JE UTII WAKO KWA MUNGU UMETIMIA?.

JE UTII WAKO KWA MUNGU UMETIMIA?.

Je unajua kuwa kama utii wako haujatimia mbele za Mungu, kuna mambo utashindwa kuyafanya?? Kama utiifu wako kwake ni mdogo basi upo hatarini sana, Kama ulikuwa hulijui hili, basi ni vizuri ukalijua leo.

Hebu tusome maandiko yafuatayo..

2Wakorintho 10:3  “Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili;

4  (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;)

5  tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo;

6  tena tukiwa tayari kupatiliza maasi yote, KUTII KWENU KUTAKAPOTIMIA

Hapo mwishoni anamalizia kwa kusema “KUTII KWENU KUTAKAPOTIMIA”. Ni wengi wanalisoma hili andiko lakini hawafiki hapo mwisho, au hata wakifika hapo mwisho basi hawatafakari vizuri maana ya maneno hayo “Kutii kwenu kutakapotimia”.

Maana yake ni kwamba kama kutii kwako mbele za Mungu hakujatimia basi HUTAWEZA KUANGUSHA NGOME, hutaweza KUANGUSHA MAWAZO YALIYOINUKA juu yako na juu ya maisha yako na familia yako na shughuli zako… kama kutii kwako hakujatimia mbele za Mungu vile vile HUTAWEZA KUTEKA NYARA, wala hutaweza KUPATILIZA MAASI yoyote yaliyoinuka kinyume chako… Kwaufupi hutaweza  kabisa kushindana vita vya kiroho!!..utaishia kusumbuliwa tu na shetani na wanadamu.

Mungu anapenda UTII, Na Utii una nguvu nyingi.. Kwa jinsi tunavyoongeza viwango vyetu vya kumtii Mungu ndivyo NGUVU ZETU ZA KIROHO ZINAVYOONGEZEKA.. Na hivyo tunakuwa na uwezo mkubwa wa kumshinda Adui na hila zake na njama zake.

Lakini leo hii kama Mungu anakuambia uache dhambi hutaki kumtii unategemea vipi Uwe na Nguvu za kuangusha Ngome ndani yako?, kama Ukiambiwa ukabatizwe hutaki kutii unategemea vipi uweze kuangusha ngome za mizimu ya ukoo wenu na mababu?.

Kama unaambiwa tu uache kuvaa mavazi hayo yasiyokupasa hutaki kutii, unategemea vipi hayo maradhi ya muda mrefu na hizo shida zikuondoke????.. Kama tu kumtii Mungu ni shida utawezaje kutiisha fikra nyingine imtii Kristo? Sawasawa na hilo andiko??.

Mtii Mungu kwanza ndipo uwe na nguvu za kuwafanya wengine wamtii Kristo…Ukikosa utii kwa Mungu ndivyo unavyojimaliza mwenyewe…

Na si kumtii Mungu leo na kesho kuendelea na mambo mengine… Hapana! Bali biblia inatufundisha kuwa utii wetu unapaswa uwe endelevu ndipo tufikie kiwango cha “kutimia” kule biblia unakokusema, ndipo matokeo yatakapoonekana.

Yakobo 4:7 “Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia. 4.8  Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili”.

Je umeitii Injili?, Je umeitii kazi ya Mungu na maagizo yake yote?

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

KUTII NI BORA KULIKO DHABIHU.

Ngome ni nini?  Kwanini Mungu anafananishwa na ngome?

Utii ni nini? na ni nani tunayepaswa kumtii au kutokumtii?

Nini maana ya Mithali 19:21Mna hila nyingi moyoni mwa mtu; Lakini shauri la Bwana ndilo litakalosimama.

Je idadi ya askari waliohesabiwa katika 1Nyakati 21:5 na 2Samweli 24:9 inajichanganya?.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments