Title 4 August 2019

MTEGEMEE MUNGU, NA SI MWANADAMU.


Yeremia 17:5 “ Bwana asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana. 

6 Maana atakuwa kama fukara nyikani, Hataona yatakapotokea mema; Bali atakaa jangwani palipo ukame, Katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu.”

Jina la Bwana libarikiwe, Biblia inasema amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake, na moyoni mwake amemwacha Bwana.

Matokeo ya kumwacha Mungu moyoni ni kumtegemea mwanadamu, unapoamini kuwa mtu fulani ndio kashikilia hatma ya Maisha yako, huko ni kumtegemea mwanadamu…

Unapoziamini methali za wanadamu na kuliacha Neno la Mungu huko ni kumtegemea mwanadamu, Unapoamka asubuhi na jambo la kwanza ni kumfikiria boss wako na hata humshukuru Mungu kwa kukuamsha salama, huko ni kumtegemea mwanadamu,

Unapotii maagizo ya watu fulani waliokuzunguka na kuyadharau maagizo ya Mungu, kwa kisingizio usipotii utakosa kazi, utakosa fursa, utakosa heshima, utakosa hadhi. Huko ni kumtegemea mwanadamu na hivyo ni kujikuta unaishi katika laana.

Biblia inasema pia amelaaniwa mtu yule amfanyaye mwanadamu kuwa KINGA YAKE. Unapomtegemea mtu fulani asilimia mia kama mlinzi wako, au kama tumaini lako, ni kuishi chini ya laana…Unapomtegemea mlinzi wako wa getini na kujitumainisha na walinzi wanaokuzunguka ni kujiweka chini ya laana, ndio! Utakuwa na walinzi sio dhambi…lakini kuweka tumaini lako la kwanza juu yao..na kusema wao, wasipokuwepo wewe umekwisha..Ni kuishi chini ya laana, Biblia inasema..

Zaburi 127 :1 “Bwana asipoijenga nyumba Waijengao wafanya kazi bure. Bwana asipoulinda mji Yeye aulindaye akesha bure. 2 Kazi yenu ni bure, mnaoamka mapema, Na kukawia kwenda kulala, Na kula chakula cha taabu; Yeye humpa mpenzi wake usingizi”.

Unapowaamini madaktari asilimia mia kwamba uzima wako upo juu ya elimu yao, na utaalamu wao, na huku moyoni mwako Imani na Mungu imepotea kabisa, huko ni kumtegemea mwanadamu hivyo ni kujiweka chini ya laana…Elimu ya udaktari yote haiwezi kutibu kifo, lakini yupo mmoja awezaye kuwafufua waliokufa, huyo ndio wa kumtegemea hivyo kujitumainisha kwa madawa, au kwa mahospitali na huku moyoni mwako Mungu hana nafasi..ni kuishi chini ya laana, mwisho wa siku daktari akitoa ripoti hii kuwa una siku kadhaa za kuishi, au wiki kadhaa, unapaniki sana, hiyo ni hatari sana…… madaktari wanapaswa wawe tu ni vyombo ambavyo Mungu anavitumia kutuhudumia, lakini sio waponyaji wako, wala watu wanaostahili kuchukua heshima ya Mungu, kwasababu Mungu anaweza kutumia njia nyingine kukuponya bila kutumia hao..hivyo tumaini letu lote ni kutoka kwa Bwana.

Lakini pia Biblia inasema..

Yeremia 17:7 “Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, Ambaye Bwana ni tumaini lake.

8 Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, Uenezao mizizi yake karibu na mto; Hautaona hofu wakati wa hari ujapo, Bali jani lake litakuwa bichi; Wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, Wala hautaacha kuzaa matunda.”

Ukimfanya Bwana ndio jawabu lako la mwisho, na kumwamini yeye kuwa ndio kila kitu…Neno linasema utakuwa kama mti uliopandwa kando kando ya maji..hautaona hofu wakati wa hari (jua/kiangazi)..wala hautahangaika wakati wa uchache wa mvua, wala hautaacha kuzaa matunda…

Dalili ya kwanza ya kujipima kama unamtegemea mwanadamu au la ni hofu ya Maisha!! Ukishaanza kuona una hofu fulani ya Maisha kuogopa unaweza kupatwa na jambo fulani baya kutoka kwa watu, usipofanya kitu fulani…labda usipotoa rushwa, au usipokubali kushirikiana nao kwenye jambo fulani na watu fulani, au usipojaribu kufuata njia zao au kuishi kama wao, au kuishi kama wanavyotaka,au kuvaa kama wao, unaanza kuwa na hofu ya kufa, au hofu ya Kesho itakuaje, nitavaaje, nitakulaje, nitaishije!…hizo ni moja ya dalili za kumtegemea mwanadamu…lakini wote wanaomtegemea Bwana biblia inasema hawatakuwa na hofu, hawatakuwa na wasiwasi kuwa Kesho,au Kesho kutwa watakosa riziki, wanajua kabisa katika shughuli zao Mungu atakuwa pamoja nao tu hata kama leo wanajiona hawana kitu, wanajua Kesho Mungu atafungua njia itapatikana tu! Hivyo hawapepeswi na maneno wala upepo wa hofu za Maisha haya…

Wakitishiwa kuwa watafukuzwa kazi wasipofanya jambo fulani, hilo haliwababishi, wakitishiwa kuwa watahatarisha kazi zao wasipomtii boss wao kwenda kumkusanyia rushwa hawaweweseki, kama Danieli alivyozingirwa na maadui waliompangia mabaya kwa mwenendo wake wa kukataa kula rushwa..

Biblia inasema pia mtu yule amtegemeaye mwanadamu hataacha kuzaa matunda, kwanini? kwasababu anakuwa kama amepandwa kando kando ya mto…Na kuzaa matunda kuko kwa namna Mbili..kuzaa matunda ya mwili kama kufanikiwa katika mambo yote ya mwilini…shughuli na kazi zinakuwa zinafanikiwa, na pia uzao wa tumbo unabarikiwa, na namna ya pili ni kuzaa matunda ya roho, ambayo ni upendo, upole, kiasi, uvumilivu, Fadhili, furaha, amani, n.k (Wagalatia 5:22) pamoja na kuwaleta watu kwa Kristo, ambayo thawabu yake ni juu mbinguni.

Bwana akubariki sana.

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

KITABU CHA UKUMBUSHO

NI JAMBO LINALOMTAMANISHA SANA BWANA TUMWOMBE BILA KUKATA TAMAA?

TWEKA MPAKA VILINDINI.


Rudi Nyumbani

Print this post

MUNGU KUSEMA NA WEWE PEKEE, HAITOSHI KUKUPA USHINDI.


Tukisoma kitabu cha Waamuzi ile sura ya 19, tunaona habari ya mtu mmoja Mlawi ambaye alikuwa na suria wake mzinifu, Hiyo pekee haikutosha yule suria aliondoka na kurudi nyumbani kwa baba yake, Lakini kwa jinsi Yule mtu alivyokuwa anampenda Suria wake miezi minne ilipoisha alifunga safari kutoka mjini kwake na kwenda kumfuata nyumbani kwa baba yake ili kumsihi arudi nyumbani.

Lakini alipokuwa njiani kurudi nyumbani na giza limeshaingia alikutana na mzee mmoja aliyetoka shamba ambaye alimwona amesimama barabarani hana pa kulala, hivyo alimkaribisha nyumbani kwake alale usiku ule ili kesho yake aendelee na safari yake, lakini kumbe huku nyuma wenyeji wa ule mji walikuwa wanawafuatilia, na usiku ule ule wakamfuata Yule mzee nyumbani wakigonga mlango wake kwake wakisema tutolee huyo mtu tulale naye, mambo yale yale yaliyotendekea sodoma yanajirudia tena Israeli, lakini Yule mzee alikuwa mkarimu sana, akawasihi awape binti yake ambaye ni bikira wamfanyie ouvu wao, wamuache Yule mgeni aliyeingia nyumbani kwake akae katika hali ya usalama, lakini walikataa, nusu wamuue Yule mzee, ndipo Yule mtu akaamua kutoka akawapa suria wake wamfanye wanachotaka kumfanya..

Kwa ukatili mkubwa sana wale watu walimbaka Yule mwanamke usiku kucha, tengeneza picha pengine wanaume zaidi ya 100 walikuwa pale nje, mpaka kunapambazuka bado wanaendelea kumfanyia uovu ule, hadi walipoona mwanga unakaribia kutoka ndipo wakamwacha wakaondoka, Yule mwanamke kufika tu mlangoni mwa ile nyumba hali ikawa mbaya zaidi akafa pale pale, Asubuhi mume wake anafungua mlango amwambie amka tuondoke zetu, anakutana na maiti mlangoni..

Kama tunavyosoma habari akamchukua Yule mwanamke akaenda kujifungia nyumbani mwake mwenyewe, akamkata kiungo baada ya kiungo akavigawa mafungu 12. Kisha akavichukua na kwenda kuviweka katika mipaka yote ya Israeli kwa idadi ya makabila yao, ndipo watu kuona kitendo kile walishtuka sana. Wakijiuliza jambo hili maana yake ni nini?. Kwani halijawahi kutokea katika Israeli tangu walipotoka Misri, Ndipo Yule mtu akaanza kuwaelezea jinsi tukio lilivyokuwa.

Watu wote wakasema haiwezekani ni lazima hao watu ambao wamefanya hivi huko Benyamini watolewe wauawe ili kuondoa ouvu Israeli. Lakini Benyamini walipoambiwa wawatoe watu hao waligoma..Kwao halikuwa kama jambo la kushtusha sana, kuonesha ni jinsi gani walivyokuwa wameoza kwa uovu kama wa Sodoma na Gomora..Ndipo makabila yote 11 ya Israeli yaliyosalia yakaapa hawatakaa wawape binti zao, na zaidi ya yote wakakusanyika kwenda kuisambaratisha Benyamini juu ya uso wa Israeli.

Siku ile ile watu mashujaa wakahesabiwa. Ndipo wakamuuliza Mungu juu ya kabila lipi lianze kwenda kupigana nao, ndipo Mungu akawajibu na kuwaambia lianze kwenda kabila la Yuda. Lakini walipokwenda mambo yalikuwa tofauti na walivyotazamia, badala ya kuwaangamiza Benyamini wale waovu wao ndio walioangamizwa, walipigwa kwa mapigo makuu, watu 22,000 wa Israeli waliuliwa siku ile.

Lakini Israeli hawakukata tamaa tena, walijipanga upya kwa mara ya pili, tunasoma.

Waamuzi 20:22 “Lakini watu hao, watu wa Israeli, walijitia nguvu, wakaviandaa vile vita mara ya pili mahali pale walipojiandaa siku ya kwanza.

23 Wana wa Israeli WAKAKWEA JUU NA KULIA MBELE ZA BWANA HATA JIONI; wakamwuliza Bwana, wakisema, Je! Niende nikaribie tena kupiga vita juu ya wana wa Benyamini ndugu yangu? Bwana akasema, Haya, kweeni, mwende kupigana naye.

24 Basi wana wa Israeli wakakaribia juu ya wana wa Benyamini siku ya pili.

25 Benyamini alitoka kupigana nao kutoka Gibea siku ya pili, wakaangamiza hata nchi watu kumi na nane elfu tena katika watu wa Israeli; hao wote walikuwa wenye kutumia upanga.

Tunaona hapo japo Mungu aliwaambia wakwee kupigana nao lakini bado hawakufua dafu, watu wengine 18,000 wa Israeli waliuliwa vibaya na jeshi dogo la Wabenyamini.

Ni rahisi kusema, mbona Mungu si mwaminifu kwetu, mbona tumelia mbele zake siku nzima na ametupa majibu kabisa tukwee lakini matokeo yanakuja tofauti?. Mbona tuna lengo zuri la kumwondolea uovu Israeli, lakini waovu ndio wanazidi kufanikiwa na kututukana.

Lakini tunasoma, mara ya Tatu walipokwenda mbele za Bwana, hawakwenda na vilio na kufunga tu peke yake, lakini pia wanamtolea Bwana Sadaka za Amani na za kuteketezwa.Tusome..

Waamuzi 20:26 “Ndipo wana Israeli wote, na hao watu wote, wakakwea, wakaenda Betheli, na kulia, wakaketi hapo mbele za Bwana, wakafunga siku hiyo hata jioni; NAO WAKASONGEZA SADAKA ZA KUTEKETEZWA NA SADAKA ZA AMANI MBELE ZA BWANA.

27 Kisha wana wa Israeli wakauliza kwa Bwana (kwa sababu sanduku la agano la Mungu lilikuwako huko siku hizo,

28 na Finehasi, mwana wa Eleazari, mwana wa Haruni, alikuwa anasimama mbele ya hilo sanduku siku hizo), wakasema, Je! Nitoke tena niende kupigana na wana wa Benyamini ndugu yangu, au niache? Bwana akawaambia, Haya, kweeni; kwa kuwa kesho nitamtoa na kumtia mkononi mwako.

29 Basi Israeli akaweka watu wavizie kinyume cha Gibea kuuzunguka pande zote.”

Tunasoma safari hii Mungu hakuwaambia wakwee tu, bali aliongezea na kuwaambia “Kesho nitawatoa na kuwatia mikononi mwenu”. Na baada ya hapo ukiendelea kusoma utaona jinsi Benyamini ilivyoshambuliwa na kuangamizwa vibaya mno, kwa nafasi yako pekee soma habari yote ilivyoishia utaona jinsi maangamizi yale yalivyokuwa makubwa…Ilikuwa bado kidogo tu lile kabila lingefutika lote, watu wa Benyamini walibakia wachache kama faru tulionao mbugani. Na kama sio Israeli kughairi mashambulizi yao na kuwaruhusu wale waliosalia wakaibe wake huko leo hii tungekuwa tunayafahamu na kuyaosoma makabila 11 tu ya Israeli.

Lakini kiini cha somo tunachojifunza hapo ni nini?.

Haijalishi unachokwenda kuomba mbele za Mungu ni chema kiasi gani, haijalishi unalia mbele za Mungu kiasi gani, haijalishi unafunga wiki, miezi au miaka kiasi gana, kuna mambo mengine hayawezi kutoka hivi hivi bila ya kuhusisha SADAKA. Kama vile hao walivyotoa sadaka za aina mbili za kuteketezwa na za amani, vivyo hivyo na sisi katika agano jipya tunazo sadaka za aina mbili, Ya kwanza ni ya kuteketezwa ambayo ni Yesu Kristo, aliyeteketezwa kwa ajili yetu,alichinjwa kwa ajili yetu.

Hivyo Kama upo nje ya Yesu Kristo ndugu halafu unamwendea Mungu na kumwomba akupiganie katika vita vyako, nataka nikuambie utaishia pabaya na kuvunjika moyo, na kuona kama Mungu hayupo. Vile vile na wewe uliye ndani ya Kristo, unamwomba Bwana akupiganie katika majaribu yako, halafu unakwenda mbele zake mikono mitupu, kuna uwezekano mkubwa wa tatizo lako kutokuondoka…

Kwasababu wapo wakristo ambao ni Hodari wa kuomba kweli kweli na kulia na kufunga mfano wa hawa wana wa Israeli. Lakini kwenye suala la kumtolea Mungu, wanadharau, wanaona kama Mungu hatazami hilo, wanasema yeye sikuzote huwa anatazama moyo. Nataka nikuambie, Mungu anapendezwa na moyo wa shukrani, pale unapomtolea Mungu mfuko wako anaona huyu mtu ananithamini, sio kwamba anayo haja ya fedha yako, lakini ni utaratibu wake, anapendezwa zaidi ya wenye moyo wa utoaji. unapomwendea Mungu na kumwomba akufanikishe katika jambo lako zito au jepesi jifunze kuambatanisha na sadaka ipeleke madhabahuni pake ndugu.

Unaweza kusema ooh! Mungu ameniambia yupo pamoja na mimi, Mungu kanionyesha maono, Mungu kanipa unabii, lakini utashangaa kwanini bado unashindwa pamoja na maono yako yote, Ni kwasababu unakuwa kama hawa Waisraeli.

Mungu kila wakati alikuwa anawaambia Kweeni, ni yeye kabisa alikuwa anawasapoti katika walichokuwa wanakifanya lakini tunaona japo walikuwa na jeshi la watu LAKI NNE, walipigwa na jeshi dogo la watu ELFU 26 tu la Wabenyamini. Na wewe vilevile usishangae kushindwa na mambo madogo, ukilinganisha na nguvu iliyoiwekeza katika hilo mbele za Mungu, Tatizo linaweza kuwepo hapo.

Anza kujifunza kumtolewa Bwana, naye atazifanya njia zako kuwa nyepesi.

Bwana akabariki. Tafadhali “Share ” Ujumbe huu kwa wengine. Na Bwana atakubariki. jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

TOFAUTI KATIKA YA ZAKA NA SADAKA NI IPI?

SADAKA ILIYOKUBALIKA.

Rudi Nyumbani

 

Print this post

UTALIPWA KATIKA UFUFUO WA WENYE HAKI.

Luka 14:12 “Akamwambia na yule aliyemwalika, Ufanyapo chakula cha mchana au cha jioni, usiwaite rafiki zako, wala ndugu zako, wala jamaa zako, wala jirani zako wenye mali; wao wasije wakakualika wewe ukapata malipo.

13 Bali ufanyapo karamu waite maskini, vilema, viwete, vipofu,

14 nawe utakuwa heri, kwa kuwa hao hawana cha kukulipa; kwa maana utalipwa katika ufufuo wa wenye haki”.

Katika habari hii, tunaona Bwana Yesu alialikwa na mtu mmoja mkuu sana miongoni mwa Mafarisayo ale chakula cha mchana nyumbani kwake, na bila shaka mtu huyu alikuwa ni tajiri, na katika karamu yake alialika watu wakuu, watu wa maana, na si watu wa kawaida kawaida tu, Lakini kuna kitu ambacho Bwana Yesu alikiona kimepunguka katika ukarimu wake mwema wa kuwaalika watu na wageni katika shughuli zake, kwani si wote wenye moyo kama huo.Wengine wanaweza wakawa ni matajiri na wakuu, lakini wakala vitu vyao peke yao, lakini huyu alikuwa watofauti kidogo.

Lakini pamoja na hayo, Bwana Yesu aligundua watu aliowaalika walikuwa ni matajiri tu, watu wenye uwezo kama yeye, Hivyo Bwana Yesu kwa kuliona hilo ili kumsidia kuifanya taabu yake isiwe bure, ndipo akamwambia kwa kumshauri wakati mwingine, kuwa atakapofanya sherehe awaalike watu wasiokuwa na uwezo wa kumlipa mfano wa hicho alichokifanya..Kwasababu akiwaalika watu wenye uwezo, wale watu nao watarudisha mapigo siku moja, watamwalika na yeye kwenye karamu zao na thawabu yake itakuwa imeshalipwa na wao, lakini mbinguni hatakuwa na kitu, hivyo ili taabu yake na wema wake uwe na nguvu idumuyo, siku nyingine akifanya karamu kubwa kama hiyo, asiiachie thawabu yake ilipizwe na wanadamu bali ije ilipizwe na Mungu katika siku ya ufufuo wa wenye haki, hivyo awaalike watu wasiokuwa na uwezo wa kumfanyia kama kile alichowafanyia.

Hata leo hii, yapo mambo mengi tunayafanya tukidhani tutalipwa tutakapofika mbinguni kwa ukarimu tunaoufanya..Kwa mfano leo hii labda kutokee mchango wa sherehe fulani ni rahisi kuchangia harusi ya boss wako, au mfanyakazi mwenzako kwasababu unajua kuna siku moja na wewe utahitaji wakuchangie kwenye sherehe yako, au ya ndugu yako. Lakini ukisikia yupo jirani yako ambaye ni maskini hana mbele wala nyuma kipato chake ni kidogo hata hakimtoshelezi yeye mwenyewe, halafu mwanawe anataka kuoa, hivyo anahitaji sapoti yako kidogo, Ukweli ni kwamba wengi wetu tutakuwa tayari kuingia mitini, ni kwasababu gani?, Ni kwasababu tunaona mbeleni huyu anaweza asiwe na msaada kwangu siku shughuli yangu, hivyo hata nisipomsaidia hainiathiri chochote.

Kiuhalisia Mungu hatakulaumu ulipochangia sherehe ya Yule boss wako na kuiacha hii ya huyu maskini, zaidi Mungu atakulipa, na kukulipa kwake kutakuwa ni kwa kupitia wao, na habari thawabu yako itakuwa imeishaipata hapa hapa duniani, juu mbinguni utakuwa huna kitu chochote. Ukinunua zawadi si zote uzipeleke kwa marafiki na ndugu, nyingine tenga wapelekee wasio na uwezo wa kukulipa,watu wasio na faida yoyote kwako. Unapokopesha usikopeshe wale tu ambao watakupa na Riba juu yake..Kopesha hata na Yule ambaye hawezi kukulipa na Riba juu yake mwenye uwezo wa kukurudishia kiwango kile kile ulichompa.

Luka 6:35 “Bali wapendeni adui zenu, tendeni mema, na kukopesha msitumaini kupata malipo, NA THAWABU YENU ITAKUWA NYINGI; nanyi mtakuwa wana wa Aliye juu, kwa kuwa yeye ni mwema kwa wasiomshukuru, na waovu”.

Na ndio sababu ambayo Bwana alimshauri huyu mtu aliyemwalika, nasi tupokee ushauri huo, tutafute thawabu zinazodumu milele. Ni kweli wakati mwingine unaweza kuona ni mzigo kuwa msaada kwa wasiokunufaisha Lakini thawabu yake, utaiona siku ile utakapofika mbinguni. Maana kiwango cha hazina yako ndicho kitakachofunua utajiri utakaokuwa nao mbinguni.

“Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho. (Wagalatia 6:9)”

Bwana akubariki.

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Zinazoendana:


UFUFUO WA UZIMA NA WA HUKUMU.

KATIKA BIBLIA KUNA UFUFUO WA AINA NGAPI?

TUZO UTAPEWA KULINGANA NA NAFASI YAKO.


Rudi Nyumbani:

Print this post

FAIDA ZA MAOMBI.

Maombi yamegawanyika katika sehemu kuu tatu 1) kushukuru 2) kuwasilisha mahitaji kwa mungu 3) Kutangaza.

1) MAOMBI YA SHUKRANI; Maombi haya ya shukrani ni Dhahiri na yanajulika na Wengi, kwamfano maombi ya kushukuru ni muhimu sana, na ni wajibu wa kila mtu, kuyafanya…Na haya yanahusisha kumshukuru Mungu kwa Uzima anaotupa, kumshukuru Mungu kwa afya anayotupa, ukizingatia wakati unapumua kuna wengine wapo ICU, wengine Mochwari n.k, pia maombi haya yanahusisha kumshukuru Mungu kwa mambo yote mabaya aliyokukingia katika wiki yote iliyoisha, mwezi wote uliopita na miaka yote iliyopita nyuma yako, njiani umepishana na mapepo mengi, shetani alikuwa amepanga mauti na ajali nyingi juu yako lakini Mungu kakuepusha nazo zote pasipo hata kukuambia, uthibitisho ni wewe kuimaliza wiki salama, na pia yanahusisha kumshukuru Mungu kwa riziki zote za kiduni anazotupatia, katika shughuli zetu na mapato yetu yote,..Kwahiyo maombi haya kwa ujumla yanahusisha kumshukuru Mungu kwa mambo yote anayoyafanya tunayoyaona na tusiyoyaona. Ni maombi yanayoonesha unyenyekevu wetu mbele za Mungu na kumwonesha Mungu wetu kuwa tunathamini na kuutambua na kuujali ulinzi wake na Fadhili zake juu yetu. Kwahiyo ni sehemu ya maombi ambayo ni muhimu sana.

2) Sehemu ya pili ya maombi ni ile ya KUWASILISHA MAHITAJI YETU MBELE ZA MUNGU. Hii inahusisha kumwendea Mungu kwa unyenyekevu kumwomba atufanyie au atupatie jambo Fulani katika Maisha yetu, Tunamwendea tukiamini kuwa yeye ndiye mpaji wetu (YEHOVA-YIRE). Tunamwomba azidi kutupa riziki zetu, azidi kuzifanikisha kazi zetu za mikono, azidi kutupa afya, azidi kutuepusha na yule mwovu na mipango yake yote, azidi kutupa Neema ya kumjua yeye Zaidi popote tuendapo atukutanishe na injili yake na kuitii, azidi kutupa mioyo ya nyama na si ya jiwe katika kutenda mapenzi yake, azidi kutupa hekima, tunamwomba Bwana azidi kutupa furaha, amani, upendo pamoja na kibali kila tuendapo, na kutufanikisha katika mambo yote katika masaa ya siku yaliyobakia, wiki na katika mwezi huu na unaokuja. Hapa tunamwomba Mungu atuepushe na kila jaribu lililopangwa na shetani kinyume chetu mbele yetu..Kama Bwana alivyosema mahali Fulani “Ombeni kwamba msiingie majaribuni. (Luka 22:40)”.

Ikiwa na maana kuwa usipoomba ni lazima utaingia majaribuni tu!..Wakina Petro usiku ule Bwana aliwaambia waamke kusali ili wasiingie majaribuni wakapuuza, wakalemewa na usingizi wakalala, masaa machache baadaye Petro alipojaribiwa na Ibilisi amkiri Yesu, alishindwa mwisho wake akamkana mara 3 lakini endapo angeomba usiku ule kama Bwana alivyomwambia na kuifunika siku yake wakati Ibilisi anamjaribu angeshinda lile jaribu, saa ile nguvu fulani ya ujasiri ingemshukia pale pale na angemkiri Bwana badala ya kumkana, au Mungu angemuepusha kabisa na jaribu hilo. Lakini kutokana na kwamba alikuwa hana hazina ya maombi ya kutosha, nguvu za roho zilikuwa chin alishindwa. Na aina zote za majaribu zinaweza kuzuiwa au kuepukwa kwa maombi… unapopita mahali na watu kukuudhi mpaka kukasirika na kugombana mpaka kutoa maneno machafu hilo ni majaribu ambalo ungeweza kulizuia kwa kuomba usiku mmoja kabla hujalala, au asubuhi kabla ya kuanza shughuli zako.

Kadhalika unapojikuta unafanya kitu kisichofaa ambacho hukutarajia au hukupanga kukifanya hilo nalo ni jaribu ambalo lingeweza kuzuiliwa kwa kuomba kabla ya kuianza siku..Na dhambi nyingine zote za bahati mbaya zinasababishwa na upungufu wa maombi. Inapotokea safari ya ghafla ambayo ni ya hasara na si ya faida hilo nalo ni jaribu ambalo endapo ungeomba lisingekukuta.nk n.K.

3) Sehemu ya tatu na ya mwisho ya maombi ni maombi ya KUTANGAZA. Hii ni sehemu ya mwisho na ya muhimu sana kwa kila Mkristo kuifanya. Na faida yake kuu ya haya maombi ni ile ile ya KUTUEPUSHA NA MAJARIBU, Maombi haya ni maombi ya kimamlaka…Maombi haya na yale ya KUPELEKA MAHITAJI yanakazi moja tu nayo ni KUTUEPUSHA NA MAJARIBU.

Sasa kabla ya kuingia kujifunza juu ya jambo hili hebu kwanza tujifunze ulinzi wa kiMungu juu ya mtu aliyezaliwa mara ya pili.

Mtu anapozaliwa mara ya pili, na kuishi Maisha yanayompendeza Mungu asilimia zote, kunakuwa kuna ulinzi Fulani wa kiujumla ambao Mungu anauachilia juu yake, kiasi kwamba huyo mtu hata iweje hawezi kupotea, shetani hawezi kumtoa mkononi mwa Mungu, labda tu huyo mtu kwa hiyari yake mwenyewe aamue kujiuza kwa shetani, lakini kwa namna nyingine yoyote hawezi kutoka mikononi mwa Mungu, anakuwa analindwa kuanzia unywele wake mpaka unyayo wako, na anakuwa amevuka kutoka mautini kuingia uzimani, …Lakini pamoja na huo ulinzi wa kiujumla kuna sehemu ndogo sana ambayo Mungu kamwachia shetani aimiliki..na hiyo ni kutokana na kwamba bado tupo katika miili hii ya dhambi, sehemu yote ya ulinzi wa kiMungu tutakuja kuipata baada ya ukombozi wa miili yetu pale tutakapovaa miili mipya ya utukufu.

Ndio maana unaona sasa japokuwa umeokoka na unaishi Maisha ya kumpendeza Mungu kwa asilimia zote lakini bado utapitia wakati mwingine wa viudhaifu vya hapa na pale, utaumwa kichwa, utajisikia kichefuchefu, mafua yatakusumbua, wakati mwingine itakubidi umeze Panadol kupunguza maumivu au uende hospitali n.k. Sasa hiyo yote ni kuonesha kuwa Mungu hajaipa miili yetu hii asilimia 100 ulinzi…ingawa hivi viudhaifu haviwezi kutuathiri kiasi cha kututoa kwenye Imani, kwasababu Mungu hawezi kuruhusu tujaribiwe kupita tuwezavyo, alisema hivyo katika Neno lake.

1Wakoritho 10: 13 “Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili”.

Kwahiyo haya majaribu madogo madogo ni lazima yaje! Na ni wazi kuwa yanaletwa na shetani kututesa tu! Na kutuhangaisha…Kwahiyo shetani anachokifanya ni kutumia hii nafasi aliyopewa ya sehemu ndogo ambayo Mungu kaiacha, kutujaribu…Na kwasababu anajua hawezi kumjaribu mwamini kwa asilimia zote, atahakikisha kuwa hiyo sehemu ndogo aliyopewa anaitumia ipasavyo.

Sasa swali? Anaitumiaje?

Anaitumia kwa KUTANGAZA, Anawatumia watu kutamka maneno Fulani Fulani juu yako, ambayo hayo yanaweza kutokea kama walivyozungumza, kwasababu Mungu alivyomuumba mwanadamu akizungumza kitu kwa Imani ni lazima kitokee hata kama mtu huyo sio mchawi. Ndio maana wazazi hata kama ni waabudu sanamu wanao uwezo wa kumbariki mtoto au kumlaani, na hizo baraka au laana zikampata huyo mtoto hivyo hivyo kama alivyozisema. Kwasababu hiyo basi shetani anaweza kutumia watu au wachawi au mapepo yake KUTANGAZA mambo Fulani mabaya juu ya mtu.

Kumbuka tena kwa msisitizo..kama umezaliwa mara ya pili na kuishi Maisha yampendezayo, haijalishi ni mambo gani makubwa watayatangaza juu yako, hayatatimia yote kwasababu kuna asilimia kubwa ya ulinzi wa kiMungu kwenye Maisha yako, lakini pia yapo baadhi madogo madogo yanayoweza kutimia na hiyo ni kwasababu hatujapewa dhamana wa ulinzi wa miili hii asilimia zote kama tulivyotangulia kusema..(huu ni msingi mkubwa ambao unahitaji kuelewa) Na sio kwamba Mungu kashindwa kutufunika asilimia zote, hapana ni kwasababu tu ndivyo imempendeza iwe hivyo…kwamba tujue kwamba bado tupo duniani?, tujue kuwa sisi bado ni wadhaifu mbele zake, na tujifunze kumtegemea yeye na kumwomba ulinzi…na pia tujue kuwa vita bado vinaendelea…mpaka siku tutakapovaa ile ya utukufu, ndipo vita vitaisha.

2Wakorintho 1:8 “Maana ndugu, hatupendi, msijue habari ya dhiki ile iliyotupata katika Asia, ya kwamba tulilemewa mno kuliko nguvu zetu, hata tukakata tamaa ya kuishi.

9 Naam, sisi wenyewe tulikuwa na hukumu ya mauti katika nafsi zetu ili tusijitumainie nafsi zetu, bali tumtumaini Mungu, awafufuaye wafu,

10 aliyetuokoa sisi katika mauti kuu namna ile; tena atatuokoa; ambaye tumemtumaini kwamba atazidi kutuokoa;”

Sasa ili kupunguza nguvu za shetani kwa majaribu yake anayoyatumia kwa NJIA YA KUTANGAZA…Na sisi tulioamini tuna wajibu huo huo, wa kuingia kwenye maombi ya kuzipunguza hizo nguvu ndogo ndogo za shetani zinazofanya kazi kwenye Maisha yetu…Na maombi hayo hatuyafanyi kwa kupeleka mahitaji mbele za Mungu, bali kwa KUTANGAZA kama yeye anavyotangaza..Ndio hapo sasa Kila siku kabla ya kuianza siku unatamka baraka katika siku hiyo, unalaani na kufuta kila kazi zote za Adui zilizopangwa katika siku hiyo kwa jina la YESU, Unalaani vidhiki na vijaribu vidogo vidogo vilivyopangwa na shetani…Na unatamka kwa maneno yanayosikika kabisa, kwasababu maneno yanaumba, kwa Mungu aliiumba dunia kwa Neno, Unatamka kwa kutangaza kuziharibu nguvu zote na kufuta maneno yote yaliyozungumzwa na watu, wachawi, au mapepo katika siku nzima…unalaani nguvu zote za giza zilizoachiwa siku hiyo zitakazokufanya uikane Imani, au upate hasara ya jambo Fulani, au zitakazokufanya ulumbane au ugombane na watu, unalaani kwa kinywa chako kila nguvu zote za giza zilizoachiwa na yule adui kukufanya usipate muda wa kusoma Neno,na kila ratiba isiyoeleweka iliyopangwa kuzimu kinyume chako na ndugu zako…Unahikikisha unagusa kila kipengele katika Maisha yako, afya yako,familia yako, kazi yako na Imani yako. Usiache kitu!, kwasababu na yule adui anajua anaomlango mdogo juu ya Maisha yako hivyo anakaza kuutumia vizuri.

Mithali 18:21 “Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake.”

Kwa kufanya hivyo utakuwa umeharibu mipango yote midogo midogo ambayo shetani alikuwa amepanga kukusumbua katika siku hiyo na wiki hiyo. Na hivyo utakuwa umejiongezea Ulinzi wa kiMungu kwa asilimia nyingine kadhaa mbele. Kama alikuwa akuletee viugomvi, viugonjwa, unashangaa siku inaisha bila hivyo vitu, kama alikuwa amekusudia kukuletea vitabu vya hapa na pale visivyoeleweka vinatoweka.

Nakumbuka mwanzoni mwanzoni nampa Bwana Maisha, nilikuwa napitia changamoto nyingi sana na nilikuwa sijui chanzo chake ni nini?..lakini baada ya kujifunza somo la maombi, niliona mabadiliko makubwa sana…

Kwa hiyo ni maombi ya Muhimu sana na kila Mwamini anatakiwa aombe. Na ni moja ya silaha 6 tulizopewa katika biblia..

Waefeso 6: 11 “Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.

12 Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.

13 Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.

14 Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani,

15 na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani;

16 zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.

17 Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu;

18 KWA SALA ZOTE NA MAOMBI MKISALI KILA WAKATI KATIKA ROHO, MKIKESHA KWA JAMBO HILO NA KUDUMU KATIKA KUWAOMBEA WATAKATIFU WOTE;

19 pia na kwa ajili yangu mimi, nipewe usemi kwa kufumbua kinywa changu, ili niihubiri kwa ujasiri ile siri ya Injili;

20 ambayo kwa ajili yake mimi ni mjumbe katika minyororo;

hata nipate ujasiri katika huyo kunena jinsi inipasavyo kunena.”

Kwa kumalizia kumbuka kuwa muda wa chini Bwana Yesu aliotuamuru tusali kwa siku ni LISAA LIMOJA.

Mathayo 26: 40 “Akawajia wale wanafunzi, akawakuta wamelala, akamwambia Petro, Je! Hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja? 41 Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.”

Umeona hapo, roho zetu zipo tayari kuomba lakini miili ndio inayokataa, hivyo mambo mengine ni unalazimisha, kama Bwana asiyekuwa na dhambi aliomba Zaidi ya lisaa limoja, unafikiri inatupasaje sisi wenye dhambi?..unakataa usingizi na uvivu wa kuomba, unalazimisha mambo, utashangaa dakika za kwanza unapata shinda lakini baaada ya dakika 10-15 mbeleni unashangaa kuna nguvu Fulani inakuvaa unajikuta unazama kwenye maombi…Na kwa vipengele hivyo vitatu ukianza na kushukuru, kisha kupeleka maombi na kutangaza baraka..huwezi kuacha kumaliza lisaa na Zaidi..

Na pia kumbuka kuwaombea na wengine, katika vipengele vyote hivyo vitatu, hata hichi unachokisoma hakijapewa guarantee ya ulinzi asilimia 100, kinahitaji maombi kiweze kuendelea kuwepo, kwahiyo uombapo ukumbuke kugusia kila eneo, pamoja na sisi tunaoandika hizi habari, Ili injili ya Mungu izidi kwenda mbele, kwa Neema za Mungu.

Bwana akubariki sana.

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Zinazoendana:

NI JAMBO LINALOMTAMANISHA SANA BWANA TUMWOMBE BILA KUKATA TAMAA?

SHUKURU KWA KILA JAMBO.

RUDIA, TENA NA TENA KUMWOMBA MUNGU USIKATE TAMAA.

NI KWA NAMNA GANI TUTASHINDA MAJARIBU?

ROHO I RADHI, LAKINI MWILI NI DHAIFU.


Rudi Nyumbani

Print this post

HATARI YA KUTOKUITAFAKARI BIBLIA VIZURI?


Shalom! Mtu wa Mungu, maandiko yanatuagiza tusiache kuonyana kila siku, maadamu iitwapo leo (Waebrani 3:13). Hivyo nakukaribisha tujifunze leo jambo moja lihusulo BIBLIA.

Nilipokuwa ninatafakari hili Neno linalosema “Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti.” Nikajiuliza hii njia ionekanayo kuwa sawa ni ipi?..Mtu akiwa mtukanaji, mtu akiwa muuaji, mtu akiwa ni fisadi n.k, njia yake haiwezi kuonekana ni sawa machoni pake, ni wazi kuwa anafahamu anapoeleka ni pabaya..Lakini njia inayoweza kuonekana ni sawa machoni pa mtu ni ipi?, ni ile inayotoka katika maandiko (BIBLIA), pale maandiko yanapomthibitishia mtu kuwa kitu hichi au kile anachokifanya kimeandikwa, basi hilo linampa amani ya kufahamu kuwa yupo katika njia sahihi.

Nataka nikuambie, biblia ni kitabu kitakatifu sana, kimekamilika na kujitosheleza kwa namna zote, hakiwezi kuongezwa wala hakiwezi kupungumzwa, lakini nataka nikuambie pia Biblia hii si ya watakatifu peke yao: Biblia si mti wenye tunda la aina moja, bali ni mti wenye matunda ya aina nyingi tofauti tofauti,. na kila mtu anachuma kinachomfaa na kuondoka kulingana na matakwa yake mwenyewe.

Na hiyo yote ni kwasababu biblia ni Neno la Mungu, na Neno la Mungu tunajua ndio lililoumba kila kitu (Yohana 1:1), halikuumba vyema tu bali hata na viovu pia, hivyo pumzi ya kila kitu inategemea hilo Neno. kwahiyo kila mtu na kila mmoja na inaweza kumnufaisha kulingana na matakwa yake mwenyewe. Shetani inamnufaisha katika lengo lake la kupoteza watu, na amefanikiwa kweli kupoteza mamilioni ya watu kwa kupitia biblia unayoisoma, hata alijaribu kuitumia hiyo hiyo kumwangusha Bwana akashindwa..

Madaktari wanaitumia hii kuwasaidia kubuni aina mbalimbali za matibabu, hata ukiangalia nembo yao kubwa maarufu inayotumiwa na Shirika la Afya ulimwenguni (WHO), utaona ni Yule nyoka wa shaba ambaye Musa aliwaagiza wana wa Israeli wamtazame ili wapone kutokana na sumu ya nyoka. Utamaduni huo ambao baadaye uligeuka kuwa wa kipagani, ulirithiwa na mataifa mengine ya kipagani kama Ugiriki wakahusisha na tiba za kienyeji na mambo hayo, na ndio huko huko mpaka ikawa maarufu katika masuala yote ya tiba duniani leo hii.

Biblia hii hii inayoisoma inatumiwa na majeshi, kubuni mbinu mpya za kupigani: Na wanafanikiwa vizuri sana. Wakati wewe unafurahia kusoma zile habari za vita vya Yoshua na waamuzi, wengine huko wanaiga mbinu za kivita. Biblia hii hii inatumiwa na wanasiasa kutengeza sera zao za kampeni na wanafanikiwa katika hilo, Msome mtu kama kwame Nkrumah raisi wa kwanza wa Ghana,si jinsi alivyoupindua utawala wa kikoloni kwa maandishi ya maandiko.

Biblia hii hii inatumiwa na wachawi na wanajimu, kuwasaidia kufanya uchawi wao: Wasingefahamu kitu kinachoitwa kafara na nguvu iliyokatika damu kama wasingesoma katika biblia..Katika Agano la kale kafara za Wanyama zilikuwa zinafanyika kwaajili ya upatanisho…Asili ya kuvaa hirizi si kutoka kwa wachawi…Wana wa Israeli waliagizwa na Mungu wazivae kwenye vipaji vya nyuso zao, ili kuwakumbusha sheria za Mungu, (vilikuwa ni viboksi vidogo vilivyokuwa vimebeba baadhi ya maneno ya kwenye Torati) lakini Baadaye shetani akaja kuiba huo utamaduni na kutengeneza za kwake kwa lengo la kulogea watu.

Wafanya-biashara na matajiri: Kanuni za kufanikiwa zote wanazitolea katika maandiko,kupanda na kuvuna. Kufanya kazi kwa bidii,n.k. zipo huko, wanazitumia na zinawaletea mafanikio makubwa sana.

Vile vile biblia hii hii inatumiwa na manabii wa Uongo, kutimiza matakwa yao: Wanasoma na kufahamu kuwa ndani ya jina la YESU, kuna uweza wa kipekee, kila kitu kinatii, hivyo hata mtu ambaye alishamkufuru Mungu siku nyingi, anaouwezo wa kulitumia hili jina ili kuamirisha chochote na kikamtii, hata kuamisha milima…hivyo anaweza kutumia fursa hiyo kujipatia mali, au kuwapoteza, kwa kisingizio cha miujiza, na anafanikiwa kabisa, na ndio maana Bwana Yesu alisema wengi watakuja siku ile wakisema Bwana Bwana…, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu. (Mathayo 7:21).

Lakini pia biblia hii hii inatumiwa na watu wengine, na inawapa UZIMA WA MILELE.

Unaweza ukaona hapo, jinsi Biblia inavyofungua milango ya mambo mengi, hata yale maovu, lakini sio milango yote mtu akiingia kwa kupitia biblia inamletea mwisho mwema. Na ndio maana ukisoma maneno ya kwanza kabisa Bwana Yesu aliyoyahubiri ni haya, TUBUNI, KWA MAANA UFALME WA MBINGUNI UMEKARIBIA(Mathayo 4:17)..Na habari zake zote zilikuwa zinalenga ufalme wa mbinguni, kama ukitafuta mahali Bwana Yesu anakufundisha utajiri na mafanikio ya kidunia nataka nikuambie unaweza ukavunjika moyo, zaidi ya yote watu waliojaribu kumfauta kujaribu kumuuliza kuhusu mambo kama hayo aliishia kuwaambia “Uzima wa mtu haupo katika mwingi wa vitu alivyonavyo”(Luka 12:15).

Alikuwepo kwa lengo moja tu la msingi, nalo ni kumpa mtu uzima wa milele. Na wote waliomfuata waliupokea bali waliomkataa hawakaupata bali walipata sehemu ya vipengele vingine katika maandiko.,Leo hii usifurahie na kusema biblia inahimiza hichi ninachokifanya..ukadhani kuwa upo sahihi wakati wote katika hiyo njia…Unapaswa ujiulize je! matokea ya hichi ninachokifanya mwisho wake ni nini?,..Ni uzima wa milele au Mauti, au huna-uhakika?. Ikiwa ni mauti au huna-uhakika, hata kama kuna vifungu vinakusapoti, achana nacho, tafuta kilicho cha msingi kwanza, na biblia imeshaturahisishia kufahamu kilicho cha msingi, nacho ni YESU KRISTO..

Yohana 14:6 “Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.”

Ni heri ukakifanya hicho, lakini huku nyuma jambo la msingi la wokovu wako na uzima wa milele lipo pamoja na wewe, hiyo haina shida kabisa,lakini unaacha mambo ya wokovu na habari za kwenda mbinguni, unasema biblia inaniambia hivi au vile …Kumbuka Yesu anasema “hapa yupo aliye mkuu zaidi ya Sulemani”.

Hivyo kwa kumalizia ni vizuri tukajua jinsi ya kuyavunja vunja maandiko na kuchagua vile vilivyo vya muhimu kwanza, ambavyo ni vya UFALME WA MBINGUNI NA HAKI YAKE NA HIVYO VINGINE VILIVYOSALIA TUTAZIDISHIWA tu Bwana ameahidi hilo, yeye si mwongo. Tunajua hizi ni nyakati za kumalizia, Kristo yupo karibuni kurudi kushinda hata sisi tunavyoweza kufikiria..Ikiwa utasikia unyakuo umepita leo na wewe umebaki utakuwa katika hali gani?. Kumbuka atakayeona uchungu zaidi sio mlevi, au jambazi, atakayeona uchungu ni Yule mkristo aliye vuguvugu ambaye aliitupilia injili za wokovu na kwenda mbinguni akageukia injili za namna nyingine za faraji, ambazo thawabu zake zinaishia hapa hapa duniani…siku hiyo huyo ndio atakayeomboleza..Kwasababu alidhani kuwa ndio njia aindeayo uzimani..Lakini mwisho wake umekupeleka kuingia katika dhiki kuu.

Utasema siku ile, Hatukupata mali kwa jina lako Bwana?, hatukufunguliwa matumbo yetu yaliyokuwa tasa kwa jina lako?, hatukufungua biashara nzuri kwa unabii wako?.nk Ni kweli mambo hayo yote uliyafanya kwa jina la Yesu lipitalo majina yote na lifungualo vifungo vyote, lakini siku ile Bwana atasema ondokeni kwangu! Kwanini? kwasababu jina hilo ulipaswa ulitumie pia kukuletea wokovu wako wa milele, si tu vitu vya ulim:wengu huu vinavyopita, jina hilo ulipaswa pia ubatiziwe kwalo, kulingana na Matendo 2:38, Matendo 8:16, Matendo 19:5 na Matendo 10:48. ili upate ondoleo la dhambi zako na upokee kipawa cha Roho Mtakatifu..Umepata fahari zote na ulimwengu mzima kwa jina hilo lakini umekosa uzima kwa jina hilo, itakufaidia nini?.

Jihadhari na njia zinazoonekana ni nzuri, zinazopendwa na kufuatwa na wengi kwa kivuli cha biblia, nyingi zinaelekea upotevuni. kumbuka njia ni nyembamba ielekeayo uzimani

Ubarikiwe sana.Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine. jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

IKO NJIA IONEKANAYO KUWA SAWA MACHONI PA MTU.

NJIA KUU YA KUINGIA KATIKA ULE MJI.

NJIA MUNGU ALIYOIWEKA KWA KILA JAMBO

NJIA YA MSALABA

NJIA YA BWANA INATENGENEZWA WAPI?


Rudi Nyumbani

Print this post