Tofauti na tunavyoweza kudhani, kwamba pale unapoongezeka viwango vya kiroho, Au pale unapopiga hatua moja kwenda nyingine kwa Mungu basi utajitambua, au utapata hisia Fulani ya kitofauti kwamba amehama ulimwengu mmoja na kwenda mwingine, au utahisi nguvu Fulani zimeongezeka ndani yako, Lakini sivyo. Ni ngumu sana kujitambua wewe mwenyewe..Bali mwingine ndiye atakayekutambua.
Tunamwaona Musa aliposhuka kutoka mlimani kuzungumza na Mungu kwa muda wa siku 40, usiku na mchana, hakujua kama lipo badiliko lolote, limetokea katika uso wake.
Lakini aliposhuka tu, mlimani wana wa Israeli ndio waliokuwa wa kwanza kumtambua na kumfunulia siri ambayo hakuijua kwa muda siku zote arobaini alizokuwa anamkaribia Bwana..
Kutoka 34:29 “Hata ikawa, Musa aliposhuka katika mlima Sinai, na zile mbao mbili za ushuhuda zilikuwa mkononi mwa Musa, hapo aliposhuka katika mlima, Musa hakujua ya kuwa ngozi ya uso wake iling’aa kwa sababu amesema naye.
30 Basi Haruni na wana wote wa Israeli walipomwona Musa, tazama, ngozi ya uso wake iling’aa; nao wakaogopa kumkaribia.
31 Musa akawaita; Haruni na wakuu wote wa kusanyiko wakarudi kwake; Musa akasema nao.
32 Baadaye wana wa Israeli wote wakakaribia; akawausia maneno yote ambayo Bwana amemwambia katika mlima Sinai”.
Hii ni kutukumbusha, Mtu uliyeokoka, ukiongeza ukaribu wako kwa Mungu, kwa hatua nyingine, ni ngumu sana kuona kama utukufu wako umeongezeka ndani yako kwa hatua moja zaidi..Mfano unapoongeza kiwango chako cha maombi, utajiona wewe ni yule yule tu, kama ulivyokuwa juzi..Lakini tayari utukufu wako umeongezeka kwa ngazi moja juu Zaidi, isiyoijua au kuihisi wewe.
Unaposema, embu ngoja nianze kujizoesha kwenda mikesha kanisani kila ijumaa, unaweza kujiona upo vilevile tu, lakini ipo hatua kubwa sana umepiga.. Ukitaka kufahamu kuwa umepiga hatua, embu sema sikumoja niache kwenda mikesha, halafu uone, huo ukame utakaouhisi ndani ya nafsi yako, utakavyokuwa.
Unapojilinda kila siku na dhambi, ya uasherati, matusi, wizi, n.k. ni rahisi kutohisi ongezeko lolote, ndani yako, lakini fahamu kuwa utukufu wako umeongezeka sana, wale wa nje ndio watakaokuja kushuhudia, Pamoja na Mungu mwenyewe. Watu wengi wanaishiwa na nguvu njiani, kwasababu wanaona kama bidii wanayoizidisha kwa Mungu, haiwarejeshei, badiliko kubwa ndani yao, kama wanavyotarajia.
Kumbuka huwezi kuuona uso wako..Ndivyo ilivyo nasi katika roho, hatuwezi kujiona wenyewe ndani yetu jinsi tunavyokuwa kiroho..Lakini walio nje ndio watakaotuona, hata kama hawatosema.
Ufalme wa Mungu ni kama mbegu, inayotupwa katika Shamba, ambayo biblia inasema, inakua kwa jinsi asivyojua mtu, Lakini mwisho wa siku ghafla tu, inatoa yenyewe matunda
Marko 4:26 “Akasema, Ufalme wa Mungu, mfano wake ni kama mtu aliyemwaga mbegu juu ya nchi;
27 akawa akilala na kuondoka, usiku na mchana, nayo mbegu ikamea na kukua, asivyojua yeye.
28 Maana nchi huzaa yenyewe; kwanza jani, tena suke, kisha ngano pevu katika suke.
29 Hata matunda yakiiva, mara atapeleka mundu, kwa kuwa mavuno yamefika”.
Hivyo, usihangaike sana, kujichunguza chunguza, kwasababu hutaona lolote. Lakini fahamu kuwa kila hatua unayoiongeza kwa Mungu, ina utukufu mkubwa sana kwako. Ndugu Usipunguze maombi, hata kama huoni chochote, usipunguze kushuhudia wengine Habari njema, usipunguze kumtolea Mungu kwa mali zako, hata kama huoni marejesho yoyote kutoka kwake, usipunguze kwenda ibadani na kuhudhuria mikesha. Kinyume chake ndio uzidishe, kuyatenda hayo.
Mwisho wa siku utukufu wako utaangaza sana kama ilivyokuwa kwa mtumishi wa Mungu Musa, hadi wengine watakuogopa kwa jinsi ulivyomkaribia Mungu sana.
Ubarikiwe na Bwana.
Tafadhali shea na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi// Ushauri/ Maswali/Whatsapp.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
UTAJI ULIOKUWA JUU YA USO WA MUSA.
TUTAWEZAJE KUMZALIA MUNGU MATUNDA?
DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.
About the author