Jina la Bwana na mwokozi wetu, Mkuu wa uzima, Mfalme wa wafalme, Yesu Kristo libarikiwe.
Hajawahi kutokea duniani Mtu wa muhimu, na wa Baraka kama Yesu. Leo tutaangalia kwa sehemu, ni jinsi gani ni wa muhimu kwetu.
Je unajua kwa undani ni kwanini maandiko yanasema, Bwana Yesu alipigwa kwaajili yetu?
Isaya 53:5 “Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona”
Sio kwamba Mungu alikuwa anataka kutuhukumu ndio akaona amtafute mwanae aje kufa kwa ajili yetu Hapana! Ni kwamba tayari Mungu alikuwa ameshatuhukumu, adhabu ilikuwa imeshapitishwa.. ilikuwa ipo njiani kutufikia, na ndipo Bwana Yesu akaingilia kati kufa kwaajili yetu.
Ni sawa na mtu ambaye tayari amesharusha jiwe kumlenga mwingine, na lile jiwe wakati lipo njiani kumfikia mlengwa, anatokea mwingine kukubali kupigwa kwa niaba ya Yule aliyekusudiwa kupigwa jiwe hilo. Ndicho Bwana Yesu alichokuja kukifanya.. Hakuja kuifuta hukumu, bali alikuja kuichukua ile hukumu na kuwa yake.. ndio maana ilikuwa hana budi afe!..
Hivyo Kile kifo hakikuwa cha kwake, hakukusudiwa yeye, kilikuwa ni chetu tulikusudiwa sisi, ile aibu haikuwa ya kwake ilikuwa ni yetu!… Yale maumivu hakukusudiwa yeye, tulikusudiwa sisi, kifo cha mateso hakukusudiwa yeye, tulikusudiwa sisi.. Maana yake ni kwamba endapo, Mwokozi Yesu asingetokea.. ni kipindi kifupi sana mbele yetu kilikuwa kimebaki.. ghadhabu ya Mungu ingetumaliza wote, tungekufa kikatili na kwa aibu kama watu wa gharika, na sodoma na ghomora, tungesikitika, na kulia, na kuhuzunika, na kuteseka kwa maumivu, na hatimaye kufa na kuishia katika lile ziwa la moto.
Isaya 53:4 “Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa.
5 Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.
6 Sisi sote kama kondoo tumepotea; Kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe; Na Bwana ameweka juu yake Maovu yetu sisi sote”.
Kumbuka hapo maandiko yanaposema “Ameyachukua masikitiko yetu”.. haimaanishi magonjwa yetu, wala shida zetu, wala huzuni tulizo nazo sasa, wala masikitiko tuliyonayo… La! Haimaanishi hivyo, (ingawa si kosa kutafsiri hivyo), lakini maana yake ya awali kabisa sio hiyo bali inamaanisha zile huzuni ambazo tungezipata baada ya sisi kupigwa na Bwana, na yale masikitiko ambayo tungeyapata baada ya kuipata ile adhabu ya Mungu.. yeye ndiyo kayachukua hayo.. yeye ndio atahuzunika badala yetu baada ya kupigwa na Mungu, yeye ndiye atasikitika katika kuadhibiwa kule.. hiyo ndio maana ya kubeba masikitiko yetu..
Ndio maana kuna mahali Bwana Yesu alisema “nina huzuni nyingi kiasi cha kufa, Marko 14:34”
Umeona umuhimu wa Yesu kwetu?… Je unamthamini Bwana?.. bado tu hujaona umuhimu wa Yesu maishani mwako?
Kumbuka ghadhabu ya Mungu bado ipo, tena ina nguvu mara dufu kwa wale wote wanaoidharau kazi ya msalaba..
Waebrania 10:29 “Mwaonaje? Haikumpasa adhabu iliyo kubwa zaidi mtu yule aliyemkanyaga Mwana wa Mungu, na kuihesabu damu ya agano aliyotakaswa kwayo kuwa ni kitu ovyo, na kumfanyia jeuri Roho wa neema?”
Umempokea Yesu?.. Kama bado unasubiri nini?.. kumbuka mlango wa neema hautakuwa wazi milele.. ingia leo ndani ya safina, kwa kutubu dhambi zako zote, ukimaanisha kuziacha na ubatizwe ubatizo sahihi wa maji tele na kwa jina la Yesu Kristo, na upokee kipawa cha Roho Mtakatifu.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
TABIA YA WAZI INAYOWATOFAUTISHA MANABII WA UONGO NA WALE WA UKWELI.
Kuna mahali Bwana wetu Yesu alisema maneno haya..
Ufunuo 16:15 “ (Tazama, naja kama mwivi. HERI AKESHAYE, NA KUYATUNZA MAVAZI YAKE, ASIENDE UCHI HATA WATU WAKAIONE AIBU YAKE.)”
Umewahi kujiuliza ni kwanini, Bwana aseme heri akeshaye “na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi”?.
Katika hali ya kawaida mtu hawezi kutoka mahali na kwenda uchi labda awe na matatizo ya akili, lakini kwa mtu mwenye akili timamu, haiwezekani kutoka nje akiwa uchi na kutembea hivyo barabarani na watu kumwona..
Lakini Bwana alivyosema hayo, alikuwa na maana!. Kwamba inawezekana pia mtu kutoka nje akiwa uchi, na watu kuiona aibu yake. Endapo atakuwa yupo katika mazingira Fulani.. Hebu tusome kisa kimoja kwenye biblia kisha tuendelee mbele.
Marko 14:48 “Yesu akajibu, akawaambia, Je! Ni kama juu ya mnyang’anyi mmetoka wenye panga na marungu, kunitwaa mimi?
49 Kila siku nalikuwa mbele yenu hekaluni nikifundisha, msinikamate; lakini haya yamekuwa ili maandiko yapate kutimia.
50 ndipo wakamwacha, wakakimbia wote.
51 NA KIJANA MMOJA ALIMFUATA, AMEJITANDA MWILI WAKE NGUO YA KITANI; WAKAMKAMATA;
52 NAYE AKAIACHA ILE NGUO YA KITANI, AKAKIMBIA YU UCHI”.
Umeona mazingira kama hayo?.. Kijana alikuwa ni moja wa wanafunzi wa Yesu!, Lakini alipoona hali imekuwa tete!!.. Anakwenda kufa na Bwana!.. na ameshakamatwa, lile vazi lake zuri la KITANI, aliliacha!, pale na kumkimbia Bwana, akakimbia uchi!.. na watu wakaiona aibu yake.
Jambo hilo hilo linaendelea katika roho leo hii.. Tunapoamua kuwa wanafunzi wa Yesu, tunakuwa tunavikwa na Bwana VAZI ZURI LA KITANI, Ambalo vazi hilo tafsiri yake ni “utakatifu”..tunalithibitisha hilo katika…
Ufunuo 19:8 “Naye amepewa kuvikwa kitani nzuri, ing’arayo, safi; kwa maana kitani nzuri hiyo ni MATENDO YA HAKI YA WATAKATIFU”.
Hivyo tunapoamua kumfuata Bwana, na kuwa wanafunzi wake ni lazima tujikane nafsi tubebe misalaba yetu, pamoja na mavazi yetu mazuri ya kitani. Tuwe tayari kufa tukiwa na Bwana. Lakini kama hatumtaki Bwana tufahamu kuwa hatuwezi kumkimbia bado tukiwa na yale yale mavazi yetu ya kitani(matendo ya haki).. ni lazima tuache mavazi yetu pale ndipo tukimbie uchi!, na watu wataiona aibu yetu.
Je! na wewe leo umeyaacha mavazi yako nyuma, na kukimbia uchi! Kwasababu tu umepitia mtikisiko kidogo kwenye imani yako??, kwasababu umetengwa na wazazi?, kwasababu umechukiwa na ndugu?, kwasababu boss wako hataki wewe usali, hivyo na wewe umeamua kumwachia Bwana mavazi yako(yaani matendo yako ya haki) na kukimbia uchi (kurudia machafu ya ulimwengu)??.. Kumbuka tena Bwana anasema maneno haya…
Ufunuo 16:15 “(Tazama, naja kama mwivi. HERI AKESHAYE, NA KUYATUNZA MAVAZI YAKE, ASIENDE UCHI HATA WATU WAKAIONE AIBU YAKE.)”
Je unayatunza mavazi yako?.. Usimwachie Bwana mavazi yako na kukimbia uchi kwasababu ya majaribu.. Kabla ya kuamua kumfuata Bwana Yesu, kumbuka kujikana nafsi, ujue kuwa kuna majaribu utakutana nayo mbeleni, ambayo yanaweza hata kuhatarisha maisha yako, katika hayo hupaswi kuyavua mavazi yako, ili kuusalimisha mwili wako.
Marko 8:35 “Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, huyu ataisalimisha”.
Bwana atusaidie, na kutubariki.
ANAKUJA KAMA MWIVI!.
Maran atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Kati ya watoto ambao Daudi aliwapenda sana na wakati huo huo wakamsumbua sana, ni Absalomu. Absalomu alikuwa ni kijana mzuri wa umbo, na vilevile alikuwa ni kijana aliyetumia mbinu za kipekee sana katika kutimiza malengo yake.
Absalomu, alileta taharuki kuu mbili Israeli, Taharuki ya kwanza, ni ile ya kumuua ndugu yake, aliyeitwa Amnoni, mwana wa mfalme, na ya pili ni ile ya jaribio lake la kuupindua ufalme wa Baba yake (Daudi).
Kama wewe ni msomaji wa biblia, kitabu cha 2Samweli sura ile ya 13-19, utakutana na habari hizo, utakumbuka kuwa huyu Absalomu alikuwa ni dada yake wa tumbo moja aliyeitwa Tamari, lakini ikatokea siku moja ndugu yake wa mama mwingine aliyeitwa Amnoni, akamtamani, na mwisho wa siku akamwingilia kwa nguvu, bila kufuata utaratibu, hivyo akamletea aibu kubwa binti Yule, pamoja na ndugu yake. Sasa huyu Absalomu, ambaye ni kaka wa mama mmoja na Tamari, alipopata habari akaudhika sana kwa kitendo kile, akamchukia Amnoni kupindukia.
Lakini tabia moja ya Absalomu,ilikuwa si ya kuchukua maamuzi ya muda huo huo, na ndio maana utasoma, hakuzungumza naye neno lolote lile liwe la heri au la shari, bali alitulia kimya tu. Sio kwamba moyoni alikuwa hawaki.
2Samweli 13:22 “Ila Absalomu hakusema na Amnoni wala kwa heri wala kwa shari; kwa maana Absalomu alimchukia Amnoni kwa kumtenza nguvu umbu lake Tamari”.
Akaanza chini chini kupanga mipango yake, ambayo ilikuja kutimia MIAKA MIWILI MBELE. Na mipango hiyo ilikuwa ni ya kumwangamiza ndugu yake.
Ukisoma utaona alianza kazi ya ukataji manyoya, na alipofanikiwa baada ya miaka miwili mizima akamwalika baba yake na ndugu zake waje washereheke pamoja naye, hivyo akatumia sasa fursa ile kumwomba baba yake yule ndugu yake aliyembaka dada yake, awepo, akakubali, na alipoenda, akamvizia saa amelewa, akatuma watumishi wake wamuue. Lengo lake likawa limetimia hapo hapo. Amnoni akafa. Kirahisi hivyo. Unaweza kujiuliza ni kwanini, Absalomu hakuchukua hatua za haraka tangu mwanzoni? Jibu ni kuwa ipo tabia ambayo Mungu anataka tujifunze kwa mtu huyu, jinsi alivyokuwa mtu wa mikakati.
Baadaye, baba yake alipopata taarifa akataka kumuua, lakini Absalomu akakimbilia taifa lingine akakaa huku muda wa miaka mitatu mizima.Sasa, kwa muda wako fuatilia kisa hicho katika biblia, lakini nataka tuone jinsi tabia yake ile ile ya uvumilivu na malengo ilivyomletea mafanikio mengine makubwa mbeleni.
Ukisoma biblia utaona, ulifika wakati akarudi Israeli, na kwenda kuonana na baba yake, Lakii akiwa kama mgeni alidhamiria ndani ya moyo kuwa mfalme wa Israeli. Kama ilivyo kawaida yake alijua njia pekee sio kuanza kukurupuka na kuleta mapinduzi kwa haraka hapana, hatafanikiwa bali, alijua uvumilivu na bidii, ni nguzo muhimu sana za kutimiza malengo yake.
Hivyo akaanza mikakati yake, biblia inatuambia, akawa anaamka kila siku asubuhi sana na mapema, labda saa 10 alfajiri, anakwenda kusimama, karibu la lango la kuelekea kwa mfalme, ili kukutana na watu wenye shida zao,ambao wanahitaji kutatuliwa. Alipokutana nao, kila mmoja kabla ya kufika kwa mfalme alimbusu, akajinyenyekeza kwake, akamsikiliza shida zake, akamjibu kwa upole, ikawa kila mtu aliyetoka pale alimpenda sana, na mwisho akawa anawaambia, maneno ya uongo, kuwa hakuna mtu anayewajili, kama wakimfanya yeye kuwa mfalme awatafanyia mema mengi..
2Samweli 15:1 “Ikawa baada ya hayo, Absalomu akajiwekea tayari gari na farasi, na watu hamsini wa kupiga mbio mbele yake.
2 Tena Absalomu huondoka asubuhi na mapema, na kusimama kando ya njia ya lango; kisha ikawa, mtu ye yote aliyekuwa na neno, lililokuwa halina budi kufika kwa mfalme ili kuhukumiwa, Absalomu humwita mtu huyo kwake, na kumwuliza, Wewe u mtu wa mji gani? Naye akasema, Mtumwa wako ni mtu wa kabila fulani ya Israeli.
3 Naye Absalomu humwambia, Tazama, maneno yako ni mema yenye haki; lakini hapana mtu aliyeagizwa na mfalme kukusikiliza.
4 Tena Absalomu husema, Laiti mimi ningewekwa kuwa mwamuzi katika nchi hii, ili kila mtu mwenye neno au daawa aje kwangu, nimpatie haki yake!
5 Tena ikawa hapo alipokaribia mtu ye yote kumsujudia, hunyosha mkono wake, na kumshika, na kumbusu.
6 Hivyo ndivyo Absalomu alivyowatendea Israeli wote, waliomwendea mfalme ili wapate hukumu; na hivyo Absalomu akawadanganya watu wa Israeli.
7 Hata ikawa mwisho wa miaka minne, Absalomu akamwambia mfalme Tafadhali uniache niende nikaondoe nadhiri yangu, niliyomwekea Bwana huko Hebroni”.
Aliendelea hivyo kwa muda wa MIAKA MINEE (4), Mfululizo, akiamka asubuhi, kwa ajili ya kukutana na shida zao hao watu.. Ndipo watu wote, wakamtambua, wakampenda sana, kwa unyenyekevu wake, na kujali kwake, wakamsikiliza hata kwa uongo wake, Absalomu akafanikiwa kujikusanyia wimbi kubwa la watu waliompenda..akapata nguvu, huku baba yake hajui chochote.
Ndipo siku ya siku ilipofika, ghafla, Daudi akasikia mtoto wake Absalomu, amekusanya majeshi ya watu, yanataka kuja kumpindua. Daudi kuona vile ikampasa akimbilie msituni kuokoa maisha yake. Na kama sio Bwana alikuwa upande wake, ule ufalme ulikuwa ni wa Absalomu. Kwasababu watu wengi sana waliandamana naye. Na vita vilivyopiganwa Israeli kipindi hicho vilikuwa ni vikubwa sana, hatuna nafasi ya kueleza habari yote, lakini kwa muda wako soma kwenye biblia utajionea.
Mpaka wakati ambapo Absalomu anakufa, Mfalme Daudi alikuwa ameshapata somo kubwa sana.
Ni nini tunajifunza?
Kumbuka hadithi zote tunazozisoma katika agano lake, zimebeba funzo kubwa kwetu, haijalishi ni za mtu mwovu au mwema. Leo sisi kama watoto wa Mungu, tumekuwa watu wa kutazamia mapinduzi ya wakati huo huo. Tunataka yote tunayoyatazamia yatokee ndani ya usiku mmoja. Kumbe hiyo siyo kanuni, ili tuteke, wakati mwingine tunahitaji uvumilivu na bidii. Itakupasa uhubiri injili kila siku kwa muda wa miaka kadhaa, bila kuona chochote, ndipo baadaye sana uanze kuvuna matunda ya kusumbuka kwako.
Itakugharimu ufanye mazoezi mengi sana ya kuimba, utunge nyimbo nyingi tu, ndipo baada ya kipindi fulani pengine miaka kadhaa, Bwana ndio azifanye nyimbo zako kuwa Baraka kwa watu wengi. Kama unataka karama ya uponyaji itende kazi ndani yako, itakugharimu uwe mvumilivu wa kuchukuliana na matatizo ya watu wengi, kuwaombea kwa bidii, hata kama hutaona lolote katika siku za kwanza kwanza, itakubidi uendelee hivyo hivyo, hata kwa miaka kadhaa pengine, lakini mwisho wake Bwana atakujalia kipawa hicho kwa viwango vingine. Uvumilivu na bidii, inapaswa iwe sehemu ya maisha yetu.
Absalomu, hakuwa mtu wa papo kwa papo, lakini uvumilivu wake na mikakati yake ilimsaidia sana baadaye, kuitikisa Israeli. Hivyo usikate tamaa, unapoona chochote unachomfanyia Mungu sasa, hakizai kama vile unavyotazamia.. Kamwe usife moyo, kinyume chake ongeza bidii. Na wakati utafika utaona matunda ya taabu zako.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Nini maana ya siku moja kwa Bwana ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja? (2Petro 3:8)
Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze biblia.
Katika uvuvi, upo uvuvi wa kutumia ndoano, na pia upo uvuvi wa kutumia nyavu.
Uvuvi wa kutumia ndoano ni uvuvi ambao unahusisha kukamata samaki mmoja mmoja, Hivyo unachukua muda mrefu kidogo na pia una matokeo madogo. Na katikauvuvi huu ni vitu viwili tu vinahusika katika kukamata samaki, navyo ni Ndoano yenyewe, pamojana Chambo!.
Na chambo inayotumika ni kipande kidogo cha mnofu ambacho kitamvutia samaki, hivyo kila samaki anaponaswa basi mvuvi hana budi kuweka chambo nyingine kwaajili ya samaki mwingine. Huu ni uvuvi mzuri lakini unamatokeo madogo na unachukua muda mrefu..
Lakini upo uvuvi mwingine usiotumia chambo ya mnofu lakini una matokeo makubwa. Na huo simwingine Zaidi ya uvuvi wa nyavu! naTaa.
Uvuvi huu mara nyingi unafanyika usiku, ambapo wavuvi wanakwenda kwenye bahari kuu na kisha kuwasha TAA ZAO zenye mwanga mkali. Na wanapoziwasha basi wale samaki wanavutiwa naule mwanga na hivyo kusogelea chombo na hatimaye kunaswa katika zile nyavu. Na matokeo yake ni makubwa sana, samaki wanapatikana wengi na kwa muda mfupi.
Hii inatufundisha nini, CHAMBO YA MWANGA ni bora kuliko CHAMBO YA MNOFU. Na sisi tunaohubiri Bwana Yesu katufananisha na wavuvi. Na ulimwenguni bahari. Na kama vile wavuvi wanavyokwenda kuvua usiku, kadhalika na sisi tunakwenda kuvua watu katika ulimwengu wenye giza nene. (Ulimwengu uliopotea, watu waliozama katikagiza la ulimwengu, ambao shetani kawapofusha macho wasione).
Lakini chambo yetu sisi si minofu ya nyama..Hiyohaitakuwa na matokeo yoyote katikati ya giza nene la bahari kuu. Chambo tunayohitaji ni TAA ZINAZONG’AA SANA.
Mathayo 5:4 “Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima.
15 Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani.
16 VIVYO HIVYO NURU YENU NA IANGAZE MBELE YA WATU, WAPATE KUYAONA MATENDO YENU MEMA, WAMTUKUZE BABA YENU ALIYE MBINGUNI”.
Kama vile Taa za wavuvi zinavyovutia samaki wengi wakati wa usiku, kadhalika na sisi MATENDO YETU (ambayo ndio mianga kwa ulimwengu), hayo ndio yanayohubiri sana na yanayo wavuta wengi kwa Kristo kuliko, miujiza tutakayoifanya, au lugha tutakazoongea, au karama zetu au kingine chochote kile.
Kumbuka siku zote chambo iliyo bora ni TAA ZETU ZINAZOWAKA (Ambayo ndio matendo yetu), kwa jinsi taa zetu zinavyozidi kung’aa ndivyo mianga yetu inapoonekana mbali na kuvutia samakiwengi Zaidi..lakini taa zetu zikiwa hafifu, hakuna samaki yeyote tutakayemvuta kwa nyavu zetu.
Wafilipi 2:15 “mpate kuwa wana wa Mungu wasio na lawama, walaudanganyifu, wasio na ila kati ya kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka; ambao kati ya hao mnaonekana kuwa KAMA MIANGA katika ulimwengu”.
Je Nuru yako inaangaza katikati ya huu ulimwengu wa giza??
Bwana atusaidie na kutubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?
Kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?
Walawi 19:14 “Usimlaani kiziwi, wala usitie kwazo mbele ya kipofu, bali umche Mungu wako; Mimi ndimi Bwana”.
Vifungu hivyo vinatuonyesha, tabia ya watu ambao wanatumia udhaifu wa watu wengine kuwaletea madhara au matatizo zaidi badala ya kuwasaidia.
Kibinadamu ukikutana na kipofu njiani, na anataka asaidiwe kuvuka barabara, bila shaka utamwonea huruma na kwenda kumshika mkono umvushe, huwezi kwenda kumvizia wakati gari linapita ndio umsogeze barabarani agongwe afe, afe huo sio utu.
Lakini cha ajabu ni kwamba hao watu wapo. Kwa mfano utakuta mtu anataka kununua bidhaa fulani, lakini kwa bahati mbaya mteja huyo hajui sana ubora wa bidhaa hizo, labda tuseme simu. Sasa muuzaji badala atumie busara kumwelekeza bidhaa bora, kinyume chake anatumia fursa ile, kwenda kumletea feki, na kumuuzia kwa bei ile ile ya orijino, kisa tu haijui orijino ipoje. Na mwisho wa siku mnunuzi anaitumie siku mbili tatu, imeharibika, anaitupa, anakuwa amepata hasara. Sasa huo ndio ukwazo Bwana anaouzungumzia hapo mtu anaomwekea kipofu.
Hilo jambo linamkasirisha sana Mungu, Na kwa bahati mbaya wafanyabiashara wengi sana wanayo tabia hii. Ni tabia ya shetani, ambayo alikuwa nayo tangu zamani, Utakumbuka pale Edeni alipoona Hawa ni kipofu, hajui mema na mabaya, akatumia udhaifu huo kumdanganya, badala ya kumwelekeza kuyashika maagizo ya Mungu, na mwisho wake ukawa ni Hawa kutumbukia shimoni. Sasa wapo baadhi ya wanadamu waliokosa UTU namna hii, wanatumia udhaifu wa watu wengine kujitafutia faida zao.
Au utakuta ni mama ntilie, anaona akipika chakula bora hapati faida ya kutosha, anachowaza ni kwenda kutia hamira kwenye ubwabwa wake, ili uvimbe awauzie wateja wengi zaidi, kwasababu anajua wateja wanapenda chakula kingi, Na amekuwa akifanya hivyo kwa muda mrefu, Hiyo yote ni kisa tu haonekani kwa wateja, wakati mwingine anapikia na mafuta ya trasfoma.. Hiyo ni dhambi inayomchukiza sana Mungu.
Walawi 19:14 “Usimlaani kiziwi, wala usitie kwazo mbele ya kipofu, bali umche Mungu wako; Mimi ndimi Bwana”.
Mwingine ni mtumishi wa Mungu, anakutana na mtu mwenye matatizo fulani, pengine ya kiafya, au ya kifamilia, au ya kiroho sasa yeye badala amuhudumie kama mtumishi wa Bwana,anatumia nafasi hiyo ya udhaifu wake, kumtisha, na kumpa shuhuda za uongo, lengo tu ni atumie fursa hiyo kuchukua pesa zake. Watu kama hawa nimeshakutana nao sana. Huko ndio kutia kwazo mbele ya kipofu, na kumlaani kiziwi.
Tunapaswa tuwe kama Ayubu, ambaye alisema..
Ayubu 29:15 “Nalikuwa macho kwa kipofu, Nalikuwa miguu kwa aliyechechemea”.
Tuwasaidie wale ambao wanahitaji msaada, vilevile tuwaongoze mahali sahihi wale ambao wanahitaji kusaidiwa. Tumche Bwana wetu, Tupate siku nyingi na za heri za kuishi katika dunia yake.
Shalom.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
SI KWA UWEZA WALA KWA NGUVU BALI KWA ROHO YANGU, ASEMA BWANA.
Shalom, Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo. Karibu tujifunze maneno ya Bwana wetu.
Katika mambo ya uvuvi, zipo kanuni za uvuvi za kufuatwa, wengi wetu tunadhani, kazi ya mvuvi ni ya kwenda tu kutupa nyavu baharini, kukusanya samaki, kisha kuwatoa nje, halafu basi analala, anaamka tena kesho na nyavu yake hiyo hiyo, anakwenda kuitupa habarini na kuvua samaki wengine tena.. Ndugu Kama umekuwa ukifikiria hivyo basi umekosea.. Vinginevyo kazi ya uvuvi ingekuwa ni rahisi sana.
Kwa kawaida, wavuvi ni sharti, kila wamalizapo uvuvi mmoja, wazioshe nyavu zao kama sio kuzitengeneza, Kwasababu wanapokwenda kuvua sio tu samaki peke yake wanajinasa kwenye nyavu, bali pia kunakuwa na takataka nyingine nyingi zinakwama kwenye neti, sana sana magugu ya baharini, masalia ya magamba ya viumbe , na matope, kiasi kwamba nyavu zile zikiachwa, siku kadhaa bila kuoshwa, vinavundisha nyavu.
Na si hilo tu, kunakuwa na samaki waliokufa, katikati ya neti, nao pia wakaachwa kipindi kifupi sana wanaozesha , na hiyo inapelekea kukaribisha panya kula neti, na kuifanya iwe dhaifu sana, hususani kwenye kamba zake,
Na bado wanasema, ili samaki wawezi kukamatwa kiwepesi, ni sharti ni yenyewe iwe kama vile haionekani itupwapo habarini ,lakini kama inauchafu mwingi, wanasema samaki wakiona, wanaogopa na kukimbia.
Pia nyavu hiyo hiyo inapaswa itengenezwe/au ifanyiwe ukarabati, kwasababu wakati mwingine, kunakuwa ni miamba yenye ncha kali chini inayochana nyavu, au samaki wenye miiba mikali ambao wakipita mara moja tu katikati wanachana nyavu. Hivyo kama mvuvi kila unapoliza kuvua ni sharti ukague neti yako kama inamatundu uizibe.
Hivyo suala la kusafisha na kukarabiti neti ni lazima kwa mvuvi yeyote kila anapomaliza kuvua, haijalishi siku hiyo amepata samaki au hajapata. Haijalishi atakuwa amechoka au hajachoka, Ni lazima aisafishe, kwasababu ni lazima tu itakuwa na uchafu.
Na ndio maana wakati ule Bwana Yesu alipokuwa anapita pwani aliwaona akina Petro, wametoka kuvua samaki, na hawajapata chochote usiku kucha, lakini kanuni ilikuwa ni lazima wazioshe nyavu zao, haijalishi walipata au hawakupata.
Luka 5:1 “Ikawa makutano walipomsonga wakilisikiliza neno la Mungu, yeye alikuwa amesimama kando ya ziwa la Genesareti,
2 akaona vyombo viwili vimekaa kando ya ziwa, LAKINI WAVUVI WAMETOKA, WANAOSHA NYAVU zao.
3 Akaingia katika chombo kimoja, ndicho chake Simoni, akamtaka akipeleke mbali kidogo na pwani. Akaketi, akawafundisha makutano ali chomboni.
4 Hata alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki.
5 Simoni akajibu akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu”.
Umeona, sasa soma tena vifungu hivi, uone kuna wakati pia walizitengeneza nyavu zao, na sio kuosha tu peke yake.
Marko 1:19 “Akaendelea mbele kidogo, akamwona Yakobo wa Zebedayo, na Yohana nduguye, nao pia walikuwa chomboni, WAKIZITENGENEZA NYAVU ZAO.
20 Mara akawaita, wakamwacha baba yao Zebedayo ndani ya chombo pamoja na watu wa mshahara, wakaenda, wakamfuata.
SASA MAMBO HAYO KATIKA ROHO YANAFUNUA NINI?
Sisi kama wahubiri, sisi kama watumishi wa Mungu tunaofanya kazi ya kuwavua watu kwa Kristo, huwa tunajisahau sana na kudhani kuwa kuhubiri tu kunatosha, Au kufundisha tu, au kushuhudia tu. Hatujui kuwa tunapaswa kila siku TUSAFISHE na kutengeneza NYAVU zetu, tunazozitumia kuvulia.
TUNATENGENEZAJE NYAVU ZETU?
Na tunazitengeneza kwa NENO LA MUNGU. Ikiwa na maana tunapaswa Neno la Mungu likae kwa wingi ndani yetu, tusome Neno, tujue misingi na kanuni za uvuvi Kristo anazozitaka, tujue ni nini tunapaswa tufundishe, na nini tusifundishe kwa wakati husika, ujumbe upi tutoe, na upi tusitoe kwa watu fulani. Vinginevyo tukipuuzia, tutajikuta samaki watapenya kwenye nyavu zetu, tukawakosa, kwasababu zina matundu matundu.
TUNAOSHAJE NYAVU ZETU?
Vile vile, Kuosha nyavu zetu. Ni kwa kujitakasa maisha yetu. Maana yake kuishi maisha yanayompendeza Mungu, maisha ya ushuhuda, maisha matakatifu. Ikiwa tuna ushuhuda mbaya katika mazingira yanayotuzunguka, na huku bado tunahubiri injili ni kuonyesha kuwa NYAVU zetu ni chafu. Hivyo Samaki watatukimbia wanapoona uchafu huo kwetu. Na ndio maana pale tunapovua hatuona matunda yoyote, kumbe ushuhuda wetu ndio unaowakimbiza mbali na sisi.
Hivyo ni wajibu wetu, sisi kama wahubiri kuzingatia hayo mambo mawili kila siku. Kwasababu wavuvi nao wanafanya hivyo kila siku. Nasi tuifuate kanuni hiyo rohoni. Na hakika tutamletea Kristo matunda mengi.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Nini maana ya “Siku moja nyuani mwa Bwana ni bora kuliko siku elfu”?
Nakusalimu katika jina kuu la Bwana wetu Yesu Kristo. Ni siku nyingine tena Bwana ametupa neema ya kuiona, hivyo nakukaribisha sasa tuzidi kuyatafakari maneno matukufu ya Mungu wetu, Maadamu katujalia kuiona leo.
Kwanini leo hii imekuwa ngumu sana kuipeleka injili kwa watu walio nje, ili wamwamini Yesu Kristo (Tukisema walio nje, tunamaanisha watu wa kidunia, au watu walio katika dini nyingine), Tunaweza kusema Mungu anawajua walio wake, ni kweli, lakini hicho sio kisingizio, ipo sababu nyingine ambayo tumeikosa sisi kama kanisa na sababu yenyewe ni kukosa UMOJA.
Tukiupata huo kama kanisa basi hatutamia nguvu nyingi sana kuulezea ulimwengu uzuri wa Yesu, bali huo umoja wenyewe tu utauaminisha ulimwengu yeye ni nani.
Bwana Yesu alilizungumza hilo katika..
Yohana 17:21 “Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ILI ULIMWENGU UPATE KUSADIKI YA KWAMBA WEWE NDIWE ULIYENITUMA.
22 Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja.
23 Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ILI ULIMWENGU UJUE YA KUWA NDIWE ULIYENITUMA, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi”.
Umeona, kumbe ulimwengu unaweza kumwamini Yesu, kuwa ndiye mwokozi wa ulimwengu, ikiwa tu tutajitengeneza sisi kwanza katika umoja. Lakini tunapaswa tujue si kila umoja, ni umoja sahihi unaotokana na Mungu..Hapo Bwana hazungumzii umoja wa kichama au umoja wa kidini, au umoja wa kimadhehebu, kama unaoendelea sasa hivi ulimwenguni.. bali umoja anaouzungumzia hapo ni umoja wa Roho,. Kwasababu haiwezekani watu wawili wanaamini vitu viwili tofauti, halafu wawe na umoja, huo sio umoja utakuwa ni umoja wa kimaslahi tu, lakini sio wa Roho.
Waefeso 4:3 “na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani.
4 Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.
5 Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja.
6 Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote”.
Umeona vifungu hivyo? Agizo mojawapo ni kwamba tuutambue ubatizo mmoja na sahihi ni upi, kisha wote tuwe nao, ambao ni ule wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo sawasawa na Matendo 2:38, 8:16, 10:48, 19:5, kisha wote tumpokee Roho mmoja, ambaye ndiye Roho Mtakatifu, tuwe na Bwana mmoja ambaye ni YESU KRISTO jiwe kuu la pembeni, na sio mtume mwingine, au mtakatifu mwingine pembeni yake hapana,.. Na vilevile tuwe na Imani moja, ambayo mzizi wake na shina lake ni BIBLIA TAKATIFU na sio dini au dhehebu.
Tukizingatia hayo, kisha tukashirikiana na ulimwengu ukatuona, basi hatutatumia nguvu kubwa kuwaamishi Kristo kwao, kwani huo umoja wenyewe tu utawahubiria watu uzuri wa Kristo. Lakini tukizidi kuupoteza umoja huo, kila mtu na imani yake, dhehebu lake,. Ni ngumu sana kuugeuza ulimwengu. Hivyo ni wajibu wetu sisi, kama kanisa la Kristo tujipime, je! Umoja huu uliosahihi upo ndani yetu? Kama haupo, basi ipo kasoro. Tujitahidi sana tuunde kwa bidii zote, ili Bwana aaminiwe katikati ya mataifa, matunda mengi yaje kwake..
Hilo ni agizo la Bwana, na sio la mwanadamu.
“Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ILI ULIMWENGU UJUE YA KUWA NDIWE ULIYENITUMA, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi”.
Shalom.
Maran atha.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Jibu: Shalom.
Neno “Amali” maana yake ni “kazi ngumu” hususani ile inayohusisha mwili, kama vile kazi ya kibarua cha kulima au kukata mti.
Katika biblia neno hilo limeonekana mara nne..
Mhubiri 4: 4 “Tena nikafikiri AMALI ZOTE, na kila kazi ya ustadi, ya kwamba inatoka katika mtu kupingana na mwenzake. Hayo nayo ni ubatili na kujilisha upepo”.
Mistari mingine inayoainisha neno hilo ni pamoja na Mhubiri 4:8, Mhubiri 5:19, na Mhubiri 8:15.
Neno “Ijara” maana yake ni “mshahara anaolipwa mtu kwa siku”. kumbuka mshahara anaolipwa mtu kwa mwezi hauitwi Ijara, Ijara ni mshahara wa siku tu, mara nyingi unawahusu vibarua.
Walawi 19:13 “Usimdhulumu jirani yako, wala kumnyang’anya mali yake; IJARA YAKE aliyeajiriwa isikae kwako usiku kucha hata asubuhi”.
Isaya 3:11 “Ole wake mtu mbaya; shari itakuwa kwake, kwa maana atapewa IJARA ya mikono yake”
Isaya 40: 10 “Tazameni, Bwana Mungu atakuja kama shujaa, Na mkono wake ndio utakaomtawalia; Tazameni, thawabu yake i pamoja naye, Na ijara yake i mbele zake”.
Mistari mingine inayoanisha neno hilo ni 2Nyakati 15:7, Mhubiri 4:9, Mhubiri 9:5, Isaya 5:23, Mika 1:7, Zekaria 8:10, na 2Wakorintho 5:10.
Hivyo hakuna Amali isiyo na Ijara. Vile vile kazi ya Mungu ina ujira wake, kama Bwana alivyosema katika kitabu cha Ufunuo..
Ufunuo 22:12 “Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo.
13 Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho.
14 Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango yake”.
Maran atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Mbu ni mdudu ambaye endapo akitua juu ya mwili wa mtu, kama hatasumbuliwa kwa namna yoyote ile, basi atanyonya damu na mwisho wa siku tumbo lake litajaa sana mpaka kupasuka akiwa pale pale ananyonya!..na hapo ndio unakuwa mwisho wa maisha yake!.
Utafiti unaonyesha, kuwa wakati mbu ananyonya damu, mfumo wa taarifa wa tumbo lake na ufahamu wake unakatika, hivyo hajijui kuwa kama hapa kashiba au bado, yeye ile njaa ya kwanza ipo pale pale, anaendeleo kunyonya tu, mpaka anafia pale pale..
Biblia inasema pia katika Mhubiri 5:10 kuwa..
Mhubiri 5:10 “APENDAYE FEDHA HATASHIBA FEDHA, Wala apendaye wingi hatashiba nyongeza. Hayo pia ni ubatili.
11 Mali yakiongezeka, hao walao nao waongezeka na mwenyewe hufaidiwa nini, ila kuyatazama kwa macho yake tu?”
Sio vibaya kutafuta fedha, ni jambo la muhimu, lakini lisiwe jambo linalotawala maisha kiasi kwamba, unapoangalia kushoto, au kulia unaona fedha, au unawaza fedha!. Ukiwa katika hali kama hiyo, nataka nikuambie “kupenda fedha kupo ndani yako hata kama hutakiri kwa kinywa”.
Hekima ya ulimwengu huu inatuambia na kutufundisha, kuwa muda wote tuwaze fedha, tufikiri fedha, tuziishi fedha, tuzitafute lakini hekima ya Mungu haisemi hivyo.. hekima ya kiMungu inasema hivi…
Waebrania 13:5 “MSIWE NA TABIA YA KUPENDA FEDHA; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa”.
Hekima hii kwa ulimwengu inaonekana ni upumbavu!, lakini kwa watu wa Mungu ni nguvu ya Mungu.
Hekima ya kiMungu pia inasema, shina moja la mabaya yote ni kupenda fedha!
1Timotheo 6:10 “Maana SHINA MOJA LA MABAYA YA KILA NAMNA NI KUPENDA FEDHA; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi”.
Mtu anayependa fedha anakuwa hashibi fedha siku zote, akipata elfu hashukuru wala haridhiki, atatamani tena laki, akipata laki hali yake ni ile ile, atataka milioni, akipata milioni atataka milioni 100, wala hutaona badiliko lolote kwake, hashukuru wala hatosheki..ni kama mbu anayenyonya damu, pasipo kujijua kuwa tayari tumbo lake limeshajaa na linakaribia kupasuka, yeye anaendelea tu!, mwisho wa siku anapasuka matumbo!.
Ndicho kilichomtokea Yuda, alianza kupenda fedha kidogo kidogo, na kwasababu kupenda fedha ni roho!, ikampelekea asitosheke kuiba fedha iliyokuwa inapatikana katika mfuko wa Bwana!, akapiga hatua nyingine ya kutamani hata apate fedha nyingi zaidi, kwa kumsaliti Bwana Yesu! Pasipo kujua kuwa tayari tumbo lake limejaa na linakaribia kupasuka!, yeye aliendelea kuzisaka fedha kwa nguvu, na ulipofika wakati matumbo yake yalipasuka kama maandiko yanavyosema…
Matendo 1:18 “(Basi mtu huyu alinunua konde kwa ijara ya udhalimu; akaanguka kwa kasi akapasuka matumbo yake yote yakatoka.
19 Ikajulikana na watu wote wakaao Yerusalemu; hata konde lile likaitwa kwa lugha yao Akeldama, maana yake, konde la damu.)”
Biblia inatuonya tusiwe na tabia ya kupenda fedha.., haijatukataza kufanya kazi!, bali tusiwe watu wa kupenda fedha!…unaweza kuipenda kazi unayoifanya lakini usiwe na tamaa ya kupenda fedha katika hiyo!, kiasi kwamba upate kingi au kidogo!, moyo wako hauutaabiki!!, maadamu umetoa huduma iliyo bora, furaha yako inakuwa ni ule uaminifu katika kazi yako, yaani siku ukiona hujafanya kazi kwa uaminifu ndio moyo wako unauma, na sio siku umeona hujapata faida nyingi!… Na wengi wanaoipenda kazi zao kuliko faida na fedha, ndio wanaofanikiwa kuliko wale ambao kipaumbele chao ni fedha tu!.. Hao wapo tayari mwingine alie ili wao wapate faida, au mwingine adhurike wao wapate fedha, kama Yuda!, wapo radhi wakuuzie hata sumu, au wafanye biashara haramu ilimdari tu matumbo yao yajae…
Ndio maana wanafananishwa na mbu anayenyonya damu!.. mbu ananyonya uhai wa mtu, ambayo ni damu yake..ndio maana mwisho wake unakuwa ni kupasuka matumbo!..
Bwana atusaidie, tuwe watu wa kumpenda yeye zaidi ya kupenda fedha!.
Mathayo 6:33 “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa”
Maran atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
ONDOA TAKATAKA KATIKA FEDHA, NA CHOMBO KITATOKEA KWA MTAKASAJI.
Kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?
Leo hii dunia imekuwa na sikukuu nyingi sana za maonyesho. Na sikukuu hizo Mungu ameruhusu makusudi kabisa ziwepo ili kutupa picha halisi ya jinsi sikukuu yake kubwa ya maonyesho itakavyokuwa mbinguni.
Kwamfano kipindi hiki, kwa taifa kama la Tanzania, lipo katika sikukukuu ya maonyesho ya wafanyabiashara maarufu kama saba saba (7’7). Na mwezi ujao kutakuwa na maonyesho mengine makubwa ya wakulima yajulikanayo kama nane nane (8’8). Kama ulishawahi kutembelea maonyesho haya, au yanayofanana na haya nadhani utakuwa unaelewa ni nini hasaa kinaendelea kule.
Kwa ufupi ni kwamba utakutana na mabanda mengi sana, na kila banda lina onyesho lake la kipekee, kiasi kwamba mpaka utakapomaliza mabanda yote, hutatoka kama ulivyo. Utakutana na mambo mengi sana usiyoyajua, ni jinsi gani vitu vinatengezwa, ni technolijia gani inafanya kitu kiwe hivi au vile n.k.
Sasa, mambo hayo na kwa Bwana Yesu pia yapo. Ipo siku kubwa sana ya maonyesho, ambayo itafanyika huko mbinguni, Sikukuu hiyo biblia inatuonyesha tumeandaliwa sisi, mahususi ili kuuona utukufu wa Yesu aliopewa na Baba yake kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, kwa ajili yetu sisi.
Yohana 17:24 “Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami po pote nilipo, WAPATE NA KUUTAZAMA UTUKUFU WANGU ULIONIPA; kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu”.
Umeona hapo? Anasema, lengo la yeye kutaka tuwepo na yeye popote alipo ni kusudi kwamba tuutazame utukufu wake aliopewa… Ndugu hadi sasa Bwana Yesu ameshajiandaa kutuonyesha ukuu wake, huko mbinguni.. Tengeneza picha jinsi siku hiyo itakavyokuwa, tutakapotembezwa katika mabanda ya mbinguni(tukitumia lugha ya kibinadamu).. Tunatoka sehemu moja anatuonyesha nchi nzuri ya dhahabu, tukidhani ndio basi, tunatoka hapo anatupeleka kwingine anatuonyesha makasri mazuri ya kifalme, halafu anasema hayo yote ni ya kwenu, niliyokuja kuwaandalia huku kwa miaka 2000, kama nilivyowaambia katika Yohana 14
Yohana 14:1 “Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi.
2 Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali.
3 Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo”.
Anatoka hapo anatupeleka tena katika banda lingine, anatuonyesha viumbe wa kimbinguni, ambao hutujawahi hata kuwaona huku duniani, anakuambia hawa watawatumikia nyinyi.. Tunatoka hapo anawapeleka na kwa malaika zake wote, anatutambulisha kwa mmoja baada ya mwingine, kisha Bwana anasema hawa nao watawahudumia siku zote.. Tunatoka hapo tunakwenda kuonyeshwa vyombo vizuri za muziki, ambavyo kwa hivyo tutakuwa tunamwimbia Mungu daima. Mnaenda sehemu nyingine mahali pa mafunzo mnaambia hapa mtafundishwa jinsi ya kuwa na uwezo wa kiroho kama wa malaika, mnatoka hapo mnapelekwa tena kwingine kuonyeshwa mambo ya ajabu, ambayo kimsingi hatuwezi kuyaeleza hapa, kwasababu ni mambo ambayo jicho halijawahi kuona wala, sikio kusikia, wala halijawahi kuingia katika moyo wa mwanadamu yoyote.
1Wakorintho 2:9 “lakini, kama ilivyoandikwa, Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, (Wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu,) Mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao”.
Siku hiyo ndiyo tutakapojua Bwana Yesu ni mkuu namna gani. Leo hii huwezi kujua lolote, kwasababu wakati wa yeye kudhihirisha utukufu wake haujafika, lakini siku si nyingi, atatunyakua na kutupeleka huko aliko. Tukauone utukufu wake aliopewa na Baba yake.
Tutaona mambo mengi sana, kila mahali tutakapokuwa tunapelekwa tutabakia kutoa macho tu, kwasababu tutasema hiki nacho tumepewa sisi? Hata hiki? Hata kile? Na Yesu atasema NDIO niliwaandalia nyinyi haya yote..Kama hatujaelewa Tutauliza maswali, na yote yatajibiwa, tutatembea katika maonyesho hayo makuu kwa muda wa miaka saba mfululizo.
Kwakweli tukose vyote sasa lakini sio hilo. Tukose mali sasa, tukose umaarufu, tukose vya kidunia, tusikose karamu kuu ya mwanakondoo, mbinguni. Lakini kwa bahati mbaya ni kuwa watu wengi watayakosa maonyesho hayo makuu, kwasababu kama mpaka leo hii, mtu akiambiwa aokoke kwa kumaanisha kabisa kumfuata Yesu, anaona kama analetewa habari za kilokole, unategemea vipi mtu huyo, ataingia kwenye karamu hiyo na maonyesho hayo?
Hatakwenda popote,atabaki tu hapa duniani, hata akifa leo, hiyo siku yenyewe ikifika, hatoweza kufufuliwa aende katika UNYAKUO. Ndugu huo ndio wakati ambao kutakuwa na kilio na kusaga meno kama Bwana Yesu alivyosema.. Hutalia kwasababu inaingia kwenye dhiki kuu tu, bali utalia sana kwasababu umekosa tendo hilo kuu la karamu ya Bwana Yesu, ambayo itaambatana na MAONYESHO hayo MAKUBWA SANA.
Yohana 17:24 “Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami po pote nilipo, WAPATE NA KUUTAZAMA UTUKUFU WANGU ULIONIPA; kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu”.
Maneno hayo ni lazima yatimie. Haleluya.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo: