Swali: Utajuaje ufahamu wako umetekwa au ni viashiria gani vitakavyotambulisha kuwa ufahamu umetekwa na adui?
Jina la Bwana YESU libarikiwe.
Kabla ya kujipima kama ufahamu umechukuliwa au la!..Ni vizuri kwanza tukajua kibiblia mtu mwenye ufahamu anatafsiriwaje?
Turejee kile kitabu cha Ayubu 28:28.
Ayubu 28:28 “Kisha akamwambia mwanadamu, Tazama, kumcha Bwana ndiyo hekima, NA KUJITENGA NA UOVU NDIO UFAHAMU”
Kwahiyo kumbe Mtu anayeweza kujitenga na Uovu ndiye mwenye ufahamu…maana yake kinyume chake yule asiyeweza kujitenga na uovu hana Ufahamu…au kwa lugha nyingine “UFAHAMU WAKE UMETEKWA”.
Na hapo neno linasema “kujitenga na uovu” na sio “kujizuia na uovu”… maana yake “unakaa nao mbali”... Kama ni ulevi mtu anakaa nao mbali, kuanzia mazingira ya kulewa mpaka makundi ya walevi (wote anajitenga nao).
Kama ni uasherati na uzinzi, mtu anakaa nao mbali kuanzia mawasiliano, mavazi, makundi…vile vile anajitenga na mazingira yote yanayochochea hiyo dhambi ikiwemo mazungumzo na mitandao.
Kama ni usengenyaji, mtu anajitenga na mazingira hayo na makundi yote..
Kama ni utukanaji vivyo hivyo, Kama ni wizi/ufisadi au utukanaji na hasira ni hivyo hivyo..
Lakini kinyume chake mtu asiyeweza kujitenga na hayo yote basi UFAHAMU WAKE UMECHUKULIWA (UMETEKWA)!!...Upo chini ya Milki ya mkuu wa giza. Anatumikishwa na mamlaka za giza.
Haijalishi kama ni mchungaji, au askofu, au Nabii, au Mtume, au mwimbaji wa kwaya, au Papa, au Raisi wa nchi, au mtu mwingine yoyote mwenye kuheshimika katika jamii au kanisa.
Mtu asiyeweza kujiepusha na UOVU ufahamu wake haupo (Umefungwa na kamba za kuzimu)., haijalishi ana uwezo mkubwa kiasi gani wa kupambanua mambo ya kimwili, haijalishi ana elimu kubwa kiasi gani na anategemewa na watu wengi kiasi gani katika kutatua mambo…bado ufahamu wake haupo!.
UTAURUDISHAJE UFAHAMU WAKO?.
Hakuna mtu ambaye kwa nguvu zake ana uwezo wa kuurudisha ufahamu wake!… Isipokuwa kwa msaada wa Mungu tu…Na msaada huu unaanza pale tunapoamua kufanya mageuzi katika maisha yetu kwa kutubia dhambi zetu na kumkiri Mwokozi YESU.
Ambapo kama tutatubu kwa kumaanisha kweli basi atatupa kipawa cha Roho wake mtakatifu ambaye kupitia huyo basi ataurejesha ufahamu uliochukuliwa na ile nguvu ya kuushinda uovu na kujitenga nao itakuwa juu yetu.
Faida ya kwanza ya ufahamu wa mtu kurudi ndani yake ni UZIMA WA MILELE lakini pia UZIMA WA MAISHA ya duniani, kwani ufahamu wa roho ndio unaofungua kufahamu mambo mengine yote.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Mafundisho mengine:
Rudi Nyumbani
Print this post