DHABIHU ZA ROHO NI ZIPI? (1Petro 2:5)

DHABIHU ZA ROHO NI ZIPI? (1Petro 2:5)

SWALI: Dhabibu za roho ni zipi, zinazotajwa kwenye maandiko haya?

1Petro 2:5  “Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo”.

Dhabihu ni sadaka za kuteketezwa zilizokuwa zinatolewa katika agano la kale. Hizi zilikuwa na lengo la kufanya upatanisho wa makosa ya watu, kwamfano  alipochinjwa mwanakondoo, au ng’ombe au mbuzi, au njiwa (Walawi 1:3-16) na kuteketezwa kisha ule moshi wake ukapanda juu basi huo ndio unakuwa  uthibitisho wa sadaka yake kukubaliwa. Na mtu huyo makosa yake yanakuwa yamefunikwa kwa muda.

Hivyo katika agano jipya pia tunayo dhabihu yetu, ambayo kwa kupitia hiyo tunapokea upatanisho wa makosa yetu, na dhabihu yenyewe ni YESU KRISTO mwokozi wetu ambaye yeye kama mwanakondoo alichinjwa kwa ajili yetu ili sisi tupokee ondoleo la dhambi, hivyo yoyote ambaye yupo sasa ndani ya Kristo Yesu tayari ameshamtolea Mungu dhabihu ya upatanisho wake.

Lakini tunapokuwa ndani ya Kristo, hatuna budi kuonyesha kuwa tumekombolewa na yeye, kwa matendo yetu. Hivyo ni lazima tutaonyesha tabia kama za mtu anayekwenda kutoa dhabihu mbele za Bwana, na sio kama za mtu aliyejiamulia tu. Na tabia zenyewe ndio hizo zinazojulikana  kama dhabihu za roho ambazo sisi tunazitoa.

Zifuatazo ndio dhabihu za roho  zenyewe.

1) Shukrani

Zaburi 50:14 Mtolee Mungu dhabihu za kushukuru; Mtimizie Aliye juu nadhiri zako.

Zaburi 50:23 Atoaye dhabihu za kushukuru, Ndiye anayenitukuza. Naye autengenezaye mwenendo wake, Nitamwonyesha wokovu wa Mungu.

Ukiwa mtu wa shukrani kwa Mungu, Ni kuonyesha kuwa umetambua kazi ya msalaba ndani yako. Na shukrani hizi ni lazima ziwe katika Sifa za kinywa chako, pamoja na matoleo kwa kile Mungu anachokubariki. Ni muhimu sana wewe kama mkristo kuwa mtu na namna hii. Wote waliokwenda kutoa sadaka za namna hii mioyo yao ilijaa shukrani kwa Mungu wao, hawakwenda hivi hivi tu.

2) Moyo uliopondeka

Zaburi 51:16 Maana hupendezwi na dhabihu, au ningeitoa, Wewe huridhii sadaka ya kuteketezwa.  17 Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika; Moyo uliovunjika na kupondeka, Ee Mungu, hutaudharau.

Moyo uliopondeka ni moyo wa toba, wa majuto ya dhambi, ambao unakufanya utaabike moyoni mwako kwasababu ya makosa yaliyotendeka, na hivyo unakufanya uwe mnyenyekevu sana mbele za Mungu.

Mtu mwenye moyo huu, mbele za Mungu anaonekana kama amejitambua yeye ni mkosaji, na hivyo Yesu amefanyika upatanisho kwa ajili yake, tofauti na mtu ambaye mambo yote kwake ni sawa, hata baada ya kuona kosa bado anaukaza moyo wake, kujifanya kama hana hatia yoyote mbele za Mungu. Yatupasa wakati wote tuwe watu wa kujinyenyekeza mbele za Mungu. Watu wa kutaka rehema zake.

3) Kuitoa miili yetu;

Warumi 12:1  “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana. 2  Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.

Unapoutunza mwili wako mbali na mambo ya kidunia, kisha ukaufanya utumike kwa ajili ya kazi ya Mungu, hapo ni sawa na unamtolea Mungu dhabihu yenye kupendeza, yaani unaenda mbele za Mungu na badiliko, unasema msalaba mbele, udunia nyuma. Lakini ukiwa unavaa ovyo ovyo, unazini, unatumia mikorogo, unajichora mwili wako, unakunywa pombe, unavuta sigara, unatoa mimba, hapo hufanyi ibada yoyote mbele za Mungu. Kwasababu lazima ufahamu kuwa miili yetu ni hekalu la Roho Mtakatifu (1Wakorintho 3:16).

Hivyo, wewe ambaye umeokoka, zangatia mambo hayo matatu, SHUKRANI, MOYO ULIOPONDEKA, NA KUUTOA MWILI WAKO. Wokovu wako utakuwa na maana sana mbele za Mungu.

Bwana akubariki.

Je! Umeshaokoka?. Kama bado wasubiri nini? Unatambua kuwa haya ni majira ya siku za mwisho, na Kristo amekaribia kurudi?.  Dalili zote zimeshatimia, Embu tubu sasa mgeukie Kristo akuokoe uwe upande salama. Ikiwa upo tayari kufanya hivyo, basi waweza fungua hapa kwa ajili ya mwongozo was ala hiyo.>>> KUONGOZWA SALA YA TOBA

Bwana akubariki.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Dhabihu ni nini?

KUTII NI BORA KULIKO DHABIHU.

Mahali pa juu palikuwa ni wapi kama tunavyosoma katika biblia?

Swali: Kurushwa upesi kunakozungumziwa katika Danieli 9:21 ndio kupi?

Mnanaa, Bizari na Jira ni viungo gani? (Mathayo 23:23)

Sadaka ya Moyo ipoje? (Walawi 22:21).

Kwanini samaki wasio na mapezi na magamba hawakuruhusiwa kuliwa?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments