Monthly Archive Oktoba 2020

Kuchelea ni nini?(2Wakorintho 11:3)

Nini maana ya neno kuchelea kama tunavyolisoma katika biblia?


Kuchelea ni hofu au wasiwasi, husanani ule unaotokana na kuzuka kwa madhara Fulani.

Kwa mfano tusome mstari huu;

2Wakorintho 11:2 Maana nawaonea wivu, wivu wa Mungu; kwa kuwa naliwaposea mume mmoja, ili nimletee Kristo bikira safi.

3 Lakini nachelea; kama yule nyoka alivyomdanganya Hawa kwa hila yake, asije akawaharibu fikira zenu, mkauacha unyofu na usafi kwa Kristo.

Hapo ni Paulo anaonyesha wasiwasi wake, kwa kanisa la Kristo kudanganywa na ibilisi haraka, na kuuacha unyofu wa moyo. Na ndio maana ukiendelea kusoma mistari inayofuata utaona Paulo, akiwatahadharisha, wasipokee injili nyingine, au Yesu mwingine au roho mwingine ambao wao hawakumuhubiri kwao..Ili wawe salama na uongo wa ibilisi.

2Wakorintho 12:20 “Maana nachelea, nisije nikawakuta si kama vile nitakavyo kuwakuta, nikaonekana kwenu si kama vile mtakavyo; nisije nikakuta labda fitina na wivu, na ghadhabu, na ugomvi, na masingizio, na manong’onezo, na majivuno, na ghasia”;

Vifungu vingine vinavyozungumzia Neno hili, ni kama vifuatavyo;

Matendo 23:9 “Pakawa na makelele mengi. Waandishi wengine wa upande wa Mafarisayo wakasimama, wakateta, wakisema, Hatuoni uovu wo wote katika mtu huyu; bali ikiwa roho au malaika amesema naye, ni nini?

10 Ugomvi mkubwa ulipotokea, yule jemadari akachelea Paulo asije akararuliwa nao, akaamuru askari washuke na kumwondoa kwa nguvu mikononi mwao, na kumleta ndani ya ngome”.

(Hapo ni jemedari alikuwa anaonyesha hofu yake ya kuuliwa kwa Paulo katikati ya baraza lile)

Soma tena;

Matendo 27:29 “Wakachelea tusije tukapwelewa mahali penye miamba, wakatupa nanga nne za tezi, wakaomba kuche”.

Soma pia Wagalatia 4:11.

Bwana akubariki.

Tazama pia maana ya maneno mengine chini.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

Kutahayari ni nini katika biblia?(2Timotheo 2:15)

Mlima Gerizimu na Ebali ni ipi, na umuhimu wao rohoni ni upi?

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia..!!

Daawa ni nini kama tunavyosoma katika biblia?

Mavyaa ni nani kibiblia?(Mika 7:6)

Rudi Nyumbani:

Print this post

Kutahayari ni nini katika biblia?(2Timotheo 2:15)

Kutahayari maana yake ni kuweka katika aibu, kuaibisha, kuaibishwa, kuaibika.

Hivi ni baadhi ya vifungu vinavyolieeleza Neno hilo;

2Timotheo 2:15 “Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli”.

Hapo ni Paulo akimwambia Timotheo, ajitahidi kuishi maisha yanayopendeza Mungu, ili asiwe na sababu ya kuona aibu katika kuitenda kazi ya Mungu. Kwamfano kama Timotheo angekuwa ni mlevi, na huku anahubiri injili, asingekuwa na ujasiri wa kuwahubiria walevi, angeona aibu, lakini akijionyesha kwa matendo yake kuwa hanywi pombe, hataona aibu kuwahubiria walevi, hata tahayari.

Vifungu vingine ni kama hivi;

2Wakorintho 7:14 “Kwa maana, ikiwa nimejisifu mbele yake katika neno lo lote kwa ajili yenu, sikutahayarishwa; bali, kama tulivyowaambia mambo yote kwa kweli, vivyo hivyo na kujisifu kwetu kwa Tito kulikuwa kweli”.

(Maana yake sikuaibishwa)

2Wathesalonike 3:14 “Na ikiwa mtu awaye yote halishiki neno letu la waraka huu, jihadharini na mtu huyo, wala msizungumze naye, apate kutahayari”;

(Maana yake apate kuona aibu)

Ayubu 11:3 “Je! Majivuno yako yawanyamazishe watu wawe kimya? Nawe hapo ufanyapo dhihaka, je! Hapana mtu atakayekutahayarisha”?

(Maana yake atakayekuaibisha)

Soma pia;

Isaya 50:7 “Maana Bwana MUNGU atanisaidia; kwa sababu hiyo sikutahayari, kwa sababu hiyo nimekaza uso wangu kama gumegume, nami najua ya kuwa sitaona haya”.

2Wakorintho 7:14, Isaya 44:11.

Bwana akubariki.

Tafadhali angalia chini maana ya maneno mengine ya ki-biblia.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

Neno Korbani linamaanisha nini? (Marko 7:11)

USIPIGE MATEKE MCHOKOO!

UTAJI ULIOKUWA JUU YA USO WA MUSA.

WINGU KUBWA LA MASHAHIDI.

Mshulami ni msichana gani?

Rudi Nyumbani:

Print this post

SIFONGO NA SIKI NI NINI?

SWALI: Sifongo na siki ni nini, alizopewa Bwana Yesu pale Msalabani?

JIBU: Tusome..

Yohana 19: 28  “Baada ya hayo Yesu, hali akijua ya kuwa yote yamekwisha kumalizika ili andiko litimizwe, akasema, Naona kiu.

29  Kulikuwako huko chombo kimejaa siki; basi wakatia sifongo iliyojaa siki juu ya ufito wa hisopo, wakampelekea kinywani.

30  Basi Yesu alipokwisha kuipokea ile siki, alisema, Imekwisha. Akainama kichwa, akaisalimu roho yake”

Sifongo ni kiswahili cha neno la kiingereza “sponge” ambalo sisi tumezoea kujitaja neno hilo kama SPONCHI au SPONJI...Sasa yapo masponchi ya aina nyingi…yaliyozoeleka sana ni yale yaliyotengenezwa na malighafi ya godoro, Mara  nyingi yanatumika kwa kuoshea vyombo na matumizi mengine, kwasababu yanakuwa yanauwezo wa kufyoza maji na kutengeneza povu. Enzi za zamani (za Bwana Yesu) yalikuwepo pia masponji, ambayo yalikuwa yanakaribiana sana kufanana na haya ya kwetu ya sasa. (Tazama picha chini, mfano wa sifongo za kale)

sifongo

Hivyo Sifongo ni sponji. Sasa tukirudi kwenye maandiko tunasoma yule askari, alitwaa hiyo Sifongo na kulitia kwenye SIKI, na lengo la kufanya hivyo ni ili hiyo SIKI ijifyonze kwenye hiyo sifongo.

SASA SIKI Nİ NİNİ?

Siki ni kiungo ambacho kinakuwa katika kimiminika, kinachotengenezwa kwa kuchachushwa kama vile zinavyotengenezwa pombe…Na kimiminika hicho kazi yake ni kuongeza ladha kwenye chakula au kukihifadhi chakula kisiharibike…Zipo siki za aina nyingi kulingana na jamii za watu na tamaduni. Huku kwetu Afrika hususani Afrika mashariki, Siki haziwi katika mfumo wa kimiminika kizito sana…lakini nchi nyingine zinatengenezwa viwandani na kuwa kama Maji (mfano wa hizo ni zile vanilla zinazotumika kwenye ice-cream na keki ambazo zinakuwa zinahifadhiwa kwenye kachupa kadogo), na pia maeneo ya Mashariki ya kati, ikiwemo Taifa la Israeli, siki zao zilitengenezwa na Zabibu, hivyo zilikuwa hazina tofauti sana na Divai.

Kwahiyo siki iliyotumika pale msalabani ilikuwa ni kama Divai, lakini si divai kabisa…Na zilitumika katika matumizi ya vyakula.  Hivyo wale askari walichovya sifongo kwenye siki na kuiweka kwenye mti, ili ifike juu pale msalabani alipokuwepo Bwana Yesu.(Tazama mfano wa siki ya divai katika picha ya juu kabisa ya somo hilo)

Na kwasababu siki kwaasili ni UNA UKALI, na ni chungu na ina tindikali nyingi, walifanya vile ili Mwili wa Bwana Yesu ukaukiwe maji…kwasababu walimsikia akisema Naona kiu.

Sasa ipo siri kubwa sana katika tukio hilo lililotendeka hapo juu msalabani, Kama utapenda kufahamu zaidi siri hiyo basi unaweza kufungua hapa >> YESU ANA KIU NA WEWE

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

Hanithi ni nini katika biblia? (kumbukumbu 23:17)

Mlima Gerizimu na Ebali ni ipi, na umuhimu wao rohoni ni upi?

Pomboo ni nini katika biblia?(Kutoka 25:5, Ezekieli 16:10)

Mkomamanga ni nini? Na katika biblia unawakilisha nini?

Rudi Nyumbani:

Print this post

YESU ANA KIU NA WEWE.

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe. Karibu tuyatafakari maandiko pamoja.

Kama tunavyojua hakuna wokovu kwa mwingine yoyote, isipokuwa kwa Bwana wetu Yesu, haijalishi dunia itasema nini, haijalishi imani nyingine zote zitasema nini lakini ukweli upo pale pale, Kristo alikufa, akafufuka, akapaa mbinguni na sasa YU HAI.. Na yupo pamoja na wale aliowaita akitembea nao mpaka ukamilifu wa Dahari. Na wote wamtumainiao, ni kama mlima wa Sayuni, hawatatikisika kamwe, wanadumu milele..(Zab.125:1).

Kuna tukio lililotokea pale msalabani..ambalo liliwashangaza wengi…Lakini kabla hatujalizungumzia hilo jambo hebu tuyazungumzie kwanza mateso ya Bwana wetu Yesu pale msalabani.

Siku ile ya mateso ya Bwana, bila shaka mimi na wewe tungekuwepo pale..tungemwaga machozi yasiyokuwa ya kawaida ya uchungu kwa jinsi alivyojeruhiwa…Biblia inasema “uso wake uliharibiwa sana kuliko watu wote”( Isaya 52:14), wengi wetu ng’ombe wakati anachinjwa tu hata hatudhubutu kutazama, ajali ikitokea mahali, hata hatudhubutu kuzitazama zile maiti, mwizi akipigwa tu na kuingizwa kwenye tairi achomwe, hisia tunazozipata hazielezeki……Sasa siku ile Bwana anasulubiwa laiti tungekuwepo wengine tungezimia.

Kwanza jana yake hakulala usiku kucha, alikuwa akizungumza na wanafunzi wake na kuwapa wosia mrefu, na kuomba… mpaka ilipofika alfajiri jogoo wa kwanza anawika, alikuwa tayari kashashikwa na wale maaskari, kulipopambazuka tayari alikuwa ameshateswa vikali, wakaanza kumtembeza na kumwangaisha, kwa miguu kutoka kwa mfalme huyu kwenda kwa huyu…kutoka kwa Pilato kwenda kwa Herode, halafu anarudishwa tena kwa Pilato, huku kichwani anataji ya miiba..na huku anapigwa na kutemewa mate…Baadaye anapewa msalaba aubebe…na apande nao Golgotha…Pale Golgotha ni eneo la kilima kirefu…Mwili wote ulikuwa umeshaishiwa nguvu hata kutembea alishindwa ikabidi asaidiwe ule msalaba.

Na baadaye akitundikwa msalabani…Damu ilimwagika nyingi na mwili uliishiwa nguvu na maji.

Sasa Yule Yesu aliyesema maneno haya….

“Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Mimi nitampa yeye mwenye kiu, ya chemchemi ya maji ya uzima, bure! (Ufunuo 21:6)”

Na tena aliyesema maneno haya…..

Yohana 7:37 “Hata siku ya mwisho, siku ile kubwa ya sikukuu, Yesu akasimama, akapaza sauti yake akisema, MTU AKİONA KİU, NA AJE KWANGU ANYWE.

38 Aniaminiye mimi, kama vile maandiko yalivyonena, mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake”.

Na leo hii anakuja kusema maneno haya…

Yohana 19:28“Baada ya hayo Yesu, hali akijua ya kuwa yote yamekwisha kumalizika ili andiko litimizwe, akasema, NAONA KİU”

Ni jambo la kushangaza kidogo! Ambalo hata sisi tunaweza kulihoji..Siku chache nyuma alisema “wote wenye kiu waje kwangu kunywa maji, na leo anasema ANAONA KIU, yaani anataka sisi ndio tumpe maji??”..Bila shaka huyu anaweza kuwa amerukwa na akili… Na kweli! Anavyoonekana ameshochoka na kakauka mwili, ni lazima atataka maji ya kunywa tu!..bila shaka wengi walicheka na kubeza…Na ili kumkomoa kabisa wakampa SIKI, ili ikaushe maji yote mwilini, ili ASIKIE KIU KISAWASAWA.

Lakini baadaye kidogo kuna jambo lilitokea lililowashangaza na kuwabadilisha mitazamo yao…na wengine waliokoka pale pale..

Ule mwili waliounyesha siki!, Ule mwili uliokuwa umeonekana umekauka maji yote, na damu yote…Ule mwili ulioonekana umekufa kwa KIU kikali na kwa KUMWAGIKA DAMU nyingi, na kwa maumivu makali…dakika chache baadaye, ULIMWAGA LITA KADHAA ZA MAJI MBELE YA MACHO YAO. Ndipo walipojua kuwa huyu Mtu alikuwa hasikii KIU cha MAJI, bali alikuwa anasikiu kingine.

Hebu tusome kidogo..

Yohana 19:32 “Basi askari wakaenda, wakamvunja miguu wa kwanza, na wa pili, aliyesulibiwa pamoja naye.

33 Lakini walipomjia Yesu na kuona ya kuwa amekwisha kufa, hawakumvunja miguu;

34 lakini askari mmojawapo alimchoma ubavu kwa mkuki; NA MARA İKATOKA DAMU NA MAJİ.

35 Naye aliyeona ameshuhudia, na ushuhuda wake ni kweli; naye anajua ya kuwa anasema kweli ili ninyi nanyi mpate kusadiki”.

Achana na zile picha unazoziona kwenye tamthilia, kimchirizi kidogo tu cha maji kinatoka ubavuni mwa Bwana.. Haikuwa hivyo ndugu!…ingekuwa hivyo huyu askari, asingeokoka hapo!..Pale maji yaliyotoka ni mengi mno, na yalitoka kwa presha nyingi..ndio maana askari huyu aliamini pale pale, kwasababu alishachoma maiti nyingi lakini kwa hiyo ya Bwana kwake lilikuwa ni tukio jipya.

Ndipo wale askari walipojua kuwa Yesu Kristo ni chemchemi ya Maji yaliyo hai..Na pale hakuwa anasikia kiu cha maji yao, bali kiu cha kuwapa wao maji ya uzima!…Na pale pale msalabani akaanza kuwapa, wakanywa yale maji, nao pia wakatoka kwenda kushuhudia habari za mwokozi.

“Naye aliyeona ameshuhudia, na ushuhuda wake ni kweli; naye anajua ya kuwa anasema kweli ili ninyi nanyi mpate kusadiki”

Na leo hii Kristo yu hai, na tangazo lake ni lile lile…

Ufunuo 21:6 “Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Mimi nitampa yeye mwenye kiu, ya chemchemi ya maji ya uzima, bure!”

BWANA ANA KIU NA WEWE NDUGU…ANA KIU YA KUKUPA WEWE MAJI YA UZIMA. Maji haya aliyatoa baada ya kupigwa kwake, Ndio shauku yake kuona unayapata hayo maji, anakuona una kiu, hivyo anataka kuikata hiyo kiu…Una kiu ya kupata furaha, yeye anayo furaha, una kiu ya kupata amani, yeye anayo amani, una kiu ya kupata raha, yeye anatoa raha (Mathayo 11:28), Una kiu ya kuthaminika, yeye anaweza kukuthaminisha…Anatamani kukupa hayo yote kuliko wewe unavyotamani.

Hivyo unachopaswa kufanya ni kumkaribisha tu katika maisha yako kama bado hujafanya hivyo, na unafanya hivyo kwa kutubu na kuziacha dhambi zako, kwa moyo wako wote, ili umsafishie sehemu ya kuwekea maji atakayokupa…Na ukishatubu, tafuta ubatizo sahihi wa kimaandiko ambao ni wa maji tele na wa kuzamishwa kwa jina la Yesu, na baada ya hapo Roho Mtakatifu ataingia ndani yako, kukusaidia kuishi maisha yanayompendeza yeye pamoja na kukupa zawadi zote hizo hapo juu…Atakata kiu yako kwa namna ambayo utashangaa wala haihitaji mtu kukuhadithia.. Wewe onja tu!maji ya Bwana halafu utakuja kutoa ushuhuda mwenyewe…

Zaburi 34:8 “Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema; Heri mtu yule anayemtumaini”.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

WINGU KUBWA LA MASHAHIDI.

MASHAHIDI 40 WALIOUAWA MJINI SEBASTE, NI UJUMBE KWETU.

JIEPUSHE NA MANENO YA MANABII WA UONGO.

USO WAKE ULIKUWA UMEHARIBIWA SANA ZAIDI YA MTU YE YOTE.

Rudi Nyumbani:

Print this post

Mlima Gerizimu na Ebali ni ipi, na umuhimu wao rohoni ni upi?

Mlima Gerizimu na Ebali ni ipi?


Mlima Gerizimu ni mlima unaopatikana katika mji wa Samaria Israeli, unatazamana uso kwa uso na mlima Ebali, tazama picha juu, milima hii miwili ilikuwa maarufu kwa wana wa Israeli kukutanika kwa ajili ya kufanya sherehe ya kujikumbusha juu ya Baraka na laana katika Torati waliopewa na Mungu.

Kwani walipokuwa Jangwani Musa aliwaagiza watakapovuka Yordani na kufika katika nchi ya ahadi, watue katika milima hii miwili, kisha watafute mawe mawili makubwa, kisha waiandike Torati yote waliyopewa juu ya mawe hayo, kisha Nusu ya wana wa Israeli watasimama juu ya mlima Gezirimu na Nusu yake watakuwa upande wa pili juu ya mlima Ebali, na hapo katikati kwenye bonde watasimama makuhani na sanduku la Agano, na madhabahu ya mawe ambayo watakuwa wameitengeneza, kisha Walawi watazisoma  Baraka na Laana zote zilizoandikwa kwenye torati, sasa pindi wana walawi wanazisoma Baraka, ile nusu ya kwanza iliyo katika mlima Gerizimu watajibu wa kusema Amen( yaani Na iwe hivyo), mpaka watakapomaliza, na wakati wanazisoma Laana, vilevile ile nusu ya pili iliyo katika mlima Ebali, watajibu kwa kusema nao Amen(Na iwe hivyo). Kwa urefu wa habari hiyo soma Kumbukumbu 27 yote.

gerizimu na ebali

Hivi ni baadhi ya vifungu vinavyoijata milima hiyo miwili.

Kumbukumbu 11: 29 “Tena itakuwa, atakapokuleta Bwana, Mungu wako, na kukutia katika nchi uendeayo kuimiliki, ndipo uiweke baraka juu ya mlima wa Gerizimu, na laana uiweke juu ya mlima wa Ebali”.

Kumbukumbu 27:12 “Hawa na wasimame juu ya mlima wa Gerizimu kwa kuwabarikia watu, mkiisha vuka Yordani; Simeoni, na Lawi, na Yuda, na Isakari, na Yusufu, na Benyamini”;

Tunaona kweli siku walipovuka Yordani, Yoshua alilitekeleza agizo hilo la Musa, na kufanya kama alivyoagizwa. Tunasoma hilo katika;

Yoshua 8:33 “Na Israeli wote, na wazee wao, na maakida yao, na makadhi yao, wakasimama upande huu wa sanduku na upande huu, mbele ya makuhani Walawi, waliolichukua sanduku la agano la Bwana, huyo aliyekuwa mgeni pamoja na huyo mzalia; nusu yao mbele ya mlima Gerizimu, na nusu yao mbele ya mlima Ebali, kama Musa, mtumishi wa Bwana, alivyoamuru, ili wawabarikie watu wa Israeli kwanza”.

Mlima huu Gerizimu ulikuja kujulikana kama mlima wa Baraka.

Je! Milima hii katika agano jipya iliitwaje?

Japokuwa katika agano haijatajwa moja kwa moja, lakini mlima Gerizimu unadhiniwa kuwa ndio mlima ule, uliotajwa na Yule mwanamke msamaria, pale alipomwambia Bwana maneno haya;

Yohana 4:20 “Baba zetu waliabudu katika mlima huu, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo kuabudia”.

Unaona Wasamaria bado waliendelea kuadhimisha mlima huu wa Gerizimu, kama mlima mtakatifu wa kuabudia, na kupokea Baraka kwa Mungu, lakini Yesu alimwambia milima au ma-hakalu hayana umuhimu tena katika kumtolea Mungu ibada ya kweli kwani ilikuwa ni kivuli tu cha mambo ya agano jipya.

Hivyo kwa kuhitimisha ni kuwa mlima Gerizimu, na Ebali ni milima iliyotumika kwa ajili ya sherehe ya kubariki, na vilevile kutoa laana kwa wavunjaji Torati.

Milima hii hata sasa rohoni inasimama, kwa wale wanamcha Mungu, Baraka za Neno la Mungu zitawafuata, kwani Mungu anawaweka katika gerizimu ya rohoni, lakini wale wasio mcha Mungu vilevile laana za Neno la Mungu ambao ni upanga, zitawafuata, kwani rohoni wanakuwa wamewekwa juu ya mlima Ebali,

Na kumcha Mungu kunaanza na kuokoka, kama hujaokoka, basi laana ipo tayari juu yako, Hivyo kama na wewe upo tayari leo kumpa Yesu maisha yako ayaokoe. Basi uamuzi huo ni wa busara sana kwako, hivyo fungua hapa kwa ajili ya kuongozwa sala ya Toba >>> KUONGOZWA SALA YA TOBA

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

Mto Frati upo nchi gani, Umuhimu wake katika biblia ni upi?

Israeli ipo bara gani?

Mkomamanga ni nini? Na katika biblia unawakilisha nini?

FANYIKA SIPORA WA KRISTO, UNYAKUO UPO KARIBU.

CHUKIZO LA UHARIBIFU

Rudi Nyumbani:

Print this post

Nini maana ya “katika wingi wa hekima mna wingi wa huzuni”.

SWALI: Biblia ina maana gani kusema “Katika wingi wa hekima mna wingi wa huzuni” Je! si sahihi kutafuta hekima?

Mhubiri1:17 “Nikatia moyo wangu ili kuijua hekima, na kujua wazimu na upumbavu; nikatambua ya kwamba hayo yote nayo ni kujilisha upepo.

18 Yaani, Katika wingi wa hekima mna wingi wa huzuni, Naye aongezaye maarifa huongeza masikitiko”.

JIBU: Ukisoma Sura hiyo ya kwanza yote, na zinazofuata utaona Sulemani alikuwa anaeleza jinsi alivyojibidiisha katika kutafuta mambo ya ulimwenguni, na hekima yake na kazi zote “zinazofanywa chini ya mbingu (Mhubiri 1:13)”.

Lakini hasemi alikuwa anayatafuta  mambo ya ki-mbinguni, hapana, na ndio maana utaona kila mahali anaishia kusema ni ubatili mtupu, sehemu zote, yaani maudhui ya kitabu cha mhubiri kinaeleza hatma ya kazi zote na shughuli zote zinazofanywa na wanadamu chini ya jua, na ndio maana mwishoni kabisa  mwa kitabu hicho utaona sasa Sulemani anatoa jibu la jambo la muhimu ambalo mwanadamu anapaswa alitafute siku zote za maisha yake..Anasema na hilo si lingine zaidi ya kumcha Mungu basi. (Soma Mhubiri 12:13).

Sasa tukirudi kwenye mstari huo anaposema “Katika wingi wa hekima mna wingi wa huzuni,Naye aongezaye maarifa huongeza masikitiko” Hamaanishi Hekima ya kimbinguni au maarifa ya kimbinguni,..Hapana!, kinyume chake hekima ya kimbinguni na maarifa ya kimbinguni ndio yanayomfanya mtu awe na amani na furaha na utulivu wa nafsi..Kumjua Yesu ambaye ndio hekima ya Mungu (sawasawa na 1Wakorintho 1:24), ni mwisho wa masumbuko yote, unakuwa umefunguliwa milele, hakuna huzuni yoyote wala masikitiko.. Unapolisoma gombo( ambalo ni Neno la Mungu), ndipo unapopata maarifa sahihi ya kuishi hapa duniani, na unafungua milango yote iliyofungwa.

Hivyo maarifa yanayozungumziwa hapo ni haya maarifa ya kiduniani tuliyonayo, kwasababu, pale mtu anapokuwa na elimu kubwa sana, inadhaniwa kuwa ndio itampa furaha ya kweli katika moyo wake, lakini matokeo yanaonyesha kuwa hilo sio kweli, Sulemani alilipata hilo akadhani ndio lingempa furaha aliyokuwa anaitazamia, lakini akagundua kuwa ni ubatili.

Ni jambo la kawaida, wanasayansi wanaokesha maabara usiku kucha, kutafiti na kugundua, asilimia kubwa huwa maisha yao sio ya furaha, kwasababu wanakuwa na hofu ya vitu vingi, hilo likitokea, au lile likizuka itakuwaje, maadui zetu wakitengeneza bomu la atomiki kama hili tunalotengeneza sisi itakuwaje? Dawa au kemikali hii madhara yake yatakuwaje miaka 10 mbele? N.k.n.k.. Maarifa yao na hekima zao zinapozidi kuongezeka huzuni nazo zinazidi kuongezeka…

Hivyo mwisho wa siku inakuwa ni huzuni juu ya huzuni tu na masikitiko juu ya masikitiko na ndio maana biblia inatuasa, tupende kuongeza maarifa kwa Mungu wetu zaidi kuliko sehemu nyingine yoyote kwasababu huko ndiko tutapata furaha ya kweli idumuyo na utulivu na amani isiyoisha.

Bwana Yesu (ambaye ndio hekima ya Mungu) anasema;

Mathayo 11:28 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;

30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi”.

Kwa Bwana Yesu ndipo penye pumziko la kweli.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

Hanithi ni nini katika biblia? (kumbukumbu 23:17)

WOSIA WA BWANA YESU KWA WANAFUNZI WAKE.

Bwana Yesu alimaanisha nini aliposema; Mafarisayo Hupanua HIRIZI zao, na kuongeza MATAMVUA yao?

SIKUKUU YA VIBANDA.

BWANA alimaanisha nini kwenye mstari huu Marko 2:21″ Hakuna mtu ashonaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kukuu;?

Rudi Nyumbani:

Print this post

Hanithi ni nini katika biblia? (kumbukumbu 23:17)

Hanithi ni nini?


Hanithi kibiblia ni mwanaume anayeingiliwa kinyume na maumbile, (Kwa lugha ya sasa wanajulikana kama mashoga), watu wote waliokuwa wanafanya hivi vitendo, waliitwa mahanithi,  na adhabu yake ilikuwa ni mpaka kifo.

Kumbukumbu 23:17 “Pasiwe na kahaba katika binti za Israeli, wala pasiwe na hanithi katika wana wa Israeli wanaume”.

Zamani katika Israeli watu wote waliokuwa wanahudumu kwenye madhabahu za miungu kama vile maashera n.k., walikuwa na desturi ya kufanya hivi vitendo kwa heshima ya miungu yao.

1Wafalme 14:23 “Maana hao pia wakajijengea mahali pa juu, na nguzo, na maashera, juu ya kila kilima kirefu, na chini ya kila mti wenye majani mabichi.

24 Na mahanithi walikuwako katika nchi, wakafanya sawasawa na machukizo yote ya mataifa Bwana aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli”.

 

1Wafalme 15:11 “Basi, Asa akafanya yaliyo mema machoni pa Mungu, kama alivyofanya babaye Daudi.

12 Akawafukuza mahanithi katika nchi, akaziondoa sanamu zote walizozifanya baba zake”.

 

2Wafalme 23:7 “Akaziangusha nyumba za mahanithi, waliokuwamo nyumbani mwa Bwana, wanawake walipofuma mapazia ya Ashera”.

Hii ni roho ambayo mpaka sasa inatenda kazi, na katika hizi siku za mwisho, ilitabiriwa itajirudia kwa nguvu kama ilivyokuwa katika siku za Sodoma na Gomora, Unaweza kuona leo hii wimbi hili la watu linavyozidi kuongezeka kwa kasi duniani kiasi kwamba hata sheria za nchi zinaruhusu, na baadhi ya dini za uongo, na mpaka wanayo bendera yao duniani, kama unavyoweza kuiona katika picha juu, bendera hiyo yenye rangi ya upinde wa mvua, ndio kauli mbiu yao kuwa Mungu hataiangamiza dunia tena kama alivyoahidi, hivyo ndivyo wanavyojidanganya.. Lakini hawajui kuwa Mungu alisema  kweli hataigharikisha dunia kwa maji, lakini alisema ataiangamiza kwa moto.

2Petro 3:6 “kwa hayo dunia ile ya wakati ule iligharikishwa na maji, ikaangamia.

7 Lakini mbingu za sasa na nchi zimewekwa akiba kwa moto, kwa neno lilo hilo, zikilindwa hata siku ya hukumu, na ya kuangamia kwao wanadamu wasiomcha Mungu”.

Unaona? Hiyo ni dalili ya wazi kuwa hii dunia inakwenda kuangamizwa wakati sio mwingi.

Lakini sisi tuyoanapo hayo, ni wajibu wetu kujiimarisha na kusimama imara katika hichi kipindi kifupi tulichobakiwa nacho, kwasababu Unyakuo upo karibu.

Swali ni Je! Tumejiwekaje tayari kwa Kurudi kwa Bwana mara ya pili?

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

JINSI SODOMA NA GOMORA ILIVYOKUWA INAVUTIA SANA..

MAONO YA NABII AMOSI.

HIZI NI NYAKATI ZA KUJIINGIZA KWA NGUVU.

DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.

Rudi Nyumbani:

Print this post

Uzima wa milele ni nini?

Uzima wa milele ni nini kama unavyotajwa sehemu mbalimbali?


Jibu fupi, uzima wa milele ni maisha yasiyokuwa na mwisho. Yaani unaishi tu, na utaendelea kuishi, hivyo hivyo kwa siku zisizokuwa na ukomo, miaka milioni moja itapita, bado utaendelea kuishi, miaka trilioni moja itapita bado utaendelea kuishi, na hapo hata bado hujaanza kuishi, utaendelea na kuendelea, kamwe hakuna siku itakayofika na ukasema leo ni ukomo wa mimi kuwa hai, kamwe hutakaa ufe, utakuwa hai hivyo hivyo daima..huo ndio uzima wa milele.

Jambo kama hilo ukilifikiria sana, kuna mahali hata akili yako itafika na kugota, jaribu uone,, kwasababu ni jambo ambalo tangu umezaliwa halijawahi  kuwa sehemu ya maisha yako, tangu ulipokuwa mdogo mpaka unakua umekuwa ukijua kuwa siku moja maisha yako yatakwisha kwa kifo, lakini pale unaposikia kuwa hutakaa ufe tena, akili yako inaweza kushindwa  kulipokea jambo hilo kwa wakati huo.Lakini ukweli ni kwamba hilo litawezekana, lakini sio kwa kila mtu anayeishi leo hii duniani, bali kwa kundi Fulani tu la watu, si watu wote wataishi milele.

Na ndio maana biblia inasema, Karama ya Mungu ni uzima wa milele.

Warumi 6:23 “Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu”.

Karama ni zawadi, hivyo zawadi kubwa kuliko zote ambayo Mungu anaweza kumpa mwanadamu, si nyingine zaidi ya uzima wa milele. Yaani maisha yasiyokuwa na ukomo..Huoni kama hiyo ni zawadi iliyopitiliza?

Lakini kama hiyo mistari inavyojieleza, Mungu haitoi karama hiyo hivi hivi tu, bali  inasema anaitoa “katika Yesu Kristo Bwana wetu”. Yaani kwa kupitia Yesu Kristo, maana yake ni kuwa usipookolewa na Yesu huwezi kupokea uzima wa milele kwa namna yoyote ile, haijalishi una matendo mema kiasi gani.

Huwezi kuupata uzima huo kwa mwanadamu mwingine yoyote duniani au mbinguni, anayejiita, mtume, au nabii, au kuhani n.k. hakuna mwanadamu yoyote zaidi ya Yesu Kristo peke yake ndiye anayeweza kuachilia karama hiyo ya uzima wa milele ndani ya Mtu.

Na ndio maana yeye mwenyewe alisema.

Yohana 3:36 “Amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya Mungu inamkalia”.

Hivyo kila mtu anayemwamini na kumpokea, anakuwa tayari na uhakika huo kuwa ndani yake uzima wa milele upo. Hata akifa leo, siku ile ya ufufuo atafufuliwa na kuungana na watakatifu wengine, na kwa pamoja wataishi milele na Mungu mbinguni milele.

Yohana 3:16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele”.

Sasa, mtu anampokeaje Yesu?. Anampokea Yesu kwanza kwa kutubu dhambi zake kwa kumaanisha kuziacha, na baada ya hapo anakua tayari kubatizwa katika ubatizo sahihi, Na kupokea Roho Mtakatifu. Hivyo kama wewe ni mmojawapo wa ambao hawana uzima wa milele ndani yao, na upo tayari leo kumruhusu Yesu ayabadilishe maisha yako.

Basi fungua hapa kwa ajili ya kuongozwa sala ya Toba na maagizo mengine >>>> KUONGOZWA SALA YA TOBA

Na ikiwa umefuatisha maagizo hayo kwa dhati na kwa moyo wako wote, basi uwe na uhakika kuwa umeshapokea karama hiyo ya uzima wa milele ndani yako

Kwahiyo endelea kujifunza Neno la Mungu, na tafuta kanisa la kiroho litakalokusaidia kukua kiroho na Bwana atakuwa na wewe sikuzote. Mpaka siku ile ya paraparanda ya mwisho.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

USIUZE URITHI WAKO.

Nini maana ya maneno haya ya Bwana? “Nami nikiinuliwa juu ya nchi,NITAWAVUTA WOTE KWANGU”(Yohana12:32).

NAO WALIOKUWA WAMEKUSUDIWA UZIMA WA MILELE WAKAAMINI.

JE! UMEBATIZWA UBATIZO SAHIHI?

MADHARA YA KUPUUZIA MAAGIZO YA MSINGI MUNGU ANAYOKUPA.

Rudi Nyumbani:

Print this post

Mkomamanga ni nini? Na katika biblia unawakilisha nini?

Mkomamanga ni nini?


Komamanga ni tunda lenye mbegu ndogo ndogo nyingi ndani yake, ambalo linaliwa kwa kumumunywa mumunywa mbegu zake mpaka utamu wote uishe, au kwa kukamuliwa juisi, ni tunda lenye ladha nzuri sana, na kisayansi linavirutubisho vingi sana mwilini, kama hukuwahi kulifahamu tunda hili tazama picha juu.

Katika biblia tunda hili linawakilisha mfanikio, au uzuri wa aidha taifa, au kitu au mtu.

Kwamfano ukisoma mstari huu;

Kumbukumbu 8:6 “Nawe uzishike amri za Bwana, Mungu wako, upate kwenda katika njia zake, na kumcha.

7 Kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yuakuingiza katika nchi nzuri, nchi yenye vijito vya maji, na chemchemi, na visima, vibubujikavyo katika mabonde na milima;

8 nchi ya ngano na shayiri, na mizabibu, na mitini, na mikomamanga; nchi ya mizeituni yenye mafuta, na asali”;

Utaona Mungu akilitaja tunda hili pamoja na mizabibu, na mitini, kuonyesha uzuri wa nchi ya ahadi ambayo Mungu aliwaambia wana wa Israeli wataiingia, kuonyesha ni jinsi gani nchi hiyo itakavyokuwa nzuri na yenye mafanikio makubwa..

Na ndio maana utaona hata sehemu nyingine, walipoasi, Mungu alitumia miti hii hii ya matunda kama mfano kuonyesha, alivyowafunguia milango ya Baraka na mafanikio katika mambo yao maovu, soma.

Hagai 1:18 “Tafakarini, nawaomba; tangu siku hii ya leo na siku zijazo; tangu siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kenda, naam, tangu siku hiyo ulipowekwa msingi wa hekalu la Bwana tafakarini haya.

19 Je! Mbegu ingali ghalani? Naam, huo mzabibu, wala mtini, wala mkomamanga, wala mzeituni, haikuzaa kitu; tangu siku hii ya leo nitawabariki”.

Soma tena;

Yoeli 1:12 “Mzabibu umesinyaa, mtini nao umevia; Nao mkomamanga na mtende na mtofaa; Naam, miti yote ya mashamba imekauka; Maana furaha imekauka katika wanadamu”.

Pia tunda hili, linawakilisha mafanikio ya kazi za mtu.

Wimbo 6:11 “Nalishukia bustani ya milozi, Ili kuyatazama machipuko ya bondeni; Nione kama mzabibu umechanua, Kama mikomamanga imetoa maua”.

Wimbo 8:1 Laiti ungekuwa kama ndugu yangu, Aliyeyanyonya matiti ya mamangu! Kama ningekukuta huko nje, Ningekubusu, asinidharau mtu.

2 Ningekuongoza nyumbani mwa mamangu, Naye angenifundisha; Ningekunywesha divai iliyokolea,Divai mpya ya mkomamanga wangu.

Soma pia 1Samweli 14:2,

Hivyo kwa ujumla, tunda hili, limetumika kuwakilisha hali ya mafanikio ya taifa, mtu au kitu.

Lakini pamoja hayo ipo nchi ya mikomamanga halisi, kuliko ile ya Kaanani, ambayo wana wa Israeli waliingia lakini bado waliugua, walikufa, waliteseka n.k. , Nchi hiyo si nyingine  zaidi ya Yerusalemu mpya. Huko hakuna shida, wala njaa, wala magonjwa, wala vifo, wala ajali, wala dhiki, lakini  swali ni je! wewe na mimi tunayo nafasi humo?

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

MADHABAHU NI NINI?

JIHADHARI NA UONGO WA SHETANI UNAOKARIBIANA NA UKWELI.

MWEZI WA ABIBU/NISANI NI MWEZI GANI?

FANYIKA SIPORA WA KRISTO, UNYAKUO UPO KARIBU.

Wafilisti ni watu gani.

UNYAKUO.

Rudi Nyumbani:

Print this post

YAFUATAYO NI MAWAZO YA ADUI HIVYO USIYASIKILIZE.

Adui yetu shetani, usiku na mchana anatafuta kutumeza, kama biblia inavyosema katika..1Petro 5:8 “ Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzungukazunguka, AKITAFUTA MTU AMMEZE”.

Hivyo anazo njia nyingi za kummeza mtu, na kila siku anabuni njia mpya…Lakini anayo moja maarufu anayoitumia ambayo ni ya MAWAZO.Anachofanya ni kupanda mbegu Fulani mbaya ndani ya mtu, ambayo hiyo mbegu inavyozidi kukuwa ndani yake inamletea kukata tamaa na mwisho kuanguka kabisa. Sasa yafuatayo ni baadhi ya Mawazo ambayo, ukiona yanakuja ndani yako, fahamu kuwa ni mawazo ambayo yamebuniwa na ibilisi, hivyo Yakatae na kuyapuuza.

  1. Mawazo ya kwamba Umemkufuru Roho Mtakatifu, au una dhambi isiyosameheka:

Hii ni silaha moja maarufu ya adui shetani kwa watu wa Mungu. Anayatengeneza mawazo haya ndani ya mtu, na kumfanya aishiwe nguvu ya kuendelea kumtafuta Mungu na kuwa na amani.

Hivyo wazo lolote linalokuja ndani yako kwamba tayari umemkufuru Roho Mtakatifu, kwasababu pengine ulishawahi kusema maneno Fulani wakati Fulani, kuikejeli injili. Au ulifanya dhambi Fulani kubwa sana, ambayo haielezeki, au ulirudi nyuma baada ya wokovu wako, na sasa unataka kutubu uanze upya, Ukiona hilo wazo linakuja ndani yako, kukuambia kuwa ulishamkufuru Roho Mtakatifu, Fahamu kuwa hilo ni wazo la ibilisi asilimia 100, hivyo lipuuzie usilipe nafasi hata kidogo. Hakuna mwanadamu aliyemkufuru Roho Mtakatifu na bado ana hofu ya Mungu..Lakini usipolipuuzia hili wazo na kuendelea kukaa nalo moyoni, litazidi kukua na mwishowe litakufanya usiendelee kumtafuta Mungu, na litakufanya uwe unakosa amani na furaha kila wakati.

  1. Mawazo ya kujiona kama Mungu anakuchukia:

Hii ni silaha nyingine ya shetani, kuharibu watu wa Mungu..Ukiona upo kwenye hili tatizo kwamba unaona kama Mungu anakuchukia, hakupendi anawapenda tu baadhi ya watu Fulani, au watumishi wake..Jua tayari upo katika shambulizi la adui yako shetani, tayari upo katika anga

zake anakuharibu kidogo kidogo. Fahamu kuwa Mungu hamchukii mtu yeyote yule hata yule mwovu kuliko wote, ingekuwa anakuchukia sidhani kama angekuumba uishi katika hii dunia, mpaka umejiona umetokea kwenye hii dunia, jua ni kwaajili ya upendo wake kwako. Hivyo hilo wazo la kujiona hupendwi ni kutoka kwa adui.

  1. Mawazo ya kujiona kwamba Mungu hasikii maombi yako:

Mungu anasikia maombi ya kila mwanadamu..kama kilio cha dhambi tu kinamfikia mbinguni, kwanini maombi yasimfikie?. Yanamfikia isipokuwa majibu ya maombi yanatofautiana mtu na mtu. Wapo ambao watapeleka maombi yao watajibiwa kama walivyoomba na wapo ambao hawatajibiwa, sasa wale ambao hawatajibiwa maombi yao, ipo sababu, na Mungu wa upendo atahakikisha wanaijua hiyo sababu kwa njia yeyote ile, ili warekebishe wapokee majibu ya maombi yao.. Kamwe hawezi kumwacha mtu yeyote hewani tu!, bila kumpa sababu ya kwanini hajapokea majibu ya maombi yake..Kinachowakwamisha wengi ni kukata tamaa

kirahisi…Unapokata tamaa tayari umekatisha safari yako ya kupokea baraka zako ukiwa katikati.

Kwa mfano, mtu anaweza kwenda kumwomba Mungu naomba unipe mume bora, au mke bora..lakini ukimwangalia ni kahaba, hivyo Mungu mwema hawezi kumpa kitu kizuri kabla hajamtengeneza kwanza…Kwahiyo wakati anasubiria majibu ya maombi yake, Mungu anamletea mhubiri, ambaye atamhubiria wokovu, na njia bora ya kuishi Maisha ya kumpendeza Mungu, anapotii na kukubali kubadilika na kuacha njia zake mbaya..Mungu ndipo anamletea jibu la

maombi yake aliyomwomba, analetewa mwenzi mwema wa Maisha, ambaye hatamsumbua na aliye mcha Mungu kama yeye. Lakini kama hatatii bado anataka kuendelea kukaa na ukahaba wake ndio atakaa hivyo hivyo kwa muda mrefu mpaka siku atakapofunguka akili, atarudia kuomba yale yale maneno lakini hataona majibu…

Hizo tu ndizo sababu za Mungu kuchelewesha majibu, lakini si kwamba Mungu hasikii maombi… Anayasikia, isipokuwa katika ujubuji wake ndio suala lingine.

Hivyo ukikosa kujiamini na kufikiri Mungu hajawahi kusikia maombi unayoomba chumbani kwako, au barabarani unapotembea, au kazini unapofanyia kazi…basi jua umeshambuliwa rohoni na adui shetani. Kazana kujua kwanini hujapata majibu lakini usifikiri kwamba hujasikiwa kabisa. Tayari umeshasikiwa, na uliloliomba limeshafanyiwa kazi, wewe fuatilia ombi lako lipo katika hatua gani sasa.

Marko 11:24 “Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu”.

  1. Mawazo ya kufikiri kwamba Siwezi kumpendeza Mungu wala kuwa mtakatifu:

Ndugu ukifikiri kwamba unaweza kufikia kiwango cha utakatifu kiasi kwamba huna kosa kabisa..basi fahamu kuwa hutaweza kamwe kumtumikia Mungu, kumbuka bado tunaishi duniani,

na lazima tutakuwa na kasoro nyingi, ambazo nyingi hatuzijui kama tunakosea…Sasa kama Mungu angezihesabu hizo biblia inasema hakuna mtu angesimama. Baada ya kuokoka ukiamka asubuhi usianze kukaa kuhesabu makosa yako, ukifanya hivyo kamwe hutaweza kumtumikia Mungu, na shetani atakusumbua sana na kila dakika atakuletea mawazo wewe ni mbaya, wewe hustahili, wewe hufai, wewe umeshamkosea Mungu, hufai, hufai n.k

Ukiamka asubuhi anza kuhesabu ni mazuri mangapi umemfanyia Mungu wako, na kama hujafanya kabisa ndipo uhuzunike, na tafuta kufanya, na jioni ukirudi..Mwambie Bwana asante kwa hichi kizuri ulichoniwezesha kukufanyia siku ya leo, na pia naomba nisamehe makosa yangu

yote niliyokukosea wewe pasipo kujua siku ya leo. Na kama unayakumbuka baadhi uliyoyafanya hakikisha kesho unayarekebisha, na ukishatubu tu usianze kujilaumu laumu!..Ukifanya hivyo utaruhusu mashambulizi ya shetani kukuvamia na kukuletea mawazo yale yale kwamba Mungu

alichukizwa na wewe jana, hivyo hawezi kuendelea kutembea na wewe leo…Kwahiyo siku zote Vaa ngao ya Imani, ili uweze kuizima hiyo mishale ya adui. Mungu wetu wa upendo hakai huko mbinguni na karatasi na kalamu akitiki mabaya tunayoyafanya baada ya sisi kuokoka…hafanyi hivyo, yeye yupo kutazama mema yetu, maadamu tumeshaokoka na

kumwamini na tumeweka mbali Maisha ya dhambi. Basi tunakuwa tunahesabiwa haki kwa Neema na si kwa matendo. Na hivyo kidogo kidogo anatutakasa mpaka unafika wakati tunakuwa wakamilifu kabisa kwake.

Hivyo hizo ni silaha 4 za adui yetu shetani. Sasa kama hizi Habari ni mpya kwako, na kama zimekufungua macho, basi ni dalili ya kwamba ulikuwa huna Ngao mkononi mwako, hivyo

ulimfungulia shetani nafasi ya kukushambulia ndio maana husongi mbele kiimani, na hiyo ni kutokana na kwamba pengine nafasi ya kutafuta kumjua Mungu Zaidi katika Maisha yako ni ndogo, au ulikuwa umesongwa na hivyo kulifahamu Neno imekuwa ngumu kwako, kwahiyo nakushauri mtu wa Mungu usiruhusu tena kusongwa..Neno hili wakristo wote waliofanikiwa ambao umeona wamesimama na hawapelekwi ni kwasababu, wana ngao za Imani mikononi

mwao, ni kwasababu Hivyo vipengele 4 hapo juu wamevishinda tangu zamani. Hivyo ni wewe peke yako umebaki.

Anza kumtafuta Mungu kwa bidii, anza kusoma Neno kwa bidii, usipitishe siku bila kushika biblia, na usomapo usisome kwa kutimiza wajibu, Ukilisoma Neno la Mungu na kulielewa ndivyo linavyokaa ndani yako, na linakupa Imani na maarifa, na ndivyo linavyokuweka huru, Ukilikosa hilo kamwe usitegemee kumshinda shetani, na wala kamwe usitegemee kama utaweza kumtumikia Mungu. Kwasababu shetani hawezi kuruhusu umtafute Mungu kirahisi rahisi hivyo, ni lazima akuletee hivyo vita vya kimawazo, akishinda hivyo atakuletea na vya nje, sasa ni wajibu wetu kufahamu kuwa tupo vitani. Ni lazima upambane kumjua Mungu.

Mathayo 11:12 “Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka”

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

ESTA: Mlango wa 8, 9 & 10. (SIKU KUU YA PURIMU)

KWANINI LEO HII KUNA KUNDI KUBWA LA WAKRISTO WALIORUDI NYUMA?

NIMEOKOKA, ILA MUNGU NDIYE ANAYEJUA NITAKWENDA WAPI.

FAHAMU JINSI KRISTO ANAVYOPONYA WATU ROHO.

JE NI DHAMBI KUWA NA MAHUSIANO KABLA YA NDOA?

Rudi Nyumbani:

Print this post