JE! UNA MHESHIMU MUNGU?

JE! UNA MHESHIMU MUNGU?

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo, Mkuu wa Uzima libarikiwe…Karibu tujifunze Neno la Mungu, na leo kwa Neema zake tutajifunza Maana ya kumheshimu Mungu ni ipi?, Tukijifunza kupitia maandiko matakatifu.

Maana ya kumpa mtu heshima…haina tofauti sana na “kumpandisha mtu hadhi”, Biblia inaposema “waheshimu Baba yako na Mama yako” haina tofauti sana na kusema fanya jambo lolote ambalo likawaletea wazazi wako heshima mbele za Mungu na mbele za jamii inayowazunguka…Kwa kufanya hivyo ni sawa na umewaheshimu wazazi wako.

Kwamfano mtoto anapokuwa ni msafi wa tabia na mwenendo, anasalimia wakubwa, mpole, mtulivu, msikivu, mwelekevu na watu wote wa nje wakamwona..jambo la kwanza watu watakwenda kuwatazama wazazi wake na kuwasifia wazazi kwamba wanajua kumlea mtoto katika maadili, hivyo wazazi wa yule mtoto wanapata heshima kwa kupitia mwanao.Kwahiyo hapo huyo mtoto tayari katimiza amri ya Mungu ya kuwaheshimu mzazi wake, hata kama wazazi wake nyumbani hawajamfundisha hayo maadili.

kadhalika kijana wa kike, anapovaa mavazi ya nusu uchi na anatembea mtaani au barabarani, hata kama kapewa ruhusu ya kuvaa hayo mavazi na wazazi wake mwenyewe lakini bado mbele za Mungu na wanadamu HAJAWAHESHIMU MZAZI WAKE..Ni kwasababu gani?..Ni kwasababu Kwa mavazi yale anasababisha kuwadhalilisha wazazi wake na ndugu zake mbele za watu walio nje na mbele za Mungu. Na hili ndio tatizo kubwa kwa vijana wengi wa kike wanadhani kwasababu tu wazazi wao wanavaa nguo fupi na zaidi ya yote wanapewa ruhusa na wao kuvaa nguo fupi kama za wazazi wao, basi wanadhani mbele za Mungu tayari wanawaheshimu wazazi wao.

Wanaona wazazi wao wanakunywa pombe, na pengine hata wazazi wao wanawaacha na wenyewe wanywe pombe, wanadhani kuwa ndio wanawaheshimu wazazi wao.

Binti usijidanganye kumheshimu mzazi wako sio kumtii tu! bali ni kumpa hadhi kama mzazi, hata kama mzazi wako anakuruhusu au anakuhimiza uvae nguo za nusu uchi, au vimini, au suruali wewe kataa..mwambie Mama/Baba sitaki kukuvunjia heshima kwa kuvaa hizo nguo,.

Na pia kwa kijana wa kiume hata kama mzazi wako anatoboa masikio, au anakuruhusu nawe utoboe masikio, au anafuga rasta au anakunywa pombe hivyo anataka na wewe uwe mlevi kama yeye…wewe usikubali kwani kinyume chake kwa kukataa kwako ndiko utakuwa umemheshimu…ukitii kwa kukubali kuwa mlevi kama yeye, utakuwa hujamheshimu, hivyo kama maandiko yanavyosema “wote wasiowaheshimu wazazi wao watakuwa na siku chache za kuishi duniani”..Na wewe utakuwa ni mmoja wao..Lakini endapo ukakataa na watu wakikuona wewe sio mlevi kama baba yako, hata kama watamdharau baba yako kwa ulevi wake lakini pia kwa sehemu fulani watampa heshima baba yako kwa kulea mtoto mwenye adabu mbele za watu.

Na hivyo wewe kijana utakuwa umempandisha hadhi mzazi wako(umempa heshima yake).N.k Na mambo mengine yote ambayo unaweza kufanya yakampandisha hadhi mzazi wako mbele za Mungu na mbele za wanadamu, ukiyafanya hayo ndio utakuwa umemheshimu mzazi wako na kwa Mungu wa Mbingu na nchi.

pia ni hivyo hivyo, hatumheshimu Mungu wetu kwa KUMPA SHIKAMOO hapana! Mungu haheshimiwi hivyo, Yapo mambo matatu tunayoweza kufanya yakampa Mungu HESHIMA kubwa sana, nayo ni 1) IMANI2)UTAKATIFU…….3)MWONEKANO

Hayo mambo matatu ndio yatakayomfanya Mungu apate heshima kutoka kwetu., Lakini leo hatutazungumzia hayo mawili ya kwanza, bali tutazungumzia hilo moja la mwisho, ambalo ni MWONEKANO, tutaliangalia ni kwa namna gani litampa Mungu heshima.

Mavazi yamekuwa ni tatizo kubwa sana, kwa watu wanaojiita ni watu wa Mungu, hasa hasa kwa wanawake..Utakuta mwanamke hata kwenye Ibada anakwenda na suruali, au kimini, au anakwenda kajipaka uso rangi na mdomoni kaweka kila rangi. Na anaujasiri wote wa kukaa kiti cha mbele kabisa na anapaza sauti yake kwa nguvu akiabudu na kusifu, na ni kila siku anafanya hivyo.

Binti unayesoma haya, nakwambia kwasababu pengine uliambiwa lakini hukuelewa au ulipuuzia…Kwa mwonekano huo HUMWESHIMU MUNGU HATA KIDOGO. Kama tu ni aibu kutembea na Baba yako mzazi njiani ukiwa umevaa hizo nguo, si zaidi KUSIMAMA MBELE YA MUNGU WA MBINGU NA NCHI ukiwa na hizo nguo?..Hebu chukua muda kutafakari hili jambo, usilichukulie kiwepesi tu! Usidhani pale unapokwenda kuabudu hakuna macho ya Mungu, yapo na anaangalia kama tunavyoangalia sisi wanadamu, kwasababu Mungu huyo huyo aliyeuimba roho ndio huyo huyo aliyoumba mwili. Kwahiyo acha kusikiliza Ubeti wa shetani uliotungiwa kuzimu kwamba MUNGU ANAANGALIA ROHO HAANGALII MWILI.

Hebu tujifunze kwenye maandiko kidogo watu waliomheshimu Mungu kwa mwonekano wao.

Yohana 21 : 1-25

“1 Baada ya hayo Yesu alijidhihirisha tena kwa wanafunzi wake, penye bahari ya Tiberia, naye alijidhihirisha hivi.

2 Simoni Petro, na Tomaso aitwaye Pacha, na Nathanaeli wa Kana ya Galilaya, na wana wa Zebedayo, na wengine wawili wa wanafunzi wake, walikuwapo pamoja.

3 Simoni Petro aliwaambia, Naenda kuvua samaki. Nao wakamwambia, Sisi nasi tutakwenda nawe. Basi wakaondoka, wakapanda chomboni; ila usiku ule hawakupata kitu.

4 Hata asubuhi kulipokucha, Yesu alisimama ufuoni; walakini wanafunzi hawakujua ya kuwa ni Yesu.

5 Basi Yesu akawaambia, Wanangu, mna kitoweo? Wakamjibu, La.

6 Akawaambia, Litupeni jarife upande wa kuume wa chombo, nanyi mtapata. Basi wakatupa; wala sasa hawakuweza kulivuta tena kwa sababu ya wingi wa samaki.

7 Basi yule mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda akamwambia Petro, Ndiye Bwana. Naye Simoni Petro, aliposikia ya kwamba ni Bwana, akajifunga vazi lake, (maana alikuwa uchi), akajitupa baharini.

8 Na hao wanafunzi wengine wakaja katika mashua; maana hawakuwa mbali na nchi kavu; ila yapata dhiraa mia mbili; huku wakilikokota lile jarife lenye samaki.

9 Basi waliposhuka pwani, wakaona huko moto wa makaa, na juu yake pametiwa samaki, na mkate”.

Ukisoma habari hiyo kwa makini utaona kwamba Petro alikuwa anavua na wenzake akiwa uchi (sasa uchi unaozungumziwa hapo sio uchi kabisa wa kukosa nguo zote, hapana bali ni uchi ambao mtu anakuwa amebakiwa tu na nguo ya ndani). Kutokana na desturi za uvuvi, wavuvi wengi wanapunguza nguo zao wakati wa kuvua ili wawe wepesi wa kuogelea na wanakuwa vile kwasababu wanakuwa wanaenda mbali na makazi ya watu, kwahiyo kwa mwonekano wao hawawezi kuiharibu jamii..

Kwahiyo hapa Petro alikuwa yupo na nguo ya ndani tu, gafla akatokea Bwana ufukweni na hawakumtambua lakini walipomtambua tu! PETRO ALIVAA VAZI LAKE HARAKA NA KISHA AKAJITUPA BAHARINI!.

Hebu tafakari hilo tukio!! Petro huyo ni mwanaume, na akatokea Yesu ambaye pia ni mwanaume kama yeye lakini Petro kwa kumheshimu Bwana akavaa haraka vazi lake, na hata baada ya kuvaa akaona haitoshi, ili kujisitiri zaidi akajitupa kwenye maji. Kwasababu anajua aliyesimama mbele yake ni nani?…alijua kabisa ni zaidi ya mwanadamu ni Mungu, na hivyo mbele zake anapaswa ajisitiri.

Kwa tukio hilo unaweza ukaona kabisa kamwe wanafunzi wa Yesu walikuwa hawajiachii mbele zake, ikiwa na maana kuwa walikuwa wanajisitiri mbele zake kila wakati, walikuwa hata hawadhubutu kubaki kifua wazi mbele zake ingawa wote walikuwa ni wanaume kama yeye.

Sasa kama hawa wanafunzi wa Bwana Yesu walio wanaume walikuwa wanajisitiri hivyo mbele za Bwana, unadhani wale wanawake waliokuwa wanamfuata walikuwaje mbele zake??..unadhani wakina Mariamu Magdalena walikuwa wanavaaje mbele zake, unadhani wangeweza hata kuonyesha vifua vyao mbele yake? walikuwa wanajisitiri kuliko kawaida, pengine hata walikuwa wanaficha wakati mwingine hata nyuso zao mbele zake.

Lakini leo hii unamwambia binti wa Mungu, kwa kumhurumia na kwa upendo, jisitiri unapoingia mbele za Mungu, na sio tu mbele za Mungu bali kila mahali, uendako unamwonyesha na maandiko kuhusiana na yeye kujisitiri (1Timthotheo 2:9)…anakuambia Mungu haangalii mavazi anaangalia roho, Injili ambayo haijulikani ilitoka wapi.

Mwanaume hawezi kwenda kwenye ibada na kaptura, au malapa lazima kuna kitu ndani yake kitamhukumu, na ukiona kaenda na malapa basi ni kweli huyo mtu hana viatu au anamajeraha..Lakini mwanamke ataingia kapaka wanja, lipstick, kapaka uso rangi, kapuliza pafyumu mita 5 mbele watu wanasikia, mgongo wote uko wazi, kavaa sketi fupi ambayo ni aibu kuelezea mfano wake, na ndani hakuna kitu kinamchoma!! Lazima kuna tatizo ndani ya huyo mtu.

1 Samweli 2: 30 “Kwa sababu hiyo, Bwana, Mungu wa Israeli, asema, Ni kweli, nalisema ya kuwa nyumba yako, na nyumba ya baba yako itakwenda mbele zangu milele; LAKINI SASA BWANA ASEMA, JAMBO HILI NA LIWE MBALI NAMI; KWA MAANA WAO WANAONIHESHIMU NITAWAHESHIMU, NA WAO WANAONIDHARAU WATAHESABIWA KUWA SI KITU”.

Mwanamke unapokwenda kwenye ibada na mwonekano usio wa heshima, jua unakwenda kukutana na Bwana Yesu mwenyewe, unamshushia Yesu Kristo heshima yake, na hivyo na yeye hawezi kukuheshimu ndivyo Neno lake linavyosema, Watu wasio wakristo wanasema dini yenu ni ya namna gani? watu wanamwabudu Mungu uchi. Jina la Mungu linatukanwa kwa ajili yako. Utajikuta unakwenda kujitafutia laana badala ya Baraka..Hata kama hilo kanisa unalokwenda mchungaji wake anawaruhusu wanawake kuvaa hivyo au haongei chochote…wewe usiende kujitafutia laana mbele za Mungu, vaa kwa kujisitiri, vaa nguo za heshima jisitiri mbele za Mfalme Mkuu Yesu Kristo, na mbele za wanadamu Kama Petro aliyeteuliwa na Bwana alijisitiri mbele zake, na alikuwa ni mwanamume alifanya hivyo wewe mwanamke ni nani usifanye hivyo. Vaa nguo yako ndefu, funika kichwa chako, hata watu wasione kifua chako ndivyo utakavyokuwa UMEMHESHIMU MUNGU, na HIVYO MUNGU ATAKUHESHIMU.

Kama wewe umempandisha Mungu hadhi kwa mwonekano wako, na watu wa nje wakamweshimu Mungu wako kwa kupitia wewe, na yeye pia Mungu atakuheshimu, atakupandisha hadhi. Lakini kama ukimshusha na yeye atakushusha.
Kwasababu lolote utakalolifanya liwe baya au jema, Bwana atakulipa hilo hilo.. “alisema mkinionea haya nami nitawaonea haya mbele za Baba yangu, tukimkiri naye atatukiri”.

Ni matumaini yangu kuwa Bwana atakupa macho ya kuyaona hayo ewe mwanaume/mwanamke..kwamba utamheshimu Mungu kwa mwonekano wako ili naye akuheshimu.

Mungu akubariki sana.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

MAVAZI YAPASAYO NI YAPI?.

MAVAZI YA NDANI NA YA NJE

WEWE SI MALI YAKO MWENYEWE!

WEWE NI HEKALU LA MUNGU.

TWEKA MPAKA VILINDINI.


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments