FUKUZA TAI WOTE JUU YA SADAKA YAKO.

FUKUZA TAI WOTE JUU YA SADAKA YAKO.

Fukuza tai wote..

Shalom, Jina la mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe daima,.

Karibu tujifunze Neno la Mungu..

Lipo jambo naamini utaongeza katika Habari hii nzuri ya Ibrahimu ambaye tunamwita baba wa Imani, nasi leo tuige hii Imani yake..Embu tusome sasa..

Mwanzo 15:7 “Kisha akamwambia, Mimi ni Bwana, niliyekuleta kutoka Uru wa Wakaldayo nikupe nchi hii ili uirithi.

8 Akasema, Ee Bwana MUNGU, nipateje kujua ya kwamba nitairithi?

9 Akamwambia, Unipatie ndama wa miaka mitatu, na mbuzi mke wa miaka mitatu, na kondoo mume wa miaka mitatu, na hua, na mwana njiwa.

10 Akampatia hao wote, akawapasua vipande viwili, akaweka kila kipande kuelekea mwenzake, ila ndege hakuwapasua.

11 Hata tai walipotua juu ya mizoga Abramu akawafukuza.

12 Na jua lilipokuwa likichwa usingizi mzito ulimshika Abramu, hofu ya giza kuu ikamwangukia”.

Kama tunavyosoma Habari hiyo, kuna wakati Ibrahimu alimwomba Mungu amthibitishie kuwa alichomwahidia ni kweli, kama Gideoni alivyofanya..hivyo Mungu akampa maagizo Ibrahimu juu ya sadaka atakayomwandalia ili aitoe, Hivyo Pengine Ibrahimu akaamka asubuhi na mapema sana, na kwenda mbali kabisa na maeneo ya watu porini, kisha akaindaa akaiweka juu ya kuni, labda kwenye saa moja moja hivi asubuhi alikuwa ameshamaliza shughuli yote ya kuindaa, kinachofuata kwake ni kusubiria sasa aone hatua Mungu anayoichukua..Lakini kilichotokea kwake kilikuwa ni nje ya matarajio yake, alitazamia Mungu angeshuka kwenye muda ule ule, au saa mbili mbili hivi, lakini hakuona chochote,

Akasubiria tena labda kwenye saa nne nne, au saa tano, hakuona chochote, anaingalia tu ile sadaka, aone ni kitu gani Mungu atakwenda kufanya lakini hakuna chochote kilichotokea muda wote huo, mpaka Jua la saa saba linaanza kuwa kali, anaona sasa asogee pembeni kidogo kwenye mti wenye kivuli aendelee kuikodolea macho ile sadaka yake aliyoitoa mapema asubuhi lakini hakuona chochote, mchana kutwa mpaka inafika alasiri, bado akiwa huko porini mwenyewe haoni chochote, akiingalia tu ile nyama, ikianza kukakamaa na mainzi kuongezeka, mpaka sasa wale tai wa angani ambao kazi yao ni kupita porini kutafuta mizoga, wanaiona ipo pale kwa muda mrefu wakidhani pengine ni simba aliila na kuiacha, wakaanza kushuka sasa waile..

Lakini Ibrahimu hakukata tamaa na kuwaachia Tai wale waile sadaka yake aliyoitaabikia tangu asubuhi, japokuwa hamwoni Mungu akimjibu kwa lolote, badala yake kila walipojaribu kutua aliondoka pale kichakani alipokuwa amekaa, na kwenda kuwafukuza..

Aliendelea kufanya hivyo mpaka jua linaanza kuchwa(yaani kuzama), biblia inatuambia, hofu ya giza kuu ikaanza kumwangukia, ni wazi kuwa eneo lile halikuwa eneo lenye makazi ya watu, ni pori nene, hata sadaka yake akawa haioni tena vizuri, ni kama vile Mungu kaitelekeza, au pengine hajairidhia, au pengine alimkosea, lakini katikati ya hofu ile na mashaka yale, muda huo huo alipitiwa na usingizi mzito,..Na ndani ya usingizi ule Mungu akaanza kuzungumza naye, na kumwambia mambo yanayokuja kutokea mbele yake yeye na uzao wake na kumpa ahadi na kumbariki na kumwonyesha nchi atakayompa..

Na alipoamka tu, akashangaa kuona moto umetokea katikati ya ile Sadaka yake, na tayari umeshakwisha kuiteketeza..Ni furaha kiasi gani.kuona unajibiwa maombi yako wazi wazi na Zaidi ya yote Mungu anazungumza na wewe.

Lakini ni nini Mungu anataka tujue ndani ya Habari hiyo?

Wengi wetu, tunakuwa na moyo wa kumtolea Mungu sana katika siku za mwanzoni, na tukishamaliza huwa tunatazama ni wapi Mungu atatubariki, Labda utakuta mtu zamani, alikuwa anatoa ZAKA kwa wakati mbele za Mungu, alikuwa ni mwaminifu kutoa kile alichomwahidia Bwana,..Lakini baadaye alipoona mwezi wa kwanza, na wa pili, na wa tatu, unapita na bado haoni badiliko lolote, au haoni faida yoyote aliyoipata tangu aanze kumtolea Mungu, Zaidi ndio hali inazidi kuyumba hapo ndipo anapokata tamaa na kuacha kuendelea kumtolea Mungu..

Wengine, wanaweza kuwa na nia ya kuendelea kweli kumtolea Mungu, lakini sadaka zao wanaziruhusu zidokolewe na TAI, tofauti na pale mwanzoni wanasema moyoni moyoni aah! Mwaka mzima huu ninatoa fungu la 10, na sioni baraka zozote wacha mwezi huu niiongezee kwenye karo ya shule ya Watoto, kisha mwenzi ujao nitatoa, wengine wanasema, aah, dharura hii imenipata Rafiki yangu anaomba nimtolee mchango wa harusi ngoja mwezi huu nisitoe zaka yangu kwa Mungu..

Ndugu Ibrahimu, hakuruhusu, sadaka yake idokolewe na TAI, japokuwa hakumwona Mungu kwa wakati alioutegemea, lakini aliilinda sadaka yake, kuhakikisha kuwa kile alichoagizwa ndicho atakachokitoa kikiwa kamili hadi dakika ya mwisho muda wote,haijalishi Mungu atawahi au atachelewa.

Lakini tunaona kabla ya Ibrahimu kuingia katika giza kuu, Mungu alimjia na kumtokea, na kuiteketeza sadaka yake..Na kumbariki..

Ndivyo hivyo hata sisi, hatupaswi kuangalia na kusema, tangu nilipoanza kumtolea Mungu, sikuwahi kuona baraka yoyote, wewe endelea kumtolea kwa uaminifu, tu, usiruhusu, sadaka yako imegwe megwe na mambo yasiyokuwa na maana..Haijalishi huoni mabadiliko yoyote kwa miezi au miaka sasa..Lakini endelea kuwa mwaminifu na Mungu aliyemwaminifu Zaidi ya waaminifu, upo wakati ameuweka wa kushusha moto juu ya sadaka yako.. Ukifika huo wakati wewe mwenyewe hutahitaji kusema huyu ni Mungu, kwani mambo yatakuwa wazi mbele ya macho yako.

Tunaona mfano wa Kornelio katika agano jipya, jinsi sadaka zake, zilivyogeuzwa na kuwa ukumbushombele za Mungu (Matendo 10), Jambo lililomfanya sio awe mkristo, lakini hadi sasa tunaisoma Habari yake, katika maandiko.

Vivyo hivyo na sisi, wakati mwingine Mungu anaujaribu uaminifu wetu..Hivyo unapoona huoni faida yoyote sasa katika kumtolea Mungu, usiwe mjinga ukaacha kumtolea au ukaruhusu sadaka zako kudonolewa donolewa, na sababu zisizokuwa na maana yoyote, nataka nikuambie mwisho wa siku hutaambulia chochote, kwasababu Mungu hapokei sadaka kilema.(Malaki 1:14)

Ubarikiwe.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

TUMTOLEE MUNGU VILE VINAVYOTUGHARIMU ZAIDI.

KWANINI UBATIZO NI WA MUHIMU.

SI KWA FAIDA YA MWENYEZI, BALI KWA FAIDA YETU.

MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA KITABU CHA RUTHU:

KUTUBU SIO KUOMBA REHEMA.

NI WAPI MAHALI SAHIHI PA KULIPA ZAKA?

TOA SADAKA ISIYO NA KASORO KWA BWANA.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
4 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
JOHN GEORGE
JOHN GEORGE
11 months ago

Nini hasa kina mpendeza bwana kutoa kama sadaka katika madhabahu yake pesa ama bidhaa?

Godfrey Vicent
Godfrey Vicent
1 year ago

Jina la Bwana YESU ASIFIWE? Nimependa sana masomo yenu naomba muwe mnanitumia masomo yenu Asante na mungu awabariki sana