Swali: Je vitu kama giza, na maji viliumbwa siku ya ngapi, maana tunaona wakitajwa tu wanyama na mimea, je hivi vingine viliumbwa lini?
Jibu: Ni kweli katika kitabu cha Mwanzo tunaona uumbaji unaanza kwa kusema “giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji”, lakini haitaji ni lini giza liliumbwa wala ni lini maji yaliumbwa, badala yake tunaona uumbaji unaendelea na vitu vingine kama mimea pamoja na wanyama na wanadamu?..
Mwanzo 1:1 “Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi.
2 Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji”.
Jibu la swali hili lipo katika mstari huo wa kwanza..
Mwanzo 1:1 “Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi”.
Neno “hapo mwanzo”… halimaanishi kile kipindi cha siku saba (7) bali linamaanisha mwanzo kabisa wa uumbaji kabla ya kitu kingine chochote, Mungu aliumba mbingu (hii yenye mawingu na sayari) pamoja na mbingu ile yenye Malaika watakatifu.
Na vile vile aliumba “NCHI” Au kwa lugha nyingine ARDHI/DUNIA. Na ili ardhi iweze kukamilika ni lazima iwe na malighafi zake zote kama udongo, mchanga, mawe, milima, mabonde, chuma, madini, moto na maji na mengineyo.
Vile vile ili mbingu ikamilike lazima iwe na nyota na mwanga uwepo na giza liwepo, kwahiyo vitu hivi vyote viliumbwa Hapo Mwanzo, kabla ya zile siku sita za uumbaji.
Na baada ya Mungu kuumba Mbingu na nchi, hatujui ni kitu gani kilitokea kikaifanya nchi/dunia yenye milima na mawe na madini na mabonde na maji kuwa UKIWA! Au kwamba Mungu ndio aliiumba ikae hivyo ukiwa kwa kipindi Fulani cha muda..hatujui!, labda tutakuja kujua tutakapomaliza maisha haya na kufika huko kwake, tutamwuliza, lakini tunajua kuwa alisema hakiumba ukiwa, bali ikaliwe na watu.
Isaya 45:18 “Maana Bwana, aliyeziumba mbingu, asema hivi; Yeye ni Mungu; ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya; ndiye aliyeifanya imara; hakuiumba ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na watu; Mimi ni Bwana, wala hapana mwingine”
Hivyo kama hakuiumba ikae ukiwa bali ili ikaliwe na watu, basi hana budi kuiikarabati na kumweka mwanadamu humo, na ndipo hapo siku sita za uumbaji wa wanyama na wanadamu na miti zilipoanza..
Lakini kiuhalisia tayari mbingu na nchi zilikuwa umeshaumbwa hapo kabla, na malighafi zake zote (kama maji, udongo, mawe, madini, giza, hewa n.k)..na ndio maana hatuoni vikitajwa katika uumbaji.
Lakini pamoja na hayo, upo unabii unaoonyesha kuwa dunia itakuja kuwa tena ukiwa siku za mwisho, kipindi ambacho ghadhabu ya Bwana MUNGU itakapokuja kumwagwa juu wa wanadamu wote wakosaji, ambayo hata mmoja wetu hapaswi kuwepo..
Isaya 13:9 “Tazama, siku ya Bwana inakuja, siku kali, ya hasira na ghadhabu kuu, ili iifanye nchi kuwa ukiwa, na kuwaharibu watu wake, wenye dhambi, wasikae ndani yake.
10 Maana nyota za mbinguni na matangamano havitatoa nuru yake; jua litatiwa giza wakati wa kucha kwake, na mwezi utaacha nuru yake isiangaze”.
Isaya 24:1 “Tazama, Bwana ameifanya dunia kuwa tupu, aifanya ukiwa, aipindua, na kuwatawanya wakaao ndani yake”.
Jambo litakalotokea siku hiyo ni lile tunalolisoma katika kitabu cha 2Petro 3:10-12 na Isaya 34:4.
Lakini wateule, waliomwamini Bwana na kuoshwa kwa damu yake, hawatakuwepo katika siku hiyo ya ghadhabu yake, kwani watakuwa mbinguni pamoja na Bwana.
Bwana atubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Rudi Nyumbani
About the author