MMESIKIA KWAMBA IMENENWA?

MMESIKIA KWAMBA IMENENWA?

Zipo sheria zilizotoka kwa Mungu, na pia zipo sheria zilizotengenezwa na wanadamu lakini Mungu akaziruhusu zitumike kwa watu wake. Kwamfano katika biblia tunasoma kuwa wana wa Israeli waliruhusiwa kutoa talaka kwa wake zao, pia waliruhusiwa kuua (endapo mwanamke/mwanaume atakamatwa katika uzinzi, ilikuwa sharti auawe, kumbukumbu 22:22), Na pia wana wa Israeli, waliruhusiwa walipize kisasi kwa watu waovu, ikiwemo, jino kwa jino, uzima kwa uzima n.k.. Maana yake ni kwamba mtu akmpiga mwenzake mpaka kamng’oka jino, sharti na yeye jino lake ling’olewe, kama kamkata mtu mguu na yeye mguu wake utakatwa, kama kaua na yeye atauawa pia n.k (soma Kumbukumbu 16:21).

Sasa sheria hizi zilikuwepo katika Torati, lakini si Mungu aliyeziagiza.. Mungu tangu awali hakuagiza mtu kumwacha Mke wake au mume wake na kwenda kuoa/kuolewa na mwingine (Mwanzo 2:24), hali kadhalika, hakuaziga mtu kuua!..(Tutakuja kuliona hilo vizuri mbeleni katika somo hili, wakati Bwana Yesu analiweka hilo sawa).

Hivyo hizi sheria zilitungwa na watu wa Kale, kufuatia taratibu zao, kwaufupi zilikuwa ni desturi karibia za dunia nzima, kipindi hata wana wa Israeli wakiwa Misri, sheria hizi walizitumia huko Misri pia, sheria za kuoa na kuachana!, sheria za kulipiza kisasi, (jino kwa jino, jicho kwa jicho n.k)..hivyo walipotolewa huko Misri na kuletwa katika nchi ya Ahadi, bado mioyo yao ilikuwa imeshikamana na hizo sheria na walikuwa hawapo tayari kuachana nazo..MIOYO YAO ILIKUWA MIZITO!! (Migumu). Kwahiyo kutokana na ugumu wa mioyo yao hiyo, kutokuwa tayari kuziacha hizo sheria, ndipo Mungu akaziruhusu waendelee nazo kwa kitambo mpaka Nyakati mpya zitakapofika za Matengenezo (Yaani kipindi cha Bwana na mwokozi wetu Yesu). Ndio maana Bwana Yesu alipokuja akaanza kwa kusema…

Mathayo 19:3 “Basi Mafarisayo wakamwendea, wakamjaribu, wakimwambia, Je! Ni halali mtu kumwacha mkewe kwa kila sababu?

4 Akajibu, akawaambia, Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke,

5 akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja?

6 Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe.

7 WAKAMWAMBIA, JINSI GANI BASI MUSA ALIAMURU KUMPA HATI YA TALAKA, NA KUMWACHA?

8 AKAWAAMBIA, MUSA, KWA SABABU YA UGUMU WA MIOYO YENU, ALIWAPA RUHUSA KUWAACHA WAKE ZENU; LAKINI TANGU MWANZO HAIKUWA HIVI.

9 Nami nawaambia ninyi, Kila mtu atakayemwacha mkewe, isipokuwa ni kwa sababu ya uasherati, akaoa mwingine, azini; naye amwoaye yule aliyeachwa azini”.

Hapo katika mstari wa 8, Bwana Yesu anasema.. “Kwasababu ya ugumu wa mioyo yao Musa aliwapa Ruhusa ya kuwaacha wake zao”..

Sasa hapo kuna jambo moja muhimu la kuzingatia.

  • Ni Musa ndiye aliyewapa ruhusa.

Kama tulivyozungumza awali, tayari Wana wa Israeli walikuwa na sheria zao kichwani za kuwaongoza, ambazo walitokanazo huko Misri, hawakuwa tayari eti kuishi na wake zao milele, hata kama wamekosea adabu (walichojua ni kwamba mwanamke akikukosea adabu, unamweka kando na kuchukua mwingine).. Na pia mtu hawezi kupewa ruhusa, kama alikuwa hatafuti hiyo ruhusa.. Hapo biblia inasema.. “Musa aliwapa ruhusa”.. Maana yake tayari hicho kitu cha kuachana kilikuwa kwenye vichwa vyao, na walikuwa wanakishinikiza, na pia hawakuwa tayari kusikia mashauri yoyote kinyume na hayo. Hivyo Mungu akamwambia Musa awaruhusu waendelee na sheria yao hiyo, na Musa akawaruhusu, lakini haikuwa mpango kamili wa Mungu.(Warumi 1:28)

Kama tu ule wakati walipong’ang’ania kutaka mfalme, jambo ambalo Mungu hakuwaagiza, wala halikuwa mapenzi ya Mungu.. lakini waling’ang’ania hivyo hivyo na Mungu akaruhusu wajipatie mfalme (1Samweli 8:7), jambo ambalo halikumpendeza Mungu kabisa. Na ndio hivyo hivyo  baadhi ya hizi sheria, zilikuja kutokana na ugumu wa mioyo yao kukataa kusikiliza mashauri bora ya Mungu, wakaruhusiwa kuendelea kuishi kwa sheria zao hizo zisizofaa…

Ndio maana agano la kale, halikuwa agano lililo kamili, mpaka Bwana Yesu alipokuja kulikamilisha..na kusema.. “mmesikia imenenwa”….”mmesikia imenenwa”…. “lakini mimi nawaambia”….. Na sehemu nyingine anasema… “Kwasababu ya ugumu wa mioyo yao, Musa aliwaruhusu kufanya hayo, lakini haikuwa hivyo tangu mwanzo”.

Ndugu sio mpango wa Mungu kulaani watu, sio maagizo wala mpango wa Mungu kuoa wanawake wengi, sio maagizo ya Mungu kumlaani adui yako..utauliza hiyo ipo wapi kwenye biblia…

Mathayo 5:43 “Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; 44 lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi,

45 ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki”.

Vile vile Sio maagizo ya Mungu sisi kulipiza visasi,hata kama tumefanyiwa jambo baya kiasi gani, katika ukristo hatuna jino kwa jino wala jicho kwa jicho, Sisi tunaushinda ubaya kwa wema na si ubaya kwa ubaya.

Warumi 12:20 “Lakini, Adui yako akiwa na njaa, mlishe; akiwa na kiu, mnyweshe; maana ufanyapo hivyo, utampalia makaa ya moto kichwani pake.

21 Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema”.

Jukumu tulilo nalo ni kuomba Bwana atuepushe na madhara yao, na kuwaombea waokolewe.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

JE YESU AMEJIAMINISHA KWAKO?

Je watu ambao hawajasikia kabisa injili watahukumiwa?

 Nini maana ya “Uchungu wa mauti ni dhambi, na nguvu za dhambi ni torati”

Alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru

UTHABITI WA AGANO LA MUNGU KWA MKRISTO.

NJIA YA MSALABA

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments