HAPANA MFUPA WAKE UTAKAOVUNJWA.

HAPANA MFUPA WAKE UTAKAOVUNJWA.

Nakusalimu katika jina lipitalo majina yote la Bwana wetu Yesu Kristo. Karibu tena tujifunze maneno ya uzima..

Wakati ule wanamsulibisha Bwana Yesu, walipoona jua linakaribia kuchwa na waliowasulibisha bado hawajafa, wayahudi walienda kumuomba Pilato awavunje miguu ili waviharakishe vifo vyao, ikumbukwe kuwa kulingana na sheria za wayahudi ilikuwa ni tendo la kinajisi, kuiacha maiti ya mhalifu msalabani mpaka jioni ya sabato,  

Hivyo njia waliyoiona inafaa ni kwenda kumuomba Pilato awavunje miguu yao, ili kusaidia wafe haraka, kwani kwa kuvunjwa kule kungewapelekea damu nyingi kuvuja kwa ndani, na vilevile kushindwa kunyanyua miguu juu, ambayo huwa kwa kawaida inarahisisha kupumua. Hivyo kwa kitendo kile cha kuwavunja ingewachukua tu  dakika kadhaa  mpaka wafe.

Lakini kama ingekuwa sio kwa ajili ya torati yao, kwa kawaida uuaji wa kirumi huwa mtu haondolewi pale msalabani mpaka afe mwenyewe. Na hiyo inaweza kuchukua siku kadhaa, na wanafanya hivyo kwa makusudi kabisa ili mtu huyo afe kifo cha mateso, wahakikishe mpaka wale tai wala mizoga wanashuka juu yake kuila maiti yake ndio wanamtoa.

Sasa kama tunavyojua habari ni kwamba  waliwavunja wale wahalifu wote miguu lakini walipofika  kwa Bwana Yesu ili wamvunje walimwona tayari ameshakwisha kufa, hivyo hawakumvunja mfupa wake hata mmoja badala yake wakamchoma mkuki ubavuni kuhakikisha kifo chake kama ni kweli.. Tusome..

Yohana 19:31 “Basi Wayahudi, kwa sababu ni Maandalio, miili isikae juu ya misalaba siku ya sabato, (maana sabato ile ilikuwa siku kubwa), walimwomba Pilato miguu yao ivunjwe, wakaondolewe.

32 Basi askari wakaenda, wakamvunja miguu wa kwanza, na wa pili, aliyesulibiwa pamoja naye.

33 Lakini walipomjia Yesu na kuona ya kuwa amekwisha kufa, hawakumvunja miguu;

34 lakini askari mmojawapo alimchoma ubavu kwa mkuki; na mara ikatoka damu na maji.

35 Naye aliyeona ameshuhudia, na ushuhuda wake ni kweli; naye anajua ya kuwa anasema kweli ili ninyi nanyi mpate kusadiki.

36 Kwa maana hayo yalitukia ili andiko litimie, Hapana mfupa wake utakaovunjwa”.

SASA NI KWANINI MIFUPA YAKE HAIKUVUNJWA? KULIKUWA NA ULAZIMA GANI WA JAMBO HILO KUPEWA UZITO KATIKA MAANDIKO?..

Sababu zipo mbili.

  1. Sababu ya kwanza ni kumthibitisha Kristo kuwa kweli yeye ndiyo pasaka wetu.

Ikumbukwe kuwa wakati ule wana wa Israeli walipokuwa wanatoka Misri, Mungu alipowapa maagizo ya kumchinja yule pasaka(kondoo) na kisha damu yake waipake kwenye miimo ya milango yao ili yule malaika atoaye roho akipita asiingie milangoni mwao, Na  tunaona waliambiwa wamuandae pasaka huyo akiwa hana kasoro yoyote, na pia watakapomla asivunjwe mfupa wake wowote.

Kutoka 12:45 “Akaaye kwenu hali ya ugeni, na mtumishi aliyeajiriwa, wasimle pasaka.

46 Na aliwe ndani ya nyumba moja; usiichukue nje ya nyumba nyama yake yo yote; WALA MSIVUNJE MFUPA WAKE UWAO WOTE”.

Unaona, hivyo Kristo kutovunjwa mifupa yake, ilikuwa ni kumthibitisha kuwa yeye ndiye yule pasaka wetu kweli kweli ( yaani mwanakondoo)  , atakayechukua dhambi za watu sawasawa na Yohana mbatizaji alivyoonyeshwa katika Yohana 1:29

2) Sababu ya Pili ilikuwa ni kuonyesha kuwa mwili wa Kristo hauvunjwi.

Pamoja na kupitia mateso yote yale msalabani, kuteswa  na kupigwa, kudhihakiwa, kugongelewa misumari, lakini bado viungo vyake viliendelea kushimana vilevile, havikuachana hata kimoja. Hiyo inafunua rohoni kuwa sisi kama viungo vya Kristo kama vile biblia inavyotuambia katika..Waefeso 5:30

“Kwa kuwa tu viungo vya mwili wake”.

Kwamba tunapaswa tushikamane kwa umoja na upendo. Hata kama tutapitia shida au dhiki nyingi kiasi gani. Tukumbuke kuwa mwili wa Kristo huwa hauvunjwi, miili mingine ndiyo inayovunjwa lakini wa Kristo huwa hauvunjwi.

ikiwa Imani yetu ni mmoja, ubatizo wetu ni mmoja, Bwana wetu ni mmoja, hatupaswi kutengana kwasababu zisizokuwa na maana, hatupaswi kuwekeana matabaka, au vinyongo, au viburi bali tushikamane kwa umoja ili tuujenge mwili wa Kristo.

Ni wajibu wa kila mmoja wetu kilitimiza hilo agizo kama Bwana Yesu mwenyewe alivyotuambia.

Yohana 17:22 “Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja”.

Hivyo tuweke akilini kuwa mtu yeyote anayeuvunja mwili wa Kristo, anakwenda kabisa kinyume na kanuni ya Mungu kwenye kanisa lake..

Shalom

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments