Kama unao uhakika huo basi ni jambo jema lakini swali, ni kitu gani kinachokupa uhakika huo?.
Je! Ni imani uliyonayo?..au Ni dhehebu ulilonalo?, Au ni matendo unayoyafanya?…au ni nini?.
Kama ni Imani (kwamba unamwamini na akija ni lazima uende naye) basi fahamu kuwa anaweza akaja na usiende naye ijapokuwa unayo imani.
Kama ni dhehebu ndilo linalokupa uhakika wa kwenda na Bwana pindi atakaporudi, basi fahamu kuwa hio pekee haitoshi..
Pamoja na dhehebu lako bora, na jina lako bora bado unaweza usimwone siku atakaporudi..
Je ni Matendo yako mema ndiyo yanayokupa uhakika? (Kwamba hudhulumu mtu, hutukani,huibi, unasaidia wengine n.k)
Kama ni matendo tu, ndio yanayokupa uhakika wa kwenda na Bwana, basi fahamu kuwa atakaporudi unaweza pia usimwone.
Sasa ni kitakachopaswa kumpa mtu uhakika ya kwamba atakapokuja BWANA basi ataenda naye??.
Hebu tuangalie jibu lake katika biblia, kupitia maneno ya Bwana YESU (Atakayerudi).
Yohana 3:1 “Basi palikuwa na mtu mmoja wa Mafarisayo, jina lake Nikodemo, mkuu wa Wayahudi.
2 Huyo alimjia usiku, akamwambia, Rabi, twajua ya kuwa u mwalimu, umetoka kwa Mungu; kwa maana hakuna mtu awezaye kuzifanya ishara hizi uzifanyazo wewe, isipokuwa Mungu yu pamoja naye.
3 Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu”
Umeona sifa ya mtu atakayemwona Bwana siku ile?.
Si dhehebu kwasababu Nikodemo alikuwa ni wa dhehebu la Farisayo lililo bora (Matendo 26:5), wala si Imani kwa Mungu, kwasababu Nikodemo alikuwa tayari anamwamini Mungu na pia amemwamini YESU.
Lakini Bwana YESU anaonyesha kuwa hayo yote hayawezi kumsaidia mtu, isipokuwa kuzaliwa mara ya pili (kuwa kiumbe kipya katika roho).
Ni nini maana ya kuzaliwa mara ya pili???..Bwana YESU amefafanua katika mistari inayofuata kwamba ni kuzaliwa kwa maji na kwa Roho Mtakatifu (yaani ubatizo wa maji kama ishara ya utangulizi wa utakaso, na ubatizo wa Roho Mtakatifu).
Ubatizo wa Roho Mtakatifu ndio ukamilifu wa utakaso wa Mtu, na mtu anapoupokea huo pamoja na ubatizo wa Maji, anafanyika kuwa kiumbe kipya kupitia kazi za Roho Mtakatifu ndani yake.
Jambo hili limewekwa vizuri zaidi na Mtume Paulo kupitia waraka wake kwa Tito.
Tito 3:4 “Lakini wema wake Mwokozi wetu Mungu, na upendo wake kwa wanadamu, ulipofunuliwa, alituokoa;
5 si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu”.
Je swali umejazwa Roho Mtakatifu kama tiketi ya kumwona Bwana na kwenda naye siku ile?.
Waliojazwa Roho Mtakatifu, wanaongozwa na Roho Mtakatifu, na mtu aliyejaa Roho Mtakatifu, hawezi kuwa mtu wa kidunia, wala kuupenda ulimwengu..kwasababu roho iliyopo ndani yake inamsukuma kufikiri yaliyo ya juu.
Mtu alijaa Roho mtakatifu kama muhuri wa kumwona Bwana, hawezi kufanana kimwonekano na watu wa ulimwengu, badala yake anakuwa nuru kwao, na hawezi kushirikiana na matendo ya giza.
Na kama hauna uhakika Bwana akirudi hautaenda naye, ni vizuri ukapata huo uhakika…
Pengine unaweza kuhitimisha kwa kusema siku atakapokuja, kama nitaenda naye au sitaenda naye…“Mungu anajua”…lakini hebu fikiri hili…
“Mwalifu anatangaza kuwa atakuja kukudhuru”
Halafu wewe unasema siku atakapokuja, “yeye anajua kama atanidhuru au hatanidhuru”.
Umeona?..kama hautachukua tahadhari ni wazi kuwa atatimiza lengo lake..lakini kama utajidhatiti basi utapata uhakika kama atatimiza lengo lake au la!.. wala huwezi kamwe kumwachia maamuzi afanye yeye!!.
Vivyo hivyo na sisi ni lazima tuwe na uhakika kwamba atakapokuja tutakwenda naye au hatutakwenda naye, na si kumwachia yeye atufanyie maamuzi..
Tukimwachia yeye tutakuwa tumemfanya yeye kuwa mwenye upendeleo, na yeye hana upendeleo.
1Petro 1:17 “Na ikiwa mnamwita Baba, yeye ahukumuye kila mtu pasipo upendeleo, kwa kadiri ya kazi yake, enendeni kwa hofu katika wakati wenu wa kukaa hapa kama wageni”
Maran atha.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
NIMEOKOKA, ILA MUNGU NDIYE ANAYEJUA NITAKWENDA WAPI.
Waoga ambao hawataurithi uzima wa milele ni watu wa namna gani?(Ufunuo 21:8).
BIBLIA INAITAJA NJIA KUU YA MFALME, NJIA HII NI IPI?
About the author