UFANYE WEMA WAKO UTAJWE KWA UZURI.

UFANYE WEMA WAKO UTAJWE KWA UZURI.

Neno la Mungu linatufundisha kuushinda “Ubaya kwa wema”..

Warumi 12:20  “Lakini, Adui yako akiwa na njaa, mlishe; akiwa na kiu, mnyweshe; maana ufanyapo hivyo, utampalia makaa ya moto kichwani pake.

21  USISHINDWE NA UBAYA, BALI UUSHINDE UBAYA KWA WEMA”.

Maana yake ukifanyiwa ubaya, usilipe ubaya, bali Lipa “Wema”, ili yule aliyekufanyia ubaya ajione yeye ndiye mwenye makosa na hivyo baadae arejee na kutubu.

Lakini pia biblia hiyo hiyo inazidi kutufundisha kuwa WEMA wetu pia usitajwe kwa UBAYA

Warumi 14:16 “Basi, huo wema wenu usitajwe kwa ubaya”.

Kumbe pia “Wema” unaweza kutajwa kwa “Ubaya”

Unaweza kweli usirudishe Ubaya kwa ubaya, na ukarudisha wema kwa ubaya…lakini bado huo wema ulioufanya ukaonekana ni “mbaya”.

Hivyo ni lazima pia “tuutakase wema wetu”.. Hata Maji ijapokuwa yanaweza kutumika kusafisha nguo, lakini nayo pia yanaweza kuchafuka.. hata sabuni pia ijapokuwa inatumika katika kutakasa, lakini nayo pia inaweza kuchafuka!..

Vile vile na “Wema” ijapokuwa ni mzuri na unahitajika lakini pia unaweza pia Kuchafukana na kuonekana “mbaya”.

Sasa ni Kitu gani kinchouchafua Wema wetu?

      1. Nia

Nia ni kitu kimoja kinachoweza kuufanya Wema wetu usiwe tena wema bali UNAFIKI… Kwamfano utaona mtu anaweza kufanya “wema”..lakini Nia yake ni ili  ASIFIWE na watu, au aonekane ni mtu wa kidini, aliyesimama kiimani! Na wala ndani yake hamna upendo wala dhamiri njema!. Sasa wema wa namna hii ndio “Wema unaotajwa kwa Ubaya”.

Mathayo 23:28 “Vivyo hivyo ninyi nanyi, kwa nje mwaonekana na watu kuwa wenye haki, bali ndani mmejaa unafiki na maasi”.

     2. Roho ya KISASI

Roho ya kisasi ni ile hali ambayo mtu atarudisha wema… Lakini moyoni anawaza kisasi (kwa kusema Mungu ampige).. Ndugu ikiwa umefanyiwa ubaya, epuka kauli hii “Namwachia Mungu atampiga”… Kauli hii inaonekana ni njema sana na ya busara, lakini nataka nikuambie, busara yake haijakamilika (hiyo kauli ina kasoro).. Ni kweli umefanya wema, baada ya wewe kutendewa mabaya,

Sasa kuliko umtakie mabaya kutoka kwa Mungu ni heri umwombee rehema ili yamkini Mungu amsamehe (hiyo itakupandisha thamani sana mbele za Mungu, kwasababu sifa ya Kwanza ya Mungu ni rehema kabla ya visasi).. …tunalithibitisha vipi hili kibiblia?

Mithali 24:17 “Usifurahi, adui yako aangukapo; Wala moyo wako usishangilie ajikwaapo,

18 Bwana asije akaliona hilo, likamkasirisha; Akageuzia mbali naye hasira yake”

Kama Bwana ataamua kumlipa kisasi kwa aliyoyafanya kwako basi hiyo ni juu yake (Bwana) na si juu yako wewe, kwani kisasi ni juu yake yeye (Warumi 12:19-2), na hatuwezi kumshauri juu ya visasi..

kwani kuna waliojaribu kumshauri na ikashindikana…wapo waliomwombea kisasi Sauli kwa kuwaua watakatifu wa Kristo, lakini kisasi walichomwombea au walichomtakia (kwamba apigwe na Mungu) kiligeuka kuwa Wokovu kwa Sauli na Kuwa Paulo Mtume, kwahiyo masuala ya visasi si juu yetu sisi wakristo, hiyo ni juu ya Mungu, tunachopaswa kufanya ni kufanya wema na kuwaombea rehema maadui zetu, kwamba Bwana awasamehe, mengine tunamwachia yeye..

Jambo hili ni kama mtihani mkubwa lakini ndio NENO LA MUNGU!!..wala sio “ulemavu wa akili, wala sio unyonge”..bali ni Neno la Mungu lenye nguvu na linaloishi…

Luka 6:27 “Lakini nawaambia ninyi mnaosikia, Wapendeni adui zenu, WATENDEENI MEMA wale ambao wawachukia ninyi,

28 wabarikieni wale ambao wawalaani ninyi, waombeeni wale ambao wawaonea ninyi.

29 Akupigaye shavu moja, mgeuzie la pili, naye akunyang’anyaye joho yako, usimzuilie na kanzu.

30 Mpe kila akuombaye, na akunyang’anyaye vitu vyako, usitake akurudishie”.

Bwana atusaidie… WEMA WETU UTAJWE kwa uzuri na si kwa Ubaya.

Maran atha!

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

UFANYE WEMA WAKO KATIKA MAARIFA.

AINA SABA (7), ZA SIFA KIBIBLIA.

KISASI NI JUU YA BWANA.

Nini maana ya ‘kuhuluku’ kama tunavyosoma katika biblia?

TEMBEA NDANI YA SUKOTHI YAKO.-Maafundisho maalumu kwa watumishi

Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Devis Julius administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments