Category Archive Home

MANENO ALIYOWEZA KUTAMKA YESU TU PEKE YAKE.

Yapo maneno ambayo huwezi kuzungumza, isipokuwa kwanza unaelewa vizuri ni nini unazungumza vinginevyo unaweza kujiweka kwenye kitanzi mwenyewe na kuingia matatizoni..

Kuna wakati Bwana aliwaambia wale watu wanaoshindana naye maneno haya…

“Ni nani miongoni mwenu anishuhudiaye ya kuwa nina dhambi..”? (Yohana 8:46)

Maneno haya si mepesi kabisa, Kumbuka juu kidogo tu kwenye sura hiyo hiyo swali la namna hii hii aliwauliza wale watu waliomfumania yule mwanamke katika uzinzi, lakini majibu yake ni kuwa sio tu kutomtupia yule mwanamke mawe, bali pia waliona aibu kuendelea kubaki maeneo yale, kwa mtihani huo mgumu waliopewa.

Yohana 8:7 “Nao walipozidi kumhoji, alijiinua, akawaambia, Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe.

8 Akainama tena, akaandika kwa kidole chake katika nchi.

9 Nao waliposikia, wakashitakiwa na dhamiri zao, wakatoka mmoja mmoja, wakianzia tangu wazee hata wa mwisho wao;

akabaki Yesu peke yake, na yule mwanamke amesimama katikati”.

Unaona? Lakini hapa na yeye pia anajiweka katika hicho kitanzi na kuwauliza watu.. Ni nani miongoni mwenu anishuhudiaye ya kuwa nina dhambi?

Jaribu kujiweka wewe katika hiyo nafasi ukiwa kama kijana wa miaka 33 ambaye tayari umeshapitia mambo mengi katika maisha, halafu unasimama katikati ya umati wa watu wanaoshindana na wewe, unawauliza ni nani kati yenu anayenishuhudia kuwa nina dhambi?

Je! Wewe unaweza kusema hayo maneno?(Mimi siwezi)..Ndugu zako wote wamesimama karibu nawe , marafiki zako wote uliowahi kuishi nao na kusoma nao, wote pia wamesimama karibu hapo, majirani zako nao wapo, wafanyakazi wenzako wanasimama hapo vilevile halafu unawauliza wote “Kati yenu ninyi ni nani anayenishuhudia kuwa nina dhambi”..

Ni nani alishawahi kuniona au kusikia nimemsengenya mtu, ni nani nilishawahi kumdanganya au alishawahi kunisikia nadanganya, ni wapi nilishawahi kutamani, ni wapi nilishawahi kumvunjia mtu heshima, au kumwonea wivu, au kumwekea kinyongo, au kuonyesha unafki, kumfokea, kumtukana? ..Kama yupo hapa asimame, au ajitokeze, asimeme wewe siku fulani nilikuona ukikwepa kodi kwenye ile biashara yenu ya useremala…

Lakini wote waliosimama pale, hakuonekana hata mmoja aliyekuwa na la kumshitaki Yesu..sio jambo rahisi kama tunavyofikiri,

Na ndio maana mahali pengine biblia inasema..

1Petro 2:22 “Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake.”

Ni Yesu peke yake, katika ulimwengu mzima, katika vizazi vyote, ambaye tangu amezaliwa mpaka anakufa, hakuwahi kutenda dhambi hata moja, japokuwa alipitia majaribu mazito ya dhambi kuliko hata sisi.

Ndugu yangu Kwa YESU pekee mimi nimetia nanga! Sijui kwako?, kwasababu hakuna mwingine kama yeye, huyu pekee ndio wa kumtumainia, ni huyu pekee ndio wa kumtegemea kutusaidia kushinda huu ulimwengu kama yeye alivyoshinda, ni huyu huyu pekee ndio atakayetuokoa tukimwamini. Mimi na wewe tukimfanya kuwa rafiki wa maisha yetu, jambo la kwanza na la ajabu ni kuwa anatusamehe dhambi zetu zote, halafu anatuhesabia haki bure pasipo matendo yetu kwa neema, kiasi kwamba mbele za Mungu tunaonekana kuwa tumestahili haki yote.

Kisha baada ya hapo anamtuma Roho wake Mtakatifu ndani yetu. Ambaye kazi yake ni kutupa sisi nguvu ya kuishinda dhambi kama yeye alivyoishinda, na kutuongoza katika kuijua kweli yote.

Hivyo kama bado hujaokoka, saa ya wokovu ni sasa, fanya haraka mkaribishe Yesu maishani mwako. Kama umezichoka dhambi kweli, kama hutaki nafsi yako ipotee, basi mkimbilie Yesu haraka maadamu muda upo, Lakini tukikataa kuyasikia maneno yake basi yeye naye atatuacha, na kutuona tu kama sio watu tuliochaguliwa na Baba yake soma..

8:46 “Ni nani miongoni mwenu anishuhudiaye ya kuwa nina dhambi? Nami nikisema kweli, mbona ninyi hamnisadiki?

47 Yeye aliye wa Mungu huyasikia maneno ya Mungu; hivyo ninyi hamsikii kwa sababu ninyi si wa Mungu”.

Natumaini wewe leo utayasikia maneno yake.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

RABI, UNAKAA WAPI?

NENO HILI NI GUMU,NI NANI AWEZAYE KULISIKIA?

Yeshuruni ni nani katika biblia?

KUMBUKA, VIVUKO VYA YORDANI VINAKUNGOJA MBELENI.

NA MTU MMOJA AKAVUTA UPINDE KWA KUBAHATISHA, AKAMPIGA MFALME

UNYAKUO.

Rudi Nyumbani:

Print this post

AHADI ZA MUNGU.

Ahadi za Mungu ni za kweli kabisa,.. Lakini tatizo kubwa linalotukabili  sisi wanadamu ni kutokujua njia Mungu anazozitumia kutimiza ahadi zake.

Na hiyo inawafanya watu wengi waishie kukata tamaa pale anapoona mbona ahadi za Mungu zimechelewa, pengine nimemkosea Mungu, au Hanisikii..

Fahamu kuwa wakati wa Mungu kutimiza ahadi zake, sio lazima uwe ule wakati ulioupanga wewe Tena mara nyingi huwa anauchagua ule wakati ambao haufahau, wakati ambao mambo yote yanaokana yameharibika, mipango imevurugika, umeshachelewa, hapo ndipo Mungu anasimama ili kutimiza ahadi zake kwako.

  • Utamwona Ibrahimu, alipokuwa na miaka 75 Mungu alimwambia nitakupa mwana, na nitakufanya kuwa taifa kubwa.. Jaribu kufiria katika uzee ule, ungedhani labda, baada ya mwaka mmoja tu, ndio Mungu angemtimizia ahadi yake, ili viungo vya uzazi visife kabisa..Lakini tunaona Mungu aliendelea kusubiri, hadi miaka karibia 25 mbeleni, akiwa sasa na umri karibia na miaka 100 ndio Mungu anamtembelea na kumpa mtoto.

Na hakupewa tu mtoto basi, bali na mwili wake pia ulirudishwa na kuwa kama wa kijana, yeye pamoja na mke wake Sara.

Lakini Ibrahimu katika kipindi chote hicho hapo katikati hakumkosea Mungu imani na ndio maana akaitwa baba wa Imani, tunasoma hilo katika..

Warumi 4:18 “Naye aliamini kwa kutarajia yasiyoweza kutarajiwa, ili apate kuwa baba wa mataifa mengi, kama ilivyonenwa, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako.

19 Yeye asiyekuwa dhaifu wa imani, alifikiri hali ya mwili wake uliokuwa umekwisha kufa, (akiwa amekwisha kupata umri wa kama miaka mia), na hali ya kufa ya tumbo lake Sara.

20 Lakini akiiona ahadi ya Mungu hakusita kwa kutokuamini, bali alitiwa nguvu kwa imani, akimtukuza Mungu;

21 huku akijua hakika ya kuwa Mungu aweza kufanya yale aliyoahidi.

22 Kwa hiyo ilihesabiwa kwake kuwa ni haki”.  

  • Unaona? Vivyo hivyo Yusufu naye , tayari alishapewa neon la ahadi katika ndoto, kuwa upo wakati atakuzwa kiasi kwamba mpaka ndugu zake watakuja kumwinamia. Lakini hilo halikutimia kwa wakati ule ule alioonyeshwa, kinyume chake akiwa na umri wa miaka 17 aliuzwa na ndugu zake, akawa mtumwa kule Misri mpaka anafikia miaka 30 ndio hizo ndoto zinakuja kutimia.

Na hazikutimia akiwa nyumbani mwa Potifa hapana, bali zilitimia akiwa gerezani, mahali ambapo hapana tumaini lolote, la kuishi. Kwa kipindi karibu cha miaka 2 akiwa kule gerezani, siku moja isiyokuwa na jina Mungu alimtembelea na kumwinua, akatoka na kufanywa kuwa Waziri mkuu na makamu wa Raisi wa taifa kubwa lililokuwa lina nguvu kuliko yote ulimwenguni wakati ule (Misri).

Hivyo zipo ahadi za Mungu nyingi katika biblia ambazo tukianza kuzichambua hapa moja baada ya nyingine hatuwezi kumaliza zote..

Ahadi za Mungu kwa mkristo:

Hiyo ni kutupa tu hamasa mimi na wewe ambao pengine umesubiria ahadi za Mungu kwa muda mrefu sasa na bado hujaona matokeo yoyote. Unachopaswa kufanya ni kusubiri ndugu yangu, huku ukiendelea kumtumikia Mungu kwa moyo ule ule wa kwanza.

Unaweza ukawa ni mtumishi wa Mungu, na umejaribu kuacha kila kitu ili tu uifanye kazi yake..Nataka nikuambie endelea hivyo hivyo, upo wakati utafika ile hadi yake ya kuwa UTAPATA MARA MIA, itatimia juu yako, haijalishi ni miaka miwili tokea sasa, au 5 au 10 au 20, lakini fahamu kuwa ukiendelea kung’ang’ania njia yako bila kuiacha, utavuna ulichopanda.

Mungu atakulipa tu, mema, ukiwa hapa hapa duniani, na vyote ulivyovipoteza utarejeshewa vyote mara mia. (Marko 10:28-30) Hivyo endelea kumtumikia MUNGU.

Vilevile Bwana aliposema, usisimbukie maisha ule nini, unywe nini, avae nini, bali utafute kwanza ufalme wake na haki yake na hayo mengine utazidishiwa. Basi fahamu kuwa ukijikita kuutafuta kwanza uso wa Mungu, na kutaka kumjua yeye, ni ahadi yake kuwa  hatakuacha ufe njaa, bali atahakikisha kuwa anakuhudumia ili uendelee kuishi,..Kwasababu unautafuta ufalme wake..Hiyo ni kweli kabisa hawezi kudanganya.. Ahadi za Mungu ni thabiti.

Vivyo hivyo na ahadi nyingine yoyote aliyowahi kukuahidia , endelea tu kuingoja, wakati wake utafika tu,. Kikubwa usiuache wokovu wako na utakatifu wako kama wewe umeokoka.

Lakini kama hujaokoka, basi hakuna ahadi yoyote ya Mungu inayoweza kutimia juu yako. Hivyo unachopaswa kufanya ni kumpa Kristo maisha yako ili ayaokoe, kwani hizi ni siku za  mwisho na Unyakuo upo karibu,..Moja ya hizi siku mabadiliko makubwa sana yatatokea duniani. Na dhiki kuu itaanza, hivyo mgeukie muumba wako kabla ya hizo za hatari hazijakufikia kwa ghafla.

Bwana akubariki.

Ahadi za Mungu ni Yakini.

Mada Nyinginezo:

KWA KUVUMILIA AKAIPATA ILE AHADI.

TABIA YA KIPEKEE USIYOIJUA KUHUSU NENO LA MUNGU.

UNYAKUO.

MKUMBUKE MKE WA LUTU.

FAHAMU JINSI KRISTO ANAVYOPONYA WATU ROHO.

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia..!!

Rudi Nyumbani:

Print this post

YEREMIA

Yeremia alikuwa ni nabii aliyezaliwa Israeli (Kwa asili alikuwa ni Myahudi)..na alitokea nyakati za mwisho mwisho kabisa, karibia na wakati wa Israeli kuchukuliwa mateka Babeli. Ni nabii aliyetabiri na kushuhudia kuteketezwa kwa mji wa Yerusalemu na watu kuchinjwa na baadhi kuchukuliwa mateka. Tafsiri ya jina lake ni “Yehova atapandisha au atanyanyua” .Unaweza kutazama tafsiri za baadhi ya majina hapa >>>Maana ya majina na tafsiri zake

Kama jina lake lilivyo, Yeremia alitabiri Israeli kunyanyuliwa tena na Mungu baada ya kushushwa chini..alisema..Bwana atawarudia tena watu wake baada ya kukaa ugenini miaka 70.

Yeremia 25:11 “Na nchi hii yote pia itakuwa ukiwa, na kitu cha kushangaza; nayo mataifa haya watamtumikia mfalme wa Babeli miaka sabini.

12 Na itakuwa miaka hiyo sabini itakapotimia, nitamwadhibu mfalme wa Babeli, na taifa lile, asema Bwana, kwa sababu ya uovu wao, nayo nchi ya Wakaldayo pia; nami nitaifanya kuwa ukiwa wa milele”.

Yeremia tofauti na manabii wengine, yeye aliitwa na Mungu katika utumishi akiwa na umri mdogo na ni moja ya manabii waliopitia mateso mengi sana katika huduma zao, lakini Mungu hawaacha!..na Mungu alimtuma kwa mataifa mbali mbali…Manabii wengine wa Israeli kama Samweli, Ezekieli,Musa, Malaki na wengineo hawakutumwa kwa watu wa Mataifa, isipokuwa kwa watu wa jamii yao tu (yaani kwa wasraeli wenzao!). Yeremia na wengine wachache ndio pekee waliotumwa watoke nje ya mipaka ya Israeli kusema na watu wa Mataifa ya mbali.

Yeremia 1:4 “Neno la Bwana lilinijia, kusema,

 5 Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa.

  6 Ndipo niliposema, Aa, Bwana MUNGU! Tazama, siwezi kusema; maana mimi ni mtoto.

7 Lakini Bwana akaniambia, Usiseme, Mimi ni mtoto; maana utakwenda kwa kila mtu nitakayekutuma kwake, nawe utasema kila neno nitakalokuamuru. ”

Mungu alimtuma Yeremia kwa mataifa mengi ulimwenguni, kuyatangazia hukumu…kwamba yote yatawekwa chini ya utawala mgumu wa Nebukadneza kama yasipotubu na kuacha njia zao mbaya…na mataifa hayo yote hayakuisikiliza sauti ya Yeremia nabii na yote kuishia kuwekwa chini ya mikono ya Nebukadneza (kasome Yeremia 25:15-28) ikianza na Yuda. (Na Yeremia  aliifanya kazi hiyo ya Mungu kwa uaminifu mpaka alipokuwa mzee.)

Kwa maelezo ya urefu kuhusu Nabii huyu, vitabu alivyoandika, na huduma yake ilivyokuwa kwa mapana fungua hapa >> Vitabu vya Biblia (sehemu ya 7)

Wito wa Mungu hauna mipaka, Mungu anaweza kukuita na kukutuma katika umri mdogo kama Yeremia, na vile vile anaweza kukuita na kukutumia katika umri mkubwa, kama Elisha. Kwa wito wowote ule tutakaoitwa na Mungu, tunapaswa tuwe waaminifu.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 4

MAOMBI YA TOBA.

Kwanini Kristo hakuitwa Imanueli badala yake akaitwa Yesu?

PARAPANDA ITALIA.

Rudi Nyumbani:

Print this post

Yesu ni Mungu?, Na Kama ni Mungu kwanini alikufa?

SWALI: Je! Yesu ni Mungu? Na Kama ni Mungu kwanini alikufa?


JIBU: Yesu alikuwa ni Mungu katika mwili (1Timotheo 3:16)…lakini hakuja kutafuta kuabudiwa wala kusujudiwa!…Mpaka Mungu amevaa mwili na kuja ulimwenguni, maana yake hajaja kutafuta kuabudiwa, kama angekuwa amekuja kutafuta utukufu wake basi, kulikuwa hakuna haja ya kuuvaa mwili na kushuka duniani, naamini Mbingu ilikuwa inamtosha…. hivyo ni lazima atakuwa amekuja kwa kusudi lingine na si la kutafuta utukufu. Hapo ndipo wengi wa wasio wakristo wanaposhindwa kuelewa, na baadhi ya walio wakristo.

Unapoona askari wa kuongoza barabarani (Traffic man), kaondoka barabarani na kaenda nyumbani kubadilisha nguo zake hizo nyeupe…na akavaa nguo za kiraia na kuingia mtaani basi ni dhahiri kuwa huko mtaani alikokwenda hajakwenda kutafuta kuongoza magari bali kaenda kutafuta mambo yake mengine ya kawaida..labda anaenda hospitalini au sokoni au kusalimia ndugu na marafiki, au kufuatilia mambo yake mengine ambayo ni tofauti na ya kikazi….. (ni kweli bado atabaki kuwa askari, lakini yupo nje ya ofisi yake), hivyo hataweza kuyatumia yale mamlaka aliyonayo ya kuongoza magari,…na akiwa barabarani na nguo zake za kiraia, hata watu wanaweza wasimtambue kama ni askari, atakuwa kama raia wengine tu, na magari atakuwa anayakwepa tu kama raia wengine, na atazingatia sheria zote za barabarani kama raia wengine…

Na Bwana Yesu ni hivyo hivyo…alipokuwa mbinguni alikuwa ni Mungu, anayestahili kuabudiwa na kuheshimiwa…aliposhuka duniani alikivua kile cheo cha Kiungu…na kuwa kama mwanadamu (kwa lengo la kuja kumkomboa mwanadamu na si kuabudiwa kama Mungu)..na baada ya kumaliza akarudi mbinguni alikotoka katika cheo chake.

Hivyo akiwa kama mwanadamu alikuwa hana budi aishi kama wanadamu wengine, hana budi awe mtu wa ibada kama watu wengine, hana budi ale, anywe, alale, achoke, apitie yote mwanadamu wa kawaida anayopitia na hata ikiwezekana afe…ili tu kusudi lake lililomleta duniani litimie la kumkomboa mwanadamu…lakini alikuwa bado ni Mungu.

Wafilipi 2: 5 “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu;

6 ambaye yeye mwanzo alikuwa YUNA NAMNA YA MUNGU, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho;

7 bali ALIJIFANYA kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu;

8 tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba”.

Umeona hapo mstari wa 7?..unasema “ALIJIFANYA”..kama unakielewa Kiswahili vizuri utakuwa unajua maana ya “KUJIFANYA”..Maana yake ni kama kujigeuza/kuigiza kuwa kitu Fulani na kumbe sio…kwa lengo la kutimiza kusudi Fulani tu!…Hivyo Bwana Yesu aliyejifanya kuwa hana utukufu…ili ashuke aje kutukomboa na kutuonyesha njia jinsi mwanadamu kamili anayemcha Mungu anapaswe awe.

Hivyo kufa kwa Bwana Yesu, hakumfanyi yeye asiwe Mungu..na pia muujiza mkubwa duniani na mbinguni sio kutokufa!!… Huo ni muujiza mdogo sana…..“miujiza mkubwa ni uwezo wa mtu kuutoa uhai wake na kisha kujirudishia ule uhai”..Huo ndio muujiza mkubwa kuliko yote!..na uwezo huo alikuwa nao Yesu pekee yake.

Yohana 10:17 “Ndiposa Baba anipenda, kwa sababu nautoa uhai wangu ili niutwae tena.

18 HAKUNA MTU ANIONDOLEAYE, BALI MIMI NAUTOA MWENYEWE. NAMI NINAO UWEZA WA KUUTOA, NINAO NA UWEZA WA KUUTWAA TENA. Agizo hilo nalilipokea kwa Baba yangu”.

Sasa utauliza ni wapi, Yesu aliutoa uhai wake mwenyewe?…kasome Luka 23:46-47. Bwana Yesu aliutoa uhai wake mwenyewe! Hakuna mtu aliyemsaidia kuutoa..hata Pilato alishangaa imekuwaje amewahi kufa kiasi kile (Marko 15:44). Na aliurudisha uhai wake mwenyewe baada ya siku tatu (kule kaburini hakuna mtu aliyeenda kumfufua au kumwombea afufuke).

Alijirudishia uhai wake mwenyewe!..Nadhani huo ni muujiza mkubwa sana.. Je wewe unaweza kufanya hivyo????

Hata mfano nikikuwekea watu wawili mbele yako mmoja hawezi kuukata mguu wake na mwingine anao uwezo wa kuukata na kuurudisha….nikakwambia kati ya hao wawili ni yupi hapo wa kuogopwa zaidi??..Bila shaka utaniambia “Yule mwenye uwezo wa kuukata mguu wake na kisha kujirudisha tena ndiye wa kuogopwa zaidi kuliko huyo mwingine”.

Kwahiyo kuupima uungu wa Bwana Yesu na kifo chake ni hoja dhaifu!!..miungu ya kipagani ndio isiyo na uwezo wa kufanya hayo..lakini Mungu wa mbingu na nchi (YESU KRISTO) anaweza kufanya mambo yote. Mpaka sasa katika historia hajatokea nabii yoyote wala mtume yeyote aliyofanya miujiza kama aliyofanya Bwana Yesu, sasa kwanini asiwe Mungu?. Na siku moja atarudi na kila jicho litamwona na kila goti litapigwa, na kila kinywa kitakiri…Wengi itakuwa ni jambo la kushtukiza sana kwao, kwasababu hawataamini kwamba kweli ndiye!..kwasababu walidanganyika wakiwa duniani kwamba hatarudi.

Lakini anatupenda na wala hataki mtu yoyote apotee bali wote tuifikie toba, ili tuokoke na tuje kutawala naye milele.

Bwana atubariki tuzidi kumjua yeye!

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

Mbona Mungu anaruhusu watu wapate shida, ilhali ana uwezo wa kutuepusha?

Katika biblia Neno “Mshenzi” linatajwa.Kwanini liwekwe?

Kile kinara cha Taa ndani ya Hekalu la Sulemani kilikuwa kinawakilisha nini?

Je! Ni kweli ubatizo wa maji hatuuhitaji tena?

DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.

Rudi Nyumbani:

Print this post

Yuko azuiaye sasa hata atakapoondolewa! ni nani huyo?

SWALI: Naomba unisaidie hii 2 wathesalonike 2:7 “Yuko azuiaye sasa Hadi atakapoondolewa, naomba unisaidie huu mstari unamaanisha Nani huyo anayezuia na Ni kwa nini?”


JIBU: Ukianzia kusoma tokea mistari ya juu kidogo utaona inazungumzia habari za mpinga-Kristo ambaye biblia inamtaja kama “Asi” kwamba mwisho wa dunia hautafika kwanza kabla ya yeye kufunuliwa hapa duniani..

Kwasababu wakati ule, watu wa kipindi kile walidhani kuwa pengine wapo tayari katika wakati wenyewe wa mwisho wa dunia, Lakini mtume Paulo aliwapa siri ambayo alifunuliwa na Roho Mtakatifu na kuwaambia, ule mwisho hautakuja kwa namna hiyo, bali ni sharti kwanza yule Asi (yaani Mpinga-Kristo) afunuliwe duniani, aonekane kazi zake na mienendo yake, na kwamba watu wakishamwona huyo sasa ndio wajue kuwa dunia itakuwa na kipindi kifupi sana cha kuendelea kuwepo, ambacho si zaidi ya miaka 7 kulingana na unabii wa kibiblia.

Lakini pamoja na hayo aliendelea kuwasisitiza kuwa japokuwa Asi mwenyewe (Mpinga-Kristo), hajafunuliwa kwa wakati wao lakini ile siri yake ilikuwa imeshaanza kutenda kazi, akiwa na maana kuwa mienendo ya mpinga-Kristo ilikuwa imeshaanza kuonekana tangu ule wakati isipokuwa tu ilikuwa katika siri..Bado haijapata nafasi yote.

2Wathasalonike 2:5 “Je! Hamkumbuki ya kuwa wakati nilipokuwapo pamoja nanyi naliwaambieni hayo?

6 Na sasa lizuialo mwalijua, yule apate kufunuliwa wakati wake.

7 Maana ile siri ya kuasi hivi sasa inatenda kazi; lakini yuko azuiaye sasa, hata atakapoondolewa.

Sasa swali ni kwanini siri hiyo ya kuasi isijidhihirishe yote tangu ule wakati hata sasa ambapo imepita zaidi ya miaka 2000?.

Mtume Paulo anasema ni kwasababu Yupo azuiaye, Na huyo sio mwingine zaidi ya “Roho Mtakatifu”. Ikumbukwe kuwa Roho Mtakatifu ndiye mtunza uhai wa vitu vyote na viumbe vyote tangu mwanzo, Mungu asingeiumba hii dunia iwe makao mazuri ya watu kama sio Roho wake kutua kwanza juu ya uso wa nchi. Hii ikiwa na maana akiondolewa basi dunia inarudia katika hali yake ya ukiwa kama ilivyokuwa hapo mwanzo.

Leo hii unaona ni kwanini watu wanamtafuta Mungu, ni kwasababu Roho Mtakatifu anafanya kazi ndani yao, ni kwanini wanaomba?, sababu ni hiyo hiyo ya Roho Mtakatifu, ni kwanini duniani hakuna vita vikali vya kiatomiki ambavyo vinaweza kuichakaza dunia mara moja nikwasababu Roho Mtakatifu anazuia..Ni kwanini Volcano, haviimezi dunia yote, ni kwasababu Roho Mtakatifu anazuia.

Lakini upo wakati ambapo, Mungu atamwondoa duniani kazi yake itakapoisha. Ambayo itaisha na watakatifu wa Mungu watakaonyakuliwa siku ile kwenda mbinguni. Maana yake kwamba ikitokea leo hii unyakuo umepita, basi na kazi ya roho Mtakatifu ya kuokoa (yaani ya kuwavuta watu kwa Mungu), na kuzuia amani duniani nayo inakuwa imeisha, Anaondoka..Ndio hapo yule Asi (yaani Mpinga-Kristo) naye anapata nafasi ya kufanya uharibifu wake wa kuleta dhiki kuu duniani, hapo ndipo mataifa yote duniani nayo yanapata nafasi ya kukusanyika kuleta vita kuu ya dunia ambayo haijawahi kutokea, hapo ndipo baadhi ya mapepo yaliyokuwa kifungoni yanaachiliwa duniani kwa muda ili kuwatesa watu, hapo ndipo dunia nayo itapoteza muhimili wake, matetemeko makubwa yatatokea duniani, volcano zitafumuka ardhini, jua litazima na mwezi kuwa damu na nyota kuanguka..na dunia itarudia kuwa ukiwa kama ilivyokuwa kabla ya Edeni.

Yaani hayo yote yatatimia ndani ya kipindi kifupi tu cha miaka saba.

Jiulize, unyakuo ukipita leo, mimi na wewe tutakuwa wapi?. Bwana alisema tutawezaje kupona tusipouthamini wokovu mkuu namna hii?

Hizi ni nyakati za hatari. Tubu dhambi kama bado hujafanya hivyo, na kama tayari basi zidi kudumu ndani ya neema ya Kristo mpaka siku ya mwisho wa unyakuo.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

Je! Shetani alitolea wapi uovu?

Nitaitofautishaje sauti ya Malaika na ya Roho Mtakatifu?

 Je! Ni sahihi kutumia maji ya upako,katika kufanya maombezi?

WAKATI ULIOKUBALIKA NDIO SASA.

JE NI HALALI KUOA WAKE WENGI AU KUTOA TALAKA?

Rudi Nyumbani:

Print this post

Agano jipya ni nini?

Agano jipya ni nini?


Tukitamka neno “agano jipya”  tunathibitisha kuwa lilishawahi kuwepo agano la zamani (La kale) hapo kabla.

Hivyo ili kufahamu agano jipya ni nini, ni vizuri kwanza ukapata msingi wa agano la Kale, lilikuwaje.

Kama tunavyojua Biblia imeundwa na maagano makuu wawili, yaani jipya na la kale.

  1. Agano la Kale:

Sasa msingi wa agano la kale ulitoka kwa mtu mmoja aliyeitwa Ibrahimu. Mungu alipomuita hakumuita ilimradi tu, bali aliingia agano naye akamwambia atambariki na kumfanya kuwa baba wa mataifa mengi, ikiwa tu atakuwa mkamilifu na atakwenda  katika njia zake..Tusome.

Mwanzo 17:1 “Abramu alipokuwa mtu wa miaka tisini na kenda, Bwana akamtokea Abramu, akamwambia, Mimi ni Mungu Mwenyezi, uende mbele yangu, ukawe mkamilifu. 

2 Nami nitafanya agano langu kati ya mimi na wewe, nami nitakuzidisha sana sana. 

3 Abramu akaanguka kifudifudi. Mungu akamwambia, akasema, 

4 Mimi, agano langu nimefanya nawe, nawe utakuwa baba wa mataifa mengi, 

5 wala jina lako hutaitwa tena Abramu, lakini jina lako litakuwa Ibrahimu, kwani nimekuweka uwe baba wa mataifa mengi. 

6 Nitakufanya uwe na uzao mwingi sana, nami nitakufanya kuwa mataifa, na wafalme watatoka kwako. 

7 Agano langu nitalifanya imara kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, na vizazi vyao, kuwa agano la milele, kwamba nitakuwa Mungu kwako na kwa uzao wako baada yako. 

8 Nami nitakupa wewe na uzao wako baada yako nchi hii unayoikaa ugeni, nchi yote ya Kanaani, kuwa milki ya milele; nami nitakuwa Mungu wao. 

9 Mungu akamwambia Ibrahimu, Nawe ulishike agano langu, wewe na uzao wako kwa vizazi vyao baada. yako. 

10 Hili ndilo agano langu utakalolishika, kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, Kila mwanamume wa kwenu atatahiriwa. 

11 Mtatahiriwa nyama ya magovi yenu, na jambo hilo litakuwa ishara ya agano kati ya mimi na ninyi”.

Unaona, Jinsi Mungu alivyokuwa mwaminifu, baadaye Mungu akaja kumtimizia kweli agano aliliomuahidia, kwa jinsi uzao wake ulivyokuwa unaongezeka duniani kwa kasi, Lakini wakati huo wote uzao wake ulikuwa haumjui Mungu vizuri, ulikuwa bado haujajua kanuni za agano hilo ambalo Mungu aliloingia na Ibrahimu baba yao linavyopaswa liwe..

Ndio hapo wakiwa kule jangwani sasa Mungu anamtumia Musa kusema nao na kuwapa sheria na amri za kuzishika ili wafanikiwe..

Sheria hizo ndizo zilizoandikwa katika vitabu vya Torati: yaani

  • Mwanzo
  • Kutoka
  • Hesabu
  • Mambo ya Walawi
  • Kumbukumbu la Torati.

Hivyo vitabu hivyo vitano vilikamilisha Sheria yote ya Agano hilo ambalo Mungu aliingia na Ibrahimu.

Lakini hiyo peke yake haikuwa inatosha wana wa Israeli kumfahamu Mungu katika ukamilifu wote, Hivyo ilipasa  Mungu azungumze nao mara kwa mara kupitia watu mbalimbali wakamilifu na manabii wake.. Mfano tunamwona mtu kama Ayubu, Esta, Ruthu, kwa kupitia maisha ya hawa Mungu aliwafundisha wana wa Israeli jinsi ya kuishi katika njia zake. Vilevile akawa anasema nao mara kwa mara kupitia manabii wake wengi na waamuzi na mfano Samweli, Isaya, Yeremia, Danieli, Yona,Malaki N.k.

Hivyo kwa kupitia hao pia, na vitabu vyao walivyoviandika, iliwasaidia wana wa Israeli walishike na kulikumbuka agano ambalo aliingia nao zamani.

Kwahiyo tunapovisoma vitabu 39 vya Agano la Kale,.. tunafahamu kuwa ni jumuisho la sheria zote na kanuni zote za Mungu kwa wale alioingia nao agano kupitia Ibrahimu.

Sasa mpaka hapo umeshapata msingi wa Agano la kale kwa ufupi lilipoanzia..


      2.  Tukirudi kwenye agano jipya..

Hilo ni agano lingine lili bora zaidi kuliko lile la Ibrahimu.,

Hili nalo  Mungu aliingia katika agano na mtu mmoja tu, kama vile alivyoingia na Ibrahimu.. Na mtu huyo si mwingine zaidi ya YESU KRISTO.

Ibrahimu alipewa tu uzao wake wa kimwili, lakini huyu alipewa uzao wa wote wenye mwili wakimwamini tu kwa kuzaliwa mara ya pili.

Na ndio maana kuna umuhimu wa kila mmoja wetu kuzaliwa mara ya pili ili tufanyike kuwa uzao wake. yeye mwenyewe alisema..

Yohana 3:3  “Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu”.

Na kubatizwa kwetu ndio ishara ya tohara yenyewe ya rohoni kama ilivyokuwa kwa Ibrahimu na watoto wake wote walipotahiriwa kwa kutolewa magovi. Vivyo hivyo na sisi tunapaswa tukabatizwe kama ishara ya kutahiriwa mioyo yetu.

Lakini tukishazaliwa mara ya pili, hilo tu peke yake haitoshi, ni sharti pia tujue kanuni, na amri Mungu anazozitaka za agano hili ili tuweze kudumu ndani yake. Kama Uzao wa Ibrahimu ulivyopewa.

Hapo ndipo vitabu vya Injili ya Yesu Kristo, na vile  vya mitume, viliandikwa kwa ajili yetu ili sisi sote tutakapovisoma na kuvishika basi tuweze kudumu na kuimarika katika hilo agano jipya la Damu ya Yesu Kristo.

Ndipo hapo tunakutana na vitabu 27 vya agano jipya.

Hivyo kwa kwa hitimisho fupi.. Agano jipya ni agano Mungu aliloingia na Yesu pamoja na uzao wake wote. Ambao mimi na wewe tunahesabiwa katika uzao huo  kwa kumwamini Yesu na kubatizwa.

Tukifanikiwa kufanya hivyo basi na baraka zote, Mungu alizomuahidia Yesu Kristo, na sisi sote pia tunazishiriki na kuzirithi, ikiwemo uzima wa milele.

Bwana akubariki.

Je! Na wewe upo ndani ya agano jipya? Kama bado basi fanya hima ukaribishe Yesu leo ndani ya maisha yako akuokoe ufanyike uzao wa kifalme. Kumbuka hii ni neema ambayo sisi watu wa mataifa hatukustahili, hivyo uiichezee hata kidogo..

1Petro 2:9  “Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu; 10  ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa la Mungu; mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema”.

Haleluya.

Mada Nyinginezo:

TOBA IGUSAYO MOYO WA BWANA.

Je! habari ya Yusufu, inabeba ujumbe gani kwa agano jipya?

Bwana aliposema “sikuja kutangua torati bali kuitimiliza” alikuwa anamaanisha nini?

UTIMILIFU WA TORATI.

TAZAMA, MWISRAELI KWELI KWELI, HAMNA HILA NDANI YAKE!

Sanduku la Agano lilikuwa linawakilisha nini katika Agano jipya?

KUTAHIRIWA KIBIBLIA

MWAKA WA BWANA ULIOKUBALIWA.

Rudi Nyumbani:

Print this post

UPENDO WA MUNGU.

Upendo wa Mungu ni upi?


Kwanza kabla ya kufahamu upendo wa Mungu upoje, ni muhimu kufahamu aina za upendo. Zipo aina kuu tatu za upendo.

  1. Aina ya kwanza ni Upendo unaotokana na hisia, ujulikanao kama EROS. Huu ndio upendo wa mke na mume, katika biblia tunaweza kuona Sulemani akiueleza kwa mapana na marefu katika kitabu cha Wimbo ulio Bora.

Wimbo ulio bora 1:13 “Mpendwa wangu ni kama mfuko wa manemane Ukilazwa usiku maziwani mwangu. 

14 Mpendwa wangu ni kama kishada cha hina, Katika mizabibu huko Engedi. 

15 Tazama, u mzuri, mpenzi wangu, U mzuri, macho yako ni kama ya hua.  16 Tazama, u mzuri, mpendwa wangu, Wapendeza, na kitanda chetu ni majani; 

17 Nguzo za nyumba yetu ni mierezi, Na viguzo vyetu ni miberoshi.”

  1. Upendo wa pili ni ule unaozuka kutokana na mahusiano mtu mmoja alio nao kwa mwingine, almaarufu kama PHILEO,. Huu unaweza ukawa upendo wa mtu na ndugu yake, mchezaji mwenzake, mfanyakazi mwenzake, mwanafunzi mwenzake, mkristo mwenzako, n.k. ni upendo ambao kama hakuna kitu cha kuwaunganisha pamoja, au faida fulani kupatikana, hauwezi kuzaliwa.

Upendo wa namna hii sio upendo mkamilifu sana (ikiwa na maana haujafikia viwango vile vyenyewe),  mkristo, kwasababu hata wenye dhambi wanaweza kuwa nao, Na ndio maana Bwana Yesu alisema..

Mathayo 5.46  “Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo?

47  Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo?

48  Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu”.

  1. Upendo wa tatu ndio mkuu kuliko yote unajuliana kama AGAPE (UPENDO WA KI-MUNGU).

Huu ndio Upendo ambao Yesu alikuwa anaulenga kila mahali, Ni upendo usiokuwa na masharti, Unampenda mtu bila ya kuwa na sababu yoyote ya kukufanya umpende, haijalishi awe nawe anakupenda au hakupendi, anakuchikia au hakuchukii,  anakusema vibaya au hakusemi vibaya..Unapenda bila masharti, aina hii ya upendo ndio aliokuwa nao Yesu.

Biblia imeziorodhesha tabia za Upendo huo wa ki-Mungu katika kitabu cha Wakoritho wa kwanza. Tusome.

 1Wakoritho 13:4  “Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; 5  haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya;

6  haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli;

7  huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote.

8  Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika”.

Hivyo mpaka hapo sasa umeshauelewa huu upendo wa Mungu ni upi? Ni upendo usiojali wewe ni nani na ndio maana biblia ilisema..

Yohana 3:16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele”.

Hivyo kama wewe ni mwenye dhambi ujue kuwa Mungu anakupenda na ndio maana anataka kukuokoa usiende kuzimu na dhambi zako, haijalishi ulimkosea kiasi gani, leo hii yupo tayari kukusamehe na kukupa uzima wa milele, Hivyo usikiapo ujumbe huu, usiufanye moyo wako kuwa mgumu bali, mgeukie yeye na akusemehe dhambi zako.

Hizi ni siku za mwisho ukifa na dhambi zako hakika utakwenda kuzimu.

Shalom.

Upendo wa Mungu, ni wa kipekee sana.

Mada Nyinginezo:

JINSI NEEMA YA MUNGU ILIVYOKUWA KUBWA KWA MKE WA LUTU.

JINA LA MUNGU NI LIPI?

UUMBAJI BORA WA MUNGU, UPO NDANI YA MWANADAMU.

UNYAKUO.

HUYU MELKIZEDEKI NI NANI?

Kwanini Yesu Kristo ni mwana wa Adamu?

WINGU KUBWA LA MASHAHIDI.

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita..

Rudi Nyumbani:

Print this post

MWAMBA WENYE IMARA

Mwamba wenye Imara, kwako nitajifichaa…” Ni wimbo wa kenye kitabu cha Tenzi, ambao unafahamika sana…lakini historia ya wimbo huu ni haujulikani na wengi.

Wimbo huu uliandikwa na Mhubiri mmoja wa kanisa la kiprotestant aliyejulikana kwa jina la “Augustus Montague Toplady” , mwenye asili ya nchi ya Uingereza. Mhubiri huyu siku moja alipokuwa anasafiri katika ziara zake za kuhubiri katika kijiji kimoja huko kaskazini mwa Uingereza mwaka huo wa 1763 kilichoitwa “Blagdom”..alipokuwa safarini alikumbana na “Dhoruba kubwa sana ya kuogopesha”.. na hakuwa na mahali pa kujificha…lakini karibu na eneo alilokuwepo palikuwa na MWAMBA MKUBWA, ambao ulikuwa na mwanya mdogo wa kujificha. Na ndipo alipokimbilia chini ya mwamba ule kwenye ule upenyo mdogo na kujificha, mpaka dhoruba ile kali ilipopita..

Sasa akiwa katikati ya upenyo wa mwamba ule, huku anatetemeka kwa baridi, ndipo kichwani ukamjia mistari ya huu wimbo…”mwamba wenye imara…kwako nitajificha..”  Akilinganisha tukio hilo la dhoruba ya mvua kubwa na dhoruba ya kimaisha, ikamsukuma kuimba Yesu ni mwamba wake wa kujifichia..mpaka leo wimbo huo umekuwa Baraka kwa zaidi ya miaka 200.

Huo ni ujumbe wa Mungu kutuonyesha kuwa palipo na dhoruba basi kuna Mwamba…Hivyo hatupaswi kuogopa tunapopitia dhoruba, tunapoona juu kumefunga, maisha yamekwama, vita ni vingi, matatizo ni mengi…tunapofikia mahali tunaona kesho hatapafika, tunapoona mwaka huu hautaisha…Huo ndio wakati wa kumtazama Bwana aliye mwamba wetu..kwake huyo tutajificha…

Mwamba huu hautoi tu hifadhi wakati wa  dhoruba, bali pia unatoa maji baridi  na uvuli wakati wa jua kali..na huo sio mwingine zaidi ya YESU KRISTO, kama mhubiri huyu Augustus alivyoimba..

1Wakorintho 10: 4 “wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo”.

Je upo chini ya mwamba leo?..kama haupo..je wakati wa dhoruba utajificha wapi?…wakati wa tufani utakimbilia wapi?..je wakati wa jua kali utapata wapi uvuli? Na maji ya kunywa?…hivyo mkabidhi Kristo leo maisha yako naye atakuwa mwamba kwako.

Lakini kama umeshamkabidhi tayari muda mrefu..basi usitishwe na dhoruba zinazokuja mbele yako, wala usitishwe na vipindi vya hari ya jua kali na ukame…upitiapo hali kama hizo..mwamba upo karibu nawe..Ukumbuke msalaba, na mkumbuke mwokozi, mshukuru, na jinyenyekeze chini yake…na utaona maajabu baada ya kipindi kifupi… Hivyo imba wimbo huu uliovuviwa nguvu za Roho Mtakatifu kukufariji na kukutia moyo..

Mwamba wenye imara, kwako nitajificha
Maji hayo na damu, yaliyotoka humo
Hunisafi na dhambi, hunifanya Mshindi.

Kwa kazi zote pia, sitimizi sheria
Nijapofanya bidii, nikilia na kudhii
Hayaishi makosa, ni we wa kuokoa

Sina cha mkononi, naja msalabani
Nili tupu nivike, ni mnyonge nishike
Nili mchafu naja, Nioshe mi sijafa.

Nikungojapo chini, nakwenda kaburini
Nipaapo mbinguni, nakukuona enzini
Roho yangu na iwe, rahani mwako wewe

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

TENZI ZA ROHONI

WAKATI WA JUA KALI NDIO WAKATI WA KAZI:

USIHUZUNIKE.

WAKATI WA BWANA KUKUVUSHA, NI LAZIMA ARUHUSU JESHI LA ADUI KUNYANYUKA.

USIFIKIRI FIKIRI.

Rudi Nyumbani:

Print this post

HUYU SI YULE SEREMALA, MWANA WA MARIAMU?

Shalom.

Kulikuwa na sababu kwanini Yusufu awe seremala, vilevile kulikuwa na sababu pia kwanini Bwana wetu Yesu Kristo naye pia awe seremala, na sio kazi nyingine, kabla ya yeye kuanza huduma.

Tunayasoma hayo katika..

Marko 6:3 “HUYU SI YULE SEREMALA, mwana wa Mariamu, na ndugu yao Yakobo, na Yose, na Yuda, na Simoni? Na maumbu yake hawapo hapa petu? Wakajikwaa kwake”.

Soma tena..

Mathayo 13:55 “HUYU SI MWANA WA SEREMALA? Mamaye si yeye aitwaye Mariamu? Na nduguze si Yakobo, na Yusufu, na Simoni, na Yuda?”

Unaona Yesu na baba yake wote walijulikana sana mpaka kupata umaarufu kutokana na hiyo kazi yao ya Useremala, bila shaka walikuwa ni wabunifu wazuri sana, uundaji wao ulikuwa wa kipekee. Kama tunavyofahamu kazi hii, inakuwa ni pale mteja anakuja na mchoro wake na kutaka atengenezewa kitu Fulani, labda meza ya muundo fulani, au kiti au kabati zuri lenye shelfu 6 la nguo na vyombo..Sasa yeye akishamaliza kutoa maelezo yake, au mchoro wake, kwa upande wa pili anapigiwa gharama zote za material kisha anaacha pesa ya awali(advance), Halafu anaambiwa arudi labda baada ya wiki 2..

Huo muda ukishapita anarudi na kukuta kabati lake lipo tayari,safi kabisa limekamilika, anamalizia kiwango cha pesa alichobakisha, kisha analichukua kabati lake, anaondoka analipeleka nyumbani au ofisini.. Lakini ni rahisi kuliangalia ukaona kama ni kazi nyepesi, hajui taabu walisumbuka nayo wale maseremala.

Sasa Mungu kumpitisha Bwana Yesu katika ujenzi tena wa kazi ambayo ilikuwa tayari ni ya baba yake, Ni kumuonyesha kuwa upo ujenzi atakaopaswa aufanye wa kanisa ambalo kwanza lilikuwa ni la baba yake mbinguni..

Yesu kama seramala alijua ili kabati liundike, sio kusimamisha tu gogo,.. bali ilihitajika misumeno ipite, lilihitaji kufanyike vipimo vya hali ya juu, kama pa kuongezwa paongezwe na kama pa kupungwa papunguzwe,..Vilevile ilihitajika Nyundo, na misumari ya kutosha ihusike,…Na hiyo yote ni kufatana na kile alichokiona kikifanywa na baba yake au maagizo ya baba yake, na sio yake mwenyewe.

Na ndio maana alisema..

Yohana 5:19 “Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona Baba analitenda; kwa maana yote ayatendayo yeye, ndiyo ayatendayo Mwana vile vile.

20 Kwa kuwa Baba ampenda Mwana, naye humwonyesha yote ayatendayo mwenyewe; hata na kazi kubwa zaidi kuliko hizo atamwonyesha, ili ninyi mpate kustaajabu”.

Hivyo hata Kristo alipoanza kuijenga nyumba ya Mungu(Kanisa), alilijenga kwa maagizo ya baba yake, aliposema mtu yeyote akitaka kunifuata ajikane nafsi yake, ajitwike msalaba wake anifuate, alimaanisha, maagizo hayo hakujitungia mwenyewe bali aliyapokea hayo kutoka kwa Baba yake.

Aliposema aaminiye na kubatizwa ataokoka, hakujitungia mwenyewe, bali vipimo hivyo alivitoa kwa Baba yake. Kwamba ili mtu astahili uzima ni sharti amwaminiye yeye, na vilevile akabatizwe kihalili kama ipasavyo.

Aliposema duniani mna dhiki, lakini jipeni moyo,mimi nimeushinda ulimwengu, mambo hayo alionyeshwa na Baba yake kwamba kuna wakati watu wake watapaswa wapitie nyundo, na misumari mikali, na misimeno, kama yeye alivyopitia, ili wakamilishwe.

Wafilipi 1:29 “Maana mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, ila na kuteswa kwa ajili yake”

Hivyo ndugu yangu, hata mimi na wewe leo, hatuna budi kumruhusu Kristo ambaye ndiye seremala mkuu na mwaminifu wa maisha yetu atuunde tuwe kama Mungu apendavyo, tunapopitishwa na yeye katika moto, tustahimili, tunapopitishwa na yeye wakati mwingine katika dhiki, vilevile tustahimili, kwasababu tutakapokamilishwa, tutakuwa vyombo vyenye thamani nyingi sana..

Mambo hayo tutayajua vizuri tutakapofika ng’ambo kwa yale mema mazuri Mungu aliyotuandalia. Kwasababu huo ujenzi wake hauishii tu kwenye maisha yetu, bali pia kwenye Makazi yetu ya milele, aliyokwenda kutuandalia..

Yohana 14:1 “Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi.

2 Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali.

3 Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo.

4 Nami niendako mwaijua njia”.

Bwana akubariki.

Je! Umeyakabidhi maisha yako kwake?. Kama bado basi wakati wako ndio huu. Usisibiri wakati mwingine, kwasababu huo hautafika. Fanya uamuzi sasa wa kumgeukia yeye aliye mkuu wa uzima, ambaye aliyatoa maisha yake kwa ajili yako, ili upokee maisha ya milele. Natumai leo haitapita bila kumkaribisha Kristo ndani yako.

Waebrania 12:3 “Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu”

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

HUYU MELKIZEDEKI NI NANI?

WAKATI WA BWANA KUKUVUSHA, NI LAZIMA ARUHUSU JESHI LA ADUI KUNYANYUKA.

HERI NINYI MLIAO SASA, KWA SABABU MTACHEKA.

WANA JUHUDI KWA AJILI YA MUNGU, LAKINI SI KATIKA MAARIFA.

TUNAMHITAJI SANA ROHO MTAKATIFU KATIKA KUYAELEWA MAANDIKO.

Rudi Nyumbani:

Print this post

USIRUHUSU MUNGU AWEKE UADUI KATI YAKO NA WATU WAKO.

Bwana Yesu Kristo asifiwe.

Karibu tujifunze biblia, Neno la Mungu wetu, ambalo ndio mwanga wa njia yetu na taa iongozayo miguu yetu.

Ili tufanikiwe na tuwe na maisha mazuri siku zote ni lazima tujifunze kulitii na kulishika Neno la Mungu. Kinyume na hapo tutasumbuka sana bila sababu.

Watu wengi wanatafuta kutengeneza urafiki na undugu na watu wengi…wakitegemea marafiki hao wakati wa tabu watawafariji, au wakati wa shida watawasaidia, lakini wengi wanaishia kuumizwa na hao hao marafiki au ndugu, na kupata vile wasivyovitegemea. Unakuta urafiki utaanza vyema lakini utaishia kuwa uadui. Wengine wanatafuta wanawake/wanaume wakitazamia hao ndio watakaokuja kuwa waume zao au wake zao..lakini mwisho wanaishia kuumizana na kuharibiana maisha.

Ipo sababu ya mambo hayo kuwa hivyo…Na sababu hiyo ilianzia tangu Edeni. Hivyo kama tutalielewa somo vizuri kilichotokea Edeni basi, hatutarudia makosa ambayo tayari yalishafanywa na tukaona madhara yake.

Sasa hebu tuwatafakari hawa marafiki wawili ambao hapo kwanza walikuwa na mahusiano mazuri lakini yakaishia kuwa mabaya tena ya uadui. Na marafiki hao si wengine zaidi ya HAWA NA NYOKA. Wote hawa walikuwa wapo katika uwepo wa Mungu, na walikuwa wanakaribiana sana…lakini baada ya kuyaasi maagizo ya Mungu, Mungu akaweka uadui mkubwa katikati yao…Kiasi kwamba mpaka leo Nyoka na mwanadamu ni maadui wakubwa sana…Ukiuliza ni kiumbe gani wa kwanza anayeogopwa na wanawake wengi nadhani asilimi zaidi ya 90 watamtaja nyoka..Hiyo ni kutokana na uadui ambao Mungu aliuweka mwenyewe katikati yake yeye na nyoka.

Mwanzo 3: 14 “Bwana Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako;

15 NAMI NITAWEKA UADUI KATI YAKO NA HUYO MWANAMKE, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino”.

Umesoma hapo mstari wa 15?…Watu wengi hawajui kuwa UADUI ambao unatokea ghafla kati yao na ndugu zao, au marafiki zao mwingi unawekwa na MUNGU mwenyewe na wala si shetani, na huo ni kutokana na kuacha kulitii na kulishika Neno lake.

Kwamfano utakuta mwanamke… anakutana na mtu ambaye anahisi atakuwa mume wake, na moyoni anajua kabisa hapaswi kukutana kimwili na yoyote Yule mpaka atakapoolewa (kanisani ameshafundishwa sana na yeye mwenyewe anayajua maandiko)…lakini kwa kulikaidi Neno la Mungu anaamua amridhishe Yule mwanaume na kwenda kufanya naye uasherati, akidhani baada ya kitendo hicho ndio atapendwa zaidi…kumbe kinyume chake ni kuchukiwa, baada ya hapo anashangaa Yule aliyemtegemea ampende ndio hana muda na yeye tena..na mwisho wa siku anajiona kama sio mwenye bahati.

Hivyo mwanamke hupaswi kumsogelea kabisa mwanaume, katika kipindi cha uchumba…kipindi cha uchumba sio kipindi cha kutembeleana nyumbani na huku mko wawili tu, si kipindi cha kupikiana pikiana, sio kipindi cha kukutana kutana nyumbani na huku mpo wawili tu!…kwasababu hicho ndio kipindi maalumu cha shetani kupanga kuvuruga mambo…Kama umeandaa chakula mwite mtu zaidi ya mmoja kwako pamoja na huyo mnayekaribiana kuoana lakini si nyinyi wawili tu peke yenu..na pia kumbuka huruhusiwi kabisa pia kumbusu mtu ambaye bado hamjafunga ndoa.

Mambo madogo kama hayo yanadharauliwa na wengi lakini ndio yanayovuruga mipango yote…Na kamwe usifikiri ukimheshimu Mungu, utachukiwa na Yule anayetaka kukuoa au unayetaka kumuoa…Kama ndiye Bwana aliyekusudia awe wako, hawezi kukuchukia zaidi ya yote ndio atakupenda.. Lakini mkivuka mipaka na kwenda kufanya uasherati kabla ya ndoa..hapo ndio basi tena!…kuna nafasi ndogo sana, au isiwepo kabisa ya nyinyi kuoana..mtaishia kuchukiana kwa chuki ya ajabu baada ya kipindi kifupi…mpaka mtashangaa wenyewe ni nini kimetokea…Mungu atawawekea uadui katikati yenu. Kwasababu Mungu hawezi kuunganisha wazinzi pamoja, maana lengo la Mungu kuwakutanisha kwenye ndoa ni ili awabariki…sasa hawezi kuunganisha wazinzi wawili na tena kuwabariki…atakachokifanya ni kuwaweka mbali mbali, au kuwaacha muendelee na uzinzi wenu na yeye asiwe na nyinyi (warumi 1:28).

Kama wewe ni msomi wa biblia utakuwa umewahi kusoma kisa cha Yule mtoto wa Daudi aliyemtamani dada yake, na kumlazimisha alale naye…na baada tu ya kulala naye biblia inasema alimchukia kwa chuki isiyokuwa ya kawaida.

2 Samweli 13:13 “Nami nichukue wapi aibu yangu? Wewe nawe utakuwa kama mmoja wa wapumbavu wa Israeli. Basi, sasa, nakusihi, useme na mfalme; kwa maana hatakukataza kunioa.

14 Walakini yeye hakukubali kusikiliza sauti yake; naye akiwa na nguvu kuliko yeye, akamtenza nguvu, akalala naye.

15 Kisha Amnoni AKAMCHUKIA MACHUKIO MAKUU SANA; KWA KUWA MACHUKIO ALIYOMCHUKIA YAKAWA MAKUU KULIKO YALE MAPENZI ALIYOKUWA AMEMPENDA KWANZA. Amnoni akamwambia, Ondoka, nenda zako.

16 Naye akamwambia, Sivyo, kwa kuwa mabaya haya ya kunitoa ni makuu kuliko yale uliyonitendea. Lakini alikataa kumsikiliza.

17 Ndipo akamwita mtumishi wake aliyemtumikia, akasema, Mtoe sasa mwanamke huyu kwangu, ukafunge mlango nyuma yake”.

Ukianzia kusoma kuanzia mstari wa kwanza utaona, Kisa hicho ingawa mwanamke ndiye aliyelazimishwa kwa nguvu…lakini matokeo yake yalikuwa ni yale yale “CHUKI BAADA YA TUKIO”.

Kuna nguvu Fulani ya uadui inashuka kwa watu wanaovunja amri za Mungu..

Mnakubaliana kwenda kuiba au kula rushwa, mwisho wa siku ni lazima tu muishie kugombana…Mnakubaliana kufanya kazi haramu mwisho wa siku ni lazima muishie tu kuwa maadui, mnakubaliana kwenda kufanya utapeli/uuaji lazima mtaishia tu kugombana na kuchukiana na kuwa maadui, mtaanza vizuri lakini itafika kipindi mtatofautiana tu!!… fanya utafiti watu wawili wanaokaa kitako kumsengenya mwingine…huwa wanaishia na wao kugombana au kuchukiana, badala ya kuzidi kuwa pamoja..

Unakumbuka Mnara wa Babeli walianza pamoja lakini nia yao ilipokuwa katika kuujenga mji na mnara wa kishetani, ili waabudu miungu, Mungu aliwasambaratisha, wakawa hawaelewani, huyu akisema hivi mwingine anasema hivi, wakagombana na mwisho wa siku hata lugha zikazalika nyingine…kazi ngumu waliyokuwa wameianza ikaishia pale pale.

Lakini kinyume chake kama ukiyashika maagizo ya Mungu na amri zake, na kumheshimu…Bwana anasema atakupa amani hata na maadui zako…

Mithali 16: 7 “Njia za mtu zikimpendeza Bwana, Hata adui zake huwapatanisha naye”.

Hivyo zishike amri za Mungu, na mambo yatakunyookea…ukitaka uwe na amani na ndugu zako, fomula ni hiyo hiyo.. “lishike Neno la Mungu”..usiwe kama Hawa mama yetu..aliyedhani kuuimarisha urafiki na nyoka ni kula lile tunda…kinyume chake ndio aliimarisha uadui kati yake na huyo nyoka, na hiyo roho imeendelea mpaka kwa vizazi vyake hadi leo.

Bwana atusaidie

Kama hujampa Yesu maisha yako, hapo jitenge binafsi, piga magoti tubu kwa dhati kabisa na kisha acha yote uliyokuwa unayafanya yasiyompendeza Mungu, na baada ya hapo tafuta kanisa lililopo karibu nawe la kweli, dumu hapo ujifunze Neno na pia upate kubatizwa..Na Roho mtakatifu atakuwa na wewe kukuongoza katika kweli yote.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

NAO WAKADHANI YA KUWA YUMO KATIKA MSAFARA;

VITA VYA IMANI NI VITA ENDELEVU.

VITA VYA IMANI NI VITA ENDELEVU.

KILA MMOJA WENU AJUE KUUWEZA MWILI WAKE.

KILA MMOJA WENU AJUE KUUWEZA MWILI WAKE.

DAMU YA YESU INANENAJE MEMA KULIKO YA HABILI?

Rudi Nyumbani:

Print this post