpaka atakapohakikisha kila kitu kiovu kimefikia mwisho wake, Kisha baada ya hapo, atatawala sasa kama Baba (Yehova), milele na milele.

Na ndio maana ufalme wake ni wa milele na milele na milele.. Ambao hauwezi kuhasika na kwenda kwa adui, au kwa Malaika yoyote, au kwa kiumbe chochote, utabaki kwake milele na milele na milele. Utukufu na shukrani vimrudie yeye daima.

Amen.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

YESU NI NANI?

Tofauti kati ya ufalme wa mbinguni na ufalme wa Mungu ni ipi?

DANIELI: Mlango wa 11

TUMEFANYIKA KUWA WANA WA MUNGU!

UNYAKUO.

Rudi nyumbani

Print this post

MUME / MKE BORA KUTOKA KWA BWANA UTAMWONA UKIWA KATIKA MAZINGIRA GANI?

Nakusalimu katika jina kuu sana la Bwana wetu Yesu Kristo. Karibu tujifunze Neno la Mungu ili tupate maarifa sahihi ya kuishi hapa duniani.

Na leo tutaona mazingira ambayo ukikaa katika hayo basi Mungu atakujalia umwone mke/mume sahihi aliyekuchagulia toka mbali.

Tofauti na mazingira ya kiulimwengu ambayo yenyewe ili yakupe mke/mume wa kidunia ni sharti uwe katika mazingira ya kidunia..yaani uvae vimini, ujitembeze na suruali barabarani, unyoe viduku, uishi kama wasanii wa kidunia, uwepo disco na kwenye party party kila wakati n.k. ili uonekane.

Ukikaa katika mazingira kama hayo hakika dunia itakupatia unachokitafuta..

Lakini leo tutajifunza mazingira ya ki-Mungu… Ili Mungu akuonyeshe mke/mume sahihi tokea mbali je! Ukae katika mazingira gani.?

Tutamtazama Isaka mtoto wa Ibrahimu. Kama wewe ni msomaji wa biblia utakumbuka mpaka wakati mama yake anakufa hakuwa na mke bado.

Lakini siku moja Baba yake alipoona ni wakati sasa wa Isaka kuwa na mke alimtuma Kijakazi wake mmoja kwenda kumtafutia mke kutoka katika nchi ya mbali nchi sana ya baba zake. ..kwani hakutaka kumpatia mke kutoka katika miji ile waliyokuwepo.

Kuonyesha kuwa haijalishi utazungukwa na vijana wengi wazuri mahali ulipo, hiyo bado haikufanyi udhani mke/mume Mungu aliyekuchagulia ni lazima atoke hapo.

Sasa utaona mara baada ya yule kijakazi kutumwa kwenda kumtafutia Isaka mke na kumpata alipokuwa anarudi..Huku nyuma kuna tabia na desturi ambayo Isaka alikuwa nayo ambayo nataka leo tuione kwasababu hapa ndipo kiini cha somo letu kilipo.. Tusome..

Mwanzo 24:62-66

[62]Basi Isaka alikuwa amekuja kwa njia ya Beer-lahai-roi, maana alikaa katika nchi ya kusini.
[63]Isaka akatoka ili kutafakari kondeni wakati wa jioni; akainua macho yake, akaona, kuna ngamia wanakuja.
[64]Rebeka akainua macho, naye alipomwona Isaka, alishuka juu ya ngamia.
[65]Akamwambia mtumishi, Ni nani mtu huyu ajaye kondeni kutulaki? Mtumishi akasema, Huyu ndiye bwana wangu. Basi akatwaa shela yake akajifunika.
[66]Yule mtumishi akamwambia Isaka mambo yote aliyoyatenda.

Rudia tena Mstari wa 62 unasema…

‘Isaka akatoka ili kutafakari kondeni wakati wa jioni’.

Unaona, Pindi tu alipotoa mguu wake na kwenda kondeni kutafakari..alipojijengea desturi ya kwenda maporini mbali na makazi ya watu ili tu kupata utulivu na Mungu wake, kuutafakari ukuu wake na uweza wake na maajabu yake na ahadi zake..huko huko Mke wake alitokea..na akamwona tokea mbali..

Pengine yeye alidhani mjini alikoondoka ndipo wake wanapotokea lakini..alishangaa kule kule kondeni kwa mbali sana ngamia wanakuja wamembeba bibi arusi wake..

Hiyo ni kuonyesha Isaka haukuwa na hulka kama za vijana wengine walizokuwa nazo..alipendelea zaidi kumtafakari Mungu kuliko kuzurura zurura huko na huko.

Matokeo yake akampata Rebeka, mwanamke ambaye tunamsoma mpaka leo, licha ya kuwa alikuwa ni mwanamke anayemcha Mungu lakini bado alikuwa ni mzuri sana wa uso..Mwanzo 26:6-7

Ndugu, ikiwa unamuhitaji mke mzuri na anaye mcha Mungu basi kuwa kama Isaka..lakini ikiwa unamuhitaji Yezebeli basi ishi mfano wa hao vijana wa kidunia wanavyoishi leo hii..

Na hili pia lipo kwa upande wa pili wa mabinti..ikiwa unataka uolewe na mwanamume ilimradi tu mwanamume basi jiweke kama hao mabinti wa kidunia wanavyojiweka wanaotembea nusu uchi barabarani na kujipambapamba kama vile Yezebeli ili waonekane wanavutia..
Utampata unayemtafuta.

Lakini kinyume chake ni kuwa ukitulia katika kusudi la Mungu..unatumia muda mrefu kwa Mungu wako kuliko kutanga tanga..unamtakafakari tu yeye..nakwambia Mungu utakuongoza kwa Isaka wako tokea mbali..kama vile Rebeka alivyomwona Isaka akimfuta kutokea mbali..

Uhitaji kujionyesha onyesha ovyo..kwasababu anayekuletea mke/mume ni Mungu, si mwanadamu..wewe kaa katika kumtakafakari yeye maisha yako yote.

Kuoa utaoa, kuolewa utaolewa tu!..ukiishi maisha yanayopendeza Mungu si uongo utakutendea tu.

Daudi alisema..

Zaburi 37:25
[25]Nalikuwa kijana nami sasa ni mzee,
Lakini sijamwona mwenye haki ameachwa
Wala mzao wake akiomba chakula.

Mungu hawezi kuacha kumpa mteule wake kitu kilicho chema, na kizuri.. Hawezi kuruhusu mke/mume pasua kichwa atokee mbele ya njia yake, mtu anayemcha yeye. Hilo haliwezekani..

Hivyo kama bado hujaokoka. Tubu leo anza maisha yako upya na Bwana Yesu kwa kumaanisha kabisa..Toba ya kweli inaambatana na kuucha ulimwenguni, mkatae shetani na kazi zake zote na vimini vyake vyote, na suruali zote na viduku vyote..kamtafakari Mungu huko makondeni, hata kama utaonekana mshamba..

Ishi maisha ya kumlingana Bwana..Na bila shaka wakati utafika atamtuma malaika wake kwenda kukuletea mwenzi sahihi..Kama Ibrahimu alivyomtuma kijakazi wake, kumletea Isaka Rebeka.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

KWANINI NDOA NYINGI ZINAVUNJIKA? (Sehemu ya 1: Upande wa wanaume)

Sadaka ya unga na sadaka ya kinywaji zilikuwaje?

Je! “Mke wa ujana wako” ni yupi kibiblia?

Rudi nyumbani

Print this post

Nini maana ya “Mpe kileo yeye aliye karibu na kupotea;?

SWALI: Nini maana ya huu mstari,

Mithali 31:6 “Mpe kileo yeye aliye karibu na kupotea; Kampe divai yeye aliye na uchungu nafsini.

7 Anywe akausahau umaskini wake; Asiikumbuke tena taabu yake”.

Je tunaruhusiwa kunywa pombe, tunapokuwa katika shida?


JIBU: Kumbuka agano la kale lilikuwa ni agano la mwilini, hivyo walitafuta kila mbinu za  mwilini ili kutatua matatizo ya mtu, kwamfano utaona ilikuwa ili kutatua tatizo la zinaa na migororo katika ndoa, waliruhusiwa kutoa talaka, au kuoa wake wengi. Lakini jambo kama hili haukuwa mpango wa Mungu tangu mwanzo.

Mathayo 19:7 “Wakamwambia, Jinsi gani basi Musa aliamuru kumpa hati ya talaka, na kumwacha?

8 Akawaambia, Musa, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu, aliwapa ruhusa kuwaacha wake zenu; lakini tangu mwanzo haikuwa hivi”.

Na  ndio maana utaona, japokuwa waliruhusiwa kufanya hivyo, lakini bado tatizo la uzinzi halikutatuliwa lote, kwamfano Daudi alikuwa na wake wengi, pamoja na Masuria wengi, lakini bado hakuacha kwenda kutafuta wake za watu, na kuzini nao (Mke wa Uria). 2Samweli 11&12..Kwasababu kiu ya uzinzi haizimwi kwa kuoa wake wengi.

Vivyo hivyo, Na katika masuala ya kuondoa huzuni, au uchungu moyoni, walikuwa na desturi, kwamba mtu aliye katika hali hiyo, mfano kama kafiwa na watoto wake wote, au mke n.k. kama vile Ayubu Walikuwa wanawapa pombe, wanywe kwa kipindi hicho iwasahaulishe matatizo yao. Lakini hilo halikufanikiwa kwa wakati wote, kwasababu pombe ikiisha tu kichwani, huzuni yake inarudia tena pale pale..kwasababu kiu ya huzuni haiwezi kukatwa kwa pombe..Mungu aliruhusu tu iwe hivyo kwa muda, kwasababu ya mazingira waliyokuwa nayo kwa wakati ule, lakini halikuwa kusudi lake tangu mwanzo.

Na ndio maana sasa katika wakati wa agano jipya Mungu alileta suluhisho la moja kwa moja la mambo yote rohoni na suluhisho lenyewe ni ROHO MTAKATIFU.

Bwana Yesu  alisema..

Yohana 7:37 “Hata siku ya mwisho, siku ile kubwa ya sikukuu, Yesu akasimama, akapaza sauti yake akisema, Mtu akiona kiu, na aje kwangu anywe.

38 Aniaminiye mimi, kama vile maandiko yalivyonena, mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake.

39 Na neno hilo alilisema katika habari ya Roho, ambaye wale wamwaminio watampokea baadaye; kwa maana Roho alikuwa hajaja, kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa”

Roho Mtakatifu akishaingia ndani ya mtu, anafanya kazi ambayo pombe imeshindwa, madawa ya kulevya yameshindwa, anamwondolea mtu hofu yote, uchungu wote, tamaa yote, wasiwasi wote na mashaka yote, na kiu yote ya uovu milele. Na ndio maana mtu aliyejazwa na Roho Mtakatifu vizuri huwa anaonekana kama mlevi, mtu asiyejali ni nini anakipitia saa hiyo..Kama tunavyoona siku ile ya Pentekoste.

Matendo 2:15 “Sivyo mnavyodhani; watu hawa hawakulewa, kwa maana ni saa tatu ya mchana;

16 lakini jambo hili ni lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii Yoeli,

17 Itakuwa siku za mwisho, asema Mungu, nitawamwagia watu wote Roho yangu, na wana wenu na binti zenu watatabiri; na vijana wenu wataona maono; na wazee wenu wataota ndoto”.

Hivyo, sisi hatuna ruhusu ya kunywa pombe, kwasababu ndani ya pombe, biblia inasema upo UZINZI, na matendo mabaya, lakini katika Roho Mtakatifu upo uhuru. Ukinywa pombe unatenda dhambi.

Waefeso 5:18 “Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho;”

Kwahiyo mstari huo hauhalalishi ulevi, kama tu vile uoaji wa wake wengi usivyokuwa halali sasa, japokuwa uliruhusiwa katika agano la kale.

Tutambue ujumbe wa saa tunayoishi.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

JE! ULEVI NI DHAMBI?.

Nini maana ya msiwe waalimu wengi (Yakobo 1:3)?

Je Lutu alikwenda kuwahukumu watu wa Sodoma na Gomora? Kulingana na Mwanzo 19:9?

USIJITUMAINISHE JUU YA SIRA YAKO ANGALI UPO KATIKA DHAMBI.

Nini maana ya Usiwe mwovu kupita kiasi? (Mhubiri 7:17)

Rudi nyumbani

Print this post

Je! Ni kweli Yesu alirejesha kila kitu kama pale Edeni?

SWALI:Tunasema Yesu karejesha kila kitu Adamu alichopoteza pale Edeni, Lakini kiuhalisia mbona hajarejesha kila kila kitu, mbona tunaona kifo bado kipo, mbona waovu ndio wanaotawala dunia, mbona magonjwa na ajali vinakithiri duniani?


JIBU: Ni kweli kabisa Bwana wetu Yesu Kristo, amekabidhiwa umiliki wa vitu vyote, Kuanzia juu mbinguni, mpaka huku duniani, vyote vipo chini yake. Na kazi kuu aliyokuja kuifanya ni kuvirejesha vyote vilivyoharibiwa na adui, katika nafasi yake, na hata Zaidi yah apo.

Mathayo 11: 27a Akasema, Nimekabidhiwa vyote na baba yangu;..

Soma pia,

Waefeso 1:20 “…. akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho;

21 juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia;

22 akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo

23 ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote”.

Basi kama ni hivyo, utauliza ni kwanini basi, hatuoni mamlaka yake yote yakitimia ulimwenguni?

Jambo ambalo watu wengi hawajui ni  kuwa, Huduma ya Bwana wetu Yesu Kristo haijaishia pale tu alipopaa kwenda mbinguni..bali aliondoka kwa muda tu, akaahidi kurudi, Na ndio maana ujio wake,aliugawanya mara  mbili, ambapo mara ya kwanza alikuja kwa lengo la kuokoa roho za watu na mauti, ndipo hapo akalazimika kufa msalabani, ili damu ipatikane kwa ajili ya ondoleo la dhambi. Hivyo kipindi chote hicho hakuhangaika, na mambo yoyote ya mwilini, au ya kiutawala, au ya kijeografia japokuwa alikuwa amekabidhishwa vyote.

Lakini ujio wake wa pili, hautakuwa tena kama ule wa kwanza, wenye lengo la wokovu wa roho za watu..Hapana, bali atakuja mahususi kwa lengo la kuukomboa huu ulimwengu na mifumo yake yote mibovu, Hapo ndipo atakapokuja kama mtawala, yaani MFALME WA WAFALME na BWANA WA MABWANA. Katika ule utawala wa miaka 1000 (Ufunuo 19:16)

Sasa atakapokuja katika awamu hii,

1) jambo la kwanza atakalofanya ataleta Amani duniani. Kutimiza lile andiko kwamba siku ile Mbwa-mwitu atalala Pamoja na mwana-kondoo, mtoto anyonyaje atacheka kwenye tundu la nyoka. (Isaya 11:5-9, 65:25)

2) Pili atadhibiti uchungu; Watu hawatazaa t tena kwa uchungu (Isaya 65:23)

3) Tatu atabidhibiti, magonjwa na maajali: Hilo ndilo litakalowafanya watu waweze kuishi miaka mingi hata karibia na 1000. (Isaya 65:20). Biblia inasema kipindi hicho, mtu atayekufa na miaka mia ataitwa mtoto mchanga.

4) Nne atadhibiti uharibifu: Yaani Hutajenga, akakaa mwingine, wala hutapanda akala mwingine..(Isaya 65:22)

5) Tano atadhibiti dhambi: Kumbuka wakati huo shetani atakuwa amefungiwa, na mtu yeyote atakayeonyesha dalili za uvunjifu wa amani, fimbo ya chuma, itamlalia.(Ufunuo 12:5)

6) Na mwisho kabisa atamalizana na  MAUTI, huyu ndiye adui wa mwisho.

Kiasi kwamba hakutakuwa na kifo tena ulimwenguni, wala machozi, wala maombolezo.

Hapo ndipo atakamporejeshea Baba mamlaka yote. Na kazi yake itakuwa imekwisha ya ukombozi. Na ndio hapo tutaingia katika ile mbingu mpya na nchi mpya, ambayo Jicho halijawahi kuona wala sikio kusikia.

1Wakorintho 15:24 “Hapo ndipo mwisho, atakapompa Mungu Baba ufalme wake; atakapobatilisha utawala wote, na mamlaka yote, na nguvu.

25 Maana sharti amiliki yeye, hata awaweke maadui wake wote chini ya miguu yake.

26 ADUI WA MWISHO ATAKAYEBATILISHWA NI MAUTI”.

Hivyo, kwa kipindi hichi tulichopewa hapa katikati, tangu siku alipopaa hadi sasa, ni kuhakikisha kila mmoja, anaupokeo huo ukombozi wa roho yake, kwa gharama yoyote ile. Na hiyo inakuja tu kwa kumwamini Yesu Kristo, na kumpokea Roho wake.

Lakini kama mtu atakutwa katika hali ya dhambi hadi siku anayorudi mara ya pili, ajue kuwa hakuna neema tena ya ukombozi juu yake kwasababu Kristo ameshabadili ofisi. Wakati huo, atawaangamiza waovu wote kwa kuwaua kwa pumzi yake (Ufunuo 19:21). Kisha kwenda kuwatupa katika ziwa la moto.

Hivyo, uovu unaouna leo hii duniani ni wa kitambo tu, vita unavyoviona, uchungu, magonjwa na vifo, vyote vina muda mfupi. Hivi karibu Bwana anarudi, kuja kutawala na sisi kwa muda wa miaka 1000. Ndani ya hichi kipindi kila kitu kitarejeshwa katika hali yake.

Na ndio maana huna sababu ya kukimbizana na huu ulimwengu mbovu, ambao tumezungukwa na hatari ya kila namna, ndugu jiwekee hazina mbinguni, kwenye huo ulimwengu ujao wa amani unaokuja.

Lakini kwa bahati mbaya si wote watapokea neema hii ya kutawala na Kristo. Ikiwa utakufa leo katika hali yako ya dhambi. Utabakia huko huko makaburini hadi siku ile ya ufufuo, kisha uhukumiwe na kutupwa motoni.

Je! Bado unaendelea katika dhambi zako? Bado unaichezea tu hii neema? Kisa Kristo ni mpole sasa kwako unadhani atakuvumilia hivyo katika hali yako ya dhambi milele ? Ndugu yangu. Bwana Yesu Kristo ni mkuu kuliko unavyoweza kufikiri, utalithibitisha hilo, siku ile atakaporudi mara ya pili. Ambapo biblia inasema kila kinywa kitakiri, na kila goti litapigwa. Na mataifa watamwombolezea.

Heri ukampa Yesu Kristo Maisha yako angali bado una muda mchache, hivi karibuni Parapanda italia, Na Kristo atabadili ofisi yake.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

KWANINI YESU NI ADAMU WA PILI?

Kwanini Mungu aliwaita Adamu na Hawa jina moja?

TAFAKARI SANA KABLA YA KUAMUA HATIMA YAKO.

Biblia inaposema “Wote tumetenda dhambi” si inamaanisha hakuna mtakatifu duniani?

HUTATAMBUA LOLOTE, SIKU YA UNYAKUO IKIFIKA.

Rudi nyumbani

Print this post

Hakitaingia kamwe cho chote kilicho kinyonge.(Ufu 21:27)

SWALI; Naomba kuuliza katika ufunuo 21:27 kwamba hakitaingia kilicho kinyonge hili neno kinyonge linamaanisha nini? Je ni watu dhaifu mfano vilema?


Ufunuo wa Yohana 21:27
[27]Na ndani yake hakitaingia kamwe cho chote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo, bali wale walioandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo.

JIBU: “Kinyonge” kinachozungumziwa hapo si mtu mlemavu, kama ingekuwa hivyo Bwana Yesu asingesema..kiungo chako kimoja kikikukosea king’oe ni heri uingie mbinguni mlemavu kuliko kuwa viungo vyako vyote na kuishia kuzimu.(Mathayo 5:29-30)

Lakini kinyonge kinachozungumziwa hapo ni kipi?

Kitu kinyonge sikuzote ni kitu kisichokuwa na nguvu ya kustahimili mtikisiko fulani aidha mapigano,ugonjwa,Dhoruba, mateso n.k.

Vivyo hivyo katika roho mtu asiyekuwa na nguvu ya kuushinda ulimwengu huyo ni sawa na mnyonge. Na ndio maana Bwana Yesu alisema maneno haya..

Mathayo 11:12
[12]Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka.

Utajiuliza ni kwanini Bwana arejee siku za Yohana mbatizaji, na sio siku za labda, Isaya, au Musa, au Samweli? Bali Yohana Mbatizaji?

Alisema hivyo, ili kutupa picha na sisi tunapaswa tuishi Maisha ya kuukana ulimwengu, mfano wa Yohana mbatizaji..Ambaye biblia inasema Maisha yake yote, aliishi majangwani mbali na ulimwengu, na matokeo yake akawa akiongezeka nguvu rohoni kila siku (Luka 1:80).

Hivyo na sisi tunapaswa tuushinde ulimwengu, ili tuweza kuuteka ufalme wa Mungu, ikiwa uzinzi utatushinda, ikiwa anasa na tamaa za ujanani zitatushinda, basi sisi ni wanyonge, na hivyo, kamwe hatutakaa tuuingie ule mji mpya wa Yerusalemu, utakaoshuka kutoka mbinguni. Kwasababu watakaoingia kule ni watakatifu tu walioushinda ulimwengu, na si vinginevyo.

Huu si wakati wa kuikumbatia dhambi..na kusema kwamba mimi siwezi kuushinda ulimwengu, ni wajibu wako kushindana mpaka ushinde…hupaswi kuwa mnyonge. Kumbuka wewe ukishindwa haimaanishi kuwa mwingine kashindwa.

Lakini tutawezaje kufikia hapo?

Tutafika kwa njia moja tu nayo ni  kwa kumaanisha kabisa kuacha dhambi, na kujitwika misalaba yetu na kumfuata Yesu kwa gharama zozote zile.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Rudi nyumbani

Print this post

Kutia mkono chini ya paja kama ishara ya kiapo, kulimaanisha nini?

Tofauti na desturi za mataifa mengi ya sasa zilivyo, kwamba mtu akitaka kuapa, huwa anashika kitabu Fulani cha dini kama vile biblia, au anaweka mkono wako kifuani ndipo anatamka kiapo chake..Zamani kulingana na desturi wa wayahudi ilikuwa ni mtu anaweka mkono wake, chini ya paja la anayemwapisha.

Pajani kibiblia ni sehemu ambayo ipo karibu sana na viungo vya uzazi.. Sehemu nyeti, ambapo hapawezi kufikiwa kama jambo lililopangwa halihitaji umakini sana. Ni sawa na leo watu wanavyotumia biblia mahakamani kuapa, ni kitabu nyeti sana, kiasi kwamba mpaka kimetumiwa hiko ni kuonyesha umakini wa kile unachotakiwa kukifanya.

Na ndivyo ilivyokuwa kwa Ibrahimu, na Yakobo. Kwamfano Ibrahimu alipotaka mwanawe Isaka apatiwe mke kutoka katika nyumba ya Ndugu yake, aliyekuwa mbali sana, alimwita mtumwa wake, akamwapisha kwamba akamletee binti sawasawa na alivyomwagiza, Hivyo ili kuthibitisha kuwa mtumwa wake atayatekeleza yale aliyoagizwa, akachukua mkono wake, na kuulia katika paja lake, kuonyesha pia kwamba yupo tayari kutii kila agizo lililoamriwa juu yake.

Mwanzo 24:2 “Ibrahimu akamwambia mtumishi wake, mzee wa nyumba yake, aliyetawala vitu vyake vyote, Tafadhali uutie mkono wako chini ya paja langu, 3 nami nitakuapisha kwa Bwana, Mungu wa mbingu, na Mungu wa nchi, kwamba hutamtwalia mwanangu mke katika binti za Wakanaani ambao nakaa kati yao;”…

9 Yule mtumishi akaweka mkono wake chini ya paja la Ibrahimu bwana wake, akamwapia katika neno hilo. 10 Kisha huyo mtumishi akatwaa ngamia kumi katika ngamia za bwana wake akaenda zake, maana mali zote za bwana wake zilikuwa mkononi mwake, akaondoka, akaja mpaka Mesopotamia, mpaka mji wa Nahori.

Jambo kama hilo tunaliona pia kwa Yakobo, siku ile alipokaribia kufa, alimwita Yusufu na kumwambia, aweke mkono wake chini ya paja lake, ali amwapie, kwamba hatamzika kule Misri bali, katika nchi ya Baba yake.

Mwanzo 47:29 “Siku za kufa kwake Israeli zikakaribia; akamwita mwanawe Yusufu, akamwambia, Kama nimeona kibali machoni pako, weka mkono wako chini ya paja langu, ukanifanyie rehema na kweli; nakusihi usinizike katika Misri.

30 Lakini nitakapolala pamoja na baba zangu, unichukue toka Misri, unizike katika kaburi lao. Akasema, Nitafanya kama ulivyosema.

31 Akanena, Niapie. Naye akamwapia. Israeli akajiinamisha kwenye mchago wa kitanda”.

Lakini sisi katika agano jipya, hatujapewa ruhusa ya kuapa bali Bwana Yesu alisema, maneno yetu yawe Ndio, ndio.. Au Sio,..sio..Na si zaidi. (Mathayo 5:33-37). Hakuna sababu ya kuapa, kwasababu hatuna mamlaka ya kutangua au kuthibitisha chochote katika maisha yetu kana kwamba vipo chini ya uwezo wetu.
Sisi si Mungu.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Naomba kujua nini maana ya kuteguka uvungu wa paja?

Je Bwana Yesu alikuwa na mchoro (tattoo) katika paja lake? (Ufunuo 19:16).

JE! NI KWELI UMEMFUATA YESU?

Kwanini Yesu aliwakataza mitume wake kumdhihirisha?

Rudi nyumbani

Print this post

NI KIZAZI KIPI WEWE UPO?

Kibiblia  Kizazi ni kundi la watu linalozuka ghafla lenye tabia zinazofanana, linaweza kuzuka aidha kutokana na mabadiliko ya nyakati, au mabadiliko ya mazingira. Kwamfano, Wana wa Israeli walipokuwa Misri, chini ya Yusufu, waliishi kwa raha sana, Lakini Yusufu alipokufa pamoja na Yule Farao, kilinyanyuka kizazi kingine kisichokumbuka wema wa Yusufu, na hapo ndipo utumwa mgumu ulipoanza.

Vilevile, Wana wa Israeli walipofika katika nchi yao ya  Ahadi, mwanzoni waliishi maisha ya kumcha Mungu sana, lakini wakati ulipopita mrefu kilinyanyuka kizazi kingine kisichomjali Yehova, hapo ndipo Israeli ilipoanza kuingia katika matatizo mengi sana.(Waamuzi 2:10)

Na katika hichi kipindi cha Siku za mwisho, tunapaswa tuwe makini sana, Zipo tabia ambazo utaziona kwa watu wengi sana, lakini kiuhalisia hazikuwepo huko nyuma. Hivyo ni vizuri ukafahamu aina ya vizazi vilivyopo duniani sasa hivi  kulingana na biblia ili ujue wewe upo wapi na jinsi gani unapaswa ujiupeshe navyo.

  1. Kizazi cha uzinzi na zinaa:

 Bwana Yesu alisema..

Mathayo 12:39 “Akajibu, akawaambia, Kizazi kibaya na cha zinaa chatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya nabii Yona”.

Ni kizazi cha watu kinachozuka kinapenda tu usherati na uzinzi kuliko kitu kingine chochote ulimwenguni. Leo hii tazama  mawazo ya vijana wengi yalivyo, sikiliza mazungumzo yao,  mambo wanayoyafanya kwa siri,vitu wanavyotazama mitandaoni, video za ngono, ni jambo la kawaida kwao, na kibaya zaidi sio tu vijana, hadi wazee na watoto wamo katika kundi hili. Jambo ambalo hapo zamani halikuwepo. Hiyo ni kuthibitisha kuwa ni hiki ni kizazi kingine kimezuka, ambacho ni hatari sana.

Bwana Yesu alisema..

Marko 8:38 “Maana kila mtu atakayenionea haya mimi, na maneno yangu, katika KIZAZI HIKI CHA UZINZI na dhambi, Mwana wa Adamu atamwonea haya mtu huyo, atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu”.

Ndugu, jiupeshe, na mkondo huu, si lazima uishe kama ulimwengu unavyotaka, kizazi hiki kimeshahukumiwa na Mungu.

     2) Kizazi cha nyoka:

Kipo kizazi cha Nyoka.

Mathayo 3:7 “Hata alipoona wengi miongoni mwa Mafarisayo na Masadukayo wakiujia ubatizo wake, aliwaambia, Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja?

8 Basi zaeni matunda yapasayo toba;

9 wala msiwaze mioyoni mwenu kwamba, Tunaye baba, ndiye Ibrahimu; kwa maana nawaambia ya kwamba Mungu aweza katika mawe haya kumwinulia Ibrahimu watoto”.

10 Na shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.

Soma pia..Mathayo 12:34

Nyoka, alikuwa mwerevu sana kuliko wanyama wote mwituni, lakini alikubali kuwa chombo teule cha shetani. Uzao wake, ndio uliendelea mpaka kwa Kaini, na ndio maana watu wale walikuwa hodari sana , wagunduzi na wavumbuzi wakubwa, lakini waovu waliopindukia (Mwanzo 6:4). Ni watu ambao walikuwa hawana muda na Mungu, lakini kwa upande wa pili uzao wa Mungu, ulikuwa ni mnyenyekevu unaomtafuta Mungu usiku na mchana, vilevile na usio na masumbufu mengi ambao ulipitia kwa Sethi. (Mwanzo 4:26).

Inafunua hadi sasa, kwamba kizazi hiki kipo, Angalia dunia ya sasa, imestaarabika kuliko ile ya zamani, watu wanaelimu kubwa sana, wanagundua mambo makubwa  sana, wamekwenda mpaka mwezini, lakini ukiwagusia habari za Mungu, wanakuambia  hayo ni mawazo yako tu, hakuna Mungu,dini imetengenezwa na watu, wamejikita katika mambo ya mwilini, tu, elimu, utajiri, uvumbuzi basi, Mungu hayupo.

Ndugu, ikiwa na wewe upo katika jopo hili la watu, jiangue haraka sana, hichi ni kizazi, ambacho kipo ulimwenguni sasa.

   3) Kizazi cha watu wasiowatii wazazi wao.

Mithali 30:11 “Kuna kizazi cha watu wamlaanio baba yao; Wala hawambariki mama yao”.

Kuporomoka kwa maadili na nidhamu unakokuona leo, hakukuwepo huko nyuma. Leo utasikia mtoto anajibizana na mzazi wake, mwingine anampiga, mwingine anamzungumzia vibaya, wengine wametengeneza mpaka uadui na wazazi wao.. Kesi hizi ni nyingi sana sikuhizi..Wewe kama mtoto, wewe kama kijana, kuwa makini sana, kizazi hiki kimezuka ulimwenguni sasa. Unapoona, wenzako hawawaheshimu wazazi wao, na wewe usiwe mmojawapo.

Katika agano la kale mtu aliyejaribu kuonyesha utomvu wa nidhani kwa mzazi wake, sheria yake ilikuwa ni kifo. Jitathmini unawatii wazazi wako, Unawapenda?, unawabariki? Unawanenea mema? Unawaombea?.. Hata kama mzazi anakuudhi, huna ruhusu ya kurudisha baya kwa baya kwake. Vinginevyo upo chini ya laana ya kizazi hiki.

4) Kizazi cha watu wanaojiona siku zote wapo sawa:

Mithali 30:12 “Kuna kizazi cha watu walio safi machoni pao wenyewe; Ambao hawakuoshwa uchafu wao”.

Hili kundi ni kubwa sana, Mtamuhubiria mtu na kumwambia pasipo kumwamini Kristo, huwezi kuokolewa, yeye atakuambia, mimi naamini matendo yangu ni safi, ninaamini Mungu hiyo inatosha, siwezi kuhukumiwa. Atakuwa radhi, kujihesabia haki, hata kama ni mzinzi, au mlevi..Haoni hatia yoyote kwa anayoyafanya. Yeye anachoamini ni kuwa Mungu hawezi kumchoma motoni milele,.Nimeshakutana na watu wa namna hii wengi sana. Wanaodhani kuwa kwa kile wanachokiamini, ndio tiketi ya Mungu kuwaokoa siku ile.

Ndugu kama upo katika hili kundi jiepushe nalo, Ikiwa bado hujaokoka, mkimbilie Yesu, yeye pekee ndiye mwenye uwezo wa kukusafisha dhambi zako, na sio kile unachokiamini.

 5) Kizazi cha watu wenye kiburi:

Mithali 30:13 “Kuna kizazi cha watu ambao macho yao yameinuka kama nini! Na kope zao zimeinuka sana”.

Wapo watu ambao, kujishusha hakupo ndani yao. Wanajiona kuwa hakuna chochote kinachoweza kuwa msaada kwao, Mungu si kitu kwao, kwanini wakaombe, kwanini waende ibadani. Wapo radhi hata kuutukana wokovu, au kazi ya Mungu. Wanatumaini, mali zao, au ujuzi wao.

Kama tabia hizo zimeanza kuonekana ndani yako, geuka upesi.

  6) Kizazi wa watu wasio na huruma.

Mithali 30:14 “Kuna kizazi cha watu ambao meno yao ni panga; Na vigego vyao ni kama visu. Ili kuwala maskini waondolewe katika nchi, Na wahitaji katika wanadamu”.

Utu umeondoka duniani, Yupo radhi kufanya biashara haramu, bila kujali kinaleta madhara mangapi kwa jamii, anauza madawa ya kulevya, anauza bidhaa zilizoisha ubora, wanadhulumu haki za wajane na mayatima kwa faida zao wenyewe. Anaua, ili apate mali, n.k.

Tunayoyaona, hayakuwepo zamani, tusiwe watu wenye tamaa ya mali.

  7) Kizazi cha wenye adili:

Lakini pamoja na kuwepo kwa vizazi hivi vyote, vya watu waovu.. Biblia inasema pia, kitakuwepo kizazi cha watu wenye adili, wanaomcha Mungu, wanaotenda mapenzi yake.

Zaburi 112:1 “Haleluya. Heri mtu yule amchaye Bwana, Apendezwaye sana na maagizo yake.

2 Wazao wake watakuwa hodari duniani; Kizazi cha wenye adili kitabarikiwa”.

Na ndio maana unaona pia wapo watakatifu wa Mungu leo duniani. Hawa ndio Bwana anaowatazama, na siku moja itafika Kristo atawahamisha kutoka katika huu ulimwengu kwa tukio la UNYAKUO na kuwapeleka mbinguni. Swali ni je wewe upo katika kizazi kipi?

Matendo 2:40 “Akawashuhudia kwa maneno mengine mengi sana na kuwaonya, akisema, Jiokoeni na kizazi hiki chenye ukaidi”.

Jibu unalo moyoni mwako.

Kumbuka Unyakuo upo karibu sana, dalili zote zimeshatimia, huna haja ya kuendelea kutangatanga na huu ulimwengu tena. Mgeukie Kristo akuokoe, ili uwe mmojawapo wa kizazi cha watu waadilifu.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp yanayotumwa kila siku basi bofya hapa >>>  WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita..

BADO UPO YERUSALEMU TU..GALILAYA HUTAKI KWENDA?

Nini maana ya msiwe waalimu wengi (Yakobo 1:3)?

FANYIKA SIPORA WA KRISTO, UNYAKUO UPO KARIBU.

Marago ni nini? ( Waamuzi 10:18)

Rushwa inapofushaje macho?

Rudi nyumbani

Print this post

WITO WA MUNGU HAUVUKI NENO LAKE.

Bwana Yesu atukuzwe ndugu yangu. Karibu tuyatafakari maneno ya uzima pamoja..

Tunaposoma biblia..tujue kuwa tunausoma ufahamu wa Mungu. Mtu asiyeitafakari biblia halafu anakimbilia kwenda kumtumikia Mungu.. Ajue kuwa anajiweka katika hatari kubwa sana ya kuangamizwa na Mungu.

Ni sawa na mtu anayekimbilia kufanya biashara ambayo hajaifanyia utafiti kujua changamoto zake.faida zake na hasara zake..

Leo tutatazama ni kwa namna gani.

Ndugu usipumbazwe hata kidogo kuona Mungu anasema nawe..anakuonyesha maono makubwa..anakusifia..anakutokea..anakutuma ukawahubirie watu injili.. Usipumbazwe kabisa na jambo hilo. Kama maagizo yaliyopo katika Neno lake huyatii..Kufa unaweza tu kufa.

Jambo kama hilo tutaliona kwa Musa. Kila mtu anafahamu kuwa alitokewa na Mungu mwenyewe katika mwali wa moto. Mungu akampa ishara kubwa..akamtuma aende Misri kwenda kuwaokoa mamilioni ya watu..Lakini cha ajabu tunashangaa Mungu alitaka kumuua njiani..

Yaani kama sio mke wake Sipora,kumsaidia habari ya Musa ingekuwa imeishia pale na maono yake na wito wake.

Kutoka 4:21-25

[21]BWANA akamwambia Musa, Hapo utakaporudi Misri, angalia ukazifanye mbele ya Farao zile ajabu zote nilizozitia mkononi mwako; lakini nitaufanya mgumu moyo wake, naye hatawapa ruhusa hao watu waende zao.

[22]Nawe umwambie Farao, BWANA asema hivi, Israeli ni mwanangu mimi, mzaliwa wa kwanza wangu;

[23]nami nimekuambia, Mpe mwanangu ruhusa aende, ili apate kunitumikia, nawe umekataa kumpa ruhusa aende; angalia basi, mimi nitamwua mwanao, mzaliwa wa kwanza wako.

[24]Ilikuwa walipokuwa njiani mahali pa kulala, BWANA akakutana naye akataka kumwua.

[25]Ndipo Sipora akashika jiwe gumu na kuikata govi ya zunga la mwanawe, na kuibwaga miguuni pake akasema. Hakika wewe u bwana arusi wa damu kwangu mimi.

Sasa ni kwanini Mungu alitaka kumuua ni kwasababu alipuuzia maagizo ya msingi ya kuwatahiri watoto wake..Mambo ambayo Mungu alikuwa ameshawaagiza  wana wa Israeli wote wafanye hivyo kulithibitisha agano lake..Lakini yeye hakuona umuhimu huo..kisa tu Mungu amemtokea..amemtuma kama nabii mkuu Misri..hivyo hakuna sababu ya kuhangaika na yale mengine..

Ni wangapi leo hii wamepatwa na kiburi cha kukataa maagizo ya Mungu kama vile ubatizo sahihi wa maji..kwa kisingizio kuwa Mungu anazungumza na wao..Mungu kawatokea..Mungu kawaagiza waende kutumika..ubatizo hauna maana yoyote ukishamkiri tu Kristo inatosha..Wewe si zaidi sana ya nabii  Musa..Mungu hashindwi kukuua.

Unaweza kusema ni Musa tu peke yake yalimkuta haya..Yupo nabii mwingine huko mbeleni anaitwa Balaamu.. Yeye naye alitokewa na Mungu katika safari yake ya kwenda kuwalaani Israeli.

Mara ya kwanza Mungu akamuonya lakini hakusikia.. Akataka zaidi kufanya hivyo..baadaye Mungu akamruhusu na akamuhakikishia kuwa atakuwa pamoja naye..Lakini njiani Mungu alikuwa ameshamweka malaika wake tayari amuue. Kama si yule Punda kumsaidia habari yake ingekuwa naye imeisha pale…

Ni kwanini sasa iwe vile ni kwasababu alipuuzia maagizo ya awali ya Mungu “..amlaaniye Israeli na yeye atalaaniwa”(Mwanzo 12:3)..hivyo yeye akataka kulipindua hilo Neno kwa maono yake..au mitazamo yake mwenyewe. Akawa katika hatihati ya kufa..

Hesabu 22:12-13

[12]Mungu akamwambia Balaamu, Usiende pamoja nao; wala usiwalaani watu hawa, maana wamebarikiwa.

[13]Balaamu akaondoka asubuhi akawaambia wakuu wa Balaki, Enendeni zenu hata nchi yenu; kwa maana BWANA amekataa kunipa ruhusa niende pamoja nanyi….

Lakini baada ya kushurutishwa sana na wale wakuu wa Balaki..utaona alijifanya tena kwenda kumuuliza Mungu..hichi ndio kitu alichoambiwa mara ya pili

Hesabu 22:20-22

[20]Mungu akamjia Balaamu usiku, akamwambia, Kwa kuwa watu hawa wamekuja kukuita, enenda pamoja nao; lakini neno lile nitakalokuambia ndilo utakalolitenda, basi.

[21]Balaamu akaondoka asubuhi, akatandika punda wake, akaenda pamoja na wakuu wa Moabu.

[22]Hasira ya Mungu ikawaka kwa sababu alikwenda; malaika wa BWANA akajiweka njiani, ili kumpinga. Basi alikuwa amepanda punda wake, na watumishi wake wawili walikuwa pamoja naye.

Ndugu..tuzifahamu tabia za Mungu..wapo watu wengi wameonyeshwa mambo makubwa sana katika wito wao. Lakini unashangaa hakuna hata moja limetimia..hadi siku anakufa..Ni kwanini?

Nikwasababu alikwenda pasipo kujua kanuni za Mungu. Tuishi kwa Neno la Mungu na sio kwa ndoto au sauti au maono. Haijalishi wito huo utakuwa mkubwa kiasi gani..hauwezi kuzidi Neno lake.. Neno linasema mwanamke hana nafasi ya kufundisha kanisani (palipo na mchanganyiko wa wanaume na wanawake) 1Timotheo 2:12..Lakini mwingine atasema Mungu kaniita kuwa Mchungaji..kanitokea kabisa na kunitia mafuta..

Mama kuwa makini..kasome biblia yako kwanza umwelewe Mungu ndipo ukatumike..

Hivyo ili tuwe salama.. kabla ya kuitii sauti yoyote ya nje..Tuitii kwanza Sauti ya Mungu iliyo katika Neno lake.  Ndio hayo mengine yafuate.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp ya kila siku basi jiunge kwa kubofya hapa >>> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

USIPOTEZWE NA MANENO YA MANABII WA UONGO.

JE UNAIFANYA KAZI YA MUNGU?

MAJARIBU MATATU YA YESU KRISTO

TAFUTA MSAMAHA HALISI, NA SI MSAMAHA TU!

UTAWALA WA MIAKA 1000.

Nini maana ya “wazimu” katika biblia?

JINSI PAULO ALIVYOPAMBANA NA UJINGA WA ROHONI.

PINDO LA VAZI LAKE SASA LIMEREFUSHWA.

Rudi nyumbani

Print this post

Atamaniye faida huifadhaisha nyumba yake mwenyewe;

SWALI: Nini maana ya huu mstari..

Mithali 15:27

[27]Atamaniye faida huifadhaisha nyumba yake mwenyewe;

Bali achukiaye zawadi ataishi.


JIBU: Mstari huo ni mgumu kueleweka kidogo kwasababu kiswahili kilichotumika hapo ni kile cha zamani..

Ukiangalia tafsiri nyingine..mstari huo unamaana hii.. Atamaniye kupata vingi kwa njia isiyohalali huifadhaisha nyumba yake mwenyewe bali achukiaye rushwa ataishi.

Jambo ambalo ni kweli..kwamfano Mtu anayejiingiza katika biashara ya madawa ya kulevya kwa tamaa tu ya kupata fedha nyingi..hajui kuwa mwisho wake ni kujibomoa yeye mwenyewe na pamoja nyumba yake yote.

Habakuki 2:9

[9]Ole wake yeye aipatiaye nyumba yake mapato mabaya, ili apate kukiweka kioto chake juu, apate kujiepusha na mkono wa uovu!

Mwingine utakuta anatoa rushwa ili bidhaa zake zisilipishwe kodi..lakini hajui mwisho wake utakuwa mbaya siku moja.

Lakini kinyume chake biblia inasema atakayeyakwepa hayo yote ataishi..

Sikuzote tamaa ya  za haraka haraka mwisho wake huwa ni mitegoni..

Mhubiri 4:6

[6]Heri konzi moja pamoja na utulivu,

Kuliko konzi mbili pamoja na taabu;

na kujilisha upepo.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Pia kama utapenda uwe unafikiwa na masomo ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP basi bofya hapa ujiunge moja kwa moja  >>>> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

SABATO ILIFANYIKA KWAAJILI YA MWANADAMU NA SI MWANADAMU KWAAJILI YA SABATO!

Maana ya huu mstari ni ipi? Mithali 14:4 ‘Zizi ni safi ambapo hapana ngombe;bali nguvu za ngombe zaleta faida nyingi’.

UMEDI NA UAJEMI ZILITAWALAJE?

KUNA AINA NGAPI  ZA MAOMBI?

HUANGUA MAYAI YA FIRA, NA KUSUKA WAVU WA BUIBUI;

Print this post

Ratli/ Ratili ni nini katika biblia?

Ratili ni kipimo cha uzito kilichotumika enzi za kale..chenye uzito sawa na Gramu 500 hivi. Karibia na nusu kilo.

Neno hilo utalisoma katika vifungu hivi kwenye biblia..

Yohana 19:39

[39]Akaenda Nikodemo naye, (yule aliyemwendea usiku hapo kwanza), akaleta machanganyiko ya manemane na uudi, yapata ratli mia.

Pia..

Yohana 12:3

[3]Basi Mariamu akatwaa ratli ya marhamu ya nardo safi yenye thamani nyingi, akampaka Yesu miguu, akamfuta miguu kwa nywele zake. Nayo nyumba pia ikajaa harufu ya marhamu.

Unaweza kupata picha Mariamu alibeba manukato yaliyokuwa na uzito wa karibia nusu kilo..na yote akammwagia Bwana Yesu..manukato ambayo ingetosha tu kuchukua kidogo na kumpaka lakini yeye aliyamimina kwake kama maji.

Kwasasa mafuta hayo kwa wingi wake ni thamani isiyo pungua milioni 6 kwa fedha za kitanzania..kufunua ni jinsi gani Mariamu alimthaminisha Yesu kuliko mtu mwingine yeyote au mfalme yeyote duniani..

Si ajabu kwanini matendo ya watu kama hawa tunayasoma hadi leo katika maandiko..Ni kutufundisha kuwa na sisi pia tukitoa vitu vyetu vya thamani nyingi sana kwa ajili ya Mungu..

Mungu naye ni lazima arudishe fadhila kwetu kwa kutupa kumbukumbu la daima..ndivyo alivyofanya kwa yule mwanamke pale watu walipomng’unikia kwa upotevu wote ule..Bwana alisema..

Marko 14:8-9

[8]Ametenda alivyoweza; ametangulia kuupaka mwili wangu marhamu kwa ajili ya maziko.

[9]Amin, nawaambia, Kila ihubiriwapo Injili katika ulimwengu wote, na hili alilotenda huyu litatajwa kwa kumbukumbu lake.

Swali ni je na sisi tunaweza kumthamini Bwana kwa namna hiyo? Bwana atupe macho hayo.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

VIPIMO MBALIMBALI VYA KIBIBLIA.

Santuri ni nini? (Danieli 3:5,10)

Panda/ Sauti ya panda ni nini kibiblia?(Danieli 3:5)

Kinubi ni nini katika biblia? (1Samweli 16:16, 23)

Rudi nyumbani

Print this post