MAPEPO YANATAFUTA HIFADHI NDANI YAKO KWA BIDII SANA.

MAPEPO YANATAFUTA HIFADHI NDANI YAKO KWA BIDII SANA.

Jina la Bwana wetu Yesu libarikiwe, karibu tujifunze biblia.

Je umewahi kujiuliza, mapepo yanapomtoka mtu yanakwenda wapi?..Je yanakufa au yanakwenda kuzimu?. Jibu ni kwamba idadi kubwa ya mapepo yanapomtoka mtu yanakwenda kutafuta kumwingia mtu mwingine, au yanarudi kutafuta kuingia pale yalipotoka kama mtu yule atakuwa hajajitakasa. Bwana wetu Yesu alitupa ufunuo huo..

Mathayo 12.43  “Pepo mchafu, amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika, asipate.

44  Halafu husema, Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka; hata akija, aiona tupu, imefagiwa, na kupambwa.

45  Mara huenda, akachukua pamoja naye pepo wengine saba walio waovu kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza….”.

Kwahiyo mapepo hayafi, bali yanapomtoka mtu yanarudi kwenye mzunguko. (Kama tu fedha inavyozunguka, inapotoka kwako haiendi kuchomwa wala kutupwa, bali inaenda kwa mwingine, na baadaye kurudia tena kwako kama umestahili kuipata).

 Sasa ni muhimu kufahamu kuwa mapepo yapo kwenye mizunguko kila siku. Na ni muhimu pia kufahamu kuwa mapepo, pamoja na shetani wanaomba mbele za Mungu, (yaani wanapeleka hoja za maombi), na katika hayo mengine wanakubaliwa, na kufanyiwa kama walivyoomba. Ndio maana kuna umakini sana wa kuzidi kujitakasa, kwasababu biblia inasema shetani ni mshitaki wetu, maana yake anapeleka habari zetu mbele za Mungu, na katikati ya hizo habari anaingiza na maombi yake kututaka sisi.

Utaona alifanya hivyo kwa Ayubu, na alifanya hivyo kwa mfalme Ahabu..

1Wafalme 22: 19 “Mikaya akasema, Sikia basi neno la Bwana; Nalimwona Bwana ameketi katika kiti chake cha enzi, na jeshi lote la mbinguni wamesimama upande wa mkono wake wa kuume na wa kushoto.

20 Bwana akasema, Ni nani atakayemdanganya Ahabu, ili akwee Ramoth-Gileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi.

 21 Akatoka pepo, akasimama mbele za Bwana, akasema, Mimi nitamdanganya.

22 Bwana akamwambia, Jinsi gani? Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo kinywani mwa manabii wake wote. Akasema, Utamdanganya, na kudiriki pia; ondoka ukafanye hivyo.

23 Basi angalia, Bwana ametia pepo wa uongo kinywani mwa manabii wako hawa wote; naye Bwana amenena mabaya juu yako”.

Hivyo mapepo yanaomba kama sisi tunavyoomba, na kama yamestahili, yanapewa haki yao kama sisi tunavyopewa. Kwasababu Mungu ni mwenye haki, kila kiumbe alichokiumba anakipa kulingana na kinachostahili.. Kwamfano kama mtu ambaye hamtaki Mungu kabisa wala kumpenda ijapokuwa anajua yupo, lakini kamchagua shetani na kumwabudu, akiwa na akili zake timamu kabisa, mtu huyo ni milki ya halali ya shetani, ni haki ya shetani kuwa naye, hivyo ni haki ya shetani kumfanya lolote.

Sasa kwa mtu ambaye hajajitakasa, mapepo yanayozagaa huko na huko, yanaomba kwa Mungu kibali cha kumwingia, na zinapokosekana kabisa sababu za mtu huyo kuepushwa na mapepo hayo, ndipo mapepo hayo yanashinda hoja na hatimaye yanapewa ruhusa ya kumwingia .(Hivyo ndivyo watu wanavyoingiliwa na mapepo).

Kwamfano mtu ambaye ni mwasherati sana, tayari katika ulimwengu wa roho, idadi kubwa sana ya mapepo yameshatuma maombi ya kumwingia mtu huyo, lakini yanajaribu kuzuiliwa kwa muda, ili mtu Yule angalau atumiwe wahubiri wawili watatu watakaomwonya aache njia yake mbaya, lakini hasikii, siku zinasogea.. Bila kujua kuwa yupo kwenye hatari kubwa, lakini anaendelea hivyo hivyo, mwishowe yale mapepo yanashinda hoja na kupewa haki yao, ndio hapo yanaruhusiwa kumwingia huyo mtu.

Matokeo ya mapepo hayo kumwingia mtu ni aidha kumsababishia mauti ya ghafla ya mwilini na rohoni, na mikosi na magonjwa yasiyo na tiba mfano HIV, (na wengi hawafahamu kuwa wanaopata ugonjwa kama wa Ukimwi wala hawajaambukizwa na mtu mwenye ugonjwa huo. Wengi ni unaanzia tu kwao, kwasababu lile ni pepo, kama vile lilivyomwingia mtu wa kwanza kupata ugonjwa huo, ndivyo linavyomwingia mtu yeyote sasahivi,  aliye mwasherati, sio lazima uambukizwe kutoka kwa mtu mwenye huo ugonjwa). Hiyo ni kutokana na mapepo hayo yameshinda hoja juu yako, kwasababu ya maisha anayoishi yasiyompendeza Mungu.

Unaweza kuuliza ni wapi tena maroho hayo yalionekana kumwomba Mungu…Tusome.

Mathayo 8.28  “Naye alipofika ng’ambo, katika nchi ya Wagerasi, watu wawili wenye pepo walikutana naye, wanatoka makaburini, wakali mno, hata mtu asiweze kuipitia njia ile.

29  Na tazama, wakapiga kelele, wakisema, Tuna nini nawe, Mwana wa Mungu? Je! Umekuja kututesa kabla ya muhula wetu?

30  Basi, kulikuwako mbali nao kundi la nguruwe wengi wakilisha.

31  Wale pepo wakamsihi, wakisema, Ukitutoa, tuache twende, tukaingie katika lile kundi la nguruwe.

32  Akawaambia, Nendeni. Wakatoka, wakaingia katika nguruwe; na kumbe! Kundi lote wakatelemka kwa kasi gengeni hata baharini, wakafa majini”.

Hapo mapepo yanamwomba Bwana, na tena yanamsihi yasiende shimoni, bali yaende kwa nguruwe wale…Yalikuwa na sababu zote kwanini yaombe vile.

Na hata leo ni hivyo hivyo, wewe ni muasherati mapepo yanaomba ruhusa juu yako, na hata pengine yamesharuhusiwa bila wewe kujua, hayo yatakuongoza baharini kukuua kama yalivyofanya kwa wale nguruwe.

Umekuwa mtu wa vinyongo, na kutokusamehe, tayari umefungua mlango wa mapepo kukuvamia na kukuharibu..Umekuwa mwabudu sanamu na mchawi wewe tayari ni ngome ya adui.

Umekuwa mtu wa kuvaa kizinzi, na moyoni unajua kabisa mavazi kama hayo hata ukiitwa kwenye interview ya kazi huwezi kwenda nayo, lakini unaendelea kuyavaa na kukatisha nayo mtaani na hata kuingia nayo kanisani, fahamu kuwa wewe ni kituo cha mapepo.

Lakini leo umesikia neno hili, fungua moyo wako tubu, mwambie Bwana sitaki kuwa kituo cha mapepo, bali unataka kuwa kituo cha Roho Mtakatifu ndani yako. Na kama umedhamiria kutubu kabisa, unachopaswa kufanya baada ya toba hiyo ni kugeuka kikweli kweli, kama kulikuwa na watu hujawasamehe moyoni mwako kutokana na sababu Fulani Fulani, kuanzia dakika hii unawasamehe wote, haijalishi wamefanya kosa gani, kwasababu hata sisi Kristo alitusamehe.

Pia kama ulikuwa ni mzinzi na mwasherati, kuanzia dakika hii unakiri kuuacha kwa vitendo, maana yake Yule uliyekuwa unafanya naye uzinzi, unakata mawasiliano naye, na pia kama ulikuwa unavaa nguo za kizinzi unachoma, wala usiende kuzigawa, unazichoma zote usiache hata moja, na kama ulikuwa unatazama picha za pornograph na unasikiliza miziki ya kidunia katika simu yako unafuta yote kuanzia saa hii, wala usingoje kesho, kwasababu hujui yatakayozalika ndani ya siku moja, biblia inasema hivyo.

Na baada ya kufanya hayo na mengine yote yanayofanana na hayo, hapo toba yako itakuwa ni ya matendo, hivyo Roho Mtakatifu atashuka ndani yako kuhakikisha uyarudii matapishi na kuithibitisha imani yako, na hata kama kulikuwa ndani yako kuna mapepo, yataondoka yenyewe kwasababu Toba inayoambatana na matendo ina nguvu ya kufungua minyororo kuliko kitu kingine chochote, wala huhitaji kukemewa mapepo tena, (Toba ya namna hiyo hakuna pepo litakalosalia), ulichobakisha ni wewe kwenda kutafuta ubatizo sahihi wa maji tele (Yohana 3:23), na kwa Jina la Yesu Kristo kuukamilisha wokovu wako, kama bado hujabatizwa hivyo.

Na kuanzia hapo hakuna hoja yeyote ya shetani itakayoshinda juu yako, na mapepo yatawekwa mbali na wewe, na utaishi maisha yasiyo na usumbufu wowote kutoka kwa adui.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

SI MAPEPO YOTE NI YA KULIPUKA.

ONDOKA YESU, TUACHIE MAPEPO.

Je! ile habari ya watu wawili wenye pepo inajichanganya?

ZIFAHAMU HOJA SABA ZENYE NGUVU MBELE ZA MUNGU.

IFAHAMU HUZUNI NA FURAHA YA MALAIKA.

Rudi nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments