Kuhubiri injili kwa husuda na fitina ndio kupi?

Kuhubiri injili kwa husuda na fitina ndio kupi?

SWALI: Mtume Paulo alikuwa anamaanisha nini aliposema..”Wengine wanahubiri habari za Kristo kwa sababu ya husuda na fitina; na wengine kwa nia njema.”(Wafilipi 1:15)? Huko kuhubiri injili kwa husuda ndio kukoje?


JIBU: Ili kuelewa Paulo alimaanisha nini ni vema tukaisoma habari yote tokea juu..

Wafilipi 1:12-18

[12]Lakini, ndugu zangu, nataka mjue ya kuwa mambo yote  yametokea zaidi kwa kuieneza Injili;

[13]hata vifungo vyangu vimekuwa dhahiri katika Kristo, miongoni mwa askari, na kwa wengine wote pia.

[14]Na wengi wa hao ndugu walio katika Bwana, hali wakapata kuthibitika kwa ajili ya kufungwa kwangu, wamezidi sana kuthubutu kunena neno la Mungu pasipo hofu.

[15]Wengine wanahubiri habari za Kristo kwa sababu ya husuda na fitina; na wengine kwa nia njema.

[16]Hawa wanamhubiri kwa pendo, wakijua ya kuwa nimewekwa ili niitetee Injili;

[17]bali wengine wanamhubiri Kristo kwa fitina, wala si kwa moyo mweupe, wakidhani kuongeza dhiki za kufungwa kwangu.

[18]Yadhuru nini? Lakini kwa njia zote, ikiwa ni kwa hila, au ikiwa ni kwa kweli, Kristo anahubiriwa; na kwa hiyo nafurahi, naam, nami nitafurahi.

Waraka huu Paulo aliuandika akiwa gerezani..Sasa akiwa huko kifungoni kulizuka makundi mawili ya watu ambao walianza kuihubiri injili kama ile ile aliyoihubiri..

Kundi la kwanza lilikuwa na Nia njema kwa Bwana kama ile aliyokuwa nayo Paulo. Kuzihurumia roho za watu na kuifanya kazi ya injili kwa kujitoa kwa upendo bila kujali kama wanapata faida yoyote au la..

Lakini kundi la pili lilikuwa la tofauti..lilianza kuhubiri kwalengo la kumkomoa Paulo na kutaka kujionyesha kuwa na wao wana mamlaka kama yake..N hiyo yote ni kwasababu ya kukua na kujulikana sana kwa huduma ya Paulo ulimwenguni..Hivyo wivu ulipowajaa  wakatumia fursa ya kufungwa kwake kuhubiri injili kwa lengo la kumuonyesha Paulo hana chochote cha ziada kushinda wao. 

Na wengine wakawa wanahubiri huku wakimnenea habari mbaya ili tu kumzidishia vifungo vyake kwa maaskari.

Lakini cha ajabu ni kuwa taarifa hizo zilipokewa tofauti na Paulo..badala ya kuchukia ndio kwanza akafurahia..kwasababu hata kwa njia hiyo injili inahubiriwa na watu wanaokoka..

Ni jambo gani tunaweza kujifunza kwa Paulo na hao wahubiri injili kwa fitina..

Hiyo ni kuonyesha kuwa injili inaweza kuhubiriwa na mtu yeyote na ikaleta matokeo yale yale ya wokovu..hata sasa wapo wahubiri wengi wa uongo wanawavuta watu wa Kristo..lakini hilo haliwafanyi wao kupokelewa na Kristo siku ile ya hukumu..

Bwana Yesu aliliweka wazi hilo katika; 

Mathayo 7:21-23

[21]Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.

[22]Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?

[23]Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.

Hivyo tuwe makini na kuhubiri kwetu..Je Nia yetu ni kwa Bwana? au kwa lengo la kushindana na mtumishi fulani au mtume fulani au mchungaji fulani au nabii fulani…

Vivyo hivyo…Sisi kama wahubiri hatuna haja ya kurudisha mashambulizi pale tunapoona watumishi wa uongo wanashindana nasi..ikiwa injili wanayoihubiri ni ya kweli basi sisi tufurahie matunda kama alivyofanya Paulo..hayo mengine tumuchie Mungu atayahukumu mwenyewe siku ile..

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Fitina maana yake nini kwenye biblia?

Ni kwa namna gani malaika wa mbinguni wanaweza kutuhubiria sisi injili?

Je! Watu ambao hawajawahi kusikia injili kabisa siku ya mwisho watahukumiwa?

UTAYAFIKIAJE MANENO SAFI YA MUNGU?

Rudi nyumbani

Print this post

NINI TUNAJIFUNZA KWA THEOFILO MTUKUFU?

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze biblia neno la Mungu wetu, ambalo ni taa iongozayo miguu yetu na Mwanga wa njia yetu.

Leo tutajifunza juu ya mtu mmoja aliyeitwa Theofilo, ambaye biblia haijaeleza habari zake kwa urefu lakini amehusika pakubwa sana katika kuieneza injili.

Lakini kabla ya kwenda kumtazama huyu Theofilo hebu tuweke msingi kidogo kwa kuelewa juu ya baadhi ya nyaraka za kwenye biblia.

Katika maandiko hususani agano jipya tunaona nyaraka kadhaa, zikiandikwa kwa watu fulani, ambazo hizo zimekuwa msaada hata kwetu sisi wa nyakati hizi.

Kwamfano tunaona waraka ambao Paulo alimuandikia Timotheo, au Tito au Filemoni…Nyaraka hizo zilikuwa zinawasaidia hao watu kuwajenga na kuwaimarisha katika utumishi wao, lakini tunaona Mungu aliziruhusu zienee na kusomwa na watu wengi hata mpaka wakati  wetu huu.

Hawa wakina Tito, Filemoni, na Timotheo hawakujua kuwa barua hizo walizotumiwa na Paulo zitakuja kusomwa na maelfu ya vizazi mbeleni..wao pamoja na Paulo hawakulijua hilo.

Ni sawa na wewe leo umwandikie Barua ndugu yako aliyeko mbali, lakini ipite miaka mingi sana huko mbele uje usikie hiyo barua uliyomuandikia inasomwa duniani kote..bila shaka utashangaa…Ndivyo ilivyokuwa kwa Paulo na hawa wakina Timotheo, Tito na Filemoni..waliandikiana barua wao kwa wao kwa lengo la kuimarisha utumishi wao.. lakini kumbe Mungu alikuwa ana malengo makubwa sana na hizo barua..

Hapa tumechukua mifano ya hawa watatu Timotheo, Tito na Filemoni kwasababu ndio wanaojulikana sana..

Lakini pia katika maandiko pia kulikuwa na mtu mwingine wa kipekee sana, ambaye hajulikani sana lakini alichangia pakubwa sana katika uandishi wa vitabu vya biblia.. mtu huyu si maarufu sana ukilinganisha na hawa wakina Timotheo..

Na mtu huyo si mwingine zaidi ya THEOFILO MTUKUFU.

Kama vile kulivyokuwa na waraka wa kwanza na wa pili Paulo aliomwandikia Timotheo, kulikuwepo pia na waraka wa kwanza na wa pili kwa Luka aliomwandikia huyu mtu anayeitwa Theofilo.

Wengi wetu hatujui kuwa kitabu cha Luka na cha Matendo ya Mitume, ni nyaraka maalumu kwa mtu Fulani, hazikulengwa kwa watu wote, au kwa kanisa kwa ujumla…bali zilikuwa ni barua maalumu kwa mtu Fulani ambaye ndiye huyu Theofilo, yaani maana yake ni kwamba kitabu cha Luka na Matendo ya Mitume.. kwa lugha nyingine kingeweza kuitwa Waraka wa Kwanza kwa Theofilo, na waraka wa pili kwa Theofilo..Kwasababu vitabu hivyo viwili vilikuwa ni waraka kwa Theofilo kama kitabu cha Timotheo wa kwanza na wa pili.

Sasa huyu Theofilo alikuwa ni nani?

Kwa ufupi ni kwamba huyu Theofilo, alikuwa ni mkuu fulani, ambaye inasemekana alikuwa Mrumi, na wala hakuwa myahudi. Alikuwa ni mtu mwenye cheo, lakini alikuwa ni mtu wa kipekee sana.

Kwani ulifika wakati akasikia habari zinazomhusu Yesu, na Mitume wake pamoja na Paulo. Lakini hakuwa na uhakika nazo, huku anasikia hichi kule anasiki kile n.k Kipindi anasikia hizo habari, tayari Bwana Yesu ameshaondoka na Mtume Paulo alikuwa ameshakuwa mzee sana, na Mitume walikuwa wameshatawanyika duniani kote..

Hivyo alichikifanya kwasababu alikuwa ni mtu mkubwa, na mwenye cheo, kwa hekima alikwenda kumtafuta mtu mmoja anayeitwa Luka ambaye alikuwa anatembea sana na Mtume Paulo katika safari zake.

Na lengo la kumtafuta huyu Luka ni ili apate taarifa za kutosha na uhakika wa mambo aliyokuwa anayasikia na kuambiwa na watu yamhusuyo Yesu na Mitume wake. Hivyo akamsihi na kumwomba amuandikie kwa waraka mambo yote, tukio moja baada ya lingine tangu kuzaliwa kwa Yesu, kupaa kwake na Matendo yake yote, pamoja na matendo yote ya Mitume.

Hatujui alimsapoti Luka kwa kiwango gani, kwaajili ya kuifanikisha hiyo kazi, lakini aliifanya kwa moyo.

Na Luka kwasababu alikuwa ni mmoja wa watu waliokuwa wanapenda Mungu na mwenye elimu kubwa ya ufalme wa Mungu, na hata ya kidunia,(kwani alikuwa ni Tabibu) alimuandikia huyu Mtukufu Theofilo, tukio moja baada ya lingine, tangu kuzaliwa kwa Yesu, mpaka kupaa kwake mbinguni, na hakuishia hapo tu..bali akaendelea kumwandikia habari za mitume wake aliowaacha baada ya kupaa kwake..

Akamwandikia matendo yao, jinsi walivyohubiri injili kwa nguvu za Roho na kufanikiwa kuanzia Yerusalemu mpaka mwisho wa dunia.. Na huko huko akamwelezea pia habari za Paulo jinsi alivyoipeleka injili kwa mataifa yote, safari zake na mafanikio yake yote.

Na Luka baada ya kukusanya taarifa hizo na kuziandika, ndipo akamtumia huyu Theofilo nyaraka hizo…Na nyaraka hizo ndizo tunazozisoma leo ambazo ni kitabu cha LUKA NA MATENDO YA MITUME.

Na bila shaka Theofilo baada ya kuzipokea nyaraka hizo mbili, aliridhika pakubwa sana, utata ukaondoka kichwani mwake na akamtukuza Mungu..na kuelewa na kupata uhakika wa mambo yote..

Hebu kwa ufupi tusome muhtasari wa nyaraka hizo Luka alizomwandikia Theofilo, na kisha tuende kutazama ni nini tunachoweza kujifunza kutoka kwa huyu mtu.

Luka 1:1 “Kwa kuwa watu wengi wametia mikono kutunga kwa taratibu habari za mambo yale yaliyotimizwa katikati yetu,

2 kama walivyotuhadithia wale waliokuwa mashahidi wenye kuyaona, na watumishi wa lile neno tokea mwanzo,

3 NIMEONA VEMA MIMI NAMI, KWA KUWA NIMEJITAFUTIA USAHIHI WA MAMBO HAYO YOTE TANGU MWANZO, KUKUANDIKIA KWA TARATIBU, THEOFILO MTUKUFU,

4 UPATE KUJUA HAKIKA YA MAMBO YALE ULIYOFUNDISHWA”.

Huo ni waraka wa kwanza wa Luka aliomwandikia Theofilo Mtukufu..waraka mwingine wa pili ni kama ufuatao..

Matendo  1:1 “ Kitabu kile cha kwanza nalikiandika, THEOFILO, katika habari ya mambo yote aliyoanza Yesu kufanya na kufundisha,

2 hata siku ile alipochukuliwa juu, alipokuwa amekwisha kuwaagiza kwa Roho Mtakatifu wale mitume aliowachagua;

3 wale aliowadhihirishia nafsi yake, kwa dalili nyingi, baada ya kuteswa kwake, ya kwamba yu hai, akiwatokea muda wa siku arobaini, na kuyanena mambo yaliyouhusu ufalme wa Mungu”.

Huo ni waraka wa pili wa Luka aliomwandikia huyu Theofilo.

SASA NI NINI TUNAJIFUNZA KWA THEOFILO?.

Kabla ya kujua ni nini tunajifunza hebu tafakari ni mambo mangapi mazuri na ya kujenga tunayoyapata ndani ya hivyo vitabu viwili vya LUKA na MATENDO YA MITUME?.

Kama wewe ni msomaji wa biblia utajua ni jinsi gani, vitabu hivyo viwili vilivyokuwa vya muhimu na vyenye mafunzo mengi ya kiimani.

Theofilo aliona si vyema kusikia habari za Yesu juu juu tu, alitaka kujua alizaliwaje, katika mazingira gani, ndugu zake ni wakina nani, alihubiri nini, kwa muda gani, na alikufaje, alifufukaje na yupo wapi sasa hivi..Pengine alitaka hivyo kwa ajili ya faida yake na ya watoto wake na ndugu zake..

Lengo ni ili asipelekwe pelekwe na kila upepo wa elimu uliozagaa huko na huko, ili asichukuliwe na upotoshaji unaomhusu Yesu na wanafunzi wake..Hivyo akamtafuta Luka ambaye alikuwa ni mwenye elimu nyingi, na mwanafunzi wa Imani ya kikristo, amwandikie kwasababu aliamini ndiye chanzo salama na sahihi cha taarifa kwa wakati huo.

Na Luka akatimiza kiu yake kwa kumtafutia habari hizo kwa urefu na kumwandikia zote.

Ndio maana hapo Luka unaona anamwambia “NIMEONA VEMA MIMI NAMI, KWA KUWA NIMEJITAFUTIA USAHIHI WA MAMBO HAYO YOTE TANGU MWANZO, KUKUANDIKIA KWA TARATIBU, THEOFILO MTUKUFU”

Na kama tulivyojifunza, huyu Theofilo hakuridhika kusikia habari za Yesu tu! Na matendo yake..bali alizidi kutamani kujua Matendo ya Mitume wa Yesu kwa urefu.. kwani alikuwa anasikia tu habari za Mitume wake juu juu, alikuwa anamsikia tu Paulo, lakini yeye akataka kujua huyu Paulo ni nani, ni jinsi gani alimpokea Yesu, safari zake zilikuwaje, ni nini aliyopitia akiwa safarini, hatua kwa hatua..na Luka akamwandikia habari zote hakuacha kitu!

Hebu jiulize kwa kupitia safari na maisha ya Paulo tunayoyasoma katika kitabu cha Matendo ya Mitume tumejifunza mangapi leo?, Bila shaka ni mengi sana.. tumejifunza kumbe katika safari ya imani kuna kupanda na kushuka, wakati mwingine kuna kupitia dhiki na vifungo n.k.

Hivyo Theofilo kwa kutamani kuyajua hayo, na kutafuta kwa bidii taarifa hizo za Bwana Yesu, imekuwa msaada na kwetu sisi pia.

Kadhalika na sisi tunajunza hayo hayo…

Kwamba hatuna budi kuwa kama Theofilo..kuhusiana na masuala ya ufalme wa Mbinguni..

 tunapotia bidii kutafuta kulijua Neno la kweli la Mungu, taarifa zile haziji kutusaidia sisi peke yetu, bali pia wengine, na hata vizazi vijavyo.. kwasababu kwa kutafuta huko..kutakuja kuwafaa wengine na kuwabariki wengine huko mbeleni, na kuwa kumbukumbu bora kwetu.

Unapoona Neno katika maandiko hulielewi kwanini usitafute kwa bidii kulijua na kisha kuliandika au kuwafundisha wengine au watoto wako kwa msaada wa wao?..Leo utaona halina maana lakini hujui Mungu kalikusudia nini mbeleni.

Pengine Theofilo aliutaka ule waraka kwa faida yake tu na watoto wake, kumbe Mungu alikuwa na mpango na huo waraka kwa mamilioni ya watu huko mbeleni. Hata sisi kuna mambo ambayo tunaweza kuyafanya sasa, tukidhani yanaishia hapa tu kumbe Mungu ana malengo nayo kuwa msaada kwa maelfu ya watu mbeleni..

Hebu jiulize ni taji kubwa kiasi gani alilonalo huyu Theofilo?.. ambaye hata hakuwa Myahudi?..

Siku ile atasimama na kumwambia Bwana kwa utafiti wake na bidii yake ya kutaka kujua habari za Kwake na Mitume wake, imekuwa Baraka watoto wake na ndugu zake, lakini Bwana atamwonyesha mabilioni ya watu katika vizazi vya mbeleni waliobarikiwa kwa jitihada yake hiyo..

Kwasasa huyu Theofilo hajui chochote kwasababu kalala, lakini siku ya ufufuo, ndipo atakapojua jinsi thawabu yake ilivyo kubwa..Na naamini kama angejua angetafuta pia habari nyingine nyingi ili apate taji bora zaidi.

Kwa bidii yake kitabu cha Luka na Matendo ya Mitume kimeweza kuwepo!.

Mathayo 8:11 “Nami nawaambieni, ya kwamba wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi pamoja na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni”

Na sisi Bwana atujalie tufanye jambo ambalo litatusaidia sisi na vizazi vijavyo..

Marana atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

WEKA KUMBUKUMBU YA MAMBO BWANA ANAYOKUFANYIA KWASABABU YATAKUFAA MBELENI.

WALA MSIUANGALIE MWILI, HATA KUWASHA TAMAA ZAKE.

Uchaji ni nini kama tunavyosoma katika 1Timotheo 2:10?

USIPUNGUZE MAOMBI.

Rudi nyumbani

Print this post

FAHAMU JINSI MUNGU NA SHETANI WANAVYOZUNGUMZA NA WATU.

Ulishawahi kuyatafakari kwa makini haya maneno ya Bwana Yesu?

Yohana 8:38 “Niliyoyaona kwa Baba ndiyo niyanenayo; nanyi vivyo hivyo mliyoyasikia kwa baba yenu ndiyo myatendayo”.

Maneno hayo aliwaambia wayahudi (Mafarisayo na waandishi) kipindi kile walipotaka kumuua?. Lakini unaweza kujiuliza ni lini walishakaa chini na kumsikiliza shetani, akizungumza nao kisha akawapa maagizo ya kumwangamiza Bwana Yesu? Ni lini?

Hatuwezi kudhani kuwa shetani alishawahi kukaa chini, na kuanza kunong’ona kwenye masikio yao, na kuwaambia “sasa wanangu wakati wa kumuua Yesu umefika haya nendeni”, Hilo halipo, lakini Bwana Yesu hawezi kusema uongo, ni lazima aliwaona wakimsikiliza shetani, kisha wakaitii sauti yake, na wakafanikiwa kuyafanya yale yote waliyoagizwa na shetani kutenda.. Na ndio maana ukiendelea kusoma pale, utaona anasema..

Yohana 8:44 “Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na TAMAA ZA BABA YENU NDIZO MPENDAZO KUZITENDA. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo”.

Ndugu, sauti ya shetani, kamwe usitazamie utaisikia katika maono au ndoto, au kwa mapepo, hali kadhalika sauti ya Mungu vivyo hivyo, Utaisikia sauti ya Mungu kwa kutazama tu yale Mungu anatenda.. Vilevile utaisikia na kuielewa sauti ya shetani pale unapotazama ni nini anatenda..

Kwamfano, tukianzana na hawa wayahudi, ilifikia wakati walimwonea Yesu wivu kisa Mungu anamtumia kwa ukamilifu wote kuwavuta watu wote kwenye nuru, hapo ndipo wakaingiwa na wazo la kutaka kumuua, wazo ambalo walishawahi kuona watu fulani huko nyuma wakilifanya likawaletea matunda, na wao pia wakalichukua. Kumbe hawajui hilo wazo ndio sauti ya shetani yenyewe ikiwapa maelekezo.

Hata leo, wazo la wewe kutaka kurudi nyuma kuzini, tayari hiyo ni sauti ya shetani, na ndio hapo unaitii kwa kuanza kutazama picha za ngono mitandaoni,  unafanya punyeto, unakwenda disco, unatazama muvi zenye maudhui ya mapenzi mapenzi wakati wote, hujui kuwa ni tamaa za ibilisi unazozifanya.. yaani katika ulimwengu wa roho, Yesu anakuona umeketi na shetani kwenye meza moja, ukimsikiliza sauti yake kwa makini sana.

Lakini vivyo hivyo kwa watoto wa Mungu pia kanuni ni ile ile, nao wanamsikiliza Mungu kwa kumtazama vile atendavyo, Kama vile Bwana Yesu alivyosema “Niliyoyaona kwa Baba ndiyo niyanenayo”. Sio maono, hapana, Bwana aliona kazi nyingi za Mungu ulimwenguni hivyo akaziiga akazitenda..

Kwamfano moja ya kazi ambazo Yesu aliziona Baba yake anazifanya akaiga ni pamoja na kuwa na HURUMA,  KUSAMEHE, KUWAPENDA MAADUI na KUFADHILI hata kwa wasio na shukrani.

Luka 6:35 “Bali wapendeni adui zenu, tendeni mema, na kukopesha msitumaini kupata malipo, na thawabu yenu itakuwa nyingi; nanyi mtakuwa wana wa Aliye juu, kwa kuwa yeye ni mwema kwa wasiomshukuru, na waovu.

36 Basi, iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma.

Unaona, hivyo na wewe ukionyesha tabia hizo, kuonyesha fadhili kwa watu wasio na malipo kwako, basi rohoni unaonekana umeketi na Mungu kwenye meza moja ukimsikiliza kwa makini akikupa maagizo ya kufanya, hiyo ni zaidi ya sauti, au ndoto, au maono elfu kumi, unayoweza kuyasikia.

Mathayo 5:46 “Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo?

47 Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo?

48 Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu”.

Kwahiyo, tujifunze kuitambua sauti ya Mungu wetu kwa kuzitazama kazi zake, vilevile tujifunze kuielewa sauti ya adui yetu ibilisi, ili tuweze kumkwepa na yeye, kwasababu kamwe tusitazamie, sikumoja atakuja kutunong’oneza kwenye masikio yetu “nenda ukazini”, hilo halipo.

Je! Umeokoka? Je! Unafahamu kuwa tupo katika muda wa nyongeza tu, siku yoyote Kristo anarudi. Unasubiri nini huko nje? Utajisikiaje usikie unyakuo umepita halafu wewe umebaki, utamweleza nini Bwana Yesu. Tubu dhambi zako leo kwa kumaanisha kabisa kumrudia Mungu wako, injili tuliyobakiwa nayo sio ya kubembelezewa wokovu tena, ni wewe mwenyewe kuona na kuchukua hatua. Muda umeisha.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Je ni kweli imani ya mtu ndiyo itakayomuokoa, na si kitu kingine?

UNYAKUO.

TUMEFANYIKA KUWA WANA WA MUNGU!

Bahari mbalimbali zilizoorodheshwa kwenye biblia.

Rudi nyumbani

Print this post

Kisima cha joka na lango la jaa ni nini?(Nehemia 2:13)

SWALI:Bwana Yesu asifiwe naomba kuelewa “Kisima cha joka”  na “lango la jaa” vina maana gani kama tunavyosoma katika Nehemia 2:13


JIBU: Nehemia alipopata taarifa juu ya uharibifu wa mji wa Yerusalemu, alifunga na kumwomba Mungu kwa muda mrefu, ili aende kuujenga tena mji huo, ndipo Mungu akasikia maombi yake na kumfungulia mlango wa kwenda Israeli kwa ajili ya kazi hiyo ya ukarabati.

Sasa kama tunavyosoma alipofika,hakusubiri sana, bali aliondoka usiku wa tatu yeye ni baadhi ya watu wachache, ili kuuchunguza kwanza mji, jinsi kuta zake zilivyoharibiwa. Na kati ya sehemu tano (5) alizopita mojawapo ilikuwa ni hapo penye kisima cha joka, na lango la jaa.

Kisima cha joka: Ni kisima kilichokuwa kando ya kuta za mji, kinaaminika, kiliitwa hivyo kutokana na umbile la mdomo wake jinsi ulivyofanana na nyoka., japo wengine wanaamini kuwa hapo kale kilitumiwa na wapagani kwa ajili ya miungu yao ya majini, waliyoitambua kwa jina la joka. Hivyo jina la kisima hicho liliendelea kuwa hilo hadi wakati wa baadaye, Japo hilo halijathibitishwa ni kulingana tu na mapokeo kwasababu biblia haijaeleza sababu ya kuitwa vile.

Lango la Jaa: Jaa kwa jina lingine ni jalala, hivyo, lango hili lilitumika kutolea uchafu wote wa mji (kinyesi). Huko nako Nehemia alifika.

Nehemia 2:11 Basi nikafika Yerusalemu, nikakaa huko muda wa siku tatu.

12 Kisha nikaondoka usiku, mimi na watu wachache pamoja nami; wala sikumwambia mtu neno hili alilolitia Mungu wangu moyoni mwangu, nilitende kwa ajili ya Yerusalemu; wala hapakuwa na mnyama pamoja nami, ila mnyama yule niliyempanda mwenyewe.

13 Nikatoka nje usiku, kwa njia ya LANGO LA BONDENI, nikashika njia IENDAYO KISIMA CHA JOKA, na LANGO LA JAA; nikazitazama kuta za Yerusalemu, zilizokuwa zimebomoka; na malango yake yameteketezwa kwa moto.

14 Kisha nikaendelea mpaka lango la chemchemi, na ziwa la mfalme; lakini hapakuwa na nafasi ya kupita kwa yule mnyama aliyekuwa chini yangu.

15 Kisha nikapanda usiku kando ya kijito, nikautazama ukuta; kisha nikarudi nyuma, nikaingia kwa lango la bondeni, nikarejea hivyo.

Lakini  baada ya hayo yote tunaona, Nehemia haraka na mapema alianza ujenzi wa kuta za mji. Na kazi ikaja kukamilika kwa ufasaha wote,licha ya kupitia vipingamizi na vikwazo vingi kutoka kwa maadui zao.

Ni ujumbe gani tunaupata kutoka katika mawazo hayo ya Nehemia?

Ni kwamba hatuwezi kukarabati kitu bila kujua uharibifu wake upo wapi. Ni jinsi gani wakristo, tunapaswa tufumbue macho yetu tuone, uharibifu shetani aliousababisha kwenye kazi ya Mungu, jinsi watoto wanavyoharibiwa, jinsi vijana walivyopotoka kila kukicha, jinsi maasi yanavyoendelea kanisani.., Tukiyaona hayo hapo ndipo wote kwa pamoja tutaona sababu ya kumtumikia Mungu, kwa ushirikiano.

Vinginevyo tutaona kila siku mambo yote ni sawa tu, kama wale watu wa Mji Nehemia alivyowakuta wame RELAX.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Jaa ni nini katika biblia?

“Shinikizo” ni nini kibiblia, Na maana yake rohoni ni ipi?

saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada

Jehanamu ni nini?

UFUNUO: Mlango wa 12

Rudi nyumbani

Print this post

Makerubi wenye sura nne, ni kweli wapo? na je! wanyama wataenda mbinguni?

SWALI: Wale  Makerubi wenye sura nne, ni kweli wapo au ni mfano wa picha tu? Na je! wanyama wataenda mbinguni?


Jibu: Awali ya yote ni muhimu kufahamu kuwa viumbe vyote na kila kitu tunachokiona duniani kimeumbwa kwa taswira ya viumbe na vitu vya mbinguni.

Kuanzia mwanadamu mpaka wanyama, ndege pamoja na mimea na vito, vyote vimeumbwa kwa taswira ya vitu vya mbinguni… Isipokuwa vya mbinguni vina utukufu mwingi kuliko vya duniani.

Kwamfano tukianza na mwanadamu.. Maandiko yanasema kaumbwa kwa “sura na mfano wa Mungu”.. Maana yake kimwonekano, mwanadamu anafanana na Mungu, lakini si Mungu.

Kadhalika tukimtazama ng’ombe, simba na tai.. Nyuso zao hizo zimeumbwa kwa taswira ya aina fulani ya malaika waliopo mbinguni, wajulikanao kama Makerubi.. Kwasababu Makerubi wana nyuso Nne, maandiko yanasema hivyo.

Ufunuo 4:6 “Na mbele ya kile kiti cha enzi kulikuwa na mfano wa bahari ya kioo, kama bilauri; na katikati ya kile kiti cha enzi, na pande zote za kile kiti, WALIKUWAKO WENYE UHAI WANNE, wamejaa macho mbele na nyuma.

7 NA HUYO MWENYE UHAI WA KWANZA ALIKUWA MFANO WA SIMBA; NA MWENYE UHAI WA PILI ALIKUWA MFANO WA NDAMA; NA MWENYE UHAI WA TATU ALIKUWA NA USO KAMA USO WA MWANADAMU; NA MWENYE UHAI WA NNE ALIKUWA MFANO WA TAI ARUKAYE”.

Kadhalika wapo farasi wa kimbinguni, (Ufunuo 19:14) na wapo wa kiduniani.. na vile vile vipo vito vya kimbinguni na vya kiduniani..

Kwahiyo, tukirudi kwenye swali letu? Je ni mbinguni wapo kweli wale wenye uhai wanne?, jibu ni ndio wapo! na si nadharia tu!.. tukifika huko tutawaona.. Nabii Ezekieli aliwaona kwenye maono, Yohana naye aliwaona na sisi pia tutawaona.

Na kama hivyo ndivyo, je wanyama nao wataenda mbinguni?

Jibu ni hapana! Hakuna Twiga, wala mbwa, wala simba, wala ng’ombe wala tai arukaye, atakayeenda mbinguni.. Hivyo vyote ni viumbe vya kidunia.. vimeumbwa kutoka mavumbini, na havina nafsi iliyo hai.. maana yake vikifa vimekufa vinarudi mavumbini, havina ufufuo..Na mavumbi hayawezi kuingia mbinguni.

Ni mwanadamu peke yake aliye na ahadi ya kuingia mbinguni, (Na si wanadamu wote bali wale waliooshwa dhambi zao kwa damu ya Mwanakondoo) ambapo siku ya unyakuo itakapofika watafufuliwa na kisha kuvaa miili ya kimbinguni, lakini hawataingia mbinguni na hii miili ya mavumbi.. bali watabadilishwa na kuvikwa ya kimbinguni.

1Wakorintho 15:50 “Ndugu zangu, nisemayo ni haya, ya kuwa nyama na damu haziwezi kuurithi ufalme wa Mungu; wala uharibifu kurithi kutokuharibika.

51 Angalieni, nawaambia ninyi siri; hatutalala sote, lakini sote tutabadilika,

52 kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika.

53 Maana sharti huu uharibikao uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa”.

Sasa wanyama wenyewe hawana hiyo ahadi ya kufufuliwa na kuvikwa miili ya utukufu, na wala Kristo hajawafia wao.. ndio maana unaona hakuna mahali popote katika maandiko, inayoonyesha mfano wa mnyama yoyote kufufuliwa.

Na kama wapo wanadamu tu ambao wataikosa mbingu.. mnyama ni nani aweze kuingia?

Waliokombolewa kwa damu ya mwanakondoo, hao peke yao ndio walioahidiwa kwenda mbinguni.. lakini wanadamu wengine wote, ikiwemo wanyama na miti, na nzige, na bakteria hawana nafasi mbinguni..wakifa wamekufa, kama vile mti ukifa unavyopotea, hauna ufufuo wowote.

Sehemu pekee ambayo maandiko yanasema wanyama watakuwepo, ni katika ule utawala wa miaka elfu, hapa duniani tutakapotawala na Kristo. Huko ndiko wanyama watakuwepo. Kwa maelezo marefu kuhusu utawala huu unaweza  kuupata kupitia hapa > Utawala wa miaka elfu

Lakini itoshe kusema tu kwamba! Mbinguni hakitaingia kinyonge

Ufunuo 21:27 “Na ndani yake hakitaingia kamwe cho chote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo, bali wale walioandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo”.

Je na wewe unafanya machukizo? Je umeokoka?.. kama bado basi fahamu kuwa hutakwenda mbinguni, kwasababu huko haviingi vinyonge na wafanyao machukizo, huko hawaingii waasherati, walevi, wazinzi, watu wanaoupenda ulimwengu kuliko kumpenda Mungu.. n.k

Hivyo mpokee Yesu leo, uoshwe dhambi zako, ili uwe na uhakika wa kuingia mbinguni katika makao ya furaha ya daima.

Unyakuo upo karibu na Bwana yuaja.


Mada Nyinginezo:

Naomba kufahamu maana ya “sura ya kijiti” katika Marko 12:26.

Biblia inamaanisha nini inaposema “Mwenye haki huufikiri uhai wa mnyama wake”?

Je! Kuna malaika wangapi mbinguni?

HEKIMA YA KIMUNGU, INAINGIAJE MIOYONI MWETU?

Bahari mbalimbali zilizoorodheshwa kwenye biblia.

Rudi Nyumbani:

Print this post

UTAYAFIKIAJE MANENO SAFI YA MUNGU?

Watu wengi wanasoma biblia lakini si wote wanayafikia maneno SAFI YA MUNGU. Jambo ambalo watu wengi hatujui ni kuwa tunadhani, tunapoisoma biblia kwa mara moja, tayari tumeshayafikia “maneno safi ya Mungu”, yale yenye uwezo wa kubadilisha Maisha yetu katika ubora wote.

Ni vizuri ukafahamu hii biblia tunayoisoma, haipo wazi kama unavyodhani, ni kitabu kilichoficha maneno SAFI YA MUNGU (Pure word of God), Ambayo hayapatikani hivi hivi tu, kwa usomaji wa kawaida tuliouzoea sikuzote. Watu ambao wanauwezo wa kufikia hapa, basi Maisha yao ya kiroho yanakuwa na mageuzi makubwa sana, kutokana na nguvu ya Neno hilo.

Leo kwa neema za Bwana tutaona mtu anawezaje kuyafikia maneno haya;

Biblia imefananisha Neno la Mungu na madini ya fedha (Silver), sehemu nyingine na Dhahabu.

Sasa ukisoma, Zaburi 12:6 inasema..

Zaburi 12:6 “Maneno ya Bwana ni maneno safi, Ni fedha iliyojaribiwa kalibuni juu ya nchi; Iliyosafishwa mara saba”.

Maana yake ni kuwa, ili uweze kufahamu haya “Maneno safi ya Mungu” yanapatikanaje, unapaswa utazame jinsi Fedha/dhahabu safi, inavyopatikana na kusafishwa.

Kwa kawaida, madini haya yanapochimbwa, huwa hayang’ai kama unavyoona katika maduka ya VITO vya thamani. Bali yanakuwa kama miamba tu, au maudongo udongo, yaani dhahabu halisi inakuwa imechanganyikana sana na uchafu wa aina  mbali mbali.

Hivyo wanachokifanya ili kuitoa takataka hizo katikati ya madini, ni kwenda kuiyeyusha katika joto kali sana. Hiyo inapelekea, uchafu kujitenga na fedha, kwani zile takataka zote zinapanda juu, na ile fedha/dhahabu, inabaki chini, kisha wanauzoa ule uchafu wote uliokuja juu, baadaye wanaicha igande tena kisha inatokea dhahabu yenyewe.

Sasa kwa kawaida,wafua fedha/dhahabu, wengine wanairudia hiyo hatua mara mbili au tatu, na kwa jinsi wanavyoirudia mara nyingi na kuondoa hata zile takataka ndogo sana, ndivyo, dhahabu hiyo inavyozidi kuleta mng’ao mzuri sana na wakuvutia sana.

Hivyo Mungu alitumia mfano huo kuonyesha pia jinsi NENO LAKE SAFI, linavyopatikana. Ni kama fedha iliyosafishwa MARA SABA katika moto,. Ikiwa na maana kuwa, zipo hatua saba, za kulifikia NENO safi la Mungu, alilokusudia limletee matokea makubwa katika Maisha yake..

Sasa hii mara saba, mtu anaifikiaje?

Ukiwa ni mtu wa kusoma biblia mara moja tu, na kujiona kuwa tayari umeshajua kila kitu, ufahamu kubwa hapo bado hujalifikia hili Neno safi la Mungu. Kulifikia kunahitaji utulivu, na pia kulitafakari tena na tena, na tena, na tena, kila siku, na sio kusoma tu kama gazeti.

Kwamfano leo unaweza kusoma habari za wana wa  Israeli jinsi Mungu alivyowatoa katika nchi ya Misri, kwa mara ya kwanza ukaielewa kama stori tu, lakini ukigotea hapo, ukasema tayari nimeshaelewa hapo, sina haja ya kurudia tena siku nyingine.. Nakuambia biblia kwako itakuwa haina tofauti na vitabu kingine cha kihistoria ulichowahi kusoma huko nyuma.

Lakini ukasema siku nyingine nitatafakari, kisha ukamwomba Mungu, na kukaa katika utulivu ukairudia habari ile, utaona jambo jipya, limefunuliwa ndani yako, ambalo hukuwahi kulijua hapo mwanzo..

Wakati mwingine tena ukamwomba Roho Mtakatifu akusaidie, kisha ukarudia tena kusoma habari ile ile, utashangaa jambo lingine jipya unalipata ambalo siku za nyuma hukulipata..

Hivyo hivyo unavyozidi kuendelea, kurudia na kurudia ndivyo unavyolisafisha Neno la Mungu ndani yako,, Na matokeo yake ni kuwa, nguvu za Neno lake zinapenya katika roho yako, na kuleta mabadiliko makubwa sana, maishani mwako.

Shida inakuja pale, tunapodhani tumeimaliza biblia yote, pale tunaposoma habari Fulani na kujisemea moyoni, Aaah, tayari, yule kipofu Yesu aliishia kumpaka mate machoni akapona.. hivyo tunapita juu juu tu, kama sio kuiruka habari yote.

Wakati mwingine kanisani, unafundishwa, somo ambalo pengine ulishawahi kulisikia huko nyuma, na wewe badala ya kuwa mtulivu rohoni kusikiliza kwa makini, unasema, tayari hili nalifahamu..

Kumbuka, maneno safi ya Mungu, yanapatikana katika matanuru saba.

Hivyo natumai, kuanzia sasa sote, tutaacha kuwa wavivu wa kuyatafakari maandiko. Kwasababu lengo letu ni kuona nguvu za  Neno la Mungu kweli zikifanya katika Maisha yetu ya wokovu. Tujitahidi sana kujifunza biblia.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

JINSI ROHO MTAKATIFU ANAVYOWAFUNULIA WATU MAANDIKO.

EPUKA KUPELELEZA KILA KITU MUNGU ANACHOKUAHIDIA.

Biblia inamaana gani kusema “vipo sita, naam saba”?

YESU NI MFALME WA AINA GANI KWAKO? 

DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.

Rudi nyumbani

Print this post

Je Adamu na Hawa, walikuwa hawafanyi mema kabla ya kula tunda?

SWALI: Ni mema gani na mabaya gani, Adamu na Hawa waliambiwa watayajua?, Kwasababu Kama ni mema siwalikuwa wanayafanya hapo kabla?


JIBU: Ili tuweze kuelewa vizuri, tujifunze katika mifano ya kawaida ya maisha.

Haiwezekani mtu kujijua kwamba yeye ni mrefu kama hajakutana na mtu mfupi katika maisha yake..

Yeye siku zote atajiona yupo kawaida tu..lakini siku atakapokutana na aliowazidi kimo ndipo atakapojijua kumbe yeye ni mrefu.

Kadhalika haiwezekani kujijua kama kwasasa una afya kama hujawahi kupitiaga kuumwa…zaidi ya yote hutajua hata maana ya kuwa na afya ni nini.

Lakini siku ile utakapougua na hamu yote ya kula kupotea, ndipo utakapojijua kuwa kumbe siku kadhaa nyuma ulikuwa ni mwenye afya sana.

Vile vile haiwezekani kujijua kuwa unatenda wema kama hujawahi kuujua ubaya…

Wewe utakuwa unaufanya tu! Na kuona kawaaida, Lakini hutajua kama unachofanya ni kitu chema…siku utakapokuja kuuona ubaya, ukifanywa na mwingine..ndipo utakapojua kuwa kumbe wewe ulikuwa mwema. N.k

Sasa hiyo ni mifano tu ya kimaisha,Sasa tukirudi pale Edeni,jambo ni lile lile, Adamu na Hawa walikuwa wanatenda mema lakini walikuwa hawajijui kama wanatenda mema, mpaka siku walipofanya ubaya na kuona madhara yake.

Ndio maana Mungu aliwakataza Adamu na Hawa wasile yale matunda, maana yake wasiujaribu ubaya…kwasababu siku watakapoujaribu ndipo watakapojijua kuwa kumbe siku kadhaa nyuma walikuwa katika mema.

Maana yake watajujua kumbe walikuwa katika utakatifu..

Hiyo ndio maana ule mti ukajulikana kama ni mti wa UJUZI WA MEMA NA MABAYA …Na si mti tu wa UJUZI WA MABAYA..hapana! bali mema na mabaya.. kwasababu mambo hayo mawili yanakwenda pamoja…hayaachani…

Kadhalika na sisi tunapokuwa dhambini tunakuwa tunajiona tupo sawa na njia zetu hizo, Hatujioni kama tupo hatarini, wala matatizoni, tunaona ni kawaida maisha ndivyo yalivyo..

Lakini siku tunapompokea Yesu, na kuonja Mema.. ndipo macho yetu yanafumbuliwa na kuelewa kwamba kumbe maisha tuliyokuwa tunaishi yalikuwa ni maisha mabaya, yalikuwa yana kasoro nyingi, yalikuwa ni ya mateso, yalikuwa ya tabu na hatari…lakini tulipokuwa huko dhambini tulikuwa hatulioni hilo..

Na YESU KRISTO, Ndiye ule MTI WA UZIMA.
Kwamba kila atakayeonja matunda ya mti ule hatatamani tena mabaya..na macho yake yatafumbuliwa, na kujitambua na hivyo kujitenga mbali na dhambi..

Adamu na Hawa walipokula na kujijua kuwa wapo dhambini walitamani kurudi, lakini walishindwa kwasababu njia ilifungwa.

Lakini sasa njia imefunguliwa, ipo wazi na njia hiyo si nyingine zaidi ya YESU KRISTO.
Ni kwasababu gani leo unaona ulevi unaoufanya ni kawaida?..ni kwasababu bado hujampokea Yesu na macho yako kufumbuliwa..siku utakapoocha kipawa cha Roho Mtakatifu ndipo utajiona kuwa hizo pombe zilikuwa ni sumu, huo uasherati ulikuwa ni kitanzi na wala hauna raha yoyote zaidi ni mateso..

Ndipo utakapojua kuwa kumbe maisha ya chuki, vinyongo na visasi yalikuwa ni maisha ya shida.

Bwana leo anatuita wote..na anasema tuonje!..Maana yake tujaribu kula matunda hayo ya mti wa uzima, tuone kama tutatamani kubaki dhambini.

Zaburi 34:8 “Onjeni mwone ya kuwa BWANA yu mwema; Heri mtu yule anayemtumaini”.

Je! Umempokea Kristo?

Kama bado mlango wa kutubu upo wazi sasa, lakini hautakuwa hivyo siku zote. Mpokee Yesu leo akutue mizigo na utapata raha ambayo hujawahi kuipata.

Mathayo 11:28 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha

29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu”

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

JINSI EDENI ILIVYOKUWA.

Biblia imemaanisha nini iliposema “hawezi mtu kusema, Yesu ni Bwana, isipokuwa katika Roho Mtakatifu”

JIFUNZE KUELEWA MAANA YA KUOA/KUOLEWA KABLA YA KUINGIA HUKO.

MTI WA UZIMA NA MTI WA MAARIFA.

Kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?

Rudi nyumbani

Print this post

YAPO MAJIRA YA KUONJWA NA BWANA.

Bwana alisema…

Zaburi 34:8

[8]Onjeni mwone ya kuwa BWANA yu mwema; 

Heri mtu yule anayemtumaini.

Maana yake ni kuwa Mungu ametoa nafasi kwa kila mtu ambaye yupo mbali na neema  kuonja au kujaribu kwanza uzuri ulioko ndani yake kabla hajauingia moja kwa moja..kwamfano kujaribu kungalia kama ndani ya Kristo kuna furaha, au amani, au upendo n.k.

Na pale mtu anapoona kuwa ipo basi anawajibika kumuishia Mungu maisha yake yote, lakini kama hajaiona basi anaruhusiwa kughahiri uamuzi wake..Na Ukweli ni kwamba hakuna aliyemjaribu Kristo akatamani kutoka baada ya hapo.

Lakini sio sisi tu tunaonja vya Mungu.. Mungu naye pia anayotabia ya kutuonja sisi auminifu wetu na uelekevu wetu kwake kama tunakidhi kweli vigezo vya yeye kutupa moja kwa moja kile tulichomuomba…au kutukaribia moja kwa moja milele.

Sasa hatua kama hii ukishafikia tambua kuwa unapaswa ung’ang’ane kweli kweli kwasababu huwa hakiwi kipindi cha raha sana.

Tukirudi kwenye biblia…tunaona wana wa Israeli walipotoka Misri, Mungu alikuwa nao karibu katika kiila hatua waliyopiga, walichokitaka walikipata wala hawakuachwa bila majibu..mpaka wanavuka bahari ya shamu wote wakawa wanamwimbia Mungu na kumchezea kwa shangwe kwa jinsi alivyowatendea miujiza mikubwa..Hivyo hilo likamvutia Mungu sana..Mungu akashawishika kushuka atembee nao milele katika furaha na raha..

Lakini kabla ya yeye kufanya vile ilimpasa kwanza AWAONJE..aone kama ni kweli wamekidhi vigezo vya yeye kuwa Mungu wao au la.

Hivyo alichofanya ni kuwaacha siku tatu kwa Kiu kule janwani pindi tu walipovuka bahari ya shamu, jambo ambalo hawajawahi kulipitia kabisa maisha yao yote tangu walipoanza kutembea na Mungu.. 

Tusome…

Kutoka 15:22-25

[22]Musa akawaongoza Israeli waende mbele kutoka Bahari ya Shamu, nao wakatokea kwa jangwa la Shuri; wakaenda safari ya siku tatu jangwani wasione maji.

[23]Walipofika mahali palipoitwa Mara hawakupata kuyanywa yale maji ya Mara, kwa kuwa yalikuwa machungu; kwa ajili ya hayo jina lake likaitwa Mara.

[24]Ndipo watu wakamnung’unikia Musa, wakisema, Tunywe nini?

[25]Naye akamlilia BWANA; BWANA akamwonyesha mti, naye akautia katika hayo maji, maji yakawa matamu. Basi akawawekea amri na hukumu huko, AKAWAONJA HUKO.

Unaona mstari wa 25 inasema Mungu akawaonja huko.kama kweli walimpenda kutoka moyoni au ni kwa miujiza tu..au kwa mikate tu..au kwa mafanikio tu..

Lakini tunaona wana wa Israeli walinung’unika badala ya kujinyenyekeza..Hivyo Mungu hakuona ukamilifu ndani yao.akajua kumbe walimpendea kwasababu walipata  raha tu lakini sio kwasababu ni Mungu wao..Laiti wangejinyenyeza ni wazi kuwa tangu ule wakati na kuendelea wasingekaa kusikia kitu kinachoitwa shida au taabu au masumbufu…

Ndugu yangu..Mungu akidhamiria kushuka kwako moja kwa moja kukaa na wewe au kukupa kitu fulani ulichomuomba ni sharti kwanza AKUONJE..uaminifu wako kama alivyofanya kwa Ibrahimu kumtoa mwanae Isaka..Hiyo ndio kanuni yake ambayo wana wa Israeli walishindwa kuielewa..

Soma pia Kumbukumbu 8:1-3 utaona Bwana akilisisitiza neno hilo hilo..

Hivyo ndugu uliyeokoka..lijue jambo hilo, liweke akiba moyoni mwako. Kabla hujawa rafiki wa Mungu wa milele ni sharti kwanza akuonje..ukikidhi vigezo basi ndio kimekuwa chako milele.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

BIRIKA LA SILOAMU.

WAOMBEENI WANAOWAUDHI.

UFUNUO: Mlango wa 14

KUOTA MAFURIKO,KUOTA MAJI MENGI,KUOTA MAWIMBI.

Rudi nyumbani

Print this post

Risasi inayotajwa kwenye Ezekieli 27:12 ni ya namna gani?

 Je! ni risasi hizi tunazozijua za bunduki, au ni risasi ya namna gani?.


Jibu: Katika biblia kuna maneno yaliyotumika ambayo yakiletwa katika nyakati zetu, yanabadilika maana kabisa.. kwamfano utaona Neno “fisadi” likitajwa katika biblia.. Maana halisi ya neno hilo sio “mtu anayedhulumu fedha za umma”.. Bali maana halisi ya neno hilo ni “mtu anayefanya uasherati uliovuka mipaka”.

Hali kadhalika kuna neno kama “Fedha”.. Neno hili kama lilivyotumika nyakati za kale ni tofauti na linavyotumika leo, Leo hii ukizungumzia Fedha, moja kwa moja akili zinakwenda katika “Hela” iwe ya noti au sarafu. . Lakini kiuhalisia maana halisi ya neno Fedha sio “Hela”.. Bali ni madini aina ya “Fedha” kama vile yalivyo madini aina ya dhahabu.. Hata pale katika maandiko Bwana aliposema Fedha na dhahabu ni mali yangu,(Hagai 2:8) hakumaanisha “Hela na dhahabu”… bali alimaanisha madini aina ya fedha, na madini aina ya dhahabu, ndio mali za Bwana. ..

Sasa kwanini madini haya ya fedha leo ndio yamegeuzwa maana na kuwa Hela/pesa?..kiasi kwamba hela yoyote leo inaitwa fedha.

 Ni kwasababu tangu zamani hata sasa malighafi inayotumika kutengenezea sarafu nyingi, ni madini hayo ya fedha.. utaona sarafu nyingi, kama zile za sh.10, au 20 au 500 hazijatengenezwa kwa chuma, wala dhahabu bali zimetengenezwa kwa madini ya fedha,..hivyo hiyo ikafanya Hela zote zijulikane kama fedha..siku hizi hata Noti zote zinajulikana kama ni fedha, jambo ambalo kiuhalisia sio sawa.

Na madini ya fedha yanaweza kutumika kwa matumizi mbalimbali sio tu kutengenezea sarafu, bali pia vyombo vya chakula, urembo n.k..isipokuwa tumizi lililo maarufu ni hilo la kutengenezea Sarafu.

Kwa mantiki hiyo hiyo pia kwa Neno “Risasi”. Leo hii ukitaja neno risasi moja kwa moja akili za wengi zinakwenda kwenye kile kipande kidogo cha chuma kinachotoka ndani ya bunduki.

Lakini kiuhalisia hiyo sio maana ya Risasi.. Risasi ni aina nyingine ya madini, ijulikanayo kwa jina hilo.. kama vile ilivyo fedha, dhahabu, almasi, chuma, shaba  n.k.. Vivyo hivyo kuna madini aina ya Risasi ambayo kwa lugha ya kiingereza yanaitwa “Lead”.

Na madini haya yajulikanayo kama Risasi yanamatumizi mengi mbali mbali kama vile Fedha ilivyokuwa na matumizi mbali mbali sio tu kutengeneza sarafu, bali pia vitu vingine.. Kadhalika madini haya ya Risasi matumizi yake ambayo ni maarufu leo hii ni kutengenezea hicho kisilaha kidogo kijulikanacho kama risasi leo… lakini hayo sio matumizi pekee ya madini hayo, bali ina matumizi mengine mengi ambayo ndio hasaa yaliyokuwa yanatumika enzi za zamani.

Nyakati za biblia madini hayo ya Risasi, yalikuwa yanatumika sana sana katika kutengenezea vyombo vya kupikia, na kuhifadhia vitu vya moto sana, kwasababu yalikuwa ni magumu kuyeyuka hata kwa moto mkubwa, madini ya chuma yanawahi kuyeyuka kabla ya Risasi, kadhalika madini haya yalitumika kwaajili ya maandishi, yalikuwa ni bora kwa kuhifadhi maandishi kwa muda mrefu, tofauti na mengine yote. (Ayubu 19:24).

Hivyo yalikuwa ni madini ya kibiashara sana enzi za zamani na hata sasa.. Nyakati hizi yamezidi matumizi mpaka kufikia kutengeneza vifaa vya kisilaha kama hizi risasi zinazotumika katika bunduki.

Katika biblia madini hayo yameonekana yakitajwa katika sehemu kadhaa..

Ezekieli 27:12 “Tarshishi alikuwa mfanya biashara kwako, kwa sababu ya wingi wa utajiri wa kila aina; kwa fedha, na chuma, na bati, na risasi, walifanya biashara, wapate vitu vyako vilivyouzwa”.

Unaweza kuyapata pia katika vitabu vifuatavyo… Hesabu 31:22, Yeremia 6:29 na Zekaria 5:7

Lakini katika roho sisi watu wa Mungu tunafananishwa na vitu hivyo vya thamani.. kama fedha, dhahabu, almasi n.k

Kama vile chuma na dhahabu ili viwe imara na ili ving’ae ni lazima vipitishwe kwenye moto, na watu wa Mungu waliookoka ili wawe wa thamani mbele za Mungu ni lazima wapitishwe kwenye moto (yaani majaribu mbali mbali).

Kadhalika ili risasi iwe bora ni lazima ipitishwe nayo kwenye moto.. Na sisi tunafananishwa na risasi za Bwana.. na matumizi makubwa ya risasi katika zama zetu hizi ni SILAHA, Kadhalika na sisi ni silaha za Bwana, dhidi ya majeshi yote ya adui..Ili tuwe imara hatuna budi kupitishwa katika moto.. Ndivyo maandiko yanavyosema…

Ezekieli 22:18 “Mwanadamu, nyumba ya Israeli imekuwa taka za fedha kwangu; wote wamekuwa shaba, na bati, na chuma, NA RISASI, kati ya tanuu; wamekuwa taka za fedha.

19 Basi Bwana MUNGU asema hivi; Kwa sababu ninyi nyote mmekuwa taka za fedha, tazama, nitawakusanya kati ya Yerusalemu.

20 Kama vile watu wakusanyavyo FEDHA, NA SHABA, NA CHUMA, NA RISASI, NA BATI, KATI YA TANUU, ILI KUVIFUKUTIA MOTO NA KUVIYEYUSHA; ndivyo nitakavyowakusanya ninyi katika hasira yangu, na ghadhabu yangu, nami nitawalaza huko, na kuwayeyusha.

21 Naam, nitawakusanya, na kuwafukutia moto wa ghadhabu yangu, nanyi mtayeyushwa kati yake”.

Je umempokea Yesu?.. je wewe ni dhahabu safi?, ni fedha safi?, ni Risasi safi kwa Bwana?.. kama bado unasubiri nini?..Unawezaje kuishi maisha ya namna hayo yasiyo na thamani yoyote mbele za Mungu..Mpokee Kristo leo, na ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo, upate ondoleo la dhambi, na Bwana atakupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu, atakayekuongoza katika kweli yote.

Bwana akubariki.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Ni kwa namna gani malaika wa mbinguni wanaweza kutuhubiria sisi injili?

APENDAYE FEDHA HASHIBI FEDHA.

Fuawe ni nini? Kama tunavyosoma katika Isaya 41:7

KUNA UMUHIMU WA KUWA MTU WA KURIDHIKA.

ONDOA TAKATAKA KATIKA FEDHA, NA CHOMBO KITATOKEA KWA MTAKASAJI.

Ufisadi una maanisha nini katika biblia?

Rudi nyumbani

Print this post

Neno Saumu lina maana gani katika biblia?

JIBU: Saumu ni neno lenye asili ya lugha ya “kiaramu” lenye maana ya “kujizua kufanya jambo/kitu fulani kwa ajili ya ibada”.

Hivyo pale mtu anapoacha kula kwa kipindi fulani, kwa ajili ya sala..Mtu huyo yupo katika saumu.au kwa jina tulilolizoea tunasema yupo katika mfungo.

Neno hilo utalipata katika vifungu hivi kwenye biblia..

Zekaria 8:19

[19]BWANA wa majeshi asema hivi, Saumu ya mwezi wa nne, na saumu ya mwezi wa tano, na saumu ya mwezi wa saba, na saumu ya mwezi wa kumi, zitakuwa furaha na shangwe, na sikukuu za kuchangamkia, kwa nyumba ya Yuda; basi zipendeni kweli na amani.

Yoeli 1:14

[14]Takaseni saumu, iteni kusanyiko la dini, 

Wazee na wakusanye wenyeji wote wa nchi; Waende nyumbani kwa BWANA, Mungu wenu, Na kumlilia BWANA,

Soma pia Yoeli 2:15.utaliona neno hilo.

Saumu ya kweli ni ipi?

Lakini pia tofauti na wengi tunavyodhani..kwamba saumu inayompendeza Mungu ni ile ya chakula tu..ni kweli hiyo anaitazama lakini sio kiini cha saumu anayotaka kuiona ndani ya mtu.. Saumu anayoipokea ni ile ya kufunga vifungo vya uovu na dhambi.

Isaya 58:3-8

[3]Husema, Mbona tumefunga, lakini huoni? Mbona tumejitaabisha nafsi zetu, lakini huangalii? Fahamuni, siku ya kufunga kwenu mnatafuta anasa zenu wenyewe, na kuwalemea wote watendao kazi kwenu.

[4]Tazama, ninyi mwafunga mpate kushindana na kugombana, na kupiga kwa ngumi ya uovu. Hamfungi siku hii ya leo hata kuisikizisha sauti yenu juu.

[5]Je! Kufunga namna hii ni SAUMU niliyoichagua mimi? Je! Ni siku ya mtu kujitaabisha nafsi yake? Ni kuinama kichwa kama unyasi, na kutanda nguo za magunia na majivu chini yake? Je! Utasema ni siku ya kufunga, na ya kukubaliwa na BWANA?

[6]Je! Saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira?

[7]Je! Siyo kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? Umwonapo mtu aliye uchi, umvike nguo; wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe?

[8]Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na afya yako itatokea mara; na haki yako itakutangulia; utukufu wa BWANA utakufuata nyuma ukulinde.

Umeona? Hivyo na wewe ufungapo basi fahamu kuwa Mungu anatazamia kuona mageuzi makubwa ya maisha yako dhidi ya dhambi na kutenda haki. Usifunge tu kidini ili kutumiza sheria.Funga kwa lengo la kuwa mkamilifu mbele zake.

Vinginevyo unaweza ukafunga hata siku 40 usiku na mchana bila kula, kama Musa na Mungu bado akaona unafanya kazi bure.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

NJIA SAHIHI YA KUFUNGA.

KWARESMA IPO KIMAANDIKO?

Maana Ya Maneno Katika Biblia.

Mafundisho

Rudi nyumbani

Print this post