MWEKE SHETANI MBALI NA WEWE.

MWEKE SHETANI MBALI NA WEWE.

Shetani anaweza kuwekwa mbali nasi au akaondoka mbele yetu kwa namna kuu tatu.

  1. Ya kwanza ni kwa kumfukuza
  2. Ya pili ni kwa kuseta chini ya miguu yetu
  3. Na Ya tatu ni ya kumfanya yeye mwenyewe atukimbie.

1) Kumfukuza ni kwa kumkemea:

Wakati mwingine shetani anatukaribia sana ili kutujaribu tuanguke katika dhambi. Na tusipokuwa makini atafanikiwa hivyo pindi tunapojikuta katika mazingira kama hayo hatua inayofuata ni kumfukuza kwa kumkemea kwa vinywa vyetu.

Bwana Yesu alimfukuza shetani mara nyingi, utaona kule jangwani, alimfukuza, akamwambia “Nenda zako shetani” Neno hilo linamaanisha ondoka hapa, ni sawa na kufukuzwa.. ndipo akamwacha baada ya kukemewa mfano asingemfukuza angefululiza kumjaribu tu pale..

Mathayo 4:8 “Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mlima mrefu mno, akamwonyesha milki zote za ulimwengu, na fahari yake,

9 akamwambia, Haya yote nitakupa, ukianguka kunisujudia.

10 Ndipo Yesu alipomwambia, Nenda zako, Shetani; kwa maana imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake

11 Kisha Ibilisi akamwacha; na tazama, wakaja malaika wakamtumikia.”.

Wakati mwingine alikuwa na Petro, shetani naye akamvaa ili alipindishe kusudi la Mungu juu yake.. Lakini  utaona Bwana Yesu wakati ule ule alimkemea na kumwambia nenda nyuma yangu shetani kwani huyawazi yaliyo ya Mungu bali ya wanadamu.

Mathayo 16:22 “Petro akamchukua, akaanza kumkemea, akisema, Hasha, Bwana, hayo hayatakupata.

23 Akageuka, akamwambia Petro, Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu”.

Hata sisi, shetani anaweza kutusogelea kwa njia mbalimbali, hivyo hatuna budi kutumia vinywa vyetu kumkemea, pale pale. Wewe ni dada unaona mwanaume anakutongoza, anaanza kuzungumza na wewe mazungumzo ya kizinzi, hapo hapo unapaswa umkemee, lakini ukimwamwacha ataendelea hivyo hivyo na mwisho wa siku atakuvaa moja kwa moja kama alivyomvaa Yuda wakati ule. Na kitakachokuwa kimebakia kwako ni kujiua kiroho, kama sio kimwili kabisa.

Hivyo lazima tutumie vinywa vyetu kumfukuza shetani, tunapomwona anatusogelea sogelea, Kama vile tunavyotoa pepo, Kama alivyofanya Bwana.

2) Pili, ni kwa kumseta chini ya miguu yetu.

Njia hii ni tofauti kidogo na ile ya kwanza hapa, hutumii mdomo tena, bali unatumia matendo Zaidi.. Biblia inasema..

Warumi 16:19 “Maana utii wenu umewafikilia watu wote; basi nafurahi kwa ajili yenu, lakini nataka ninyi kuwa wenye hekima katika mambo mema, na wajinga katika mambo mabaya.

20 Naye Mungu wa amani atamseta Shetani chini ya miguu yenu upesi. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja nanyi. [Amina.]

Unaona, unapokuwa mjinga katika kutenda mambo maovu, na mwenye hekima katika kutenda mambo mema, kidogo kidogo, unazipunguza nguvu za ibilisi kwa kiwango kikubwa sana juu yako, na baadaye Mungu anamseta chini ya miguu yako mara moja, kama tunavyojua kitu kikisha kaa chini ya miguu yako, hakina nguvu tena, hakina ujanja wowote, kimeshindwa…Unaweza kukifanya vyovyote vile unavyotaka

Vivyo hivyo na sisi tukiwa watu wa namna hiyo, kamwe shetani hatokaa atuweze, Kwa urefu wa somo hilo tutumie ujumbe inbox, tukutumie. Wakati mwingine shetani anakuwa mgumu kwetu kumshinda, kwasababu ya mienendo yetu isiyompendeza Mungu. Tunakuwa wepesi kukimbilia mambo maovu,  na mambo ya Mungu tunakuwa wazito. Tukisikia kuna thamthilia Fulani imetoka, au series, tunakuwa wakwanza kuzifuatilia, lakini tu kufuatilia mafundisho ya biblia hilo hatuna muda nalo.. Kwa namna hiyo shetani atatusumbua sana.

Jaribu kuyaelekeza maisha yako kwa Mungu muda mrefu, utaona jinsi gani shetani anavyokuwa mwepesi kumshinda na hila zake, ni kwasababu tayari Mungu anakuwa ameshamseta chini ya miguu yako, hana nguvu yoyote ya kukushinda.

3) Na njia ya tatu ni ya kumfanya yeye mwenyewe kukimbia:

Hii ni ndo njia kuu, ukishaona mpaka adui yako anakukimbia kila akikuona anakula kona, basi ujue huo ni Zaidi ya ushindi, na kila utakapokwenda, yeye ndo anahama hapo kabla hujafika na sio wewe.. Sasa hapa ndipo tunapopaswa tupafikie watu wote.

Yakobo 4:6 “Lakini hutujalia sisi neema iliyozidi; kwa hiyo husema, Mungu huwapinga wajikuzao, bali huwapa neema wanyenyekevu.

7 BASI MTIINI MUNGU. MPINGENI SHETANI, NAYE ATAWAKIMBIA”.

Unaona, ukimtii Mungu, ukinyenyekea chini ya Mungu, ukayashika maagizo yake, ukawa unazikataa kazi za shetani, Hapo hakuna kingine cha ziada Zaidi ya shetani mwenyewe kutafuta mahali pengine..

Anakukimbia kabisa, kama Wafilisti walivyomkimbia Daudi wakati ule anapigana na Goliathi. Sote tunapaswa tufikie hatua hii. Hakuna kumpa upenyo wowote, mpaka afikie hatua akituona akimbie mwenyewe.

Lakini hiyo itawezekana tukiwa watiifu kwa Mungu, na kuyapinga mawazo yake mara kwa mara.

Bwana akubariki.

Kumbuka hizi ni siku za mwisho. Na hilo shetani analijua, hivyo kajidhatiti kweli kweli, tena akiwa na ghadhabu nyingi biblia inatuambia hivyo (Ufunuo 12:12), ili akutafute mtu kama wewe ambaye hujaokoka, au hujasimama vema katika Imani. Swali ni je! Umeokoka? Je! Umebatizwa katika ubatizo sahihi wa kuzamwishwa katika maji mengi, na kwa jina la YESU KRISTO..

Kama hayo hayapo ndani yako, ndugu yangu, hutaweza kumfukuza shetani akujiapo, hutaweza kumseta chini ya miguu yako, apiginapo na wewe, na wala hataweza kukukimbia. Bali atakuvaa kama alivyofanya kwa Yuda, na mwishowe atakupeleka kukua kiroho kama sio kimwili kabisa.

Hivyo kama hujamkaribisha Yesu katika maisha yako, muda ndio huu, tubu, dhambi zako kwa kumaanisha kabisa kuziacha, kisha tafuta ubatizo sahihi wa kimaandiko, Na Bwana atakumiminia kipawa cha Roho Mtakatifu, ikiwa utahitaji ubatizo huo, basi wasiliana na sisi kwa namba hizo hapo chini.

Na Mungu akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

ZIFAHAMU HUDUMA KUU (10) ZA SHETANI DUNIANI.

JINSI SHETANI ANAVYOZUIA MAJIBU YA MAOMBI YETU.

MLANGO MWINGINE WA ADUI KUTULETEA MAJARIBU.

INJILI YA MANENO LAINI ITAKUGHARIMU.

MZUNGUKO WAKO NI UPI?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments