Moja ya nguzo muhimu sana katika Imani ya Kikristo ni SADAKA, Sadaka ni nguzo muhimu sana, kwasababu hata Kristo mwenyewe alifanyika sadaka kwa ajili yetu ili sisi tuokolewe…Kama Kristo asingejitoa nafsi yake kwa ajili yetu sisi tusingekuwa popote, tungekuwa ni wana wa Jehanamu wote, hakuna hata mmoja ambaye angepona.
Kwahiyo kama Kristo alivyojitoa kwetu na sisi pia lazima tujitoe kwa wengine…Ndio maana sadaka ni Muhimu, Roho iliyokuwa ndani ya Kristo ilimpeleka kujitoa nafsi yake kuwa fidia kwa roho nyingi, halikadhalika na sisi kama tumeipokea Roho ile ile ambayo ilikuwa ndani yake, ni lazima itatusukuma na sisi kujitoa kwa ajili ya wengine, kulingana na karama tulizopewa…
Sadaka sio lazima kutoa mali, bali hata kujitoa Maisha ili kwamba wengine wapate uzima, kama Bwana Yesu hakutoa fedha ili sisi tuokolewe bali aliitoa damu yake na Maisha yake kwa kuishi na kufundisha watu njia ya wokovu ili waokolewe. Hiyo ni sadaka kubwa sana na kuu kuliko zote, kutoa Maisha kwaajili ya mwingine ili aokoke. Kama Biblia inavyotuambia katika..
1 Yohana 3:16 “Katika hili tumelifahamu pendo, kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake kwa ajili yetu; imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu”.
Na sadaka sio mchango. Mchango ni kitu unachotoa kuchangia jambo Fulani liendelee mbele lakini sadaka, ni kitu kinachohusisha wewe kupungukiwa ili mwingine aongezewe, au wewe kupoteza ili mwingine apate, hiyo ndiyo maana ya sadaka…haina tofauti sana na neno MUHANGA..Kwahiyo sadaka ni KITU kikubwa Zaidi ya Mchango…Hivyo unapomtolea Mungu sadaka kwaajili ya kazi yake, zingatia kutoa kitu kikubwa Zaidi ya mchango, toa kitu ambacho kimekugharimu sana….ukitoa mchango utapata thawabu lakini sadaka ina thawabu kubwa Zaidi.
Sasa leo hatutaingia sana kuzungumzia Umuhimu wa Sadaka au nguvu ya sadaka, lakini tutazungumzia UDHAIFU WA SADAKA.
Utauliza, sadaka ina madhaifu?..Jibu ni ndio, sadaka ina madhaifu na mipaka..Inayo nguvu ya kubadilisha mambo lakini pia inayo mipaka ambayo haiwezi kupita..kuna mambo ambayo haiwezi kubadilisha…Hebu tusome mistari michache ifuatayo kisha tuendelee…
1 Samweli 15:20 “Sauli akamwambia Samweli, Hakika mimi nimeitii sauti ya Bwana, nami nimemleta Agagi, mfalme wa Waamaleki, tena nimewaangamiza Waamaleki kabisa. 21 Ila watu waliteka nyara, kondoo na ng’ombe walio wazuri, katika vitu vilivyowekwa wakfu, kusudi wavitoe dhabihu kwa Bwana, Mungu wako, huko Gilgali. 22 Naye Samweli akasema, je! Bwana huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya Bwana? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu. 23 Kwani kuasi ni kama dhambi ya uchawi, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la Bwana, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme”
1 Samweli 15:20 “Sauli akamwambia Samweli, Hakika mimi nimeitii sauti ya Bwana, nami nimemleta Agagi, mfalme wa Waamaleki, tena nimewaangamiza Waamaleki kabisa.
21 Ila watu waliteka nyara, kondoo na ng’ombe walio wazuri, katika vitu vilivyowekwa wakfu, kusudi wavitoe dhabihu kwa Bwana, Mungu wako, huko Gilgali.
22 Naye Samweli akasema, je! Bwana huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya Bwana? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu.
23 Kwani kuasi ni kama dhambi ya uchawi, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la Bwana, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme”
Habari hiyo inamzungumzia Mfalme wa kwanza wa Israeli aliyeitwa Sauli, ambaye alilikaidi Neno la Mungu, aliambiwa akaangamize vitu vyote na watu wote (Waamaleki) asiache chochote, hata ng’ombe na mbuzi na kondoo wote auwe, lakini yeye akaangamiza vyote lakini akawaacha wafalme wa ile nchi hai pamoja na ng’ombe walionona na kondoo na kuvileta Israeli kwaajili ya kumtolea Mungu dhahibu, (dhabihu ni sadaka ya kuteketezwa). Kwa moyo wake alijua Mungu anapendezwa Zaidi na Sadaka kuliko kuyashika maagizo yake.. Hakujua kuwa nguvu ya sadaka sio kubwa kuliko nguvu ya kushika maagizo yake. Hivyo akajitumainisha kwa sadaka zile na Mungu akamkataa..
Huo ndio udhaifu wa Sadaka!..Ni kweli Mungu aliagiza watu wamtolee sadaka zilizonona, tena wasimtolee vilema, kwasababu ukimtolea sadaka kilema ilikuwa ni kujitafutia kulaaniwa badala ya kubarikiwa.(soma Malaki 1:13-14). Lakini sadaka hiyo hiyo, ina mipaka. Haiwezi kubadilisha mambo yote, haiwezi ikalivuka Neno la Mungu. Hatuwezi kumuonga Mungu kwa sadaka zetu, ili abadilishe Neno lake..Hapana! tutaongeza baraka tu kwa sadaka lakini si kulibadilisha Neno lake, akisema kuwa roho ya mwenye dhambi itakufa, hata tutoe fedha kiasi gani kama hatutalitii hilo neno na kuacha dhambi! Hizo sadaka hazina msaada wowote, kufa tutakufa tu!…Akisema waasherati na walawiti na waabudu sanamu sehemu yao ni katika lile ziwa la moto! Hata tutoe hazina zote za ulimwengu na kujitoa hata miili yetu, kama hatutatii na kuacha hivyo vitu…Jehanamu haiepukiki.
Sasa habu tuangalie mfano wa Mwisho ambao ni Bwana Yesu mwenyewe aliuota kuonesha udhaifu wa Sadaka!..Tusome.
Mathayo 5:23 “Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, 24 iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako. 25 Patana na mshitaki wako upesi, wakati uwapo pamoja naye njiani; yule mshitaki asije akakupeleka kwa kadhi, na kadhi akakupeleka kwa askari, ukatupwa gerezani. 26 Amin, nakuambia, Hutoki humo kamwe hata uishe kulipa senti ya mwisho”
Mathayo 5:23 “Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako,
24 iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako.
25 Patana na mshitaki wako upesi, wakati uwapo pamoja naye njiani; yule mshitaki asije akakupeleka kwa kadhi, na kadhi akakupeleka kwa askari, ukatupwa gerezani.
26 Amin, nakuambia, Hutoki humo kamwe hata uishe kulipa senti ya mwisho”
Mfano huo Bwana Yesu alioutoa kutufundisha kuwa tusiitegemee sadaka, kubadilisha Neno la Mungu..Katika habari hiyo anasema “kabla ya kuitoa sadaka yako, patana kwanza na mshtaki wako”…Ikiwa na maana kwamba kama kuna mtu anakudai, au kuna mtu umemdhulumu, au kuna mtu umegombana naye, na wewe ndiye mwenye makosa na hivyo bado kidogo atakwenda kukushitaki… usikimbilie kwenda kutoa sadaka! Kana kwamba hiyo sadaka uliyoitoa itakukuokoa….Kitu cha kwanza Kimbilia kwanza kwenda kupatana naye, kwasababu usipopatana naye ukachelewa kidogo tu! na yeye akaenda kuripoti polisi, na polisi wakaja kukuchukua na kukuweka ndani! Biblia inasema hutatoka huko…Na hiyo sadaka uliyoitoa ambayo ulitegemea kukusaidia, wakati huo haitakusaidia chochote kukutoa huko gerezani…Mungu hatakuwa upande wako hata kidogo…Hivyo Bwana anasema…Nenda kwanza kapatane naye kabla hajakwenda kukuripoti…sadaka utatoa tu! Nenda kwanza kapatane naye! kwasababu Neno lake linasema…
Warumi 12:18 “Kama yamkini, kwa upande wenu, mkae katika amani na watu wote”.
Sasa ukikaa kwa vurugu na watu wote, hata utoe fedha kiasi gani kwa Mungu! Haitaruka Neno lake hilo kwamba “mkae na amani na watu wote”…Huo ndio udhaifu wa sadaka, haipiti Neno la Mungu….. “kutii ni bora kuliko dhabihu na kusikia kuliko Mafuta ya Beberu”.
Hivyo ndugu, inawezekana unatoa sadaka nyingi nzuri sana, hilo ni Jema Mungu atakulipa kwa ukarimu wako, lakini sadaka hiyo haiwezi kulipita Neno la Mungu linalosema…
Ufunuo 21:8 “Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili”.
Wala kulipita Neno hili..
Wagalatia 5:19 “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, 20 ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, 21 husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu”.
Wagalatia 5:19 “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi,
20 ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi,
21 husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu”.
Sadaka nzuri ni ile inayoambata na kulitii Neno la Mungu.
Uchaguzi unao wewe ambaye hujampa Kristo Maisha yako!..Kumwamini Yesu, na kutubu na kuamua kumgeukia huku ukidhamiria kuacha dhambi kabisa, utakapoamua kugeuka na kusema Kuanzia leo hii mimi na ulimwengu basii!! Kristo akiiona nia yako ndani yako kwamba kweli umedhamiria kuacha kwa vitendo, basi atakupa nguvu ya Roho wake Mtakatifu ambaye atakusadia kuweza kuzishinda dhambi kama ulivyosema kutoka katika kinywa chako mwenyewe. Mlango wa Neema bado upo wazi, lakini tunaishi kipindi cha kumalizia, ambapo parapanda siku yoyote inalia na watakatifu wataondolewa ulimwenguni, na ulimwengu kuharibiwa. Hivyo usikiapo maneno haya usifanye moyo wako mgumu, kama ulishampa Kristo Maisha yako, lakini umekuwa vuguvugu ni wakati wakuwa moto, kwasababu walio vuguvugu wote, Kristo alisema atawatapika.
Bwana akubariki sana.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Print this post