Yusufu alipochukuliwa Misri alikuja kuwa mtu mkuu, kama tunavyosoma katika biblia, lakini kilichomtofautisha yeye na ndugu zake mbele za Mungu, sio ule ukuu aliokuwa nao, wala sio kile cheo alichokipata, hapana, bali ni mahali ambapo moyo wake ulikuwepo pindi alipokuwa Misri, utaona japokuwa aliishi kule kwa miaka mingi sana, tangu akiwa kijana mdogo kabisa, lakini moyo wake wote ulikuwa katika nchi ya ahadi ya baba zake, na ndio maana utaona alipokaribia kufa aliwaambia wana wa Israeli, kuwa siku watakapopandishwa kutoka katika nchi ya Misri na Mungu, basi mifupa yake wasiiache kule, bali waibebe mpaka nchi ya kaanani.
Kutoka 13:19 “Musa akaichukua ile mifupa ya Yusufu pamoja naye; maana, alikuwa amewaapisha sana wana wa Israeli, akisema, Mungu hana budi atawajilia ninyi; nanyi mtaichukua mfupa yangu kutoka hapa pamoja nanyi’.
Tofauti na wale watoto wengine 11 wa Yakobo, japokuwa walikaribishwa tu Misri, hawakuwepo kule maisha yao yote, lakini walipofika, waliishi kama ndio nyumbani kwao, mawazo ya kurudi Kaanani hayakuwepo, na ndio maana hata waliposikia habari za Yusufu kuondolewa mifupa yake, hilo halikuwawazisha nao waseme hivyo, kwasababu uzuri wa Misri ulishawaridhisha mioyo yao.
Utaona hiyo tabia Yusufu aliyokuwa nayo aliirithi kutoka kwa baba yake Yakobo, kwani alipokuwa Misri kwa kipindi kifupi, aliwaambia, atakapokufa wahakiishe hawamziki katika nchi ile, bali katika nchi ya Baba zake walizozikiwa (yaani Kaanani).
Mwanzo 49:29 “Akawaamuru, akasema, Mimi ninakwenda kukusanywa pamoja na watu wangu; mnizike pamoja na baba zangu, katika pango iliyomo shambani mwa Efroni, Mhiti; 30 katika ile pango iliyomo shambani mwa Makpela, iliyo mbele ya Mamre katika nchi ya Kanaani, aliyoinunua Ibrahimu pamoja na shamba kwa Efroni Mhiti, pawe milki yake ya kuzikia. 31 Humo walimzika Ibrahimu, na Sara mkewe; humo wakamzika Isaka, na Rebeka mkewe; nami humo nikamzika Lea”;
Mwanzo 49:29 “Akawaamuru, akasema, Mimi ninakwenda kukusanywa pamoja na watu wangu; mnizike pamoja na baba zangu, katika pango iliyomo shambani mwa Efroni, Mhiti;
30 katika ile pango iliyomo shambani mwa Makpela, iliyo mbele ya Mamre katika nchi ya Kanaani, aliyoinunua Ibrahimu pamoja na shamba kwa Efroni Mhiti, pawe milki yake ya kuzikia.
31 Humo walimzika Ibrahimu, na Sara mkewe; humo wakamzika Isaka, na Rebeka mkewe; nami humo nikamzika Lea”;
Unaona, hicho pia ndicho kilichomtofautisha Yakobo kwa Esau.. sikuzote, wana wa urithi, hawatazami ya hapa, bali wanatazama ya mbele, wanaishi kama wapitaji, na mazingira huwa hayawakwamishi hata kidogo kutokuwaza makao yao ya milele, utajiri hauwakwamishi, vyeo vyao vya muda, haviwafanyi wasahau makao yao halisi, hata hali ngumu za kimaisha haziwakwamishi wasiwaze kurejea nchini mwao siku moja.
Na ndicho utakiona pia kwa Danieli, japokuwa alichukuliwa utumwani Babeli, hadi akawa mtu mkuu katika nchi ile ya kipagani, Lakini kila siku (mara tatu kwa siku) alikuwa haachi kuomba dua juu ya Yerusalemu, madirisha yake yalikuwa yamefunguliwa kuelekea Yerusalemu ilipo, mbali sana, maelfu kwa maelfu ya kilometa, lakini aliiwaza kila wakati na kuiombea kana kwamba alikuwa Israeli. Tofauti na wayahudi wote waliochukuliwa utumwani Babeli kwa wakati ule.(Danieli 6:10)
Utamwona Nehemia naye, japokuwa alikuwa ni mnyweshaji wa Mfalme wa Umedi na Uajemi, lakini akili yake yote, na mawazo yake yote, yalikuwa Yerusalemu, akawa anaulizia habari za mji na hekalu linaendeleaje kila wakati, hadi siku moja aliposikia hali ya mji sio nzuri, kuta zake zimeharibiwa, alilia na kufunga na kuomboleza kwa muda mrefu (Nehemia 1)
Watu kama hao wanaonyesha ni kama kwa bahati mbaya tu walikuwepo katika nchi ya ugenini, wengine walitumainia kabla hawajafa wataiona Yerusalemu, lakini mpaka wanakufa hawakuiona, lakini mioyo yao ilikuwa huko.
Waebrania 11:13 “Hawa wote wakafa katika imani, wasijazipokea zile ahadi, bali wakaziona tokea mbali na kuzishangilia, na kukiri kwamba walikuwa wageni, na wasafiri juu ya nchi. 14 Maana hao wasemao maneno kama hayo waonyesha wazi kwamba wanatafuta nchi yao wenyewe. 15 Na kama wangaliikumbuka nchi ile waliyotoka, wangalipata nafasi ya kurejea.”.
Waebrania 11:13 “Hawa wote wakafa katika imani, wasijazipokea zile ahadi, bali wakaziona tokea mbali na kuzishangilia, na kukiri kwamba walikuwa wageni, na wasafiri juu ya nchi.
14 Maana hao wasemao maneno kama hayo waonyesha wazi kwamba wanatafuta nchi yao wenyewe.
15 Na kama wangaliikumbuka nchi ile waliyotoka, wangalipata nafasi ya kurejea.”.
Swali Na sisi ambao tunasema ni wapitaji hapa duniani (Kizazi cha watakao nyakuliwa) Je siku zote tunaishi maisha ya kuutafakari urithi wetu wa kimbinguni tuliowekewa, Je tunaitafakari hiyo Yerusalemu mpya ya kimbinguni? Au tunaishi tu hapa duniani kama tumefika?
Shughuli za ulimwengu zinatuzidi mpaka hatuyawazi tena mambo ya mbinguni? hatuwezi kusema tupo busy, zaidi ya Yusufu ambaye dunia nzima alikuwa anaihudumia kwa chakula, na isitoshe alikuwa ni waziri mkuu wa taifa kubwa ulimwenguni, lakini aliiwaza Yerusalemu kiasi cha kukataa kuzikwa kwenye nchi isiyo yake..Sisi hatuwezi kuwa bize zaidi ya Danieli na Nehemia ambao wao walikuwa ni wakuu katika nchi ya Babeli na Umedi, lakini walilia usiku na mchana juu ya Yerusalemu mji wao..wengine mpaka wakaenda kuukarabati.
Lakini sisi tunao mji ulio mkuu kuliko yao. Tunapoishi hapa duniani tukumbuke kuwa, biblia inasema, kule hakitaingia kilicho kinyonge, maana yake ni kuwa hawataingia wasiokuwa na mpango nao, hawataingia ambao hawaulizii habari zake sasa, watakaoingia kule ni wale tu waliostahili kuingia humo, Si kila mtu atauingia huo mji wa kimbinguni, haijalishi utasema leo umeokoka,
Hivyo tuanze sasa kuishi maisha ya kama watu waonaomngojea Bwana wao (Luka 12:36), kwasababu muda tuliobakiwa nao ni mchache sana, Siku ya ukombozi wetu imekaribia, Parapanda wakati wowote italia, kisha tutakwenda mbinguni kwenye karamu ya mwana-kondoo, na baada ya hapo utafuata utawala wa miaka 1000, wakati huo wote tutakuwa tukijiandaa kwa ajili ya mbingu mpya na nchi mpya na hiyoYerusalemu mpya ishukayo kutoka mbinguni.
2Petro 3:13 “Lakini, kama ilivyo ahadi yake, mnatazamia mbingu mpya na nchi mpya, ambayo haki yakaa ndani yake”.
Ufunuo 21:1 Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita, wala hapana bahari tena. 2 Nami nikauona mji ule mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, umewekwa tayari, kama bibi-arusi aliyekwisha kupambwa kwa mumewe. 3 Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao.
Ufunuo 21:1 Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita, wala hapana bahari tena.
2 Nami nikauona mji ule mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, umewekwa tayari, kama bibi-arusi aliyekwisha kupambwa kwa mumewe.
3 Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao.
Tukose vyote, tupitwe na vyote, lakini tusikose mambo hayo ambayo biblia inasema jicho halijawahi kuona wala sikio kusikia.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA KITABU CHA RUTHU:
WAKATI WA KRISTO KUSIMAMA,UMEKARIBIA SANA.
MAMBO 5 AMBAYO KILA MKRISTO ANAPASWA KUFAHAMU.
VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 2
JE! KUNA UCHAWI KATIKA KUTENDA WEMA?
Rudi Nyumbani:
Print this post