NYWELE ZAKO ZIKUFUNDISHE, SAUTI YA MUNGU.

NYWELE ZAKO ZIKUFUNDISHE, SAUTI YA MUNGU.

Kwanini Mungu akuumbe hivyo ulivyo? Kwanini asingeweka pembe kichwani kwako, au kwanini asingekuwekea  vilemba vya nyama kama vile vya kuku kichwani, au antena mbili kama zile za konokono au mdudu, bali amekuwekea nywele kichwani pako.

Sauti ya Mungu ipo katika maumbile yetu. Sisi kujikuta hivi tulivyo sio kwamba, ndio umbile bora zaidi ya yote Mungu aliloona linamfaa mtu, hapana,  tungeweza kuumbwa vizuri zaidi hata ya mwonekano huo tulionao, lakini tumebuniwa hivi, kwa kusudi la kipekee ambalo tunapaswa tulijue, na sio kwa kusudi la urembo.

Kwamfano usipoweza kuelewa utendaji kazi wa mwili wako jinsi viungo vinavyoshirikiana huwezi kuelewa jinsi kanisa la Kristo linavyopaswa kufanya kazi likutanikapo, kwasababu sisi tunaitwa viungo mbalimbali ndani ya mwili wa Kristo.Umeona? Bwana akasema kiungo kimoja kikiumia, vyote vimeumia.

Hivyo tumeumbwa, kimalengo sio kimwonekano bora au kiuzuri,. Ni sawa na mtu aulizwe kati ya jiko, na maua kipi kina umuhimu zaidi kuwepo ndani mwako. Ni wazi kuwa atasema jiko,kwasababu litamsaidia kupika. Hakulichagua kwasababu lina mwonekano bora, lakini kwasababu lina matumizi muhimu zaidi ya vingine.

Vivyo hivyo na wewe ujitazamapo mwili wako, usijitazame kiuzuri kuliko  viumbe vingine, au wanadamu wenzako, bali fikiria tu katika picha ya matumizi ya kila kiungo ulichopewa, kinakufundisha nini kuhusu muumba wako au kinatimiza kusudi gani kwa Mungu wako. Hilo ndio lengo hasaa la wewe kubuniwa hivyo ulivyo.

Leo tutaanza na NYWELE, kisha wakati mwingine tutatazama na viungo vingine;

Utazamapo nywele zako Bwana anataka ujue yafuatayo;

  1. Mambo yako yote, yapo katika hesabu za Mungu.

Mathayo 10:30  lakini ninyi, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. 31  Msiogope basi; bora ninyi kuliko mashomoro wengi

Ni kawaida  kudhani kuwa Mungu hathamini, au hajui kila kitu, au anasahau sahau. Lakini sivyo, ukimfuata Mungu, vitu vyako vyote vinavyotoka na kuingia vipo kimahesabu, hakuna kitu kinachotokea kwa ghafla tu, bila yeye kujua au kuruhusu, Hivyo mashaka yakija, kumbuka nywele zako zilivyo nyingi lakini zimehesabiwa, vivyo hivyo mambo yako yote yamehesabiwa.

  1. Huwezi epukana na maadui.

Zaburi 69:4 Wanaonichukia bure ni wengi Kuliko nywele za kichwa changu. Watakao kunikatilia mbali wamekuwa hodari, Adui zangu kwa sababu isiyo kweli. Hata mimi nalilipishwa kwa nguvu Vitu nisivyovichukua

Jinsi nywele zako zilivyo nyingi, maadui nao vivyo hivyo. Na maadui zetu sio wanadamu bali ni mapepo ambayo mara nyingine huweza pia yavaa wanadamu, kutudhuru. Hivyo usiwe mtu wa kunung’unika au kulamimika, ujue kila mwanadamu yupo vitani. Kama Bwana wetu Yesu Kristo hakuwa na dhambi hata mmoja lakini alikuwa na jopo la maadui kwanini wewe usiwe nao. Hivyo kuwashinda ni kuwa mwombaji daima, na kutembea katika njia za Bwana sikuzote. Ukikumbuka kuwa maadui ni jambo la kawaida, kama tu nywele zako zilipo hapo kichwani.

  1. Si kila kitu unaweza kufanya. hivyo kuwa na kiasi.

Mathayo 5:36  Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kufanya unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi.

Wakati mwingine, tunajiaminisha na kujihakikishia mambo na kuweka na viapo juu yake kana kwamba mambo yote yapo ndani ya uwezo wetu. Kauli kama, “leo nife,kama sitakupa hiyo fedha” au “Mungu anipige hapa hapa kama ninalokuambia ni uongo” Kauli  kama hizi, za kuongezea hakikisho lingine juu, hazitokani na Mungu, maneno yetu tumeambiwa yawe ndio ndio, au sio sio, zaidi ya hapo yanatokana na Yule mwovu. Kwahiyo popote unapojiona unakaribia kuzidi mipaka kumbuka hizo nywele zilizo juu yako hujawahi kuzifanya ziwe hivyo ulivyo, Bwana ndiye azibadilishaye, hivyo jiwekee mipaka.

  1. Zithamini nguvu zako za rohoni.

Nywele zako hufunua nguvu zako za rohoni. Wanadhiri wote wa Mungu hawakuruhusiwa kukatwa nywele, Samsoni alipewa nguvu, kwa agano la kutokatwa nywele, kufunua kuwa watakatifu wote nywele zao za rohoni ndio nguvu zao. Lakini unapoacha mpango wa Mungu adui anazikata, kama ilivyokuwa kwa Samsoni. Lakini baadaye alipojua amefanya makosa ziliota tena lakini katika gharama za ‘kutoona’ tena.

Waamuzi 16:22 Lakini zile nywele za kichwa chake zikaanza kukua tena baada ya kunyolewa kwake.

Tunza nguvu zako, usiruhusu kiwembe chochote cha mwovu kikupitie. Kwasababu hata zikirejea tena, hutakuwa kama hapo mwanzo.

  1. Uwe na nyakati za maombolezo.

Yeremia 7: 29 Zikate nywele zako, Ee Yerusalemu, uzitupe, Ukafanye maombolezo juu ya vilele vya milima; Kwa maana Bwana amekikataa na kukitupa Kizazi cha ghadhabu yake.

Zamani, kukatwa nywele zote kuisha kabisa ilikuwa ni ishara ya kuingia kwenye maombolezo, kwasababu utukufu wako umeuvua.

Maombolezo, kwa agano jipya sio kulia kama msiba, hapana bali kuingia kwenye maombi ya ndani kabisa, ya kuutafuta uso wa Mungu, ambayo huambatana na mifungo. Na leo, ni kila mara tunakwenda saluni kukata nywele zetu. Tujue Bwana anatutaka kama vile tukatavyo nywele zetu mara kwa mara ndivyo tukumbuke maombi ya kujimimina sana mbele zake.

Je! Somo hilo unajifunza mwilini mwako?

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Je Bwana Yesu alikuwa na nywele ndefu?

ILI TUONEKANE WAKAMILIFU MBELE ZA MUNGU.

MWOMBENI BWANA WA MAVUNO APELEKE WATENDA KAZI.

Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Devis Julius administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments