Monthly Archive Julai 2021

BADO TUTAHITAJI TU KUSAIDIANA.

Siku moja nikiwa njiani nilikutana na mama mmoja mwenye mtoto, akaniomba shilingi elfu moja apande gari aelekee nyumbani kwake chanika, basi kwa kuwa hiyo pesa nilikuwa nayo nikampa, lakini baadaye kidogo, nilipanda gari, nikasahau kuwa sikuwa na hela nyingine yoyote ya cash mfukoni, tukiwa safarini kondakta, akaniomba nauli, nikajisachi sina pesa, ila ninayo kwenye simu, nikamwambia kondakta sina pesa hapa, naomba tukifika kituoni, nikatoe nikupe, lakini kondakta akaonekana kama sio mwelewa akadhani kama natumia ujanja tu ili nisimpe nauli yake..

Wakati naendelea kufikiria, na huku nikiangalia safari yangu haiishii mwisho wa kituo, nitashukia njiani hata nikienda kutoa atakuwa radhi kunisubiri?,.kulikuwa ni kijana mmoja anaonekana kama maskini, akatoa shilingi elfu moja akanipa, akaniambia chukua hii kondakta atakusumbua, nikamwambia ninayo nauli wacha tu tufike kituoni nitampa, lakini alinishurutisha kuichukua ile hela.

Nikakaa nayo kwa muda, nikitafakari, nikawa sina jinsi baadaye kidogo nikampa yule konda na yule kijana akashuka kwenye gari. Nikapata somo, wakati nadhani wenye shida ndio wanahitaji msaada, kumbe hata wewe usiye na shida utahitaji msaada ule ule kama wa yule mwenye shida.

Mama yule alikuwa na haja ya sh. Elfu moja, muda mchache baadaye uhitaji huo huo ulinigeukia mimi, japokuwa nilikuwa nayo. Ndugu yangu, utatembea, na gari lako, utatembea na mabilioni yako benki, utatembea na afya yako nzuri, lakini kamwe usiache kuwasaidia wenye uhitaji, kwasababu uhitahitaji ule ule wakati Fulani utaupitia hata wewe isipokuwa tu katika maumbile mengine.

Katika utajiri wako huo huo, unaweza ukafa njaa, kama tu vile yule mtu asiye na chakula kabisa, katika afya yako hiyo hiyo unaweza ukasumbuliwa na magonjwa kama tu mtu yule aliyelazwa pale muhimbili, katika nyumba yako nzuri, unaweza kulala nje kama tu yule mtu alalaye mabarazani, Vilevile katika elimu yako kubwa, hiyo hiyo unaweza kuwa mjinga sawa tu na yule ambaye hajasoma kabisa. Kamwe usifikirie kwasababu umeshapata kitu Fulani, ndio tayari umeepukana na tatizo hilo, ambalo watu wengine wanalipitia kwa kukikosa hicho. Lipindue hilo wazo kuanzia sasa.

Bwana atusaidie tujifunze unyenyekevu kwa watu wote, na kusaidiana sisi kwa sisi, kwasababu biblia inasema.

Mhubiri 1:6 “Upepo huvuma kusi, hugeuka kuwa kaskazi; hugeuka daima katika mwendo wake, na upepo huyarudia mazunguko yake.

7 Mito yote huingia baharini, walakini bahari haijai; huko iendako mito, ndiko irudiko tena”.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

HALI ZETU JINSI ZINAVYOWEZA KUATHIRI UTOAJI WETU.

NIFANYALO WEWE HUJUI SASA; LAKINI UTALIFAHAMU BAADAYE.

NIFANYALO WEWE HUJUI SASA; LAKINI UTALIFAHAMU BAADAYE.

WALA MSIUANGALIE MWILI, HATA KUWASHA TAMAA ZAKE.

KITABU CHA YUDA: SEHEMU YA 3

ILI NIWE KIELELEZO KWA WALE WATAKAOMWAMINI BAADAYE.

Rudi nyumbani

Print this post

UYATIE MACHOZI YANGU KATIKA CHUPA YAKO EE! BWANA.

Mhubiri mmoja maarufu huko India, siku moja alionyeshwa maono, anasema alipokuwa anakwenda katika ziara zake za kuhubiri katika kijiji kimoja, ilikuwa ni desturi yake kukutana na baadhi ya wenyewe wa maeneo hayo nyumbani kwao na kuzungumza nao, Sasa anasema alipokuwa anakaribia  nyumbani kwa mwanamke mmoja aliyemfahamu, yule mwanamke alipomwona anaingia uwani mwake, akatoka jikoni moja kwa moja kwenda kukutana naye, na kabla hata hajamuamkia vizuri, muda huo huo alimwangukia magotini kwake, akaanza kulia.  Wakati muhubiri huyu anafanya jitahada za kumwinua, amuulize shida yake, muda huo huo anasema alimwona Bwana Yesu amesimama pembeni yake, akimwangalia, kisha kitambo kidogo akamwona anamkaribia huyu mwanamke aliyekuwa Analia, akaenda kwenye shavu lake la kushoto, na kuweka mikono yake, na kukinga machozi yake, mpaka yalipojitengeneza kama kibwawa.

Na ghafla akamwona Bwana Yesu akipaa mbinguni, na yeye yupo naye, akafika sehemu nzuri sana, ambapo kwa mbele aliona kitu kama sanduku la agano limewekwa, kisha akamwona Bwana Yesu akiyamimina machozi ya yule mama juu ya sanduku lile la agano. Kisha akaanza kumwombea kwa Baba, kwa kuuugua sana na kwa machozi mengi.. Aliomba pale kwa kitambo, mpaka ikasikika sauti kama ya radi ikisema, AMESIKIWA. Anasema Hapo ndipo Bwana Yesu alipoacha kuomba. Akageuka akamwangalia huyu mhubiri, akamwambia mwambie binti yangu, maombi yake manne aliyokuwa anamwomba Mungu yamesikiwa.

Na dakika hiyo hiyo alijikuta amesimama karibu na yule mwanamke, kisha akamwinua na kumweleza alichoonyeshwa, yule mwanamke akaruka ruka kwa kuraha na kicheko kwa kujibiwa kule.

Kwanini, nimeandika ushuhuda huo, nikwasababu, biblia inasema machozi ya watakatifu yanathaminiwa sana na Mungu, jambo ambalo watakatifu wengi, pengine hawalijui, wanadhani kulia kwao ni bure, Si kweli, Mungu anayakusanya machozi yetu na kuyahifadhi katika chupa, biblia inasema hivyo;

Zaburi 56:8 “Umehesabu kutanga-tanga kwangu; Uyatie machozi yangu katika chupa yako; (Je! Hayamo katika kitabu chako?)

Umeona Machozi yetu kwa Bwana, yanatiwa katika chupa, kama vile divai nzuri inavyotunzwa katika viriba vipya. Na wakati huo huo bado yanaandikwa katika kitabu cha Mungu cha ukumbusho. Kaka/Dada Umekuwa ukilia kwasababu ya dhiki unazopitia kutokana na Imani yako,  kumbuka kuwa Mungu anasikia, umekuwa ukilia kwasababu ya misiba iliyokukuta hivi karibuni Mungu anasikia, kwasababu ya magonjwa yasiyotibika, Mungu anasikia, Kwasababu ya injili Mungu anasikia na kuyatunza hayo machozi kama vile alivyoyatunza ya akina Paulo.

Matendo 20:19 “nikimtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote, na kwa machozi, na majaribu yaliyonipata kwa hila za Wayahudi;

20 ya kuwa sikujiepusha katika kuwatangazia neno lo lote liwezalo kuwafaa bali naliwafundisha waziwazi, na nyumba kwa nyumba”,

Unapaswa ukumbuke kuwa huduma ya Bwana wetu Yesu Kristo ya kutuombea haikuishia tu alipokuwa duniani, hapana, bali bado inaendelea hadi leo hii mbinguni, biblia inasema hivyo;

Waebrania 7:25 “Naye, kwa sababu hii, aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu hai sikuzote ili awaombee”.

Hivyo usiogope ni nini unapitia leo,  wala usikate tamaa, kumbuka Yesu, faraja yetu yupo. zidi kumtumaini yeye na kumtegemea yeye, kwasababu daima yupo na wewe, kukusaidia, mkono wake hautakuacha kamwe.

Hakika sifa na heshima, na utukufu, ni kwa Bwana wetu YESU KRISTO milele na milele,

Amen.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

WAOMBEENI WANAOWAUDHI.

Kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?

UFUNUO: Mlango wa 18

Bwana Yesu alimaanisha nini kusema “Saa yangu haijawadia?”

NAYE AKASIMAMA JUU YA MCHANGA WA BAHARI.

Rudi nyumbani

Print this post

Tofauti kati ya uchafu wa mwilini na rohoni ni  ipi?

SWALI: Naomba kujua tofauti kati ya uchafu wa mwilini na rohoni ni  ipi ?, kama tunavyosoma katika 2Wakorintho  7:1

2Wakorintho 7:1 “Basi, wapenzi wangu, kwa kuwa tuna ahadi hizo, na tujitakase nafsi zetu na UCHAFU WOTE WA MWILI NA ROHO, huku tukitimiza utakatifu katika kumcha Mungu”.


JIBU: Ili tuwe wakamilifu kwa kiwango cha  kuweza kuzikaribia ahadi za Mungu, Tujue kuwa Mungu anataka tuwe watakatifu kote kote yaani Mwilini na rohoni.

Sasa hapo anaposema tujitakase na Uchafu wote wa mwilini. Anamaanisha kuwa tujiweke mbali na dhambi zote zinazozalika katika miili yetu. Mfano wa dhambi hizi ni kama vile, uzinzi, ulevi, wizi, uvutaji sigara, utukanaji, uvaaji mbovu, kama vile vimini na suruali kwa wanawake, kujichubua, kujipaka make-up, kutoa mimba, kuvaa milegezo,  kujichoraji tattoo, na ushoga, utumiaji wa madawa ya kulevya na mambo mengine yote yanayofanana na hayo, ambayo asili yake ni mwilini.

Na pale aliposema tuweke kando Uchafu wa rohoni, Anamaanisha dhambi zote zinazotoka ndani ya mtu, ambazo hazihusiani na mwili moja kwa moja, mfano wa dhambi hizi ni kama vile, wivu, hasira, tamaa, mawazo mabaya, unafki, uchoyo, husuda, fitna, majigambo, kiburi, ibada za sanamu, uongo. Hizi ni dhambi ambazo zinazalika ndani, na Mungu anazichukia sana, kama vile tu anavyozichukia zile zinazozalika katika mwili.

Hivyo tujue kuwa Mungu anaangalia kote kote, Kuna watu wanadhani kuwa Mungu anaangalia roho tu, hatazami mwili. Ndugu, mwili wako unathamani sawa na roho yako mbele za Mungu, kwasababu siku ile ya mwisho si roho yako tu itaokolewa, bali hata na mwili wako pia (kasome biblia utalithibitisha hilo). Hivyo mtukuze Mungu katika mwili wako, usidanganywe na mafundisho ya manabii wa Uongo,  wanaokuambia Mungu anatazama roho haangalii mwili. Hizi ni nyakati za mwisho, Tii Neno la Mungu Zaidi ya maneno ya mwanadamu. Kwasababu hilo ndilo litakalokutetea siku ile, na hilo ndilo litakalokuhumu siku ile. Neno la Mungu ni upanga. Liogope sana.

Waebrania 4:12 “Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.

13 Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu”.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Ngome ni nini?  Kwanini Mungu anafananishwa na ngome?

SISI NI WINDO BORA SANA, LA DHAMBI.

Nini maana ya “mkilichukia hata vazi lililotiwa uchafu na mwili”?

Jaa ni nini katika biblia?

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

Rudi nyumbani

Print this post

Ni madhara gani yatampata mtu yule anayetafsiri Neno isivyopaswa!

Jibu: Kuna hatari kubwa sana ya kulihubiri Neno isivyopaswa, Ni vizuri kulielewa Neno vizuri kabla ya kulifundisha.. Leo nitakuambia ni kwanini.

Miaka ya nyuma nikiwa bado ni mchanga katika Imani, nilikuwa natamani sana kuhubiri, kwasababu tu nilikuwa naona watu wanahubiri.. Hivyo na mimi, nilikuwa na shauku ya kuhubiri, hata ikiwezekana kuielezea biblia yote,. Hivyo hiyo ikanifanya, nisiwe na muda mwingi wa kulitafakari Neno, wala kulielewa sana wala kulichimba kwa undani, badala yake nilishika tu biblia na kuhubiri kwa jinsi nilivyolielewa Neno, nikiamini kuwa kila nitakachokisema kitakuwa ni cha Roho Mtakatifu!.. kumbe sikujua nilikuwa nafanya jambo la hatari sana kwangu.

Siku moja niliota ndoto nimekaa kwenye kiti, kama sehemu ya dining hivi,  halafu chini ya miguu yangu kuna kama sufuria inatokota maji, na miguu yangu ilikuwa ndani ya hayo maji ila nilikuwa sijui kama miguu yangu ipo kwenye hayo maji ya moto tena yanayotokota kabisa, kwasababu nilikuwa sisikii maumivu yoyote. Baada ya muda kukaja kama sahani mbele yangu ambayo ilikuwa na mchemsho wa nyama, ilipokuja ile sahani nikawa naanza kuzila zile nyama, zilipopungua nikawa kama nazivuta nyingine kwa chini, zinakuja juu ya hiyo sahani kubwa iliyopo mbele yangu..

Halafu baada ya muda wakaja watu Fulani mbele yangu ambao huwa nawahubiria..nikawa nawapa na wenyewe zile nyama wale…wakawa wanakula huku wanashukuru, wote tukawa tunafurahia mlo.. wakati hilo jambo linaendelea, nikajikuta naitazama miguu yangu, kumbe zile nyama nilizokuwa nakula na kuwalisha wengine zilikuwa ni nyama kutoka kwenye miguu yangu, hivyo zilivyokuwa zinazidi kwenye ile sahani ndivyo nilivyokuwa naimaliza miguu yangu. Baada ya hapo nikashtuka kutoka usingizini!, nikiwa na hofu!

Nikiwa kitandani natafakari maana ya hiyo ndoto!, Roho Mtakatifu akazungumza na mimi, na kuniambia… Ndivyo ninavyojimaliza mwenyewe kwa kuwalisha watu wake chakula kinachotoka katika akili zangu badala ya kutoka kwake!.

Tangu siku hiyo nikaacha! Kukimbilia kuhubiri kabla ya kuhakikisha kuwa jambo hilo halitoki katika akili zangu bali linatoka kwa Bwana. Nikajifunza kama jambo sijalielewa vizuri katika maandiko nitangoja mpaka nilielewe ndipo niwafundishe wengine!.. Nisije nikawalisha watu nyama kutoka katika mwili wangu mwenyewe.. Mwisho wa siku mimi ndiye nitakayepata madhara wa kwanza kabla ya wao!..

Hivyo Bwana alinionyesha hatari hiyo na tahadhari yake, na nikamshukuru sana mpaka leo, nazidi kuwa makini..

Hivyo ndugu!.. kamwe usihubiri, wala kufundisha wengine, jambo ambalo wewe mwenyewe hulielewi vizuri… ukifanya hivyo katika roho unajimaliza mwenyewe kabla ya kuwamaliza wale unaowafundisha.. Usiwe na haraka na utumishi!, bali keti chini kwanza kumtafuta Mungu, na kujifunza mambo kwa kina!

Jambo moja lisilojulikana na wengi ni kufikiri kuwa jambo la kwanza linalompendeza Mungu ni sisi kuhubiri!.. la! Nataka nikuambie jambo la kwanza linalompendeza Mungu ni sisi kukaa kujifunza(kuwa wanafunzi wake). Ndio maana ilibidi awaweke mitume wake chini ya madarasa kwa miaka mitatu kabla ya kuwatuma..

Jambo hili linawafanya wengi wairuke hatua ya kuwa wanafunzi wa Yesu.. vile vile inawafanya waruke kanuni ya vigezo vya kuwa mwanafunzi ambavyo Bwana Yesu alivisema katika…

Luka 14:27 “Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu”.

Wengi tunairuka hii hatua, na kutaka kuwa waalimu, kabla hatujawa wanafunzi!..kumbuka huwezi kuwa mwanafunzi kama hujajikana nafsi, wala kuuchukua msalaba wako. Siku zote kumbuka hilo! Huwezi kuwa mwalimu kwa wengine kama wewe hujapitia uanafunzi..na huwezi kuwa mwanafunzi kama hukujikana nafsi na kubeba msalaba wako kumfuata Yesu.

Bwana atubariki na kutusaidia.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

INJILI YA MANENO LAINI ITAKUGHARIMU.

Kwa herufi gani kubwa nimewaandikia kwa mkono wangu mimi mwenyewe.

Kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?

DAMU YA ZAKARI BIN BARAKIA.

Kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?

Rudi nyumbani

Print this post

Barazani pa Mungu ni wapi? Kama tunavyosoma katika Yeremia 23:18?

Jibu: Tusome,

Yeremia 23:18 “Maana, ni nani aliyesimama katika baraza la Bwana, hata akalifahamu neno lake na kulisikia? Ni nani aliyelitia moyoni neno langu, na kulisikia”

Ili tuweze kuelewa vizuri,  hebu tuendelee kidogo kusoma hadi mstari wa 22

“19 Tazama, tufani ya Bwana, yaani, ghadhabu yake, imetokea; ni dhoruba ya kisulisuli; itapasuka, na kuwaangukia waovu vichwani.

 20 Hasira ya Bwana haitarudi, hata atakapokwisha kuyatimiza makusudi ya moyo wake; katika siku za mwisho mtalifahamu neno hili kabisa.

21 MIMI SIKUWATUMA MANABII HAO, lakini walikwenda mbio; sikusema nao, lakini walitabiri.

22 Lakini kama wangalisimama katika BARAZA YANGU, ndipo wangaliwasikizisha watu wangu maneno yangu, na kuwageuza waziache njia zao mbaya, na uovu wa matendo yao.”

Katika mistari hiyo, Bwana alikuwa anazungumza juu ya manabii wa uongo, ambao hawakuketi kusikia kutoka kwa Mungu bali walijitungia nabii zao na kuwapa watu…na nabii  hizo walizowapa watu hazikuwa zinawafanya watu waache dhambi zao, bali zilikuwa zinawafanya watu wazidi kustarehe katika dhambi, manabii hao wa uongo walikuwa wanawatabiria watu kuwa kuna amani na shwari na Bwana hajawakasirikia ilihali hakuna amani yoyote, na Bwana amewakunjia uso, kutokana na maasi yao.

Sasa ndio Bwana anawaambia wana wa Israeli kupitia kinywa cha Yeremia kuwa.. manabii hao wanaowatabiria uongo, hawakuketi barazani pa Mungu na kusikia Mungu anasema nini, bali wamejituma wenyewe…

Hivyo Barazani pa Mungu panapozungumziwa hapo ni “mahali ambapo Mungu anakutana na watu wake katika roho na kuwapa ujumbe”.

Mfano wa watu walioketi barazani pa Bwana, na kupokea ujumbe ni nabii Isaya..

Isaya 6:1 “ Katika mwaka ule aliokufa mfalme Uzia nalimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu sana na kuinuliwa sana, na pindo za vazi lake zikalijaza hekalu.

 2 Juu yake walisimama maserafi; kila mmoja alikuwa na mabawa sita; kwa mawili alifunika uso wake, na kwa mawili alifunika miguu yake, na kwa mawili aliruka…………….

6 Kisha mmoja wa maserafi wale akaruka akanikaribia; naye alikuwa na kaa la moto mkononi mwake, ambalo alikuwa amelitwaa kwa makoleo toka juu ya madhabahu;

 7 akanigusa kinywa changu kwa kaa hilo, akaniambia, Tazama, hili limekugusa midomo yako, na uovu wako umeondolewa, na dhambi yako imefunikwa”.

8 Kisha nikaisikia sauti ya Bwana, akisema, Nimtume nani, naye ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu? Ndipo niliposema, Mimi hapa, nitume mimi.

 9 Naye akaniambia, Enenda, ukawaambie watu hawa, Fulizeni kusikia, lakini msifahamu; fulizeni kutazama, lakini msione”

Mfano mwingine ni Nabii Ezekieli, Nabii Danieli na Nabii Musa. Sehemu nyingi, Bwana amemketisha Musa barazani kwake na kumpa ujumbe kwa wana wa Israeli.

Pamoja na hayo, Mungu pia anaketi katika baraza na malaika wake mbinguni, na kuzungumza nao na kuwatuma.. na pia shetani na mapepo wake wanaweza kuhudhuria barazani mwa Mungu kuwashitaki wateule..

Nyakati 2:18 “Mikaya akasema, Sikieni basi neno la Bwana; Nalimwona Bwana ameketi katika kiti chake cha enzi na jeshi lote la mbinguni wamesimama mkono wake wa kuume na wa kushoto.

 19 Bwana akasema, Ni nani atakayemdanganya Ahabu mfalme wa Israeli, ili akwee Ramoth-gileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi.

 20 Akatoka pepo, akasimama mbele za Bwana, akasema, Mimi nitamdanganya. Bwana akamwambia, Jinsi gani?

21 Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo vinywani mwa manabii wake wote. Akasema, Utamdanganya, na kudiriki pia; ondoka, ukafanye hivyo”

Hivyo katika agano la kale, barazani pa Mungu palifikiwa na wanadamu wachache tu!… yaani manabii wa Bwana!, hao ndio Bwana aliowaita barazani pake na kuwapa ujumbe kwa wana wa Israeli. Lakini katika zamani hizi za agano jipya, Wote waliompokea Roho Mtakatifu wanapakaribia barazani pa Bwana, na kuisikia sauti yake anataka nini pamoja na mashauri yake.  Hatuhitaji tena Nabii Fulani anyakuliwe mbinguni akasikie ni nini Bwana anasema juu yetu, kisha aje kutuambia… Kwasababu tayari Roho Mtakatifu aliye ndani yetu, anatwaa yale yaliyo ya Kristo, katika baraza lake lililo mbinguni na kutupasha habari..

Yohana 16:13  “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.

14  Yeye atanitukuza mimi, kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari”.

Hivyo Baraza la Mungu leo ni Roho Mtakatifu!.. Tukimpata huyo basi, tutajua yote Mungu anayotaka tuyajue, hatutahitaji kunyakuliwa mbinguni tukayasikie..la!, wala hatuhitaji kumshusha Kristo chini aje atuambie! tukiwa hapa hapa duniani tutayajua na kuyasikia..kwasababu Roho Mtakatifu aliye ndani yetu, atatupasha habari..

Warumi 10:6  “Bali ile haki ipatikanayo kwa imani yanena hivi, Usiseme moyoni mwako, Ni nani atakayepanda kwenda mbinguni? (Yaani, ni kumleta Kristo chini), …….

8  Lakini yanenaje? Lile neno li karibu nawe, katika kinywa chako, na katika moyo wako; yaani, ni lile neno la imani tulihubirilo”

Ndio maana kuna umuhimu mkubwa sana wa kumpokea Roho Mtakatifu, kwasababu yeye ndio baraza la Mungu. Kwake yeye tunapokea mashauri na maonyo na mafunzo. Na biblia inasema katika Warumi 8:9 kuwa wote wasio na Roho Mtakatifu hao si wake.. ikimaanisha kuwa pasipo Roho Mtakatifu haiwezekani kumwona Mungu.

Na Roho Mtakatifu anafanya kazi kamili kwa aliyemwamini Bwana Yesu, na kuoshwa dhambi zake kwa damu yake. Na aliyebatizwa katika ubatizo sahihi, wa maji mengi na kwa jina la Yesu kulingana na Matendo 2:38.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Mahali pa juu palikuwa ni wapi kama tunavyosoma katika biblia?

Nini maana ya “heri mtu asiyekaa barazani pa wenye mizaha?”

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

ESTA: Mlango wa 4

NINI TUNAJIFUNZA KWA MWANA MPOTEVU NA NDUGUYE?

Rudi nyumbani

Print this post