Monthly Archive Febuari 2021

Je kwa mkristo aliyeokoka, ni dhambi kunyoa ndevu zake?

SWALI: Je kwa mkristo aliyeokoka, ni dhambi kunyoa ndevu zake kulingana na huu mstari?

Walawi 19:26 “Msile kitu cho chote pamoja na damu yake; wala msifanye kuloga, wala kutumia utambuzi.

27 MSINYOE DENGE PEMBE ZA VICHWANI, WALA MSIHARIBU PEMBE ZA NDEVU ZENU.

28 Msichanje chale yo yote katika nyama ya miili yenu kwa ajili ya wafu, wala msiandike alama miilini mwenu; mimi ndimi Bwana.

29 Usimnajisi binti yako, ili kumfanya awe kahaba; isiwe hiyo nchi kuuandama ukahaba, na nchi kujawa na uovu mkuu”.

JIBU: Wana wa Israeli wakiwa jangwani Mungu aliwapa maagizo hayo, ya kutokunyoa ndege(para) kwenye pembe za vichwa vyao, na wala wasichonge ndevu (kwa pembeni) wanyoapo.

Sasa Mungu kuwapa maagizo hayo, haikuwa kwasababu wataonekana na mwonekano tofauti, hapana bali mitindo hiyo ilikuwa ni inamaana kubwa Zaidi kwa watu wale, kwani ziliwakilisha ibada za miungu yao ya kipagani na ushirikina.  Wakati ule wamisri na waarabu waliokuwa wanaishi majangwani, walikuwa wananyolewa nywele zote za pembeni na kuachwa na KIDUKU cha mvuringo hapo juu, na wengine walikuwa wananyoa para kabisa,(Isaya 15:2, Yeremia 48:37) walifanya hivyo  kwa heshima ya miungu yao. Vilevile na kuchongwa kwa pembe za ndevu zao, kwa lengo hilo hilo.

Sasa Ili Mungu kuwatofautisha watu wake na mionekano ya kipagani, akawazuia wasifanye vile kama wao. Mungu alilichagua taifa la Israeli liwe takatifu, lijulikane kama ni taifa la Yehova, sio taifa ambalo watu akilitazama waone desturi za miungu ya kipagani ndani yao. Na ndio maana utaona mpaka “chale” alikataza wasichanjwe, mpaka michoro ya mwilini (Tatoo) wasichore, kwasababu zote hizo zilikuwa ni desturi za wachawi na miungu ya kipagani.

Kama vile wafanyavyo wachina leo hii, utawaona wamenyoa vichwa vyao vyote, na kuacha kifuniko kidogo cha nywele hapo juu, sio kwamba ni fashion hapana, bali ni wanatangaza desturi za miungu yao.

Hata leo hii, Ni ajabu sana kumuona mkristo ananyoa KIDUKU, wala hata hajui asili yake ni nini au anatangaza nini.. Na hata kama hana nia ya kutangaza upagani, lakini pia hajui kuwa Mungu ametuita kujitofautisha na watu wa ulimwenguni, kama alivyofanya kwa waisraeli.

kunyoa kiduku

Unaponyoa kiduku, halafu ni mkristo, unatoa nuru gani kwa jamii inayokuzunguka.  Ni wazi kuwa unatangaza usanii wa wanamiziki, unapovaa nguo iliyochanika chanika magotini, unatangaza nini?.. Unapofuga rasta, unamtangaza Mungu gani hapo, wewe kama mkristo unatangaza nini..? Kumbuka sisi ni barua tunayosomwa na watu wote.

Pia upo unyoaji wa ndevu wa kisasa ambao unaweza ukawa hauna maana ya ibada ya kipagani, lakini staili ya unyoaji wake zikakutambulisha wewe ni nani, kama utanyoa ndevu kwengine kote  halafu hapo katikati  unaziacha zirefuke ziwe kama za mbuzi, au unanyoa kisha unaziwekea mitindo mitindo uonekane kama msanii Fulani kwenye tv, wewe kama mkristo unapaswa ujue bado ni rafiki wa dunia. Na sio wa Mungu.

Hivyo kama wewe ni mnyoaji wa viduku, au wa hizo staili ni heri ukaacha, kwasababu Mungu hapendezwi ni mkristo wa namna hiyo.

Warumi 12:1 “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana.

2 Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu”.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Je kuweka mapambo kama mikufu, vikuku na kutoboa pua ni dhambi?

Kikuku/vikuku ni nini katika biblia?

Nini maana ya ombeni kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi wala siku ya sabato?.

UFUNUO: Mlango wa 15

Swali: Je Ni sahihi kwa Mkristo kupeleka kesi mahakamani?

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 9 (Kitabu cha Ayubu).

Rudi nyumbani

Print this post

Nini maana ya ombeni kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi wala siku ya sabato?.

Jibu: Ili tupate kuelewa vizuri, tutaisoma habari hii hii katika vitabu vitatu tofauti vya Injili. Tukianza na kitabu cha Mathayo, biblia inasema…

Mathayo 24:15  “Basi hapo mtakapoliona chukizo la uharibifu, lile lililonenwa na nabii Danieli, limesimama katika patakatifu (asomaye na afahamu),

16  ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani;

17  naye aliye juu ya dari asishuke kuvichukua vitu vilivyomo nyumbani mwake;

18  wala aliye shambani asirudi nyuma kuichukua nguo yake.

19  Ole wao wenye mimba na wanyonyeshao siku hizo!

20  OMBENI, ILI KUKIMBIA KWENU KUSIWE WAKATI WA BARIDI, WALA SIKU YA SABATO.

21  KWA KUWA WAKATI HUO KUTAKUWAPO DHIKI KUBWA, AMBAYO HAIJATOKEA NAMNA YAKE TANGU MWANZO WA ULIMWENGU HATA SASA, WALA HAITAKUWAPO KAMWE.

22  Na kama siku hizo zisingalifupizwa, asingeokoka mtu ye yote; lakini kwa ajili ya wateule zitafupizwa siku hizo”.

Habari hii inazungumzia unabii wa Kuanguka kwa mji wa Yerusalemu, Baada ya wayahudi kumkataa Bwana Yesu. Yesu mwenyewe aliwaambia, kuwa utafika wakati, ambao Mungu atawaadhibu kwa kuikataa hiyo neema, tena akawaambia siku hizo zipo karibu kutokea ambapo, maadui zao (Yaani Warumi ambao wanawatawala sasa), watakapowazunguka pande zote na kuubomoa mji wao pamoja na hekalu, na kuwatawanya baadhi yao huko na huko, kama wakati wa uhamisho wa Babeli, na hayo yote ni kutokana na wao kumkataa Masihi, hivyo ile neema ya ulinzi kutoka kwa Mungu itaondoka juu yao, na adui atawavamia na kuwaharibu…

Habari hiyo tunaisoma katika kitabu cha Luka..

Luka 19:41  “Alipofika karibu aliuona mji, akaulilia,

42  akisema, Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako.

43  Kwa kuwa siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande zote;

44  watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako”.

Sasa Bwana alipoutoa huo unabii, watu waliokuwa wanamdharau na kumkataa hususani viongozi wa dini, Mafarisayo na Masadukayo, waliyapuuzia maneno hayo, na kumwona kama amerukwa na akili. Lakini wanafunzi wa Yesu walijua kabisa kuwa maneno ya Yesu hayatapita, jambo hilo lazima litimie, ndipo wakamfuata wakamwuliza ni lini hayo mambo yatatokea?. Ndipo Bwana akawaambia…

Luka 21:20 “… hapo mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, ndipo jueni ya kwamba uharibifu wake umekaribia.

21  Ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani, na walio katikati yake wakimbilie nje, na walio katika mashamba wasiuingie.

22  Kwa kuwa siku hizo ndizo za mapatilizo, ili yatimizwe yote yaliyoandikwa.

23  Ole wao wenye mimba na wanaonyonyesha katika siku hizo! Kwa kuwa kutakuwa na shida nyingi katika nchi, na hasira juu ya taifa hili.

24  Wataanguka kwa ukali wa upanga, nao watatekwa nyara na kuchukuliwa katika mataifa yote; na Yerusalemu utakanyagwa na Mataifa, hata majira ya Mataifa yatakapotimia”.

Hapo sasa Bwana Yesu anazungumza na wanafunzi wake  tu, na si watu wote..hapana! bali wanafunzi wake tu, anawaambia jinsi mambo yatakavyokuwa na anawaambia jinsi ya kuepukana na hiyo siku ya mapatilizo.. Anawaambia watakapoona tu mji wa Yerusalemu umezungukwa na Majeshi..basi watambue kwamba ile ule unabii aliowaambia ya kwamba Yerusalemu itateketezwa umekaribi kutimia…

Sasa anaendelea kuwaambia wanafunzi kwamba watakapoona hayo majeshi, wasingoje chochote, waondoke mji wa Yerusalemu wasije na wao wakaangamia huko kwasababu ni siku ya kisasi cha Mungu. Hivyo waondoke wasafiri waende mji mwingine..wakakae huko..

Na pia waombe kuwa siku hizo za kuondoka zisitokee msimu wa Baridi wala siku ya Sabato..

Sasa kwanini siku ya Baridi na sabato?

Maeneo ya Yerusalemu miezi ya Machi na Aprili, kunakuwa na baridi sana, wakati mwingine mpaka kutengeneza barafu, sasa kwa ufahamu wa kawaida tu, kusafiri na punda kwenye barafu au wakati wa joto ipi bora?..bila shaka ni heri kusafiri kipindi cha joto kuliko cha barafu.. Hiyo ndio maana Bwana Yesu akasema waombe hayo yasitokee msimu wa baridi.

Lakini sio hilo tu! Akawaambia pia waombe yasitokee siku ya Sabato?

Sasa kwanini siku ya sabato?…Je Bwana Yesu alikuwa anamaanisha watu waishike sabato?. Jibu ni la.. Kumbuka wayahudi walikuwa wanashika sheria ya Musa, na pia siku ya sabato watu walikuwa hawaruhusiwi kufanya kazi, wala kutembea umbali mrefu…kulikuwa ni kipimo kidogo tu cha mwendo kwa siku, ambacho mtu hapaswi kukizidisha hicho katika siku ya sabato. Kipimo hicho kilikuwa kinaitwa “MWENDO WA SABATO”.

Matendo 1:12 “Kisha wakarudi kwenda Yerusalemu kutoka mlima ulioitwa wa Mizeituni, ulio karibu na Yerusalemu, wapata mwendo wa sabato”.

Ulikuwa ni mita kadhaa tu, Hivyo haikuruhusiwa mtu yeyote kutoka kusafiri, au kwenda kuzurula zurura. Na ilikuwa ni sheria mtu yeyote akionekana anafanya kazi siku hiyo au anatembea tembea hovyo ilikuwa ni kifo. (Unaweza kusoma sheria hiyo ya kutembe vizuri katika kile kitabu cha Kutoka 16:25-30) /www wingulamashahidi org/

Sasa hebu jiulize katika mazingira kama hayo, (yaani siku ya sabato), ndio majeshi yamezunguka Yerusalemu, ambapo ndio wakati wa kuondoka…utawezaje kuondoka?? Maana nchi hairuhusu mtu kusafiri, maana yake utajikuta unakaa huko huko mjini mpaka maangamizi yanakukuta. Ndio maana Bwana akawaambia “waombe kwamba siku hizo za kukimbia zisitokee msimu wa baridi, wala siku ya sabato”. Kwasababu kama zikitokea katika mojawapo ya mazingira hayo, basi dhiki yake itakuwa ni kubwa sana, ambayo haina mfano wake. Na watakaoathirika wa kwanza ni wanawake, tena hususani wale wenye mimba, au wanaonyonyesha…Hebu jiulize tena, mwanamke mjamzito au mwenye kichanga mkononi, ambacho muda wote kinahitaji malezi na joto la mama,  atakimbiaje kwenye baridi na katika mazingira ya mji kuzuiliwa watu kusafiri??..umeona jinsi ilivyo ngumu, ndio maana Bwana akawaambia ole wao wenye mimba, na wanyonyeshao.

Sasa baada ya Bwana Yesu kuwaambia maneno hayo ya unabii, pamoja na maneno mengine mengi…Bwana Yesu siku za kupaa kwake zilifika na aliondoka, lakini wanafunzi wakabaki na ufahamu vichwani mwao, kwamba siku si nyingi Yerusalemu itakuja kuzungukwa na majeshi, na huo ndio wakati wa sisi kuondoka..tusingoje..

Miaka 37 baada ya Bwana Yesu kuondoka, Unabii huo ulitimia.. yaani mwaka AD 70, Wakati ambapo Yerusalemu kunaonekana kuna amani, majeshi ya Warumi yalianza kuizunguka Yerusalemu wakiwa na silaha, watu wakajua ni jambo la kawaida tu, suluhisho la amani kwa mazungumzo litapatikana, pengine wakatokea watu wa kutabiri kutakuwa na amani, hakuna shida, hakuna haja ya hofu, kwasababu wakati huo Rumi ndio uliyokuwa inatawala dunia.

Lakini Mitume wa Yesu baadhi ambao bado walikuwa wanaishi, waliowaonya wakristo juu ya unabii huo wa Bwana, hivyo miongoni mwa wakristo, tukio hilo lilipotokea hawakusubiri wala kupoteza muda.. Wengi wao waliondoka Yerusalemu.. Na kukimbilia nchi za kando kando…waliyakumbuka yale maneno ya Bwana aliyosema.. “hapo mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, ndipo jueni ya kwamba uharibifu wake umekaribia  Ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani, na walio katikati yake wakimbilie nje, na walio katika mashamba wasiuingie”. Hivyo wakristo waliokuwa na shughuli zao, huko waliziacha na kuondoka Yerusalemu kipindi hicho hicho, ingawa walionekana wendawazimu.

Lakini hao wengine wasioujua unabii  waliendelea kubaki wakijua hayo majeshi yataondoka tu…wengine wakawa wanaendelea na shughuli zao za kiuchumi, huku mazungumzo ya amani yanaendelea…siku chache mbele, mambo yakabadilika, yale majeshi yaliyokuwa yametulia tu mipakani, yakaingia Yerusalemu kama maji, yakaua watu wengi, na yakaangusha majengo yote ikiwemo hekalu, wala halikubakia jiwe juu ya jiwe, kama Bwana Yesu alivyotabiri, waliosalimika ni wale walioondoka tu. Na hayo yote biblia inasema yaliwapata kwasababu hawakutambua majira ya kujiliwa kwao.

Ndugu huo ni mfano wa dhiki kuu halisi ambayo inakuja huko mbeleni, Dhiki kuu yenyewe ipo karibu kutokea, itaanza ghafla tu, wakati kama huu ambao watu wanasema kuna amani na utulivu…ambapo baada ya unyakuo kupita watakatifu watakapoondolewa duniani, wale waliobaki, ambao wataikataa ile chapa, watateswa kwa mateso yasiyo ya kawaida, na baada ya kuteswa kwa miaka kadhaa bila kuruhusiwa kufa ndipo watakufa..

Hivyo unyakuo sio wa kukosa kabisa… na maneno ya Bwana Yesu kamwe hayapiti. Alisema Yerusalemu itazungukwa na maadui na hakuna jiwe litasalia juu ya jiwe..jambo hilo limetimia… Na maneno mengine yote aliyoyasema ni lazima yatatimia, hakuna ambalo halitatimia.

Marko 13:31 “Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe”

Je umempokea Kristo?..Je una uhakika hata parapanda ikilia leo utanyakuliwa?..Kama huna uhakika basi huo tayari ni uthibitisho kwamba hutaenda, kwahiyo ni vyema ukatafuta uhakika kuanzia leo kwa kuyatengeneza maisha yako katika Yesu.

Bwana akubariki

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

IMESALIA RAHA YA SABATO KWA WATU WA MUNGU.

NYAYO TUNAZOPASWA KUZIFUATA.

NITAFANYA YERUSALEMU KUWA JIWE LA KUWALEMEA .

CHUKIZO LA UHARIBIFU

DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.

Rudi nyumbani

Print this post

Nini maana ya tumeumbwa kwa mfano na sura ya Mungu?

Swali: Biblia inasema tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, maana yake nini?

Jibu: Tusome.

Mwanzo 1:26 “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.

 27 Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba”.

Mfano wa Mungu, ni UTU WA NDANI, yaani vitu vyote vinavyopatikana ndani ya roho na nafsi ya mwanadamu, kama vile Furaha,upendo, amani, hasira, wivu, ghadhabu, huruma n.k. Huo ndio mfano wa Mungu, ndio maana utaona kama Mungu alivyo na hasira, mwanadamu naye ana hasira, kama Mungu alivyo na wivu, mwanadamu naye ana wivu, kama Mungu anavyotawala, mwanadamu naye anatawala n.k.. Hiyo yote ni kwasababu kaumbwa kwa mfano wa Mungu. Ndio maana biblia pia inawataja wateule wa Mungu kama miungu.

Yohana 10:34  “Yesu akawajibu, Je! Haikuandikwa katika torati yenu ya kwamba, Mimi nimesema, Ndinyi miungu?. Ikiwa aliwaita miungu wale waliojiliwa na neno la Mungu; (na maandiko hayawezi kutanguka)”.

Lakini sura ya Mungu ni utu wa nje… yaani mwonekano wa nje kama macho, pua, mdomo, mikono, miguu, masikio n.k. Kwaufupi umbile la miili yetu ni nakala ya umbile la Mungu. Hii miili haikubuniwa tu, na tukapewa sisi, hapana!. Bali Mungu aliinakili kutoka katika umbo lake mwenyewe na mwonekano wake.

Na hilo umbo akalitengeneza kwa malighafi ya nyama, ndio likawa sisi… Lakini la kwake limetengenezwa kwa malighafi gani? Hakuna anayejua, lakini linafanana kimwonekano na miili yetu.

Ni sawa na ile midoli ya plastiki, inayoning’inizwa masokoni, ile imetengenezwa kwa sura ya mwanadamu…mwili wa mdoli ule ni malighafi yake ni  plastiki na wa mwanadamu ni wa nyama, lakini kimwonekano inafanana, ingawa mwanadamu si mdoli.. Kadhalika na sisi tunafanana na Mungu kimwonekano, lakini malighafi iliyounda umbo lake hilo la kiroho, hakuna anayejua.

Kwahiyo sisi tumeumbwa kwa mfano kamili wa Mungu, Ndio maana sehemu nyingi Mungu anahubiri tufanane na yeye katika utu wetu wa ndani…kwasababu inawezekana kabisa sisi kufanana na yeye kwamaana katuumba kwa mfano wake. Kama yeye ni mwenye upendo, na sisi anataka tuwe na upendo wakati wote kama yeye, kwasababu, katuumba kwa mfano wake. Hawezi kututwika mzigo mzito ambao anajua hatutaweza kuubeba.. Kwahiyo alivyotuambia kwamba tuwe na upendo, na wakamilifu, anajua kabisa jambo hilo linawezekana kwetu, kwasababu sisi ni kama yeye..

Mathayo 5:48  “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu”

Wanyama hawajaumbwa kwa mfano wa Mungu ndio maana hawajaamriwa tuliyoamriwa sisi, kwasababu pengine yangekuwa ni juu ya uwezo wao,. Lakini sisi, mema yote yapo chini ya uwezo wetu endapo tukiamua… “Kuwa wakamilifu duniani na kufanana na Mungu inawezekana kwa asilimia zote”.(Zaburi 16:3).

Na hatuamui kwa midomo tu bali kwa vitendo, pale tunapotubu  na kumpokea Roho Mtakatifu, hapo unashuka uwezo juu yetu wa kutugeuza kuwa kama Mungu,.. Ulikuwa unamchukia ndugu yako, sasa hiyo chuki inahama, badala ya kumchukia ndugu yako unakuwa unachukia dhambi, hivyo unakuwa kama Mungu. N.k

Bwana azidi kutubariki sote.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Nini maana ya ‘Maandalio ya moyo ni ya mwanadamu’ ?

Nguo za magunia katika biblia ni zipi?

Kikuku/vikuku ni nini katika biblia?

Nini maana ya “yasiyokuwapo hayahesabiki”(Mh 1:15)

THAWABU ZA SIRI, ZA WATAKATIFU MBINGUNI.

Rudi nyumbani

Print this post

Je watu ambao hawajasikia kabisa injili watahukumiwa?

SWALI: Watu ambao hawajasikia kabisa injili, halafu wakafa katika kutokujua chochote kuhusu Yesu, je wao huhesabika kuwa hawana dhambi? Kufuatana na andiko hili?

Yohana 15:22 “Kama nisingalikuja na kusema nao, wasingalikuwa na dhambi; lakini sasa hawana udhuru kwa dhambi yao”.


JIBU: Yesu hakumaanisha kuwa mtu yoyote ambaye hakusikia habari zake, kuwa hatahukumiwa kabisa hapana, bali alimaanisha kuwa watu wa namna hiyo hawatahukumiwa kwa maneno yake, bali watahukumiwa kwa kitu kingine..

Na ndio maana biblia inasema..

Warumi 2:11 “kwa maana hakuna upendeleo kwa Mungu.

12 Kwa kuwa wote waliokosa pasipo sheria watapotea pasipo sheria, na wote waliokosa, wenye sheria, watahukumiwa kwa sheria”.

Unaona hapo anasema,..”waliokosa” pasipo sheria “watapotea” pasipo sheria, hasemi wataokolewa pasipo sheria, hapana bali watapotea..kwasababu walikosa katika mambo mengine, na ndio katika hayo hayo Mungu atawahukumia, lakini hatatumia ile sheria ya torati kuwahukumu, kwasababu hiyo hawakuijua hapo kwanza.

Ni vizuri tukafahamu kuwa kuna mambo ya asili ambayo Mungu kayaweka mioyoni mwa wanadamu wote, kiasi kwamba hata kama hajawahi kusikia sheria imekataza kuua, wao wenyewe hawataua, kwasababu wanajua ni makosa..Ukienda kwenye jamii za watu ambao wanaishi maporini hawajui utandawazi ni nini, hawajafikiwa na chochote, bado utawakuta  na ustaarabu wao wa maisha na utakuta wamejiwekea mipaka ambayo wanajua kabisa yoyote atakayeivuka ni makosa.

Wanajua kabisa mwanaume kulala na mwanaume mwenzake ni makosa, wanajua, kuiba mali ya mwingine sio sawa, wanajua, kuwapiga wazazi wao ni vibaya, n.k.…hayo mambo hawahitaji kufundishwa na Mungu au mtu yeyote, ni sheria ambayo tayari ipo ndani ya mioyo yao.

Ukisoma tena sehemu nyingine utaona Bwana YESU anasema..

Luka 12:47 “Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana.

48 Na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo”.

Unaona tena, anasema yeye asiyejua, lakini amefanya yastahiliyo mapigo atapigwa kidogo.. Kwahiyo, hakuna mwanadamu yoyote ambaye hataingia hukumuni, wote wataingia.

Lakini mbaya Zaidi itakuwa kwetu sisi ambao tumeshasikia habari za Kristo, lakini hatuzitendei kazi, tumeshasikia habari za wokovu wa msalaba lakini tunazipuuzia, sasa sisi tutahukumiwa kwa injili yake. Na adhabu yetu itakuwa ni kubwa sana, kuliko za watu ambao hawajawahi  kabisa kusikia habari za Yesu.

Hivyo tuikwepe hukumu ya Mungu. Inatisha.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Hamjui ya kuwa mtawahukumu malaika? Ina maana gani?

 Nini maana ya “Uchungu wa mauti ni dhambi, na nguvu za dhambi ni torati”

Maashera na Maashtorethi ni nini?

TAZAMA, NASIMAMA MLANGONI.

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 6

Je! Kusoma biblia kwenye simu ukiwa kanisani ni dhambi?

Rudi nyumbani

Print this post

MWEKE SHETANI MBALI NA WEWE.

Shetani anaweza kuwekwa mbali nasi au akaondoka mbele yetu kwa namna kuu tatu.

  1. Ya kwanza ni kwa kumfukuza
  2. Ya pili ni kwa kuseta chini ya miguu yetu
  3. Na Ya tatu ni ya kumfanya yeye mwenyewe atukimbie.

1) Kumfukuza ni kwa kumkemea:

Wakati mwingine shetani anatukaribia sana ili kutujaribu tuanguke katika dhambi. Na tusipokuwa makini atafanikiwa hivyo pindi tunapojikuta katika mazingira kama hayo hatua inayofuata ni kumfukuza kwa kumkemea kwa vinywa vyetu.

Bwana Yesu alimfukuza shetani mara nyingi, utaona kule jangwani, alimfukuza, akamwambia “Nenda zako shetani” Neno hilo linamaanisha ondoka hapa, ni sawa na kufukuzwa.. ndipo akamwacha baada ya kukemewa mfano asingemfukuza angefululiza kumjaribu tu pale..

Mathayo 4:8 “Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mlima mrefu mno, akamwonyesha milki zote za ulimwengu, na fahari yake,

9 akamwambia, Haya yote nitakupa, ukianguka kunisujudia.

10 Ndipo Yesu alipomwambia, Nenda zako, Shetani; kwa maana imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake

11 Kisha Ibilisi akamwacha; na tazama, wakaja malaika wakamtumikia.”.

Wakati mwingine alikuwa na Petro, shetani naye akamvaa ili alipindishe kusudi la Mungu juu yake.. Lakini  utaona Bwana Yesu wakati ule ule alimkemea na kumwambia nenda nyuma yangu shetani kwani huyawazi yaliyo ya Mungu bali ya wanadamu.

Mathayo 16:22 “Petro akamchukua, akaanza kumkemea, akisema, Hasha, Bwana, hayo hayatakupata.

23 Akageuka, akamwambia Petro, Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu”.

Hata sisi, shetani anaweza kutusogelea kwa njia mbalimbali, hivyo hatuna budi kutumia vinywa vyetu kumkemea, pale pale. Wewe ni dada unaona mwanaume anakutongoza, anaanza kuzungumza na wewe mazungumzo ya kizinzi, hapo hapo unapaswa umkemee, lakini ukimwamwacha ataendelea hivyo hivyo na mwisho wa siku atakuvaa moja kwa moja kama alivyomvaa Yuda wakati ule. Na kitakachokuwa kimebakia kwako ni kujiua kiroho, kama sio kimwili kabisa.

Hivyo lazima tutumie vinywa vyetu kumfukuza shetani, tunapomwona anatusogelea sogelea, Kama vile tunavyotoa pepo, Kama alivyofanya Bwana.

2) Pili, ni kwa kumseta chini ya miguu yetu.

Njia hii ni tofauti kidogo na ile ya kwanza hapa, hutumii mdomo tena, bali unatumia matendo Zaidi.. Biblia inasema..

Warumi 16:19 “Maana utii wenu umewafikilia watu wote; basi nafurahi kwa ajili yenu, lakini nataka ninyi kuwa wenye hekima katika mambo mema, na wajinga katika mambo mabaya.

20 Naye Mungu wa amani atamseta Shetani chini ya miguu yenu upesi. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja nanyi. [Amina.]

Unaona, unapokuwa mjinga katika kutenda mambo maovu, na mwenye hekima katika kutenda mambo mema, kidogo kidogo, unazipunguza nguvu za ibilisi kwa kiwango kikubwa sana juu yako, na baadaye Mungu anamseta chini ya miguu yako mara moja, kama tunavyojua kitu kikisha kaa chini ya miguu yako, hakina nguvu tena, hakina ujanja wowote, kimeshindwa…Unaweza kukifanya vyovyote vile unavyotaka

Vivyo hivyo na sisi tukiwa watu wa namna hiyo, kamwe shetani hatokaa atuweze, Kwa urefu wa somo hilo tutumie ujumbe inbox, tukutumie. Wakati mwingine shetani anakuwa mgumu kwetu kumshinda, kwasababu ya mienendo yetu isiyompendeza Mungu. Tunakuwa wepesi kukimbilia mambo maovu,  na mambo ya Mungu tunakuwa wazito. Tukisikia kuna thamthilia Fulani imetoka, au series, tunakuwa wakwanza kuzifuatilia, lakini tu kufuatilia mafundisho ya biblia hilo hatuna muda nalo.. Kwa namna hiyo shetani atatusumbua sana.

Jaribu kuyaelekeza maisha yako kwa Mungu muda mrefu, utaona jinsi gani shetani anavyokuwa mwepesi kumshinda na hila zake, ni kwasababu tayari Mungu anakuwa ameshamseta chini ya miguu yako, hana nguvu yoyote ya kukushinda.

3) Na njia ya tatu ni ya kumfanya yeye mwenyewe kukimbia:

Hii ni ndo njia kuu, ukishaona mpaka adui yako anakukimbia kila akikuona anakula kona, basi ujue huo ni Zaidi ya ushindi, na kila utakapokwenda, yeye ndo anahama hapo kabla hujafika na sio wewe.. Sasa hapa ndipo tunapopaswa tupafikie watu wote.

Yakobo 4:6 “Lakini hutujalia sisi neema iliyozidi; kwa hiyo husema, Mungu huwapinga wajikuzao, bali huwapa neema wanyenyekevu.

7 BASI MTIINI MUNGU. MPINGENI SHETANI, NAYE ATAWAKIMBIA”.

Unaona, ukimtii Mungu, ukinyenyekea chini ya Mungu, ukayashika maagizo yake, ukawa unazikataa kazi za shetani, Hapo hakuna kingine cha ziada Zaidi ya shetani mwenyewe kutafuta mahali pengine..

Anakukimbia kabisa, kama Wafilisti walivyomkimbia Daudi wakati ule anapigana na Goliathi. Sote tunapaswa tufikie hatua hii. Hakuna kumpa upenyo wowote, mpaka afikie hatua akituona akimbie mwenyewe.

Lakini hiyo itawezekana tukiwa watiifu kwa Mungu, na kuyapinga mawazo yake mara kwa mara.

Bwana akubariki.

Kumbuka hizi ni siku za mwisho. Na hilo shetani analijua, hivyo kajidhatiti kweli kweli, tena akiwa na ghadhabu nyingi biblia inatuambia hivyo (Ufunuo 12:12), ili akutafute mtu kama wewe ambaye hujaokoka, au hujasimama vema katika Imani. Swali ni je! Umeokoka? Je! Umebatizwa katika ubatizo sahihi wa kuzamwishwa katika maji mengi, na kwa jina la YESU KRISTO..

Kama hayo hayapo ndani yako, ndugu yangu, hutaweza kumfukuza shetani akujiapo, hutaweza kumseta chini ya miguu yako, apiginapo na wewe, na wala hataweza kukukimbia. Bali atakuvaa kama alivyofanya kwa Yuda, na mwishowe atakupeleka kukua kiroho kama sio kimwili kabisa.

Hivyo kama hujamkaribisha Yesu katika maisha yako, muda ndio huu, tubu, dhambi zako kwa kumaanisha kabisa kuziacha, kisha tafuta ubatizo sahihi wa kimaandiko, Na Bwana atakumiminia kipawa cha Roho Mtakatifu, ikiwa utahitaji ubatizo huo, basi wasiliana na sisi kwa namba hizo hapo chini.

Na Mungu akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

ZIFAHAMU HUDUMA KUU (10) ZA SHETANI DUNIANI.

JINSI SHETANI ANAVYOZUIA MAJIBU YA MAOMBI YETU.

MLANGO MWINGINE WA ADUI KUTULETEA MAJARIBU.

INJILI YA MANENO LAINI ITAKUGHARIMU.

MZUNGUKO WAKO NI UPI?

Rudi nyumbani

Print this post