UFUNUO Mlango wa 2: Sehemu ya kwanza.

UFUNUO Mlango wa 2: Sehemu ya kwanza.

(Sehemu ya kwanza)

Jina kuu la BWANA wetu YESU KRISTO litukuzwe milele yote. Karibu katika mwendelezo wa uchambuzi wa kitabu cha Ufunuo, Leo tutaitazama ile sura ya pili. Kama tulivyotangulia kusoma katika ile sura ya kwanza, Tuliona Yohana akionyeshwa Sura na umbo la YESU KRISTO , na wasifa wake ambao alionyeshwa kwa lugha ya picha,(Kumbuka Bwana Yesu kiuhalisia hana muonekano kama ule), jinsi alivyokuwa anaonekana na nywele nyeupe kama sufu, macho ya moto, miguu ya shaba, upanga unaotoka kinywani mwake, mwenye sauti kama maji mengi, aendaye katikati ya vile vinara saba vya dhahabu n.k. hizo zote zilisimama kama viashiria (Nembo) vya tabia yake, ambayo kila moja ina nafasi yake katika hichi kitabu cha Ufunuo na ndio maana zilitangulizwa kuelezwa mwanzoni kabisa mwa kitabu hichi.

Hivyo katika sura ile ya kwanza mwishoni tuliona jinsi Yohana anaambiwa ayaandike yale aliyoyaona na ayapeleke kwa yale makanisa saba. 

Ufunuo 1: 19 Basi, uyaandike mambo hayo uliyoyaona, nayo yaliyopo, na yale yatakayokuwa baada ya hayo.

20 Siri ya zile nyota saba ulizoziona katika mkono wangu wa kuume, na ya vile vinara saba vya dhahabu. Zile nyota saba ni malaika wa yale makanisa saba; na vile vinara saba ni makanisa saba.”

Ni muhimu kufahamu Barua hizi Yohana alizopewa hazikuyahusu tu yale makanisa 7 yaliyokuwa Asia ndogo kwa wakati ule, bali pia na kwa makanisa yatakayokuja huko mbeleni na ndio maana hapa anaambiwa ayaandike mambo hayo YALIYOPO na YATAKAYOKUJA baada ya hayo. Ikiwa na maana kuwa yale yaliyoko ndio yale makanisa 7 yaliyokuwa Asia katika wakati wa Yohana, na yale yatakayokuja ni Makanisa 7 tuliopo sisi baada ya Yohana kuondoka. Kwahiyo Tunaposoma leo hii kitabu cha ufunuo tunajua kuwa yale makanisa 7 yaliyokuwa katika kipindi cha Yohana yameshapita. Na tangu kipindi cha Bwana YESU kuondoka hadi sasa ni takribani miaka 2,000 na kanisa la Kristo limekuwa likipita katika vipindi tofauti tofauti saba ndani ya huo muda wa miaka 2000, vijulikanavyo kama NYAKATI SABA ZA KANISA.

Sasa tukirudi katika sura ya pili. Tunaona Bwana Yesu akianza kutoa ujumbe kwa kanisa moja baada ya lingine, Kuanzia kanisa la Efeso mpaka Laodikia ambalo ndio la mwisho. Tunasoma;

KANISA LA EFESO:

Ufunuo 2:1 “Kwa malaika wa kanisa lililoko Efeso andika; Haya ndiyo anenayo yeye azishikaye hizo nyota saba katika mkono wake wa kuume, yeye aendaye katikati ya vile vinara saba vya dhahabu”.

Awali ya yote tunaona Bwana Yesu anajitambulisha hapa kama “yeye aendaye katikati ya vile vinara saba vya dhahabu na aliyeshika zile nyota saba”. Kumbuka hapa hajajitambulisha yeye kama yeye mwenye macho ya moto au uso ung’aao kama jua. Lakini alisema yeye aendaye katikati ya vile vinara saba vya dhahabu ikiwa na maana kuwa uelekeo wake wote utakuwa katika kuchunguza kinara cha hilo kanisa na yale makanisa mengine. Kumbuka kinara ni taa iliyokuwa inawekwa katika nyumba ya Mungu (Hekaluni) Kwa ajili ya kutia Nuru kule ndani (Patakatifu) ili shughuli za kikuhani ziende sawasawa (Kutoka 27:20), na kilikuwa hakizimwi muda wote, sharti ni lazima kimulike daima usiku na mchana pasipo kuzimwa. Vivyo hivyo hapa Bwana alipoanza kwa kujitambulisha hivyo alikuwa anatazamia nuru isiyozimika ndani ya hilo kanisa husika (nyumba yake) ambalo analitolea habari zake hapo chini.

Siri ya zile nyota saba ulizoziona katika mkono wangu wa kuume, na ya vile vinara saba vya dhahabu. Zile nyota saba ni malaika wa yale makanisa saba; na vile vinara saba ni makanisa saba.
(katika nyumba ya Bwana kinara cha taa kilikuwa na mirija/matawi saba, na kilikuwa kinatia nuru nyumba ya Mungu daima)

Na NURU hii ni ipi Bwana aliyokuwa aliitazamia kuiona inaangaza?. Biblia inatuambia

1Yohana 2: 8 Tena nawaandikia amri mpya, neno lililo kweli ndani yake na ndani yenu; kwa kuwa giza linapita na ile nuru ya kweli imekwisha kung’aa.

9 Yeye asemaye kwamba yumo NURUNI, naye amchukia ndugu yake, yumo gizani hata sasa.

10 Yeye ampendaye ndugu yake, akaa katika nuru, wala ndani yake hamna kikwazo.

11 Bali yeye amchukiaye ndugu yake, yu katika giza, tena anakwenda katika giza, wala hajui aendako, kwa sababu giza imempofusha macho.

Na pia tukisoma 1Wakorintho 13 inasema Upendo huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote, Upendo haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli n;k. Hivyo kwa ujumla NURU ni UPENDO. Ambao huo unaanza kwanza kwa KUMPENDA BWANA MUNGU WAKO kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote na kwa akili zako zote,na kwa nguvu zako zote, (Kwa kuzishika na kuzifuata amri zake) na pia kumpenda jirani yako kama nafsi yako. Kwa kuzingatia hayo mawili KINARA CHAKO kitakuwa kinatoa Nuru ya kutosha.

Sasa tukirudi katika Kanisa lile la EFESO, tunaona Bwana aliendelea kulitolea habari zake na kusema:

Ufunuo 2:2-5 “Nayajua matendo yako, na taabu yako, na subira yako, na ya kuwa huwezi kuchukuliana na watu wabaya, tena umewajaribu wale wajiitao mitume, nao sio, ukawaona kuwa waongo;

3 tena ulikuwa na subira na kuvumilia kwa ajili ya jina langu, wala hukuchoka.

Lakini nina neno juu yako, ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza.

Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu.

6 Lakini unalo neno hili, kwamba wayachukia matendo ya Wanikolai, ambayo na mimi nayachukia.”

Kwanza kabisa maana ya neno EFESO ni “Kuacha mema yaondoke”. Hivyo hili kanisa kama jina lake lilivyo mwanzoni lilianza kuenenda katika Nuru ya Neno ambao ni UPENDO wa kiungu, lilikuwa japokuwa linapitia majaribu mengi liliendelea kumpenda Mungu, lilivumilia mabaya,Hii tunaona katika utawala wa Rumi chini ya kiongozi mkatili Nero, aliyewaua wakristo wengi wakati ule kwa kuwasingizia kuwa wameuchoma mji na hali sio wao. Kanisa hili pia mwanzoni lilijiweka katika utakatifu wa hali ya juu, liliwapima manabii wa uongo na kugundua kuwa sio, kwa muda mrefu sana. Walikuwa na uwezo pia wa kuyagundua matendo ya WANIKOLAI na kuyapinga katikati ya Kanisa. Kumbuka neno “Nikolai” tafsiri yake ni “Kuteka madhabahu” Hivyo kulikuwa na tabia zilizokuwa zimeanza kujitokeza katikati ya baadhi ya makanisa, watu(wasio wa Mungu) walianza kijipachikia vyeo vilivyoua uongozi wa Roho Mtakatifu. kwamfano watu badala ya kwenda kumuomba Mungu msamaha, walianza kuwafuata wanadamu wenzao wawaombee au wawaondolee dhambi zao kwa niaba ya Mungu, Badala karama za roho ziongoze kanisa, vyeo vya kibinadamu vikaanza kuongoza kanisa n.k. Huku ndiko kuteka madhabahu na hayo ndiyo yaliyokuwa matendo ya Wanikolai, ambayo kanisa la Kristo la kweli lilichukizwa nayo na Bwana vilevile.

Lakini Kanisa hili la Efeso lilifikia kipindi ule upendo waliokuwa nao hapo kwanza ukaanza kupoa (wakaanza kuacha mema yaondoke katikati yao kama vile Jina la kanisa lao lilivyo), uvumilifu kwa ajili Imani, utakatifu na subira vikaanza kupoa, zamani walikuwa wanawajaribu manabii wa uongo na kuwaondoa katikati yao lakini sasa hawafanyi hivyo tena.. Na ndio maana Bwana hapa anatokea na kuanza kukichunguza kinara chao na kuwaambia NURU yao imeanza kufifia na kukaribia kuzima Ukiendelea kusoma utaona Bwana anawaambia watubu 

” 5 Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye MATENDO YA KWANZA. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu.”

Kama tulivyoona Pale mwanzoni katika ile sura ya kwanza juu ya ule mwonekano wake, jinsi alivyoonekana akipita katikati ya vile vinara vya taa, ikiwa na maana kuwa anapeleleza na kufanya masahihisho, kinara kilichofifia na kukaribia kuzima anakiondoa na kile kinachozidi kuwaka anakiongezea nuru, kwasababu biblia inasema “mwenye nacho ataongezewa asiye nacho hata kile kidogo alicho nacho atanyang’anywa” Hivyo kama wasingeimarisha matendo yao, hata ile nuru waliyokuwa nayo kidogo ingeondolewa kwao. Na ile taabu yao ya mwanzo waliyoisumbukia ingekuwa ni sawa na bure.

Sasa kanisa hili la Efeso lenye tabia hizi lilianza kati ya kipindi cha 53WK hadi mwaka 170WK. Na Malaika wa kanisa hilo alikuwa ni Mtume Paulo. Kumbuka Neno “malaika” tafsiri yake ni “mjumbe”  hivyo wapo wajumbe wa kimbinguni(ndio malaika wa rohoni) na wapo wajumbe wa duniani. Hawa wanaotajwa katikati ya haya makanisa saba ni wajumbe wa kiduniani (yaani wanadamu). Kwahiyo malaika wa Kanisa hili la Efeso alikuwa ni Mtume Paulo. Kwasababu yeye ndiye mtume aliyepewa neema ya kupeleka Injili kwa mataifa. Na mafunuo mengi aliyopewa yalikuwa ni msingi katika makanisa ya wakati ule, na hata sasa.

Kadhalika na sisi tuliopo katika Kanisa la mwisho (Laodikia) ambalo tutakuja kusoma habari zake hapo baadaye na sisi pia tunaonywa tusipotubu kinara chetu kitaondolewa.. Kumbuka BWANA pale anaonekana akipita katikati ya vile vinara saba na sio “Kinara kimoja“. Hivyo anavichunguza vyote kuanzia cha kwanza mpaka cha mwisho. Na kama asipoiona ile nuru aliyoikusudia iwepo katika kinara chetu vile vile kitaondolewa.. Na tunafahamu madhara ya Nuru kuondolewa, anamaanisha giza linaachiliwa liingie ndani yako.

Ndugu Mwanzoni ulipoanza kuamini ulikuwa mtakatifu lakini sasa hivi utakatifu wako umepoa, ulikuwa unasali, ulikuwa unavaa vizuri, ulikuwa na huruma kwa ndugu, ulikuwa na upendo, ulikuwa na uvumilivu juu ya imani yako hata kama watu wanaokuzunguka wanakudhihaki, ulikuwa huwezi kuabudu sanamu au kuchukuliana na mafundisho ya uongo lakini sasahivi unayapokea mafundisho ya uongo na kuyafurahia, Injili zisizokufanya utazama ufalme wa mbingu ndio unazozipenda, huwezi tena kusali, kujisitiri huwezi tena, hukutazamii tena kuja kwa Bwana umechoka na kuishiwa nguvu. Hizo ni dalili za Kinara chako kuzima..Jitahidi kabla hakijaondolewa. Maana siku kitakapoondolewa ndugu hali yako ya mwisho itakuwa mbaya kuliko ile ya kwanza. Ule upendo uliokuwa nao kwanza wa Mungu unaondoka kabisa ndani yako, unafanana tena na watu wasiomjua Mungu, au unakua kama vile mtu ambaye hajawahi kumjua Mungu kabisa.

Hivyo tujitahidi na sisi TAA zetu ziwe zinawaka katika hizi siku za kumalizia kwasababu Bwana hivi karibuni anarudi.. yeye mwenyewe alisema; katika Luka 12: 35 Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na TAA ZENU ZIWE ZINAWAKA; 36 nanyi iweni kama watu wanaomngojea bwana wao, atakaporudi kutoka arusini, ili atakapokuja na kubisha, wamfungulie mara.”

Ubarikiwe sana.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Endelea hapo chini sehemu ya pili ya sura hii ya pili ya kitabu cha Ufunuo,.ambapo tutakuja kuona ujumbe wa kanisa la pili (SMIRNA).

Tafadhali “Share” kwa wengine ujumbe huu na Mungu atakubariki.

1.Ufunuo: Mlango wa 2: Sehemu ya 2

Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
5 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Hosea
Hosea
1 year ago

Mungu aendelee kukutumia mtumishi.

Anonymous
Anonymous
2 years ago

Mungu wa Israel akuonekanie mwalimu wetu

Kifaru Malale
Kifaru Malale
3 years ago

Mungu akubariki Mtumishi wa mungu…..