Tunaposoma biblia tunajifunza mambo mengi sana, yahusuyo tabia za Mungu, na moja ya tabia ya kipekee sana ya Mungu ni “kutokumlazimisha mtu kufanya jambo Fulani”. Kuna kipindi nilitamani na nilimuomba sana Roho Mtakatifu anivae na kuniendesha pasipo mimi mwenyewe kujitambua kama vile mtu aliyepagawa na mapepo.
Kwasababu watu wenye roho za mashetani huwa wanaendeshwa mpaka wanakuwa hajitambui tena mfano vichaa. Niliendelea kuomba hivyo mpaka siku Bwana aliponipa ufahamu na kugundua kuwa Mungu hatendi kazi kwa namna hiyo japo anao uwezo huo, lakini hamvai mtu na kumfanya mateka kama vile pepo linavyofanya.
Roho Mtakatifu ni msaidizi na mshauri na pia ni mpole, kamwe hamlazimishi mtu kuchukua uamuzi Fulani, Na ndio maana mtu anapoamua kuwa mwovu, haendi kumlazimisha aokoke, yeye anachofanya ni kumshawishi na kumshauri na kumpa kila sababu ya kuacha dhambi, lakini akikataa anamwacha aendelee kufanya anachokitaka lakini akikubali anaendelea naye.