Monthly Archive Januari 2021

TANGAZO

Jumapili ya tarehe 24 tutakuwa na ibada yetu ya pili. Tunawakaribisha Wakazi wa Daresalaam Na wengineo.

Pamoja na ushirika tutakuwa na muda wa kuuliza maswali ya biblia, Ushauri na maombezi

Hivyo mnakaribishwa wote.

Mahali ni Tegeta Nyuki.

Muda ni saa 3:00 asubuhi mpaka saa 6:30.

Karibuni sana.

Mwl. Denis.
Wingu la Mashahidi.

Kwa mawasiliano: piga +255693036618 au +255789001312

Shalom.

Print this post

KUJIFUNUA KWA YESU KWA PILI.

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe daima. Ni wasaa mwingine tena ambao Mungu ametujalia kuufikia hivyo  nakukaribisha tuyatafakari  kwa pamoja maneno ya uzima ndugu yangu.

Biblia inatuambia kuwa Bwana Yesu alipofufuka kutoka kwa wafu, aliwatokea baadhi ya watu, ambao idadi yao ilikuwa kama  watu 500,(1Wakorintho 15:6) , Lakini ulishawahi kujiuliza ni kwanini iwe hivyo? Je hao watu 500 walikuwa na kitu gani cha ziada kuwashinda wengine wote mpaka watokewe wao tu?

Ni vizuri tukafahamu kuwa hii ni kawaida ya Kristo, kwamba kuna wakati  ataonekana na watu wote, lakini pia upo wakati hataonekana  na watu wote bali wachache tu aliowachagua, Na ndicho kilichotokea hapa, miaka yote 33 aliyoishi duniani, kila mtu angeweza kumtembelea kama angetaka, kila mtu angeweza kwenda kumtazama kama angetaka, lakini mara baada ya kufufuka kwake, hakuna mtu yeyote angeweza kumwona, isipokuwa Yule tu aliyejidhihirisha kwake.

Na ndio maana aliwaambia wayahudi maneno haya Yohana 7:34 “Mtanitafuta wala hamtaniona; nami nilipo ninyi hamwezi kuja”.

Sasa hawa watu 500 ambao walipata neema ya kumwona Yesu baada ya kufufuka kwake, hawakuwa ni watu tu ambao bahati imewaangukia, hawana habari na Yesu, au hawajawahi kumfuatilia au kumsikia,.. Hapana, biblia inatuambia walikuwa ni watu ambao waliambatana naye, tangu akiwa Galiliya mpaka Yerusalemu, yaani tangu ncha moja ya taifa la Israeli mpaka ncha nyingine ya Israeli.

Matendo 13:29 “Hata walipokwisha kumaliza yote aliyoandikiwa, wakamtelemsha katika ule mti, wakamweka kaburini.

30 Lakini Mungu akamfufua katika wafu;

31 akaonekana siku nyingi na wale WALIOPANDA NAYE KUTOKA GALILAYA HATA YERUSALEMU, ambao sasa ndio walio mashahidi wake mbele ya watu”.

Hawa ndio waliotokewa na Yesu mara ya pili, Ni watu ambao walitembea na Yesu, tangu zamani sana, ni watu ambao waliokuwa wanazungumzia habari zake, Mfano wake utaona ni wale watu wawili waliokuwa wanaelekea kile kijiji cha Emau baada ya kufufuka kwake(Luka 24:13)..

Hao ndio watu ambao Yesu aliona kuna umuhimu wote wa kuwatokea  katika utukufu mwingine baadaye. Siku zote wale wanaomuheshimu Mungu, Mungu nao anawaheshimu, wanaomkaribia Mungu, Mungu naye anawakaribia wao.(Yakobo 4:8). Na mmojawapo kati ya hawa ndiye aliyefanywa mtume kuchukua nafasi ya Yuda.

Sasa kutokea kwake mara ya pili kwao, haikuwa maonyesho tu. Bali Kristo aliwapa karama nyingine ambayo iliwafanya kuwa tofauti kabisa na watu wengine. Na karama yenyewe ni kuwa MASHAHIDI WA YESU.  Hao ndio waliochaguliwa na Mungu kuisambaza injili ya Kristo ulimwenguni kote, kwa nguvu za Roho wa Mungu zilizoachiliwa juu yao,

Matendo 10:40 “Huyo Mungu alimfufua siku ya tatu, akamjalia kudhihirika,

41 SI KWA WATU WOTE, BALI KWA MASHAHIDI WALIOKUWA WAMEKWISHA KUCHAGULIWA NA MUNGU, NDIO SISI, TULIOKULA NA KUNYWA PAMOJA NAYE BAADA YA KUFUFUKA KWAKE KUTOKA KWA WAFU.

42 Akatuagiza tuwahubiri watu na kushuhudia ya kuwa huyu ndiye aliyeamriwa na Mungu awe Mhukumu wa walio hai na wafu”.

Soma pia Matendo 2:31-32

Unaona Ikiwa leo hii, hatutaki kujibidiisha kumtafuta Yesu, hatutaki kujifunza Neno lake, hatutaki kusikia habari zake,tunaona kama zinatuchosha, na bado tunasema tumeokoka, tufahamu kuwa, zipo hatua ambazo kamwe hatutakaa tumfikie Yesu.

Tunakosa shabaha pale tunapodhani kumjua Yesu ni kuokoka tu, na kutoa pepo halafu basi. Hatujui kuwa YESU NDIO SIRI YA MUNGU mwenyewe.. ambao utimilifu wote wa Mungu unakaa kwa namna ya kimwili (Wakolosai 2:9). Kiasi kwamba tukifikia utimilifu wote wa kumjua yeye, basi hakuna kitu chochote hapa duniani tutakachoshindwa kufanya, au kukijua.  Na shetani hapa ndipo anapopapiga vita, kwasababu anajua siku mtu akimfahamu Yesu ipasavyo basi habari yake ndio imeishia hapo.

Waefeso 4:13 “hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo;

14 ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu”.

Kwahiyo na sisi tuonyeshe bidii ya kutafuta kumjua yeye, nasi tufikie hatua ya kutufanywa na mashahidi wake kweli kweli , kama alivyofanya kwa mitume wake na wale wengine mwanzoni.

Lakini tukiridhika na Yesu wa kuokokea tu, vivyo hivyo na yeye atajifunua kwetu kama huyo, lakini tukionyesha bidii ya kumtafuta, na kutaka kujua njia zake, na yeye atajifunua kwetu katika nguvu za kufufuka kwake, tutamjua kwa mapana na marefu yake, kama alivyofanya kwa wale watu wachache sana (500). Tutakuwa watu wengine kabisa.

Tuanze kulipigia hatua na hili.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

KUNA MAJIRA MUNGU ATAIVURUGA MIPANGO YETU.

Nini maana ya “mkilichukia hata vazi lililotiwa uchafu na mwili”?

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

Mafundisho

Mataifa ni nini katika Biblia?

Rudi nyumbani

Print this post

KWASABABU MUDA TULIOBAKIWA NAO SI MWINGI.

Mtume alituasa wakati huu wa mwisho ni wakati wa kutojishikamanisha sana na mambo ya mwilini, au ya ulimwenguni. Embu tutafakari kwa pamoja hivi vifungu hapa chini. Anasema.

1Wakorintho 7:29 “Lakini, ndugu, nasema hivi, muda ubakio si mwingi; basi tokea sasa wale walio na wake na wawe kama hawana;
30 na wale waliao kama hawalii; na wale wafurahio kama hawafurahi; na wale wanunuao, kama hawana kitu.
31 Na wale wautumiao ulimwengu huu, kama hawautumii sana; kwa maana mambo ya ulimwengu huu yanapita.
32 Lakini nataka msiwe na masumbufu. Yeye asiyeoa hujishughulisha na mambo ya Bwana, ampendezeje Bwana;
33 bali yeye aliyeoa hujishughulisha na mambo ya dunia hii, jinsi atakavyompendeza mkewe.
34 Tena iko tofauti hii kati ya mke na mwanamwali. Yeye asiyeolewa hujishughulisha na mambo ya Bwana, apate kuwa mtakatifu mwili na roho. Lakini yeye aliyeolewa hujishughulisha na mambo ya dunia hii, jinsi atakavyompendeza mumewe.
35 Nasema hayo niwafaidie, si kwamba niwategee tanzi, bali kwa ajili ya vile vipendezavyo, tena mpate kumhudumia Bwana pasipo kuvutwa na mambo mengine”.

Unaweza kupata picha alikuwa analenga nini hapo? Ni kwamba hatutakiwi tuvutwe kwenye mambo ya ulimwengu sana, mpaka tukasahau kuwa tunahitaji kumtumikia pia Mungu, angali tukiwa hapa dunia ndani ya hichi kipindi kifupi tulichobakiwa nacho.

Hii inatokea pengine mkristo mmoja ameingia katika ndoa, anasahau kabisa mambo ya Mungu, anaanza kujitaabisha na masuala ya mumewe au mkewe ampendezeje, maombi ameacha, kujifunza neno hafanyi tena.. Sasa katika mazingira kama haya Paulo alisema ukiingia kwenye ndoa, na uwe kama hujaoa, au uwe kama hujaolewa, usilikuze sana jambo hilo, mpaka likakufanya ukawa mlegevu kwa Mungu, kwasababu muda tuliobakiwa nao ni mchache.

Kwani  mambo ya kuoa au kuolewa ni ya hapa tu duniani, tukifika huko ng’ambo hayatakuwepo, hivyo si mambo ya kuyatilia mkazo sana, na kusahau mambo ya uzima wa milele  mbinguni.

Mwingine amezama katika masomo, kiasi kwamba hata muda wa kuongea na Mungu wake anakosa kabisa..

Mwingine utakuta ameingia katika biashara, na kwa bahati nzuri Mungu amemfanikisha sana, matokeo yake ni kuwa anasahau kabisa mambo ya rohoni anajikita muda wote katika biashara zake, hatengi tena muda wa kusali, au kwenda ibadani, au wa kumfanyia Mungu kitu.

Biblia inatuambia,

31 “Na wale wautumiao ulimwengu huu, kama hawautumii sana; kwa maana mambo ya ulimwengu huu yanapita”.

Ni kweli tupo katika huu ulimwengu, hatuna budi kuutumia kwa sehemu, lakini tumeaswa, tuwe kama vile hatuutumii, tuwe kama tumejiegesha tu, tusizame huko moja kwa moja, kiasi cha kutufanya tusahau kama sisi ni wapitaji, wenyeje wetu upo mbinguni.

Bali sisi tuishi kama wale mashujaa 300 wa Gideoni, ambao wenyewe, walipopelekwa mtoni kunywa maji, hawakunywa kama Ng’ombe kwa kupeleka midomo yao moja kwa moja kwenye maji, bali walikunywa kwa kuchota kwa mikono yao na kuyalamba kama mbwa midomoni,. Ikiwa na maana kuwa hata maadui zao wangeweza kuja wakati wanakunywa maji yao wasingeweza kuwaua kwa haraka kwasababu wangewaona tokea mbali , tofauti na wale wengine ambao midomo yao ilielekea kwenye maji moja kwa moja, hawaelewi kitu kingine.(Waamuzi 7:4-7)

Vivyo hivyo na sisi, tunaishi hapa duniani, lakini tunapaswa tuishi kwa kuchukulia kawaida kila kitu, ili tusimpe shetani nafasi ya kutuvuta katika mambo mengine, tusizame moja kwa moja kwenye ulimwengu, tunapaswa  tupate na nafasi kwa Mungu, kama ni shule, kama ni biashara, kama ni kazi, kama ni ndoa, kama ni sherehe, kama ni jambo lolote lile, sio la kuliumizia kichwa chako sana, au kulisumbukia, au kuliwazia kupitiliza, au kulifurahia sana.

Tukifanya Hivyo biblia inatuambia tutapata muda pia kwa Bwana. Na matokeo yake, hata siku ile ikifika haitatujilia kwa ghafla kama vile mwizi usiku. Maana biblia inasema ndivyo itakavyoujilia ulimwengu mzima. Na hiyo yote ni kwasababu watakuwa buzy katika mambo ya mwilini wakati huo.

Luka 31: 34 “Basi, jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya; siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo;
35 kwa kuwa ndivyo itakavyowajilia watu wote wakaao juu ya uso wa dunia nzima”.

Kwahiyo kila siku  tulifahamu hili, kuwa sikumoja inapopita, ndivyo tunavyoikaribia ile siku Kuu ya Unyakuo. Hivyo ni wajibu wetu na sisi kuhakikisha ni kwa namna gani tunampendeza Mungu wetu katika hichi kipindi kifupi tulichobakiwa nacho.

Wafilipi 4: 6 “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu”.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

JIFUNZE KUELEWA MAANA YA KUOA/KUOLEWA KABLA YA KUINGIA HUKO.

UFUNUO: Mlango wa 14

Nini maana ya “yasiyokuwapo hayahesabiki”(Mh 1:15)

Kutabana ni nini? (Mika 5:12)

FAHAMU UWIANO MUNGU ANAOHITAJI KUUONA KWETU.

Rudi nyumbani

Print this post

KWANINI MIMI?

Kuna wakati unaweza kupitia mahali ukajikuta upo katika hali ambayo hujui sababu ni nini, haujui kosa lako ni lipi mpaka upokee mapigo mazito kama hayo.  Unabakia kujiuliza maswali kwanini mimi?

Ayubu alipitia mazingira kama hayo, katika maisha yake yote alijitahidi sana kuwa mkamilifu na mwelekevu mbele za Mungu, hakuruhusu dhambi imtawale katika maisha yake yote, alikuwa ni mwombaji, na mkaribishaji mzuri wa wageni, hivyo Mungu akambariki sana.

Lakini ukafika wakati, akashangaa ghafla mambo yamebadilika, mifugo yake yote imeibiwa, mali zake zote zimepotea, kama hilo halitoshi akasikia watoto wake wote 10 wamekufa kwa ajali mbaya sana ndani ya siku moja.. Wakati yupo katikati ya msiba, ghafla tena anaanza kuugua kwa magonjwa ya ajabu, kiasi kwamba inambidi akae kwenye majivu muda wote, alikondoa kiasi cha kuona mifupa tu.

Embu jiweke wewe katika hiyo nafasi, unadhani haitakuwa rahisi kumkufuru Mungu? Ni rahisi sana, na ndicho alichokifanya mke wa Ayubu. Lakini Ayubu hakumkufuru Mungu, yeye hakufikia hatua hiyo mbaya bali aliishia kusema KWANINI MIMI?

Kwanini mimi na si mtu mwingine,…Na hiyo kwanini mimi ilimpelekea mpaka kuanza kulaani, kila kitu kwenye maisha yake, akailaani mpaka siku ya kuzaliwa kwake, akaona kama vile yeye si mtu mwenye bahati, ni heri tu asingezaliwa duniani.

Ayubu 3:2 “Ayubu akajibu, na kusema;

3 Na ipotelee mbali ile siku niliyozaliwa mimi, Na ule usiku uliosema, Mtoto mume ametungishwa mimba.

4 Siku hiyo na iwe giza; Mungu asiiangalie toka juu, Wala mwanga usiiangazie.

5 Ishikwe na giza, giza tupu, kuwa yake; Wingu na likae juu yake; Chote kiifanyacho siku kuwa giza na kiitishe………

11 Mbona si kufa mimi tokea mimbani? Mbona nisitoe roho hapo nilipotoka tumboni?

12 Mbona hayo magoti kunipokea? Au hayo maziwa, hata nikanyonya?

13 Maana hapo ningelala na kutulia; Ningelala usingizi; na kupata kupumzika;”

Ayubu, kila kukicha alitamani afe.(Ayu 7:4)

Hiyo hali inawakumba watu wengi sasa hivi hususani pale wanapopitia matatizo fulani madogo au makubwa, aidha wanapofiwa na wazazi wao, au watoto wao, au wanapopoteza mali zao, au vitu vyao ya thamani, au wanapokumbana na magonjwa mazito yasiyotibika, kama vile kansa, kisukari, au ukimwi, wanajiuliza ni tatizo gani walilolifanya mpaka wayapate magonjwa hayo, mbona wanakula vizuri tu, mbona hawatendi dhambi, inakuwaje wakumbane na hizo shida kwenye miili yao.

Wengine, wanauliza kwanini mimi nizaliwe kipofu, nilimkosea nini Mungu, kwanini nizaliwe mfupi, kwanini niwe mlemavu, kwanini nina mapungufu haya n.k..

Sasa katika haya maswali , kwanini! kwanini! kwanini!.. Mungu naye alianza kumuuliza Ayubu maswali mengine ya ziada, ambayo alitaka na yeye ampe majibu yake. Ukisoma Ayubu 38 na kuendelea utaona maswali aliyoulizwa Ayubu ni yapi, ambayo tunajua yote alishindwa kuyatolea majibu yake..Kwamfano maswali haya aliulizwa;

Ayubu 38:28 “Je! Mvua ina baba? Au ni nani aliyeyazaa matone ya umande?

29 Barafu ilitoka katika tumbo la nani? Na sakitu ya mbinguni ni nani aliyeizaa?

30 Maji hugandamana kama jiwe, Na uso wa vilindi huganda kwa baridi.

31 Je! Waweza kuufunga mnyororo wa Kilimia, Au kuvilegeza vifungo vya Orioni?

32 Je! Waweza kuziongoza Sayari kwa wakati wake? Au waweza kuongoza Dubu na watoto wake?

33 Je! Unazijua amri zilizoamuriwa mbingu? Waweza kuyathibitisha mamlaka yake juu ya dunia?

34 Waweza kuiinua sauti yako mpaka mawinguni, ili wingi wa maji ukufunikize?

35 Waweza kuutuma umeme, nao ukaenda, Ukakuambia, Sisi tupo hapa?

36 Je! Ni nani aliyetia hekima moyoni? Au ni nani aliyetia ufahamu rohoni?”

Akagundua kuwa kumbe ni mambo mengi sana huku duniani, Mungu hajatupa majibu yake, , lakini tunaendelea tu kuishi nayo, wala hatuumizi vichwa vyetu kutaka kuyajua, na maisha yanaendelea kama kawaida. Sasa kwanini tutake kutolea majibu kila hali tunayopitia.

Ayubu baada ya kulijua hilo, alikaa kimya. Akamwambia Mungu hakika nilikosea kuzungumza kuzungumza maneno yasiyofaa. Na baada ya Mungu kugundua kuwa Ayubu kalijua hilo, akaugeuza uteka wake akampa mara dufu zaidi ya vile alivyovipoteza. Na sisi pia, tuliookoka, mambo yanapogeuka na kuwa ndivyo sivyo, sio wakati wa kuanza kulaumu, kwanini iwe mimi na sio Yule,..Kumbuka kila mtu anayo mapito yake, sio kila tatizo utalipatia jawabu lake sasa hivi,  pengine utakuja kujua mbeleni au usijue kabisa, kikubwa mshukuru Mungu, na usonge mbele.Wakati utafika jaribu hilo litaisha, usianza kuuliza maswali ambayo hujui majibu yake, utaishi kulaumu, Mtumaini Mungu.

Songa mbele kama mkristo uliyeokoka..Timiza wajibu wako wa kumwomba Mungu na kumshukuru, na kuishi maisha ya utakatifu, Upo wakati Mungu atakuondolea huo ugonjwa, au hilo tatizo, au hiyo shida.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

HUDUMA YA (ELIFAZI, SOFARI, NA BILDADI).

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 9 (Kitabu cha Ayubu).

Maswali na Majibu

JINSI SHETANI ANAVYOZUIA MAJIBU YA MAOMBI YETU.

KWANINI KRISTO AFE?

Rudi nyumbani

Print this post

Nini maana ya “Andiko huua, bali Roho huhuisha (2Wakorintho 3:6)

Jibu: Tusome..

2Wakorintho 3:6  “Naye ndiye aliyetutosheleza kuwa wahudumu wa agano jipya; si wa andiko, bali wa roho; kwa maana andiko huua, bali roho huhuisha”.

Kuhuisha maana yake ni “kutoa uzima/uhai”, Mungu pekee ndiye anayetoa uzima na kutupa sisi. Hivyo hapo iliposema andiko huua, bali Roho huhuisha Maana yake ni kwamba, maandiko bila ufunuo wa Roho yanaweza kuipoteza roho ya mtu na kuiua kabisa (aidha mtu huyo akafa kiroho au hata kimwili kabisa). Lakini yakitumiwa kwa uongozo wa Roho, yanampa mtu uzima, na hata kama alikuwa amekufa anaweza kufufuka tena.

Sasa tutazame ni kwa namna gani andiko linaweza kumuua mtu kimwili, na baadaye kiroho.

  • Jinsi linavyoweza kumuua mtu kimwili:

Walawi 24:19 “Na mtu akimtia mwenziwe kilema; vile vile kama alivyofanya, naye atafanyiwa vivyo;

 20 jeraha kwa jeraha, jicho kwa jicho, jino kwa jino; vile vile kama alivyomtia mtu kilema, naye atalipwa vivyo”.

Kumbukumbu 19:21 “Wala jicho lako lisiwe na huruma; uzima kwa uzima, jicho kwa jicho, jino kwa jino, mkono kwa mkono, mguu kwa mguu”.

Hapo anasema UZIMA kwa UZIMA, maana yake ni kwamba, mtu aliyetoa uhai wa mwenzake kwa makusudi sharti na yeye uhai wake uondolewe, au kama kamvunja jino, na la kwake pia litaondolewa, kama kampiga na kumtoboa jicho, na la kwake pia litatobolewa.

Kwahiyo hili andiko na mengine mengi yakichukuliwa kama yalivyo yanaua. Na watu wengi walikuwa wanakufa kwa maandiko hayo, ilikuwa mwanamke akifumaniwa katika uzinzi, hukumu yake ilikuwa ni kifo cha kupigwa mawe mpaka afe.

Lakini Roho Mtakatifu alipokuja, aliliweka hilo sawa kwa kinywa cha Bwana wetu Yesu Kristo na kusema..

Mathayo 5: 38  “Mmesikia kwamba imenenwa, Jicho kwa jicho, na jino kwa jino

39 Lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili.

40  Na mtu atakaye kukushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia.

41  Na mtu atakayekulazimisha mwendo wa maili moja, nenda naye mbili.

42  Akuombaye, mpe; naye atakaye kukopa kwako, usimpe kisogo

43  Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako;

44  lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi,

45  ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki”.

  • Ni kwa namna gani andiko pia linaweza kumuua mtu kiroho.

Mfano wa andiko linaloweza kumuua mtu kiroho ni hili…

1Timotheo 5:23 “Tokea sasa usinywe maji tu lakini tumia mvinyo kidogo, kwa ajili ya tumbo lako, na magonjwa yakupatayo mara kwa mara”.

Andiko hili limewapofusha watu macho na kuwafanya wawe walevi, na wasiojali  na shetani, amelipigilia msumari hili, lengo lake ni watu wafe bila kutubu ili waende jehanamu ya moto. Roho za wengi, zimekufa katika andiko hili.

Na andiko lingine ni hili.. Mhubiri 9:5 “kwa sababu walio hai wanajua ya kwamba watakufa; lakini wafu hawajui neno lo lote, wala hawana ijara tena; maana kumbukumbu lao limesahauliwa”.

Andiko hili limeua watu wengi sana kiroho, na kuishia kuamini kwamba hakuna maisha baada ya kifo, na kwamba hakuna jehanamu wala kinachoendelea..Hivyo wengi kwa andiko hili, wameona ni bora kuishi maisha ya kujipenda hapa duniani, na ya kutokujali, kwasababu baada ya kifo hakuna kitakachoendelea, hata akifanya uasherati, hakuna kwenda kuhukumiwa..Hivyo wengi wamekufa na dhambi zao kwa andiko hili. www wingulamashahidi org

Bwana Yesu, Mkuu wa Uzima alisema…

Luka 16:19  “Akasema, Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, na kula sikuzote kwa anasa.

20  Na maskini mmoja, jina lake Lazaro, huwekwa mlangoni pake, ana vidonda vingi,

21  naye alikuwa akitamani kushibishwa kwa makombo yaliyoanguka katika meza ya yule tajiri; hata mbwa wakaja wakamramba vidonda vyake.

22  Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa.

23  Basi, kule kuzimu aliyainua macho yake, alipokuwa katika mateso, akamwona Ibrahimu kwa mbali, na Lazaro kifuani mwake.

24  Akalia, akasema, Ee baba Ibrahimu, nihurumie, umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake majini, auburudishe ulimi wangu; kwa sababu ninateswa katika moto huu.

25  Ibrahimu akasema, Mwanangu, kumbuka ya kwamba wewe uliyapokea mambo mema yako katika maisha yako, na Lazaro vivyo alipata mabaya; na sasa yeye yupo hapa anafarijiwa, na wewe unaumizwa.

26  Na zaidi ya hayo, kati yetu sisi na ninyi kumewekwa shimo kubwa, ili wale watakao kutoka huku kwenda kwenu wasiweze; wala watu wa kwenu wasivuke kuja kwetu.

27  Akasema, Basi, baba, nakuomba, umtume nyumbani kwa baba yangu,

28  kwa kuwa ninao ndugu watano, ili awashuhudie, wasije wao pia wakafika mahali hapa pa mateso.

29  Ibrahimu akasema, Wanao Musa na manabii; na wawasikilize wao.

30  Akasema, La, baba Ibrahimu, lakini kama akiwaendea mtu atokaye kwa wafu, watatubu.

31  Akamwambia, Wasipowasikia Musa na manabii, hawatashawishwa hata mtu akifufuka katika wafu”.

Hapo Roho anasema kuna hukumu baada ya kifo.

Hivyo ni muhimu sana kumpata Roho Mtakatifu, wakati wa kulisoma Neno la Mungu, kwasababu bila yeye ni vigumu kulielewa Neno la Mungu na kila utakapolisoma ni rahisi kutoa tafsiri zako, na si za Roho Mtakatifu.

Kama bado hujampokea Yesu, huwezi kamwe kuyaelewa maandiko, yatakuwa ni magumu, na kila utakapoyasoma utakuwa unapata maana ambazo sio sahihi, lakini pale tu utakapoamua kufanya uamuzi wa kumpokea Yesu moyoni mwako, na ukadhamiria kutubu na kuziacha dhambi zote unazozifanya kwa wazi na kwa siri, na ukawa tayari kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji tele (Yohana 3:23) na kwa Jina la Yesu Kristo, siku hiyo hiyo Roho Mtakatifu ataanza kufanya kazi ndani yako na kuumba jambo jipya.

Bwana akubariki

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

Kuwatema farasi, maana yake ni nini?

Wapendwa nini maana ya hili andiko “Ushuhuda wa YESU ndio ROHO YA UNABII” (ufunuo 19:10)?

IFAHAMU HUZUNI NA FURAHA YA MALAIKA.

INJILI YA MANENO LAINI ITAKUGHARIMU.

Rudi nyumbani

Print this post

WAKATI AHADI INAPOKARIBIA, HUWA KUNA MAMBO YANATOKEA.

Shalom, nakusalimu katika jina lipitalo majina yote la Bwana wa mabwana na Mfalme wa wafalme YESU KRISTO, Mungu mkuu, Sifa na heshima, na utukufu ni vya kwake milele. Yeye ndiye mwokozi wetu, na huo ndio ukweli pekee uliodumu na utakaodumu duniani kwa wakati wote.

Tukisoma kile kitabu cha Matendo ya mitume 7:17 inasema..

 “17 Basi wakati wa ile ahadi ambayo Mungu alimpa Ibrahimu ulipokuwa unakaribia, wale watu wakazidi na kuongezeka sana huko Misri,

18 hata mfalme mwingine akainuka juu ya Misri, asiyemfahamu Yusufu.

19 Huyo akawafanyia hila kabila yetu, na kuwatenda mabaya baba zetu, akiwaamuru wawatupe watoto wao wachanga, ili wasiishi”.

Lipo jambo moja tunaweza kulitazama leo hii, biblia inatuambia wakati ile ahadi Mungu aliyomuahidia Ibrahimu kuwa siku moja uzao wake, utakwenda kuirithi nchi ya Kaanani aliyomuahidia, ulipokaribia, biblia inasema, kuna tukio lilifuata baada ya pale, na tukio lenyewe ni wana wa Israeli kuongezeka kwa kasi sana kule Misri.

Jambo ambalo liliwashtusha wamisri waseme ni nini kimewapata hawa watu mpaka wanazaliana kwa spidi kasi hivi, yaani pengine ndani ya miaka kumi tu , idadi imejizidisha mara 3 ukilishangisha na miaka mingine yote iliyopita huko nyuma, miaka mitatu tena mingine vivyo hivyo. Hilo liliwashtusha sana wamisri mpaka kuona tunazidiwa sasa tubuni njia mbadala..

Kutoka 1:7 “NA WANA WA ISRAELI WALIKUWA NA UZAZI SANA, NA KUONGEZEKA MNO, NA KUZIDI KUWA WENGI, nao wakaendelea na kuongezeka nguvu; na ile nchi ilikuwa imejawa na wao. 8 Basi akainuka mfalme mpya kutawala Misri, asiyemjua Yusufu.

9 Akawaambia watu wake, Angalieni, watu wa wana wa Israeli ni wengi tena wana nguvu kuliko sisi.

10 Haya! Na tuwatendee kwa akili, wasije wakaongezeka; tena, ikitokea vita, wao nao wasije wakashikamana na adui zetu na kupigana nasi, na kutoka katika nchi hii.

11 Basi wakaweka wasimamizi juu yao wawatese kwa mizigo yao. Nao wakamjengea Farao miji ya kuwekea akiba, Pithomu na Ramesesi.

12 LAKINI KWA KADIRI YA WALIVYOWATESA NDIVYO WALIVYOONGEZEKA NA KUZIDI KUENEA. Nao walichukiwa kwa sababu ya wana wa Israeli”.

Umeona? Lakini biblia inatuambia kuongezeka kwao, hakukuwa bure tu bali kulikuwa na sababu, na sababu yenyewe ni kuwa ILE AHADI YA MUNGU ilikuwa inakaribia kwenda kutimizwa juu yao.

Nachotaka uone ni kuwa, sikuzote, ahadi ya Mungu inapokaribia kutimizwa, Mungu huwa anahimiza mambo fulani fulani yafanyike haraka sana ndani ya kipindi kifupi sana kisichoweza kudhaniwa. Wana wa Israeli pengine walikaa zaidi ya miaka 300, kule Misri na uongezekaji wao ulikuwa wa wastani tu, au wa kawaida sana, lakini walipokaribia karibia miaka 400 hapo, ndipo idadi ya watu ikaongezeka kwa ghafla sana.

Jambo hili linafunua nini  kwa agano jipya?

Wengi wetu hatuijui vizuri historia ya ulimwengu, tunadhani mambo yalivyo sasahivi ndivyo yalivyokuwa miaka ya nyuma. Ndugu,fahamu karne ya 20 na ya 21, ndizo karne pekee ambazo zinawashangaza watu wengi sana ulimwenguni hususani wale wanaofuatilia habari za historia, tukisema karne ya 20 tunamanisha kuanzia mwaka wa 1901.

Mambo mengi sana yametimia yaliyokuwa yanazungumziwa na Bwana Yesu, pengine yalionekana kama ni uongo kwasababu hayakuwahi kutimia kwenye miaka yote ya huko nyuma. Lakini ilipotimia karne ya 20 yakaanza kuonekana, Jambo mojawapo ni kuchipuka tena kwa taifa la Israeli, ambalo linafananishwa na mtini. Pili, kutokea kwa vita vya dunia viwili, kulipuka kwa magonjwa yasiyohesabika, na yasiyotibika, hata mafua unayofahamu wewe, hayakuwepo miaka ya 1800,  zote hizo zilizungumziwa katika Mathayo 24, Marko 13 na Luka 21

Na mbaya zaidi, kulipuka kwa wimbi la manabii wengi wa uongo duniani. Hili tumelishuhudia sana sana kwenye hii karne yetu ya 21, kote huko nyuma hakukuwahi kuwa hata na mtu aliyejiita nabii, lakini leo hii ni kitu cha kawaida sana..

Mambo mengine ni Kuongezeka kwa maasi, watu kupenda anasa kuliko kumpenda Mungu, kuongezeka kwa teknolojia, smartphones, n..k ambapo kunatimiza ule unabii wa Danieli unaosema maarifa yataongezea(Danieli 12:4)…

Hayo yote ni kwasababu ile ahadi ya Mungu ya kulinyakuwa kanisa lake inakaribia kutokea hivi karibuni, kwahiyo Mungu anazidisha spidi ya mambo yote yatokee haraka haraka. Na mambo yote yakishatimia ghafla, atatokea Kristo na kulinyakua kanisa lake.

Ni kitendo cha kufumba na kufumbua, hutaona mtu. Tupo ukingoni mwa wakati, Mungu anahimiza mambo yake haraka haraka sasa hivi, Si wakati wa kuwa kama mke wa Lutu, mguu mmoja nje, mwingine ndani, ni wakati wa kumfuata Yesu wewe, kama wewe.

Luka 17:32 “Mkumbukeni mkewe Lutu.

33 Mtu ye yote atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza; na ye yote atakayeiangamiza ataiponya.

34 Nawaambia, usiku huo watu wawili watakuwa katika kitanda kimoja; mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa.

35 Wanawake wawili watakuwa wakisaga pamoja; mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa.

36 Watu wawili watakuwa shambani, mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa.]”

Swali ni Je, umezaliwa mara ya pili, Je, wewe bado ni rafiki wa dunia? Je bado unaishi maisha ya kuwapendeza marafiki na wazazi? Mkumbuke mke wa Lutu.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Ni vitu vipi hivyo viwili visivyoweza kubadilika? (Ebr 6:18)

Je ni wanyang’anyi wawili waliomtukana Bwana Yesu au mmoja?

Bwana Yesu alikufa akiwa na umri gani?

VIKAANGUKA MACHONI PAKE VITU KAMA MAGAMBA.

Rudi nyumbani

Print this post

VIKAANGUKA MACHONI PAKE VITU KAMA MAGAMBA.

Wakati mwingine Mungu anatumia njia za dhahiri kabisa kufunua yale yanayoendelea rohoni. Kwamfano utaona wakati ule Yesu anakutana na yule kichaa, na kuyaamuru yale mapepo yamtoke, tukio lililofuata  baada ya pale ni wale nguruwe kupelekwa moja kwa moja ziwani na yale mapepo na kuuliwa huko. Hiyo ni kufunua kuwa mapepo hayana malengo mengine zaidi ya kuua tu na kuangamiza, wala hakuna pepo zuri au jini zuri kama watu wa dini nyingine wanavyodhani, maadamu una  pepo ndani yako, basi ujue lengo lao ni moja, kukuangamiza tu.

Na ndio maana utaona lile pepo ambalo wanafunzi wa Yesu walishindwa kulitoa, baba wa yule kijana alisema, mara nyingi linamtupa mwanangu kwenye maji..mara nyingine kwenye moto(Marko 9:22)..Fikiria wewe unadhani lengo lake lilikuwa ni nini kama sio kumwangamiza. Hivyo hata leo hii, ukiwa na pepo la uzinzi, ujue kuwa shabaha ni wewe ukutane na ukimwi, ufe kabla ya wakati wako, au hata ukumbane na mabalaa mengi mengi yasiyoeleweka,ili tu uondoke katika hali ya dhambi ujikute kuzimu.

Sasa, tukirudi katika habari ya mwanzo, tulisema Mungu huwa anaruhusu wakati mwingine mambo Fulani yaonekane kwa dhahiri ili kufunua hali  halisi ya mtu ilivyo rohoni.

Sehemu nyingine tena utaona ni pale mtume Paulo, alipokuta na Yesu alipokuwa anaelekea Dameski kafanya kazi yake ya kuliharibu kanisa la Mungu, Na Bwana alipomtokea kama tunavyojua habari, ni kuwa nuru ya Yesu ilimwangazia pande zote, sasa kutokana na kuwa nuru ile ilikuwa kali, ilimfanya awe kipofu wa muda. Mpaka alipokwenda kuombewa na mtu mmoja aliyeitwa Anania baada ya siku tatu ndipo akaona tena.

Lakini baada ya kuombewa kwake, biblia inatuambia, vitu kama magamba vilidondoka machoni pake. Tusome.

Matendo 9:17 “Anania akaenda zake, akaingia mle nyumbani; akamwekea mikono akisema, Ndugu Sauli, Bwana amenituma, Yesu, yeye aliyekutokea katika njia uliyoijia, upate kuona tena, ukajazwe Roho Mtakatifu.

18 MARA VIKAANGUKA MACHONI PAKE VITU KAMA MAGAMBA, akapata kuona, akasimama, akabatizwa;

19 akala chakula, na kupata nguvu. Akawa huko siku kadha wa kadha pamoja na wanafunzi walioko Dameski.

haya magamba yalikuwa kwenye macho ya Paulo sikuzote lakini hakuwahi kuyajua, mpaka siku anaombewa na kudondoka ndipo anajua kitu hicho kilikuwa

Hiyo ilikuwa inafunua hali halisi ya Paulo ilivyokuwa rohoni. Alikuwa amepofushwa kikweli kweli na shetani, kwa kuwekewa haya  magamba ya adui, bila hata ya yeye maskini  kujijua.

Sasa haya magamba ya adui yapoje?

Haya, hayana malengo ya kuziba kila mahali katika maisha ya mtu hapana, haya yapo mahususi kukuziba lile eneo linalohusiana na kumjua Mungu.  Unaweza ukawa na elimu yako nzuri, unaweza ukawa na hata na fedha nyingi, lakini unaweza ukashindwa kuiona njia Ya wokovu wa Mungu.

Pengine utakuwa mwepesi hata katika kufanya mambo mengine yote, utakuwa mwepesi kuelewa hata kanuni nyingine za maisha ya kila siku, lakini utakosa wepesi wa kuifahamu njia ya wokovu.

Ukihubiriwa habari za msalaba, kwako zinakuwa kama ni habari  za kishamba vile, hata ukielezwa habari za kuzimu  hazikushtui tena, haijalishi utatolewa na shuhuda nyingi kiasi gani, kwako ni kawaida tu, na ndio maana unaendelea na ulevi wako na uzinzi wako badi leo hii, sasa ukiona upo katika hali hiyo basi ufahamu magamba hayo ya rohoni yameshawekwa kwenye macho yako pasipo wewe kujijua. Pengine ulichobakiwa nacho ni kuisifia tu dini yako.

Na hali hiyo inaweza kuwa mbaya kiasi kwamba ukawa hata unaupinga wokovu, na kufanya vita nao kama ilivyokuwa kwa Paulo…Lakini jiulize  unadhani Paulo alikuwa amekusudiwa kuwa mtu wa namna ile, ? Jibu ni hapana, ndio maana baada ya kuondolewa magamba hayo, akaupenda wokovu kwa namna isiyo ya kawaida, akawa mhubiri nambari moja wa njia ya wokovu.

Hii ni kazi ambayo shetani anaifanya kila kukicha, watu wanapofushwa macho yao ya rohoni, wasimjue Mungu, au wasione umuhimu wa wokovu, angali wakiwa bado hapa duniani.

2Wakorintho 4:3 “Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea; 4 ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu”.

Magamba haya ukiyaendekeza ndani ya maisha yako, madhara yake utakuja kuyaona baada ya kifo. Kwasababu siku utakapokufa moja kwa moja utajikuta kule kuzimu, Na wewe huko utakuwa katika majuto yasiyokoma, kama ya yule tajiri wa Lazaro(Luka 16:19-31)… Mahali ambapo aliomba sana ndugu zake wasifike huko..

Ndugu yangu watu wanaoshuka kuzimu kila siku idadi yake haihesabiki, na wote huko laiti tungeonyeshwa hali zao zilivyo, jinsi wanavyojuta, jinsi wanavyosema tulipofushwa kiasi gani mpaka tukaudharau msalaba, na leo tupo hapa, tusingeuchukulia wokovu wetu juu juu tu. Hivyo tubu dhambi zako, mgeukie Kristo, na yeye atakuokoa. Epuka magamba haya ya ibilisi.

Kwasababu siku hizi ni za mwisho, na Kristo yupo mlangoni kurudi.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

NJIA YA KUPATA WOKOVU.

MZAZI, JALI MAISHA YA KIROHO YA MTOTO WAKO.

JE! JICHO LAKO LINAONA NINI KATIKATI YA MAJARIBU?

CHUKIZO LA UHARIBIFU

Rudi nyumbani

Print this post

JINSI PAULO ALIVYOPAMBANA NA UJINGA WA ROHONI.


Contact

Paulo katika kazi yake ya utume, hakuwa tu na jukumu la kuwahubiriwa watu Kristo  ili wamwamini, kisha wapokee ondoleo la dhambi halafu basi..Hapana, bali pia ni mtu ambaye alikuwa anatia bidii nyingi sana katika kuwajuza watu juu ya ukweli wote wa Mungu na siri nyingine zilizojificha katika maandiko tangu zamani.

Na ndio maana utaona alisema..

Waefeso 5:17 “KWA SABABU HIYO MSIWE WAJINGA, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana”.

Paulo alipiga vita ujinga ambao watu wanao kuhusu Mungu, kwasababu alijua ni jinsi gani unavyoweza kumgharimu mkristo kwa sehemu kubwa. Ujinga ni ile hali ya mtu kukosa maarifa ambayo kama angeyapata basi yangemsaidia kuishi au kutenda mambo fulani kwa ufanisi mahali alipo.. Kwamfano, mtu ukikosa kufahamu kuwa duniani kuna kitu kinachoitwa teknolojia, na kwamba ukitaka kuwasiliana na mtu aliye mbali utatumia kifaa kinachoitwa simu,

Sasa wewe hataki kusikia habari za simu, badala yake unataka tu kukaa maporini , kuwinda swala, kuna wakati utafika utahitaji kuwasiliana na ndugu zako wa mbali, hapo ndipo itakugharimu utumie  miguu yako au punda kwenda kuwafuata na hiyo pengine itakuchukua mwezi mzima kwenda na kurudi, kiasi kwamba kama angepata maarifa ya simu, au vyombo vya moto basi kuwasiliana kwako au kusafiri kwako kungekuwa ni kurahisi sana na kwa haraka.

Vivyo hivyo na katika Ukristo, tunakosa maarifa mengi sana, na hiyo inapelekea pengine tunashindwa kuufurahia wokovu wetu , au kuona safari  hii ni ngumu sana, au kushindwa kabisa kustahimili mengi.  Siku zote Hatuwezi kumtumikia Mungu, juu ya kiwango cha ufunuo tulichonacho kuhusu yeye. Kiwango chako cha kumwelewa Mungu ndicho kitakachoeleza maisha ya wokovu unayoishi sasa.

Sasa Mtume Paulo ni mtu ambaye alikuwa anatamani kupata maarifa ya kutosha kuhusu ufalme wa mbinguni, na ndio maana siri nyingi zihusuzo kanisa, na Mungu tunazipata katika nyaraka zake.Na ndio maana sehemu nyingi utaona anasema Neno hili SITAKI MKOSE KUFAHAMU. Akiwa na maana hataki tuwe wajinga..

Embu tuangalie baadhi ya vitu ambavyo alitaka sisi tusikose kufahamu.

  1. Tumaini la ufufuo wa wafu:

Anasema..

1Wathesalonike 4:13 “Lakini, ndugu, hatutaki msijue habari zao waliolala mauti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na matumaini”.

Ukiendelea kusoma pale utaona anaeleza jinsi siku ya unyakuo itakavyokuwa, kwamba utatangulia kwanza ufufuo wa wafu, hivyo wewe kama ni mkristo, ukiifahamu siri hiyo kwamba lipo tumaini la kufufuliwa na kuonana wa wapendwa wetu katika Imani waliotutoka, hatutakuwa na huzuni ya kupitiliza, kama watu wa kidunia walivyo, hatutakuwa wa kulalamika, na kulaumu laumu muda wote.

2) Kuhusu hukumu watakayokabidhiwa watakatifu.

1Wakorintho 6:2 “Au hamjui ya kwamba watakatifu watauhukumu ulimwengu? Na ikiwa ulimwengu utahukumiwa na ninyi, je! Hamstahili kukata hukumu zilizo ndogo?”

Watakatifu watakaoshinda hawatahukumu tu ulimwengu, bali mpaka na malaika, Je ulishawahi kulifikiria hilo wewe utawahukumuje malaika? Fikiria tena hilo, uone ni  mambo makubwa kiasi gani Mungu amewaandalia watu wake huko mbeleni.

3) Siri ya Yesu iliyojificha katika agano la Kale.

1Wakorintho 10:1 “Kwa maana, ndugu zangu, sipendi mkose kufahamu ya kuwa baba zetu walikuwa wote chini ya wingu; wote wakapita kati ya bahari;

2 wote wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu na katika bahari;

3 wote wakala chakula kile kile cha roho;

4 wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo”.

Paulo anatufunulia siri nyingine kuwa hatupaswi kusoma agano la kale kama historia Fulani tu, tunapaswa tujue ndani ya historia zile Kristo amejificha, na Hivyo tunapaswa tusomapo tumwone Kristo, kwasababu vyote vile vilimfunua yeye. Hivyo Paulo anatuasa tusiwe wajinga pia katika hilo, tusome mawazo yetu tukiyaelekeza kwa Kristo.

4) Kuhubiri injili kuna dhiki.

2Wakorintho 1:8 “Maana ndugu, hatupendi, msijue habari ya dhiki ile iliyotupata katika Asia, ya kwamba tulilemewa mno kuliko nguvu zetu, hata tukakata tamaa ya kuishi”.

Wengi tunadhani katika kumtumikia Mungu ni mremeko tu wakati wote, hapana, Bwana Yesu kiongozi wetu alipitia dhiki, mitume pia walipitia dhiki wakati mwingine, vivyo hivyo na wewe, unapaswa ulielewe hilo, ili kusudi kwamba litakapotokea, usije ukawa mjinga kwa kuacha kuifanya kazi ya Mungu, ukasema huyu ni shetani, kwani Mungu sikuzote haruhusu watu wake wapitie dhiki.

5) Miili yetu ni Hekalu la Roho Mtakatifu.

1Wakorintho 3:16 “Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?

17 Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi”.

Anataka tufahamu kuwa hii miili tuliyopewa na dhamana, ni mali ya mwingine sio yetu, hivyo tuithamini kwasababu tukiiharibu kwa uzinzi, au pombe, au michoro, au chochote kile, tutaharibiwa na sisi. Hilo tusiwe wajinga, wengi wameuliwa na Mungu kwa njia hiyo.

6) Utumishi wa Madhabahuni.

1Wakorintho 9:13 “Hamjui ya kuwa wale wazifanyao kazi za hekaluni hula katika vitu vya hekalu, na wale waihudumiao madhabahu huwa na fungu lao katika vitu vya madhabahu?”

Paulo hataki watu wawe  wajinga pia kufahamu, watumishi wa Mungu wana haki ya kula vya madhabahuni, kwasababu ndivyo Mungu alivyoagiza na wala sio mwanadamu. Hivyo sio jambo la kujadiliana nalo au kushangaa utakapokutana nalo.

7) Karama za Rohoni.

1 Wakorintho 12:1 “Basi, ndugu zangu, kwa habari ya karama za roho, sitaki mkose kufahamu”.

Hapa yapo makundi mawili ya wakristo, lipo kundi ambalo haliamini kabisa, au haliruhusu karama za Mungu kutenda kazi katika kanisa la Kristo, wakisikia kuna mtu anakarama ya kuona maono wanasema ni shetani, wakiona kuna mtu ananena kwa lugha wanasema huyo sio Roho. Hivyo utakuta kanisa limebakiwa kuongozwa na wenyeviti na makatibu, na maaskofu- jina, na makasisi, basi, hakuna chochote cha Zaidi ya litrujia kufuatwa.

Kundi lingine,  ni lile lisiloweza kumbanua karama za Roho, huduma za Roho, Utendaji kazi na Ujazo/Ubatizo  wa Roho Mtakatifu. Haya yote Mtume Paulo alitaka tusiwe wajinga, matokeo yake ni kuwa leo hii utakutana na watu wengi wenye karama huku wakiendelea na maisha yao ya kale wakidhani kuwa wana Roho Mtakatifu kumbe walishaachwa zamani, japokuwa karama zao zinaendelea kufanya kazi.

8) Mpango wa Mungu kwa mataifa.

Warumi 11:25 “Kwa maana, ndugu zangu, sipendi msiijue siri hii, ili msijione kuwa wenye akili; ya kwamba kwa sehemu ugumu umewapata Israeli, mpaka utimilifu wa Mataifa uwasili”.

Hii ni siri kubwa ambayo  tukiijua  hatutaishi maisha ya patapotea kwenye ukristo wetu, siku tukifahamu kuwa Utimilifu wa mataifa utawasili, na kwamba kuanzia huo wakati na kuendelea sisi hatutakuwa na neema tena ya kuupokea wokovu, bali itarudishwa tena Israeli kwa kipindi kifupi, ndipo tutakapoishi maisha ya umakini sana katika Ukristo wetu.

Wengi wetu tunadhani, tutaendelea tu hivi hivi mpaka Yesu atakaporudi, Ndugu, Wokovu utaishia kwa wayahudi sio sisi. Kwahiyo tukiwa wajinga tukidhani kuwa tutaendelea hivi hivi, tujue tupo katika hatari kubwa sana ya kuuokosa, Unyakuo. Bwana Yesu kuna wakati atasimama, na kuufunga mlango. Wakati huo utakuwa ni hapa hapa duniani, na sio mbinguni. Kwasababu Utimilifu wa mataifa utakuwa umewasili. Mungu atakuwa ameshamalizana na sisi, utakuwa ni wakati wa wayahudi tena.

Embu jiulize, Je, ikiwa neema hiyo inarudishwa kule Israeli, utampatia wapi tena Kristo, na wakati Roho Mtakatifu hayupo tena juu yako. Ikiwa leo hii, unamkataa unampinga, angali neema ipo, unadhani nafasi hiyo itakuwepo tena? Hivyo usiichezee hii neema ambayo ndio tunakaribia kumaliza nayo. Dalili zote zinaonyesha kuwa hatuna muda mrefu Unyakuo utapita. Wafu watafufuliwa, na sisi tutaungana nao kwenda kumlaki Bwana Yesu mawinguni.

Hivyo tubu dhambi zako mgeukie Mungu.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

MPAKA UTIMILIFU WA MATAIFA UTAKAPOWASILI.

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita..

UTAWALA WA MIAKA 1000.

CHUKIZO LA UHARIBIFU

Rudi nyumbani

Print this post

JE UNAIFANYA KAZI YA MUNGU?

Marko 13:32  “Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba.

33  Angalieni, kesheni, [ombeni], kwa kuwa hamjui wakati ule utakapokuwapo.

34  Mfano wake ni kama mtu mwenye kusafiri, ameiacha nyumba yake, amewapa watumwa wake amri, na kila mtu kazi yake, naye amemwamuru bawabu akeshe.

35  Kesheni basi, kwa maana hamjui ajapo bwana wa nyumba, kwamba ni jioni, au kwamba ni usiku wa manane, au awikapo jimbi, au asubuhi;

36  asije akawasili ghafula akawakuta mmelala.

37  Na hilo niwaambialo ninyi, nawaambia wote, Kesheni”.

Nyumba ya Mungu inayozungumziwa hapo ni Kanisa lake, na kanisa sio jengo, bali ni mkusanyiko wa watu waliomwamini Kristo, (walioitwa kutoka katika ulimwengu wa dhambi, na kuingizwa katika neema ya kumjua yeye Wakolosai 1:13). Jengo ni mahali kanisa linapokutanika kumwabudu Mungu, kumshukuru, kumwimbia na kufarijiana, kuonyana pamoja na kukumbushana mambo ya msingi katika safari ya Imani.

Sasa katika mfano huo tunaona Bwana anaunganisha vitu viwili kwa pamoja; Anaunganisha shughuli za nyumba yake na ujio wake. Maana yake kuna vitu anategemea avikute vinaendelea kufanyika katika nyumba yake, na kila mtu ambaye ni amemwita na kumtoa katika ulimwengu wa dhambi,  kwa ufupi ni kwamba anataka akute kila mtu yupo kwenye shughuli yake fulani, aliyompangia aifanye..

Kama ndani ya nyumba ulipangiwa kazi yake kuhakikisha usafi wa nyumba pamoja na choo, anataka akija akukute upo bize katika shughuli yake hiyo, na choo akikute kisafi muda wote, kadhalika kama mtu kazi yake ilikuwa ni ulinzi anataka akija amkute yupo macho muda wote, anazunguka huku na huko kuhakikisha usalama wa nyumba n.k.

Na katika kanisa la Kristo kuna kazi, hatujaitwa tukae tu…Bali tuifanye kazi yake, kwa karama alizotupa… Na vipawa alivyotupa sio vya maonyesho, mlinzi wa getini hajakabidhiwa ile bunduki na zile sare ili ajisifu yeye ana silaha, au ni shujaa, au atembee na hiyo silaha mtaani na kujionyesha, kwamba ni nani kama yeye, na kwamba yeye ni zaidi ya wote, ana uwezo wa kuua wote kwa dakika moja. Hapana, bali alipewa silaha hiyo kwaajili ya ulinzi wa pale alipowekwa,Sio kwa sifa.

Na karama za rohoni zote hatujapewa kwaajili ya sifa zetu, bali kwaajili ya kazi ya nyumba ya Mungu, kama una karama ya kinabii, au kiinjilisti au nyingine yoyote hujapewa kwa lengo la kujisifu, bali ili uwatumikie wengine katika nyumba ya Mungu. Kama Mungu kakubariki sauti nzuri ya kumwimbia, hujapewa hiyo kwaajili ya sifa zako, wala Mungu hajakupa kwasababu anataka kukuinua kuliko wengine, bali amekupa ili kwa kuimba kwako watu watubu wamgeukie yeye, huku wewe mwenyewe ukiwa kielelezo. Hiyo ndio kazi uliyoitiwa uifanye.

Kwahiyo Kristo anataka akija akute kazi yake inafanyika ipasavyo, kila mtu katika eneo lake.

“Mfano wake ni kama mtu mwenye kusafiri, ameiacha nyumba yake, amewapa watumwa wake amri, na kila mtu kazi yake, naye amemwamuru bawabu akeshe”.

Kwahiyo ni kama vile tupo katika jaribio, kila mtu anajaribiwa uaminifu wake kwa Mungu kulingana na kile Mungu alichokiweka ndani yake.

Na anasema anakuja haraka sana, na ujira wake (yaani mshahara wake) upo mkononi mwake..

Ufunuo 22:12 “Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo.  Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho”.

Kwahiyo huu sio wakati wa kuchezea karama au karama Mungu alizoziweka ndani yetu, ni wakati wa kuzifanyia kazi, kwasababu muda uliobaki ni mchache mpaka Kristo awasili, si wakati tena wa kulala, na kusema nitatubu kesho, nitamtumikia Mungu kesho, ni wakati wa kusema kila kitu kinachohusiana na ufalme wa mbinguni naanza kukifanya leo.

Na kama hujaokoka, huwezi kumtumikia Mungu..utafanyaje kazi katika kampuni ambalo hujaajiriwa??..Hivyo unapoamua kuokoka (yaani kumkabidhi Yesu maisha yako) unasajiliwa katika ufalme wa mbinguni, na hivyo Roho Mtakatifu anakupangia kazi kama anavyotaka yeye na si kama unavyotaka wewe au mtu mwingine yeyote. Kwahiyo kama hujampokea Yesu tubu leo kwa dhati huku ukiziacha kwa vitendo dhambi zote ulizokuwa unazifanya hapo awali. Kama utahitaji msaada zaidi katika hatua hii ya kumpokea Yesu, unaweza kutujuza inbox, au mtafute mtu yeyote aliye mtumishi wa Mungu karibu na wewe atakusaidia.

Na pia kama umeshaokoka, lakini unashindwa kuelewa karama/au huduma Mungu anayotaka umtumikie kwa hiyo, wasiliana na sisi tutakupa mwongozo wa jinsi ya kujua Neema ya Mungu iliyo juu yako.

Mwisho, kumbuka Bwana Yesu alisema katika Luka 9:23 “Akawaambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake KILA SIKU, anifuate.”.

Kwahiyo katika kumfuata Yesu ni lazima tujikane kila siku, na si siku moja tu wala mara moja tu.

Bwana atubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

Bawabu ni nani/nini?

UJIO WA BWANA YESU.

TAWI LIZAALO HULISAFISHA ILI LIZIDI KUZAA.

UTAKASO NI SEHEMU YA MAISHA YA MKRISTO YA KILA SIKU.

MATARAJIO YA KILA MWANADAMU DUNIANI NI YAPI?

Rudi nyumbani

Print this post

Majina mbalimbali ya Mungu na maana zake.

Mungu ni mmoja tu, lakini katika umoja wake amekuwa akijifunua katika majina mengi, kulingana na  uweza wake alionao, au majira Fulani yaliyopita, au matukio ya namna tofauti tofauti  yaliyotokea. Ni sawa, ni raisi Fulani aitwe JOHN, lakini huyo huyo anaweza akaitwa baba sehemu fulani, akaitwa mjomba sehemu nyingine , mhandisi kwa watu fulani, amiri jeshi mkuu eneo Fulani, babu sehemu nyingine n.k.

Unaona utaona vyeo vyote hivyo vimekuja aidha kulingana na wakati, au matukio, au nafasi aliyopo au ujuzi alionao n.k. Na vivyo hivyo Mungu wetu , alijifunua katika  majina mengi, ambayo leo hii tutayatazama kwa ufupi.

ELOHIMU: Mungu mwenye uweza, muumbaji  wa milele, mwenye nguvu (Mwanzo 1: 1, 17:7, Yeremia 31:33)

ADONAI: Mungu Mwenye enzi yote,kimbilio imara Mwa 15:2‐8, Kut 6:2‐3

EL-ELYONI:  Mungu Aliye juu zaidi ‐Mwa14:18, Dan 4:34

YEHOVA-RAFA: Mungu-Atuponyaye. (Kutoka 15:26.).

YEHOVA EL – SHADAI: Mungu Ututoshelezaye (Mwanzo 17:1)

YEHOVA-NISI: Mungu ni Bendera yetu (Berani ya vita) (Kutoka 15:26).

YEHOVA-YIRE: Mungu atupaye (Mwanzo 22:14)..

YEHOVA-ROHI: Bwana ndiye mchungaji wangu (Zab 23)

YEHOVA-MEKADISHKEMU: Bwana atutakasaye (Kutoka 31:13)

YEHOVAH SABAOTHI: Bwana wa Majeshi (1 Samweli 1:3)

YEHOVA SHAMA: Bwana Yupo Hapa (Ezekiel 48:35).

YEHOVA EL-OHEENU: Bwana Mungu Wetu (Zaburi 99:5,8,9)

YEHOVA SHALOM: Bwana ni Amani Yangu (Waamuzi 6:24)

YEHOVA TSIDKEMU: Bwana ni Haki Yetu (Yeremia 23:6)

YEHOVA OLAMU: Mungu wa milele Zaburi 90:1-3

YEHOVA  EL- GIBBORI: Mungu Mwenye Nguvu ( Isaya 9:6-9)

YE-SHUA (YESU): Mungu utuokoaye.(Mathayo 1:21 )

Jina Hili la YESU ndio jina tulilonalo mpaka sasa. Kwa kupitia hili ndio tunapata wokovu, kwa jina hili ndio tunamshinda adui, kwa jina hili ndilo tunapata Baraka, na kwa jina hili ndio tunaishi.

Lakini biblia inatuonyesha pia jina hili sio la kudumu, Upo wakati Kristo atakuja na jina jipya,(Ufunuo 19:12 ) jina hilo wakati huo litakuwa sio la Ukombozi tena, sio la kurehemu tena, bali litakuwa ni jina la kifalme. Na ndio maana wakati huu ambao angali bado neema ipo, usiruhusu, ikupite ikiwa wewe ni bado mwenye dhambi, Leo hii Kristo bado yupo kama kuhani mkuu akitupatanisha sisi na Mungu, ikiwa na maana kuwa mlango wa rehema bado upo wazi kwa kila mtu atakayetaka kuuingia, Lakini hautakuwa wazi sikuzote. Kwani dalili za kurudi kwa Yesu mara ya pili zimeshatimia zote, tunachongojea ni unyakuo tu.

Ikiwa upo tayari leo kumpa Yesu maisha yako leo ayaokoe basi huo utakuwa ni uamuzi wa busara sana kwako, Hivyo fungua hapa, kwa ajili ya kuongozwa sala ya Toba >> KUONGOZWA SALA YA TOBA

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

JINA LA MUNGU NI LIPI?

JE! DAMU INA UMUHIMU WOWOTE KATIKA MAISHA??

RABI, UNAKAA WAPI?

RUDIA, TENA NA TENA KUMWOMBA MUNGU USIKATE TAMAA.

WAPE WATU WANGU RUHUSA ILI WAPATE KUNITUMIKIA.

Rudi nyumbani

Print this post