Fumo ni mkuki, lakini katika biblia Neno mkuki linatumika kwa namna mbili, upo mkuki wa kuchomea, na pia upo mkuki wa kurusha.
Ule mkuki wa kuchomea ndio unaoitwa Fumo, ambao askari wanaubeba, na kuchoma maadui zao pale wanapowakaribia, na kwa kawaida unakuwa ni mizito kidogo na mrefu na wenye ncha kali. Lakini ule mwingine wa kurusha wenyewe kibiblia unajulikana kama mkuki tu hivyo hivyo, isipokuwa wenyewe ni mwepesi kidogo na umetengenezwa hivyo ili utakaporushwa uweze kufika mbali zaidi adui alipo. Zote hizi ni silaha za kivita.
Hivyo unaweza kukutana na haya maneno mawili kwenye biblia yakakuchanganya.. kwa mfano baadhi ya vifungu vinayatajwa maneno yote mawili ni kama vifuatavyo.
1Samweli 17:45 “Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana”.
Ayubu 41:26 “Mtu akimpiga kwa upanga, haumwingii; Wala fumo, wala mshale, wala mkuki wenye ncha”.
Vifungu vingine ambavyo utakutana na hili neno “Fumo” Ni kama vifuatavyo;
Hesabu 25:7 “Naye Finehasi mwana wa Eleazari, mwana wa Haruni kuhani, alipoona jambo hilo, akaondoka hapo katikati ya mkutano, akashika fumo mkononi mwake;
8 akamwandama huyo mtu wa Israeli na kuingia ndani ya hema nyuma yake, naye akawachoma wote wawili kwa fumo lake, yule mume wa Israeli na huyo mwanamke kati ya tumbo lake. Basi pigo likazuiwa kwao wana wa Israeli”.
1Samweli 17:7 “Na mti wa fumo lake ulikuwa kama mti wa mfumaji; na kichwa cha mkuki wake kilikuwa shekeli mia sita za chuma uzito wake; na mtu aliyemchukulia ngao yake akamtangulia”.
1Samweli 26:12 “Basi Daudi akalitwaa lile fumo, na lile gudulia la maji, kichwani pa Sauli; nao wakaenda zao, wala hapana mtu aliyeliona jambo hili wala kulijua, wala kuamka; maana wote walikuwa wamelala; kwa kuwa usingizi mzito kutoka kwa Bwana umewaangukia”.
Soma pia 2Samweli 1:6, Ayubu 39:23,
Halikadhalika na sisi kama wakristo rohoni ni lazima tuwe na FUMO zetu na MIKUKI yetu mikononi mwetu, ili tuitwe askari kamili wa Kristo, hizo ndio zile silaha za mkono wa kuume zinazozungumziwa katika 2Wakorintho 6:7… Kwa hizo, ndivyo tutakavyoweza kumpiga shetani, tukizikosa, tujue kuwa shetani hatoweza kutuogopa, na silaha yenyewe ni ufahamu wa kuyatambua mamlaka tuliyopewa katika jina la YESU na DAMU yake. Na kuyatumia..
Yeye mwenyewe alisema..
Luka 10:19 “Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru”.
Kila mmoja wetu ambaye anasema ameokoka anapaswa ajue kuwa mamlaka hayo amepewa, Hivyo simama kama shujaa, hubiri, haribu kazi za shetani, wafungue watu, mwaribu shetani na kazi zake zote katika maombi. Kwasababu Fumo zetu na mikuki yetu ipo mikononi mwetu.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Birika ni nini?, na yale Matao matano katika birika la Bethzatha ni nini?.
Nini maana ya ombeni kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi wala siku ya sabato?.
Jibu: Kipo kifaa kinachoitwa Birika tulichozoea kukijua, ambacho kinatumika kuhifadhia chai au maji. Lakini pia neno hilo hilo birika lina maana ya “Bwawa” au “Dimbwi dogo”, lilolotengenezwa kwa kazi Fulani mahususi, Na Bwawa hilo linaweza kuwa limetengenezwa kwa utaalamu mkubwa au pasipo utaalamu mkubwa, kufuatia matumizi ya bwawa hilo.
Sasa katika biblia yalikuwepo mabirika mengi, yalikuwepo yaliyotengenezwa kwa kunyweshea wanyama maji mfano hayo ni lile la Yakobo..
Mwanzo 30:38 “Akazisimamisha fito hizo alizozibambua katika mabirika ya kunyweshea maji, pale walipokuja wanyama wanywe; wakachukua mimba walipokuja kunywa.”
Unaweza pia kusoma mfano wa hayo katika 2Nyakati 26:10.
Na pia yalikuwepo mabirika yaliyochimbwa ardhini kwa ajili ya kuhifadhia maji, mfano wa hayo, ni lile Yusufu alilotupwa na ndugu zake..
Mwanzo 37:23 “Ikawa Yusufu alipofika kwa ndugu zake, wakamvua Yusufu kanzu yake, kanzu ile ndefu aliyoivaa,
24 wakamtwaa wakamtupa katika birika; na hiyo birika ilikuwa tupu, hamna maji”.
Unaweza kusoma pia 1Samweli 13:6..
Na pia yalikuwepo mabirika yaliyotengenezwa kwaajili ya kuogea/kunawia. Mfano wa hayo ni yale yaliyotengenezwa katika hema ya Mungu na katika nyumba ya Mungu, maalumu kwa makuhani kujisafisha kabla ya kuingia ndani ya hema, au nyumba ya Mungu kufanya kazi za kikuhani..
Kutoka 30:17 “Bwana akanena na Musa, na kumwambia
18 Fanya na BIRIKA LA SHABA, na tako lake la shaba, ILI KUOGEA; nawe utaliweka kati ya hema ya kukutania na madhabahu, nawe utalitia maji.
19 Na Haruni na wanawe wataosha mikono yao na miguu yao humo;
20 hapo waingiapo ndani ya hema ya kukutania; watajiosha majini, ili wasife; au hapo watakapoikaribia madhabahu ili watumike, kumteketezea Bwana sadaka ya moto”
Pia unaweza kusoma juu ya birika hizo katika nyumba ya Mungu katika 1Wafalme 7:38-43 na 2Nyakati 4:6.
Pia yalikuwepo mabirika yaliyotengenezwa kwaajili ya kuogea makahaba..
1Wafalme 22:37 “Hivyo akafa mfalme, akachukuliwa Samaria, wakamzika mfalme huko Samaria.
38 Wakaliosha gari penye BIRIKA LA SAMARIA, na mbwa wakaramba damu yake; (BASI NDIPO WALIPOOGA MAKAHABA); sawasawa na neno la Bwana alilolinena”.
Lakini pia tunasoma katika agano jipya, yakitajwa tena aina nyingine ya mabirika. Na hayo si mengine zaidi ya birika la Siloamu (Yohana 9:7) na Birika la Bethzatha (Yohana 5:2).
Birika ya Bethzatha ilijengwa kwa lengo la kuhifadhi maji yatakayotumika hekaluni. Birika hii ilijengwa kwa kuzungushiwa “Matao matano”. Matao ni nguzo zilizosimamishwa kuzunguka birika hilo, na kulitia uvuli…na nafasi iliyokuwepo kati ya nguzo na nguzo ilikuwa ndio maingilio ya birika hiyo..
Yohana 5:2 “Na huko Yerusalemu penye mlango wa kondoo pana birika, iitwayo kwa Kiebrania Bethzatha, nayo ina matao matano .
3 Ndani ya hayo jamii kubwa ya wagonjwa walikuwa wamelala, vipofu, viwete, nao waliopooza, [wakingoja maji yachemke ”.
Kama tunavyoijua habari, Yule mngonjwa ambaye aliugua kwa miaka 38, na hakuwa na mtu wa kumwingiza birikani, pindi maji yanapochemka (yaani nguvu za Mungu zinaposhuka ndani ya yale maji), lakini alipokutana na Bwana Yesu, aliponywa siku ile ile pasipo kuingizwa birikani.
Hiyo ni kutufundisha kuwa hakuna matumaini kwenye maji ya upako, wala visima vya upako. Huyu aliugua miaka 38, na alikuwa anatumainia maji ya upako. Na kama sio Bwana Yesu kumhurumia pengine angekufa bila kupata msaada wowote.
Kristo mponyaji wa mwili na roho yupo, isipokuwa sisi tumemtupa nje, na badala yake tunatafuta miujiza kwa njia zisizo rasmi.
Hebu jifunze kwenye huo mfano… “Hapo inasema ndani ya hayo matao, JAMII KUBWA ya wagonjwa walikuwa wamelala, wakisubiri maji yachemke.”…wamelala!! wakisubiri!!..na matokeo ya kusubiri ndio hiyo miaka 38 bila matumaini!…Na wakati wakiwa wanasubiri kumbe mponyaji yupo ulimwenguni akitembea huko na huko akiponya na kufungua watu.. lakini hili kundi lingine kubwa huku limelala likisubiri!! Huku likijitumainisha na maji ya upako!…na kisima cha upako!!.
Na si ajabu huyu Bwana peke yake ndio angalau alikuwa na moyo wa kupokea kitu kipya, ndio maana Bwana akamfuata yeye peke yake.. lakini hao wengine wengi waliokuwa wanasubiria, tunaona Bwana hakuwafuata kuwaponya.. kwanini??.. Ni dhahiri kuwa wengi wao walishamsikia huko nje akifundisha na kuponya lakini kwasababu wanaamini zaidi katika maji yale ya upako, wakamdharau, pengine wamesikia Yesu akikuponya anakwambia acha dhambi, acha kisasi, kuwa mtu wa kusamehe, na ili hali wenyewe hawataki kuacha hayo.. Wenyewe wanataka wakishapona waendelee na maisha yao, wasipewe pewe maelekezo ya maisha, ndio maana wakalipenda zaidi lile birika kwasababu ukishaponywa huambiwi chochote…hata kama ulikuwa kahaba na muuaji, ukishaponywa unaweza kuendelea na ukahaba wako.
Ndugu, jihadhari na miujiza BUBU, ambayo unaambiwa njoo ogea maji haya, upone… lakini hugusiwi habari ya dhambi zilizokufunga!.. Unaambiwa njoo ugea maji haya, lakini huambiwi huyo mke/mume unayeishi naye si wako!..huambiwi kwamba unaishi katika uzinzi na ukifa unaenda jehanamu!!.. Na ndio maana unahangaika miaka na miaka kununua maji haya na yale, mafuta haya na yale, kuzunguka katika kisima hiki na kile, kutafuta uponyaji lakini hupati!!..Ni kwanini?.. Ni kwasababu umemtupa Kristo na maneno yake nje!, halafu unatafuta uponyaji kwa njia mbadala..
Ndugu achana na hivyo visima bubu, Kristo kashavilaani!!…achana na hayo mabirika na madimbwi hayana msaada kwa nyakati hizi!!!…haijalishi yanalitaja jina la Mungu kiasi gani!..hili birika la Bethzatha lilikuwepo karibu sana na Hekalu la Mungu, lakini Kristo hakulitukuza!!!….Na wewe ndio maana pengine umekaa muda mrefu, ukitumainia hivyo visima na hakuna chochote!!.. Achana navyo, mtafute yeye..atakuponya na kukupa Maelekezo bora ya maisha ambayo yataiokoa roho yako, na hata kukuponya….
Na pia kama hujampokea Yesu, saa ya wokovu ni sasa, mwamini leo, na ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa maji tele na kwa Jina la Yesu. Na utakuwa umemfungulia Roho Mtakatifu njia ya kukuongoza katika kweli yote ya maandiko. Bwana Yesu yupo karibu na hicho kisima akitafuta tafuta ni nani aliye tayari kusikia, na kumkubali.. Uwe wewe leo! Katika Jina la Yesu.
Maran atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
SWALI: Nini maana ya hili neno,
Mathayo 21:44 “Naye aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjika-vunjika; naye ye yote ambaye litamwangukia, litamsaga tikitiki.
45 Wakuu wa makuhani na Mafarisayo, waliposikia mifano yake, walitambua ya kuwa anawanenea wao”.
JIBU: Shalom.
Maneno hayo aliyasema Bwana Yesu kuonyesha tabia ya jiwe hilo analolizungumzia.
Hapo anaposema mtu atakayeanguka juu yake atavunjika-vunjika, ni kuonyesha kuwa jiwe hilo ni “Gumu sana”, na sio laini, useme labda ni la udongo au kitu kingine, hapana ni ligumu kiasi kwamba ukilidondokea tu ni lazima uvunjike hakuna namna.
Vilevile aliposema, na yeyote atakayeangukiwa nalo,litamsaga tikitiki, ni kuonyesha kuwa jiwe hilo ni “zito sana” na kubwa.. kama lingekuwa ni jiwe dogo tu, na jepesi, lisingeweza kumsaga saga mtu pale linapomwangukia. Lakini mpaka linamponda ponda ni kuonyesha kuwa jiwe hilo ni zito sana.
Hivyo hapo ni Bwana alikuwa anaonyesha UGUMU, na UZITO wa jiwe hilo. Na jiwe lenyewe ni yeye mwenyewe.
Lakini badala watu wajenge juu ya jiwe hilo, wawe salama, kinyume chake Wapo watu wanaangukia juu ya jiwe hilo na wengine wanaangukiwa nalo.
Ikiwa wewe ni adui wa injili ya Kristo, unashindana na kazi za Mungu kutwa kuchwa, kazi yako ni kuididimiza kazi ya Mungu isisonge mbele, unafanya uchawi, unaloga, unapiga vita watu wa Mungu au unawavuta watu wasimjue Mungu kama alivyokuwa yule Elima mchawi aliyekutana na Paulo kule Pafo.. Ujue kuwa unahatarisha Maisha yako kwasababu ndivyo unavyoliangukia jiwe hili, na matokeo yake ni kuwa utavunjika vunjika, usiwe na faida yoyote hapa duniani.
Vilevile wapo watu muda wote, ni kuyaasi maagizo ya Kristo kwa makusudi, japokuwa wanaufahamu ukweli, hawa wapo kanisani, utawaona wanazini kwa makusudi na utakuta ni wachungaji au washirika wakongwe, wanafanya dhambi zao kwa siri, japokuwa kwa nje wanaonekana ni wema.. Sasa watu kama hawa, Upo wakati hili jiwe litawaangukia, na likishawaangukia hapo hakuna kupona tena, unasagika tikitiki. Wakati ambapo ghadhabu ya Mungu juu yako imefikia kilele, huwa hakuna kupona tena.
Na ndio maana Bwana Yesu aliyasema maneno hayo, kufuatana na habari aliyokuwa anaizungumzia juu kidogo, ya wale wakuu wa makuhani na mafarisayo ambao kazi yao ilikuwa ni kumvizia wamuue, ndipo akawapa mfano huo, Na kweli jitihada zao ziliishia kuangamizwa na Warumi mwaka 70 WK, ili kutimizwa ule unabii wa Yesu kuwa watazungukwa na maadui zao, watauliwa nao hawataachiwa jiwe juu ya jiwe. Mpaka leo tunavyozungumza wayahudi hawana mwelekeo wowote wa kiimani, kutokana na ile tabia yao ya kushindana na jiwe hilo.
Na jiwe hili ndilo litakalokuja kuangusha falme zote za duniani,
Danieli 2:34 “Nawe ukatazama hata jiwe likachongwa bila kazi ya mikono, nalo jiwe hilo likaipiga sanamu miguu yake, iliyokuwa ya chuma na udongo, likaivunja vipande vipande.
35 Ndipo kile chuma, na ule udongo, na ile shaba, na ile fedha, na ile dhahabu, vilivunjwa vipande vipande pamoja vikawa kama makapi ya viwanja vya kupepetea wakati wa hari; upepo ukavipeperusha hata pasionekane mahali pake; na lile jiwe lililoipiga hiyo sanamu likawa milima mikubwa, likaijaza dunia yote.
36 Hii ndiyo ile ndoto, nasi tutaihubiri tafsiri yake mbele ya mfalme”.
Nasi pia sisi tunapaswa tuwe makini sana na hii neema ya Yesu Kristo, badala ya kuliangukia jiwe hilo, au kuangukiwa nalo ni heri tujenge juu yake. Kwasababu yeye ndio mwamba salama. Tukijenga Maisha yetu kwa Kristo, basi tutayafurahia Maisha, ya hapa na kule ng’ambo tutakapovuka.
Je! Yesu yupo moyoni mwako? Kama hayupo ni heri ukamgeukia hivi sasa akufanye kuwa kiumbe kipya, na kukupa tumaini jipya la uzima wa milele. Acha kutanga tanga na hii dunia hizi ni siku za mwisho.
Bwana awabariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Zipo sheria zilizotoka kwa Mungu, na pia zipo sheria zilizotengenezwa na wanadamu lakini Mungu akaziruhusu zitumike kwa watu wake. Kwamfano katika biblia tunasoma kuwa wana wa Israeli waliruhusiwa kutoa talaka kwa wake zao, pia waliruhusiwa kuua (endapo mwanamke/mwanaume atakamatwa katika uzinzi, ilikuwa sharti auawe, kumbukumbu 22:22), Na pia wana wa Israeli, waliruhusiwa walipize kisasi kwa watu waovu, ikiwemo, jino kwa jino, uzima kwa uzima n.k.. Maana yake ni kwamba mtu akmpiga mwenzake mpaka kamng’oka jino, sharti na yeye jino lake ling’olewe, kama kamkata mtu mguu na yeye mguu wake utakatwa, kama kaua na yeye atauawa pia n.k (soma Kumbukumbu 16:21).
Sasa sheria hizi zilikuwepo katika Torati, lakini si Mungu aliyeziagiza.. Mungu tangu awali hakuagiza mtu kumwacha Mke wake au mume wake na kwenda kuoa/kuolewa na mwingine (Mwanzo 2:24), hali kadhalika, hakuaziga mtu kuua!..(Tutakuja kuliona hilo vizuri mbeleni katika somo hili, wakati Bwana Yesu analiweka hilo sawa).
Hivyo hizi sheria zilitungwa na watu wa Kale, kufuatia taratibu zao, kwaufupi zilikuwa ni desturi karibia za dunia nzima, kipindi hata wana wa Israeli wakiwa Misri, sheria hizi walizitumia huko Misri pia, sheria za kuoa na kuachana!, sheria za kulipiza kisasi, (jino kwa jino, jicho kwa jicho n.k)..hivyo walipotolewa huko Misri na kuletwa katika nchi ya Ahadi, bado mioyo yao ilikuwa imeshikamana na hizo sheria na walikuwa hawapo tayari kuachana nazo..MIOYO YAO ILIKUWA MIZITO!! (Migumu). Kwahiyo kutokana na ugumu wa mioyo yao hiyo, kutokuwa tayari kuziacha hizo sheria, ndipo Mungu akaziruhusu waendelee nazo kwa kitambo mpaka Nyakati mpya zitakapofika za Matengenezo (Yaani kipindi cha Bwana na mwokozi wetu Yesu). Ndio maana Bwana Yesu alipokuja akaanza kwa kusema…
Mathayo 19:3 “Basi Mafarisayo wakamwendea, wakamjaribu, wakimwambia, Je! Ni halali mtu kumwacha mkewe kwa kila sababu?
4 Akajibu, akawaambia, Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke,
5 akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja?
6 Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe.
7 WAKAMWAMBIA, JINSI GANI BASI MUSA ALIAMURU KUMPA HATI YA TALAKA, NA KUMWACHA?
8 AKAWAAMBIA, MUSA, KWA SABABU YA UGUMU WA MIOYO YENU, ALIWAPA RUHUSA KUWAACHA WAKE ZENU; LAKINI TANGU MWANZO HAIKUWA HIVI.
9 Nami nawaambia ninyi, Kila mtu atakayemwacha mkewe, isipokuwa ni kwa sababu ya uasherati, akaoa mwingine, azini; naye amwoaye yule aliyeachwa azini”.
Hapo katika mstari wa 8, Bwana Yesu anasema.. “Kwasababu ya ugumu wa mioyo yao Musa aliwapa Ruhusa ya kuwaacha wake zao”..
Sasa hapo kuna jambo moja muhimu la kuzingatia.
Kama tulivyozungumza awali, tayari Wana wa Israeli walikuwa na sheria zao kichwani za kuwaongoza, ambazo walitokanazo huko Misri, hawakuwa tayari eti kuishi na wake zao milele, hata kama wamekosea adabu (walichojua ni kwamba mwanamke akikukosea adabu, unamweka kando na kuchukua mwingine).. Na pia mtu hawezi kupewa ruhusa, kama alikuwa hatafuti hiyo ruhusa.. Hapo biblia inasema.. “Musa aliwapa ruhusa”.. Maana yake tayari hicho kitu cha kuachana kilikuwa kwenye vichwa vyao, na walikuwa wanakishinikiza, na pia hawakuwa tayari kusikia mashauri yoyote kinyume na hayo. Hivyo Mungu akamwambia Musa awaruhusu waendelee na sheria yao hiyo, na Musa akawaruhusu, lakini haikuwa mpango kamili wa Mungu.(Warumi 1:28)
Kama tu ule wakati walipong’ang’ania kutaka mfalme, jambo ambalo Mungu hakuwaagiza, wala halikuwa mapenzi ya Mungu.. lakini waling’ang’ania hivyo hivyo na Mungu akaruhusu wajipatie mfalme (1Samweli 8:7), jambo ambalo halikumpendeza Mungu kabisa. Na ndio hivyo hivyo baadhi ya hizi sheria, zilikuja kutokana na ugumu wa mioyo yao kukataa kusikiliza mashauri bora ya Mungu, wakaruhusiwa kuendelea kuishi kwa sheria zao hizo zisizofaa…
Ndio maana agano la kale, halikuwa agano lililo kamili, mpaka Bwana Yesu alipokuja kulikamilisha..na kusema.. “mmesikia imenenwa”….”mmesikia imenenwa”…. “lakini mimi nawaambia”….. Na sehemu nyingine anasema… “Kwasababu ya ugumu wa mioyo yao, Musa aliwaruhusu kufanya hayo, lakini haikuwa hivyo tangu mwanzo”.
Ndugu sio mpango wa Mungu kulaani watu, sio maagizo wala mpango wa Mungu kuoa wanawake wengi, sio maagizo ya Mungu kumlaani adui yako..utauliza hiyo ipo wapi kwenye biblia…
Mathayo 5:43 “Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; 44 lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi,
45 ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki”.
Vile vile Sio maagizo ya Mungu sisi kulipiza visasi,hata kama tumefanyiwa jambo baya kiasi gani, katika ukristo hatuna jino kwa jino wala jicho kwa jicho, Sisi tunaushinda ubaya kwa wema na si ubaya kwa ubaya.
Warumi 12:20 “Lakini, Adui yako akiwa na njaa, mlishe; akiwa na kiu, mnyweshe; maana ufanyapo hivyo, utampalia makaa ya moto kichwani pake.
21 Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema”.
Jukumu tulilo nalo ni kuomba Bwana atuepushe na madhara yao, na kuwaombea waokolewe.
Maran atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Nini maana ya “Uchungu wa mauti ni dhambi, na nguvu za dhambi ni torati”
SWALI: Ni muda gani Bwana Yesu alisulibiwa. Je! Ni saa 3 asubuhi kama tunavyosoma kwenye Marko, au saa 6 mchana kama tunavyosoma katika Yohana.
JIBU: Tusome vifungu vyenyewe.
Marko 15:24 “Wakamsulibisha, wakagawa mavazi yake, wakayapigia kura kila mtu atwae nini.
25 Basi ilikuwa saa tatu, nao wakamsulibisha”.
Yohana 19:14 “Nayo ilikuwa Maandalio ya pasaka, yapata saa sita. Akawaambia Wayahudi, Tazama, Mfalme wenu!
15 Basi wale wakapiga kelele, Mwondoshe! Mwondoshe! Msulibishe! Pilato akawaambia, Je! Nimsulibishe mfalme wenu! Wakuu wa makuhani wakamjibu, Sisi hatuna mfalme ila Kaisari”.
Shalom.
Sababu ya utofauti wao ni kuwa uandishi wa Marko ulitumia mfumo wa saa za kiyahudi, wakati uandishi wa Yohana ulitumia mfumo wa saa za Kirumi.
Mfumo wa kiyahudi, kwa kawaida siku mpya huwa zinaanzia saa 12 asubuhi, Ndio maana kuna mahali Bwana Yesu alisema “Je! Saa za mchana si kumi na mbili? (Yohana 11:9)”
Inapoanza saa 1 ndio saa ya kwanza, inapofika saa mbili ndio saa ya pili, vivyo hivyo na saa ya tatu na kuendelea. Hivyo katika Marko, inatuambia Bwana Yesu alisulibiwa taa tatu asubuhi. Na ndio maana katika Marko tunaona Bwana Yesu alisulibiwa saa 3 asubuhi.
Lakini sasa tukirudi kwenye mfumo wa muda wa kirumi ambao, Yohana aliutumia, anatuambia muda wa saa 6 wayahudi ndio walimleta kwa Pilato, ni rahisi kudhani maandiko yanajipinga lakini hapana, kwa mfumo wa muda wa kirumi, saa moja ilikuwa inaanza saa 6 usiku. Kama ilivyo sasa.
Hivyo Walipomkamata na kumpeleka kwa Pilato, ni kwamba saa 6 zilikuwa zimeshapita tangu siku ilipoanza, ambayo ni sawa na saa 12 asubuhi. Hivyo shamra shamra zote, mpaka kumpiga mijeledi na kumtwika msalaba wake na kumpeleka Goligotha, ilikuwa imeshafika saa 3 asubuhi, ndipo akasulibiwa. Sawa sawa na maandiko ya Marko.
Kwa hiyo kwa kuhitimisha ni kuwa, Bwana wetu Yesu Kristo alisulibiwa saa 3 asubuhi,akafa saa 9 alasiri, na katika huo muda kuanza saa 6 mchana mpaka saa 9 alasiri ndio kulikuwa na lile giza, kisha akakata roho. Lakini Bwana Yesu hakusulibiwa saa 6 mchana.
Luka 23:44 “Hapo ilikuwa yapata saa sita, kukawa giza juu ya nchi yote hata saa kenda,
45 jua limepungua nuru yake; pazia la hekalu likapasuka katikati.
46 Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.
47 Alipokwisha kusema hayo alikata roho. Yule akida alipoona yaliyotukia, alimtukuza Mungu, akisema, Hakika yake, mtu huyu alikuwa mwenye haki”.
Bwana akubariki.
Je! Umeokoka? Je! Una habari kuwa tunaishi katika kizazi ambacho kinaweza kushuhudia tukio la kurudi kwa pili kwa Bwana Yesu Kristo, duniani? Kama bado unashikilia udhehebu au udini, fahamu kuwa Kristo haji kunyakuwa watu wa namna hiyo. Atakuja kunyakuwa watu waliozaliwa kweli mara ya pili, kwa maji na kwa Roho na kusimama katika utakatifu. Hao ndio watakaokwenda kwenye unyakuo. Na kundi hilo litakuwa ni dogo sana, kama biblia inavyotabiri ,lakini wengine wote waliosalia wataingia katika dhiki kuu ya mpinga-Kristo.
Swali nj je! Wewe utakuwa miongoni mwa hilo kundi dogo litakalokwenda kumlaki Bwana mawinguni? Jibu, unalo, injili umesikia, na uzuri ni kwamba wokovu unapatikana bure, ukiukosa ni umejitakia mwenyewe kwa akili zao.
Maran Atha.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Haijalishi utaudhiwa na watu kiasi gani, haijalishi utakuwa na maadui wengi kiasi gani, lakini kamwe Mungu hawezi kuwachukia kama unavyowachukia wewe.
Jicho lako linavyowaona wewe ni tofauti na Mungu anavyowaona, wewe unatamani waangamizwe wapotee, lakini Mungu anatamani waokolewe. Wewe unatamani mabaya yawakute lakini Bwana Mungu anatamani watubu ili wasipatwe na mabaya. Ukiifahamu vyema tabia hiyo ya Mungu, utaacha kupoteza muda, kuwatakia shari maadui zako. Badala yake utawaombea Bwana azidi kuwapa neema watubu, na madhara yao yasikupate.
Lakini ukiwaombea kwa Mungu wafe!.utakuwa unapoteza muda, kwasababu kabla hawajawa maadui zako, Mungu alijua kuwa watakuja kuwa maadui zako na akawaumba hivyo hivyo.. angekuwa na hasira nao sana, kama ulizonazo wewe, angewaangamiza kitambo sana, au hata asingewaumba kabisa.
Kwahiyo mpaka unaona wameumbwa fahamu kuwa tayari ni mpango kamili wa Mungu wao wawepo duniani, na tena Mungu kawaumba kwasababu anawapenda.
Ni maneno magumu hayo lakini ndio ukweli.. Kama mtu fulani unamchukia kwasababu kakusengenya, na unatamani Mungu amwue, hayo maombi yako yatafika ukingoni!..kwasababu Mungu hatamwua kama unavyotaka wewe. Lakini ukitaka maombi yako yawe na nguvu ni heri uombe Bwana Mungu ampe roho ya kutubu, hapo utakuwa umeomba sawasawa na mapenzi yake.
Kama kuna mtu amekufanyia jambo baya, au anakufanyia mabaya yanayokuudhi sana. Na wewe ukaenda kuketi kuomba kwa Bwana Mungu kwamba amwue na kumpoteza kabisa, nataka nikuambie hayo maombi yako unapoteza muda. Kwasababu Bwana Mungu hakumuumba ili amwue, bali aifikilie toba na kubadilika… Ndio lengo lake!..kamwe huwezi kumfundisha Mungu ubaya.
Ezekieli 18: 23 “Je! Mimi ninafurahia kufa kwake mtu mwovu? Asema Bwana MUNGU; si afadhali kwamba aghairi, na kuiacha njia yake, akaishi?”
2Petro 3:9b “….bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba”.
Mtu fulani kakuibia mali yako ambayo ni ya thamani, halafu unapiga magoti ukiomba kwamba Mungu amuue na kumuangamiza huko alipo, hayo maombi hayafiki popote. Maombi yenye tija na yanayompendeza Mungu, ni haya>> “Bwana wasamehe kwa kuwa hawajui watendalo”.
Mtu fulani kakuendea kwa mganga ili upatikane na madhara fulani, na wewe unapiga magoti na kusema “Bwana waangamizwe na kufa kabisa, hata maiti zao zisionekane”..huku ukinukuu mstari huu katika agano la kale Kutoka 22: 18 “Usimwache mwanamke mchawi kuishi”. Mbona unapomfumania mkeo, au mumeo kwenye uzinzi hunukuu huu mstari wa Agano la kale na kuutumia??.
Kumbukumbu 22: 22 “Akifumaniwa mtu mume amelala na mwanamke aliyeolewa na mume, na wafe wote wawili, mtu mume aliyelala na mwanamke, na yule mwanamke naye; ndivyo utakavyoondoa uovu katika Israeli”.
Au sio Mungu mmoja aliyezungumza hayo maneno??… Kama ni Mungu mmoja aliyesema usimwache mwanamke mchawi kuishi, ndio huyo huyo aliyesema mtu akishikwa kwenye uzinzi awe mwanamke au mwanaume sharti auawe, (tena amezungumza hayo kwa kinywa cha Nabii huyo huyo mmoja, Musa)..basi kwanini unachukua mstari mmoja na kuacha mwingine??.
Hivyo ni vyema kufahamu utendaji kazi wa Mungu katika agano la kale ni tofauti na utendaji kazi wake katika agano jipya..Katika agano la kale, kutokana na ugumu wa mioyo ya watu, watu walipewa ruhusa ya kuua wazinzi, kuua waabudu sanamu wote wanaoziabudu nje na kumwabudu Mungu wa Israeli, walipewa pia ruhusa ya kuwapiga kwa mawe wachawi, na watu wote wenye pepo waliokuwa wanaishi katika nchi, walipewa ruhusa ya kuua watu waliomlaani/kumtukana Mungu, walipewa ruhusa ya kuwatenga watu wenye ukoma n.k. Na hiyo yote ni kutokana na ugumu wa mioyo yao, na wala si kwasababu ulikuwa ni mpango kamili wa Mungu. Mpango kamili wa Mungu ulikuja kuletwa na Bwana Yesu pale aliposema..
Mathayo 5:21 “Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue, na mtu akiua, itampasa hukumu.
22 Bali mimi nawaambieni, Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza; na mtu akimwapiza, itampasa jehanum ya moto”.
Mathayo 5.38 “Mmesikia kwamba imenenwa, Jicho kwa jicho, na jino kwa jino;
39 Lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili.
40 Na mtu atakaye kukushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia.
41 Na mtu atakayekulazimisha mwendo wa maili moja, nenda naye mbili”.
Mathayo 5:43 “Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako;
44 lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi,
45 ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki”.
Kwahiyo hakuna jino kwa jino katika Ukristo, wala hakuna kumpiga kwa mawe mtu yeyote anayefumaniwa katika uzinzi, wala hakuna kumuua mchawi yeyote, wala haturuhusiwi kuwachukia maadui zetu. Haja za mioyo yetu kwa Mungu, na sala zetu, ni kwamba Bwana atuepushe na madhara yote yanayoweza kufanywa na wao wanaotuchukia, na Bwana azifedheheshe kazi zao, ili mwisho wanapoona kuwa hazina madhara yoyote kwetu, watubu na kumfuata Mungu wetu sisi, hilo ndio lengo la kwanza la Mungu. Lakini si wafe katika dhambi zao hizo.
Kwahiyo huwezi kumfundisha Mungu uovu, yeye atabaki kuwa mkamilifu siku zote, anawaangazia jua lake waovu na wema, huwezi kumbadilisha yeye kuwa hivyo, hata uombe maombi ya namna gani, isipokuwa anachokitaka kwetu ni sisi kuwa kama yeye, tuwe na huruma kama yeye, tuwe wenye rehema kama yeye, tuwe wenye fadhili kama yeye, tuwe watakatifu kama yeye.
Mathayo 5:46 “Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo?
47 Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo?
48 Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu”.
Bwana atubariki wote.
Kama hujampokea Yesu, jitafakari mara mbili unasubiri nini?. Injili si habari za kuburudisha kama tunazozisoma katika magazeti, bali ni ushuhuda, maana yake kila unapoisoma mahali au kuisikia mahali, inarekodiwa kuwa ulishawahi kuisikia, kwahiyo kama ukiipuuzia na kuiacha, na yule mwovu akaja kuchukua kile kilichopandwa ndani yako, kuna hatari kubwa sana itakayokukuta baada ya maisha haya.
Hivyo mpokee leo Kristo leo maishani mwako na wala usingoje kesho, kwasababu hujui yatakayozaliwa ndani ya siku moja, biblia inasema hivyo katika Mithali 27:1, na pia katafute ubatizo sahihi wa maji tele (Yohana 3:23) na kwa Jina la Yesu Kristo (Matendo 2:38),kama bado hujabatizwa ubatizo sahihi. Na Roho Mtakatifu atashuka juu yako kukuongoza katika kweli yote.
Maran atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo. jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
Nakusalimu katika jina lipitalo majina yote la Bwana wetu Yesu Kristo. Karibu tena tujifunze maneno ya uzima..
Wakati ule wanamsulibisha Bwana Yesu, walipoona jua linakaribia kuchwa na waliowasulibisha bado hawajafa, wayahudi walienda kumuomba Pilato awavunje miguu ili waviharakishe vifo vyao, ikumbukwe kuwa kulingana na sheria za wayahudi ilikuwa ni tendo la kinajisi, kuiacha maiti ya mhalifu msalabani mpaka jioni ya sabato,
Hivyo njia waliyoiona inafaa ni kwenda kumuomba Pilato awavunje miguu yao, ili kusaidia wafe haraka, kwani kwa kuvunjwa kule kungewapelekea damu nyingi kuvuja kwa ndani, na vilevile kushindwa kunyanyua miguu juu, ambayo huwa kwa kawaida inarahisisha kupumua. Hivyo kwa kitendo kile cha kuwavunja ingewachukua tu dakika kadhaa mpaka wafe.
Lakini kama ingekuwa sio kwa ajili ya torati yao, kwa kawaida uuaji wa kirumi huwa mtu haondolewi pale msalabani mpaka afe mwenyewe. Na hiyo inaweza kuchukua siku kadhaa, na wanafanya hivyo kwa makusudi kabisa ili mtu huyo afe kifo cha mateso, wahakikishe mpaka wale tai wala mizoga wanashuka juu yake kuila maiti yake ndio wanamtoa.
Sasa kama tunavyojua habari ni kwamba waliwavunja wale wahalifu wote miguu lakini walipofika kwa Bwana Yesu ili wamvunje walimwona tayari ameshakwisha kufa, hivyo hawakumvunja mfupa wake hata mmoja badala yake wakamchoma mkuki ubavuni kuhakikisha kifo chake kama ni kweli.. Tusome..
Yohana 19:31 “Basi Wayahudi, kwa sababu ni Maandalio, miili isikae juu ya misalaba siku ya sabato, (maana sabato ile ilikuwa siku kubwa), walimwomba Pilato miguu yao ivunjwe, wakaondolewe.
32 Basi askari wakaenda, wakamvunja miguu wa kwanza, na wa pili, aliyesulibiwa pamoja naye.
33 Lakini walipomjia Yesu na kuona ya kuwa amekwisha kufa, hawakumvunja miguu;
34 lakini askari mmojawapo alimchoma ubavu kwa mkuki; na mara ikatoka damu na maji.
35 Naye aliyeona ameshuhudia, na ushuhuda wake ni kweli; naye anajua ya kuwa anasema kweli ili ninyi nanyi mpate kusadiki.
36 Kwa maana hayo yalitukia ili andiko litimie, Hapana mfupa wake utakaovunjwa”.
SASA NI KWANINI MIFUPA YAKE HAIKUVUNJWA? KULIKUWA NA ULAZIMA GANI WA JAMBO HILO KUPEWA UZITO KATIKA MAANDIKO?..
Sababu zipo mbili.
Ikumbukwe kuwa wakati ule wana wa Israeli walipokuwa wanatoka Misri, Mungu alipowapa maagizo ya kumchinja yule pasaka(kondoo) na kisha damu yake waipake kwenye miimo ya milango yao ili yule malaika atoaye roho akipita asiingie milangoni mwao, Na tunaona waliambiwa wamuandae pasaka huyo akiwa hana kasoro yoyote, na pia watakapomla asivunjwe mfupa wake wowote.
Kutoka 12:45 “Akaaye kwenu hali ya ugeni, na mtumishi aliyeajiriwa, wasimle pasaka.
46 Na aliwe ndani ya nyumba moja; usiichukue nje ya nyumba nyama yake yo yote; WALA MSIVUNJE MFUPA WAKE UWAO WOTE”.
Unaona, hivyo Kristo kutovunjwa mifupa yake, ilikuwa ni kumthibitisha kuwa yeye ndiye yule pasaka wetu kweli kweli ( yaani mwanakondoo) , atakayechukua dhambi za watu sawasawa na Yohana mbatizaji alivyoonyeshwa katika Yohana 1:29
2) Sababu ya Pili ilikuwa ni kuonyesha kuwa mwili wa Kristo hauvunjwi.
Pamoja na kupitia mateso yote yale msalabani, kuteswa na kupigwa, kudhihakiwa, kugongelewa misumari, lakini bado viungo vyake viliendelea kushimana vilevile, havikuachana hata kimoja. Hiyo inafunua rohoni kuwa sisi kama viungo vya Kristo kama vile biblia inavyotuambia katika..Waefeso 5:30
“Kwa kuwa tu viungo vya mwili wake”.
Kwamba tunapaswa tushikamane kwa umoja na upendo. Hata kama tutapitia shida au dhiki nyingi kiasi gani. Tukumbuke kuwa mwili wa Kristo huwa hauvunjwi, miili mingine ndiyo inayovunjwa lakini wa Kristo huwa hauvunjwi.
ikiwa Imani yetu ni mmoja, ubatizo wetu ni mmoja, Bwana wetu ni mmoja, hatupaswi kutengana kwasababu zisizokuwa na maana, hatupaswi kuwekeana matabaka, au vinyongo, au viburi bali tushikamane kwa umoja ili tuujenge mwili wa Kristo.
Ni wajibu wa kila mmoja wetu kilitimiza hilo agizo kama Bwana Yesu mwenyewe alivyotuambia.
Yohana 17:22 “Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja”.
Hivyo tuweke akilini kuwa mtu yeyote anayeuvunja mwili wa Kristo, anakwenda kabisa kinyume na kanuni ya Mungu kwenye kanisa lake..
Shalom
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Maana ya neno “Mintarafu” ni “kuhusiana na”. Kwamfano ukitaka kutamka sentesi hii >> “sifahamu chochote kuhusiana na ujio wa pili wa Kristo” …. unaweza kusema… “Sifahamu chochote mintarafu ujio wa pili wa Kristo”..Hivyo neno mintarafu linasimama kuwakilisha neno “kuhusiana na”.
Katika biblia takatifu yenye vitabu 66, neno hilo limeonekana mara mbili tu. Na mara zote hizo mbili ni ndani ya kitabu kimoja cha Zaburi.
Zaburi 17:4 “Mintarafu matendo ya wanadamu; Kwa neno la midomo yako Nimejiepusha na njia za wenye jeuri.
5 Nyayo zangu zimeshikamana na njia zako, Hatua zangu hazikuondoshwa”.
Na pia tunasoma katika..
Zaburi 87: 5 “Naam, mintarafu Sayuni itasemwa, Huyu na huyu alizaliwa humo. Na Yeye Aliye juu Ataufanya imara. 6 Bwana atahesabu, awaandikapo mataifa, Huyu alizaliwa humo”.
Hivyo ndugu, kama hufahamu chochote kuhusiana na ujio wa pili wa Kristo, basi fahamu kuwa upo hatarini sana, ni vyema ukatafuta kwa bidii kujua saa, nyakati na majira tunayoishi.
Hizi ni siku za mwisho na Kristo yupo mlangoni. Je umejiandaa?
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
SWALI: Naomba kufahamu ufunuo wa mstari huu ni upi?
Kutoka 22:6 “Ukiwaka moto, na kushika penye miiba, na ngano zilizofungwa miganda, au ngano ambazo hazijakatwa, au shamba, likateketea; yeye aliyeuwasha huo moto lazima atalipa”.
JIBU: Kama vile biblia inavyotuambia katika kitabu cha Yakobo kuwa, moto ni kitu kidogo sana lakini kinawasha msitu mnene….Ndivyo ndimi zetu zilivyofananishwa na kitu kama hicho..
Yakobo 3:5 “…. Angalieni jinsi moto mdogo uwashavyo msitu mkubwa sana.
6 Nao ulimi ni moto; ule ulimwengu wa uovu, ule ulimi, umewekwa katika viungo vyetu, nao ndio uutiao mwili wote unajisi, huuwasha moto mfulizo wa maumbile, nao huwashwa moto na jehanum.
Hiyo ni kututahadharisha kuwa tunapaswa tuwe makini sana na vinywa vyetu, kwasababu madhara yatakayotokana navyo, Mungu atayadai yote mikononi mwetu, kwa mfano unapopanda mbegu za fitina katikati ya ndugu, (maneno ya uongo au ya chuki) ikapelekea mpaka wakatengana, au wakafikisha mahakamani, au wakapigana, au wakauana, ujue kuwa madhara hayo yote, Na hasara yote iliyotokea Mungu ataidai mikononi mwako.
Kumbuka moja ya mambo sita ambayo Mungu hapendezwi nayo ni pamoja na kupanda mbegu za fitina katikati ya ndugu.(Mithali 6:19).
Unapochonganisha ndoa za watu, ikapelekea mpaka wakaachana, pengine mpaka ndugu za pande zote mbili wakachukiana, watoto wakaishi bila pendo la wazazi wote, ujue kuwa wewe uliyehusika, utachukua makosa yao yote, Hutanusurika. Hata kama hukukusudia hiyo fitina ilete madhara makubwa kiasi kile.
Ukisababisha mpaka ndugu katika Bwana wakatenda dhambi kwa kujengeana chuki na vinyongo kwasababu ya usengenyaji wako, na uzushi wako, ufahamu kuwa wewe uliyehusika, utayachukua makosa yao yote.
Yakobo 3:6 “Nao ulimi ni moto; ule ulimwengu wa uovu, ule ulimi, umewekwa katika viungo vyetu, nao ndio uutiao mwili wote unajisi, huuwasha moto mfulizo wa maumbile, nao huwashwa moto na jehanum”.
Hivyo kabla hatujasema jambo fulani, au kabla hatujatoa taarifa za mtu kwa mwingine, tunapaswa tutafakari kwanza, na pia tuzithibitishe habari zenyewe, na tujiulize je kuna umuhimu wowote wa sisi kuzisema? Au kutoa siri Fulani kwa wengine? Kama upo basi ni vizuri kufanya hivyo. Lakini kama hakuna, ni heri tukazilinda ndimi zetu. Kwasababu madhara yatakayotokana na maneno yetu baadaye Mungu atayadai yote mikononi mwetu.
Hiyo ndio maana ya huo mstari;
Kutoka 22:6 “Ukiwaka moto, na kushika penye miiba, na ngano zilizofungwa miganda, au ngano ambazo hazijakatwa, au shamba, likateketea; yeye aliyeuwasha huo moto lazima atalipa”.
Shalom.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Kutoka 22:31 “Nanyi mtakuwa watu watakatifu kwangu mimi; kwa hiyo msiile nyama yo yote iliyoraruliwa huko kondeni na mnyama wa mwitu; mtawatupia mbwa nyama hiyo”.
Shalom,
Katika agano la kale Mungu aliwapa wana wa Israeli agizo la kutokula nyama yoyote ambayo hawakuiwinda wao. Hiyo yote ni kwasababu ya usalama wa miili yao. Na alifanya hivyo pia kulifundisha kanisa lake rohoni, jinsi linavyopaswa lienende katika maisha ya utakatifu.
Kwa namna ya kawaida ukikutana na swala aliyekufa porini, huwezi kumla kwasababu hujui kilichompelekea kuuliwa ni nini, pengine aliumwa na nyoka, halafu wewe unakwenda kumla, bila shaka utajikuta unaingia katika matatizo yasiyokuwa ya lazima. Au pengine aliuliwa kweli na simba, lakini baada ya muda mfupi wakatokea fisi, wakaanza kuila ila ile nyama, na wewe baadaye ukaikuta ukaichukua, hujui pengine waliacha bakteria gani wenye madhara, wewe unakula tu.
Na ndio maana Mungu aliwakataza sio tu kula mnyama aliyeraruliwa bali pia wasile kibudu cha aina yoyote.
Walawi 22:8 “Nyamafu au mnyama aliyeraruliwa na wanyama asile, asijitie unajisi kwa hiyo nyama; mimi ndimi Bwana”.
Ni sawa tu na sasahivi, ukienda dukani halafu ukauziwa soda iliyofunguliwa, ni wazi kuwa huwezi kuinywa..Kwasababu hujui aliyeifungua alikuwa na lengo gani, pengine alitia sumu ndani yake, au kama sio sumu, ni dhahiri kubwa hata ubora wake utakuwa umepungua, na imesha expire.. hivyo utakapokunywa utakuwa umejihatarisha wewe mwenyewe.
Na ndivyo ilivyo leo hii rohoni, Mungu anataka kila mkristo ajue wajibu wake.. Asiwe ni mtu wa kulishwa lishwa tu kila fundisho ambalo linaletwa mbele yake, bila ya yeye mwenyewe kulihakiki kwanza katika maandiko yake matakatifu ubora wake. Mungu anataka tuwe wenye tabia hii kuhakiki.
Ni lazima ulipime kwa Neno la Mungu, na ndio maana kuna umuhimu sana, wa wewe kama mkristo kusoma biblia kila siku, huku ukimwomba Roho Mtakatifu akusaidie kuyaelewa. Vinginevyo utalishwa hata yasiyokupasa. Hata ukiambiwa mti Fulani uliopandwa hapo uwani kwako ni ishara ya mauti, utaamini, na kwenda kuukata kwasababu hujui maandiko, ukiambiwa mjusi sebuleni ni roho ya mkosi, utakwenda kushindana na mijusi yote duniani, kwasababu hujui maandiko yanazungumzia nini kuhusiana na hayo mambo.
Neno la Bwana linatuambia..
1 Yohana 4:1 “Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani”.
Swali ni Je! wewe umekuwa ni wa kula kila unachokutana nacho njiani?..Je, ulishawahi kujishughulisha mwenyewe kutafuta mawindo yako? Au kuhakiki kuwa hicho unacholishwa ni salama, kimefungashwa vizuri na kwamba unajua chanzo chake ni nini?
Kama sivyo, anza sasa kufanya hivyo, kwasababu katika siku hizi za mwisho biblia inasema manabii wengi wa uongo watawadanganya wengi, hata yamkini wale walio wateule. Kwahiyo thibitisha ubora wa chakula chako kila siku. Mungu ametoa ruhusa kabisa kwa sisi kufanya hivyo. Usiseme tu AMEN! AMEN! Kwa kila fundisho unalolisikia au unalolisoma mitandaoni, lithibitishe kwanza ndipo ulipokee. Kama bado huelewi chanzo chake ni wapi, liache lipite kwa hao wengine, ambao biblia imewataja kama mbwa, kwasababu sikuzote mbwa hawachagui, wala hawajui kama hichi kimechacha, au kimeoza, au kina sumu, maadamu tu kinamwonekano wa kuliwa kwao ni chakula.
Lakini sisi sio mbwa, wa kupokea kila ufunuo au fundisho. Tuyahakiki yote. Tujitaabishe kuwinda mawindo yetu wenyewe. Watu wengi wamedanganywa na hawajui kuwa wamedanganywa kwa njia hii…Na ndio maana wengi wao wanashikilia udhehebu na udini, hata kama wataambiwa hakuna ziwa la moto, kwasababu kasisi wao kalithibitisha hilo wataamini.
Kutoka 22:31 “Nanyi mtakuwa watu watakatifu kwangu mimi; kwa hiyo msiile nyama yo yote iliyoraruliwa huko kondeni na mnyama wa mwitu; mtawatupia mbwa nyama hiyo”.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Nini maana ya “saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada?”