Title February 2021

PINDO LA VAZI LAKE SASA LIMEREFUSHWA.

Isaya, alionyeshwa maono mengine ya ajabu mbinguni, Pengine hakuelewa umuhimu na maana ya maono yale, lakini sisi wa leo ndio tunaweza kuelewa vizuri.. Alipochukuliwa katika maono mbinguni alimwona Mungu akiwa ameketi katika kiti chake cha enzi kilichonyanyuliwa juu sana, juu kweli kweli. Na moja ya vitu ambavyo vilishangaza macho yake, ni kuhusu lile vazi lake, kwani lilipofika chini, halikuishia palepale bali liliendelea kumwagika, mpaka kufunika hekalu zima juu mbinguni.

Maono hayo aliyoonyeshwa Isaya yalichukua picha ya ufalme wa kidunia, hususani kwenye zile ngome kubwa sana, kama vile Ashuru na Misri zilizokuwa zinaitikisa dunia wakati ule wa nabii Isaya. Wafalme wao walivaa mavazi ambayo yalimwagika kwa nyuma, kuashiria utukufu wa enzi zao, hivyo  yalikuwa yakisogea umbali kadhaa tu. tazama mfano wa picha juu.

Lakini vazi hili aliloonyeshwa Isaya lilikuwa ni la kipekee sana, lenyewe lililijaza Hekalu zima mbinguni, kuonyesha utukufu wake ni Zaidi sana ya ule utukufu wa mavazi  ya kidunia aliyoyazoea.

Isaya 6:1 “Katika mwaka ule aliokufa mfalme Uzia nalimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu sana na kuinuliwa sana, NA PINDO ZA VAZI LAKE ZIKALIJAZA HEKALU.

2 Juu yake walisimama maserafi; kila mmoja alikuwa na mabawa sita; kwa mawili alifunika uso wake, na kwa mawili alifunika miguu yake, na kwa mawili aliruka.

3 Wakaitana, kila mmoja na mwenzake, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ni Bwana wa majeshi; dunia yote imejaa utukufu wake”.

Sasa, Isaya alionyeshwa tu katika lugha ya picha, lakini sisi tunaoishi agano jipya tunajua maana halisi ya Pindo la vazi la Mungu ni nini, na lina umuhimu gani kwetu. Mtu wa kwanza aliyelitambua hilo ni yule mwanamke aliyetokwa na damu kwa muda wa miaka 12 bila kupata tiba yoyote. Lakini siku alipokwenda kuligusa pindo la vazi la Yesu, alijua lilibeba ufunuo gani, japo alilipata  kwa shida sana kwasababu halikuwa refu, na umati mkubwa wa watu ulikuwa unamsonga lakini alipobahatika kugusa tu, muda ule ule ugonjwa wake sugu, uliisha.

Mathayo 9:20 “Na tazama, mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, alikuja kwa nyuma, akaugusa upindo wa vazi lake.

21 Kwa maana alisema moyoni mwake, Nikigusa tu upindo wa vazi lake nitapona.

22 Yesu akageuka, akamwona, akamwambia, Jipe moyo mkuu, binti yangu; imani yako imekuponya. Yule mwanamke akapona tangu saa ile”.

Mpaka baadaye watu wengi, walipoligundua hilo, kumbe hata katika pindo tu la vazi lake kuna uponyaji, na sio lazima upate vazi lake zima..wakawakusanyana makutano mengi, wakawa wanaomba Bwana akipita angalau awaruhusu watu wale waliguse pindo la vazi lake, wapone.. Na wote waliogusa kweli waliponywa..

Marko 6:56 “Na kila alikokwenda, akiingia vijijini, au mijini, au mashambani, wakawaweka wagonjwa sokoni, wakamsihi waguse ngaa pindo la vazi lake; nao wote waliomgusa wakapona”.

Ni nini Bwana alikuwa anawaonyesha?

Sasa kwa kipindi Yesu alipokuwa duniani, vazi lake lilikuwa ni la kawaida tu, haliburuzi kwasababu alikuwa hajawa bado mfalme, lakini sasa anaketi kama MFALME MKUU huko mbinguni, na kama tunavyojua wafalme wenye nguvu sana ni lazima wavae mavazi ambayo pindo zake zinaburuza chini,walau kwa mita kadhaa.

Lakini Isaya anaonywesha maono, ya Kristo akiwa kwenye kiti chake cha Enzi, na vazi lake halipo pale tu alipo, bali limeburuza mpaka kufikia hatua ya kulijaza hekalu zima. Haleluya..

Na kama tunavyojua HEKALU la Kristo ni Kanisa lake, yaani mimi na wewe.

1Wakorintho 3:16 “Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu”?

Hiyo ni kuonyesha kuwa Kristo anaponya kweli kweli, na uponyaji wake sasa, si kama ule wa zamani,  ambapo alikuwa bado hajaketi kama Mfalme mwenye vazi refu,.. Lakini Kama tu alivyokuwa duniani aliponya kwa namna isiyokuwa ya kawaida vile, vipi wakati huu ambapo, uponyaji wake umesambaa katika kanisa lake lote, mahali popote, sehemu yoyote, wakati wowote..Mwite tu Kristo atakuponya. Kama unao ugonjwa unakusumbua, mwite Kristo atakuponya hapo ulipo. Kwasasa huhitaji nabii Fulani, au mtume Fulani, au mchungaji Fulani, au mwalimu Fulani akuombee, wewe mwenyewe ulipo vazi lake, linakufikia ukiwa hapo chumbani kwako unamwomba..Vazi hilo limefika kwako.

Vilevile, ataiponya na Roho yako, ikiwa tu utamwita kwa moyo wa kweli wa kumaanisha. Kristo amemwaga utukufu wake kweli kweli, usiruhusu neema ya wokovu ikupite hivi hivi, kwasababu upo wakati atasimama katika kiti chake che enzi, na neema itakuwa imekwisha kabisa.. bali atasimama kuhukumu.

Je!, unatambua hilo? Unatambua kuwa kanisa tunaloishi ndio kanisa la mwisho lijulikanalo kama Laodikia? Na kwamba hakutakuwa na kanisa lingine Zaidi ya hili kulingana na maandiko katika kitabu cha Ufunuo 1-3. Unasubiri nini mpaka neema ikupite, ukifa leo huko utakapokwenda utakuwa mgeni wa nani, mambo ya dunia ndio unayoyahangaikia lakini mambo ya ufalme wa mbinguni, umeyatupilia kando, hujui kuwa ndio shetani anavyotaka uendelee kuwa hivyo, ili siku ile ikujie ghafla uachwe. Yatafakari maisha yako, ufanye uamuzi sahihi, kwasababu hapa duniani hatuna muda mrefu rafiki yangu. Ulijue tu hilo. Unyakuo upo karibu sana.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Nini maana ya “mkilichukia hata vazi lililotiwa uchafu na mwili”?

kwanini yule kijana aliitupa ile nguo ya kitani chini na kukimbia uchi?

Ni nani aliyesema “Nitume mimi”? katika (Isaya 6:8)

UFUNUO: Mlango wa 11

JE! NI WAPI UTAPOKEA HISIA ZA KWELI ZA KI-MUNGU?

Rudi nyumbani

Print this post

JE! NI WAPI UTAPOKEA HISIA ZA KWELI ZA KI-MUNGU?

Yapo mambo mengi yasiyo ya kawaida aliyoyafanya Bwana Yesu..Lakini kuna mojawapo ningependa tujifunze leo.. Na jambo lenyewe linapatikana katika habari hii..

Marko 7:32 “Wakamletea kiziwi, naye ni mwenye utasi, wakamsihi amwekee mikono.

33 Akamtenga na mkutano faraghani, akatia vidole vyake masikioni mwake, akatema mate, akamgusa ulimi,

34 akatazama juu mbinguni, AKAUGUA, akamwambia, Efatha, maana yake, Funguka”.

Uponyaji wa mtu huyu, ulikuwa ni wa kitofauti sana na ponyaji nyingine zote Yesu alizozifanya.. Kwani nyingine zilihitaji Yesu kutamka tu, au kutoa maagizo Fulani machache n.k., lakini hili lilihitaji jambo lingine la kipekee sana.. Nalo ni hisia za ndani kabisa za rohoni.

Bwana alipomwita huyu mtu, na kujua tatizo lake, moja kwa moja akamwekea vidole vyake masikioni, kisha akatema mate akamgusa ulimu..Sasa hakuishia hapo tu kama alivyofanya kwa baadhi ya watu wengine aliowaponya, labda kuwapa maagizo Fulani, kama alivyofanya kwa huyu tunayemsoma katika Yohana 9:6 …

Yohana 9:6 “Alipokwisha kusema hayo, alitema mate chini, akafanya tope kwa yale mate. Akampaka kipofu tope za macho,

7 akamwambia, Nenda kanawe katika birika ya Siloamu, (maana yake, Aliyetumwa). Basi akaenda na kunawa; akarudi anaona”.

Hapana, lakini kwa huyu, ilihitaji Yesu achukue hatua nyingine Zaidi ya rohoni.. Ya kuugua, Ya kuona huruma ya kupitiliza juu ya mtu huyu ambaye alikaa katika hali hiyo ya utasi na uziwi kwa muda mrefu..Ilihitaji aihisi hali yake kwa undani Zaidi isivyokuwa kawaida.

Hivyo ili kupata hisia hizo ilimbidi sasa, ajue ni wapi atazitolea, kwasababu hivi hivi tu haziji vinginevyo atakuwa unafanya kinafki..Ndipo hapo akatazama juu mbinguni..

Alijua huruma ipo kwa Mungu tu mbinguni, alijua upendo upo juu, alijua uponyaji wa kweli unatoka kwa Baba yake juu na si kwa mwingine awaye yote..sasa kitendo cha yeye kuelekeza uso wake mbinguni, ilimsaidia kuvuta kwa haraka ile huruma ya ki-Mungu ndani yake, na hapo hapo akajikuta ANAUGUA sana moyoni..huruma ikamjaa isiyokuwa ya kawaida, na pindi aliporudisha macho yake tu chini, hakumwona yule mtu kama alivyomwona hapo mwanzo.. Bali alimwona kwa jicho la huruma nyingi sana, na ndipo saa hiyo hiyo aliposema EFATHA..yaani funguka..Na yule mtu akawa mzima kabisa.

Ni nini tunajifunza?

Hatuwezi kuwahurumia wengine, hatuwezi kuwaganga wengine mioyo, hatuwezi kuwasaidia wengine ikiwa tu hisia hizi hatuna ndani yetu, ikiwa macho yetu, wakati wote hatuyaelekezi mbinguni, tusitegemee tutaugua mioyoni mwetu kwa Kristo alivyokuwa anaugua kwa ajili yetu.

Mpaka kupelekea kuwa tayari kuuawa kwa ajili yetu sisi tulio dhambini..

Bwana Yesu alisema..

Luka 6:36 “Basi, iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma”.

Luka 7:12 “Na alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye.

13 Bwana alipomwona alimwonea huruma, akamwambia, Usilie”.

Huruma za Yesu utazisome sehemu nyingi sana kwenye maandiko kwa muda wako unaweza kuvipitia hivi vifungu Marko 6:34, Mathayo 9:36, 20:34,

Kumbuka Upendo wa kweli, huruma ya kweli inatoka kwa Mungu tu peke yake. Ndicho Yesu alichokifanya.. hakuwatazama wanadamu ndipo kuugua kuje ndani yake, hakuitazama milima, hakuwatazama wanyama bali alitazama juu mbinguni Baba yake mwenye rehema alipo, ndipo huruma ikamjaa moyoni.

Nasi pia tuyaelekeze macho yetu mbinguni, ili tupokee hisia hizi za kweli za Mungu, hisia ambazo zitavuta uponyaji wa ki-Mungu kwa haraka sana. Hisia ambazo zitajenga kuombeana na kusaidiana, Na kuhudumiana.

Na kuelekeza macho yetu mbinguni, maana yake si kuangalia angani, hapana, bali ni kumsoma Mungu wetu kwa bidii, na kujua anataka nini kwetu, na hiyo inakuja kwa kulitafakari Neno lake, pia kwa kusali, na kufunga na kumfanyia ibada..

Hayo yote tukiyafuata itatupelekea kuzipokea hisia hizi za Kristo kwa wingi wote, na matokeo yake tutafukuza roho zote za chuki, na vinyongo, na hasira, fitina, wivu na mashindano ndani yetu.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

BWANA AYAGANGE NA MACHO YETU PIA.

MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA WARAKA WA PILI WA YOHANA.

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

Je! Kuna malaika wangapi mbinguni?

JE! HAMPOTEI KWA SABABU HII?

Rudi nyumbani

Print this post

JE! HAMPOTEI KWA SABABU HII?

Jina la Bwana wetu Yesu libarikiwe daima. Karibu tuyatafakari maandiko pamoja ndugu yangu.

Wakati ule masadukayo walimfuata Bwana Yesu, na kumuuliza maswali ambayo, ndio yaliyowafanya waamue kuwa  masadukayo kama walivyo wasioamini  kuwa kuna kitu kinachoitwa ufufuo wa wafu. Na swali lenyewe lilikuwa ni kuhusu ndoa baada ya kifo..Walikuwa na sababu nzuri kabisa za kufikirika kwa akili za kibinadamu, kwamba kama kiyama ipo basi Musa asingeruhusu mtu kuoa mke wa mtu baada ya kufa, ili huko ng’ambo kusiwe na migongano ya kindoa,.Lakini kama aliruhusu kuoa mke wa marehemu, ni wazi kuwa mambo yote ni ya hapa hapa duniani, hakuna kufufuliwa wafu.

Embu Tusome kwa ufupi habari yenyewe na pale mwishoni lipo jambo ambalo Bwana atatufundisha siku ya leo..

Anasema..

Marko 12:18 “Kisha Masadukayo, watu wasemao ya kwamba hakuna kiyama, wakamwendea, wakamwuliza na kusema,

19 Mwalimu, Musa alituandikia ya kwamba ndugu ya mtu akifa, akamwacha mkewe wala hana mtoto, ndugu yake amtwae yule mkewe akampatie ndugu yake mzao.

20 Basi kulikuwa na ndugu saba, wa kwanza akatwaa mke, akafa, asiache mzao.

21 Wa pili naye akamtwaa akafa, wala yeye hakuacha mzao. Na wa tatu kadhalika;

22 hata na wote saba, wasiache mzao. Mwisho wa wote yule mwanamke akafa naye.

23 Basi, katika kiyama atakuwa mke wa yupi katika hao? Maana wote saba walikuwa naye.

24 Yesu akajibu, akawaambia, JE! HAMPOTEI KWA SABABU HII, KWA KUWA HAMYAJUI MAANDIKO WALA UWEZA WA MUNGU?

Kama tunavyosoma hapo kulingana na maneno ya Bwana Yesu, aliona watu hao wamepotea, na kupotea kwako kulichangiwa na sababu mbili kubwa, ya kwanza 1) Walikuwa hawayajui maandiko 2) Walikuwa hawaujui uweza wa Mungu.

Hizi ni sababu kuu ambazo zinaweza kumfanya mtu apotee hata leo hii, aidha katika Dini za uongo kama hawa Au arudi nyuma katika ulimwengu kabisa aseme, haya mambo hayawezekani.

  1. Tukianzana na kutokuujua uweza wa Mungu

Hawa mafarisayo, waliishi kwa fikra za kibinadamu na sio kwa fikra za Ki-Mungu, hawakukaa kujiuliza hao malaika wanaishije ishije huko mbinguni, bila kuoana au kuzaliana lakini bado wanaishi kwa furaha mbele za Mungu. Hata leo hii, Hawakujua kuwa Mungu pia anao uwezo wa kuwafanya kama Malaika. Akaondoa katika miili yao tamaa za mwili, wakawa ni miili ya utukufu isiyokuwa na mapungufu, isiyosinzia, isiyoumwa, isiyochoka kama wao..Hilo hawakuliwaza, kwasababu hawakuujua uweza wa Mungu kuwa unaweza kufanya na hilo pia.

Imani kama hizo hata leo zipo katika baadhi ya dini, wakidhani kuwa mtu akifa atakwenda kupewa wake 70 huko mbinguni. Hiyo yote ni kwasababu hatuujui uweza wa Mungu.

Kukosa kuujua uweza wa Mungu hata sasa, kunawafanya watu wengi, wapotee sana, wakidhani pia Mungu hawezi kuwaokoa wanadamu wakiwa hapa duniani..kwa kuwafanya wawe watakatifu..Na hiyo inawapelekea wajidanganye hivyo hivyo kwamba hakuna mtu anayeweza kushinda dhambi akiwa duniani, na matokeo yake wanakufa katika dhambi zao, na mwisho wa siku wanajikuta wapo kuzimu.

Kumbe hawajua uweza huo wa kufanywa wakamilifu hautoki kwa mwanadamu bali kwa Mungu pale mtu anapomwamini na kumpokea. Alisema..

Yohana 1:12 “Bali wote waliompokea ALIWAPA UWEZO wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake;”

Mtu akimwamini Kristo, na kumtii yeye, kitu kinachotokea kwake ni kupokea uwezo mpya, wa kufanyika mwana wake wa kushinda dhambi. Ukishindwa kuyajua hayo, basi ni rahisi sana kupotea..

2) Sababu ya pili ni: Ni kutojua Maandiko.

Tukirudi kwenye lile swali lao walilomuuliza tunaona mbele kidogo Bwana akiwauliza, HAMJASOMA?. Akitazamia kuwa kama wangekuwa wamesoma vema wasingekuwa na swali kama hilo..

Marko 12:26 “Na kwa habari ya wafu ya kwamba wafufuliwa, hamjasoma katika kitabu cha Musa, Sura ya Kijiti, jinsi Mungu alivyomwambia, akisema, Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo?

27 Yeye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai. HIVYO MWAPOTEA SANA”.

Unaona? Dini ambayo ilikuwa imeshakita mizizi yenye wafuasi wengi, kama baadhi ya dini nyingi leo hii duniani lakini kumbe ilikuwa imeshapotea kwa kutoyajua tu maandiko.

Leo hii watu wengi wamepotoshwa kwa kutoyafahamu maandiko, ukiona unaabudu sanamu, Ukiona unashikilia sabato na kusema huo ndio muhuri wa Mungu, wakati biblia inasema muhuri wa Mungu ni Roho Mtakatifu (Waefeso 4:30) ujue umepotoshwa na dini, ukiona unaabudu sanamu na kudhani kuwa zile ni viunganishi au vipatanishi na Mungu basi ujue umepotoshwa.

Hivyo sote kwa pamoja ni sharti tuufahamu uweza wa Mungu, kwamba hapa duniani wokovu upo, na watakatifu pia wapo, na kwamba pasipo utakatifu hakuna mtu atakayemwona Mungu asipokuwa nao sawasawa na (Waebrania 12:14) vilevile tuyasome maandiko, tuyatafakari sana, kila siku ili tusije tukazama katika madanganyo ya dini au madhehebu, au upotofu wa kidunia uliopo leo hii duniani.

Tukizingatia hayo mawili kama Bwana Yesu alivyosema, tusahau kupotea.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Tofauti kati ya ufunuo, unabii na maono ni ipi?

KUMBE MUNGU ANAWEZA KUKULIPA KWA USICHOSTAHILI!

Neema ni nini?

Je! Ni dhambi kumpiga au kumuua mnyama bila sababu yoyote?

CHANGIA SASA.

MAPEPO YANATAFUTA HIFADHI NDANI YAKO KWA BIDII SANA.

Rudi nyumbani

Print this post

Tofauti kati ya ufunuo, unabii na maono ni ipi?

  1. UFUNUO

Ufunuo ni jambo ambalo hapo kabla lilikuwa limesitirika au limefungwa lakini sasa limefunuliwa. Kwa mfano katika biblia, utaona, Watu wengi walishindwa kumtambua Yesu ni nani, wengine walidhani ni Yeremia, wengine, mmojawapo wa manabii wa kale, wengine ni Yohana mbatizaji, Lakini Yesu alipowauliza mitume wake, Petro akasema, wewe ndiye Kristo mwana wa Mungu aliye hai. Yesu kusikia vile tunaona akamwambia maneno haya;

Mathayo 16:17 “Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu HAVIKUKUFUNULIA HILI, bali Baba yangu aliye mbinguni.

18 Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda”.

Unaona, Petro alifunuliwa, siri ambayo ilikuwa haijulikani na watu hapo kabla.

Vivyo hivyo na sisi tunahitaji ufunuo wa Roho Mtakatifu kuyaelewa  maandiko vinginevyo tutakuwa tunakisia tu au hatuyaelewi pale tunapoyasoma.

2) MAONO.

Ni taarifa ya rohoni ambayo mtu anapokea kutoka kwa Mungu,aidha anapokuwa usingizini, au akiwa macho. Anajikuta anaona vitu ambavyo hakupanga kuviona, na taarifa hizo zinaweza kuwa kwa mafumbo, au kwa uwazi, na zinaweza kueleza matukio yaliyopita au ya hapo hapo, au yale yatakayokuja baadaye.

Katika biblia tunaona watu wengi sana wakionyeshwa Maono..

Matendo 10:1 “Palikuwa na mtu Kaisaria, jina lake Kornelio, akida wa kikosi kilichoitwa Kiitalia,

2 mtu mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi, na kumwomba Mungu daima.

3 Akaona katika maono waziwazi, kama saa tisa ya mchana, malaika wa Mungu, akimjia na kumwambia, Kornelio!

4 Akamtazama sana, akaogopa akasema, Kuna nini, Bwana? Akamwambia, Sala zako na sadaka zako zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu.

5 Sasa basi, peleka watu Yafa, ukamwite Simoni, aitwaye Petro”.

3) UNABII

Ni taarifa ya wakati ujao, (utabiri wa rohoni), ambayo Mungu anautoa moja kwa moja, hiyo inaweza kuwa katika maneno ya mtu anayozungumza bila yeye kujua, mfano utasoma mstari huu kuhani mkuu alitoa unabii pasipokujua kama yeye aliutoa.

Yohana 11:51 “Na neno hilo yeye hakulisema kwa nafsi yake; bali kwa kuwa alikuwa Kuhani Mkuu mwaka ule, alitabiri ya kwamba Yesu atakufa kwa ajili ya taifa hilo”.

au kwa njia ya kuambiwa au kuhubiriwa,

Ufunuo 11:3 “Nami nitawaruhusu mashahidi wangu wawili, nao watatoa unabii siku elfu na mia mbili na sitini, hali wamevikwa magunia”.

Hii ikiwa na maana kuwa katikati ya mafundisho, au mahubiri, Mungu huwa anatoa unabii wa mambo yajayo ndani yake.

1Timotheo 1:18 “Mwanangu Timotheo, nakukabidhi agizo hilo liwe akiba, kwa ajili ya maneno ya unabii yaliyotangulia juu yako, ili katika hayo uvipige vile vita vizuri”;

Kwa njia ya kuonyeshwa au kwa maono.

Yuda 1:14 “Na Henoko, mtu wa saba baada ya Adamu, alitoa maneno ya unabii juu ya hao, akisema, Angalia, Bwana alikuja na watakatifu wake, maelfu maelfu”,

Pia  kitabu chote cha Ufunuo ni kitabu kitabu cha unabii, ambacho Yohana alionyeshwa kwa njia ya maono.

Ufunuo 22:6 “Kisha akaniambia, Maneno haya ni amini na kweli. Naye Bwana, Mungu wa roho za manabii, alimtuma malaika wake kuwaonyesha watumwa wake mambo ambayo hayana budi kuwako upesi.

7 Na tazama, naja upesi; heri yeye ayashikaye maneno ya unabii wa kitabu hiki”.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

CHUKIZO LA UHARIBIFU

Mafundisho

UFUNUO: Mlango wa 1

Tofauti kati ya ndoto na Maono ni ipi?

THAWABU YA UAMINIFU.

Rudi nyumbani

Print this post

THAWABU YA UAMINIFU.

Kwa kawaida Mungu huwa hatoi karama zake zote kwa mkupuo, bali huwa anakupa kwanza kidogo kisha anaupima auminifu wako au uadilifu wako katika hicho, kisha akishaona umekithaminisha ndipo baadaye anakumwagia vyote vilivyobakia kwa wingi.

Leo tutaitazama mifano miwili ya watu walioambiwa maneno hayo naamini kwa kuisoma itakuongeza nguvu katika eneo hili la uaminifu,, wa kwanza tutauona kutoka katika maandiko na wa pili katika shuhuda za watu walitutangulia kwenye Imani.

Katika biblia, tunaona mtu mmoja aliyeitwa Yoshua, kuhani mkuu, ambaye Mungu alimwambia maneno haya;

Zekaria 3:6 “Kisha malaika wa Bwana akamshuhudia Yoshua, akisema,

7 Bwana wa majeshi asema hivi, Kama ukienda katika njia zangu, na kama ukishika maagizo yangu, ndipo utakapoihukumu nyumba yangu, nawe utazilinda nyua zangu, NAMI NITAKUPA NAFASI YA KUNIKARIBIA KATI YAO WASIMAMAO KARIBU”.

Huyu Yoshua alichaguliwa na Mungu kuwa kuhani mkuu wakati ule ambapo wana wa Israeli wanaondolewa tena Babeli, kumbuka huyu si yule Yoshua aliyewavusha wana wa Israeli Yordani, kutoka jangawani hapana, bali ni mwingine kabisa.

Sasa wakati akiwa Yerusalemu, Mungu akamchagua na kumtakasa, akamtia mafuta, awe kuhani wake, kuwapatanisha wayahudi wote.. Lakini tunasoma ahadi nyingine hakuzipokea palepale, bali zilitegemea kwanza uaminifu wake, ndipo Mungu ampatie ahadi hizo baadaye..

Mungu alimwahidi kuwa ikiwa atakuwa mwaminifu, ndipo ataihukumu nyumba yake, na vilevile atampa nafasi ya kumkaribia yeye, kati ya hao wasimamao karibu yake. Ulishawahi kujiuliza ni wakina nani hao wasimamao karibu na Mungu?.. Hapa duniani sio watu wote watakuja kusimama karibu na Mungu tutakapofika kule ng’ambo hata kama watakuwa wameokoka.

Ni sawa na leo hii, si watu wote wanaweza kusimama karibu na raisi wa nchi, kama hawajaalikwa na yeye, au kama hawana nafasi yoyote au cheo chochote katika serikali. Utagundua ni mawaziri tu, na watu wakubwa wakubwa wa serikalini, au familia yake tu ndio wanaoweza kumkaribia yeye. Lakini wengine wote mtakuwa mkimtazama kwenye Tv, au majukwaani.

Na vivyo hivyo kwa Mungu, wapo watu tayari ambao wameshawekwa karibu na Mungu,kutokana na uaminifu wao wa juu walipokuwa hapa duniani, katika maandiko tunawafahamu baadhi, wa kwanza ni Ibrahimu,

Mathayo 8:11 “Nami nawaambieni, ya kwamba wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi pamoja na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni;”

Wengine wakiwemo, akina Musa na Eliya, Wakina Danieli, watu waliopendwa na Mungu, wengine ni Ayubu, Samweli, akina Daudi aliyeupendeza moyo wa Mungu, Henoko, Mitume 12 wa Yesu, ambao Bwana aliwaahidia wataketi katika viti 12 wakiyahukumu makabila 12 ya Israeli, Yohana mbatizaji ambaye katika uzao wa wanawake hakuna aliyewahi kuwa mkuu Zaidi yake, wengine ni kama Mtume Paulo ambaye alitenda kazi kuliko wakristo wote wa wakati ule. Na pia wale mashahidi wawili ambao tunawasoma katika  ufunuo ambao wanafananishwa na ile mizeituni miwili,N.k.

Ufunuo 11:4 “Hao ndio ile mizeituni miwili na vile vinara viwili visimamavyo mbele za Bwana wa nchi”.

Sasa hawa wote, ni watu ambapo wanasimama karibu sana na Mungu.. Hivyo Yoshua naye kama kuhani mkuu aliahidiwa ofa hiyo, kwamba kama akiwa mwaminifu, na yeye pia ataingizwa katika kundi  hilo dogo la watu watakaosimama karibu na Mungu, tengeneza picha unasimama karibu na Mungu muumba wa Mbingu na nchi na malaika..si jambo dogo hilo. Na sisi pia tutamani nafasi hizo.

Vivyo hivyo, leo tutamtazama mtu mwingine ambaye alitokea katika kizazi chetu aliyeitwa WILLIAM BRANHAM.

Ikiwa hujawahi kumfahamu mtu huyu, ushuhuda wake ulikuwa ni wa kipekee sana, hatuwezi eleza habari yake yote hapa,  lakini, kwa ufupi ni kuwa alizaliwa mwaka 1909, huko Marekani, katika familia ya kimaskini sana, elimu yake iliishia darasa la saba tu, lakini tangu akiwa mdogo Mungu alianza kumuonyesha maono mengi, ambayo mengine hakujua tafsiri yake ni nini, mengine aliyaona yakitimia muda mfupi baadaye,..Lakini alipokuwa mtu mzima, akiwa kama mchungaji wa kanisa dogo la kibaptisti baada ya kupitia shida nyingi, ikiwemo kufiwa na mke na mtoto wake, hakuacha kumtafuta Mungu kwa bidii.

Siku moja usiku wakati anasali kama saa 9 hivi, kumuuliza Mungu ni nini maana kusudi lake duniani, alitembelewa na Malaika wa Bwana, akamwambia, nimetumwa kutoka uweponi mwa Mungu, kukuambiwa kuwa maisha yako ya kutokueleweka, ni kukuonyesha kuwa Mungu amekuchagua kulibeba kusudi lake kwa watu..Akaambiwa atapewa karama ya uponyaji, na kama akiwa mwaminifu utafika wakati utakuwa na uwezo wa kujua hata siri za mioyo ya watu, na hukuna ugonjwa wowote utakaoisimama mbele yako hata saratani yenyewe..(Kwa kipindi hicho ugonjwa wa saratani ndio uliokuwa tishio duniani)

Ni kweli mtu huyu baada ya hapo alionyesha uaminifu wake kwa Mungu, na yote aliyoahidiwa yalikuja kutimia muda mfupi sana katika huduma yake .. alianza kufahamu siri za mioyo ya watu, wote waliosimama mbele yake katika mstari kuombwa, Na Zaidi ya hayo Mungu akamzidishia na ishara za ajabu, ilifikia wakati nguzo ya Moto ilitokea na kutua Juu yake, mbele ya kanisa akiwa anahubiri, na ikapigwa picha na kuwekwa katika makumbusho za kihistoria huko Marekani, baada ya kuthibitishwa na FBI, kuwa picha hiyo ni ya kimiujiza, ndio hiyo hapo unayoina katika katika ujumbe huu.

Si hilo tu wakati Fulani akiwa anawabatiza watu katika mto mmoja huko Marekani mwaka 1933, ghafla kulitokea nuru kubwa kama nyota na kutua juu yake, watu wote waliokuwepo pale waliiona, habari hizo zilishapishwa katika magazeti mengi maarufu huko Marekani..Na wakati alipokuwa akiwabatiza watu anasema alisikia sauti ikimwambia kama vile Yohana mbatizaji alivyotumwa kutangulia kuja kwa kwanza kwa Kristo, vivyo hivyo na ujumbe wako utatangulia kuja kwa pili kwa Kristo.

William Branham mpaka sasa, ni mwinjilisti ambaye wanazuoni na wanatheolojia wa dini wanamkumbuka kwa ishara na maajabu yaliyokuwa yanafuata naye katika huduma yake. Ya kuhubiri injili ulimwenguni kote.

Ikiwa utapenda kupata historia yake ndefu..tutumie ujumbe inbox ..

Lakini hiyo yote ni kutokana na uaminifu aliokuwa nao kwa Bwana.. Hakuhubiri udhehebu, kinyume chake, aliikemea roho za kidhehebu ambazo zinawafunga wakristo wasimtambue Mungu, na hiyo ikampelekea kuchukiwa sana na watu wa dini. Injili yake iliegemea katika kuwaelekeza watu kwa Yesu, na sio kwake, au kwa mtu Fulani, alikemea dhambi, hususani katika uvaaji mbaya wa wanawake.. Na matokeo yake Bwana akamtukuza na yeye. Mafundisho yake yaliegemea katika Misingi ya Neno tu.

Hivyo Ujumbe wake umekuwa kama MBIU kwa kanisa la mwisho la Laodikia ambalo ndio sisi tunaoishi, kwamba tutoke huko kwenye Kamba za udini na udhehebu tumwabudu Mungu katika Roho na Kweli.William ni mjumbe wa kanisa la letu la Laodikia.

Sasa kwa mifano hiyo miwili ,nataka  uone ni jinsi gani, Mungu anauthamini uaminifu wa mtu. Hata Musa kule jangwani aliuthamini kwanza muujiza wa kijiti kuteketea moto, ndipo Mungu akampa na mingine kikubwa Zaidi.  Kila mmoja wetu anapaswa awe mwaminifu katika kitu alichopewa na Mungu. Leo hii utaona Mungu kampa mchungaji kanisa, na kwa neema zake limeanza kukua kidogo, lakini itapita miaka miwili, mitatu, utasikia amefumaniwa katika uzinzi, mwingine amejilimbikizia mali zote za kanisa.. huko ni kukosa uaminifu kwa kile ulichopewa na Mungu.

Mungu anaweza kukupa karama Fulani katika kanisa, lakini baada ya kipindi Fulani unaanza kujiona wewe ni wewe, unaanza kuonyesha kiburi, huko ni kukosa uaminifu kwa kile kidogo ulichopewa. Unabadilika kama Yeroboamu unasahau kuwa ni Mungu ndiye aliyekupa,.. Kila mmoja wetu alieyokoka, kuna kitu Mungu amempa lakini tukishindwa kuwa waamifu navyo, tukavidharau, tukawa hatuvitendei kazi, kamwe tusitazamie kuwa Mungu atakaa atupe ahadi nyingine za juu zaidi ambazo alikuwa amekusudia kutupa.

Hivyo kuanzia leo mimi na wewe tuanze kujenga uaminifu kwa vile vichache Bwana alivyotupa.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

HISTORIA YA WILLIAM BRANHAM

KAMA MKRISTO FAHAMU ZIPO HATUA UTAPIGISHWA NA MUNGU.

KITABU CHA YUDA: SEHEMU YA 1

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

UFUNUO: Mlango wa 19

Rudi nyumbani

Print this post

Je! ni sahihi kwa mkristo kujifukiza?

SWALI: Nina swali mtumishi. Je mkristo aweza kujifukiza katika kipindi hiki cha changamoto za kupumua. Biblia inasema nini juu ya hili. Je, neno hili kwenye Ayubu 5:3 inazuia kujifukizia?

Ayubu 5:3 “Nimewaona wapumbavu wakishusha mizizi; Lakini mara niliyalaani maskani yake”.

JIBU: Kujifukiza ni tiba mojawapo kama zilivyo tiba nyingine. Mtu mmoja anaweza kuumwa na akaenda kumeza dawa za hospitalini, na mwingine akaenda kuchemsha mwarobaini akanywa. Na wote wakawa wazima.

Jambo ambalo si sahihi, ni pale tiba hiyo inapotolewa “sadaka kwa sanamu” nikiwa na maana kuwa pale inapohusianishwa na uganga au Imani potofu ambazo mara nyingi zinaambatanisha na masharti Fulani ambayo hata hayana uhusiano wowote na hiyo dawa kwamfano labda utaambiwa unywapo sema maneno Fulani, au nenda kainywee makaburini, au usinywe mbele ya watoto wako, au unyapo hakikisha upo uchi n.k… Sasa hizo ndio Mungu amekataza kwasababu ni ibada za sanamu.

Lakini tukirudi kwenye huo Mstari wa Ayubu 5:3 haizungumzii mizizi hii tunayoifahamu kama dawa, hapana, bali habari hiyo inazungumzia jambo lingine kabisa jinsi wenye dhambi wanavyoweza kujiimarisha kiasi cha kukita mizizi chini, wakijiwekea hazina nyingi, na kujijengea maboma makubwa, lakini hata hivyo, Mungu atawalaani na kuziangamiza maskani zao. Ukianzia kusoma tokea mistari ya juu utapata picha kamili ya habari hiyo.

Hivyo, kwa mkristo kujivukiza, si makosa, lakini pia ni vizuri tukajua sababu ya magonjwa haya kulipuka ni nini. Mungu hajayaleta ili tuyatafutie tiba hapana, Bali haya ni mapigo kutoka kwa Mungu na hilo lipo wazi yanayotutambulisha kuwa sisi kama dunia tumemsahau yeye, na pia  tunaishi katika siku za mwisho sawasawa na maneno ya Yesu katika , (Luka 21:11).

Swali ni je! Umeokoka? Je Yesu yupo ndani yako? Kama jibu ni hapana, basi ujue upo katika wakati wa hatari sana. Na wewe upo ndani ya hiyo hiyo ghadhabu ya Mungu iliyoachiliwa wakati huu tunaoishi, Hivyo fanya uamuzi wa busara, mkaribishe Yesu maishani mwako katika dakika hizi za majeruhi tunazoishi, Kabla mabaya hayajakufikia.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

https://wingulamashahidi.org/2019/09/01/je-ni-vema-kwa-mkristo-kwenda-hospitali-au-kutumia-miti-shamba-anapougua/

Rudi nyumbani

Print this post

Nini maana ya “Ulipo mzoga, ndipo watakapokutanika tai?

SWALI: Shalom naomba kufahamu maana ya huu mstari..

Luka 17:37 “Wakajibu, wakamwuliza, Wapi, Bwana? Akawaambia, Ulipo mzoga, ndipo watakapokutanika tai”.


JIBU: Kabla ya wanafunzi wa Yesu kumuuliza Bwana hilo swali “WAPI?”..Kuna maneno ambayo yalitangulia juu kidogo, ambayo tukiyasoma yatatusaidia kuelewa vizuri huo mstari ulimaanisha nini, embu tusome kidogo.

Luka 17:22 “Akawaambia wanafunzi, Siku zitakuja mtakapotamani kuona siku moja katika siku zake Mwana wa Adamu, msiione.

23 Tena watawaambia, Tazama, kule! Tazama, huku! Msiondoke mahali mlipo, wala msiwafuate”;

Ukisoma kwenye Mathayo imeeleza kwa undani zaidi, inasema..

Mathayo 24:23 “Wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule msisadiki.

24 Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule.

25 Tazama, nimekwisha kuwaonya mbele.

26 Basi wakiwaambia, Yuko jangwani, msitoke; yumo nyumbani, msisadiki”.

Maneno hayo Yesu aliyatanguliza kama angalizo la nyakati za hatari zitakazotokea siku za mwisho, akiwaonya kwamba wengi watakuja wakiwavuta watu kwao wakiwaambia Kristo yupo huku au kule, kwa maneno yao ya ushawishi, wakijinadi, tuna hichi au kile, sisi tuna miujiza mikubwa, sisi tuna upako wa mafuta mabichi, sisi ni wataalumu wa tiba za kiroho, sisi tuna makanisa makubwa kuliko yote duniani n.k.

Hivyo Yesu kwa kulijua hilo kwamba litakuja kutokea akawapa tahadhari wanafunzi wake kwamba wasitoke kuwafuata, wasiwe wepesi kuwaendea, wabaki mahali walipo, wasiende popote, kwasababu watawapotosha..

Sasa katika mazingira hayo ya kutokwenda mahali popote ndipo wanafunzi wake mwishoni wakamuuliza swali, NI WAPI sasa patakuwa sahihi pa kwenda..au tutakwenda wapi?

Ndipo Yesu akawaambia palipo na mzoga ndipo watakaposanyika Tai.. Ikiwa na maana mahali palipo na chakula cha Tai ndipo watakapokuja hapo na kukusanyika..

Na kama tunavyojua ndege aina ya tai wanaouwezo wa kuona mbali sana, leo hii kama kuna mnyama kafa porini na angani hakuna ndege yoyote, ukikaa baada ya muda mfupi utawaona tai wengi wamekusanyika hapo.. utajiuliza wametokea wapi na wakati anga lilikuwa jeupe halina ndege hata mmoja? Ni kwasababu jicho la Tai huwa linaona chakula kutokea mbali sana. Tai anaona mahali ambapo wewe huwezi kumwona.

Ni kama tu vile, mahali Fulani pawe na kinyesi cha mnyama au mtu, dakika si nyingi utaona nzi wengi wamekusanyika, na utajiuliza wametoka wapi wadudu hao na mahali hapo ni porini..Jibu ni kwamba, Mungu kawaumbia uwezo mkubwa wa kunusa vitu vya asili yao, tokea mbali, na ndio maana utawaona hata kama eneo hilo limejificha namna gani, wataenda tu.

Vivyo hivyo na wana tai wa Mungu, Kristo kawawekea uwezo Fulani wa kujua chakula chao halisi kilipo haijalishi ni wapi walipo watakipata tu. Tai si kama kuku, ambaye anaona vya hapo chini tu, bali Tai anaona vya mbali sana. Vivyo hivyo na sisi kama ni wanatai, ni lazima tuwe wa kufuata kile chakula kilicho chetu tu..Si kila chakula cha kukikurupukia kisa kipo karibu na sisi, au kinavutia..

Bali tuwe na macho ya tai ya kujua chakula chetu kipo wapi..

Hizi siku za mwisho, usiwe wa kukurupukia kila aina ya mafundisho, au imani. Kristo ameshatuonya..

Tafuta chakula cha wakati wako unaoishi.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

Mada Nyinginezo:

Rudi nyumbani

Print this post

Kwanini Yesu aliwakataza mitume wake kumdhihirisha?

SWALI: Shalom ndugu wapendwa! Naomba kuuliza kwa nini Yesu awakataze akina Petro wasiseme kwa watu kwamba yeye ni KRISTO kama ilivyo kwenye Mathayo 16:20

JIBU:

Kwa faida ya wengi tusome habari yote inayoelezea hilo tukio..

Mathayo 16:13 “Basi Yesu akaenda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani?

14 Wakasema, Wengine hunena u Yohana Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii.

15 Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?

16 Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.

17 Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni.

18 Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.

19 Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.

20 NDIPO ALIPOWAKATAZA SANA WANAFUNZI WAKE WASIMWAMBIE MTU YE YOTE ya kwamba yeye ndiye Kristo”.

Sasa ukisoma vitabu vyote vya injili utagundua sio tu katika tukio hilo aliwakataza wanafunzi wake wasimdhihirishe, bali pia yapo matukio mengine mbalimbali aliwakataza watu wasimdhihirishe, utaona kuna wakati aliwazuia makutano aliowaponya wasimtangaze..(Mathayo 8:4) Wakati mwingine aliyazuia pia  mapepo aliyoyatoa yasimtangaze,

Marko 3:11 “Na pepo wachafu, kila walipomwona, walianguka mbele yake, wakalia wakisema, Wewe ndiwe Mwana wa Mungu. 12 Akawakataza sana, wasimdhihirishe”.

na pia utaona kuna wakati Bwana alipojidhihirisha kwa mitume wake, wale 3 kule mlimani kwa mavazi ya kumeta-meta aliwaambia maneno hayo hayo.

Lakini kwanini awazuie watu kumdhihirisha?

Sio kwamba aliogopa, au alikuwa hataki kujulikana hapana, lakini aliwazuia kwasababu Ushuhuda wake ulikuwa bado haujakamilika. Ilimpasa kwanza ayatimize yote aliyoandikiwa kama mkombozi wa huu ulimwengu, kisha yakishakamilika, ndipo sasa habari hizo zihubiriwe rasmi kwa watu wote, Na ndio maana utaona sehemu nyingine anasema, subirini mpaka nitakapofufuka kutoka katika wafu ndipo mhubiri habari zangu, myasimulie haya.

Mathayo 17:5 “Alipokuwa katika kusema, tazama, wingu jeupe likawatia uvuli; na tazama, sauti ikatoka katika lile wingu, ikasema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye.

6 Na wale wanafunzi waliposikia, walianguka kifulifuli, wakaogopa sana.

7 Yesu akaja, akawagusa, akasema, Inukeni, wala msiogope.

8 Wakainua macho yao, wasione mtu ila Yesu peke yake.

9 Na walipokuwa wakishuka mlimani, Yesu aliwaagiza, akasema, MSIMWAMBIE MTU YE YOTE HABARI YA MAONO HAYO, HATA MWANA WA ADAMU ATAKAPOFUFUKA KATIKA WAFU.

Hapo ndio lile Neno la Yesu alilolisema katika Mathayo 10:27 lilipokuja kutimia..

Mathayo 10:27 “Niwaambialo ninyi katika giza, lisemeni katika nuru; na msikialo kwa siri, lihubirini juu ya nyumba”.

Ni jambo la kawaida hata sasa  kitu chochote ambacho kitatumiwa na uma, huwa kinajaribiwa kwanza na watu wachache, kisha kikishathibitishwa, au kukamilishwa ndipo kinapoachiwa kwa uma mzima kutumiwa.

Hivyo, sababu ya yeye kuzuia mambo yake mengi yasidhihirishwe kwa wakati ule ni kwasababu ushuhuda wake ulikuwa haujamilika bado. Lakini sasa umeshakamilika na ndio maana tunazitangaza habari za Yesu wazi wazi kwa wote bila kumficha mtu chochote.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

NI VIZURI SISI KUWAPO HAPA.

Nini maana ya “Tumejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii”?

TUMEFANYIKA KUWA WANA WA MUNGU!

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

Kwanini  vizazi vya ukoo wa Yesu vinajipinga katika Mathayo na Luka.

Kiango na Pishi ni nini (Mathayo 5:15)?

Rudi nyumbani

Print this post

NI VIZURI SISI KUWAPO HAPA.

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe daima, Ni siku nyingine tena Mungu ametupa neema ya kujifunza, hivyo nakukaribisha tuyatafakari pamoja maneno ya uzima maadamu siku ile inazidi kujongea.

Lipo jambo alilizungumza Petro, wakati ule ambao Bwana Yesu aliwachukua yeye pamoja na Yakobo na Yohana juu ya ule mlima mrefu.. Tukilisoma naamini litatupwa mwanga wa jinsi ya kutembea  vema katika safari yetu hii ya wokovu, Tusome habari yenyewe kwa ufupi na mbeleni kuna jambo kubwa ambalo Mungu atatufundisha siku ya leo.

Luka 9:28 “Baada ya maneno hayo yapata siku nane, aliwatwaa Petro na Yohana na Yakobo, akapanda mlimani ili kuomba.

29 Ikawa katika kusali kwake sura ya uso wake ikageuka, mavazi yake yakawa meupe, yakimeta-meta.

30 Na tazama, watu wawili walikuwa wakizungumza naye, nao ni Musa na Eliya;

31 walioonekana katika utukufu, wakanena habari za kufariki kwake atakakotimiza Yerusalemu.

32 Petro na wale waliokuwa pamoja naye walikuwa wamelemewa na usingizi; lakini walipokwisha amka waliuona utukufu wake, na wale wawili waliosimama pamoja naye.

33 Ikawa hao walipokuwa wakijitenga naye, PETRO ALIMWAMBIA YESU, BWANA MKUBWA, NI VIZURI SISI KUWAPO HAPA; NA TUFANYE VIBANDA VITATU; KIMOJA CHAKO WEWE, NA KIMOJA CHA MUSA, NA KIMOJA CHA ELIYA; HALI HAJUI ASEMALO.

34 Alipokuwa akisema hayo, lilitokea wingu likawatia uvuli, wakaogopa walipoingia katika wingu hilo.

35 Sauti ikatoka katika wingu, ikisema, Huyu ni Mwanangu, mteule wangu, msikieni yeye.

36 Na sauti hiyo ilipokwisha, Yesu alionekana yu peke yake. Nao wakanyamaza, wasitangaze kwa mtu siku zile lo lote katika hayo waliyoyaona”.

Katika mazingira hayo utaona, wakati Yesu akiwa uweponi mwa Mungu, ghafla Musa na Eliya walitokea wakaanza kuzungumza naye.. Mazungumzo hayo inaelekea yalikuwa ni marefu kidogo, kwasababu hawakuja kama malaika kuleta ujumbe tu na kuondoka hapana, bali walikuja kama wageni, kuzungumza naye, na mada kuu ilikuwa ni kuhusu kifo chake, jinsi atakavyoteswa na kukataliwa na watu kule Yerusalemu.

Kumbuka wakati huo mitume walikuwa wamelala, lakini walipoamka ghafla, wakamwona Yesu waliyemzoea akiwa katika mwonekano mwingine kabisa, na pembeni yake walikuwa watu wengine wawili wamesimama, na cha kushangaza walikuwa wakiongea naye kama vile wanajuana.

Hivyo Petro kuona tukio kama lile Bwana akiwa na wageni wa kimbinguni, huku akitazama na mazingira ya pale mlimani, hakuna hata chochote CHA KUWATIA UVULI, akaona si vema, asikae tu hivi hivi akimtazama Bwana akizungumza na wageni wake kwenye jua.

Ghafla akajikuta tu anazungumza, na kumwambia Bwana, Ni vizuri sisi kuwapo hapa.. akiwa na maana ni kama vile bahati wao kupanda naye kule mlimani kwasababu, walau wanaweza kumsaidia kufanya kitu.. Ndipo Petro akasema wacha tuwatengenezee vibanda vitatu, kimoja chako wewe, kimoja cha Eliya na kingine cha Musa.. Ili walau mpate uvuli juu ya mlima huu mrefu, mwendelee kuzungumza kwa utulivu zaidi.. hivyo wacha sisi tushuke chini tukachukue vifito tuanze kazi..

Embu tengeneza picha, Petro alijua Bwana amepatwa na ugeni wa kimbinguni, alijua wale watu hawana haja ya kukaa kwenye vibanda,, lakini kutokana na mazungumzo yao kuwa eneo tupu la wazi kama lile hakuona aibu kuonyesha kujali kwake kwao… Kama vile Ibrahimu wakati ule alipotembelewa na wale watu watatu, alipowaalika na kuwanjia ndama.

Na biblia inatuambia mara baada ya Petro kuzungumza maneno yale.. saa hiyo hiyo, wingu kubwa jeupe, likashuka mahali pale, likawatia UVULI wote, walipoona vile waliogopa sana, kukaribia kuzimia kwasababu jambo kama hilo hawajawahi kuliona katika maisha yao yote, na saa hiyo hiyo, sauti ikatoka KATIKATI ya lile wingu ikisema..

“Huyu ni mwanangu mpendwa wangu msikieni yeye”…Maneno kama hayo kuyasikia ilihitaji mbingu ikupasukie kwanza, walioweza kusikia sauti ya Mungu moja kwa moja kutoka mbinguni ikimshuhudia Yesu ni hawa watatu, pamoja na Yohana mbatizaji Ambaye yeye wakati anambatiza Yesu, mbingu zilimpasukia na kusikia maneno hayo hayo.(Mathayo 3:16-17)

Lakini hiyo yote, ilikuwa ni kwasababu gani?

Ni kwasababu alifikiria kwanza kumwekea Bwana uvuli kwa vile vibanda walivyokuwa wanataka kumjengea yeye. Ndipo Mungu akawatia UVULI halisi wa Mbinguni kwa wingu lake yeye mwenyewe.

Tengeneza picha mfano wasingejaribu kufikiria vile kwa ajili ya Bwana wao.. Ni wazi kuwa wasingeshukiwa na wingu lolote na wala wasingekaa waisikie sauti ya Mungu moja kwa moja ikuzungumza nao. Ushuhuda ambao wangebakiwa nao ni ule wa kumwona Eliya na Musa, na Yesu kuwa na mavazi meupe basi. Hakuna Zaidi.

Vivyo hivyo na sisi leo, Je, tunamtazama Kristo akihudumu katika hali gani? Na sisi tutakuwa  ni watu wa kutazama tu, au wa kusikiliza tu, au tutasema kama Petro, NI VEMA SISI KUWAPO MAHALI HAPA. Tukifikiria hata kwa uchache Mungu aliotujalia, au alivyotupa hivyo vinatosha kwa Mungu, ahitaji wingi wako, anahitaji nia yako, na moyo wako wa dhati.. Kama wafuasi wa Kristo hatupaswi kukaa kuangalia injili inahubiriwa katika hali ya taabu. Ni kweli utukufu wa Mungu utaendelea kuonekana, lakini zipo faida ambazo tutazikosa kama hatutakuwa na mawazo  kama ya Petro, alivyosema NI VEMA MIMI KUWEPO HAPA, wacha nikachukue fito nimwekee Bwana kivuli, sihitaji niwe na matofauti kwanza.

Wakati mwingine tunashindwa kumsikia Mungu kipekee kwasababu ya sisi kutoelewa kanuni za utendaji kazi wake.

Kumbuka Neno la Mungu (BIBLIA) ndiyo dira ya safari yetu hapa duniani. Siri zote za Mungu na njia zote za  kumfikia yeye utazipata huko tu, na sio kwa mwanadamu yoyote, au kwa mwanazuoni yeyote, au msomi yoyote, au kwenye kitabu kingine chochote.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

CHANGIA SASA.

PATANA NA MSHITAKI WAKO KWANZA.

ESTA: Mlango wa 8, 9 & 10. (SIKU KUU YA PURIMU)

UFUNUO: Mlango wa 19

TUMTOLEE MUNGU VILE VINAVYOTUGHARIMU ZAIDI.

DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.

Rudi nyumbani

Print this post

Fuawe ni nini? Kama tunavyosoma katika Isaya 41:7

Isaya 41:7 “Seremala akamtia moyo mfua dhahabu, na yeye alainishaye kwa nyundo AKAMHIMIZA YULE APIGAYE FUAWE, akiisifu kazi ya kuunga, akisema, ni kazi njema; naye akaikaza kwa misumari isitikisike. ”.


JIBU: Fuawe ni chuma kizito, zilichotengenezwa na wafuaji kwa ajili ya kazi ya kuchonga au kukarabati vitu vyenye asili ya chuma, kama fedha, dhahabu, shaba, n.k. kwa kuviponda ponda  juu ya chuma hicho ili vitokee katika  maumbile waliyoyatazamia Tazama picha chini.

Ilikuwa kama wanataka kuunda umbile Fulani la chuma au shaba au fedha, walikiingiza kwanza kwenye moto kiyeyuke ili kiwe kirahisi kupondwa.. Ndipo kikishatolewa kililetwa kwenye hii fuawe sasa kwa ajili ya kugongwa kwa lengo la kukipa umbile lake.

Hivyo tukirudi katika mstari huo, anasema seremala akamtia moyo mfua dhahabu, hapa alikuwa anamzungumzia mtengeneza vinyago, vya mbao, ambaye baada ya kuvichonga sasa alikuwa tayari kuvipeleka vinyago vyake kwa walainishao yaani wafuaji, ili wawandalie dhahabu au fedha ya  kuvifunika vinyago vyake na huyo mfua fedha, aishaiweka dhahabu aliipeleka  sasa kwa huyu mpiga fuawe, mchongaji wa mwisho wa kinyago, ili kuleta umbo kamili la kinyago kile, Soma pia (Isaya 40:19)

chuma kizito fuawe

Lakini Mungu hapo alikuwa anaonyesha taabu zao, na gharama zao nyingi wanazoingia kwa mambo yasiyokuwa na faida, Kwa kujiundia vinyago visivyoweza kuzungumza wala kusikia, wala kuokoa, wala kutoa ahadi za ulinzi baadaye.. Lakini tunaona hapo mistari iliyofuata Mungu akiwaahidia watu wake Israeli ahadi nono, ambazo vinyago haviwezi kutoa, akiwaambia..

Isaya 41:8 “Nawe, Israeli, mtumishi wangu; Yakobo, niliyekuchagua; mzao wa Ibrahimu, rafiki yangu;

9 wewe niliyekushika toka miisho ya dunia, na kukuita toka pembe zake, nikikuambia, Wewe u mtumishi wangu; nimekuchagua wala sikukutupa;

10 usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu”.

11 Tazama, wote walioona hasira juu yako watatahayarika na kufadhaika; watu washindanao nawe watakuwa si kitu, na kuangamia.

12 Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe; watakuwa si kitu; watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu yako.

13 Kwa maana mimi, Bwana, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kuume, nikikuambia, Usiogope; mimi nitakusaidia.

14 Usiogope, Yakobo uliye mdudu, nanyi watu wa Israeli; mimi nitakusaidia, asema Bwana, na mkombozi wako ni Mtakatifu wa Israeli.

15 Tazama, nitakufanya kuwa chombo kikali kipya cha kupuria, chenye meno; utaifikicha milima, na kuisaga; nawe utafanya vilima kuwa kama makapi.

16 Utawapepeta, na upepo utawapeperusha; upepo wa kisulisuli utawatawanya; nawe utamfurahia Bwana, utajitukuza katika Mtakatifu wa Israeli.

17 Maskini na wahitaji wanatafuta maji, wala hapana; ndimi zao zimekauka kwa kiu; mimi, Bwana, nitawasikia, mimi, Mungu wa Israeli, sitawaacha.

18 Nitafunua vijito vya maji juu ya vilima, na chemchemi katikati ya mabonde; nitageuza jangwa kuwa ziwa la maji, na mahali pakavu kuwa vijito vya maji.

19 Nitapanda katika jangwa mwerezi, mshita, mhadasi, na mbono; nitatia katika nyika mberoshi, mtidhari, na mteashuri pamoja;”

Na sisi je, tunaweza kuweka kando ibada zote za sanamu za rohoni na mwilini, mpaka ifikie hatua ya Mungu kutuahidia ulinzi mnono kama huo aliowaahidia wana wa Israeli?

Jibu tunalo,

Je umeokoka? Je, unatambua kuwa nyakati hizi ni za mwisho?.. Na kanisa tunaloishi ndio kanisa la mwisho lijulikanalo kama Laodikia? Kama unayatambua hayo sasa Unangoja nini usimkaribishe Kristo leo maishani mwako. Ikiwa upo tayari kufanya hivyo leo. Basi fungua hapa kwa ajili ya kuongozwa sala ya Toba>> KUONGOZWA SALA YA TOBA

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

kwanini Yakobo amefananishwa na mdudu?(Isa 42:14)

Kwanini biblia inaitaja mara kwa mara dhahabu ya Ofiri?

DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.

Njuga ni nini (Isaya 3:16, Zekaria 14:20)?

Bwana Yesu alimaanisha nini kusema “Saa yangu haijawadia?”

Ni nani aliyesema “Nitume mimi”? katika (Isaya 6:8)

Rudi nyumbani

Print this post