Yesu ni Mungu?, Na Kama ni Mungu kwanini alikufa?

Yesu ni Mungu?, Na Kama ni Mungu kwanini alikufa?

SWALI: Je! Yesu ni Mungu? Na Kama ni Mungu kwanini alikufa?


JIBU: Yesu alikuwa ni Mungu katika mwili (1Timotheo 3:16)…lakini hakuja kutafuta kuabudiwa wala kusujudiwa!…Mpaka Mungu amevaa mwili na kuja ulimwenguni, maana yake hajaja kutafuta kuabudiwa, kama angekuwa amekuja kutafuta utukufu wake basi, kulikuwa hakuna haja ya kuuvaa mwili na kushuka duniani, naamini Mbingu ilikuwa inamtosha…. hivyo ni lazima atakuwa amekuja kwa kusudi lingine na si la kutafuta utukufu. Hapo ndipo wengi wa wasio wakristo wanaposhindwa kuelewa, na baadhi ya walio wakristo.

Unapoona askari wa kuongoza barabarani (Traffic man), kaondoka barabarani na kaenda nyumbani kubadilisha nguo zake hizo nyeupe…na akavaa nguo za kiraia na kuingia mtaani basi ni dhahiri kuwa huko mtaani alikokwenda hajakwenda kutafuta kuongoza magari bali kaenda kutafuta mambo yake mengine ya kawaida..labda anaenda hospitalini au sokoni au kusalimia ndugu na marafiki, au kufuatilia mambo yake mengine ambayo ni tofauti na ya kikazi….. (ni kweli bado atabaki kuwa askari, lakini yupo nje ya ofisi yake), hivyo hataweza kuyatumia yale mamlaka aliyonayo ya kuongoza magari,…na akiwa barabarani na nguo zake za kiraia, hata watu wanaweza wasimtambue kama ni askari, atakuwa kama raia wengine tu, na magari atakuwa anayakwepa tu kama raia wengine, na atazingatia sheria zote za barabarani kama raia wengine…

Na Bwana Yesu ni hivyo hivyo…alipokuwa mbinguni alikuwa ni Mungu, anayestahili kuabudiwa na kuheshimiwa…aliposhuka duniani alikivua kile cheo cha Kiungu…na kuwa kama mwanadamu (kwa lengo la kuja kumkomboa mwanadamu na si kuabudiwa kama Mungu)..na baada ya kumaliza akarudi mbinguni alikotoka katika cheo chake.

Hivyo akiwa kama mwanadamu alikuwa hana budi aishi kama wanadamu wengine, hana budi awe mtu wa ibada kama watu wengine, hana budi ale, anywe, alale, achoke, apitie yote mwanadamu wa kawaida anayopitia na hata ikiwezekana afe…ili tu kusudi lake lililomleta duniani litimie la kumkomboa mwanadamu…lakini alikuwa bado ni Mungu.

Wafilipi 2: 5 “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu;

6 ambaye yeye mwanzo alikuwa YUNA NAMNA YA MUNGU, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho;

7 bali ALIJIFANYA kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu;

8 tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba”.

Umeona hapo mstari wa 7?..unasema “ALIJIFANYA”..kama unakielewa Kiswahili vizuri utakuwa unajua maana ya “KUJIFANYA”..Maana yake ni kama kujigeuza/kuigiza kuwa kitu Fulani na kumbe sio…kwa lengo la kutimiza kusudi Fulani tu!…Hivyo Bwana Yesu aliyejifanya kuwa hana utukufu…ili ashuke aje kutukomboa na kutuonyesha njia jinsi mwanadamu kamili anayemcha Mungu anapaswe awe.

Hivyo kufa kwa Bwana Yesu, hakumfanyi yeye asiwe Mungu..na pia muujiza mkubwa duniani na mbinguni sio kutokufa!!… Huo ni muujiza mdogo sana…..“miujiza mkubwa ni uwezo wa mtu kuutoa uhai wake na kisha kujirudishia ule uhai”..Huo ndio muujiza mkubwa kuliko yote!..na uwezo huo alikuwa nao Yesu pekee yake.

Yohana 10:17 “Ndiposa Baba anipenda, kwa sababu nautoa uhai wangu ili niutwae tena.

18 HAKUNA MTU ANIONDOLEAYE, BALI MIMI NAUTOA MWENYEWE. NAMI NINAO UWEZA WA KUUTOA, NINAO NA UWEZA WA KUUTWAA TENA. Agizo hilo nalilipokea kwa Baba yangu”.

Sasa utauliza ni wapi, Yesu aliutoa uhai wake mwenyewe?…kasome Luka 23:46-47. Bwana Yesu aliutoa uhai wake mwenyewe! Hakuna mtu aliyemsaidia kuutoa..hata Pilato alishangaa imekuwaje amewahi kufa kiasi kile (Marko 15:44). Na aliurudisha uhai wake mwenyewe baada ya siku tatu (kule kaburini hakuna mtu aliyeenda kumfufua au kumwombea afufuke).

Alijirudishia uhai wake mwenyewe!..Nadhani huo ni muujiza mkubwa sana.. Je wewe unaweza kufanya hivyo????

Hata mfano nikikuwekea watu wawili mbele yako mmoja hawezi kuukata mguu wake na mwingine anao uwezo wa kuukata na kuurudisha….nikakwambia kati ya hao wawili ni yupi hapo wa kuogopwa zaidi??..Bila shaka utaniambia “Yule mwenye uwezo wa kuukata mguu wake na kisha kujirudisha tena ndiye wa kuogopwa zaidi kuliko huyo mwingine”.

Kwahiyo kuupima uungu wa Bwana Yesu na kifo chake ni hoja dhaifu!!..miungu ya kipagani ndio isiyo na uwezo wa kufanya hayo..lakini Mungu wa mbingu na nchi (YESU KRISTO) anaweza kufanya mambo yote. Mpaka sasa katika historia hajatokea nabii yoyote wala mtume yeyote aliyofanya miujiza kama aliyofanya Bwana Yesu, sasa kwanini asiwe Mungu?. Na siku moja atarudi na kila jicho litamwona na kila goti litapigwa, na kila kinywa kitakiri…Wengi itakuwa ni jambo la kushtukiza sana kwao, kwasababu hawataamini kwamba kweli ndiye!..kwasababu walidanganyika wakiwa duniani kwamba hatarudi.

Lakini anatupenda na wala hataki mtu yoyote apotee bali wote tuifikie toba, ili tuokoke na tuje kutawala naye milele.

Bwana atubariki tuzidi kumjua yeye!

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

Mbona Mungu anaruhusu watu wapate shida, ilhali ana uwezo wa kutuepusha?

Katika biblia Neno “Mshenzi” linatajwa.Kwanini liwekwe?

Kile kinara cha Taa ndani ya Hekalu la Sulemani kilikuwa kinawakilisha nini?

Je! Ni kweli ubatizo wa maji hatuuhitaji tena?

DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments