UFUNUO: Mlango wa 3 part 2

UFUNUO: Mlango wa 3 part 2

Sehemu ya pili:

Bwana wetu YESU KRISTO atukuzwe. Karibu katika kujifunza kitabu cha Ufunuo, leo tukiendelea na ile sehemu ya pili ya sura hii ambapo tutajifunza juu ya kanisa la sita linalojulikana kama FILADELFIA. Tulishayatazama makanisa matano ya kwanza na tukaona kila moja ujumbe wake, thawabu zake pamoja na wajumbe au Malaika zake. Hivyo kama bado hujazipitia ni vema ukazianza hizo kwanza kisha tuendelee kwa pamoja na kanisa hili la sita.

Tunasoma…

Ufunuo 3: 7 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Filadelfia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye mtakatifu, aliye wa kweli, aliye na ufunguo wa Daudi, yeye mwenye kufungua wala hapana afungaye, naye afunga wala hapana afunguaye”.

Kama tulivyokuwa tunajifunza katika sura zilizopita kuwa ule utambulisho wa kwanza wa Bwana kabla hajatoa ujumbe unakuwa na mahusiano makubwa sana na ujumbe wenyewe wa kanisa husika..Kwamfano hapa anaanza kwa kusema ” Haya ndiyo anenayo yeye aliye MTAKATIFU, aliye wa kweli, aliye na UFUNGUO WA DAUDI, yeye mwenye kufungua wala hapana afungaye, naye afunga wala hapana afunguaye”.

Unaona hapo anasema yeye “aliye mtakatifu” hajasema “yeye aliye na hizo Roho saba” kama alivyofanya katika kanisa lililopita la Sardi, au “yeye aliye na huo upanga mkali utokao kinywani mwake kama alivyosema katika kanisa la tatu” hapana! Bali hapa anasema “yeye aliye mtakatifu na mwenye UFUNGUO wa Daudi”. Ikiashiria kuwa “Anategemea kuona UTAKATIFU kama yeye alivyo katika hilo kanisa”..Kadhalika na ufunguo pia alionao inaamaanisha “Anakwenda kufungua au kufunga kitu fulani katika hilo kanisa”. Hivyo tutakuja kuona hizo funguo za Daudi alizonazo ni zipi?..

Kwa ufupi kanisa hili la FILADELFIA lilianza mwaka 1750WK na kuisha mwaka 1906WK. Lilidumu kwa kipindi cha miaka 156, na Mjumbe/Malaika wa kanisa hili aliitwa JOHN WESLEY. Na tafsiri ya neno Filadelfia ni “UPENDO WA NDUGU”..Hivyo hili ni kanisa lililoonyesha utofauti mkubwa na makanisa mengine yote. Baada ya ule uamsho wa Luther wa kuwahubiria watu watoke katika ule mfumo wa yule mwanamke Yezebeli (Kanisa Katoliki). Bwana alimnyanyua tena Mjumbe wake mwingine mwaminifu, John Wesley na nuru ya ziada kwamba pamoja na “kuhesabiwa haki kwa imani kwa Mungu”, mtu anapaswa aongezee juu yake “UTAKATIFU

1Petro 1: 15 “bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;

16 kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu. “

Na tena inasema… Waebrania 12: 14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo UTAKATIFU, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao”

Mambo ambayo Kanisa la Sardi halikuonekana wala mjumbe wa kanisa lile Martin Luther hakulifundisha sana, yeye alitilia mkazo sana kuhusu kuhesabiwa haki kwa imani”. Hivyo mjumbe wa hili kanisa la FILADELFIA John Wesley alianza kuhubiri UTAKATIFU kwa nguvu, na kwamba usafi katikati ya maisha ya waumini ni jambo la muhimu sana.

Wesley alizaliwa huko Epworth, nchini Uingereza mwaka 1703 na alipokuwa chuoni Oxford ndipo Bwana alipoanza kubadilisha maisha yake, yeye na kaka yake aliyeitwa Charles waliunda kikundi pamoja na wengine kinachosimamia itikadi ya “Kuishi maisha kama ya Kristo aliyoishi”, kuliko maisha ya kidini, walianza kwenda kuwatembelea wagonjwa mahospitalini, na wafungwa, na kuwahurumia maskini, n.k na kujifanya wao wenyewe kuwa vielelezo(njia ya kufuata) hivyo wakajiundia uongozi wa kiroho wakauita “(METHOD yaani NJIA”)..na kuanzia huo wakati wakaitwa WAMETHODISTI. Baada ya hapo Wesley na wenzake Bwana aliwagusa kwa namna ya kipekee, wakaona umuhimu wa kwenda kufanya kazi ya umishionari duniani kote. Hapo ndipo injili ikaanza kupelekwa duniani kote kwa nguvu, kasi na kwa bidii hata zile sehemu ambazo zilikuwa ngumu kufikiwa kama Afrika zikafikiwa na nuru ya neno la Mungu, ndio wakati wamishionari wengi wakaanza kufika sehemu za Afrika, Asia na Marekani ya kusini.

Wesley alikuwa ni mtu aliyeimarika kiroho sana, anasema hakumbuki kama alishawahi kupungua nguvu rohoni hata kwa robo saa tangu siku aliyozaliwa. Alisema hakuwahi kulala zaidi ya masaa 6 siku zote za huduma yake, kila siku alikuwa akiamka saa 11 alfajiri, na kwenda kuhubiri zaidi ya mara nne kwa siku, ili kwamba kwa mwaka afikishe kwa wastani wa mafundisho 800. Alikuwa akisafiri maelfu ya maili kwa farasi kwenda kuhubiri. Kwa mwaka inakadiriwa alikuwa anasafiri zaidi ya maili 4,500 kwenda kuhubiri.

Tukiendelea na mistari inayofuata…

Ufunuo 3:8 “Nayajua matendo yako. Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga, kwa kuwa unazo nguvu kidogo, nawe umelitunza neno langu, wala hukulikana jina langu”.

Bwana anasema amewapa mlango uliofunguliwa mbele yao.? Sasa huu mlango ni upi?.

Kumbuka hapo awali BWANA alijitaja kama “yeye aliye na ufunguo wa Daudi“. Na ni kwanini aseme funguo za Daudi na asiseme funguo za Musa, au Ibrahimu?. Ni kwa nini Daudi?. Hii inatupa picha halisi kuwa upo ufunguo ambao alikuwa nao Daudi na Bwana naye akawa nao. Hivyo ni vizuri tukaufahamu huu ufunguo kwanza ni nini ili tupate msingi mzuri wa huko tunapoelekea?..

Kumbuka baada ya Wana wa Israeli kutoka Misri na kuingia katika nchi yao ya ahadi, watu wote baada ya kuiona ile nchi ni nzuri walitawanyika na kila mtu kwenda kukaa sehemu yake, walijenga na kupanda na kufanikiwa wakamsahau Mungu, Wao walifanikiwa lakini Mungu katikati yao hakuwa na nafasi yoyote, wao walikaa kwenye makasri lakini Mungu alikaa kwenye mahema ya giza. Na iliendelea hivyo kwa kipindi kirefu cha zaidi ya mamia ya miaka, na hakukuwa na mtu yeyote kutia moyo wake ufahamu kuona kwamba kwanini sanduku la Mungu linakaa kwenye mahema yenye giza leo huku kesho kule, Mungu mkamilifu anayetujali hapaswi kukosa sehemu ya kukaa, Ndipo Daudi siku moja akatia moyo wake ufahamu na kusema nimtengenezee Mungu wangu mahali pa kukaa, haiwezekani yeye akae kwenye jumba la kifahari wakati, Bwana Mungu wake hajamjengea nyumba, ndipo Daudi kwa bidii akaiteka ngome ya Sayuni (YERUSALEMU), Kisha akakusudia kuanzia huo wakati amjenge Mungu wake nyumba ( yaani HEKALU). Na ndipo Mungu akamwambia Daudi.

2 Samweli 7: 2 “Mfalme akamwambia Nathani, nabii, Angalia sasa, mimi ninakaa katika nyumba ya mierezi, bali sanduku la Mungu linakaa ndani ya mapazia.

3 Nathani akamwambia mfalme, Haya, fanya yote yaliyomo moyoni mwako; maana Bwana yu pamoja nawe.

4 Ikawa usiku uo huo, neno la Bwana likamfikia Nathani kusema,

5 Enenda, ukamwambie mtumishi wangu, Daudi, Bwana asema hivi, JE! WEWE UTANIJENGEA NYUMBA, NIKAE NDANI?

6 Kwa maana mimi sikukaa ndani ya nyumba, tangu siku ile niliyowatoa wana wa Israeli katika Misri, hata leo, lakini nimekaa katika hema na maskani.

7 Mahali mwote nilimo kwenda na wana wa Israeli wote, JE! NIMESEMA NENO LOLOTE NA MTU YO YOTE WA WAAMUZI WA ISRAELI, NILIYEMWAGIZA KUWALISHA WATU WANGU ISRAELI, NIKISEMA, MBONA HAMKUNIJENGEA NYUMBA YA MIEREZI?

8 Basi, sasa, mwambie mtumishi wangu, Daudi, maneno haya, Bwana wa majeshi asema hivi, Nalikutwaa katika zizi la kondoo, katika kuwaandama kondoo, ili uwe mkuu juu ya watu wangu, juu ya Israeli;

9 nami nimekuwa pamoja nawe kila ulikokwenda, na kuwakatilia mbali adui zako wote mbele yako; nami nitakufanyia jina kuu, kama jina la wakuu walioko duniani.

10 Tena nitawaagizia mahali watu wangu Israeli, nami nitawapanda, wapate kukaa mahali pao wenyewe, wasiondolewe tena; wala wana wa uovu hawatawatesa tena, kama hapo kwanza;”

Unaona hapo sababu kubwa iliyomfanya hata Bwana Yesu kuitwa mwana wa Daudi, ni tabia aliyoionyesha Daudi ya kumuundia Mungu wake mji wa kukaa pamoja na Hekalu la kuweka Jina lake, katika ya makuhani, kati ya wafalme, kati ya waamuzi, kati ya manabii, ni Daudi pekee ndiye aliyeliona jambo hilo?. Na Mungu alikaa kimya makusudi aone ni nani atakayekuwa na akili ya kufanya hivyo. Na akaonekana Daudi peke yake. Na huo ndio UFUNGUO Daudi aliokuwa nao KUFUNGUA ukimya wa Mungu.

Kadhalika na Bwana wetu Yesu Kristo aliposema “yeye mwenye Ufunguo wa Daudi” alimaanisha na yeye pia anaunda Yerusalemu yake na Hekalu kwa Mungu wake. Isipokuwa yeye YERUSALEMU yake ni ya rohoni sio ya mwilini,na hekalu kwa Mungu wake ni la rohoni sio la mwilini. Daudi hasaa asingeweza kabisa kumwandalia Mungu mji utakayomfanya ashuke yeye mwenyewe na kukaa katikati ya watu lakini Bwana Yesu anaandaa mji utakaoleta makao ya Mungu katikati ya watu..na huu “MJI” anaoundaa ni watakatifu wake. Tukisoma…

1 Wakorintho 3: 16 ” Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?

17 Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, AMBALO NDILO NINYI “.

Tutakuja kuona vizuri juu ya mji mtakatifu wa Mungu (Yerusalemu mpya) ni nini, tutakapofika katika Ufunuo sura ya 21.

Hivyo alipoliambia hili kanisa la Filadelfia “Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako”, Alimaanisha kuwa ni mlango wa kuujenga mji wake pamoja naye. Hivyo wale watu walipoanza kwenda huku na huko kufanya umishionari wa kuwaleta watu wengi (Ikiwemo) wapagani kwa Kristo, ndio ulikuwa mlango uliofunguliwa mbele yao. JOHN WESLEY na mamisionari wengine waliifanya kazi hiyo duniani kote, kipindi hicho pia ndio biblia kusambazwe duniani kote, hakuna nchi ambayo haikufikiwa na nuru ya Neno.

Tukiendelea ..

“9 Tazama, nakupa walio wa sinagogi la Shetani, wasemao kwamba ni Wayahudi, nao sio, bali wasema uongo. Tazama, nitawafanya waje kusujudu mbele ya miguu yako, na kujua ya kuwa nimekupenda.

10 Kwa kuwa umelishika neno la subira yangu, mimi nami nitakulinda, utoke katika saa ya kuharibiwa iliyo tayari kuujilia ulimwengu wote, kuwajaribu wakaao juu ya nchi”.

Sinagogi la shetani halikuanzia tu kwenye hili kanisa la sita, bali lilikuwepo pia katika makanisa ya nyuma, lilitajwa pia katika kanisa la pili (Ufunuo 2:9), Hili ni kanisa la uongo ambalo walikuwepo watu waliojifanya kama kanisa la kweli la Mungu na kuiga mambo yaliyokuwa yanafanywa na watakatifu lakini ndani yao walikuwa ni mbwa-mwitu wakali, wanaliharibu kundi, ni tabia ya shetani popote palipo na nuru ya kweli ya Mungu, atanyanyuka na kupanda magugu yake katikati yao. Lakini katika hili kanisa kwa kuwa walilishika Neno la subira ya Mungu kwa uaminifu wote, Mungu akayadhoofisha hayo makundi mengine ya uongo shetani aliyoyanyanyua katikati yao na kumtukuza sana bibi-arusi wake zaidi yao.

Bwana anaendelea na kusema…

“10 Kwa kuwa umelishika neno la subira yangu, mimi nami nitakulinda, utoke katika saa ya kuharibiwa iliyo tayari kuujilia ulimwengu wote, kuwajaribu wakaao juu ya nchi.

11 Naja upesi. Shika sana ulicho nacho, asije mtu akaitwaa taji yako”.

Unaona hapo Kanisa hili liliahidiwa pia kulindwa kutoka katika saa ya kuharibiwa iliyo tayari kuujilia ulimwenguni wote (Na hii saa ya kuharibiwa itakuwa ni kipindi cha dhiki kuu), Ikiwa na maana kuwa dhiki hii kuu ingepaswa itokee tangu wakati wa hili kanisa la Filadelfia lakini kwasababu ya Subira na uaminifu wao, Bwana akawaepusha, hivyo itatokea katika kanisa linalofuata la mwisho la Laodikia. Na kama anavyosema saa hiyo itakuwa ni ya “kuwajaribu hao wakaao juu ya nchi”, ina maana kuwa ulimwengu mzima utapitia jaribu moja zito la “aidha kupokea chapa ya mnyama uishi au kuikataa ufe” litakuwa ni jaribu kubwa sana kwa wale watakaoachwa kwenye unyakuo. Ndugu Unaona wakati tunaoishi?, ni hatari kubwa sana ipo mbele yetu kama tusipokuwa waangalifu?.

Na anazidi kusema 11 Naja upesi. Shika sana ulicho nacho, asije mtu akaitwaa taji yako”.

Hapa anasema “naja upesi” ikiwa na maana kuwa “hakawii” biblia inasema waebrania 10: 37 “Kwa kuwa bado kitambo kidogo sana, YEYE AJAYE ATAKUJA, WALA HATAKAWIA”.

Na pia anasema “shika sana ulicho nacho” ikiwa na maana kuwa, kile ulichokipokea ukihifadhi, kwa kuwa “mtakatifu” na kujiepusha na “mafundisho yadanganyayo” asije “MTU”, akatwa taji yako, kumbuka ni “mtu” na sio “malaika” ikifunua kuwa mataji tunapewa hapa hapa duniani, mbinguni tukifika ni kuvikwa tu. Na tukiwa hapa duniani kuna mtu anaweza akatwaa mataji yetu, SASA huyu “MTU” atafutaye kutwaa mataji yetu (au THAWABU) zetu ni nani??

2 Wathesalonike 2: 3 ” MTU awaye yote asiwadanganye kwa njia yo yote; maana haiji, usipokuja kwanza ule ukengeufu; akafunuliwa yule “MTU WA KUASI”, mwana wa uharibifu;

4 yule mpingamizi, ajiinuaye nafsi yake juu ya kila kiitwacho Mungu ama kuabudiwa; hata yeye mwenyewe kuketi katika hekalu la Mungu, akijionyesha nafsi yake kana kwamba yeye ndiye Mungu.

5 Je! Hamkumbuki ya kuwa wakati nilipokuwapo pamoja nanyi naliwaambieni hayo? “

Unaona hapo huyu MTU anayezungumziwa hapo ni mpakwa mafuta wa shetani (yaani MPINGA-KRISTO ndani ya cheo cha UPAPA), na mifumo yake yote,na mitume wote wa uongo wajigeuzao kuwa mitume wa Kristo, ambao kwa kipindi hichi cha siku za mwisho wamezagaa kila mahali, wasiofundisha toba na msamaha wa dhambi wala wasiofundisha ujio wa Bwana bali mungu wao ni tumbo..Mtume aliwataja katika…

Wafilipi 3: 17 Ndugu zangu, mnifuate mimi, mkawatazame wao waendao kwa kuufuata mfano tuliowapa ninyi.

18 Maana wengi huenenda, ambao nimewaambieni mara nyingi habari zao, na sasa nawaambia hata kwa machozi, KUWA NI ADUI ZA MSALABA WA KRISTO;

19 mwisho wao ni uharibifu, MUNGU WAO NI TUMBO, utukufu wao u katika fedheha yao, WANIAO MAMBO YA DUNIANI.

20 Kwa maana sisi, WENYEJI WETU UKO MBINGUNI; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo;

21 atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote viwe chini yake.

Na mwisho kabisa Bwana anamalizia kwa kusema…..

” 12 Yeye ashindaye, nitamfanya kuwa NGUZO katika HEKALU LA MUNGU WANGU, wala hatatoka humo tena kabisa, nami nitaandika juu yake jina la Mungu wangu, na jina la mji wa Mungu wangu, huo Yerusalemu mpya, ushukao kutoka mbinguni kwa Mungu wangu, na jina langu mwenyewe, lile jipya.

13 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. “

Bwana aliwaahidia watu wa kanisa hili la Filadelfia, wale ambao waliokuwa watakatifu, na kujiepusha na mafundisho ya uongo na kujitoa kwa bidii yote kupeleka injili huku na kule duniani kote, na kuusimamisha mji wa Bwana Yerusalemu yake ya rohoni, na hekalu ndani yake, kama Daudi alivyoadhimia kumjengea Bwana nyumba, hata BWANA kuuchagua Yerusalemu kuwa makao yake makuu, na mji wake mtakatifu, kadhalika hawa wa Filadelfia Bwana aliwaahidia kuwafanya kama nguzo, katika ule mji uliotukuka Yerusalemu mpya ambao tutakuja kuuona habari zake katika sura ile ya 21..

Tukiyajua hayo, ni wakati wa kuzifanya taa zetu ziwe zinawaka, kwa kumuamini, Bwana Yesu Kristo, na kutubu, na kubatizwa katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa na kwa JINA LA YESU na kupokea Roho Mtakatifu, na kuishi maisha yanayolingana na wokovu,(yaani maisha matakatifu), na zaidi ya yote kuipeleka habari njema kwa watu wote ulimwenguni kote, na kujihadhari “mtu” asije akayatwaa mataji yetu.

Ubarikiwe na Bwana Yesu, aliyetoa maisha yake kuwa dhabihu hai, kwa Mungu kwa ajili yetu.

Tafadhali “share” kwa wengine ujumbe huu na Mungu atakubariki. Kwa Mwendelezo >>> Ufunuo: Mlango wa 3 Part 3

Ikiwa utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara,  kwa njia ya whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255789001312. Na kama utapenda kwa njia ya E-mail basi tuandikie email yako katika boksi la maoni chini.


Mada Zinazoendana:

WEWE NI HEKALU LA MUNGU.

MPINGA-KRISTO


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

3 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Kifaru Malale
Kifaru Malale
3 years ago

amina mtumishi, bado naufungua ufahamu wangu kwa kunywa maziwa yasiogoshiwa

All
All
4 years ago

Samahani naweza kupata historia za hawa wajumbe wa kanisa kuanzia clenius mpaka Martin Luther nataka tu kushibisha ufahamu ,