Je! Israeli wote wataokolewa siku ya mwisho kulingana na Warumi 11:26?

Je! Israeli wote wataokolewa siku ya mwisho kulingana na Warumi 11:26?

Jibu: Tusome,

Warumi 11:25 “ Kwa maana, ndugu zangu, sipendi msiijue siri hii, ili msijione kuwa wenye akili; ya kwamba kwa sehemu ugumu umewapata Israeli, mpaka utimilifu wa Mataifa uwasili.

26 Hivyo Israeli wote wataokoka; kama ilivyoandikwa, Mwokozi atakuja kutoka Sayuni; Atamtenga Yakobo na maasia yake”

Ni kweli upo unabii wa Israeli wote kuokolewa katika siku za mwisho, kuna kipindi ambacho injili itahamia katika Taifa la Israeli baada ya unyakuo kupita!..wakati huo kanisa la mataifa litakuwa limeshanyakuliwa, Ndipo injili itaanza kuhubiriwa tena katika Taifa la Israeli na wale manabii wawili tunaowasoma katika kitabu cha Ufunuo 11, watahubiri kama nyakati za Yohana Mbatizaji isipokuwa zama hizo itakuwa ni kwa ishara nyingi na miujiza mfano wa ile ya Musa na Eliya.

Na kupitia injili ya hao manabii wawili, waisraeli wengi watamkubali Yesu kama Masihi, kumbuka kwasasa wayahudi wengi (yaani waisraeli wengi), hawaamini kuwa Yesu Yule aliyekuja na kufa na kufufuka kuwa ndiye Masihi aliyetabiriwa na manabii zamani, wanaamini kuwa Masihi bado hajaja, na Yesu sio Masihi, hivyo wanamsubiria mwingine!!..Biblia inasema macho yao yamefumbwa wasimtambue Yesu kuwa ndiye Masihi, ili sisi watu wa mataifa tupate neema. (Warumi 11:30-31).

Sasa swali la Msingi hapo, ni je Israeli wote wataokolewa?..hata kama ni watenda maovu?..na je kitendo tu cha kuzaliwa  Muisraeli tayari umeshapewa tiketi ya kuurithi uzima  wa milele?.

Jibu ni La!… Sio wote watakaookolewa, kwasababu wapo waisraeli wasioamini kabisa hata kama Mungu yupo, wapo wachawi na manabii wa uongo katikati ya jamii za Israeli mfano wa akina Bar-Yesu (Matendo 13:6), hao hawataokolewa na wataenda katika ziwa la moto, kama hawatatubu!..

Sasa kwanini hapo biblia iseme ni  “Israeli wote”, na si baadhi!.. kama watakuwepo baadhi ambao hawataokolewa?, kwanini iseme wote?.. Ili kuelewa vyema tusome mstari ufuatao.

Warumi 9:6  “Si kana kwamba neno la Mungu limetanguka. MAANA HAWAWI WOTE WAISRAELI WALIO WA UZAO WA ISRAELI.

7  Wala hawawi wote wana kwa kuwa wazao wa Ibrahimu, bali, Katika Isaka wazao wako wataitwa; ”

Unaona hapo?.. Sio Waisraeli wote ni waisraeli, ni sawa na kusema “Si wote wanaojiita au wanaojulikana kuwa ni wakristo ni wakristo”. Sasa hivi duniani kuna zaidi ya mabilioni ya wakristo. Lakini kiuhalisia “Wakristo wa kweli ni wachache”, ni wale wanaozishika amri za Mungu na kufanya mapenzi yake, hao wengine ni wakristo jina tu!. Kwahiyo kwenye biblia kungekuwa na mstari unaosema “wakristo wote wataokolewa” bila shaka, ingekuwa imemaanisha “wale wakristo wa kweli” na si wakristo jina!.. mtu anayejiita mkristo lakini mchawi, hawezi kuurithi uzima wa milele, mtu anayejiita mkristo lakini ni mzinzi vivyo hivyo!

Kadhalika biblia iliposema “Israeli wote wataokolewa” ilimaanisha wale “wale waisraeli kweli kweli” ambao wanakwenda katika sheria za Mungu bila kupinda panda. Hao ndio wote watakaookolewa. Mfano wa hao ni wakina Nathanieli katika Yohana 1:47 “Basi Yesu akamwona Nathanaeli anakuja kwake, akanena habari zake, Tazama, MWISRAELI KWELI KWELI, hamna hila ndani yake”

 Lakini wengine wasiompenda Mungu, maana yake ni waisraeli jina tu!, Lakini sio waisraeli hasa!!, hao hawataokolewa, Ndicho Mtume Paulo alichokuwa anakimaanisha hapo katika Warumi 9:6 kuwa “….HAWAWI WOTE WAISRAELI WALIO WA UZAO WA ISRAELI”.

Vivyo hivyo hawawi wote wakristo, walio wa uzao Kristo!!. Walio uzao wa Kristo ni wale waliozaliwa mara ya pili, hao ndio Wakristo, wengine ni wakristo jina tu!..

Je wewe ni Mkristo halisi au mkristo jina tu!.. Mkristo jina ni Yule anayekwenda kanisani lakini anafanya uzinzi kwa siri, ni yule mwenye jina la kikristo lakini ni mtu wa kidunia, mkristo jina ni Yule anayeupenda ulimwengu kuliko kumpenda Mungu, mkristo jina ni yule asiyechukua msalaba wake na kumfuata Yesu. Lakini mkristo kweli kweli ni Yule aliyeukataa ulimwengu, anayejitwika msalaba wake kila siku na kumfuata Yesu kwa gharama zozote.

Bwana atusaidie tuwe wakristo halisi!

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

AINA TATU ZA WAKRISTO.

AINA TATU ZA WAKRISTO.

JE NI HALALI KUOA WAKE WENGI, AU KUTOA TALAKA?

LIPI TUNAJIFUNZA KWA WALIOMWONA YESU ALIYEFUFUKA?

Rudi nyumbani

Print this post

Ayari ni nini kama tunavyosoma katika biblia?

Ayari ni mtu aliyekosa utu,  mchoyo  na asiyejali watu,  anayejipenda mwenyewe, na mwenye hasira nyingi na madanganyifu. Kwa ufupi ni mtu asiyependa watu kwa ujumla.

Mfano wa watu hawa katika biblia ni Nabali, ambaye pamoja na kwamba Daudi na wenzake walimfanyia wema mwingi, hakujali kuwastahi hata kwa maji au kwa chakula (1Samweli 25).. na mwingine ni yule Tajiri wa Lazaro ambaye aliishi hapa duniani katika maisha ya anasa na ya ubinafsi, akafa katika dhambi zake, akaenda kuzimu.(Luka 16)

Neno hilo utalisoma katika vifungu hivi kwenye biblia;

Isaya 32:5 “Mpumbavu hataitwa tena mwungwana, WALA AYARI HATASEMWA KWAMBA NI KARIMU.

6 Maana mpumbavu atanena yaliyo upumbavu, na moyo wake utafanya maovu, ili kutenda hila na kusema yasiyo kweli juu ya Bwana, ili kuziacha nafsi za watu wenye njaa hazina kitu, na kukikomesha kinywaji chake mwenye kiu.

7 Tena VYOMBO VYAKE AYARI NI VIBAYA; hutunga hila mbaya, ili kuwaangamiza wanyonge kwa maneno ya uongo, mtu mhitaji ajaposema maneno yenye haki.

8 Bali mwungwana huwaza mambo ya kiungwana, naye hushika sana mambo ya kiungwana”.

Kwa mfano katika habari hiyo, kama ukianzia  mistari ya juu mstari wa kwanza utapata picha kamili ni nini kilikuwa kinazungumziwa,  anasema..

Isaya 32:1 Tazama, mfalme atamiliki kwa haki, na wakuu watatawala kwa hukumu.

Huo ni unabii unaomzungumzia Kristo katika utawala wake wa amani utaokuja huko mbeleni, kwasababu yeye ndiye atakayemiliki kama mfalme, Na katika huo utawala wake, hakutakuwa na kupindisha haki, kama ilivyo sasahivi, kwa sasahivi fisadi ndio anaonekana mwerevu, Mtu mbinafsi, ndiye anayeonekana  ana akili. Wapumbavu ndio wanaopewa uongozi, mtoa rushwa ndiye anayeonekana  ni mkarimu, Ayari (mtu asiyependa watu) ndio anayehesheshimika na kuogopeka katika jamii n.k.

Lakini katika huo utawala wa Amani wa miaka 1000 wa Yesu Kristo hapa duniani, hilo jambo halitakuwepo,  anasema..

“Mpumbavu hataitwa tena mwungwana, wala AYARI hatasemwa kwamba ni karimu”.

Hii ikiwa na maana kuwa watenda haki ndio watasifika katika haki yao, bali watendao uovu, watakutana na fimbo ya chuma ya Yesu Kristo, (Ufunuo 2:27).

Fahamu kuwa, kwa Mungu hakuna upendeleo, hata leo hii ikiwa utakufa katika hali yako ya dhambi, hakuna nafasi ya pili, kama umestahili mbingu, utakwenda mbinguni, kama umestahili Jehanum, utakwenda Jehanum, nafasi ya kutubu ipo leo, haipo baada ya kufa, hivyo mgeukie Yesu Kristo ayaokoe Maisha yako. Kwasababu hizi ni siku za mwisho.. Wakati ambao mtu kufanya dhambi ndio anasifiwa.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

YESU NI MFALME WA AINA GANI KWAKO? 

JE NI KWELI SAMAKI NGUVA YUPO?

Kwa kuwa ni shida mtu kufa kwa ajili ya mtu mwenye haki;

Alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru

Mafundisho

Rudi nyumbani

Print this post

YESU NI MFALME WA AINA GANI KWAKO? 

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tuyatafakari maandiko pamoja.

Je Bwana Yesu ni Mfalme katika maisha yako?..Kama una tabia zifuatazo, hajawa bado Mfalme kwako, haijalishi utamkiri kiasi gani.

Kama unamtafuta kwaajili ya faida zako za kimwili, ikiwemo kupata mali, kupata mke, kupata mume, kupata watoto, kupata umaarufu, na mambo mengine yote ya kimwilini , Tambua kuwa yeye si mfalme kwako, haijalishi utamtangaza kwa watu kuwa ni mfalme kwako, lakini yeye hakujui!!.

Utauliza tunasoma wapi katika maandiko?.. Hebu tukitafakari kisa kifuatacho kwa ufupi kisha tutapata majibu…

Yohana 6:10  “Yesu akasema, Waketisheni watu. Na mahali pale palikuwa na majani tele. Basi watu waume wakaketi, wapata elfu tano jumla yao.

.11  Basi Yesu akaitwaa ile mikate, akashukuru, akawagawia walioketi; na kadhalika katika wale samaki kwa kadiri walivyotaka.

12  Nao waliposhiba, aliwaambia wanafunzi wake, Kusanyeni vipande vilivyobaki, kisipotee cho chote.

13  Basi wakavikusanya, wakajaza vikapu kumi na viwili, vipande vya mikate mitano ya shayiri vilivyowabakia wale waliokula.

14  Basi watu wale, walipoiona ishara aliyoifanya, walisema, Hakika huyu ni nabii yule ajaye ulimwenguni.

15  Kisha YESU, HALI AKITAMBUA YA KUWA WALITAKA KUJA KUMSHIKA ILI WAMFANYE MFALME, AKAJITENGA, AKAENDA TENA MLIMANI YEYE PEKE YAKE”.

Hebu jiulize, kwani! Bwana Yesu, hataki au hapendi kuitwa Mfalme??.. Hata hivyo ndicho anachokitengeneza sasa, anatengeneza ufalme wake, na yeye ndiye atakuwa Mfalme wa wafalme. Lakini hapa tunaona anaukataa na kuukimbia ufalme??..Ni kwanini?..Jibu ni rahisi, ni kwasababu yeye hatengenezi wala hatafuti ufalme wa kidunia.

Yohana 18:33  “Basi Pilato akaingia tena ndani ya Praitorio, akamwita Yesu, akamwambia, Je! Wewe ni Mfalme wa Wayahudi?

34  Yesu akamjibu, Wewe wasema hivi kwa nafsi yako, au watu wengine walikuambia habari zangu?

35  Pilato akajibu, Ama! Ni Myahudi mimi! Taifa lako na wakuu wa makuhani ndio waliokuleta kwangu. Umefanya nini?

36  Yesu akajibu, UFALME WANGU SIO WA ULIMWENGU HUU. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi. Lakini ufalme wangu sio wa hapa”

Hiyo ndio sababu aliwakimbia wale makutano waliotaka kumfanya awe mfalme wao… Waliona wakimpata atawasaidia kujenga miji yao, atawasaidia kunyanyua uchumi wa nchi yao, atawasaidia kupata fedha nyingi, atawasaidia kutokomeza umasikini.  Lakini Yesu aliwakimbia… na walimtafuta kwa bidii na walipompata sehemu nyingine aliwaambia maneno yafuatayo..

Yohana 6:24  “Basi mkutano, walipoona ya kuwa Yesu hayuko huko wala wanafunzi wake, waliingia mashuani wenyewe, wakaenda Kapernaumu wakimtafuta Yesu.

25  Hata walipomwona ng’ambo ya bahari, walimwambia, Rabi, wewe umekuja lini hapa?

26  Yesu akawajibu, akasema, AMIN, AMIN, NAWAAMBIENI, NINYI MNANITAFUTA, SI KWA SABABU MLIONA ISHARA, BALI KWA SABABU MLIKULA ILE MIKATE MKASHIBA.

27  Msikitendee kazi chakula chenye kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele; ambacho Mwana wa Adamu atawapa, kwa sababu huyo ndiye aliyetiwa muhuri na Baba, yaani, Mungu”.

Na jitihada zao zote za kumtafuta awe mfalme, hata hakuwa mfalme wao, Yesu aliwaepuka. Kilichowatokea wale ndicho kinachotutokea kanisa la sasa. Biblia inasema…

Waebrania 13:8  “YESU KRISTO NI YEYE YULE, JANA NA LEO NA HATA MILELE.

9  Msichukuliwe na mafundisho ya namna nyingine nyingine, na ya kigeni; maana ni vizuri moyo ufanywe imara kwa neema, wala si kwa vyakula, ambavyo wao waliokwenda navyo hawakupata faida”.

 Ndugu Bwana Yesu hajabadilika kama watu wanavyombadilisha sasa, Ni yeye Yule, jana, na leo na hata milele!!!…maana yake tabia zake ni zile zile hazijabadilika, kama aliwakimbia wale makutano, waliotaka kumfanya mfalme wao, atatukimbia na sisi pia vile vile, kama tukimwendea kwa mtindo ule.

Kama Bwana Yesu atawakana siku ile watu waliotoa pepo kwa jina lake, na huku mioyo yao ipo mbali naye??..si zaidi wewe aliyekupa mali leo na bado ni mlevi?. Hao amewapa uwezo wa kutoa pepo lakini kawakana mwisho wa siku?..jiulize wewe uliyepewa nyumba na gari na tumbo lako kufunguliwa na bado unavaa kidunia, jiulize utasalimika vipi siku ile?, wewe uliyeponywa kimiujiza na bado hutaki kujikana nafsi yako na kumfuata Yesu, utasalimika vipi?, wewe uliyeponywa ugonjwa kimiujiza na bado hutaki kuuacha ulimwengu, jiulize utasalimikaje siku ile?..

Unadhani Bwana kukupa wewe mali, au mtoto, au kukuponya ugonjwa wako uliokuwa sugu, ndio kitu cha kwanza anachokitafuta kwako??..lengo la kukufanyia hayo ni ili tu ugeuke! Utubu na uwe mkamilifu kama yeye na si kwa lengo lingine. Ukitafsiri kwamba Bwana kakuponya ugonjwa wako kwasababu anapendezwa na wewe..fahamu kuwa umepotea!..Ukitafsiri kuwa Bwana kaifanikisha biashara yako kwasababu eti anataka uwe bilionea, fahamu kuwa umepotea!!.. Ameifanikisha hiyo biashara yako kusudi kwamba utubu na umrudie yeye, uwe mkamilifu. Lakini ukidhani kuwa ni kwasababu amependezwa na wewe, na moyoni ukijitumainisha kwamba ni mfalme wako, na Bwana wako, siku ile atakukana, pamoja na kwamba ni yeye ndiye aliyekufanikisha!!

Kama hujampokea Yesu maishani,  mlango wa neema bado upo wazi, ingawa hautakuwa hivyo siku zote. Huu ni wakati wako wa kumpokea Yesu, kwa kumwamini moyoni mwako, na kukiri kwa kinywa chako, na kuamua kwa dhati kuacha dhambi zote ulizokuwa unazifanya.. Unaziacha kwa vitendo, kama ulikuwa ni mlevi unavunja vikao na makundi yote ya ulevi, kama ulikuwa ni kahaba, unachoma nguo zote za kikahaba ulizokuwa unavaa ikiwemo suruali zote, na lipstick, wanja na mengineyo, kama ulikuwa unasikiliza miziki ya kidunia unaifuta yote katika simu yako, au popote pale ulipoihifadhi, kama ulikuwa ni shabiki wa mambo ya kidunia kama mipira, filamu, na mambo yanayofanana na hayo, unayaacha yote.

Na baada ya kufanya hivyo unatafuta ubatizo sahihi, kama bado hujabatizwa, kumbuka ubatizo sahihi ni ule wa maji tele, na kwa jina la Yesu Kristo, na baada ya hapo Bwana atakupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu, ambaye atakuongoza katika kuijua kweli yote ya maandiko, na kukusaidia kuushinda ulimwengu.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp


Mada Nyinginezo:

Rudi nyumbani

Print this post

Je! tunapaswa kukiamini Kitabu cha Henoko?

SWALI: Kitabu cha Henoko ndio kitabu kipi hicho, Je! Sisi kama wakristo tunapaswa kukiamini?


JIBU: Kitabu cha Henoko ni moja ya vitabu vya Apokrifa ambavyo viliandika kati ya miaka 200 kabla ya Kristo(KK), na  miaka 400 baada ya Kristo(WK). Vitabu hivi  vinaaminiwa na baadhi ya wakristo kuwa  vilihifadhiwa kwa siri, kutokana na kuwa vilikuwa na siri za ndani sana kuhusu Mungu na historia ya ulimwengu kwa ujumla, kiasi kwamba havikuweza kujumuishwa moja kwa moja kwenye biblia yenye vitabu 66 ambayo tunayo hivi sasa.

Lakini si kweli, vitabu hivi havikujumuishwa katika biblia takatifu kwasababu vilikuwa na siri za Mungu hapana badala yake vilionekana kujaa habari nyingi za kutungwa, ambazo zinakinzana na misingi ya imani ya Kikristo.

Sasa tukirudi katika hichi kitabu cha Henoko, kiligunduliwa kwenye miaka ya 1700 huko Ethiopia, baadaye kikasafirishwa mpaka Uingereza kwa ajili ya kutafsiriwa katika lugha nyingine, Kitabu hichi kilijulikana kama Henoko wa  Kwanza (1Henoko), kwasababu kulikuja kuwa pia na matoleo mengine yaliyofuata baadaye.

Vipande vya nyaraka vya kitabu hichi pia viligunduliwa huko Israeli mnao mwaka 1947, kwenye mapango yalikuwa katika fukwe za bahari ya chumvi (dead sea), Na kwenye mapango hayo kulionekana pia machapishi ya vitabu vyote vya agano la kale isipokuwa tu kitabu cha Esta, inasadikika ni vitabu ambavyo vilikuwa vimehifadhiwa huko na watu wa kale ambao waliishi kabla hata ya Kristo kuja duniani.

Sasa kitabu hiki kinamueleza Henoko ambaye alikuwa ni mtu wa saba kutoka Adamu kama tunavyosoma katika biblia Mwanzo 5:18-24…Henoko hakuonja mauti kama ilivyokuwa kwa wanadamu wengine, bali alinyakuliwa kama Eliya. Hiyo imekuwa ikawafanya watu wengi waamini kuwa mtu huyu alipewa siri nyingi za rohoni na kuziandika kwa ajili ya watu wa baadaye.

Hivyo kitabu hichi kilipogunduliwa, kilidhaniwa  kuwa mwandishi wake  ni Henoko, japo hilo jambo halikuthibitika kuwa ni kweli. Kitabu hichi kimejaa historia zinaeleza visa vya dunia ya kwanza kugharikishwa na maji, kinasema baadhi malaika wa Mungu  ambao walikuwa ni waangalizi wa huku ulimwenguni, ambao idadi yao ilikuwa ni 200 waliwaona binti za wanadamu, kisha wakawatamani, , hivyo wakashauriana washuke duniani wajitwalie wake, waishi nao, na kweli wakafanya hivyo  wakashuka duniani wakawapa mimba wanawake, ndio wakazaa wale majitu ambayo tunayasoma katika Mwanzo 6

Zaidi ya yote, malaika hawa kwa kuwa walikuwa na ujuzi, wakawafundisha wanadamu, kubuni silaha za chuma, kufanya uharibifu, wengine wakawafundisha wanadamu kufanya uchawi, na wengine kusoma nyota za mbinguni. Pamoja na hayo watoto wao waliowazaa wakawa wakatili kupita kiasi, ndio wale wanefili, wakawa wanaharibu kila kitu ikiwemo mimea, wanyama, mpaka wanadamu. Urefu wa majitu hayo ulikuwa ni futi 4500, sawa na Jengo la ghorofa 415. Jambo ambalo ni ngumu kusadikika,  Hakuna kiumbe cha namna hiyo kinaweza kuzaliwa na mwanamke. Japo wanefili kweli walikuwa ni wakubwa lakini sio kwa kiwango hicho.

Baadaye baadhi ya malaika wa mbinguni wakampelekea Mungu habari zao,  lakini Mungu akakataa kuwasamehe, akawafunga katika vifungo vya giza, ndio hapo Mungu akamwambia Henoko kuwa atakwenda kuiangamiza dunia kwa gharika.  Hii ndio habari ambayo inafahamika sana

Zipo habari nyingine katika kitabu hicho ambazo kiuhalisia hazina uhalisia wowote  na maandiko.

Tunapaswa tujue vitabu hivi vimejaa hadithi nyingi za kutungwa, ambazo ni sumu kwa Mkristo, na ndio maana huwezi kuziona vikijumuishwa katika biblia yenye vitabu 66 vilivyovuviwa na Roho Mtakatifu, kwasababu vinakinzana na misingi ya kweli ya maandiko.

Bwana Yesu alisema..

Mathayo 22:29 “Yesu akajibu, akawaambia, Mwapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu.

30 Kwa maana katika kiyama hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika mbinguni”.

Unaona? Hakuna andiko lolote linaloonyesha kuwa malaika wanaoa, au wanazaliana, malaika hawakuumbiwa viungo vya uzazi kama tulivyonavyo sisi, hawahitaji kuzaliana, wao tayari walishaumbwa, ndivyo walivyo na idadi yao tayari ipo kamili, Lakini kusema walishuka duniani, ni fundisho la uongo ambalo wakristo wengi wanaliamini mpaka leo, na chanzo chake walikitoa katika hichi kitabu cha Henoko.

Waliowaona binti za wanadamu wakawatamani, walikuwa ni watakatifu wa Mungu, ambao hao hawakujichanganya na mambo ya ulimwengu tangu mwanzo, bali walitumia sehemu kubwa ya maisha yao, kuliita jina la Bwana na kumwabudu Mungu soma Mwanzo 4:26 utalithibitisha hilo ndio ule  uzao wote wa Sethi (Wakina Henoko, Methusela, Na Nuhu).. Lakini binti za wanadamu walikuwa ni watu wa kidunia tu, ambao walitokea katika ule uzao wa Kaini..hao ndio tangu mwanzo walikuwa na ujuzi mkubwa, na hodari na pia wakatili ukisoma pale Mwanzo 4:16-23 utaona ni jinsi gani, uzao wa Kaini ulivyokuwa hodari, wenye ujuzi mwingine, lakini pia mwovu kwa uuaji, kama Baba yao alivyokuwa.

Baadaye sasa walipojichanganya mbegu ndipo Mungu akakasirika, akaghahiri na kuuangamiza ulimwengu wote, ni sawa na leo hii, Mungu aone, watakatifu wake wote, wanaiga na kufanya mambo ya ulimwengu, wanawake wanavaa vimini, wanatembea nusu uchi barabarani, wanaume watakatifu wanakuwa mashoga n.k. kiasi kwamba huwezi kuona tofauti yoyote kati yao na ulimwenguni, hapo kinachofuata ni Mungu kuuteketeza ulimwengu, ndivyo ilivyokuwa kwa watu wa kipindi kile. Watakatifu walijitofautisha kabisa na wana wa ulimwengu..

Hivyo hakuna sababu ya mkristo kuamini, moja kwa moja vyanzo ambavyo havipo katika biblia, kwasababu vingi kati ya hivyo vinakasoro nyingi na vimejaa hadithi nyingi zilizotungwa na wanadamu lakini sio kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu.

Kwamfano kwasasa Kanisa Katoliki, limeamua kuchukua baadhi ya hivi vitabu vya Apokrifa na kuviongezea kwenye biblia takatifu yenye vitabu 66, kufikia 73. Vitabu vyenyewe ikiwemo Yudithi, Baruku, Yoshua bin Sira, Wamakabayo 1&2,  Hekima.

Vitabu hivi vinakinzana na misingi ya imani, kwamfano, vinafundisha kwenda toharani, yaani mtu mwenye dhambi anaweza kwenda mbinguni tena, lakini baada ya kupitishwa mahali panapoitwa toharani ili kutakaswa,.,Fundisho lingine ni kuwa Mungu, anasikia maombi ya wafu, mambo ambayo ni uongo, biblia inasema, mtu ameandikiwa kuishi mara moja na baada ya kifo ni hukumu (Waebrania 9:27).

Kwahiyo, vitabu vya Aprokifa, sio vya kuviamini, kama uaminivyo biblia, iwe ni kitabu cha Henoko, au kingine chochote kile nje ya vitabu 66 vya biblia sio vya kuiamini vinamakosa mengi na wakati mwingine vimejaa uongo mwingi, ambao unapotosha kabisa.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Kitabu cha YASHARI kinachozungumziwa katika 2Samweli 1:17-18, ni kitabu gani?

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 1

Chuo cha vita vya Bwana ni kipi?(Hesabu 21:14)

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 7 (Yeremia na Maombolezo)

UNYAKUO.

CHUKIZO LA UHARIBIFU

Rudi nyumbani

Print this post

Je Mungu aliumba watu wengine kabla ya Adamu?

SWALI: Je Mungu aliumba watu wengine kabla ya Adamu?, maana tunasoma katika Mwanzo 1:27, alimwumba mwanamke na mwanamke, na tena tunaona anaumba tena mtu mwingine (Adamu) katika Mwanzo 2:7.


Jibu: Kitabu cha Mwanzo Mlango wa Kwanza kimezungumzia uumbaji wa Mungu kwa muhtasari  (yaani kwa ufupi), lakini tunapokwenda katika Mlango wa pili, ndio tunaona uumbaji ukielezewa kwa urefu zaidi. Kwahiyo mlango wa kwanza ni muhtasari wa uumbaji, ndio maana utaona vitu vinaelezewa kwa ufupi tu…Kwamfano utaona Mungu anasema..

Mwanzo 1:11 “Mungu akasema, Nchi na itoe majani, mche utoao mbegu, na mti wa matunda uzaao matunda kwa jinsi yake, ambao mbegu zake zimo ndani yake, juu ya nchi; ikawa hivyo

12 Nchi ikatoa majani, mche utoao mbegu kwa jinsi yake, na mti uzaao matunda, ambao mbegu zake zimo ndani yake, kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema,

13 Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya tatu.”

Hapo, uumbaji wa miti na mimea umeelezewa kwa kifupi sana, haijaelezwa ilitokeaje tokeaje… sasa ili tujue kwa undani zaidi, hiyo miti ilitokeaje tokeaje, ndipo tunakwenda katika mlango wa 2 wa kitabu hicho hicho cha mwanzo, tunaona ikielezewa vizuri zaidi..

Mwanzo 2:4 “Hivyo ndivyo vizazi vya mbingu na nchi zilipoumbwa. Siku ile Bwana Mungu alipoziumba mbingu na nchi

5 hapakuwa na mche wa kondeni bado, wala mboga ya kondeni haijachipuka bado, kwa maana Bwana Mungu hajainyeshea nchi mvua, wala hapana mtu wa kuilima ardhi;

6 ukungu ukapanda katika nchi, ukatia maji juu ya uso wote wa ardhi”

Unaona?..Kumbe Mungu aliposema nchi itoe majani na mche utoao mbegu, siku ile ile aliinyeshea nchi mvua na ndipo nchi ikazaa miti na mimea kadha wa kadha… Maana yake hakusema tu itokee halafu ikatokea kama tulivyosoma hapo katika hiyo Mwanzo 1:11, bali kulikuwa na hatua (process). Ambazo ndizo tulizokuja kuzisoma katika hiyo Mwanzo mlango wa pili.

Kadhalika Mungu aliposema katika Mwanzo 1:27 kwamba… “Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba”.

Tunaona hapo uumbaji wa mtu umeelezwa kwa ufupi tu, haijaeleza ni jinsi gani huyo mtu alivyoumbwa, mwanaume na mwanamke walitokeaje tokeaji …je! Wote waliumbwa pamoja?..na je waliumbwa kwa malighafi gani?. Sasa majibu ya maswali hayo ndio tunayapata katika Mlango wa pili wa kitabu hicho hicho.. tusome,

Mwanzo 2:4 “Hivyo ndivyo vizazi vya mbingu na nchi zilipoumbwa. Siku ile Bwana Mungu alipoziumba mbingu na nchi

 5 hapakuwa na mche wa kondeni bado, wala mboga ya kondeni haijachipuka bado, kwa maana Bwana Mungu hajainyeshea nchi mvua, wala hapana mtu wa kuilima ardhi;

 6 ukungu ukapanda katika nchi, ukatia maji juu ya uso wote wa ardhi.

7 BWANA MUNGU AKAMFANYA MTU KWA MAVUMBI YA ARDHI, AKAMPULIZIA PUANI PUMZI YA UHAI; MTU AKAWA NAFSI HAI.

 8 Bwana Mungu akapanda bustani upande wa mashariki wa Edeni, akamweka ndani yake huyo mtu aliyemfanya”.

Umeona hapo, biblia inasema Bwana Mungu akamfanya mtu kutoka kwenye mavumbi ya ardhi, jambo ambalo halikutajwa katika ile Mwanzo 1:27, na ukiendelea kusoma katika Mwanzo 2:18-24, utaona jinsi uumbaji wa mwanamke ulivyokuwa, kwamba alitwaliwa kutoka kwa mwanaume (ubavuni mwa mwanaume), jambo ambalo halikuelezwa katika ile Mwanzo 1:27.

Kwahiyo kitabu cha Mwanzo mlango wa kwanza ni muhtasari tu wa uumbaji, umeelezea kwa ufupi sana, na mlango wa pili ndio umeelezea kwa undani kidogo. Ni sawa na unaposoma kitabu Fulani labda cha jeografia, unapokifungua mwanzo kabisa utakutana na “yaliyomo”/“table of content”. Lengo la lile ni kukupa muhtasari na kukuongoza utakachokwenda kukisoma.. Na utaona kila kichwa kimeelezea kwa ufupi sana, lakini utakapokwenda katika kurasa zenyewe utaona mada zimeelezewa kwa urefu sana. Ndicho kilichopo katika kitabu cha Mwanzo mlango wa Kwanza..na wa pili..

Hivyo si kweli kwamba kuna watu wengine waliumbwa kabla ya Adamu. Adamu na Hawa ndio wanadamu wa kwanza kuumbwa.. Na walipoasi waliondolewa katika ile bustani ya Mungu Edeni, na kuanzia huo wakati, wote tunaozaliwa tunakuwa tunalibeba anguko lake. Mpaka tutakapozaliwa mara ya pili katika uzao wa Adamu wa pili Yesu Kristo, ambaye yeye hakutenda dhambi hata mara moja, ambaye alijaribiwa kama Adamu lakini hakutenda dhambi, huyo pekee ndiye amewekwa kuwa ukombozi kwetu.

Kila amwaminiye maandiko yanasema atapata ondoleo la dhambi zake, naye atakuwa haishi chini ya laana bali chini ya Baraka, lakini wote wasiomwamini hawatapata ondoleo la dhambi zao, na siku ya mwisho watatupwa katika ziwa lile la moto, aliloandaliwa shetani na malaika zake.

Je wewe ni mmoja wa waliomwamini au ambao hawajamwamini?.. Kama bado tambua kuwa upo chini ya laana ya anguko la Adamu, na hakuna namna yoyote unaweza kuhesabiwa haki bila kumpokea Yesu maishani mwako, haijalishi utafanya mangapi mazuri, kama humtaki Yesu hutamwona Mungu, kwasababu yeye ndiye Njia ya kufika mbinguni, wala hakuna mwingine.

Hivyo mpokee leo kwa kutubu dhambi zako zote, na kwa kudhamiria kuziacha kabisa na baada ya toba yako hiyo, nenda katafute ubatizo sahihi, kumbuka ubatizo sahihi ni ule wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo ambalo ndio jina la Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Kwa kukamilisha hatua hizo tatu, yaani Imani, ubatizo na kupokea Ujazo wa Roho Mtakatifu, utakuwa umeukamilisha wokovu wako na Roho Mtakatifu atakuongoza katika kuijua kweli yote na kukupa nguvu za kuishinda dhambi.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Je! Adamu alikuwa na mwanamke mwingine anayeitwa Lilith?

MWANZO WA INJILI YA YESU KRISTO.

Majina mbalimbali ya Mungu na maana zake.

VAZI KUU AMBALO MUNGU AMETUANDALIA KILA MMOJA WETU.

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 1

Rudi nyumbani

Print this post

“Yodi” ni nini kama tunavyoisoma katika Mathayo 5:18?

Jibu: Tusome,

Mathayo 5:18 “Kwa maana, amin, nawaambia ,Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka,yodi moja wala nukta moja ya torati haitaoondoka ,hata yote yatimie”.

Yodi ni neno lililotumika katika lugha ya Kiswahili cha zamani, lenye maana ya “herufi ndogo”.. kwa lugha ya kiingereza ni “small letter”. Katika sentensi yoyote huwa kunakuwa na herufi kubwa na herufi ndogo, sasa zile ndogo ndio zinazoitwa “yodi”.. Mfano tunaposema neno “Yesu ni Mungu”..Herufi kubwa hapo ni hiyo “Y” na “M” lakini hizo nyingine zote zilizosalia kama “e” “s” “u” “n” “i”  “u” ni YODI.

Kwahiyo Bwana Yesu aliposema kwamba hakuna hata “yodi” moja wala nukta itakayoondolewa hata yote yatimie maana yake.. ni kwamba hakuna herufi yoyote (hata ile iliyo ndogo kuliko zote, ‘yodi’) itakayobadilishwa katika maneno ya torati, kwasababu maneno ya Mungu hayabadilii. Ndio maana ukianzia juu kidogo utaona anasema hakuja kuitangua torati bali kuitimiliza..

Mathayo 5:17 “Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza.

18 Kwa maana, amin, nawaambia ,Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaoondoka ,hata yote yatimie”.

Mathayo 24:35 “Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe”.

Pale torati iliposema “usizini”..Bwana Yesu hakuja kulibadilisha hilo andiko, bali alikuja kulitimiliza kwa kusema “mtu amtazamaye mwanamke amekwisha kuzini naye nafsini mwake”. Hapo hajaondoa chochote, bali ameongezea dawa. Torati inaposema “usiue” Bwana Yesu alisema “amwoneaye ndugu yake hasira hana tofauti na muuaji, hivyo itampasa hukumu tu kama muuaji”. Hapo hajaitangua wala kulibadilisha bali ameitimiliza, na sheria nyingine zote za kwenye torati ni hivyo hivyo..

Je wewe bado una chuki kwa ndugu zako au maadui zako?,ukijitumainisha kwamba wewe si muuaji?.. bado unatamani ukijitumainisha kwamba wewe sio mzinzi??, bado unavaa nusu uchi,na suruali ukijitumainisha kwamba wewe si kahaba?? (kasome Mithali 7:10 ujipime kama wewe ni kahaba au la kwa mavazi yako), bado unajichua na kunatazama pornography ukijitumainisha kwamba wewe si mwasherati?, bado ni mshabiki wa mambo ya kidunia kuliko kitu kingine chochote ukijitumainisha kwamba wewe si wa kidunia??.

Kama unafanya mojawapo ya hayo, au yote, wakati wa kumkaribisha Mwokozi ndani ya maisha yako ni huu?..Usingoje kesho wala baadaye, saa ya wokovu ni sasa, na wakati uliokubaliwa ndio huu.. wakati wa kukimbilia Kalvari, Bwana akuokoe na kukutua mzigo ndio huu, sio kesho, kwasababu hujui kesho yako itakuwaje, labda leo ndio mwisho wako wa kuishi duniani, au leo ndio siku parapanda ya mwisho itakapolia, jiulize, unyakuo leo ukipita utakuwa wapi??.. Hivyo fanya uamuzi wa kumgeukia Yesu leo kwa kutubu dhambi zako zote kwake, na kwenda kubatizwa katika ubatizo wake wa maji tele (Yohana 3:23), na kwa jina la Yesu Kristo (Matendo 2:38), na Bwana atakupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu, atakayekuongoza katika kweli yote ya maandiko.

Maran atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Kwanini Yesu aliwakataza mitume wake kumdhihirisha?

Mount Gerizim and Mount Ebal: Their Meaning and Spiritual Significance

Amri zilizo ndogo alizozizungumzia Yesu ni zipi?

RUDI KUMPA MUNGU UTUKUFU.

IFAHAMU HUZUNI NA FURAHA YA MALAIKA.

Rudi nyumbani

Print this post

Kwa kuwa ni shida mtu kufa kwa ajili ya mtu mwenye haki;

SWALI: Warumi 5:7 “Kwa kuwa ni shida mtu kufa kwa ajili ya mtu mwenye haki; lakini yawezekana mtu kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu aliye mwema”.

Bwana Yesu asifiwe mtumishi wa Mungu, Naomba ufafanuzi wa hilo andiko na pia nipate  kujua tofauti kati ya mtu mwenye haki na mtu mwema.


JIBU: Pamoja na kwamba Bwana Yesu kuja hapa duniani kuwaokoa watu waliopotea kabisa, (yaani watu wenye dhambi wasio na vimelea vyovyote wa utu, kama vile wauaji, wahalifu, mafisadi n.k.) alikuja pia kuwaokoa watu walio wema.

Sasa tukirudi kwenye mstari huo tunaona mwandishi anajaribu kutofautisha  kati ya mtu mwema na mtu mwenye haki.

Mtu mwenye haki ni yupi?

Mtu mwenye haki ni mtu mkamilifu sana, asiyekuwa na kosa lolote mbele za Mungu, Mtu wa namna hii kiuhalisia hajawahi kuwepo tangu duniani iumbwe. Kama wangekuwepo hakukuwa na sababu ya Yesu Kristo kushuka hapa duniani, na kufa kwa ajili yao, wapate wokovu, ya nini sasa? Wakati tayari wanaoukamilifu wote ndani yao..hakuna doa lolote ndani yao?

Na ndio maana hapo inasema.. ni shida mtu kufa kwa ajili ya mtu mwenye haki..

Lakini mtu mwema, ni mtu ambaye sio mwovu sana, ni mtu ambaye anajaribu kuishi maisha ya kawaida tu katika jamii, anajiheshimu, anawasaidia wengine, anao utu, anajitahidi kutenda mema kwa bidii na kufanya mambo yake kwa utulivu bila kuvunja sheria yoyote ya jamii husika au nchi n.k. Lakini katika jitihada zake zote, bado hajaweza kufikia kipimo cha yeye kuwa mtu mwenye haki mbele za Mungu..Yaani nguvu zake bado hazijajitosheleza kumfanya awe mkamilifu..hao ndio watu wema mwandishi anaowazungumzia hapo. Na ndio maana ukianzia mstari wa juu anasema;

Warumi 5:6 “Kwa maana HAPO TULIPOKUWA HATUNA NGUVU, wakati ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili ya waovu.

7 Kwa kuwa ni shida mtu kufa kwa ajili ya mtu mwenye haki; lakini yawezekana mtu kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu aliye mwema”.

Unaona anasema “hapo tulipokuwa hatuna nguvu”, ikiwa na maana tulishajaribu kujitahidi kwa nguvu zetu na kwa matendo yetu kumpendeza Mungu lakini bado tukashindwa kuufikia ule ukamilifu…Na  ndio Kristo alikuja kutufia pale msalabani, ili sasa kwa kumwamini tu yeye, tuhesabiwe haki mbele za Mungu.

Hivyo kwa kuhitimisha ni kuwa, kama tungekuwa wenye haki, basi Kristo asingekuja duniani, lakini kwasababu sote tumepungukiwa na utukufu wa Mungu,  (nikiwa na maana watu waovu sana na wa kawaida), Sote tunamuhitaji Kristo ayabadilishe maisha yetu. Kwasababu pasipo yeye, haijalishi tuna dini nzuri kiasi gani, tunafanya mazuri kiasi gani,  tunasaidia maskini wengi kiasi, bado hutuwezi kumpendeza Mungu, bila Kristo. Kwasababu hayo tayari yalishashindikana tangu zamani.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

JE NI KWELI SAMAKI NGUVA YUPO?

USIOMBE MAOMBI YASIYOKUWA NA MAJIBU NA WALA USIMTUKANE MUNGU.

Alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru

ESTA: Mlango wa 4

IFAHAMU HUZUNI NA FURAHA YA MALAIKA.

Rudi nyumbani

Print this post

KOIKOI ANGANI AJUA NYAKATI ZAKE ZILIZOAMRIWA.

Yeremia 8:7 “Naam, koikoi angani ajua nyakati zake zilizoamriwa; na hua na mbayuwayu na korongo huangalia wakati wa kuja kwao; bali watu wangu hawazijui amri za Bwana”.

Koikoi, mbayuwayu na korongo ni ndege wa ajabu sana, ni ndege wenye uwezo wa kusoma majira ya dunia, Na hiyo imewasaidia sana, kuishi maisha ya salama salmini huku duniani, pasipo kukumbana na changamoto zozote  zisizo na maana.

Hawa ni ndege ambao kikikaribia kipindi cha baridi wanahama wote maeneo yao wanayoishi kwa muda, na kusafiri umbali mrefu sana, kwenye pembe ya pili ya dunia kutafuta msimu tulivu aidha wa vuli au  wa joto ulipo wakatulie, kisha baadaye hali ya baridi ikishakwisha wanarudi katika makazi yao ya awali kuendelea na maisha yao ya kawaida.

Kumbuka baridi tunayoizungumzia ni ile baridi haswaa, ya kutengeneza barafu iliyopo huko nchi za ulaya, ambayo hata mtu wa kawaida akikaa nje masaa machache tu anageuka kuwa jiwe la barafu, haijalishi atavaa masweta makubwa kiasi gani.. Baridi ya namna hiyo watu wanaoishi huko wanatumia muda wao mwingi kuwepo ndani, na hata kazi zao wanazifanyia ndani katika nyumba zilizojengwa kitaalamu kuhifadhi joto ndani, kwani nyumba za kawaida kama hizi zetu, kule hazijengwi kwasababu zinapitisha baridi, kiasi kwamba ukibaki ndani yake, ukakaa huko mpaka asubuhi ukiamka umeganda. Huku kwetu Afrika hatuna baridi ya namna hiyo.

Sasa, ndege hawa, wanaelewa kabisa kwa namna ya kawaida hawawezi kuishi katika mazingira hayo ya baridi kali, kwasababu hata viota vyao vitaganda.. Sasa ili kulitatua hilo tatizo inawagharimu wahame kwa muda, ndio hapo wanasafiri maelfu ya kilometa wanakuja mpaka huku kwetu Afrika, au nchi nyingine zenye joto, wanakaa  huko mpaka msimu wa baridi  utakapokwisha kule Ulaya ndio wanarudi sasa, kuendeleza maisha yao ya sikuzote.

Sasa Mungu ametumia mfano wa ndege hawa wasio na akili, kutushangaa sisi wanadamu wenye akili timamu kwanini hatujui hukumu zake alizoziweka hapa duniani..anasema..

“Naam, koikoi angani ajua nyakati zake zilizoamriwa; na hua na mbayuwayu na korongo huangalia wakati wa kuja kwao; bali watu wangu hawazijui amri za Bwana”

Hii ikiwa na maana tunashindwa kujua wakati wa neema ni upi, na wakati wa hukumu za Mungu ni upi.. Sisi tupo tu hatujui majira yetu, tunadhani wakati wote, hii neema ya wokovu itaendelea kuwepo, tunadhani wakati wote, hali itakuwa kama ilivyo sasa hivi, utahubiriwa injili kama unavyohubiriwa sasa hivi..

Ndugu yangu, fahamu kuwa neema hii inakwenda kuisha siku sio nyingi, Dhiki kubwa ambayo haijawahi kutokea tangu dunia iumbwe na wala haitakaa iwepo itakwenda kutokea ulimwenguni kote..Dalili zote zinaonyesha, pengine katika wakati wetu huu tunaoishi tutayashuhudia hayo..Haya majira ya neema ndio yanaishia hivyo, muda huu tulionao ni wa nyongeza tu, dunia ingepaswa iwe imeshakwisha tangu zamani, lakini kwasababu tu ile nuru ndogo ya jioni ipo ndio maana unaona mambo bado yapo hivi..

Tumeshafikia wakati ambao Yesu hatuhubirii  tena injili ya kutuvuta kwenye wokovu, kama ilivyokuwa zamani bali anatuhubiria injili ya kuthibitisha ulichokiamini. Sikiliza anavyosema..

Ufunuo 22:10 “Akaniambia, Usiyatie muhuri maneno ya unabii wa kitabu hiki, kwa maana wakati huo umekaribia.

11 Mwenye kudhulumu na azidi kudhulumu; na mwenye uchafu na azidi kuwa mchafu; na mwenye haki na azidi kufanya haki; na mtakatifu na azidi kutakaswa.

12 Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo”.

Unaona, hiyo yote ni kwasababu ya unafki tulionao sasa, kwasababu kama tunaweza kuyatambua majira ya nchi, kwamba huu ni msimu wa masika na hivyo tunaanza kuyaandaa mashamba yetu kabla ya mvua kunyesha, au tunahama mabondeni mapema mafuriko yasitukute, inakuwaje basi, tunashindwa kuzitambua siku hizi kuwa ni siku za mwisho? Korona inakufundisha nini? Vimbunga vinakufundisha nini, Hili wimbi la manabii wa uongo unaloliona leo hii limezuka duniani kwa ghafla linakufundisha nini? . Bado tu huoni, hizo ni dalili za wazi kabisa ambazo zinatutambulisha kuwa tukio la unyakuo lipo karibu?

Yesu alisema..

Luka 12:54 “Akawaambia makutano pia, Kila mwonapo wingu likizuka pande za magharibi mara husema, Mvua inakuja; ikawa hivyo.

55 Na kila ivumapo kaskazi, husema, Kutakuwa na joto; na ndivyo ilivyo.

56 Enyi wanafiki, mwajua kuutambua uso wa nchi na mbingu; imekuwaje, basi, kuwa hamjui kutambua majira haya”?

Itakuwa ni ajabu sana tukishindwa akili na akina koikoi. Tujitathimini sana, tuamke katika usingizi huu mzito, hukumu ya Mungu juu ya ulimwengu wote ipo karibu. Kama upo nje ya safina, anza safari upesi, mkimbilie Kristo kwa kumaanisha kabisa kwa moyo wako wote akuokoe, kwasababu hatuna muda mrefu hapa duniani,

mbingu na nchi zitapita lakini maneno ya Bwana Yesu hayatapita milele.

Mbingu ipo, lakini pia kuzimu ipo, uchaguzi ni wa wako,

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

UNYAKUO.

DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.

WAENDEE WANA WA ISAKARI, UWE SALAMA.

KWASABABU MUDA TULIOBAKIWA NAO SI MWINGI.

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 9 (Kitabu cha Ayubu).

Rudi nyumbani

Print this post

Nini tofauti kati ya moyo na roho?

Moyo ni neno ambalo linaweza kuwakilisha aidha nafsi ya mtu au roho ya mtu, inategemea na linapotumika.

Kwa kawaida hakuna lugha ya kuielezea nafsi ya mtu jinsi ilivyo, au roho ya Mtu jinsi ilivyo, kwamba inafananaje, au iko namna gani, hivyo lugha nyepesi ambayo inaweza kuwakilisha vitu hivyo viwili (yaani Roho na Nafsi) ni Moyo.

Kama vile tunavyokosa lugha ya kuzielezea nguvu za Mungu zikoje zikoje, au uweza wake ukoje ukoje, una  rangi gani, una mwonekano gani, au unafanyaje kazi, hivyo tunaishia tu kusema “mkono wa Mungu umefanya hichi au kile”… tukimaanisha kwamba Nguvu za Mungu zimetenda hayo au uweza wa Mungu umefanya hayo. Hapo tumetumia kiungo cha mwili kuwakilisha kitu Fulani cha rohoni kisichoonekana. Na lengo la kufanya hivyo ni ile kitu kile kiweze kueleweka zaidi na kuleta maana.

Ingawa si wakati wote tutaziwakilisha nguvu za Mungu kwa “mkono wake” lakini pia tukitumia “mkono wa Mungu ” kuwakilisha “nguvu za Mungu” tutakuwa hatujakosea.

Na ni kwanini tunatumia  kiungo mkono na si mguu??… Kwasababu mkono ndio unaofanya mambo yote, mkono ndio unaotumika kutia sahihi ya jambo Fulani liwe baya au zuri.. Hivyo mkono siku zote unawakilisha mamlaka ya Mtu au nguvu zake.

Kadhalika ili ipatikane  lugha rahisi ya kuwakilisha roho ya mwanadamu au nafsi yake, ambayo haionekani kwa macho, ndipo lilipotumika neno “moyo” kama mbadala, Kwamfano badala ya kusema “Nina huzuni nyingi rohoni” unaweza kusema “nina huzuni nyingi moyoni”. Au badala ya kusema “nafsi yangu ina huzuni” unaweza kusema “moyo wangu una huzuni” ni kitu kile kile.

Sasa kwanini kitumike kiungo moyo na si kiungo kingine kama figo:

Kama tunavyojua kiungo pekee kinachoendesha na kuzungusha damu katika miili yetu ni moyo. Na ndio  kiungo pekee ambacho ni chepesi kuitikia mabadiliko yoyote ya hisia za mwili. Utaona likitokea jambo la kushtusha ghafla, mapigo ya moyo yataanza kwenda kasi!..pakitokea hali ya utulivu sana, mapigo ya moyo yanashuka.. Ni ngumu mtu ashtushwe halafu asikie maini, au figo zinabadilika tabia.. Moyo ni kama vile mtu mwingine wa pili, anaishi ndani ya mwili.

Hivyo tabia hiyo ya kipekee ya kiungo hicho ambacho kipo ndani ya mwili lakini kina uwezo wa kuitikia na kuelewa mambo yanayoendelea nje ya mwili, na zaidi ya yote ndicho kinachozungusha uhai ndani ya mwili, imekifanya kifananishwe na roho au nafsi ya mtu.

Kwahiyo popote pale katika maandiko neno hilo “moyo” linapotumika.. basi fahamu kuwa linawakilisha aidha “nafsi ” au “roho”. Kujua tofauti iliyopo kati ya nafsi na roho unaweza kufungua hapa >> Tofauti ya Nafsi, mwili na roho

Je umempokea Yesu?. Je umempenda Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa nguvu zako zote? Au unautumikia ulimwengu na fahari zake?..Kumbuka biblia inasema..

Mathayo 6:21 “kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako”.

Moyo wako upo wapi leo? Kama upo kwa Bwana ni vyema..lakini kama upo katika ulimwengu na fahari zake, kumbuka maandiko yanasema…

Yakobo 4:4 “Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa Mungu”

Ndugu kitendo cha kuipenda dunia tu tayari wewe ni adui wa Mungu, haihitaji useme kwamba wewe ni adui wa Mungu, hapana! Kitendo cha wewe kupenda fasheni tu, kitendo cha wewe kupenda kuvaa nusu uchi, kitendo cha wewe kuwa mshabiki wa mipira, kitendo cha wewe kupenda kutazama tamthilia na filamu za kidunia, tayari umejifanya kuwa adui wa Mungu. Na maadui wa Mungu wote! Sehemu yao itakuwa ni lile ziwa la Moto..(Luka 19:27).

Kama utapenda kumpokea leo Yesu, mlango wa neema upo wazi, ila hautakuwa hivyo siku zote..ipo siku utafungwa, tukiwa hapa hapa duniani, utafungwa kwa tendo linalojulikana kama unyakuo. Baada ya unyakuo kupita, kitakachokuwa kimebakia duniani ni dhiki kuu tu!, na baada ya hapo ni mapigo ya vitasa saba kama tunavyosoma katika Ufunuo 16. Duniani patakuwa si mahali salama kabisa. Hivyo kama upo tayari kumpokea Yesu maishani mwako leo, hapo ulipo jitenge kwa dakika chache tafuta sehemu ya utulivu kisha Ungama dhambi zako kwa kumaanisha kukiri makosa yako na kuyaacha. Baada ya hapo, acha vyote kwa vitendo ulivyokuwa unavifanya… Acha udunia wote!! Na hatua ya  mwisho tafuta ubatizo sahihi kukamilisha wokovu wako, Ubatizo sahihi ni wa kuzamishwa kwenye maji mengi na kwa jina la Yesu, kulingana na maandiko (Matendo 2:38)

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

SHETANI ANAPOKUINGIA, ANATIA MOYO MGENI NDANI YAKO.

JINSI YA KUEPUKA KUUMIZWA MOYO KUSIKOKUWA NA SABABU.

IFAHAMU HUZUNI NA FURAHA YA MALAIKA.

nini maana ya kujikana nafsi na kujitwika msalaba?

NGUVU ZA ZAMANI ZIJAZO:

Rudi nyumbani

Print this post

AKAZIDI KUENDELEA KATIKA HEKIMA NA KIMO.

Shalom, karibu tujifunze maneno ya uzima.

Wengi wetu tunadhani Bwana Yesu alizaliwa akiwa na ufahamu kamili wa kila kitu, au ujuzi wa mambo yote, Hapana alizaliwa akiwa kama sisi kabisa, hajui kitu chochote, japo alikuwa ni Mungu kweli katika mwili.

Ilipasa iwe hivyo, ili kutimiza kusudi la Mungu, la kumfananisha na sisi  katika mambo yote ili  awe kielelezo cha sisi kuifuata njia yake. Hivyo kwa kuyatazama tu Maisha ya Bwana Yesu tunaweza kujifunza mambo ambayo hata sisi wenyewe tunaweza kuyafanya.

Mpaka Bwana kufikia hatua ya kufahamu siri nyingi sana za Mungu, halikuwa ni jambo alilozaliwa nalo, hapana, biblia inasema..

“Naye Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu”.

Kuendelea katika hekima na Kimo, maana yake ni kukua kila siku katika hekima ya kumjua Mungu, yaani kutoka kiwango kimoja hadi kingine, hatua moja hadi nyingi.. Na hilo halikuja tu hivi hivi, Bali alikuwa na bidii tangu akiwa mtoto, ya kujifunza maneno ya Mungu, kwa kuwatafuta waalimu ili wamsaidie, Na alipokutana nao alikuwa akiwauliza maswali pale ambapo alikuwa haelewi na kutoa maoni yake pale ambapo alikuwa anapaelewa zaidi,..Jambo hilo unaweza  kulisoma katika…

Luka 3:46 “Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, ameketi katikati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali.

47 Nao wote waliomsikia walistaajabia fahamu zake na majibu yake.

48 Na walipomwona walishangaa, na mama yake akamwambia, Mwanangu, mbona umetutenda hivi? Tazama, baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni.

49 Akawaambia, Kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu?

50 Nao hawakuelewa na neno hilo alilowaambia.

51 Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii; na mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake.

52 Naye Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu”.

Jaribu kutafakari, kijana wa miaka 12 anatumia siku tatu usiku na mchana, kakaa tu kanisani, akijifunza Biblia, na hiyo ni desturi yake ya mara kwa mara.. Unategemea vipi kijana kama huyo akiwa mtu mzima, atakuwa sawa na watu wengine?

Ni lazima tu, atakuwa katika maarifa ya kumjua Mungu kwa kasi, na ndivyo ilivyokuwa kwa Bwana, mambo yote hayakumjia tu ghafla ndani yake, labda kazaliwa nacho, hivyo hakuwa na haja ya kuongeza maarifa au kujifunza hapana.

Leo hii, utaona mkristo, hana habari ya kujifunza Biblia, hata akienda kujifunza haulizi maswali, wachungaji wake, au manabii wake, au waalimu wake,  yeye ni kusikiliza tu na kuondoka, akiambiwa jambo Fulani hata kama ni gheni kwake, atalipokea tu na kusema AMEN! Baba..Basi..

Kwa mtu ambaye ni msomaji wa biblia, ni lazima tu atakutana na mambo mengi sana yasiyoeleweka, Na Mungu ameyaficha hivyo makusudi, ili atujengee tabia ya kupenda kutafuta, na mwisho wa siku ampe majibu.. Lakini kama utasoma tu biblia kwa kujiburudisha, au kutimiza ratiba, ufahamu kuwa huo sio mpango wa Mungu.

Mungu anataka tujifunze biblia sio, tuisome kama gazeti, Biblia ni kitabu cha mafumbo, hakuna namna mkristo akose maswali ya kumuuliza Mungu..hilo haliwezekani..Embu kaa chini usome kitabu chochote kwa kumaanisha halafu uniambie kama ni mambo yote yaliyopo kule umeyaelewa..Hilo halipo..

Lakini Yesu hakuona aibu ya kutaka kujifunza pale ambapo alikuwa haelewi, na alitumia fursa hiyo vizuri kuwafuata waalimu wake wa torati…Vivyo hivyo na wewe kama unataka kukua katika hekima na Kimo katika kumjua Mungu, wafuate wale waliokutangulia katika Imani, yaani wachungaji wako, manabii wako, mitume wako, waalimu wako, waulize maswali kwa yale uliyojifunza katika biblia..ukiona majibu yao hayajakuridhisha..tafuta tena wachungaji wengine, kawaulize, maswali, hivyo hivyo mpaka Roho Mtakatifu atakufunulia jibu sahihi..

Japo Bwana Yesu alikaa chini ya waalimu, lakini mwisho wa siku yeye ndiye aliyekuwa MWALIMU WA WAALIMU… Alikuwa ni RABI, Alijua siri nyingi za ufalme wa mbinguni, kuliko watu wote waliokuwa duniani, sio tu wale walioishi naye, mpaka pia wale waliomtangulia.

Hata wewe ukiwa ni mtu wa kutoridhika na hali ya ufahamu wako kuhusu Mungu, ukaanza kujifunza, uwe na uhakika kuwa upo wakati, utakuwa ni mtu wa viwango vya mbali sana, na Mungu atajifunua kwako kwa namna ambazo wewe mwenyewe utashangaa.

Anza sasa, kumtafuta Mungu wako, kwa bidii kama za Bwana wetu YESU KRISTO.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

HEKIMA YA KIMUNGU, INAINGIAJE MIOYONI MWETU?

KWANINI MIMI?

Tofauti kati ya Hekima, ufahamu na maarifa, ni ipi?

JINSI ROHO MTAKATIFU ANAVYOWAFUNULIA WATU MAANDIKO.

MIUJIZA YA KRISTO, HAITEGEMEI KANUNI ZA KIBINADAMU.

Rudi nyumbani

Print this post