Category Archive Home

UTAKASO NI SEHEMU YA MAISHA YA MKRISTO YA KILA SIKU.

Jina kuu la Bwana wetu Yesu libarikiwe.

Ni siku nyingine tena Bwana ametupa pumzi yake kuiona, leo tutajifunza somo linalohusiana na utakaso kwa mtakatifu. Lakini kabla hatujafika kwenye utakaso, ni vizuri tufahamu kwanza mtakatifu ni mtu wa namna gani kibiblia..

Wengi tunafahamu  labda mtu mpaka aitwe mtakatifu ni lazima awe ameshakaa kwenye wokovu miaka mingi,, lakini kibiblia sio hivyo. Bali pale mtu anapoamua kuokoka, pale anapoamua kuacha maisha yake ya dhambi, na kumgeukia Bwana Yesu, na kusafishwa na damu yake, na kubatizwa, wakati huo huo anakuwa tayari kashafanyika kuwa mtakatifu, haijalishi mambo mengine yatakuwa hayajaondoka vizuri ndani yake,..Kile kitendo tu cha kumpokea Yesu maishani mwake, mtu huyo mbinguni ni mtakatifu kwasababu hana deni la dhambi,  anakuwa sawasawa tu na mkristo mwingine aliyekaa  katika wokovu kwa miaka 50.

Lakini tatizo linakuja ni pale ambapo mtu huyo anadhani akishampokea Yesu, ndio basi inatosha, Nataka nikuambie hilo halipo katika safari ya ukristo. Utarudi nyuma tu siku sio nyingi, na utakatifu wako utakufa na utakuwa  kama vile mtu ambaye hajaokolewa.

Fahamu baada ya kuwa mtakatifu, hatua inayofuata kwako ni lazima iwe Kujitakasa.. Ndio maana Bwana Yesu alisema maneno haya..

Ufunuo 22:11 “Mwenye kudhulumu na azidi kudhulumu; na mwenye uchafu na azidi kuwa mchafu; na mwenye haki na azidi kufanya haki; na MTAKATIFU NA AZIDI KUTAKASWA”.

Unaona inasema mtakatifu azidi kutakaswa, ikiwa na maana ukiwa mtakatifu hupaswi kubakia pale pale sikuzote, ni jukumu lako kujitakasa siku baada ya siku. MTAKATIFU ni kama BETRI ya simu. Pale inaponunuliwa ndani yake huwa imeshaumbiwa nguvu ya kutosha ya kuifanya simu iwake kwa muda wa miaka mingi sana hata 10 na zaidi. Lakini Betri hiyo haitegemei tu ile nguvu iliyowekwa ndani yake kuipa uhai simu siku zote, hapana, bali inatarajia pia iwe inachajiwa mara kwa mara, hata kila siku, ili kuzisisimua nguvu zilizoko ndani yake iendelee kuifanya simu iwake  kwa muda wote huo.

Lakini kama isipochajiwa, ni wazi kuwa hautaweza kuwasha simu, na matokeo yake ni kuwa itakuwa kama jiwe tu lisilokuwa na maana yoyote, haijalishi kuwa ndani yake kuna nguvu nyingi kiasi gani.Vivyo hivyo na utakatifu nao.. utakatifu bila utakaso Umekufa.

Unapookoka leo hii, unapoamua kumpa Yesu maisha yako, hiyo peke yake haitoshi zipo hatua za kuanza kupiga, ili kuufanya ule utakatifu kuwa hai ndani yako siku baada ya siku. Yapo maisha unapaswa uanze kujizosha kuishi ili Mungu aweze kukutakasa (kukutia nguvu ) ya kuendelea kuishi maisha ya utakatifu siku baada ya siku .

Warumi 6:22 “Lakini sasa mkiisha kuwekwa huru, na kuwa mbali na dhambi, na kufanywa watumwa wa Mungu, MNAYO FAIDA YENU, NDIYO KUTAKASWA, na mwisho wake ni uzima wa milele”.

SASA MTU ANAJITAKASAJE?

Kwanza ni kwa kukujifunza Neno la Mungu kwa bidii: Unapookoka, ni jukumu lako kusoma Neno na kusikiliza Neno, hususani mafundisho yanayolenga utakatifu. hiyo itakusaidia kujua biblia inasema nini katika kila jambo unalotaka kulifanya. Hivyo kuwa rahisi kujiepusha na mambo ambayo hayampendezi Mungu.

1Petro 1:22 “Mkiisha kujitakasa roho zenu kwa kuitii kweli, hata kuufikilia upendano wa ndugu usio na unafiki, basi jitahidini kupendana kwa moyo”.

Pili ni kwa kuwa mwombaji na kufunga: Maombi ni nguzo nyingine inayomtia mtu nguvu ya kuendelea kudumu katika utakatifu Mungu anaouhitaji ndani ya mtu. Usipokuwa mwombaji huwezi kudumu katika wokovu, huwezi kuyashinda majaribu kwa namna yoyote ile. Vilevile na katika kufunga, kunakusaidia kufikiria zaidi mambo ya rohoni kuliko ya mwilini na matokeo yake kuzishinda tama zake.

Tatu ni kwa kujizoeza kuishi maisha yampendezayo Mungu: Kujizoesha ni jambo lingine la msingi sana, kwamfano mtu aliyejizoesha kuamka alfajiri sana, huwa  inafikia wakati kuamka kwake asubuhi kunakuwa ni kwepesi sana tofauti na Yule ambaye hajajizoesha kuamka mapema.. Vivyo hivyo  na katika Utakatifu, tukijizoesha kuishi maisha ya haki, baadaye yanakuja kuwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku yenyewe bila hata kutumia bidii nyingi.

1Timotheo 4:8 “Kwa maana kujizoeza kupata nguvu za mwili kwafaa kidogo, lakini utauwa hufaa kwa mambo yote; yaani, unayo ahadi ya uzima wa sasa, na ya ule utakaokuwapo baadaye”.

Nne, Ni kwa kuifanya kazi ya Mungu: Kuitenda kazi ya Mungu ikiwemo kuwahubiria wengine ni chaji nzuri sana ya utakatifu. Kwasababu inakufanya ukae katika uwepo wa  ki-Mungu muda mrefu, kwasababu unamlazimisha Roho Mtakatifu aje kufanya kazi na wewe, na sikuzote alipo Roho Mtakatifu, lazima uwepo utakatifu.

Hivyo kwa kuhitimisha, ni jukumu la kila mmoja wetu KUJITAKASA kila siku, ili aendelee kudumu, hakunaga Utakatifu wa kusema mimi nimeokoka, halafu huonyeshi bidii yoyote, hapo utakuwa unajidanganya mwenyewe, utasema tu kwa mdomo lakini kwa matendo utakuwa mbali nao.  Ni lazima tujichaji (tujitakase) ili tuweze kudumu kwenye huo utakatifu. Siku hizi za mwisho Bwana Yesu alitusisitiza sana kufanya hivyo, kwasababu maovu yameongezeka, na yeye yupo mlangoni kurudi.

2Petro 1:8 “Maana mambo hayo yakiwa kwenu na kujaa tele, yawafanya ninyi kuwa si wavivu wala si watu wasio na matunda, kwa kumjua Bwana wetu Yesu Kristo.

9 Maana yeye asiyekuwa na hayo ni kipofu, hawezi kuona vitu vilivyo mbali, AMESAHAU KULE KUTAKASWA DHAMBI ZAKE ZA ZAMANI.

Mimi na wewe tusisahau utakaso wa kila siku.

Maran atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mafundisho mengine

Mada Nyinginezo:

Nini maana ya ‘Maandalio ya moyo ni ya mwanadamu’ ?

Nini maana ya “yasiyokuwapo hayahesabiki”(Mh 1:15)

TUSIWE WATU WA KUPUNGUKIWA AKILI.

MWANZO WA INJILI YA YESU KRISTO.

Nini maana ya ‘kuhuluku’ kama tunavyosoma katika biblia?

Kwanini Mungu aliwaagiza wana wa Israeli wasikisaze chakula?

Rudi nyumbani

Print this post

Nini maana ya ‘Maandalio ya moyo ni ya mwanadamu’ ?

SWALI: Naomba kufahamu maana ya mstari huu ; Mithali 16:1 “Maandalio ya moyo ni ya mwanadamu; Bali jawabu la ulimi hutoka kwa Bwana”.


JIBU: Mstari huu unatukumbusha kuwa si kila jambo tunalolipanga katika maisha tunaweza kulitolea maamuzi  yake asilimia mia. Ni kweli Mungu anaturuhusu tupange mipango yetu mingi kwa jinsi  tupendavyo, lakini tunapaswa tukumbuke  pia sio kila mpango tulioupanga ni lazima uje kama tulivyotarajia.

Kwamfano utaona Balaamu alipomwendea Mungu ili kuwalaani Israeli, jibu la Mungu lilikuwa ni kuwabariki badala ya kuwalaani. (Hesabu 22-24).  Utaona alikwenda kweli na mipango yake kwa Mungu ili kumridhisha Balaki, akidhani utakuwa ni vema pia kwa Mungu, lakini badala yake aliambiwa aibariki Israeli badala ya kuilaani.

“Maandalio ya moyo ni ya mwanadamu; Bali jawabu la ulimi hutoka kwa Bwana”

Hivyo tunapopanga mipango yetu, tunapaswa tujinyenyekeze kwa kusema Bwana akipenda kama biblia inavyotuasa hapa,

Yakobo 4:13 “Haya basi, ninyi msemao, Leo au kesho tutaingia katika mji fulani na kukaa humo mwaka mzima, na kufanya biashara na kupata faida;

14 walakini hamjui yatakayokuwako kesho. Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa kitambo, kisha hutoweka.

15 Badala ya kusema, Bwana akipenda, tutakuwa hai na kufanya hivi au hivi.

16 Lakini sasa mwajisifu katika majivuno yenu; kujisifu kote kwa namna hii ni kubaya”.

Unaweza kweli ukawa umepanga uje kuwa daktari ukubwani, lakini mipango yako au ndoto zako  ghafla zimevuruguka kuona kwamba unalazimika kwenda kusomea kitu ambacho hujakipenda, sasa unapokuwa katika hali kama hiyo na wewe ni mkristo kumbuka huu mstari.. “Maandalio ya moyo ni ya mwanadamu; Bali jawabu la ulimi hutoka kwa Bwana”

Unaweza ukawa umepanga, ufanikishe jambo fulani, mwaka uliopita lakini haujafanikisha kutoka na vikwazo fulani, pengine ukaanza kulaumu kwanini haikuwezekana, sasa ukijikuta katika hali kama hiyo na wewe ni mkristo ambaye unaouhakika umeokolewa na Kristo, hupaswi kuwa na huzuni, ujue ipo mipango mingine mzuri zaidi ambayo Mungu kaiweka mbele yako, pengine unaweza usiione sasa hivi, lakini baadaye ukaiona na kumshukuru Mungu, na kusema asante Mungu kwa kunipitisha njia hii leo.

Hivyo kila jambo ulifanyalo, usilipe asilimia mia kwamba ni lazima liwe kama ulivyolipanga, kumbuka wewe sio Mungu, anayejua kesho kwa asilimia yote ni Mungu peke yake..Kwahiyo wewe amka asubuhi, panga mipango yako, kisha mshirikishe Mungu na  umalizie na Neno IKIWA ITAKUPENDEZA MUNGU..

Ikiwa imempendeza basi litafanikiwa kama ulivyopanga lakini ikiwa halikumpendeza basi atakuandalia njia nyingine iliyo bora zaidi.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mafundisho mengine

Mada Nyinginezo:

Nini maana ya “yasiyokuwapo hayahesabiki”(Mh 1:15)

Tofauti kati ya lijamu na hatamu ni ipi kibiblia?

JE SALA YA ROZARI TAKATIFU NI YA KIMAANDIKO?

TAZAMA, NASIMAMA MLANGONI.

CHAPA YA MNYAMA

Rudi nyumbani

Print this post

Nini maana ya “yasiyokuwapo hayahesabiki”(Mh 1:15)

JIBU: Tusome mstari wenyewe.

Mhubiri 1:15 “Yaliyopotoka hayawezi kunyoshwa, Wala yasiyokuwapo hayahesabiki”.

Hapo utaona vipengele viwili, cha kwanza ni: Yaliyopotoka hayawzi kunyoshwa. Na cha pili ni yasiyokuwapo hayahesabiki.

Tukianza na hicho cha kwanza cha Yaliyopotoka hayawezi kunyoshwa,..Tukumbuke kuwa kitabu cha Mhubiri ni kitabu kinachoeleza juhudi za mwanadamu za kutafuta suluhu ya mambo yote yaliyopo duniani kwa nguvu zake mwenyewe pasipo kumuhusisha Mungu. Na ndio maana utaona mhubiri ambaye ndiye aliyejibidisha katika kufanya hivyo, mwisho wa siku anaishia kusema ni UBATILI Mtupu, mambo yote na hekima yote ya mwanadamu ni ubatili tu, ni sawa na kuufuata upepo ambao mwanzoni unaweza kukupa matumaini kuwa utakufikisha mahali, lakini mwishowe unapotea tu ghafla njiani, hujui ulipoelekea umekuacha tu hewani. Ndivyo alivyo mwanadamu anayehangaika kukimbizana na ulimwengu huu.

Sasa aliposema “Yaliyopotoka hayawezi kunyoshwa” Ni kuwa aliona, kuna mambo ambayo yalikatazwa na Mungu, au kwa namna nyingine tuseme hayapo katika uhalisia wake, na pengine anaweza kuyaweka sawa na kuyafanya yaonekane yanafaa katika jamii, Umeona? Ndipo kwa hekima yake akajaribu kufanya hivyo aone kama yatakuwa kweli ni sawasawa, lakini mwisho wa siku akagundua hata ufanyaje kile kilichokataliwa na Mungu (yaani kupotoshwa) hakiwezi kufanywa kiwe sawasawa. Ni kujitafutia tu matatizo na shida zisizokuwa na sababu.

Mbeleni kidogo utaona anasema..

Mhubiri 7:13 “Tafakari vema kazi yake Mungu; kwa sababu ni nani awezaye kukinyosha kitu kile alichokipotosha yeye?

Ni kama leo tu, watu wanatafuta namna ya kuhalalisha ndoa za jinsia moja..wanajaribu kufanya kila mbinu, ionekane kuwa ile ni ndoa iliyokubaliwa na Mungu, lakini bado haiwezi kuwa ndoa, na hilo wanalijua, wengine mpaka wanajibadilisha jinsia waonekane kama wanaume, au wanawake, lakini bado  zile jinsia zao zinaendelea kubakia nao ndani yao.. Na matokeo yake wanaishia kupata matatizo mabaya ya kiafanya na kuishia kufa.

Ndivyo walivyo hata na mashoga, wanapojaribu kuwa kama wanawake, maumbile yao yanaharibika wanashindwa kukaa hata katika jamii na watu wengine wakihofia aibu. Kwasababu yaliyopotoshwa hayawezi kunyoshwa,  Unaona? Si hilo tu Wapo wengine wanajichubua ngozi zao ili wabadili rangi ya miili yao wawe weupe, sote tunajua mwisho wao watu wa namna hiyo ni nini, ni kuishia kupata kansa ya ngozi na kufa.

Inastaajabisha leo hii, kuona wanawake nao wanasema suruali ni mavazi ya jinsia zote. Haijalishi wataihalalisha vipi wataitengeneza kwa muundo gani unaoonekana wa kike, lakini bado vazi la suruali litabakia kuwa vazi la kiume tu, wewe unayejaribu kukinyosha kitu ambacho Mungu kakipotosha kwako unajitafutia matatizo na hukumu.

Unaweka mawigi, kucha za bandia, ili uonekane wa tofauti na Yule wa kwanza ambaye Mungu alikuumba..Embu  Itafakari vema kazi ya Mungu, na uache kukinyosha kile ambacho Mungu kakipotosha. Hiyo ndio maana ya kifungu hicho.

> Sasa tukirudi kwenye kile kipengele cha pili ambacho kinasema “Wala yasiyokuwapo hayahesabiki”.

Hii dunia imejawa na mambo mengi ya Mungu, ambayo bado mwanadamu anazidi kuyavumbua kila siku, lakini mpaka sasa takwimu zinaonyesha, bado asilimia 86 ya viumbe havijajulikana duniani, japokuwa ameishi duniani kwa muda mrefu sasa

Mambo yasiyojulikana ni mengi kuliko yanayojulikana, wanasayansi wanalijua hilo, kila siku wanavumbua mambo mapya, wanashangaa kumbe na hili lipo na lile lipo..Hiyo inawafanya wawe buzy usiku na mchana kutafuta na kutafiti tu, siku zinakuja siku zinakwenda, wanaendelea tu hivyo hivyo, wanasahau mpaka na mambo ya msingi ya roho zao.. Wanadhani katika kuvumbua huko ndio siku moja watapata jawabu la maisha ya mwanadamu hapa duniani.

Mhubiri anasema hayo yote ameshayafanya, lakini amegundua ni ubatili mtupu, kwamba yasiyokuwepo hayahesabiki, hata kama nitakuwa buzy miaka yangu yote kutafiti, kamwe sitavumbua yote. Ni sawa na kuufuata upepo. Huoni leo hii wanadamu walivyo buzy na mambo ya duniani wanasahau mambo ya mbinguni ambayo ni ya kudumu milele? Kiasi kwamba huwezi kuwaeleza chochote, nje ya sayansi wanayojitumainisha nayo.

Lakini Mhubiri mwishoni anatoa jumla ya mambo yote, anasema, linalompasa mwanadamu kufanya ni KUMCHA MUNGU, NA KUZISHIKA AMRI ZAKE (Mhubiri 12:13) basi. Na wewe pia hakuna mahali popote utakapoweza kupata jawabu la maisha isipokuwa kwa Kristo tu peke yake. Hii dunia itakutesa sana, lakini Ukimpa leo maisha yako,ayaongoze, ukaanza naye upya ameahidi kukupa pumziko la roho, hiyo ni ahadi yake.

Mathayo 11:28 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;

30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi”.

Hivyo kama upo tayari leo kutubu na kuanza naye upya, basi fungua hapa kwa maelekezo ya sala ya Toba..>>. SALA YA TOBA

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mafundisho mengine

Mada Nyinginezo:

Maana ya huu mstari ni ipi? Mithali 14:4 ‘Zizi ni safi ambapo hapana ngombe;bali nguvu za ngombe zaleta faida nyingi’.

Kiango na Pishi ni nini (Mathayo 5:15)?

Kiango na Pishi ni nini (Mathayo 5:15)?

Ukoma wa nyumba ulifunua nini zamani?

NI SAA KUMI NA MBILI (12) TU, ZA KRISTO KWAKO.

Rudi nyumbani

Print this post

Nini maana ya ‘kuhuluku’ kama tunavyosoma katika biblia?

Kuhuluku ni Neno lingine linalomaanisha KUUMBA.

Kwamfano tukisema Mungu kahuluku jua na mwezi, tunamaanisha kuwa Mungu ameumba jua na mwezi.

Vifuatavyo ni baadhi ya vifungu ambavyo vinalielezea Neno hilo;

Isaya 43:1 “Lakini sasa, Bwana aliyekuhuluku, Ee Yakobo, yeye aliyekuumba, Ee Israeli, asema hivi, Usiogope, maana nimekukomboa; nimekuita kwa jina lako, wewe u wangu”.

Isaya 45: 12 “Mimi nimeiumba dunia, nimemhuluku mwanadamu juu yake; Mimi, naam, mikono yangu mimi, imezitanda mbingu, na jeshi lake lote nimeliamuru”.

Isaya 45: 7 “Mimi naiumba nuru, na kulihuluku giza; mimi nafanya suluhu, na KUHULUKU UBAYA; Mimi ni Bwana, niyatendaye hayo yote”.

Katika huu mstari wa mwisho utaona anasema sio tu ameumba vitu vya asili na wanadamu au  mambo mema tu peke yake, hapana, bali anasema yeye pia ni Mungu anayehuluku UBAYA, Yaani anaumba ubaya. Jambo ambalo wengi hatulijui.

Ndio Mungu anaumba ubaya ndugu yangu,. Alipoleta gharika ule ulikuwa ni ubaya, lengo lilikuwa ni kuwagharikisha watu wote waovu waliokuwa duniani wakati ule. Embu Soma maneno haya anavyosema;

Ayubu 38:22 “Je! Umeziingia ghala za theluji, Au umeziona ghala za mvua ya mawe,

23 Nilizoziweka akiba kwa wakati wa misiba, Kwa siku ya mapigano na vita”?

Unaona?

> Aliposhusha  pia ule moto na  kibiriti, wakati wa Sodoma na Gomora ule ni uovu aliouumba yeye mwenyewe mahususi kwa ajili ya watenda dhambi.

> Alipoleta  tena Tauni mara kadha wa kadha kwa taifa la Israeli pale walipomwasi na kumkasirisha kule jangwani na sehemu nyinginezo, ule ulikuwa ni ubaya aliohuluku, kwa watu waasi.

> Vilevile alivyoleta CORONA ulimwengu ni Ubaya uliotoka kwake yeye mwenyewe kutuadhibu sisi wanadamu tunaoishi duniani leo hii  kwa matendo yetu maovu. Hakuna mwanasayansi yoyote aliyeuunda ugonjwa huo, Huo ni ugonjwa uliotoka kwa Mungu mwenyewe kama pigo.

> Lakini hayo yote ni mwanzo tu ubaya wenyewe ambao Mungu alishaundaa tangu zamani kwa watenda dhambi wote ikiwemo ibilisi pamoja na mapepo yake yote. Na ubaya wenyewe ndio lile ZIWA LA MOTO.

Hivyo Mungu ni wa kumuogopa sana.. Ni kweli yeye ni Mungu wa rehemu na neema nyingi, kwa wale wamtiio, lakini pia ni wa ghadhabu na hasira nyingi, kwa waovu wote. Na ndio maana leo hii anakupa Muda wa kutosha wa kutubu ili umgeukie yeye akusemehe dhambi zako. Usifurahie unatenda dhambi halafu hakuna chochote kinachokutokea, usifurahie unaua, unafanya ushirikina, unazini, lakini Mungu hakufanyi chochote ukadhani utaendelea kuwa hivyo milele. Upo ubaya mbele yako. Na ni jukumu lako kufahamu hilo ili siku ile usije ukasema sikuambiwa.

Hivyo tubu dhambi zako umgeukie Mungu, akuoshe, ili ushiriki wema wa Mungu na sio ubaya wake.

Kama upo tayari kufanya hivyo leo, basi fungua hapa kwa ajili ya SALA YA TOBA, na Maelekezo mengine >> KUONGOZWA SALA YA TOBA

Bwana akubariki.

Pia Tazama tafsiri ya maneno mengine ya kibiblia chini.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mafundisho mengine

Mada Nyinginezo:

Kiango na Pishi ni nini (Mathayo 5:15)?

Chuo cha vita vya Bwana ni kipi?(Hesabu 21:14)

NAYE AKASIMAMA JUU YA MCHANGA WA BAHARI.

Tofauti kati ya lijamu na hatamu ni ipi kibiblia?

Ngome ni nini?  Kwanini Mungu anafananishwa na ngome?

Ni kwanini mifugo ya Yakobo iliongezeka kwa wingi kiasi kile?

Nyinyoro ni nini?

Rudi nyumbani

Print this post

Kiango na Pishi ni nini (Mathayo 5:15)?

Kiango ni kifaa maalumu cha kushikilia au kuning’inzia taa, tazama picha, kwa jina lingine kinaitwa kinara. Na nilazima kinyanyuke au kiwe sehemu ya juu kidogo, ili kuruhusu mwanga wa hicho kilicho juu yake (yaani taa) kuangaza mahali pote.

kiango

Na Pishi ni bakuli dogo, au kapu ndogo. Tazama picha,

Hivi ni vifungu ambavyo utaweza kukutana na maneno hayo;

Mathayo 5:15 “Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani”.

Marko 4:21 “Akawaambia, Mwaonaje? Taa huja ili kuwekwa chini ya pishi, au mvunguni? Si kuwekwa juu ya kiango”?

Luka 11:33 “Hakuna mtu awashaye taa na kuiweka mahali palipositirika, au chini ya pishi; bali huiweka juu ya kiango, ili waingiao wapate kuuona mwanga”.

Soma pia Luka 8:16

Hivyo mpaka hapo tunaweza kupata picha sasa Bwana Yesu alimaanisha nini kutoa mfano huo, kuwa tunapoamua kuokoka hatupaswi kuuficha wokovu wetu, kuuweka chini ya bakuli bali ni sharti tuungaze kwa watu wote, kwanza kwa matendo yetu na pia kwa kuwahubiria ili kusudi kwamba wavutwe na wao katika wokovu tulionao.

Na ndio maana pale kwenye Mathayo 5:15 akamalizia na kusema..

16 “Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni”.

Shalom.

Tazama maana nyingine ya maneno ya biblia chini.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mafundisho mengine

Mada Nyinginezo:

Bwana Yesu alimaanisha nini aliposema; Mafarisayo Hupanua HIRIZI zao, na kuongeza MATAMVUA yao?

GOGU NA MAGOGU, Katika biblia ni nani?

“Shinikizo” ni nini kibiblia, Na maana yake rohoni ni ipi?

Uga ni nini? Na kazi yake ni ipi kibiblia?

SIFONGO NA SIKI NI NINI?

Rudi nyumbani

Print this post

NAYE AKASIMAMA JUU YA MCHANGA WA BAHARI.

Shalom, jina kuu la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe milele.

Karibu tujifunze Neno lake.

Ukisoma kitabu cha Ufunuo sura ya 12, utaona habari kuu inayouzungumziwa pale ni kuhusu mapambano ambayo aliyafanya tangu akiwa  mbinguni, na anayoendelea kufanya hadi sasa.

Utaona mapambano hayo yamegawanyika katika vipengele vikuu vitatu. Cha kwanza vita ile aliyoifanya mbinguni akiwa na malaika zake, ambayo alishindwa, na matokeo yake akatupwa chini,

Kipengele cha pili utaona ni ile vita aliyoifanya na yule mwanamke aliyemzaa mtoto mwanaume, ambaye nchi ilimsaidia. Na mwanamke yule analiwakilisha Kanisa la Israeli  kwa ujumla. Wakati Bwana Yesu anazaliwa, utaona shetani kwa kupitia Herode alikuwa ameshaanza kuleta maafa Israeli, kwa kuwaaua wale watoto wote waliozaliwa wakati mmoja na Yesu, lengo likiwa ni kumwinda Yesu, afe, Lakini Mungu akamuhamisha Kristo akilimbilie Misri kwa muda, na hiyo ilikuwa ni kulinusuru taifa zima.

Na kipengele  cha tatu na cha mwisho ambayo ndio kiini cha somo letu la leo  Ni vita ambayo shetani aliita kwa uzao wake wote wa huyo mwanamke uliosalia. Yaani wote watakaofanana na Kristo, waisraeli wa rohoni, hao ndio anamalizia kufanya nao vita , na vita hiyo ni endelevu, ilianza  tangu kipindi kile Kristo anaondoka duniani, mpaka leo hii, na itaisha na unyakuo.

Lakini kuna jambo moja la kuona pale, shetani alipoanza kufanya vita na kanisa la Kristo, hakusimama mbinguni tena au nyuma yetu kuleta mafuriko, kama alivyofanya kwa yule mwanamke, hapana, bali biblia inatuambia alikwenda kusimama JUU YA MCHANGA WA BAHARI.

Ufunuo 12:13 “Na joka yule alipoona ya kuwa ametupwa katika nchi, alimwudhi mwanamke yule aliyemzaa mtoto mwanamume.

14 Mwanamke yule akapewa mabawa mawili ya tai yule mkubwa, ili aruke, aende zake nyikani hata mahali pake, hapo alishwapo kwa wakati na nyakati na nusu ya wakati, mbali na nyoka huyo.

15 Nyoka akatoa katika kinywa chake, nyuma ya huyo mwanamke, maji kama mto, amfanye kuchukuliwa na mto ule.

16 Nchi ikamsaidia mwanamke; nchi ikafunua kinywa chake, ikaumeza mto ule alioutoa yule joka katika kinywa chake.

17 Joka akamkasirikia yule mwanamke, akaenda zake AFANYE VITA JUU YA WAZAO WAKE WALIOSALIA, wazishikao amri za Mungu, na kuwa na ushuhuda wa Yesu; NAYE AKASIMAMA JUU YA MCHANGA WA BAHARI”.

Sasa mchanga wa bahari unawakilisha nini?

Hapo inaposema kwenye mchanga wa habari inamaanisha kwenye  ufukwe, yaani alikwenda kusimama ufukweni, mpakani, kati ya habari na nchi kavu. Hii ikiwa na maana vita vyake hasa vipo pale mpakani, kuhakikisha kinachotoka habarini hakiji nchi kavu. Na hata kama kikitokea kimevuka nchi kavu, basi hakitapita hivi hivi tu.

Sasa kibiblia habari au palipo na maji mengi inawakilisha ulimwengu,(Ufunuo 17:15) ..Na nchi kavu ni wokovuni..Bwana Yesu alimwambia Petro njo nami nitakufanya kuwa mvuvi wa watu. Yaani kuwatoa watu kutoka kwenye ulimwengu na kuwaleta katika Nuru ya wokovu,

Hii ikiwa na maana mtu yeyote ambaye hajaokoka, kwamba yupo baharini, hivyo akishaokoka, ni anakuwa anahamishwa kutoka kwenye maji na kuletwa nchi kavu.

Hivyo sasa tunamwona hapa shetani kasimama ufukweni, lengo lake likiwa ni kukipinga kile kinachotoka kule kuja nchi kavu. Kumpinga mtu Yule ambaye anataka kutoka kwenye dunia na kuja katika wokovu. Mtu yule nayetaka kuacha kuishi maisha yake machafu na kuja katika maisha mapya ya utakatifu. Hapo ndipo vita vya ibilisi vilipo haswaa.

Hapo ndipo utakapokutana na shetani, hakuna mahali pengine utamwona ibilisi kwa uwazi wote kama hapo. Ndio vita vyake vilipo. Hatahangaika na wewe ambaye sikuzote upo dhambini, wala hutamwona akikugasi, lakini siku ambapo unafanya uamuzi ndipo utakapomwona akitaka kukusumbua, kama vile alivyotaka kumwangamiza Kristo tu alipozaliwa duniani.

Lakini ni wajibu wetu kumshinda, na tunamshinda kwa damu ya mwanakondoo na kwa Neno la ushuhuda wetu sawasawa na

Ufunuo 12:11 “Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa”.

Hivyo kaa ukijua kuwa pale unapotaka kufanya badiliko la kweli la maisha hapo ndipo pa muhimu sana, na shetani analijua hilo na ndio maana anasimamia hapo, kwahiyo ni wajibu wako kumshinda, haijalishi ataleta vita vya aina gani, Kumbuka hizi ni siku za mwisho, na Bwana Yesu alisema, ufalme wa mbinguni unapatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu ndio watakaouteka. Mathayo 11:12

Kwahiyo huna sababu ya kuanza kuogopa kudharauliwa, au kuchekwa, au kutengwa au kudhihakiwa kisa tu umeamua kuokoka au kuishi maisha ya wokovu. Jitwike msalaba wako umfuate Yesu, ili upokee taji la ushindi ufikapo kule.

Bwana akubariki

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mafundisho mengine

Mada Nyinginezo:

JINSI  DHAMBI ILIVYO NA SHINIKIZO KUBWA SANA.

ROHO ANENA WAZIWAZI

KAMA MKRISTO FAHAMU ZIPO HATUA UTAPIGISHWA NA MUNGU.

JIFUNZE KUTOA KATIKA HAZINA YAKO VITU VIPYA NA VYA KALE.

Rudi nyumbani

Print this post

JINSI  DHAMBI ILIVYO NA SHINIKIZO KUBWA SANA.

Wakati mwingine kuna mambo unasoma kwenye biblia unaishia kuogopa sana, hususani pale unapoona mtu Mungu anafanya mambo ambayo hata mwenye dhambi si rahisi ayafanye. Kwamfano embu tuwaangalie hawa watu wawili, [Daudi na Yuda]. Hawa wote tunajua walikuwa ni watiwa mafuta wa Mungu, tukianzana na Daudi, tunajua alikuwa ni shujaa sana, na katika ushujaa wake, aliweza kuchagua mashujaa wake wengine 37 waaminifu ili kumsaidia katika vita, na kuipigania Israeli.

Lakini katikati ya mashujaa hao kulikuwa na mwingine ambaye alikuwa mwaminifu sana pengine hata Zaidi ya mashujaa wengine wote, na huyo aliitwa Uria. Uaminifu wake tunausoma jinsi ulivyokuwa.. hakuwa tayari kwenda kujiburudisha nafsi yake wakati kazi ya vita haijamalizika, na wenzake wapo bado mapambanoni, haijalishi kuwa ni mfalme ndiye aliyempa ruhusu ya kuondoka, hakuwa tayari kuondoka. 

2Samweli 11:8 “Daudi akamwambia Uria, Haya, shuka nyumbani kwako, ukanawe miguu yako. Basi Uria akatoka katika nyumba ya mfalme, na tunu ya vyakula ikamfuata, iliyotoka kwa mfalme.

9 Lakini Uria akalala mlangoni pa nyumba ya mfalme, pamoja na watumishi wote wa bwana wake, wala hakushuka nyumbani kwake.

10 Watu walipomwambia Daudi ya kwamba, Uria hakushuka nyumbani kwake, Daudi akamwambia Uria, Je! Hukutoka safarini? Mbona hukushuka nyumbani kwako?

11 Naye Uria akamwambia Daudi, Sanduku, na Israeli, na Yuda, wanakaa vibandani; na bwana wangu Yoabu, na watumishi wa bwana wangu, wamepiga kambi waziwazi uwandani; nami niende nyumbani kwangu, kula na kunywa, na kulala na mke wangu? Uishivyo, na kama roho yako iishivyo, mimi sitafanya jambo hili. 12 Basi Daudi akamwambia Uria, Ngoja hapa leo tena, na kesho nitakuacha kwenda zako. Basi Uria akakaa Yerusalemu siku ile, na siku ya pili yake.

13 Naye Daudi akamwalika, akala, akanywa mbele yake; naye akamlevya; hata wakati wa jioni akatoka kwenda kulala kitandani mwake pamoja na watumishi wa bwana wake, lakini hakushuka nyumbani kwake.”

Unaweza ukajiuliza, mtu kama huyu, labda ndio angependwa kipekee na Daudi, na kupewa zawadi nyingi kwa moyo wake huo wa uaminifu na Upendo, lakini kinyume chake Daudi ndio akampangia njama za kumwangamiza. Tena kumwangamiza katika huo huo uaminifu wake.. Na akafanikiwa,  akamuua kwenye vita, pale alipowaambia mashujaa wake wamwache mwenyewe auawe.

Huyo ndio Daudi mtiwa mafuta wa Bwana,  Lakini ni nini kilichompelekea afanye vile, hakufanya vile kwasababu alipenda, bali kwasababu ya shinikizo la dhambi lililokuwa nyuma yake. Na dhambi yenyewe ilianzia pale, alimuona mke wa Uria, akamtamani, kisha akamchukua alale naye, akadhani itaishia pale pale tu, hakujua kuwa madhara Zaidi yanaweza kuja, matokeo yake akapata mimba yule mwanamke, Na Daudi alipoona hivyo akataka kumbambikizia Uria mimba ambayo si yake ,  ili tu kusitiri aibu, ndio maana akampa likizo ya ghafla, ili akalale na mkewe, lakini Uria alikuwa mwaminifu hakukwenda kulala na mke wake, alibaki kambini, ndipo Daudi ikambidi abuni mbinu nyingine ya kusitiri uovu wake, ndipo akaamua kukiua kiungo chake kiteule, kisichokuwa na hatia yoyote. Hilo ndio shinikizo la dhambi.

Mwingine ni Yuda, huyu naye alianza dhambi kidogo kidogo tu, ya wizi, hakujua tamaa hiyo itampelekea kuisaliti damu isiyokuwa na hatia, akadhani  ni mambo rahisi rahisi tu, akaendelea kuwa mwizi, mpaka ikafikia hatua ile dhambi iliyokuwa ndani yake ikamshinikiza, kupata hela nyingi Zaidi na njia pekee ambayo ingempelekea kuipata ni kwa kumsaliti Bwana wake, Mtakatifu ili wale wakuu wa makuhani wampe Hela.

Sasa usidhani kwamba kumsaliti Bwana wake ambaye alijua anampenda upeo, na kumweshimu ilikuwa ni jambo analolifurahia sana, hapana, bali lile shinikizo la dhambi ndio lililompelekea kuchukua maamuzi ambayo yalimletea majuto ya milele.

Yuda alimsaliti Bwana wake, alimsaliti jemedari wake, alimsaliti mwokozi wake aliyependa, kwa dhambi ndogo tu ya kupenda fedha na wizi.

Huoni leo hii watu wanawatoa ndugu zao kafara kwa waganga wa kienyeji, unadhani hawawapendi ndugu zao, wanawapenda lakini lile shinikizo la dhambi ambalo lilianza zamani kama tamaa tu ya mali ndilo lililowafikisha mahali ambapo inawagharimu wafanye hivyo, wasipofanya ndio wamekwisha.

Huoni leo hii mabinti wengi, wanatoa mimba ovyo, kama vile si kitendo cha uuaji wanachokifanya. Usidhani hawawapendi watoto wao, lakini lile shinikizo la dhambi pengine la kukwepa aibu, kukwepa kutengwa, kukwepa kufukuzwa shule, kukwepa  majukumu, linawafanya watende vitendo hivyo vya kinyama kila kukicha.

Hata wewe leo hii usidhani huwezi kumuua mtu kwa kumpiga risasi, usidhani huwezi kufanya mambo ya ajabu kupindukia, usiseme hivyo kama ni mtendaji wa dhambi hizo ambazo unaziona za kawaida tu, unaweza kutenda tena na ukawa ni mnyama kuliko hata magaidi wenyewe, kama utaivumilia dhambi ndani yako, Haijalishi utajiita ni mtumishi wa Mungu.

Dhambi ni ya kuiogopa sana, usiseme yule ni mke wa mtu ngoja nikazini naye  leo tu basi, hakutakuwa na shida yoyote, usijaribu kufanya hivyo ndugu, usiseme ngoja niibe kile kidogo kwenye kampuni, hakitaniletea madhara yoyote, usifanye hivyo.. Dhambi inashinikizo kubwa sana, inakupeleka mahali ambapo huwezi kuchomoka mpaka ufanye kufuru mbaya sana. Laiti Daudi au Yuda angelijua tangu mwanzo kuwa watasababisha damu  zisizo na hatia  kumwagika wasingedhubutu kufanya mambo kama yale.

Lolote unaloliona ni dogo maadamu ni dhambi jiepushe nalo tu, kwa usalama wa maisha yako ya rohoni.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mafundisho mengine

Mada Nyinginezo:

Je mtu anayeua anabeba dhambi zote za yule aliyemuua?

USIINGIE MKATABA NA DHAMBI.

ROHO ANENA WAZIWAZI

Swali: Kurushwa upesi kunakozungumziwa katika Danieli 9:21 ndio kupi?

IFAHAMU HUZUNI NA FURAHA YA MALAIKA.

Rudi nyumbani

Print this post

ROHO ANENA WAZIWAZI

Shalom..Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe.

Neno la Mungu linasema katika…

1 Timotheo 4:1 “Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani”

Maana ya kunena waziwazi ni kwamba…“ananena pasipo maficho yoyote wala pasipo siri yoyote”..yapo mambo ambayo Roho Mtakatifu akiyanena yanahitaji ufunuo mpana kutoka kwake..kwamfano utaona katika kitabu cha ufunuo sehemu kadha wa kadha, anasema “yeye aliye na sikio na asikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa”. Au kwa lugha rahisi ni sawa na kusema “yeye mwenye akili na aweze kuyajua haya yanayozungumzwa maana yake ni nini”..kwamaana inahitajika ufunuo kuyajua.

Kwamfano tunaweza kujifunza mfano mmoja, ambapo Roho hajanena waziwazi.

Ufunuo 2:26 “Na yeye ashindaye, na kuyatunza matendo yangu hata mwisho, nitampa mamlaka juu ya mataifa,

27 naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, kama vyombo vya mfinyanzi vipondwavyo, kama mimi nami nilivyopokea kwa Baba yangu.

28 Nami nitampa ile nyota ya asubuhi.

29 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa”

Hapo Roho kanena..lakini si wazi..kwasababu atakayesoma hajaambiwa nyota ya asubuhi hapo ni nini, wala hajaambiwa hao mataifa atakaowachunga ni wakina nani…maana yake mambo hayo yote yanahitaji ufunuo wa Roho kuyaelewa…hayajanenwa waziwazi..

Lakini katika hiyo 1Timotheo 4 biblia inasema Roho anena waziwazi..kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na Imani, wakisikiliza roho zidanganyazo….na mafundisho ya mashetani..

Hapo anasema wakizisikiliza roho zidanganyazo…na si wakizitazama au wakiziabudu..bali wakizisikiliza..maana yake hizo roho zinazungumza na zipo nyingi.

Sasa hizo zinazungumzaje?

Roho hizi zinazungumza kwa njia kuu mbili.

1. Katika nafsi ya mtu
2. Kupitia watumishi wa shetani, ambao wamevaa mavazi ya kondoo.

1. Katika nafsi ya mtu ni pale mtu anaposikia sauti au msukumo wa kwenda kufanya jambo lililo kinyume na mapenzi ya Mungu.. Kwamfano kama mtu atasikia sauti ikimwambia akatoe mimba, au akaue, au akaibe, akaabudu sanamu au akafanye uasherat, ukavae nguo za nusu uchi, ukapake lipatick, ukavae suruali kwa mwanamke, ukaende kwa waganga, ukaachane na mke wako/mume wako wa ndoa..n.k.kama akiisikiliza hiyo sauti na kwenda kufanya mojawapo ya hayo tayari atakuwa kasikiliza roho hiyo idanganyayo.

2. Vile vile kama atamsikia mtu au mhubiri akimshawishi kufanya mojawapo ya mambo hayo hapo juu tayari, na kwenda kufanya kama alivyosikia kutoka kwa huyo mtu au mhubiri, tayari atakuwa ameisikiliza roho hiyo na imeshamdanganya, aidha kwa kujua au kwa kutokujua..kupitia huyo mhubiri.

Hivyo Roho anatuambia waziwazi kuwa nyakati za mwisho ambazo ndizo hizi watu wengi sana watakuwa wanazisikiliza hizi roho..na si wachache bali ni wengi..Hivyo ni wajibu wetu kuwa macho,na kuwa makini sana ili tusiwe miongoni mwa hao “wengi”…ndio maana ametuambia waziwazi ili tujue hali halisi, na tuweze kujilinda.

Huu ni wakati wa kuzichunguza sana roho..niliwahi kukutana na mtu akaniambia ameokoka na anaamini sana sauti yoyote inayomjia ndani yake ni ya roho mtakatifu..Nikamuuliza anatumia nini kuipima hiyo sauti.. akasema anatumia hisia tu…hivyo hawezikudanganyika.
Ndugu hata uwe mhubiri mkubwa kiasi gani, hata uwe unanena kwa lugha, hata uwe unatabiri, au unaona maono, hata uwe kila siku unatembelewa na malaika..roho za yule adui yetu shetani hazichunguzwi kwa ujuzi au utaalamu au uzoefu fulani au kwa hisia..hapana!! bali zinachunguzwa kwa Neno la Mungu tu..

Maana yake ni kwamba hata kama nimeokoka sio kila sauti inayokuja ndani yangu ni ya kuiamini, bali ni lazima ipimwe na neno la Mungu..kama inakubaliana na Neno hiyo ni sauti kutoka kwa Mungu..lakini kama inapingana na Neno, haijalishi imekuja kwa nguvu kiasi gani, au umekuja na amani kiasi gani, au imekuja na hisia nzuri kiasi gani…hiyo si ya kuifuata ni sauti kutoka kwa yule adui. Biblia inasema..

2 Wakorintho 11:14 “Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru”.

Na neno la Mungu tunalijua kwa kusoma biblia kwa bidii sana…hiyo ndiyo silaha.
Kumbuka tena usisahau neno hili… Roho anena waziwazi, kuwa nyakati za mwisho wengi watajitenga na Imani, na kusikiliza roho zidanganyazo… ni maombi yangu kuwa mimi na wewe hatutakuwa miongoni mwa hao “wengi”.

Kama hujampokea Yesu mpaka sasa, kwasababu fulani fulani, unazozijua wewe, fahamu kuwa umeshasikiliza roho hizo na zimekudanganya…Hivyo fungua leo macho yako na mgeukie Kristo uanze upya, naye atakupokea na kukusaidia kwasababu anatamani wewe uwe na uzima kuliko wewe unavyotamani.

Maran atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mafundisho mengine


Mada Nyinginezo:

MAFUNDISHO YA MASHETANI

JIEPUSHE NA MANENO YA MANABII WA UONGO.

JIHADHARI NA UONGO WA SHETANI UNAOKARIBIANA NA UKWELI.

ROHO YA MPINGA KRISTO IKITENDA KAZI SIKU HIZI ZA MWISHO

JINSI SHETANI ANAVYOZUIA MAJIBU YA MAOMBI YETU.

Rudi nyumbani

Print this post

UTENDAJI KAZI MWINGINE WA ROHO MTAKATIFU USIOUFAHAMU.

Ulishawahi kujiuliza ni kwanini Roho Mtakatifu alicheleweshwa kushuka juu ya mitume ikawachukua muda mrefu  kidogo, Na hata baada ya Yesu kufufuka tunaona iliwapasa tena kungojea kwa muda wa siku 50? Ulishawahi kujiuliza ni kwanini? Sio kwamba walikuwa hawastahili kupokea Roho Mtakatifu tangu zamani, hapana lakini ndio tabia ya Roho Mtakatifu aliyojiwekea, na anafanya hivyo kwasababu zake maalumu.

Hawi mwepesi sana kushuka juu ya mtu kwa haraka kwasababu anajua akishashuka huwa hashuki kwa kipimo au nusunusu, au kuchunguza chunguza. Na ndio maana Bwana Yesu alisubiri kwanza, wanafunzi wake wakamilishwe katika madarasa yake, ili kusudi kwamba watakaposhukiwa na Roho kile kilicho ndani yao kitendeke kwa ufasaha ziadi kama kilivyokusudiwa.

Roho Mtakatifu anafananishwa na MVUA,  Na kama tunavyojua mvua sikuzote ikishuka huwa haichagui hapa kuna ngano au magugu, au mboga, au bangi, au mbigili kazi yake ni kwenda kustawisha tu, hiyo ndio kazi yake. Hivyo ni wajibu wa mwenye shamba kuhakikisha kitu alichokipanda shambani kwake ni chenye manufaa, ahakikishe shamba lake amelipalilia vya kutosha, kwamba hakuna mbegu za magugu chini ya ardhi,vinginevyo itakuwa ni kwa hasara yake mwenyewe pale mvua itakaponyesha na kustawisha magugu badala ya chakula.

Na ndivyo Roho Mtakatifu alivyo, anaposhuka juu ya mtu au kanisa, huwa anakuza au kukiwezesha kile ambacho kimeshapandwa ndani yake. Na ndio maana anaitwa msaidizi, Sasa Kama ulitubu dhambi zako, ukawa unaishi maisha matakatifu, ukawa unabidii katika kumtafuta Mungu, basi Roho akija juu yako, anaikuza hiyo mbegu iliyopo ndani yako, kuwezesha kumjua Mungu zaidi na kuishi hayo maisha kwa viwango vingine vya juu sana.

Na ndio hapo atakuongezea vipawa na karama ili kuhakikisha unafikia pale ambapo umepakusudia na Mungu ufike na hata zaidi. Lakini pale atakaposhuka juu yako, na bado haujajiweka tayari kwa Mungu, kinyume chake, ni mzinzi, au unayo mambo yako ya kidunia, na bado unasema ni  mkristo, atakuja kweli na akija hatakufanya uwe mtakatifu bali atakufanya uwe mwovu zaidi. Hapo ndipo wengi wetu hatujui. Tendo hili katika biblia sehemu nyingine imeitwa “nguvu ya upotevu” itokayo kwa Mungu.. Soma 2Wathesalonike 2:10-12

Utajiuliza ni wapi tena jambo  hilo tena utalipata katika biblia,  Embu vitafakari  hivi vifungu, hususa ni hivyo vilivyo katika herufi kubwa.

Waebrania 6.4 “Kwa maana hao waliokwisha kupewa nuru, na kukionja kipawa cha mbinguni, na kufanywa washirika wa Roho Mtakatifu,

5 na kulionja neno zuri la Mungu, na nguvu za zamani zijazo,

6 wakaanguka baada ya hayo, haiwezekani kuwafanya upya tena hata wakatubu; kwa kuwa wamsulibisha Mwana wa Mungu mara ya pili kwa nafsi zao, na kumfedhehi kwa dhahiri.

7 MAANA NCHI INAYOINYWA MVUA INAYOINYESHEA MARA KWA MARA, NA KUZAA MBOGA ZENYE MANUFAA KWA HAO AMBAO KWA AJILI YAO YALIMWA, HUSHIRIKI BARAKA ZITOKAZO KWA MUNGU;

8 BALI IKITOA MIIBA NA MAGUGU HUKATALIWA NA KUWA KARIBU NA LAANA; AMBAYO MWISHO WAKE NI KUTEKETEZWA”.

Embu jiulize upo katika kanisa muda mrefu, unasema umeokoka, unasali, unafanya ushirika, unaimba kwaya n.k. lakini bado una maisha ya dhambi ya siri  unayoyajua wewe.. Unatazamia nini pale Roho Mtakatifu atakaposhuka juu yako au juu ya kanisa, upaliliwe kitu gani?

Roho Mtakatifu anaposhuka ndani ya kanisa lake kulinyeshea mvua, halafu anakukuta, wewe ni gugu umepandwa ndani yake, ujue kuwa mvua hiyo itaistawisha gugu, lizidi kustawi zaidi ili siku ya kuteketezwa na kutupwa motoni likapate adhabu iliyokubwa zaidi. Ili kutimiza andiko hili;

Mathayo 13:24 “Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake;

25 lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake.

26 Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu.

27 Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi magugu?

28 Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, Basi, wataka twende tukayakusanye?

29 Akasema, La; msije mkakusanya magugu, na kuzing’oa ngano pamoja nayo.

30 Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu”.

Kumbuka kilichomfanya mfalme Sauli ashukiwe na Roho mbaya kutoka kwa Mungu, ni tabia yake ya wivu na ile ya kudharau maagizo ya Mungu, hivyo ile Roho njema ya Mungu iliposhuka juu yake na kukutana na tabia yake mbaya, ndio ikamfanya awe mbaya, kutaka kumwangamiza Daudi. Lakini kama angekuwa ni mtiifu kwa Mungu na mwenye upendo, Roho ya Mungu ingekutana na tabia hiyo njema na kumfanya kuwa mfalme Hodari zaidi na mshupavu kama alivyokuwa hapo mwanzoni. Hiyo ndio sababu kwanini biblia ilikuwa inasema “Roho mbaya kutoka kwa Mungu” ilikuwa inamjia Sauli..Hizi ndio sababu.(1Samweli 16:14-23)

Hata sasa, tunapaswa tujiangalie sana mienendo yetu katika kanisa, wapo watu baada ya kukaa kanisani   ndio wamezidi kuwa wabaya zaidi, wanafanya mambo ambayo hata watu wa kidunia hawafanyi, kama ulikuwa hujui sababu ndio hii. Sasa usidhani mtu kama huyo alianza tu kuwa mbaya, hapana, bali alidharau maagizo ya Mungu, akawa anafanya mambo yasiyofaa kidogo kidogo hivyo hivyo, na mwisho wa siku akajikuta anayafanya kwa nguvu zaidi,..Hajui kuwa tayari kashapotea milele, Na biblia inasema mtu akishafikia hatua hiyo, hawezi kufanywa upya tena atubu, anasubiria kwenda tu katika ziwa la moto. Kwahiyo tujitathimini ni mbegu za aina gani zipo ndani yetu. Ili tuwe na amani pale Roho anaposhuka juu yetu, kutuwezesha zaidi.

Tukipanda mbegu njema katika utakatifu, Roho Mtakatifu atatufanya kuwa watakatifu zaidi, tukipanda katika imani,atatuongezea imani zaidi, tukipanda katika upendo vivyo hivyo, katika kulitafakari Neno lake, atatuongezea mafunuo mengi zaidi n.k. Huo ndio uzuri wa Roho Mtakatifu, ndio maana anaitwa msaidizi.

Yohana 16:13 Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.

Hivyo katika hili eneo tunapaswa tuwe makini sana, hata Bwana Yesu alituonya hivyo. Ni heri ukafanya mizaha katika mambo ya kidunia, lakini sio ndani ya kanisa la Kristo. Kwasababu huko ndani Roho Mtakatifu yupo kuwezesha watu, kwahiyo angalie zisije zikawa ndio dhambi zako zinawezeshwa huko.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mafundisho mengine

Mada Nyinginezo:

JINSI ROHO MTAKATIFU ANAVYOWAFUNULIA WATU MAANDIKO.

NI KWA NAMNA GANI ROHO HUTUTAMANI KIASI CHA KUONA WIVU?

AOGOPACHO MTU ASIYE HAKI NDICHO KITAKACHOMJILIA.

MTEGO HUTEGWA BURE, MBELE YA MACHO YA NDEGE YE YOTE.

Rudi nyumbani

Print this post

MKESHA WA KUINGIA MWAKA MPYA KILA MWAKA NI WA KUUTHAMINI SANA.

Leo  tutaona kibiblia ni kwanini uuthamini mkesha wako wa kuingia mwaka mpya. Wengi wetu tunapuuzia, tunaona ni jambo la kawaida tu, na hivyo tunautumia msimu huu pengine kulala, au kwenda kufanya anasa, au kwenda kufanya part na ndugu au marafiki n.k.. Ni heri upange kwenda kusheherekea nao siku inayofuata kuliko siku ya mkesha wa kuukaribisha mwaka mpya.

Lipo jambo kubwa sana la kiroho katika usiku wa siku hiyo.

Ukisoma biblia utaona Mungu alipokuwa anawatoa wana wa Israeli Misri, siku hiyo  kwao ndio ilikuwa siku ya kwanza ya mwaka wao mpya.. Lakini utaona Mungu hakuwatoa mchana, au jioni, au alasiri bali aliwatoa usiku wa manane,  Sio kwamba mchana wasingeweza kusafiri, hapana, lakini siku ya kutengwa na maadui zako, na siku ya kuukaribisha mwaka mpya sikuzote ni lazima maandalizi yaanzie angali bado kuna giza nene.

Utasoma usiku ule kabla ya kuamkia tarehe moja, walimla yule pasaka(mwanakondoo), wakiwa wamevaa viatu vyao chini, kiashirio kuwa wapo mbali na vitanda vyao, na huku wamefunga mikanda yao viunoni, kuashirio kuwa wapo tayari kwa safari, kisha wamejifungia ndani wakimtafakari Mungu na kumwimbia, wakisubiria tu muda ufike wa kuondoka..

Kutoka 12: 11 “Tena mtamla hivi; mtakuwa mmefungwa viuno vyenu, mmevaa viatu vyenu miguuni, na fimbo zenu mikononi mwenu; nanyi mtamla kwa haraka; ni pasaka ya Bwana.

12 MAANA NITAPITA KATI YA NCHI YA MISRI USIKU HUO, NAMI nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; Mimi ndimi Bwana”.

Kwasababu walifahamu wanaingia katika mwaka wao mpya wa kufanywa huru mbali na maadui zao. Sasa embu fikiria kama wangekuwa wamelala, halafu asubuhi ndio wanaamka watake kuondoka Misri, hali  ingekuwaje? Ni wazi wasingetoka kwa ushindi mnono kama walivyotarajia.

Vivyo hivyo na sisi, siku kama ya leo, ndio tunavuka kuingia mwaka mpya. Usiku ambao tunayaacha mambo ya mwaka huu, na kuyakaribisha mambo ya mwaka mwingine mpya, Hivyo kama tunataka  Mungu ampige adui yetu shetani kwelikweli, ili mwaka wetu mpya tunapouanza uwe wa kuwa huru, na wa Baraka nyingi na wa mafanikio, hatuna budi leo kukesha nyumbani mwake, katika kuomba, kumwabudu na kumfanyia ibada.

Yaani tarehe moja ya mwaka mpya isikukute upo kitandani, isikukute unaangalia MUVI, isikukute unacheza gemu, isikukute unazurura zurura mtaani, isikukute unapiga piga stori na marafiki zako n.k., bali ikukute nyumbani mwa Bwana unamshukuru na kumtukuza.

Hata kama upo katika nchi ambazo, ibada zimekatazwa makanisani, bado unayo nafasi ya kujifungia mwenyewe nyumbani na familia yako ukawa unaomba na kumshukuru Mungu, kama wana wa Israeli walivyofanya. Hakikisha kuwa mwaka wako mpya unaukaribisha ukiwa macho kwa Bwana.

Itakuwa ni ajabu sana, kama mwaka huu utashindwa kumshukuru Mungu kwa wema wake aliokutendea mwaka mzima..Wewe mwenyewe unajua mambo tuliyoyapitia mwaka huu jinsi yalivyokuwa mazito , lakini umepewa neema ya kuyavuka, ujue sio kwa nguvu zako,wala fedha zako, wala afya yako wala chochote ulicho nacho.

Hivyo utumie mkesha huu, vema kwasababu hakutakuwepo tena na mwingine kama huu, kwa miezi mingine 12 ijayo. Bwana akubariki

Pia wakumbushe na wengine, jambo hilo. Na shea kwa wengine.

Mwisho kabisa, nikutakie HERI YA MWAKA MPYA WENYE MAFANIKIO YOTE YA MWILINI NA ROHONI KATIKA JINA LA BWANA YESU KRISTO.

AMEN.

Mawasiliano/ Whatsapp: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

NAKUTAKIA HERI YA MWAKA MPYA!

UNAMALIZAJE MWAKA WAKO, JE NA MUNGU AU SHETANI?

NJIA MUNGU ALIYOIWEKA KWA KILA JAMBO.

THAWABU ZA SIRI, ZA WATAKATIFU MBINGUNI.

Rudi nyumbani

Print this post