Title February 2021

Nini maana ya kuruzuku katika biblia?

Maana ya Neno “kuruzuku” ni “kutoa Riziki”. Unapompa mtu mwingine riziki hapo umemruzuku. Katika biblia tunaona neno hilo limetokea mara kadhaa Mungu akiwaruzuku watu.

Katika kitabu cha Nehemia tunaona Neno hilo likitajwa..

Nehemia 9: 21 “Naam, muda wa miaka arobaini uliwaruzuku jangwani, wasihitaji kitu; nguo zao hazikuchakaa, wala miguu yao haikuvimba”.

Na pia tunaliona neno hilo katika kitabu cha Zaburi.

Zaburi 65:9 “Umeijilia nchi na kuisitawisha, Umeitajirisha sana; Mto wa Mungu umejaa maji; Wawaruzuku watu nafaka Maana ndiwe uitengenezaye ardhi”.

Na mwisho tunaona neno hilo katika kitabu hicho hicho cha Zabur 68,

Zaburi 68:10 “Kabila yako ilifanya kao lake huko; Ee Mungu, kwa wema wako uliwaruzuku walioonewa”.

Kama Bwana alivyowaruzuku wana wa Israeli Jangwani, mahali ambapo hapakuwa na kilimo wala maji, lakini Mungu wa mbingu na nchi akawapa MANA kutoka mbinguni na maji kutoka mwambani, na nyama kimiujiza, akakupe na wewe mtu wa Mungu uliyempokea na kumwamini Yesu Kristo, riziki zote za mwilini na rohoni. Akakuruzuku kwa riziki nyingi katika jina la Yesu.

Amen

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Sadaka ya unga na sadaka ya kinywaji zilikuwaje?

NAWAAMBIA MAPEMA!

NAWE UTAGEUZWA KUWA MTU MWINGINE.

 Nini maana ya “Uchungu wa mauti ni dhambi, na nguvu za dhambi ni torati”

Rudi nyumbani

Print this post

Maziwa yasiyoghoshiwa ni nini? Kwanini biblia inatumia mfano huo?

1Petro 2:1 “Basi, wekeni mbali uovu wote na hila yote, na unafiki na husuda na masingizio yote. 2 Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu”;

Kughoshi ni kugeuza, au kutia dosari, lengo likuwa ni kukifanya kionekane kama kile cha kwanza, leo hii utasikia maneno kama ‘vyeti vimeghoshiwa’, maana yake ni kuwa wametengeza vyetu bandia ili waonekane kama na wao ni wahitimu kumbe ni uongo. Utasikia tena watu pia ‘wanaghoshi fedha’, maana yake ni kuwa wanatengeneza fedha bandia ili zionekane kama zile halisi, zifae kwa manunuzi.

Sasa mtume Paulo aliposema yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, alitumia mfano wa maziwa yanyonywao na watoto wachanga kufananisha na Neno la Mungu. Kwamba maziwa yale kwa asili huwa hayagoshiwi, hayatiwi kitu kingine chochote, wala hayaingiliwi na uchafu wowote, kwani mtoto hujafyonza moja kwa moja kutoka kwa mama yake.

Lakini kama vile leo hii utaona mambo yamebadilika watoto wachanga hawapewi tena maziwa  yanayotoka moja kwa moja katika matiti ya mama zao, badala yake wanakwenda kuletewa maziwa mengine ya kwenye makopo, ya ng’ombe, ambayo kwa kutazama unaweza kuona yanafanana sana na yale ya mama,  lakini kumbe yapo mbali sana kiubora na kiafya kwa mtoto mchanga.  Utakuta hayo ya kwenye makopo yamechanganywa na vitu vingine wanavyoviita virutubisho, na kemikali baadhi za kuyafanya yasiharibike mapema..Sasa maziwa hayo ni maziwa yaliyoghoshiwa. Mtoto ananyweshwa kama mbadala wa maziwa halisi ya mama yake, na kamwe hayawezi kuwa na ubora ule ule kama wa yale ya mama.

Vivyo hivyo na sisi kama wakristo, tunapaswa tuyafyonze maziwa yanayotoka moja kwa moja kwa Mungu wetu mwenyezi, yanayotoka katika maandiko matakatifu (yaani BIBLIA), hayo ndio matiti yetu. Ili tuukulie wokovu katika afya njema za rohoni Mungu anazozihitaji.  Lakini kama tutataka tuikulie injili nyingine ambayo si ile tunayoisoma katika maandiko tufahamu, tunajidhohofisha wenyewe.

Na ndio hapo, utashangaa kwanini mkristo anashindwa kusimama vema katika Imani, leo yupo sawa kesho kaanguka katika dhambi, utakuta mwingine yupo katika kanisa kwa miaka mingi, lakini ukitafuta matunda yoyote kwa Mungu wake hana, ukitafuta ni wangapi alishawahi waleta kwa Kristo, hupati, hayo yote ni matokeo ya kunywa maziwa ya aina nyingine yasiyomtia mtu nguvu rohoni.

Ukiona unakaa mahali na kuhubiriwa injili ya mafanikio tu wakati wote,  auhubiriwi utakatifu, au mambo ya ufalme wa mbinguni na siku za mwisho, ujue kuwa hayo ni maziwa ya kughoshiwa, yanayofanana na yale halisi, hayatakusaidia chochote katika kuushinda ulimwengu.

Lakini mtume Paulo anasisitiza kwa kusema..‘Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu’

Unaona ni wajibu wetu kuitamani injili ya kweli, injili ile iliyoandikwa na mitume kwenye biblia, ili kwamba tuweze kuukulia wokovu wetu vema inavyostahili, tusishindwe na shetani kivyepesi, pia ili tuwe watu wa kumzalia Mungu matunda katika ukristo wetu.

Kumbuka hizi ni siku za mwisho, mafundisho mengi ya uongo yameenea sasa ulimwengu mzima, na ndio maana Bwana Yesu alituonya na kusema .ANGALIE JINSI MSIKIAVYO (Luka 8:18)..Akiwa na maana tuwe makini na yale tunayohubiriwa kwasababu si yote yanajenga roho zetu.Mengi ya hayo ni feki, yanatia ubovu roho zetu.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA WARAKA WA PILI WA YOHANA.

MAMA UNALILIA NINI?

Bwana Yesu alimaanisha nini kusema “Saa yangu haijawadia?”

Je! Daudi hakuwa mtoto wa ndoa wa Yese? (Zab 51:5)

MAPEPO YANATAFUTA HIFADHI NDANI YAKO KWA BIDII SANA.

Je ni kweli imani ya mtu ndiyo itakayomuokoa, na si kitu kingine?

Rudi nyumbani

Print this post

Je ni kweli imani ya mtu ndiyo itakayomuokoa, na si kitu kingine?

JIBU: Kama ulishawahi kuwahubiria watu kadha wa kadha habari za wokovu, naamini ulishawahi  kukutana na watu baadhi wakikueleza, maneno haya, kwamba haijalishi wewe ni dini gani, au unaamini nini, imani yako ndiyo itakayokuokoa, ukiwa na imani kuwa  Mungu  yupo, hilo tu, linakutosha, hayo mengine si ya muhimu sana.

Atakuambia hata anayeabudu kupitia mti, au anayeabudu kupitia ng’ombe Mungu anamsikia hata, anayeabudu kupitia Rozari Mungu anamsikia kinachojalisha ni imani yake tu wala si kingine.

Ni kweli kabisa mawazo yao ni sahihi, kwamba imani ni daraja la kumfikia Mungu, kama vile maandiko yanavyosema katika..

Waebrania 11:6 “Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao”.

Lakini hawajui kuwa Imani ambayo haijakamilishwa haikufikishi popote, nikiwa na maana imani ambayo haijulikana msingi wake ni upi, imejengwa katika nini  haikupeleki popote.. Kitendo cha kuamini tu Mungu yupo, hata wachawi wanaamini hivyo, na ukiwauliza watakuambia ndio namwamini Mungu na pia ananisaidia, mapepo nayo yatakuambia sisi nasi tunamwamini Mungu na pia tunatetemeka tunapolisikia jina lake..

Utalithibitisha hilo katika..

Yakobo 2:19 “Wewe waamini ya kuwa Mungu ni mmoja; watenda vema. Mashetani nao waamini na kutetemeka”.

Sasa kama unasema mimi naamini Mungu, na namwogopa, ujue kuwa huna tofauti na mashetani. Kama unadhani utakwenda mbinguni kwa imani ya namna hiyo, basi ujue mashetani watakutangulia kwanza mbinguni kisha wewe utayafuata baadaye.

Bwana Yesu alisema wazi kabisa katika Yohana 14:6..”mimi ndio njia na kweli na uzima, mtu hafiki kwa Baba isipokuwa kwa njia yangu mimi.” Akiwa na maana hakuna imani yoyote itayokufikisha mbinguni isipokuwa ile ya kumwamini yeye (Yesu Kristo).

Ni sawa na leo useme unayo simu, yenye line nzuri, yenye salio la kutosha, hivyo unaweza sasa kuwasiliana na mimi wakati wowote.. Jibu ni la! kama hutakuwa na namba yangu ya simu, kamwe hutakaa  uwasiliane na mimi.. Haijalishi utakuwa na simu nzuri, au salio la kutosha au namba za watu wengine elfu kwenye kitabu chako cha kumbukumbu, kama huna namba yangu mimi binafsi, kamwe huwezi kuwasiliana na mimi.

Leo hii watu wanataka kuwasiliana na Mungu, kwa njia zao wenyewe walizojitungia, wanajaribu kupiga kila namba wanayoibuni tu vichwani mwao, wengine wanamtafuta Mungu kupitia dini zao, wengine wadhehebu yao, wengine wanyama, wengine miti,sanamu, jua, mwezi, n.k. wakidai kuwa wanamtafuta Mungu Yule Yule mmoja, ukiwaeleza dini au dhehebu halikufikishi popote, watakuambia usitupotoshe, imani yako ndio itakayokuokoa..

Ndugu, usipomuamini Yesu, hutafika popote. Na kumwamini Yesu sio kusema mimi ni mkristo, au mimi namwamini Yesu, hapana, bali kunakuja kwa kutubu kwanza dhambi zako kwa kumaanisha kuziacha, pili kwa kubatizwa katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji tele katika jina lake sawasawa na Matendo 2:38, Kisha kupokea Roho Mtakatifu. Na kuanzia hapo kuishi maisha matakatifu yanayoendana na Neno lake,(yaani BIBLIA). Sasa Kwa kufanya hivyo imani yako itakuwa imekamilishwa mahali sahihi. Hapo ndipo utakuwa na uhakika unamwabudu Mungu kweli, kupitia mwana wake Yesu Kristo.

Lakini kwa kusema tu mimi namwamini Mungu, imani yangu itaniokoa na huku hujui Mungu kakuagiza nini katika Neno lake, au anakutaka ufanye nini..Ujue kuwa umepotea, na ukifa leo utakwenda kuzimu. Vilevile ukijivunua dhehebu lako, na hutaki kumtafuta Kristo Yesu aliye njia, ujue kuwa kuzimu itakuwa pia ni sehemu yako. Hakuna njia za kubuni buni katika kumfikia Mungu.. Ni sharti umwamini Yesu, na kuoshwa dhambi zako na yeye.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

CHANGIA SASA.

KITABU CHA YUDA: SEHEMU YA 1

NITAUPATAJE UPENDO WA KI-MUNGU NDANI YANGU?

Nini maana ya “kila tendo lisilotoka katika imani ni dhambi?”

CHUKIZO LA UHARIBIFU

Rudi nyumbani

Print this post

Nini maana ya “wanawake saba watamshika mtu mume mmoja”

SWALI: Isaya 4:1 na siku hiyo wanawake saba watamshika mtu mume mmoja wakisema, tutakula chakula chetu na kuvaa nguo zetu wenyewe lakini tuitwe  tu kwa jina lako; utuondolee aibu yetun. Je; andiko hili linamaanisha nini?


Kwanini wanawake? Kwanini wawe saba? Kwanini chakula chao na nguo zao na sio za mume wao? maanake mume akioa moja ya majukumu ya kwake kufanya kwa mkewe ni kumlisha na kumvika sasa hawa wanakula na kuvaa vya kwao ni kitu gani hawa wanawake?

JIBU: ufunuo wa mstari huo ni huu..wanawake saba ni makanisa saba (katika vipindi saba vya kanisa kama inavyooneka katika ufunuo 2 & 3)..

Mtu mume mmoja ni Yesu Kristo,.Lakini hao wanawake wote 7 wanasema watakula chakula chao wenyewe na kuvaa nguo zao wenyewe bali waitwe tu kwa jina la yule mtu mume mmoja ambaye ni Yesu Kristo.Jambo hili la kusema tutakula chakula chetu na kuvaa nguo zetu wenyewe ni tabia za hayo makanisa yote 7 yalivyokuwa, kila kanisa lilikuwa na tabia yake pekee, na yote yanatafuta kumpendeza Yesu Kristo lakini kwa njia zao wenyewe,

kwahiyo hicho “chakula” kinachozungumziwa hapo ni mapenzi yao wenyewe, na mienendo yao wenyewe hawataki chakula cha Bwana wao,(ambalo ni neno la Kristo lisiloghoshiwa), wala hawataki “mavazi” ya Bwana wao (Ambao ni utakatifu na matendo mema soma ufunuo 19:8,) bali waitwe tu kwa Jina la Bwana Yesu aibu yao iwaondoke hii aibu ina maana waiepuke hukumu itakayokuja na ndio maana yale makanisa yote hayakuweza kuoana na Kristo kikamilifu yalikuwa na mapungufu yake, na sisi pia tupo katika kanisa la mwisho la saba la LAODIKIA ni kanisa vuguvugu,na ndilo lililomkinai Bwana wake kuliko mengine yote yaliyotangulia soma..

ufunuo 3:14-22,”14 Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu.

15 Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.

16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.

17 Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.

18 Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.

19 Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.

20 Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.

21 Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi.

22 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa.”

Lakini tunapaswa wote tushinde ili tuvuke kutoka kuwa masuria na kuwa bibi-arusi safi wa Yesu Kristo waliokubaliwa tayari kwenda kwenye arusi ya mwanakondoo itakayofanyika mbinguni kwa Baba.Kumbuka bibi-arusi sio sawa na suria.Kwahiyo ndugu watakaoshiri karamu ya mwanakondoo ni bibi-arusi tu, je! wewe ni bibiarusi? umepokea Roho Mtakatifu? umejiweka tayari kumpokea Bwana wako atakaporudi? matendo yako yanastahili wokovu? jibu lipo moyoni mwako. Tubu sasa umgeukie Bwana kumbuka tunaishi kizazi ambacho kitashuhudia kuja kwa pili kwa Kristo.

ufunuo 19: Na tufurahi, tukashangilie, tukampe utukufu wake; kwa kuwa arusi ya Mwana-Kondoo imekuja, na mkewe amejiweka tayari.

Naye amepewa kuvikwa kitani nzuri, ing’arayo, safi; kwa maana kitani nzuri hiyo ni matendo ya haki ya watakatifu.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

KWANINI UNAPASWA UWE BIBI ARUSI NYAKATI HIZI ZA MAJERUHI?

NAMNA YA KUMTAMBUA BIBI ARUSI WA KWELI WA KRISTO.

Rudi Nyumbani:

Print this post

Je Musa kumwoa Sipora, Mkushi alifanya dhambi?

SWALI: Katika Ezra 9:12 na Kumbukumbu 7:3, Tunaona Bwana Mungu aliwakataza waisraeli kuoana na watu wa mataifa. Je watumishi hawa walioolewa au kuoa mataifa walifanya dhambi?.

  1. Esta kuolewa na mfalme Ahasuero

      2. Boazi kumwoa Ruthu

  1. Musa kumwoa Sipora, Mkushi,

Na kama ni dhambi mbona Miriamu Mungu alimpiga kwa ukoma baada ya kuhoji kwanini kaka yake, Musa alioa mwanamke wa kimataifa?


Jibu: Esta hakufanya jambo lililo sahihi kuolewa na mfalme wa kimataifa asiyemjua Mungu wa Israeli, kulingana na sheria za Mungu, lakini Mungu aliruhusu jambo hilo litokee,  kwa makusudi maalumu, kwamba Esta aolewe na Mfalme Ahasuero (ambaye ni mtu wa kimataifa) ili Mungu awaokoe watu wake dhidi ya maadui zao.

Utaona jambo kama hilo hilo lilitokea wakati wa Samsoni, pale ambapo Samsoni alikuwa ni Mwisraeli lakini akaenda kutafuta kuoa wanawake wa kimataifa (wakina Delila). Utaona walikuwepo wanawake wengi wa kiisraeli wenye sifa zote, lakini Samsoni hakwenda kwa hao bali kwa Delila aliyekuwa mfilisti, na biblia inasema jambo lile lilitoka kwa Bwana. (Yaani Mungu aliruhusu liwe hivyo)

Waamuzi 14:3 “Ndipo baba yake na mama yake wakamwambia, Je! Hapana mwanamke hata mmoja katika ndugu zako, au katika jamaa zangu zote, hata uende kumwoa mwanamke kwa hawa Wafilisti wasiotahiriwa? Samsoni akamwambia baba yake; Mnipatie huyo, kwa maana ananipendeza sana.

4 Lakini baba yake na mama yake HAWAKUJUA YA KUWA JAMBO HILI NI LA BWANA; MAANA ALITAKA KISA JUU YA WAFILISTI. Basi wakati ule Wafilisti walikuwa wakiwatawala Israeli”.

Unaona?..Mungu aliruhusu Samsoni atafute mke wa kimataifa, ili tu kutafuta kisa cha kuwaokoa waisraeli watu wake, chini ya utawala wa wafilisti.

Na ndio hivyo hivyo kwa Esta, Mungu aliruhusu Esta aolewe na mwanaume wa kimataifa (Mfalme Ahasuero), lengo na madhumuni ni kutafuta tu kisa cha kuwaokoa Israeli dhidi ya maadui zao ambao walikuwa wanawanyanyasa chini ya utawala huo. Na kilipopatikana kisa, Maadui za Israeli wote walikufa na Israeli wakapata raha. Lakini hayakuwa mapenzi kamili ya Mungu, Esta aolewe na mwanaume wa kimataifa, wala Samsoni aoe mwanamke wa kimataifa, ilikuwa ni kinyume cha sheria za Mungu.

Lakini pamoja na hayo tunaona pia mtu mwingine akioa mke wa kimataifa, na huyo si mwingine zaidi ya Boazi, aliyemwoa Ruthu, aliyekuwa mwanamke wa kimataifa.

Sasa ni kwanini iwe hivyo?

Ni kwasababu Ruthu tayari alikuwa ameshaacha miungu ya kwao, na kumgeukia Mungu wa kweli wa Israeli, kwasababu lengo kuu la Mungu kuwaambia wana wa Israeli wasioe wanawake wa mataifa ni kuepuka kugeuzwa mioyo. (1Wafalme 11:2). Na si lengo lingine.

Hivyo  Ruthu tayari alikuwa ameshaiacha miungu ya kwao, na amemgeukia Mungu wa kweli wa Israeli kwa moyo wake wote, tofauti na Delila au Mfalme Ahasuero aliyemwoa Esta, hao walikuwa bado hawajaiacha miungu yao.

Ruthu 1:16  “Naye Ruthu akasema, Usinisihi nikuache, Nirejee nisifuatane nawe; Maana wewe uendako nitakwenda, Na wewe ukaapo nitakaa. Watu wako watakuwa watu wangu, Na Mungu wako atakuwa Mungu wangu;

17 Pale utakapokufa nitakufa nami, Na papo hapo nitazikwa; Bwana anitende vivyo na kuzidi, Ila kufa tu kutatutenga wewe nami”.

Kwahiyo unaweza kuona, Ruthu tayari moyo wake ulikuwa umeshahamia kwa Mungu wa Israeli, akili yake yote ilikuwa inamwaza Mungu wa Israeli, na watu wa Israeli, na kwa Imani hiyo akahesabika kuwa kama mmojawapo wa mwanamke wa kiisraeli, japokuwa ni mwanamke wa kimataifa.

Sawa  tu na yule Rahabu kahaba, ambaye naye pia kwa Imani, alihesabiwa kuwa mwanamke wa kiisraeli, ingawa alikuwa ni Myeriko, kwasababu aliiacha miungu ya kwao na kumwamini Mungu wa Israeli na kumkiri.

Yoshua 2: 11 “Na mara tuliposikia hayo mioyo yetu iliyeyuka, wala haukusalia ujasiri wo wote katika mtu awaye yote, kwa sababu yenu; kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, yeye ndiye Mungu, katika mbingu juu na katika nchi chini”

Waebrania 11: 30  “Kwa imani kuta za Yeriko zikaanguka, zilipokwisha kuzungukwa siku saba

31  Kwa imani Rahabu, yule kahaba, hakuangamia pamoja na hao walioasi; kwa kuwa aliwakaribisha wale wapelelezi kwa amani”..

Na swali la mwisho ni kwanini Musa alimwoa Siphora, mkushi? Na ilihali yeye ni myahudi?

Kumbuka sheria ililetwa na Mungu kwa mkono wa Musa, hivyo Musa tayari alikuwa ameshaoa kabla ya hiyo sheria kuja. Kwahiyo haikuwa sahihi kumwacha mke wake huyo wa kimataifa na kuoa mwingine ilihali ameshapata naye watoto. Hivyo Mungu alimbariki na huyo huyo mkewe, maadamu alikuwa naye pia anamcha Mungu wa Israeli. Na sio tu Musa peke yake aliyekuwa na mke wa kimataifa, bali hata Yusufu, biblia inasema mke wake alikuwa ni binti wa kuhani  wa Oni (Mwanzo 41:45), ambaye hakuwa myahudi. Lakini Mungu hakumpa maagizo amwache, kwasababu sheria hiyo bado ilikuwa haijaja.

Na sisi wakristo wa agano jipya, hatupaswi kuoa, wala kuoelewa na mtu ambaye hajamkabidhi Yesu maisha yake (Mpagani), hiyo ni kulingana na maandiko. Ni sharti kwanza awe amemwamini Yesu na kusimama katika imani ndipo ndoa ifuate. (kwa urefu juu ya somo hili unaweza kufungua hapa >>  Je Ni sahihi kuolewa/kuoa mtu wa imani nyingine?)

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Je! Ni halali kuoa/kuolewa na mtu ambaye tayari anao watoto?

Je! Ni sahihi kuoa/kuolewa na mtu uliyemzidi umri?

JIFUNZE KUELEWA MAANA YA KUOA/KUOLEWA KABLA YA KUINGIA HUKO.

Je! Ni sahihi kwa mkristo kuoa/kuolewa na mtu wa imani nyingine?

JE NI HALALI KUOA WAKE WENGI, AU KUTOA TALAKA?

Rudi nyumbani

Print this post

TENDA AGIZO LA YESU, HILO NDIO LITAKALOKULINDA.

Shalom, nakusalimu katika jina kuu la Bwana wetu Yesu Kristo, karibu tuyatafakari maneno ya uzima pamoja.

Muda mfupi kabla ya Bwana Yesu kwenda kutukuzwa na maelfu ya watu kule Yerusalemu lipo agizo ambalo aliwapa wanafunzi wake wawili, na agizo lenyewe lilikuwa ni kwenda kumletea mwana punda aliyekuwa amefungwa mahali Fulani. Wengi wetu tunaweza kuona lile lilikuwa ni agizo jepesi, lakini kiuhalisia halikuwa jepesi kama tunavyodhani, kwani walipotumwa walioambiwa sio wakaombe wapewe, hapana bali wakachukue, kana kwamba  hao punda walikuwa ni wa kwao.

Embu tusome kidogo;

Luka 19:29 “Ikawa alipokaribia Bethfage na Bethania, kwenye mlima uitwao wa Mizeituni, alituma wawili katika wale wanafunzi,

30 akisema, Nendeni mpaka kijiji kile kinachowakabili, na mtakapoingia ndani mtaona mwana-punda, amefungwa, ambaye hajapandwa na mtu ye yote bado, mfungueni mkamlete hapa.

31 Na kama mtu akiwauliza, Mbona mnamfungua? Semeni hivi, Bwana anamhitaji.

32 Na wale waliotumwa wakaenda wakaona kama alivyowaambia.

33 Na walipokuwa wakimfungua mwana-punda, wenyewe waliwaambia, Mbona mnamfungua mwana-punda?

34 Wakasema, Bwana ana haja naye”.

Utajiuliza ni kwanini, Bwana atumie kauli hiyo, mfungue na sio waombeni mniletee? Unadhani hakujua kanuni za kuchukua mali za watu wengine? Alijua sana, lakini si kila wakati aliruhusu hilo, pengine wale wanafunzi walisema kwanini Bwana asituambie tukaanze na kuomba kwanza, si tutapewa tu, kuliko kwenda na kufungua wanyama ambao si wetu, si tutaitwa wezi?

Ni sawa na leo hii mtu akuambie, nenda pale mlimani city, utakuta gari limepakiwa, ingia kisha piga ufunguo, endesha uniletee, bila shaka utasema huyu mtu hanitakii mema bali mabaya.. anataka nikachomwe moto kama mwizi.

Lakini Kristo alikuwa na sababu kufanya vile, alijua mwisho wake utakuwaje..Vilevile alijua madhara ya kutanguliza kuomba omba vibali kwenye kazi yake, alijua milolongo ambayo wangekutana nayo, alijua vikwazo ambavyo shetani angevizusha mahali pale..pengine nyie ni wakina nani, mmesajiliwa wapi, shughuli yenu ni nini, hatuwatambui hapa mtaani, msimgolee yule punda, elimu yenu ni ipi, leta uthibitisho kwanza wa barua kutoka kwa huyo Bwana wenu, n.k. vinginevyo tutawashitaki..

Lakini wao hawakuongea chochote walipofika, badala yake walianza kufanya kama Yesu alivyowaagiza, kufungua punda na pengine katika hatua ya mwisho kabisa pale walipoanza kuondoka, ndipo wahusika walipowaona, na kuwauliza nyie mnafanya nini hapo? Mnawapeleka wapi hao punda?..Wakasema Bwana anawahitaji..

Sasa wale kuona tayari punda wao wameshafunguliwa na gharama imeshaingiwa, kuwarudisha itakuwa ni hatua ndefu sana wakaona ni bora wawache tu, pengine wawape masharti Fulani madogo ya kuwatumia, au walipie gharama Fulani kidogo tu. Hilo halijalishi maadamu punda wameshapatikana.

Vivyo hivyo na hata sasa, usitegemee kwanza ruhusu za watu kufanya jambo lolote la ki-Mungu, ni ngumu sana kusikilizwa au kusapotiwa, fanya kwanza kisha baadaye wakikuuliza kwanini ulifanya waambie ni kwababu Yesu aliniagiza..hata wakikasirika lakini tayari ulishafanya, lile agizo la Yesu litakulinda.

Vikwazo vya shetani ni vingi sana, unaweza ukajikuta haumfanyii Mungu lolote kisa, visheria Fulani vidogo vidogo, au viutaratibu Fulani vinakubana. Wewe fanya tu agizo lake litakulinda mbele ya safari. Unaweza hata usifanya huduma kisa hujakamilisha taratibu hii au ile, hayo tumeyaona sana sehemu nyingi, usingojee kukamilisha taratibu za wanadamu kwanza, endelea na taratibu za Mungu, kisha hizo za wanadamu zitafuata baadaye watakapokuuliza..kwasababu ukisema uanzie kwao, utavunjika moyo mapema mpendwa. Vikwanzo ni vingi kila kukicha.

Bwana Yesu alishatoa agizo, enendeni ulimwenguni kote, mkuhubiri injili kwa kila kiumbe. Hilo agizo halisemi, mkaombe kwanza kuhubiri, hapana, wewe kahubiri kwa jinsi Mungu alivyokujalia kisha wakikufuata, waeleze hilo ni agizo la Yesu. Kwa kufanya hivyo Yesu mwenyewe atafungua njia ya kukusaidia, atakuwekea wepesi, au kupewa kibali cha kuendelea na kazi ya Bwana.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

EPUKA KUUNDA MATARAJIO YAKO, KWENYE AHADI ZA MUNGU.

LISHIKILIE SANA LILE AGIZO LA KWANZA.

Baghala ni nini katika maandiko?(2Wafalme 5:16).

Mafundisho

Fitina maana yake nini kwenye biblia?

WAOMBEENI WANAOWAUDHI.

Rudi nyumbani

Print this post

EPUKA KUUNDA MATARAJIO YAKO, KWENYE AHADI ZA MUNGU.

Kuna swali limeulizwa na wasomaji wetu hapa..

“Bwana Yesu asifiwe mtumishi, pole na hongera na majukumu, mtumishi Mimi nilitaka kufahamu kuhusu Yohana mbatizaji, yeye ndiye aliyembatiza Yesu mwana wangu tena akasema nalishuhudia Roho wa Mungu akishuka kama hua toka mbinguni akatua juu yake tena yeye aliyempeleka yaani Mungu akamwambia yule utakayeona Roho akishuka juu yake huyo ndiye atakayebatiza kwa Roho mtakatifu na kwa Moto, tena Yohana anawahakikishia kwamba ajaye nyuma yake huyo ni mkubwa kuliko yeye na ya kwamba alikuwako kabla yake…..Sasa swali kwanini alipokuwa gerezani anatuma wanafunzi wake wakamuulize kuwa yeye ndiye Yesu au tumtazamie mwingine? Ina maana alichotushuhudia mwanzo kuwa ajaye ni mkuu na alimuona Roho akishuka juu yake bado hakuamini kuwa ni yeye? Asante, Mungu akusaidie katika kujibu”.


Jibu:

Ni kawaida ya mwanadamu pale anapoahidiwa kitu au anapoonyeshwa jambo fulani na Mungu, wakati huo huo kuanza kuundia matarajio yake mwenyewe juu yake jinsi ahadi hiyo  itakavyotimia.. Sasa pale maono hayo yanapotimia nje ya hayo matarajio yake mwenyewe, inakuwa ni rahisi sana kutetereka kama sio kuiacha Imani kabisa.

Katika mazingira ya Yohana mbatizaji, Sio kwamba hakuamini alichoonyeshwa, aliamini na kujua kabisa Yesu Kristo ndio yule aliyekuwa anatarajiwa kwa muda mrefu,. Lakini shida ilianza kutokea pale alipoanza kubuni matarajio yake  mwenyewe, ambayo wakati mwingine sio kwamba yalikuwa sio sahihi, hapana pengine yalikuwa ni ya kutimia baadaye kabisa, sio kwa wakati ule.

Sasa alipoona Yesu hajaja kama mfalme, akiwa na pepeto mikononi mwake kukusanya ngano ghalani na makapi kuyachoma motoni, kama alivyoonyeshwa (Mathayo 3:12) kinyume chake amekuja katika upole na unyonge, anakataliwa na watu hiyo ikampelekea baadaye aanze kutilia shaka.. Labda pengine atakuwa sio huyu..

Umeona, hata leo hii, Mungu anawapa watu wengi ahadi ya mambo fulani, na wanajua kabisa ni Mungu amewajibu pengine walijibiwa kwa ndoto, au maono, au sauti, au ishara n.k. lakini kwa bahati mbaya, wameyatilia shaka, kama sio kuyaacha kabisa maono hayo kutokana na kuwa waliyaruhusu matarajio yao yatawale maono hayo Mungu aliyowapa.

Kwa mfano utakuta mwanamke Fulani, ameahidiwa na Mungu kwamba kabla ya miaka mitano atakuwa na watoto watatu. Sasa badala asubiri maajabu ya Mungu , yeye muda huo huo anaanza kujiundia matarajio yake, kwamba  mwaka wa kwanza atapata mmoja, kisha baada ya miaka miwili atapata mwingine , na mingine atakuja baada ya miaka mingine miwili ya mwisho kupita ili kutimiza mitano.

Sasa matarajio hayo sio mabaya, lakini yana athari pale ambapo atakapoona wakati huo unapita bila ya yeye kuona chochote, mwaka wa kwanza unapita, wa pili nao hivyo hivyo haioni chochote, watatu, na wanne hivyo hivyo.. hapo ndipo mtu huyo anapoanza kutilia shaka kudhani pengine Mungu hakusema naye, pengine Mungu hakumjibu, pengine maono yale yalimaanisha kitu kingine, pengine hivi, pengine vile, pengine kuna mahali alimkosea Mungu..

Unaona? Mwisho wa siku anayaacha kabisa, na kuanza kuhangaika tena. Lakini kama angekuwa mtulivu na kuamini kuwa ni Mungu aliyemjibu, angesubiria matarajio ya Mungu yatende kazi,  pengine Mungu amempangia mwaka wa tano ule wa mwisho apate ujauzito wa watoto mapacha watatu.

Ndicho kilichotokea kwa Yohana mbatizaji, hiyo inatufundisha kuwa Pale Mungu anapotuahidi kitu, basi tumwamini vile vile alivyotuonyesha, bila kuongezea matarajio yetu juu yake, na hapo ndipo tutakapoweza kuishi maisha ya kutotilia shaka maneno yote ya Mungu.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

MATARAJIO YA KILA MWANADAMU DUNIANI NI YAPI?

NI NINI TUNAJIFUNZA KWA DEMA NA MARKO?

WAKATI AHADI INAPOKARIBIA, HUWA KUNA MAMBO YANATOKEA.

Ni vitu vipi hivyo viwili visivyoweza kubadilika? (Ebr 6:18)

Je watu ambao hawajasikia kabisa injili watahukumiwa?

Rudi nyumbani

Print this post

NI NINI TUNAJIFUNZA KWA DEMA NA MARKO?

Biblia inatuonyesha Dema na Marko walikuwa ni watenda kazi wazuri sana pamoja na Mtume Paulo, Tunayasoma hayo katika kitabu cha Filemoni 1:24

“na Marko, na Aristarko, na Dema, na Luka, watendao kazi pamoja nami”.

Lakini pamoja na kwamba walikuwa ni watenda kazi pamoja na Paulo, tunaona kila mmoja alikuwa na historia yake tofauti, ambayo leo hii tunaweza kuitazama na kupata funzo ndani yake.

MARKO

Tukianzana na huyu Marko, mwanzoni kabisa mwa huduma ya mtume Paulo, ya kuipeleka injili kwa watu wa mataifa, utaona akiwa na Barnaba, walimchukua pia huyu Marko kama msaidizi wao katika safari yao ya utume Mungu aliowapa. Lakini kama tunavyosoma katika maandiko, walipopita nchi kadhaa wa kadha, ghafla Marko alibadilika tabia, hatujui sababu ni nini iliyomfanya awe vile pengine, aliona kazi ile ni ngumu, au aliona haina faida yoyote.. Na hatimaye akawaacha Paulo na Barnaba solemba katika kilele cha utumishi, akarudi zake alipotokea, (Soma Matendo 13:13)

Jambo hilo liliwaumiza kama sio kuwafadhaisha sana mitume hususani Paulo, kuona kwamba mtu ambaye angepaswa kuwafariji na kuwatia moyo ndio anakuwa wa kwanza kuwakimbia. Na ndio maana wakati wa ziara ya pili, Paulo alipotaka tena kusafiri kwenda kuyathibitisha makanisa, aligoma kwenda na huyo Marko shambani mwa Bwana, Kwasababu alijua kigeugeu chake.

Matendo 15:37 “Barnaba akaazimu kumchukua Yohana aliyeitwa Marko pamoja nao.

38 Bali Paulo hakuona vema kumchukua huyo aliyewaacha huko Pamfilia, asiende nao kazini.

39 Basi palitokea mashindano baina yao hata wakatengana. Barnaba akamchukua Marko akatweka kwenda Kipro”.

Lakini pamoja na hayo biblia inatuonyesha huyu Marko alikuja kugeuka baadaye , pengine alitubu na kutambua makosa yake, akaona hapa naelekea kulipoteza taji langu, hivyo akaendelea kufanya utumishi wa Mungu, na baadaye kabisa utaona mtume Paulo akimpokea tena, akisema ni mtenda kazi pamoja naye. Na huyu Marko ndiye aliyekiandika hicho kitabu cha Marko ambacho mpaka leo hii tunakisoma.

DEMA

Sasa tukimtazama na mtendakazi wake mwingine aliyejulikana kama Dema, yeye alikuwa katika utumishi mzuri sana na Paulo, pengine tangu mwanzoni kabisa mwa huduma alikuwa naye, lakini ilifika wakati pengine kwa kuona kuna ugumu fulani, akaamua kabisa kuachana na utume, hivyo akamwacha mtume Paulo peke yake vifungoni, ni heri angemwacha tu, kisha aende kuifanya kazi ya Mungu sehemu nyingine.. Lakini mtume Paulo anasema, aliupenda ulimwengu huu.

Yaani aliacha kabisa utumishi wa Mungu akayarudia mambo ya kale ya ulimwenguni, na wala hakurudi tena shambani mwa Bwana. Embu fikiria mtu huyu jinsi alivyouvunja moyo wa Mungu na Paulo. Pengine mwenzake Marko alikuwa anamwangalia, na kumwonya asifanye hivyo, kwasababu mwisho wake utakuwa ni mbaya, kwasababu yeye naye alijaribu kufanya hivyo lakini hakuona faida yoyote, lakini Dema hakusikia akaona ni heri arudie anasa zake, zile ziara zote za kuzunguka kuhubiri injili ndio mwisho, hakuna faida yoyote. Nitarudia miradi yangu mikubwa n.k.

2Timotheo 4:10 “MAANA DEMA ALINIACHA, AKIUPENDA ULIMWENGU HUU WA SASA, akasafiri kwenda Thesalonike; Kreske amekwenda Galatia; Tito amekwenda Dalmatia”.

Sasa mambo haya tunaweza kudhani hayatokei hata sasa.

Biblia inasema, TUISHINDANIE IMANI, ambayo tumekabidhiwa sisi watakatifu mara moja tu.

Yuda 1:3 “Wapenzi, nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia, ili niwaonye kwamba mwishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu.”

Unaona Mungu hategemei sana mwanzo wetu, anautazama na mwisho wetu utakuwaje. Kama Dema alikuwa ni mtendakazi mzuri sana, mpaka Mtume Paulo anajivunia kwa kumtaja katika nyaraka zake nyingi, usidhani hakukuwa na watendakazi wengine wakati ule, walikuwepo,  lakini alijivunia Zaidi  Dema pengine kwa bidii yake..

Wakolosai 4:14 “Luka, yule tabibu mpendwa, na Dema, wanawasalimu”.

Lakini mwisho wa siku anageuka na kuisaliti Imani, unadhani na sisi tusipoishindania Imani hatutaisaliti vivyo hivyo pale tunapoona mambo hayajaenda kama tunavyotaka?. Imani ya wokovu ni ya kuishindania kweli kweli haijalishi ni mazingira gani utapitia, kwasababu Bwana Yesu  alisema tangu kipindi cha Yohana mbatizaji hadi sasa ufalme wa mbinguni unapatikana kwa nguvu, na wenye nguvu ndio wanaouteka (Mathayo 11:12).

Utajiuliza ni kwanini Bwana Yesu alisema tangu kipindi cha Yohana mbatizaji na sio tangu kipindi cha akina Musa au Eliya, au Daudi?..Alisema vile kufuatana na maisha ya Yohana mbatizaji, jinsi alivyojikana nafsi kumtafuta Mungu, mtu ambaye hakujali mazingira aliyopo, hakujali nguo alizovaa, hakujali chakula alichokula, kule jangwani maadamu yupo sawa na Mungu wake, hiyo ilitosha.. Sasa kama yeye aliushindania hivyo, hata sisi hatuna budi kuishindania vivyo hivyo kama yeye, kulingana na maneno ya Yesu.

Mpaka mtume Paulo anakaribia kwenda kufa, na kusema IMANI NIMEILINDA, usidhani ilikuwa ni jambo jepesi jepesi, alipitia tabu zote lakini hakuukana au kuusaliti wokovu wake.

Itakuwa ni ajabu sana kama utataka kwanza uoelewe au upate kazi nzuri, au upate pesa ndio usimame katika wokovu, kwa namna hiyo kamwe hutakaa uustahimili wokovu, kwasababu hata kama Mungu akikupa hayo yote, kukitokea mtikisiko kidogo tu, utarudi nyuma kuuacha wokovu kama Dema.

Hivyo mapambano ya Imani yapo. Shikilia sana wokovu wako bila kuangalia au kujali mazingira, maana hiyo ndio tiketi yako ya kwenda mbinguni. siku hizi ni za mwisho. Maisha ni mafupi sana.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

TUMEKUWA TAMASHA KWA DUNIA; KWA MALAIKA NA WANADAMU.

MWANZO WA INJILI YA YESU KRISTO.

KITABU CHA YUDA: SEHEMU YA 1

Nini maana ya “kila tendo lisilotoka katika imani ni dhambi?”

NJIA YA KUPATA WOKOVU.

PINDO LA VAZI LAKE SASA LIMEREFUSHWA.

Rudi nyumbani

Print this post

TUMEKUWA TAMASHA KWA DUNIA; KWA MALAIKA NA WANADAMU.

Paulo alipouna utumishi wake, na wenzake jinsi ulivyo, na kuona magumu anayoyapitia katika huduma yake, mwisho wa siku alisema maneno haya..

1Wakorintho 4:9 “Maana nadhani ya kuwa Mungu ametutoa sisi mitume mwisho, kama watu waliohukumiwa wauawe; kwa sababu TUMEKUWA TAMASHA kwa dunia; kwa malaika na wanadamu.

10 Sisi tu wapumbavu kwa ajili ya Kristo, lakini ninyi ni wenye akili katika Kristo; sisi tu dhaifu, lakini ninyi mna nguvu; ninyi mna utukufu, lakini sisi hatupati heshima.

11 Hata saa hii ya sasa, tuna njaa na kiu, tu uchi, twapigwa ngumi, tena hatuna makao;

12 kisha twataabika tukifanya kazi kwa mikono yetu wenyewe. Tukitukanwa twabariki, tukiudhiwa twastahimili;

13 tukisingiziwa twasihi; tumefanywa kama takataka za dunia, na tama ya vitu vyote hata sasa:.

Kumbuka Matamasha ya zamani sio kama haya tuliyo nayo sasa.

Matamasha ya zamani yalikuwa yanafanyika katika viwanja vikubwa sana vya michezo, na michezo yenyewe vilevile  haikuwa  kama hii tuliyonayo sasa hivi, mfano mpira, au riadha, hapana, bali ni michezo ya kupigana miereka ya kufa na kupona, , ambayo ilikuwa inapiganwa na watu waliobebea sana katika vita, watu hawa walikuwa aidha ni wafungwa walioshindikana, kwa kesi za mauaji au watumwa, walionunuliwa kutoka mbali, hivyo walichokuwa wanafanya ni kuwachukua na kuwapeleka katika mafunzo haya ya muda mrefu kujifunza kupigana

Hivyo wakati Fulani unafika, ndio wanawaleta sasa kwenye viwanja hivyo vikubwa ili wapambane, ambapo maelfu ya watu walikuwa wanakusanyika kutazama mapigano hayo. Hayakuwa mapigano ya  miereka kama tunayoyaona sasa hivi kwenye Tv, watu wanaumizana tu kidogo halafu baadaye wanaachana hapana, bali mapigano kweli kweli ya kushika mapanga na ngao.

Kule juu kila mtu akikaa akimshangilia mchezaji wake., Na mwishoni ni lazima mmojawapo auawe. Na wakati mwingine ilikuwa ni kupigana na wanyama wakali kama vile, simba, chuo au vifaru.

Sasa wakristo wa kwanza waliokuwa wanauawa, waliingizwa kwenye viwanja hivi, vya mapambano, vilivyojulikana kama Arena. na huko ndani wanakutana na hawa wapiganaji waliobebea na kama sio hao basi waliachiliwa wanyama wakali kama Simba au chui, wapambane nao. Kwa namna ya kawaida unaelewa ni nani atashinda hapo. Kwasababu sikuzote wakristo sio wapiganaji, pengine watakachofanya tu ni kutafuta njia ya kunusuru maisha yao, lakini mwisho wa siku watauliwa tu, . Kumbuka wakati huo waelfu wa watu wapo majukwaani wanawatazama kama vile tamasha, wakishabikia, na kufurahia, kama vile timu Fulani ya simba na Yanga inacheza.

Sasa Mtume Paulo aliutolea mfano huo kuonyesha ni jinsi gani watumishi wa Mungu, wanavyoonekana duniani leo hii. Wanatolewa ili watazamwe jinsi wanavyouawa, Paulo alisema tunakufa kila siku, 1Wakorintho 15:31,

Na kama vile teknolojia ilivyokuja juu sana, watamazaji wa matamasha wameongeza, kiasi kwamba sio tu wale walio kwenye viwanja wanaona mchezo wote, bali na wa mbali pia, vivyo hivyo, dhiki hizi wa watumishi wa Mungu zinaonekana mpaka kwa malaika wa Mungu mbinguni, wanatuona na kutuhurumia.

Lakini kwanini Mungu aruhusu iwe hivyo?

Hiyo inatupa chachu ya mambo mawili, la kwanza, ni kuwa wewe kama mtumishi wa Mungu, ufanyapo kazi ya Mungu, fahamu kuwa wewe ni kama tamasha la ulimwengu, matusi ni lazima yawe sehemu ya maisha yako, dhihaka zitakuwa zako, kupigwa na wakati mwingine kufukuzwa na kuuliwa vitakuwa vyako, hivyo kama vile Bwana Yesu alivyosema..

Luka 6:22 “Heri ninyi watu watakapowachukia, na kuwatenga, na kuwashutumu, na kulitupa nje jina lenu kama neno ovu, kwa ajili ya Mwana wa Adamu.

23 Furahiwani siku ile na kuruka-ruka, kwa kuwa, tazama, thawabu yenu ni kubwa mbinguni, maana, baba zao waliwatenda manabii vivyo hivyo”.

Vivyo hivyo na wewe furahi kwasababu ufalme wa mbinguni ni wako.

Lakini kwa wewe ambaye unahubiriwa injili na unaipuuzia, unatoa maneno ya dhihaka, unacheka, unatukana, unaleta fitina, ujue kuwa, Bwana Yesu alisema maneno haya vilevile..

Mathayo 10:14 “Na mtu asipowakaribisha wala kuyasikiliza maneno yenu, mtokapo katika nyumba ile, au mji ule, kung’uteni mavumbi ya miguuni mwenu.

15 Amin, nawaambia, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma na Gomora kustahimili adhabu ya siku ya hukumu, kuliko mji ule”.

Unaona, ikiwa unaigeuza kazi ya Mungu kama tamasha tu la kusikiliza, kuambiwa, kuona wengine wanamtafuta Mungu lakini wewe unakuwa kama mshabiki tu, na hutaki kukitendea kazi kile ulichoambiwa, ujue huko ng’ambo adhabu yako itakuwa ni  kubwa sana.. Zaidi hata ya wale watu wa Sodoma na Gomora, ambao kulingana na maneno ya Bwana Yesu tunaona hadi sasa adhabu yao haijaisha, sasa jiulize wewe utakuwa wapi?

Bwana alisema pia..

Luka 12:47 “Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana.

48 Na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na Zaidi”.

Jiulize wewe unaishi kwa ajili ya nini? Kama watumishi wa Mungu wanapitia adhabu ya Mungu wakiwa hapa duniani, jiulize wewe mwenye dhambi utaonekania wapi siku ile kama mtume Petro alivyosema katika 1Petro 4:15-17 Kumbuka mbinguni hakitaingia kinyonge..Unauchukulia wokovu wako juu juu tu, ufahamu kuwa unyakuo ukipita leo, huendi popote. Hata kama utasema wewe ulibatizwa, au ulimpa Yesu maisha yako, hutakwenda popote ndugu. Usipojikana nafsi na kumfata Yesu, utabakia hapa hapa duniani. Nivyo ilivyo hukumu ipo.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

MAUAJI YA HALAIKI NDANI YA KANISA.

MATARAJIO YA KILA MWANADAMU DUNIANI NI YAPI?

Hanithi ni nini katika biblia? (kumbukumbu 23:17)

CHUKIZO LA UHARIBIFU

MWANZO WA INJILI YA YESU KRISTO.

KITABU CHA YUDA: SEHEMU YA 1

Rudi nyumbani

Print this post

MAUAJI YA HALAIKI NDANI YA KANISA.

Mwaka 1994 kulizuka vita mbaya ya kikabila huko nchini Rwanda, Vita hivyo vilidumu kwa miezi mitatu tu, lakini maafa yaliyotokea, yalizidi hata vita zilizopiganwa kwa miaka mingi katika mataifa mengine. Ni heri vifo vingekuwa vya kupigwa bunduki tu basi, lakini watu walikuwa wakiuliwa kinyama wakichinjana na wengine kuchomwa moto makanisani, mpaka leo dunia haiwezi kusahau yaliyotokea Rwanda wakati ule.

Ilikuwa ni vita vya makabila mawili tu, lakini mapambano yake yalitisha sana, kwani ndani ya muda huo mfupi watu zaidi ya laki nane waliuliwa. Hiyo inatukumbusha mauaji mengine kama haya, katika biblia,. Na yenyewe yalikuwa ni kati ya pande mbili, watu wa taifa moja. Na hao si wengine zaidi ya Yuda na Israeli.

Ilifika wakati Hawakuwezi kukaa tena pamoja, na hiyo ni kwasababu  hawakujua chanzo cha tatizo lao ni nini, mpaka wakaanza kupigana, hatujui vita hiyo ilichukua siku ngapi, pengine moja, au mbili tu, lakini watu waliouawa siku hiyo walikuwa ni laki 5 (500,000). Jaribu kutengeneza picha taifa dogo kama mji wa Daresalaam, wanaanguka watu laki tano, si jambo la kawaida kabisa, hayo ni zaidi ya mauaji ya halaiki. Katika biblia nzima hakujawahi kutokea Israeli kuwaua hata maadui zao kwa idadi kubwa kama hiyo waliouana wao kwa wao. Walikuwa na maadui wakubwa kama vile wafilisti, lakini hawakuwahi kuwaua kwa idadi kubwa namna hiyo.

2Nyakati 13:15 “Ndipo wakapiga kelele watu wa Yuda; ikawa, watu na Yuda walipopiga kelele, Mungu akampiga Yeroboamu na Israeli wote mbele ya Abiya na Yuda.

16 Wana wa Israeli wakakimbia mbele ya Yuda; naye Mungu akawaua mikononi mwao.

17 Abiya na watu wake wakawapiga mapigo makuu; hata wakaanguka wameuawa wa Israeli mia tano elfu, watu wateule.

18 Ndivyo walivyotiishwa wana wa Israeli wakati ule, wakashinda wana wa Yuda, kwa kuwa walimtegemea Bwana, Mungu wa baba zao.

19 Abiya akamfuata Yeroboamu,”

Hiyo ni kuonyesha kuwa vita vya ndani huwa ni vibaya zaidi kuliko vita vingine vyote. Na haviwi rahisi kuvizima, vinapoa tu muda lakini baadaye tena vitanyanyuka, kama ilivyokuwa kwa Israeli huo ni mfano wa vita moja tu, vilipita vita nyingine nyingi na zote zilileta maafa mengi, utadhani lile sio taifa la Mungu.

Tunaweza kudhani vita hivi havipo sasa..

Kumbuka Israeli ni kivuli cha kanisa la rohoni linaloendelea sasa hivi. Leo hii duniani kuna madhehebu zaidi ya 30,000 na yote yanadai kuwa ni ya Ki-kristo.  Hivyo ni sawa na kusema wote ni Taifa la Israeli, isipokuwa makabila tofauti tofuati. Lakini hatujui kuwa hiyo ni dalili mbaya sana. Hadi sasa tulipofikia vita za kidhehebu zimerindima, mauaji ya kiroho yanayoendelea katikati ya watu wanaomwamini Kristo, siku baada ya siku tena yanaongeza kwa idadi kubwa sana. Huyu anapigana na huyu, na yule anapigana na huyu..Mwisho wake ni nini,?

Lazima tujue Israeli iligawanyika kwasababu gani..Iligawanyika kwa sababu moja tu ya Sulemani, kuacha kuenenda katika njia za Mungu na kuenda kuitolea miungu mingine sadaka, lakini wakati huo huo, ndani yake kulikuwa na ahadi za Mungu ambazo alimuahidi baba yake, hivyo ili Mungu kutimiza haki yote ya ahadi na adhabu, ndipo akaugawanya ufalme wake na kumpa mtu mwingine, na wakati huo huo akamwachia ufalme kidogo kwa ajili ya Daudi baba yake. (1Wafalme 11:9-14) Huo ndio ulikuwa mwanzo wa Israeli kugawanyika. Lakini kama waisraeli baada ya pale wangetaka kumrudia Mungu wao, ni wazi kuwa Mungu angeurejesha ufalme kwa uzao mmoja wa Daudi na Israeli yote ingekuwa kitu kimoja.

Vivyo hivyo leo hii ni kwanini Kanisa la Kristo limegawanyika? Ni kwasababu tunaye Kristo ndani yetu, na wakati huo huo tunaabudu mambo mengine, Mungu ametuadhibu kwa kutugawanya kama ilivyo leo hii. Na matokeo ya kugawanyika ni vita. Vita hizi zitaendelea kama hatutarudi kwenye misingi ya Neno, kama hatutajua kosa letu ni nini, tutauana sana,  biblia inasema hivyo..

Bwana alisema..

Yohana 16:2 “Watawatenga na masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada”.

Imefikia hatua badala mtu akuelekeze kwa Kristo anakuelekeza kwenye dini yake, ili ujenge chuki na wale wengine wasio wa dhehebu lao, ukristo umehama sasa kutoka katika kuelekeza mapambano dhidi ya adui wa nje (shetani) hadi kujikita katika mapambano ya sisi kwa sisi. Kilichojaa ndani yetu ni udhehebu na udini, tukidhani hivyo ndivyo vinavyompendeza Mungu.

Bwana anasema, tutokea huko, tumrudie yeye.

Ufunuo 18:4 “Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni, ikisema, Tokeni kwake, enyi watu wangu, msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake”.

Ondoka kwenye kamba hizi kamba za kidhehebu, ndugu yangu. Shikamana na Kristo kwa wakati huu uliobakiwa nao hapa duniani, hakikisha huyo ndiye anayekaa katika moyo wako kuliko jambo lingine lolote.

Bwana akabariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Chuo cha vita vya Bwana ni kipi?(Hesabu 21:14)

NAYE AKASIMAMA JUU YA MCHANGA WA BAHARI.

Nini maana ya Dirii, Chepeo na Utayari?

NAMNA YA KUITAMBUA SAUTI YA MUNGU INAPOZUNGUMZA NA WEWE

SI MAPEPO YOTE NI YA KULIPUKA.

THAWABU YA UAMINIFU.

Rudi nyumbani

Print this post