Ayubu 26:6 “Kaburi li wazi mbele yake, Uharibifu nao hauna kifuniko”.
Kama tunavyojua mashimo mengi yanayochimbwa huwa yanawekwa mifuniko juu, ili kusudi kwamba ikitokea mtu mgeni akapita kwa njia ile iwe ni mchana au usiku kwa bahati mbaya asitumbukie,
Lakini biblia inatumbia kaburi la mauti lipo wazi sikuzote, na uharibifu hauna kifuniko..
Uharibifu kwa jina lingine ni kuzimu.. Akimaanisha kuwa kuzimu haina mfuniko wowote, mfano ikitokea umepita katika njia hiyo kwa namna yoyote, basi kutelezea humo na kuzama ni mara moja..haijui huyu ni mgeni, au ni mwenyeji au ni mtoto. Ukizama umezama!.
Na ndio maana leo hii mtu akifa katika dhambi, moja kwa moja atajikuta ghafla tu yupo kuzimu, (Ayubu 21:13). atajiuliza amefikaje fikaje huko. Lakini ndio hivyo tayari ameshafika huko mahali ambapo hatatoka tena milele,.atakachokuwa anasema huko ni Laiti ningejua, laiti ningefahamu, nisingefanya hiki au kile..
Biblia inatuambia..
Isaya 5:14 “Kwa hiyo kuzimu kumeongeza tamaa yake, kumefunua kinywa chake bila kiasi; na utukufu wao, na wingi wao, na ghasia yao, naye pia afurahiye miongoni mwao, hushuka na kuingia humo”.
Unaona? Unashuka kwa ghafla sana, tusitamani tufike huko. Kila inapoitwa leo, tumwombe Mungu vilevile tujitahidi kukaa mbali na dhambi kwa kadiri tuwezavyo.
Watu wote wanaochukuliwa katika maono na kupelekwa kule, na kuonyeshwa sehemu tu ya mambo yanayoendelea humo, huwa hawatamani kuhadithia, kwasababu wote wanaowaona humo, ni vilio vya majuto tu, wanatamani wapewe dakika hata moja warudi watengeneze mambo yao lakini haiwezekani tena..
Ayubu 7:9 “Kama vile wingu likomavyo na kutoweka, NI VIVYO HUYO ASHUKAYE KUZIMUNI HATAZUKA TENA KABISA.
10 Hatarudi tena nyumbani kwake, Wala mahali pake hapatamjua tena”.
Utatamani urudi duniani siku hiyo itashindikana…Mfano tu wa Lazaro na yule Tajiri…Yule tajiri aliomba akawahubiriwe ndugu zake ili wasifike mahali pale alipo pa mateso lakini ilishindikana..Na Watu wanaoshuka huko ni wengi sana wasiohesabikia. Hivyo mimi na wewe tulio hai, tuikwepe dhambi…
Tusipende kufuata mikumbo ya watu, kisa wanakwenda Disko na sisi tuende, kisa wanavaa nguo za kikahaba na sisi tuvae, kisa wanafanya uasherati na sisi tufanye..kisa wanatumia pombe na sisi tutumie ..Kamwe usiwaige hao..Kwasababu wanaoshuka huko ni wengi sana, na kuzimu haijai watu..(Mithali 27:20, Mithali 30:16)
Kumbuka hizi ni zile siku zilizotabiriwa za maasi kuongezeka. Kwahiyo usishangae kuona wimbi kubwa la watu wanaofanya dhambi hadharani bila hofu.
Zaidi macho yetu yaelekee mbinguni, kwani unyakuo upo karibu, Au hata kama hautakukuta wakati wako, basi tufahamu kuwa kifo nacho hakipo mbali, Hivyo ni wajibu wetu kujiimarisha na kujithibitisha kwamba tupo katika mstari wa Imani.
Luka 12:35 “Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na taa zenu ziwe zinawaka;
36 nanyi iweni kama watu wanaomngojea bwana wao, atakaporudi kutoka arusini, ili atakapokuja na kubisha, wamfungulie mara”.
Shalom.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312.
Jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
NA MTU MMOJA AKAVUTA UPINDE KWA KUBAHATISHA, AKAMPIGA MFALME
2Timotheo 3:6 Inazungumzia watu wanaowachukua wanawake wajinga mateka, Je! Mstari huu una maana gani?
JIBU: Ukianzia kusoma tokea mstari wa kwanza utaona pale Paulo anamwonya Timotheo juu ya baadhi ya tabia za ajabu ambazo zitaanza kujitokeza katika siku za mwisho, alimwambia..
2Timotheo 3:1 “Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari…”
Ukiendelea kusoma utaona akizihorodhesha tabia zenyewe zitakazozuka..anasema watatokea watu wanaopenda fedha, watu wenye kiburi,wasio safi, wanaopenda anasa kuliko kumpenda Mungu..n.k. Lakini ukushuka mpaka mstari wa tano anasema tabia nyingine kuwa, nyakati hizo kutaibuka pia wimbi la watu wenye mfano wa utauwa, lakini wakizikana nguvu zake, na hapa ndipo pa hatari zaidi..Tusome..
2Timotheo 3:5 “wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake; hao nao ujiepushe nao.
6 Kwa maana katika hao wamo wale wajiingizao katika nyumba za watu, na kuchukua mateka wanawake wajinga wenye mizigo ya dhambi, waliochukuliwa na tamaa za namna nyingi;
7 wakijifunza siku zote, ila wasiweze kabisa kuufikia ujuzi wa kweli”.
Unaona hapo?
Na wanawake pia wanahusishwa na watu hawa wanatajwa kuwa wao ndio waathirika wakubwa wa wimbi hilo la hao watu wanaojifanya kuwa ni watu wa Mungu(wenye mfano wa utauwa) lakini nyuma yake hawana Habari na Mungu hata kidogo (ni vyombo vya ibilisi dhahiri).
Hapa ndipo wewe kama mwanamke unapaswa ujichunge sana, tupo katika nyakati za hatari, kwasababu shetani tangu Edeni alikuwa anaufahamu mlango mwepesi wa kuuingilia ni mwanamke na si mwanaume (1Timotheo 2:14).. Leo hii utaona watu wa aina hii, hifadhi yao imekuwa wanawake wengi.., tena biblia inatumia neno
“Wanawake wajinga wenye mizigo ya dhambi na waliochukuliwa na tamaa za namna nyingi ”.
Ikiwa na maana kuwa wanawake hawa suala la wokovu kwao halina maana sana,(ni wajinga katika roho) wanachotafuta ni mambo ya mwilini tu, wabarikiwe kazi zao, wapewe waume, wapate fedha, wapigiwe maadui zao, na huku waendelee na mavazi yao ya nusu uchi barabarani, waendelee kuwasengenya majirani zao, waendelee kuzini, waendelee kuishi kidunia..
Hawataki kujishughulisha na mambo ya rohoni,(hawaupendi utakatifu hata kidogo!) wakiona tu nabii yule ni mtanashati, anachekesha, ana magari, ana majumba, ana wafuasi wengi bila kujiuliza mara mbili kwasababu tu kashajiita ni mtu wa Mungu wanaingiwa na tamaa wanakwenda kujiunganisha naye.
Hayo yote, ni mambo yaliyotabiriwa kuwa yatatokea katika siku za mwisho, na tunayaona sasa.. Na kibaya Zaidi wanawakaribisha kwenye majumba yao, wewe angalia utaliona hilo, ni mara chache sana utawaona kwenye nyumba zenye mchanganyiko wa wanaume, muda wote utawaona wanazunguka kwenye nyumba za wanawake tu, na wakigundua mwanamke huyo kaolewa hawataenda kwake au kama wakienda wataenda wakati mumewe hayupo!…(Na wanawachukua mateka kimwili na kiroho)
hiyo yote ni ili maandiko yatimie, kwamba siku za mwisho watatokea watu wa namna hiyo.
Na ndio maana mtume Yohana alipomwandika wakara yule MAMA Mteule, mtakatifu kuwa alimwonya asiwakaribishe watu kama hawa ambao wanakuja kwake lakini hawaleti mafundisho ya Kristo..
2Yohana 1:10 “Mtu akija kwenu, naye haleti mafundisho hayo [ya Kristo/utakatifu], msimkaribishe nyumbani mwenu, wala msimpe salamu.
11 Maana yeye ampaye salamu azishiriki kazi zake mbovu”.
Hivyo wewe kama mwanamke, iga mfano wa huyo “Mama mteule” Ipende kweli. Na sisi wote kwa Pamoja vivyo hivyo tu tutafute utakatifu.
Shalom.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312.
Jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
KWANINI UNAPASWA UJIWEKE TAYARI SASA, KABLA YA ULE WAKATI KUFIKA?.
JINSI SODOMA NA GOMORA ILIVYOKUWA INAVUTIA SANA..
YONA: Mlango wa 4
MKUMBUKE MKE WA LUTU.
KAMA ZILIVYOKUWA SIKU ZA NUHU NA ZA LUTU.
KUTAKUWA NA MATETEMEKO YA NCHI, NJAA NA TAUNI.
Dalili ya kwanza ya uchanga mkubwa wa kiroho ni hofu ya wachawi…Ukijiona unaogopa wachawi, au “uchawi” huo ni uthibitisho wa kwanza kabisa kwamba wewe ni mchanga kiroho, na Neno la Mungu bado halijakaa ndani yako, haijalishi upo madhabahuni unahubiri kwa miaka mingapi! Bado ni mchanga.. Mtu anayeogopa wachawi au anayewatukuza mno wachawi hana tofauti ni kima anayeogopa kinyago cha mtu shambani, kinachomtishia asile mazao…
Uchawi ni sehemu ndogo sana ya vita vya mkristo!..Idara kubwa ya shetani sio “vitunguli na vibuyu”..Hiyo ni idara ndogo sana ya shetani, ambayo hata pasipo kujijua Mungu tayari anakulinda nayo pasipo hata wewe kujijua. Sasa kama wewe ni msomaji wa biblia hebu nionyeshe mahali popote ambapo Bwana Yesu alizungumzia habari za wachawi/uchawi..au mahali popote alipokuwa anawafundisha wanafunzi wake aliwaonya wajihadhari na wachawi???…
Idara kubwa na kuu ya shetani ni roho ya mpinga-Kristo ambayo hiyo inakwenda kinyume na Kristo…Na hiyo inatenda kazi ndani ya kanisa, na inatumia watumishi wa uongo wanaojigeuza na kuwa kama watumishi wa Mungu! Na inakaribiana sana na roho ya kweli. Ndio hiyo hata Bwana alikuwa anapambana nayo,(ndio ile iliyokuwa inafanya kazi ndani ya mafarisayo na masadukayo) na ndio Bwana aliwaonya sana mitume wajihadhari na hao…
Mathayo 7:15 “Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali”.
Idara hiyo iliwasumbua sana mitume walipokuwa wanahubiri injili, mpaka wengine kuuawa, ilihusika kuwaua wakristo Zaidi ya milioni 80 duniani kote kikatili tangu kipindi cha kanisa la kwanza, inaua rohoni inaua pia mwilini, ndio hiyo hiyo inazungumziwa sehemu kubwa kwenye kitabu cha Ufunuo. Na ndio hiyo itakayokuja kufanya kazi katika kipindi cha dhiki kuu.
Sasa tukirudi kwenye mada..je! Mnyama paka kulia usiku juu ya bati ni uchawi?..
Jibu ni La!..sio uchawi…ukisikia paka analia usiku nje sio uchawi!!!….Paka wanaolia usiku ni kutokana na sababu za mazaliano..(sauti zile wanazitoa ili kuvutia mazaliano)..Paka wa aina yeyote Yule wakati wa mazaliano ni lazima atoe hizo sauti, awe ni paka wa kahaba, awe wa kanisa, au wa mtumishi wa Mungu…ni lazima ikifika kipindi cha mazaliano atoe hizo sauti, na anaweza kutoa wakati wa mchana au wakati wa usiku…na sauti hizo ni lazima zifanane na sauti za watoto wachanga!!…kama hatatoa sauti zinazofanana na za watoto wachanga basi kuna kasoro katika huyo paka!..paka asiye na kasoro yoyote ni lazima atoe hiyo sauti.
Sasa kwanini wanatoa hizo sauti zinazofanana na watoto wachanga???…Ndivyo Mungu alivyowaumba!..kama tu sauti wanazotoa kanga, au mbuzi au kuku wanapofikia wakati wa mazaliano au wakati wa kutaga!!. Na paka macho yake usiku ni lazima yang’ae yanapopigwa na mwanga…Na paka wana tabia zinazofanana na chui..ni wepesi kupenya mahali hata kama ni padogo sana..na wanapotembea si rahisi kusikika, na ni wepesi wa kutoroka mahali kwa haraka, kufumba na kufumbua unaweza usiwaone mahali walipopotelea…ndivyo walivyoumbwa!..(ili sisi tumtukuze Mungu, kwa uumbaji wake), na paka wote tabia zao ni kama za chui kupenda kutembea usiku na sehemu zilizoinuka!..
Kwahiyo ni kawaida kutembea juu ya mabati na ukuta wakati wa usiku, na hata kukimbizana!..na wanatabia pia za kuingia ndani kwa mtu hata kama hawajakaribishwa, hivyo kama hujafunga mlango anaweza kuingia mpaka ndani na hata kuzalia huko…na wanatabia ya kuwa ving’ang’anizi (utamfukuza atarudi tena, na utarudia hivyo mara kwa mara), ndivyo walivyoumbwa!!
Na sio dhambi kufuga paka! wa rangi yeyote Yule (awe mweusi, mweupe, kahawia au yeyote yule), kama ndani una panya wengi!..wanafaa kwa shughuli hizo za kuwadhibiti…au kwa fahari/(kwa kupenda tu) sio dhambi kuwafuga…tena ni vizuri zaidi kama una mapenzi nao!
Na bundi na popo ni hivyo hivyo…wameumbwa kipekee na Mungu (hawatembei mchana bali usiku na vyakula vyao vinapatikana huko huko gizani). Hawa si wanyama wa kufuga ndio maana unawaona wapo kivyao vyao..
Sasa wengi wasiokuwa na maarifa wanakuwa na hofu wanapowaona wanyama hawa wanaonyesha tabia zao hizo za kipekee walizopewa na Mungu, ambazo hazionekani kwa wanyama wengine!…na kuishia kusema ni wachawi wamewatembelea…wanaposikia paka usiku wanalia batini kama watoto wachanga, wanakosa usingizi na kuamini wachawi wamewatembelea!..wanapoona popo wametoka mitini jioni na kutanda angani, wanakosa amani..wanapoona bundi kasimama anamacho kama ya mtu, nguvu zinawaishia kabisa!!…wanajua sasa ni wachawi wanafanya kazi zao!!….kumbe ni kukosa tu maarifa!. Mwisho wa siku wanaishia kuwaua hao viumbe wakidhani ndio wamemshinda shetani!..
Na hiyo inamfanya mkristo kupoteza muda mwingi, hata wiki nzima,au mwezi mzima, au miaka na miaka kupambana katika sala dhidi ya wanyama hao(akiamini kuna uchawi ndani yao)…paka kaonekana kaingia ndani hapo hapo, maombi ya kufunga mwezi mzima yanaanza!..maji ya upako yatakwenda kutafutwa mitaa yote!, kila mtumishi ataitwa!..mwisho wa siku ni hofu hofu kila mahali…kila mtu unayekutana naye unahisi ni mchawi!, nimewahi kusikia watu wanasema na kuamini mende na mijusi, wanatumika kiuchawi!..hivyo ukiona mende ndani kwako ni wachawi kuna nguvu za giza hapo!
Usikose maarifa ndugu, wala usipoteze muda wako kwa vitu visivyokuwa na maana…Ukisikia paka wanalia batini usiku, kama wanakukera toka nje wafukuze! Wataondoka, na muda huo ombea mambo mengine ya muhimu kama, familia yako, kanisa na huduma yako kama unayo, ombea na wengine..usianze kushindana kukemea wanyama hao ambao wapo katika ulimwengu wao..Ukiona kelele za kuku usizozielewa hebu nenda kaulize kwanza uzijue tabia za viumbe hao kabla ya kuchukua maamuzi yasiyokuwa na maarifa!, kama sauti za fisi a zinakukera usiku basi hama nenda maeneo ya mjini hutazisikia kamwe..
Ni hofu tu ambazo shetani anawajengea watu waaamini kwamba yeye ni mkuu kuliko Mungu…ili wamwogope yeye zaidi ya Mungu. Wewe kama ni mkristo, unapaswa uwe na ujasiri na Imani yako useme “wachawi hawana kitu kwangu” Kama vile Bwana alivyosema “shetani hana kitu kwangu”..Kisha endelea kuishi Maisha yako ya kawaida.
Bwana akubariki!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312.
Jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
Je! Ni sahihi kutumia maji ya upako,katika kufanya maombezi?
ZIKIMBIE TAMAA ZA UJANANI! NA MTU YEYOTE ASIUDHARAU UJANA WAKO.
Isaya 66:15 “Maana Bwana atakuja na moto, na magari yake ya vita kama upepo wa kisulisuli; ili atoe malipo ya ghadhabu yake kwa moto uwakao, na maonyo yake kwa miali ya moto.
16 Kwa maana Bwana atateta na wote wenye mwili, kwa moto na kwa upanga wake; nao watakaouawa na Bwana watakuwa wengi’.
Bwana Yesu atakaporudi mara ya pili, yaani siku ile mbingu zitakapofunguka na kila jicho kumwona hatarudi tena kwa upole kama alivyokuja hapo mwanzo, biblia inatuambia atakuja na jina jipya..Siku hiyo hataitwa tena YESU, Jina linalomaanisha mwokozi, hapana kwasababu hatakuja tena kuokoa, bali atakuja na jina jipya ambalo kwasasa bado halijafunuliwa..
Jina hilo litakuwa ni la kifalme, la kimamlaka, lenye uweza na ukuu mwingi sana..Watu watakamwona siku hiyo duniani hatawaamini kuwa huyu ndiye Yule tuliyekuwa tunamsikia habari zake, akihubiriwa na watu dhaifu…Kwasababu hatakuwa vile tena..
Siku hiyo wale watakaomwona, hakuna atakayesaliwa na nguvu hata kidogo, kwasababu wataingiwa na hofu kubwa, wataomboleza kusivyokuwa kwa kawaida, na ndio maana tunapaswa tusiichezee hii neema kabisa, kwasababu haitakuwa hivi siku zote.
Mtu mmoja nilikuwa ninamweleza habari za hukumu ya mwisho, na jinsi watu waovu watakavyoangamizwa, akaniambia ninamhukumu…Nikamuuliza nimekuhukumu wapi?..Akanipa lile andiko la Yule mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, ambaye Yesu aliwaambia wale watu waliomleta kwake, kuwa asiyekuwa na dhambi awe wa kwanza kumtupia Yule mawe…Nikamwambia ni kweli mimi sitakutupia mawe lakini Kristo siku ile atakutupia mawe wewe..na utakufa, kama usipotubu sasa.
Najua unaweza kuuliza ni wapi Kristo anaua..
Soma hapa..
Ufunuo 2:22 “Tazama, nitamtupa juu ya kitanda, na hao wazinio pamoja naye, wapate dhiki kubwa wasipotubia matendo yake;
23 NAMI NITAWAUA WATOTO WAKE KWA MAUTI. Na makanisa yote watajua ya kuwa mimi ndiye achunguzaye viuno na mioyo. Nami nitampa kila mmoja wenu kwa kadiri ya matendo yake”.
Hayo ni maneno yaliyotoka katika kinywa cha Kristo mwenyewe!. ATAWAUA WAOVU..Na kama vile yale maandiko pale juu yanavyotuambia..watakaouliwa hawatakuwa wachache bali ni wengi sana..
Ndugu, kikombe cha ghadhabu ya Mungu kinakaribia kujaa, (kama hujui vizuri kasome kitabu cha Ufunuo 16) Unyakuo ukishapita yatakayofuata si mambo mazuri!, ni mambo mabaya ambayo laiti ungeonyeshwa leo, usingetamana hata adui yako awepo hicho kipindi, Kwasababu siku atakaposhuka, jua litazimwa lote, na nyota na mwezi vitaondoshwa, duniani kutakuwa giza tororo, kutakuwa na tetemeko kubwa ambalo halijawahi kutokea tangu dunia iumbwe, na baada ya yeye kushuka wale ambao watakuwa bado hai atawaua mara moja..Hakuna huruma!.
Ufunuo 19:11 “Kisha nikaziona mbingu zimefunuka, na tazama, farasi mweupe, na yeye aliyempanda, aitwaye Mwaminifu na Wa-kweli, naye kwa haki ahukumu na kufanya vita.
12 Na macho yake yalikuwa kama mwali wa moto, na juu ya kichwa chake vilemba vingi; naye ana jina lililoandikwa, asilolijua mtu ila yeye mwenyewe.
13 Naye amevikwa vazi lililochovywa katika damu, na jina lake aitwa, Neno la Mungu.
14 Na majeshi yaliyo mbinguni wakamfuata, wamepanda farasi weupe na kuvikwa kitani nzuri, nyeupe, safi.
15 NA UPANGA MKALI HUTOKA KINYWANI MWAKE ILI AWAPIGE MATAIFA KWA HUO. Naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, naye anakanyaga shinikizo la mvinyo ya ghadhabu ya hasira ya Mungu Mwenyezi.
16 Naye ana jina limeandikwa katika vazi lake na paja lake, MFALME WA WAFALME, NA Bwana WA Mabwana………..
20 Yule mnyama akakamatwa, na yule nabii wa uongo pamoja naye, yeye aliyezifanya hizo ishara mbele yake, ambazo kwa hizo aliwadanganya watu wale walioipokea ile chapa ya huyo mnyama, nao walioisujudia sanamu yake; hao wawili wakatupwa wangali hai katika lile ziwa la moto liwakalo kwa kiberiti;
21 na wale waliosalia waliuawa kwa upanga wake yeye aliyeketi juu ya yule farasi, upanga utokao katika kinywa chake. Na ndege wote wakashiba kwa nyama zao.”.
Bado tu unayapenda maisha ya dhambi? Bado tu unazidi kutazama pornografia, unafanya uasherati, unakula rushwa, unakwenda Disko, unaiba, unatembea na waume/wake za watu?…
Usilisahau hili Neno.. “WATAKAUAWA NA BWANA WATAKUWA NI WENGI”
Ni heri tumkimbilie yeye maadamu bado anaokoa sasa, Kabla Bwana hajaondoka Mtume Yohana alikuwa anaegemea kifuani kwake alikuwa anadeka kama mtoto karibu na Bwana, lakini Yohana huyo huyo anamwona Bwana Yesu Yule Yule kwenye maono Patmo kama miale ya moto, anatisha sana mpaka anaanguka chini ya miguu yake kwa hofu…Hivyo wakati wa neema ukiisha, Kristo hatakuwa Yule tunayemjua sasa…hivyo Bwana atusaidie neema hii tuithamini sana.
Maran Atha.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312.
Jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
SWALI: Je! Ni sahihi kutumia maji ya upako, mafuta ya upako au chumvi katika kufanya maombezi?
JIBU: Kwanza ni muhimu kufahamu kuwa kinachomponya mtu ni damu ya Yesu Pekee. Na ndani ya damu ya Yesu ndio kuna Jina la Yesu…Hivyo jina la Yesu linapotajwa ni tangazo maalumu la damu ya Yesu katika utendaji kazi wake, hivyo kila ugonjwa au tatizo kwa jina la Yesu linaondoka na kupotea kabisa!.
Kwahiyo haipaswi kwa vyovyote vile kufikiri au kuamini kwamba kitu kingine zaidi ya damu ya Yesu kinaweza kumponya mtu au kinaweza kuondoa matatizo ya mtu au kumbariki. Kuamini hivyo hakuna tofauti na kuabudu sanamu.
Sasa pamoja na hayo, Mungu ameruhusu uponyaji wa damu ya Yesu wakati mwingine ufuatane na maagizo Fulani…Kwamfano daktari anaweza kutoa dawa kwa mgonjwa wa ngozi na kutolea maagizo kwamba akameze vidonge hivi na maji ya kutosha..au akampa vidonge vingine na kumwambia akavitie kwenye maji kisha aogee, afanye hivyo mara tatu kwa siku tatu na huo ugonjwa huo wa ngozi utamwisha..Au anaweza asimpe kidonge chochote na badala yake akamchoma sindano tu na bado ukapona vile vile…Ni kwajinsi tu yeye atakavyopenda kuchagua njia iliyobora.
Na Roho Mtakatifu ni hivyo hivyo…katika suala la kumponya mtu, mara nyingine anaweza kuambatanisha na maagizo Fulani…aidha mtu atumie mafuta, au udongo kwa jinsi Roho Mtakatifu atakavyopenda…kama alivyofanya Bwana katika Yohana 9:6 (alimwongoza atumie tope la mate yake), au anaweza akampa mtu maelekezo atumie unga kama Elisha alivyofanya katika 2Wafalme 4:41, au chumvi kama alivyofanya Elisha katika 2Wafalme 2:21 au kutumia leso kama alivyofanya Paulo katika Matendo 19:11-12..au chochote kile…Lakini ni kulingana na uongozo wa Roho Mtakatifu…Na sio kama mtindo!..kama inavyofanyika leo na wengi wanaofahamika kama watumishi wa Mungu.
Leo hii kila tatizo linatatuliwa na chumvi wanazoziita chumvi za upako, au mafuta …hata mtu akiugua tu, suluhisho ni mafuta ya upako! Au maji ya upako!..kila kitu ni mafuta ya Upako na ni kitendo endelevu na kinachojirudia kila siku…Sasa hilo sio agizo la Roho Mtakatifu…kwasababu Roho Mtakatifu hana mtindo Fulani/staili Fulani ya kumponya mtu.
Kwasababu hata Bwana Yesu sio kila mahali watu walipomjia mwenye matatizo Fulani alikuwa anatema mate chini na kutengeneza tope na kuwapaka na kufunguliwa shida zao!…utaona alifanya hivyo mara moja tu! Na tena kuna jambo alikuwa anafundisha, Na hakuna sehemu nyingine yoyote alirudia kufanya hivyo, kuonyesha kuwa nyakati zote alikuwa anasubiria maagizo ya Roho Mtakatifu, na hakufanya agizo Fulani la Roho Mtakatifu kuwa kama mtindo.
Na sio yeye tu! Hata Elisha hakuwa na staili/mtindo wake maalumu, wala hata Mtume Paulo ambaye nguo zake na Leso yake kuna wakati ilitumika hata kuondoa mapepo(Matendo 19:12)…utaona kuwa haikuwa hivyo kila mara, na wala Paulo hakugeuza kuwa kama mtindo..kwamba kila aliyekutana naye alimtupia leso ili afunguliwe!..hutaona akizituma nguo zake korintho au Galatia watu wakafunguliwe wala hakuwahi kuhubiri hayo mambo… sehemu kubwa sana alikuwa anatumia jina la Yesu…na alikuwa anamuhubiri Kristo na si mavazi yake wala leso zake. Na mitume wengine wote wa Bwana Yesu ni hivyo hivyo…tunamsoma Mtume Petro kuna wakati hadi kivuli chake kilikuwa kikimpitia mtu mwenye ugonjwa, Yule mgonjwa anafunguliwa! (kasome Matendo 5:15). Lakini hutaona mahali popote Petro akiitumia hiyo kama ndio staili yake/mtindo wa kuwafanya watu wafunguliwe…bali utaona mara karibia zote alikuwa anatumia Jina la Yesu tu!..
Matendo 3:3 “Mtu huyu akiwaona Petro na Yohana wakiingia hekaluni aliomba apewe sadaka.
4 Na Petro, akimkazia macho, pamoja na Yohana, akasema, Tutazame sisi.
5 Akawaangalia, akitaraji kupata kitu kwao.
6 Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. KWA JINA LA YESU KRISTO WA NAZARETI, SIMAMA UENDE.
7 Akamshika mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu.
8 Akaondoka upesi akasimama, akaanza kwenda; akaingia ndani ya hekalu pamoja nao, akienda, akiruka-ruka, na kumsifu Mungu”.
Hapo Petro hakutumia “kivuli” chake!…Bali jina kuu la YESU KRISTO!.
Sasa utauliza mbona kuna watu wanayatumia maji ya upako, au mafuta ya upako kama mtindo wao na wanafunguliwa?
Wengi wanaofunguliwa ni wale ambao ni wachanga kiimani, ambao ndio kwanza wamemjua Kristo, au wameingia kwenye imani ya kikristo, Hivyo Bwana anaruhusu wapokee miujiza yao kwa njia yoyote ile..ili wazidi kumsogelea Mungu katika hivyo vipindi vya awali, lakini baada ya kipindi Fulani kupita wakaujua ukweli, au kusikia injili kwa muda mrefu na kushupaza shingo, zinabadilika kwao kuwa ibada za sanamu, na havitawapii chochote zaidi ya kuzidi kuwaweka mbali na Mungu, na hata wakati mwingine kuingiliwa na mapepo, na kupoteza hata vile walivyo navyo kwasababu ni ibada za sanamu…wanatanga huko na huko kutafuta na kununua maji ya upako, chumvi ya upako…Na kwasababu wengi wao hawapendi kuzidi kumjua Mungu wanadanganyika!
Na manabii wengi wa uongo wamezuka sasa, katika siku hizi za mwisho kama ilivyotabiriwa…Mungu ameachilia nguvu ya upotevu kwa wale wote wanaoukataa ukweli…Na nguvu hiyo ya upotevu kaiweka ndani ya manabii wa uongo…Na lengo la nguvu hiyo ni ili watu wote wanaoukataa ukweli wazidi kudanganyika!…ili tofauti ya magugu na ngano ionekane kwaajili ya mavuno.(Mavuno hayawezi kuja bila magugu na ngano kujitenga kisawasawa!..)
2Wathesalonike 2:10 “na katika madanganyo yote ya udhalimu kwa hao wanaopotea; kwa sababu hawakukubali kuipenda ile kweli, wapate kuokolewa.
11 Kwa hiyo Mungu AWALETEA NGUVU YA UPOTEVU, wauamini uongo;
12 ili wahukumiwe wote ambao hawakuiamini kweli, bali walikuwa wakijifurahisha katika udhalimu”.
Hivyo ni wakati wa kuwa makini sana na kuwa macho, na kujihadhari na roho zidanganyazo!…Kama hujapewa maagizo yoyote na Roho Mtakatifu basi usikurupuke kutumia maji,chumvi, udongo, au chochote kile ni hatari sana kwa roho yako!…Tumia Jina la Yesu tu pekee linatosha…
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 693036618/ 0789001312.
Jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
WAKATI ULIOKUBALIKA NDIO SASA.
MAMBO MENGINE HAYATOKI ISIPOKUWA KWA KUFUNGA.
JE! UMEBATIZWA UBATIZO SAHIHI?
BIRIKA LA SILOAMU.
Nini tofauti kati ya Amri, sheria na Hukumu?
Mtu astahiliye hofu ni yupi?
Luka 4:5 “ Akampandisha juu, akamwonyesha milki zote za ulimwengu KWA DAKIKA MOJA.
6 Ibilisi akamwambia, Nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake, kwa kuwa imo mikononi mwangu, nami humpa ye yote kama nipendavyo”.
Hilo ni moja ya jaribu shetani alilomletea Bwana kule jangwani..
Lakini jiulize ni kwa nini iwe kwa dakika moja?, kwanini amwonyeshe ndani ya muda mfupi kiasi hicho, kwani alikuwa na haraka gani? Chukulia mfano mtu aje na kukwambia nataka kukuonyesha plani ya mji wetu na shughuli zote zinazofanyika ndani yake kwenye CD..Ni wazi kuwa hawezi kumaliza kukuonyesha kila kitu kwa dakika moja, itachukua dakika nyingi sana kama sio masaa, lakini tunaona hapa kwa ibilisi iliwezekana..
Alifanikiwa kumuonyesha Bwana milki zote za ulimwenguni kwa kitendo cha dakika moja..Ni kwanini afanye hivyo? Sio kwamba alikuwa hawezi kumwonyesha milki zote kidogo kidogo, huo uwezo alikuwa nao lakini sikuzote ni desturi yake, kutompa nafasi mtu ya kutafakari vizuri kazi zake..
Hakutaka Bwana atafakari nyuma ya milki zile kuna nini? Bali alikuwa anamwonyesha haraka haraka, ule upande mzuri tu wa fahari hizo, ili kusudi kwamba Bwana achukue maamuzi ya haraka haraka ya kumsujudia bila hata kutafakari vema, ili awe amemshinda. Hakumwonyesha Bwana wagonjwa waliolala hoi mahospitalini waliokuwa wanahitaji msaada, hakumwonyesha watu waliofungwa kwa kuonewa, au wanaotumikishwa na nguvu za giza, hakumwonyesha maskini wa roho, wala mayatima ambao wazazi wao waliuawa na huyo huyo shetani, hakumwonyesha uchawi uliokithiri katika hiyo miji n.k ..yeye alimwonyesha tu mali, na fahari..Lakini hakumweza Bwana kwasababu pale alikutana na Mkuu wa Uzima mwenyewe ambaye anajua vyema kuzipambanua roho!.
Hii ni mbinu ambayo shetani anaitumia hata sasa kuwaangusha wengi katika dhambi..kwamfano akitaka leo kummaliza mtu na dhambi ya uasherati, mara moja atamletea katika mawazo yake uzuri wa kufanya lile jambo..Lakini hatamruhusu kutafakari ni nini kipo nyuma yake, na yeye bila kutafakari vyema, moja kwa moja ataingia humo, kuitenda, hajui kuwa nyuma yake kuna hata hatari hata ya kifo hata kupata ukimwi, nyuma yake kuna mimba zisizotarajiwa, nyuma yake kuna kupata aibu, na kibaya Zaidi kuliko vyote ni kuwa nyuma yake kuna laana itokayo kwa Mungu..
Au mwingine shetani anamletea mawazo ya kuwa Tajiri kwa dakika moja, atamwambia njoo utapata utajiri wa haraka, bila kufikiri vema kuwa akienda kule, atakutana na waganga wa kienyeji waliolaaniwa, hajui kuwa nyuma yake kuna kutoa kafara, kuna uchawi, kuna kutumikishwa, na mwisho wake ni kifo, na baada ya hapo ni ziwa la moto..au anakutana na kazi ya wizi au utapeli, pasipo kutafakari nyuma yake kuna kifo, au kifungo, mtu anaingia huko…..Sasa yeye kwasababu kaonyeshwa pesa tu za haraka haraka ambazo hazihitaji kuzihangaikia sana, anaingia humo na kupotelea humo..
Mwingine, anakutana tu na kazi Fulani ya ghafla, halafu baada ya hapo anashurutishwa akaifanye, lakini yeye badala achukue muda kumwomba Mungu na kuichunguza kazi ile, moja kwa moja atakwenda kuingia nayo mkataba na kuifanya kisa tu imemuahidia mshahara mzuri, hajui kuwa kazi ile ililetwa na shetani, ili kuharibu utaratibu wake aliokuwa nao wa kusali, wa kumtumikia Mungu, na kibaya Zaidi anakuja kugundua kazi yenyewe inafanya shughuli za kipepo kama uuzaji pombe, au bidhaa haramu na mambo mengine ya ajabu.
Mwingine atakuwa anatembea madukani, ghafla anakutana na simu ya mtu imejiegesha mahali ambapo haionekani, na saa hiyo hiyo shetani anaanza kumletea mawazo ya dakika moja ya wizi, kumwonyesha faida za simu ile akienda kuuza atapata laki kadhaa, ndani ya dakika chache baadaye..kisha atanunua hiki na kile.. Na yeye bila kuruhusu fikra zake kuwaza mbali anakwenda kuiiba, bila kujua nyuma yake, kuna kupigwa na watu, kuna kuchomwa moto, kuna kufungwa, na kibaya Zaidi kuna laana ya Mungu, kwamba hata kama hatakufa pale siku ya mwisho atakwenda motoni..
Mithali 13:11 “Mali iliyopatikana kwa haraka itapunguka; Bali yeye achumaye kidogo kidogo atazidishiwa”.
Mwingine kamwona mwanamke na hapo hapo kamtamani, bila kupata muda mrefu wa kumchunguza tabia zake, yeye wazo la dakika moja tu, anaingia humo, na ndio hapo baadaye anakuja kugundua alikuwa ni mke wa mtu aliyemwacha mume wake, au kahaba tu, na ghafla matatizo ndani ya nyumba yanaanza. Vivyo hivyo na mwanamke naye, shetani atampitishia dakika moja mwanaume mwenye fedha, na yeye bila kujitafakarisha anaingia moja kwa moja, kumbe ndio kaenda kuharibu Maisha yake moja kwa moja.
Na sehemu nyingine nyingi za Maisha ni vivyo hivyo..Shetani huwa anawaletea watu mawazo ya chap-chap ..Ya dakika moja tu yanayovutia lakini nyuma yake yana miaka mingi ya majuto.
Ndugu, tusiwe wateja wa shetani..biblia inasema..
1Yohana 2:15 “Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake.
16 Maana kila kilichomo duniani, yaani, TAMAA YA MWILI, NA TAMAA YA MACHO, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia.
17 Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele”.
Zingatia hilo, ni moja kati ya majaribu makuu 3 ya ibilisi aliyoyaona yanawazomba watu wengi kwake, na ndio maana akamchagulia na Bwana, hivyo hatashindwa kutuletea na sisi (mimi na wewe), hivyo tuwe makini sana na mambo ya humu ulimwenguni
Maran atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312 / 0693036618
Jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
MAJARIBU MATATU YA YESU KRISTO
MTAIFAHAMU KWELI NAYO HIYO KWELI ITAWAWEKA HURU.
Kati ya Unyakuo,dhiki kuu, utawala wa miaka 1000 kipi kinaanza
MOTO HUFA KWA KUKOSA KUNI.HATA UASHERATI NAO
NJIA SAHIHI YA KUMPATA MWENZA WA MAISHA KIBIBLIA.
Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita..
SWALI: Kuungama maana yake ni nini?
JIBU: Maana ya kuungama ni “kukiri jambo kwa wazi” kukubali….Kwamfano mtu anayetubu kwa kuzikiri dhambi zake kwa wazi kwamba yeye ni mwenye dhambi mbele za Mungu, mtu huyo ni “ameungama dhambi zake”
1Yohana 1:9 “Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote”.
Mathayo 3:5 Ndipo walipomwendea Yerusalemu, na Uyahudi wote, na nchi zote za kandokando ya Yordani;
6 naye akawabatiza katika mto wa Yordani, huku wakiziungama dhambi zao”.
Kadhalika kuikiri imani mbele za watu ni “kuiungama imani”..na kuukiri uongo ni kuungama uongo!
Bwana wetu Yesu Kristo alipopelekwa mbele ya Pontio Pilato, na Pilato alipomwuliza je wewe ndiwe Kristo?..Alikiri (aliungama) wazi kuwa yeye ndiye!
Luka 23:3 “Pilato akamwuliza, akisema, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Akajibu akamwambia, Wewe wasema”…..
Neno “wewe wasema” maana yake ni “kama ulivyosema”..Kwahiyo Kristo alikiri kwa wazi pasipo hofu mbele ya Pilato kwamba yeye ndiye Kristo!..Hivyo aliungawama Imani yake kwa wazi.
1Timotheo 6:13 “Nakuagiza mbele za Mungu anayevihifadhi hai vitu vyote, na mbele za Kristo Yesu, ALIYEYAUNGAMA MAUNGAMO MAZURI yale mbele ya Pontio Pilato,
14 kwamba uilinde amri hii pasipo mawaa, pasipo lawama, hata kufunuliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo”
Kadhalika na sisi kama hatujatubu mbele za Mungu…tunapaswa tuziungame dhambi zetu kwanza, (maana yake tuzikiri kwa dhati kwamba sisi ni wenye dhambi, tusipokiri na kukubali kwamba sisi ni wakosaji mbele zake kamwe hatuwezi kupata msamaha kutoka kwake!)..kisha tumwombe Mungu rehema naye atatusamehe…Na tukiishaziungaa dhambi zetu na kuipokea Imani kwa kumwamini mwanawe mpendwa Yesu Kristo tunapaswa kila siku TUUNGAME MAUNGAMO YA IMANI YETU!…maana yake tuikiri Imani ya kikristo kila mahali tuendapo, na popote pale tusimamishwapo pasipo hofu wala kujali ni nani yupo mbele yetu!..kama Bwana wetu Yesu alivyoungama..
1Timotheo 6:12 “Piga vita vile vizuri vya imani; shika uzima ule wa milele ulioitiwa, UKAUNGAMA MAUNGAMO MAZURI MBELE YA MASHAHIDI WENGI”.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312 / 0693036618.
Jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
Unajua ni kwanini Daudi alipewa jina kuu na kubwa kuliko wafalme wote na watu wote waliomtangulia katika Israeli? Ni kwasababu kuna kipindi aliwaza, Mungu amenipa vyote, amenipa ufalme, amenipa uongozi bora juu ya Israeli yote, amenipa nyumba nzuri ya kukaa, lakini mbona ni mimi tu ananifanyia wema, na mimi simfanyii chochote?. Akatazama huku na kule, akaangalia ni wapi pamepunguka, akagundua kuwa Mungu hana maskani yoyote ya kukaa, akatazama akaona lile sanduku la agano la Mungu linakaa kwenye mapazia, katika giza nene (1Wafalme 8:12) kwenye vihema vilivyochoka na kuchakaa..
Akajiwazia tu moyoni akasema hii haiwezekani, nitamjengea Mungu nyumba ya kukaa..
Lakini biblia inatuambia usiku huo huo Neno la Mungu lilimfikia Nadhani nabii wa Mungu, kwa Daudi kumwambia kwamba Mungu anasema: Je nilishawahi kusema Neno lolote kwa mwamuzi yoyote wa Israeli juu ya kujengewa mimi nyumba? Nilishawahi kumdokeza Yoshua juu ya jambo hilo? Nilishawahi kumdokeza Gideoni kuhusu kunijengea nyumba, Au Samsoni, au Ehudi au Yeftha, au Samweli juu ya jambo hilo?
Kwa namna nyingine Bwana alikuwa anamaanisha kumwambia Daudi hivi..
Sikuwahi kuwauliza chochote, ili nisionekane kama nawalazimisha, bali niliwaacha wao wenyewe waligundue hilo, lakini hakuna hata mmoja aliyelijali jambo hilo isipokuwa wewe Daudi, Sasa Basi kwa kuwa umefikiria hivyo, kunipa heshima, kunitoa katika giza nene, kwenye vihema vibovu, mimi nami nitakupa jina kuu sana, na sehemu nzuri Zaidi.
2 SAMWELI: MLANGO 7
1 Ikawa, mfalme alipokuwa akikaa katika nyumba yake, hapo Bwana alipomstarehesha, asiudhiwe na adui zake waliomzunguka pande zote,
2 mfalme akamwambia Nathani, nabii, Angalia sasa, mimi ninakaa katika nyumba ya mierezi, bali sanduku la Mungu linakaa ndani ya mapazia.
3 Nathani akamwambia mfalme, Haya, fanya yote yaliyomo moyoni mwako; maana Bwana yu pamoja nawe. 4 Ikawa usiku uo huo, neno la Bwana likamfikia Nathani kusema,
5 Enenda, ukamwambie mtumishi wangu, Daudi, Bwana asema hivi, Je! Wewe utanijengea nyumba, nikae ndani yake?
6 Kwa maana mimi sikukaa ndani ya nyumba, tangu siku ile niliyowatoa wana wa Israeli katika Misri, hata leo, lakini nimekaa katika hema na maskani.
7 Mahali mwote nilimokwenda na wana wa Israeli wote, je! Nimesema neno lo lote na mtu ye yote wa waamuzi wa Israeli, niliyemwagiza kuwalisha watu wangu Israeli, nikisema, Mbona hamkunijengea nyumba ya mierezi?
8 Basi, sasa, mwambie mtumishi wangu, Daudi, maneno haya, Bwana wa majeshi asema hivi, Nalikutwaa katika zizi la kondoo, katika kuwaandama kondoo, ili uwe mkuu juu ya watu wangu, juu ya Israeli;
9 nami nimekuwa pamoja nawe kila ulikokwenda, na kuwakatilia mbali adui zako wote mbele yako; NAMI NITAKUFANYIA JINA KUU, KAMA JINA LA WAKUU WALIOKO DUNIANI”.
Na tunaona Daudi alianza maandalizi yote ya ujenzi wa hekalu la Bwana, na mwanawe Sulemani akaja kulimalizia..
Sasa leo hii sisi ndio tunaojua vizuri ni jinsi gani Mungu amempa Daudi jina kuu kuliko wengine wengine wote waliomtangulia.. (hata Bwana wetu Yesu katokea katika huo huo uzao wa Daudi katika mwili) Lakini hiyo yote ni kutokana na kwamba hakusubiri aambiwe ndipo afanye..
Hata leo hii, zipo kazi Mungu nyingi sana zimepwaya, Na Mungu amekaa kimya anaangaalia, wala hasemi chochote, Ni kweli ataendelea kuwa na sisi kama Watoto wake, kama watumishi wake, atatutumia sisi kama manabii wake, mfano wa Samweli, Lakini kama hatutachunguza na kuchukua hatua ni wapi palipopunguka, tusitazamie kamwe kama Mungu siku moja atakuja kutuambia naomba unifanyie hiki au kile.
Vivyo hivyo ikiwa wewe umeokoka, na unajua kabisa ni jukumu lako kumtolea Mungu, kamwe usidhani ipo siku Mungu atakuuliza mbona hujanitolea, au mbona hujanifanyia hichi au kile….hilo jambo hawezi kufanya kabisa, wewe ndio unapaswa ulitambue hilo si yeye.
Unajua kabisa unapaswa ukaisambaze injili kwa wengine kwa karama Mungu aliyoiweka ndani yako, halafu unasubiria siku moja Mungu akutokee akwambie nenda kahubiri, hilo wazo lifute kabisa, ni rahisi kumwambia yule ambaye ndio kwanza anaingia kwenye wokovu lakini wewe ambaye umeshakaa miezi, na miaka,na huna ushuhuda wowote, unasubiri siku moja Mungu akuambie uipeleke Habari njema katika maono, hawezi kufanya, kwasababu anajua kabisa unajua jukumu lako, kwanini tena akuambie, si itakuwa kama anakulazimisha?..
Pale tunapochukua hatua ndipo hapo Mungu anatuongezea na hatua nyingine..(Usisubiri mpaka Mungu akuambie)
Hivyo siku ya leo ya tarehe hii na mwezu huu, biblia inatufundisha kuwa na jicho kama la Daudi, ili na sisi pia Bwana atupe jina lililo huku na kule ng’ambo tutakapofika.
Bwana atubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312 / 0693036618.
Jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
NA MTU MMOJA AKAVUTA UPINDE KWA KUBAHATISHA, AKAMPIGA MFALME
Ni kura ya aina gani waliipiga wale watu waliosafiri na Yona?
SWALI: Huu mstari una maana gani? Mhubiri 3:16-17 “Zaidi ya hayo,nikaona tena chini ya jua ya kwamba,Mahali pa hukumu upo uovu,Na mahali pa haki upo udhalimu.17 Nikasema moyoni mwangu,Mungu atawahukumu wenye haki na wasio haki, kwa kuwa kuna wakati huko kwa kila kusudi na kwa kila kazi”.
JIBU: Hizi ni hekima zilizoandikwa na mfalme Sulemani ambae alimwomba Mungu ampe hekima badala ya Mali (Jambo la kwanza na la muhimu sana ambalo na sisi pia tunapaswa tuanze kumwomba Mungu)..
Hapo katika mstari huo anasema kwa hekima ya Roho “nikaona tena chini ya jua ya kwamba,Mahali pa hukumu upo uovu,Na mahali pa haki upo udhalimu”….Zingatia hapo anaanza na neno “NIKAONA CHINI YA JUA!”..Maana yake sio mbinguni, bali ni duniani. Ikiwa na maana kuwa mbinguni mahali pa haki hapana udhalimu, vilevile Hukumu za mbinguni Mungu alipo hazina uovu,
Ayubu 34:12 “Naam, hakika, Mungu hatatenda mabaya, Wala Mwenyezi hatapotosha hukumu”.
Lakini kinyume chake hukumu za duniani (chini ya jua) ndizo zenye uovu, na haki za duniani ndio zina udhalimu…Kama Mhubiri anavyosema hapo juu.
Na hiyo ni kweli kabisa..je! huoni leo, hata mahakamani (mahali ambapo pangepaswa kutolewa hukumu ya haki)..wapo mahakimu wanaopotosha hukumu?..wanaopokea rushwa na kumnyima haki yule anayestahili haki, na kumpatia yule asiyestahili?..na wapo wengi wanaopewa kesi ambazo sio zao kwasababu tu ya rushwa..n.k
Kwahiyo ni kweli kabisa chini ya jua na si mbinguni…hukumu nyingi zinapotoshwa!..Mahali ambapo ni pa hukumu kuna uovu na mahali pa haki kuna udhalimu…mahali ambapo mtu anapaswa apate haki, ananyimwa haki yake.
Na ndio maana katika mstari wa mwisho kabisa amesema.. “Mungu atawahukumu wenye haki na wasio haki”. Maana yake ni kwamba Wale wanaosimamia haki duniani kama mahakimu watasimama katika kiti cha hukumu pia kutoa hesabu ya uhakimu wao, kadhalika na wasio haki(maana yake waovu wote) pia watasimama mbele ya kiti cha hukumu) siku ile ya mwisho, na kila mtu atahukumiwa kulingana na matendo yake.
Maran atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312 / 0693036618.
Jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
Maana ya ‘Usimjibu mpumbavu sawasawa na upumbavu wake’
Nini maana ya mstari huu: (Mtu ambarikiye mwenzake kwa sauti kuu asubuhi na mapema; Itahesabiwa kuwa ni laana kwake.Mithali 27:14 )?
https://wingulamashahidi.org/2019/09/01/maana-ya-huu-mstari-ni-ipi-mithali-144-zizi-ni-safi-ambapo-hapana-ngombebali-nguvu-za-ngombe-zaleta-faida-nyingi/
JE KUPONYWA NI UTHIBITISHO WA MUNGU KUWA NA WEWE?
https://wingulamashahidi.org/2018/06/27/maswali-na-majibu/
BWANA AKAMWAMBIA SHETANI, BWANA NA AKUKEMEE EWE SHETANI;
Na upepo wa kusi ulipoanza kuvuma kidogo, wakidhani ya kuwa wamepata waliyoazimu.
Shalom jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe.
Si kila dalili nzuri inayoonekana mbele yetu, itatuletea mwisho mwema, Kama hatutakaa chini kutaka kutafuta mashauri ya Mungu, tuwe na uhakika kuwa kuna uwezekano mkubwa sana wa kupotea..Kama vile biblia inavyotuambia katika…
Mithali 14:12 “Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti”.
Tukiiangalia mfano ile safari ya Mtume Paulo kutoka Yerusalemu kwenda Rumi kama mfungwa, haikuwa safari ya kawaida, kama sio neema ya Mungu tu kuwa pamoja na Paulo basi asingenusurukia mtu yeyote kwenye ile safari waliyosafiri yeye pamoja na wafungwa wengine, pamoja na maasakari wote na manahodha wote..Lakini hiyo yote ilisababishwa na wengi wao kuyadharau mashauri ya Mungu na kuyafuata mawazo yao wenyewe na akili zao wenyewe zinavyowatuma.
Kwani walipofika kwenye kisiwa kimoja kinachoitwa bandari nzuri, walitulia pale kwa muda wakingoja hali iwe shwari kidogo kisha waanze safari tena, Lakini ghafla kukaanza kuvuma upepo mzuri sana unaovutia ujulikanao kama upepo wa Kusi , Upepo huu ukivuma basi manahodha huwa wanafurahi kwasababu ni upepo rafiki kwa kusafiria baharini, na zaidi ya yote unawafanya safari yao kuwa nyepesi Zaidi na isiyogharimu.. Lakini Mtume Paulo kwa kuonywa na Roho aliwaambia wasisafiri, kwani mbeleni alionyeshwa watakumbana na madhara makubwa ambayo sio tu ya kupoteza shehena na merikebu bali yatahatarisha pia na maisha yao… Jambo hilo Yule Akida wa askari wala hakulizingatia, kwani aliyasikiliza zaidi mashauri ya mabaharia ambao wao kila siku wapo vilindini wenye uzoefu wa mambo hayo, pengine akajisemea moyoni huyu mfungwa maskini anatueleza nini..
Lakini biblia inatuambia walipoondoka tu kwenye kisiwa kile, hawakufikia hata mbali ule upepo wa kusi uligeuka na kuwa upepo wa Tufani wa aina nyingine ujulikanao kama Eurakilo.
Matendo 27:13 “Na upepo wa kusi ulipoanza kuvuma kidogo, wakidhani ya kuwa wamepata waliyoazimu kupata, wakang’oa nanga, wakasafiri karibu na Krete pwani kwa pwani.
14 Baada ya muda mchache ukavuma upepo wa nguvu wa namna ya tufani, uitwao Eurakilo,
15 merikebu iliposhikwa, na kutoweza kushindana na upepo, tukaiacha tukachukuliwa”.
Tufani ya namna hii ikikukumba ukiwa katikati ya bahari basi kupona hapo ni jambo ambalo haliwezekani, tufani za namna hii huwa zinakwenda kuathiri mpaka makazi ya watu nchi kavu, sasa jiulize kwa wale waliokuwa baharini ilikuwaje?..Na ndio maana ukisoma pale utaona jinsi safari ile ilivyowagharimu sana maisha,baada ya merikebu kuvunjwa, Kama sio mwenye haki mmoja kuwepo kwenye ile meli asingepona mtu kabisa..
Hayo ni mambo ambayo tunapaswa tujifunze katika maisha, tunaweza tukawa tunauzoefu mwingi wa kimaisha, tunaweza tukawa na ujuzi Fulani wa mambo, lakini tusipokaa chini na kuyatafuta mapenzi ya Mungu katika maisha yetu, badala yake tukawa tunagemea akili zetu tu, ziamue kila jambo..tufahamu kuwa Eurakilo ipo mbele yetu..siku moja itatuangamiza tu.. Haijalishi hapo mwanzo zilishatusaidia mara ngapi, ipo siku tutanasika tu.
Tunaweza tukasema mbona jambo hili au shughuli hii, inauelekeo wa kunifikisha ninapotaka kufika? Ndugu je kabla hujaliendea ulishawahi kumshirikisha kwanza Mungu? Kama ni mapenzi yake au la?
Madhara ya kutomshirikisha Mungu njia zetu ni Mengi sana.. Na mojawapo ni ghafla tu tutajikuta tumepotea, tukiangalia kumbe ni mambo Fulani yalituponza mpaka tukafikia pale.
Hivyo maandiko haya matatu yakiwapo akilini mwetu, basi kuna uwezekano mkubwa wa kuufikia mwisho mwema..
Na hili..
Na la mwisho ni hili…
Bwana atubariki na kutuongoza katika njia zetu katika Jina la Yesu Kristo.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312 / 0693036618.
Jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
IKO NJIA IONEKANAYO KUWA SAWA MACHONI PA MTU.
SIRI YA KUFANIKIWA KWA MTUME PAULO.
Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia..!!
NJONI, NUNUENI MLE NA MNYWE.
ZIKIMBIE TAMAA ZA UJANANI! NA MTU YEYOTE ASIUDHARAU UJANA WAKO.
MAPIGO YA VITASA SABA, NA SIKU YA BWANA.