Je! ile habari ya Herode kutaka kumwua Yohana mbatizaji inajichanganya?(Mathayo 14:5 na Marko 6:20).

Je! ile habari ya Herode kutaka kumwua Yohana mbatizaji inajichanganya?(Mathayo 14:5 na Marko 6:20).

Swali: Katika Mathayo 14:5 tunasoma kuwa Herode alitaka kumwua Yohana mbatizaji, lakini tukirudi katika  Marko 6:20 tunasoma habari nyingine tofauti kuwa Herode hakutaka kumwua Yohana mbatizaji, badala yake alimweshimu na kumwogopa na kumwona kama Nabii..je ni habari ipi iliyo sahihi kati ya hizo mbili?

Jibu: Awali ya yote tusome mistari hiyo..

Mathayo 14:3 “Maana Herode alikuwa amemkamata Yohana, akamfunga, akamtia gerezani, kwa ajili ya Herodia, mke wa Filipo nduguye.

4 Kwa sababu Yohana alimwambia, Si halali kwako kuwa naye.

5 NAYE ALIPOTAKA KUMWUA, ALIWAOGOPA WATU, MAANA WALIMWONA YOHANA KUWA NABII.

Hapa ni kweli tunasoma kuwa Herode alikusudia kumwua Yohana.. Lakini tusome tena Marko 6:17-20

Marko 6:17 “Kwa maana Herode mwenyewe alikuwa ametuma watu, akamkamata Yohana, akamfunga gerezani, kwa ajili ya Herodia, mkewe Filipo ndugu yake, kwa kuwa amemwoa;

18  kwa sababu Yohana alimwambia Herode, Si halali kwako kuwa na mke wa nduguyo.

19  Naye yule Herodia akawa akimvizia, akataka kumwua, asipate.

20  MAANA HERODE ALIMWOGOPA YOHANA; AKIMJUA KUWA NI MTU WA HAKI, MTAKATIFU, AKAMLINDA; NA ALIPOKWISHA KUMSIKILIZA ALIFADHAIKA SANA; NAYE ALIKUWA AKIMSIKILIZA KWA FURAHA.”

Hapa tunasoma Herode hakutaka kumwua Yohana, kwasababu alimwogopa na kuamini kuwa ni mtu wa haki. Sasa swali je! Habari hizi mbili zinajichanganya?

Jibu ni La! Hazijichanganyi!!, kwasababu waandishi wa vitabu hivyo walivuviwa na Roho Mtakatifu na pia biblia kamwe haijawahi kujichanganya, vinginevyo ingekuwa ni kitabu cha uongo!, lakini tunaona ni kitabu chenye nguvu na kilichojaa mafunuo yaliyo halisi, hivyo kinachojichanganya ni fahamu zetu na tafakari zetu katika kuyaelewa maandiko na si biblia.

Sasa tukirudi katika hiyo habari ya Herode,  tukianzia mistari ya juu katika vitabu vyote viwili, tunasoma Mfalme Herode (Antipa) alisikia habari za Yohana Mbatizaji na mahubiri yake, na Yohana katika kuhubiri kwake alimtaja Herode na kumwambia si halali yeye kuwa na mke wa ndugu yake (Mathayo 14:3-4).

Lakini kwasababu Herode ni mtu wa heshima, na asingetaka masuala yake ya kindoa yachafuliwe hadharani tena na mtu aliye myahudi, alitafuta njia ya kumwua Yohana Mbatizaji, lakini alikosa kwasababu muda wote Yohana alikuwa akizungukwa na watu, (Mathayo 14:5) na wayahudi wote walimwamini Yohana kama nabii wa Mungu, hivyo laiti kama Herode angechukua maamuzi ya haraka ya kumwua Yohana mbele ya umma ingekuwa ni hatari kwa ufalme wake, kama tu jinsi mafarisayo walivyoogopa kumkosoa Yohana mbele ya umati, kwa hofu ya kupigwa mawe (Luka 20:6), au kama jinsi wakuu wa makuhani walivyoogopa kumkamata Bwana Yesu wamwue, kwaajili ya makutano (Luka 22:2).

Hivyo njia aliyotumia Herode ni kumkata Yohana na kumfunga gerezani, ikiwa nia yake ni kumtenga na makutano na mwisho aweze kufanikisha nia yake ya kumwua. Na wakati huo huo mkewe Herodia, alikuwa akimsapoti Herode katika mpango huo.

Lakini tunavyozidi kuisoma habari hiyo tunaona Herode alikuja kubadilisha mawazo baadaye.. kwani baada ya kumtia Yohana mbatizaji gerezani, kuna vipindi ambavyo havijatajwa huenda Herode alikuwa anaenda gerezani kumsikiliza Yohana, au alikuwa analetewa mahubiri ya Yohana kutoka gerezani (kwasababu hata Yohana alivyokuwa gerezani bado wanafunzi wake walikuwa wanaweza kwenda kumtembelea na kumpelekea habari au yeye mwenyewe kuwatuma wapeleke habari, soma Luka 7:18-20).

Na hayo yakamfanya  Herode abadili mtazamo na maamuzi, na kumwamini kuwa ni mtu wa Mungu, ijapokuwa anamweleza maneno ya kumchoma na kumkera (Soma Marko 6:20), hivyo akaamua kubadili mawazo na kufikiri kutomuua!.

Lakini mkewe Herodia akawa na wazo lile lile la kumuua, na Herode akawa anatafuta njia ya kumlinda Yohana asiuawe na Herodia (Marko 6:19). Wakiwa katika hayo mazingira, Herodia akapata nafasi siku ile ya sikuku ya kuzaliwa kwa Herode ambapo alimtumia binti yake kukitaka kichwa cha Yohana Mbatizaji, na kutokana na nadhiri Herode alizoziweka mbele ya binti yake na mbele ya umati wote wa watu, alishindwa kukataa..kwani ingeudhoofisha ufalme wake, hivyo akaruhusu Yohana akakatwe kichwa ingawa si kwa mapenzi yake!.

Mathayo 14:6 “Hata ilipofika sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti Herodia alicheza mbele ya watu, akampendeza Herode.

7  Hata akaahidi kwa kiapo ya kwamba atampa lo lote atakaloliomba.

8  Naye, huku akichochewa na mamaye, akasema, Nipe hapa katika kombe kichwa cha Yohana Mbatizaji.

9  Naye mfalme akasikitika; lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya wale walioketi chakulani pamoja naye, akaamuru apewe;

10  akatuma mtu, akamkata kichwa Yohana mle gerezani”.

Kwahiyo kwa hitimisho ni kwamba… Herode alibadili mawazo yake juu ya Yohana, hivyo biblia haijichanganyi.

Lakini pia ni funzo gani tunalipata katika habari hii ya Herode na Herodia mke wa ndugu yake?

Funzo kuu tunalolipata ni kuwa si halali mtu kumwacha mke wake au mume wake na kwenda kuoa au kuolewa na mwingine.

Luka 16:18 “Kila amwachaye mkewe na kumwoa mke mwingine azini; naye amwoaye yeye aliyeachwa na mumewe azini”.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mada Nyinginezo:

Je! habari ya muda aliotawala Mfalme Yekonia inajichanganya? (2Wafalme 24:8 na 2Nyakati 36:9).

Swali: Je idadi ya askari waliohesabiwa katika 1Nyakati 21:5 na 2Samweli 24:9 inajichanganya?.

Yohana mbatizaji alibatizwa na nani?

Je ni nyaraka zipi mtume Paulo aliziandikia gerezani?

MAPAMBO YA WANAWAKE WALIOUKIRI UCHAJI WA MUNGU.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Lucas
Lucas
8 months ago

Amen…🙏🙏🤝