Jibu: Ni vizuri kufahamu kuwa kuna vitu vimeumbwa na Mungu na kuna vitu vimeumbwa na viumbe wa Mungu.
Kwa mfano Mungu hajaumba gari, wala treni, wala pikipiki. Gari tunaloendesha limeumbwa na wanadamu, vile vile hajaumba ndege, wala kiti, mambo hayo yote ni sisi wanadamu ndiyo tuliyoyatengeneza… tumeichukua malighafi hii iliyoumbwa na Mungu, tukaichanganya na malighafi ile, tukatengeneza gari. N.k
Vile vile Mungu hajaumba chapati tunazokula wala maandazi, wala pilau.. alichokiumba ni malighafi hizo, yaani unga, mafuta, chumvi na maji.. Kwa utashi wetu sisi wanadamu, ndio tukachukua malighafi hizo na kuzichanganya pamoja na kuzichoma ndipo vikatokea vyakula hivyo tunavyokula kama maandazi au chapati au chakula kingine chochote.
Kadhalika Mungu hajaumba dhambi, wala matatizo wala shida.. Mambo hayo ni sisi tumeyatengeneza wenyewe, kupitia malighafi au vitu ambavyo Mungu kaviumba. Tunapochukua ukweli na kuuchanganya na vitu vingine na kuugeuza hapo ndipo unapozaliwa uongo!.. Ndio DHAMBI YENYEWE!!
Kitendo cha kukutana kimwili si kibaya lakini kinapofanyika wakati usio sahihi, au na mtu asiyesahihi kinageuka kuwa uzinzi au uasherati, Hivyo uasherati ni kitu sahihi kilichochanganywa na muda usio sahihi na mtu asiyesahihi. Kwahiyo Mungu hajaumba uasherati, bali ni watu ndio walioumba uasherati.
Hivyo dhambi zote zimeumbwa na wanadamu pamoja na shetani na malaika zake. Na si Mungu aliyeziumba kwasababu yeye ni mtakatifu, na wala hachangamani na uchafu. Ndio maana anaichukia dhambi.. Kwasababu ingekuwa ni yeye kaiumba asingeichukia.. Mtu hawezi kuchukia kitu alichokitengeneza yeye mwenyewe..
Na kila siku dhambi zinaendelea kuumbwa na wanadamu.. Ndio maana biblia inasema siku za mwisho maasi yataongezeka, maana yake kila siku maovu mapya yanazaliwa..Ndio maana katika kilele cha maovu haya Bwana lazima aiangamize hii dunia.
Hivyo hatuna budi kukaa mbali na dhambi, kwasababu Mungu wetu ni mtakatifu na wala hachangamani na dhambi.
Mathayo 5:48 “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu”.
Na hatuwezi kuishinda dhambi tukiwa nje ya agano la mwanae mpendwa Yesu. Tunaishinda dhambi na kuacha kuiumba kwa kuungama dhambi zetu zote, kwa kumaanisha kutozitenda tena, na kisha kwenda kubatizwa ubatizo sahihi na kupokea Roho Mtakatifu.
Maran atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Nini maana ya “Bwana Yesu ni mzaliwa wa kwanza wa waliokufa?”(Ufunuo 1:5)
Ipo faida ya kufuata mambo yako na kutojishughulisha na mambo ya wengine!.. Lakini pia ipo hasara kubwa ya kutojishughulisha na mambo ya wengine na kufuata mambo yako tu!. Faida ya kufuata mambo yako ni kwamba utakuwa huru katika mambo yako, na hautaishi kwa wasiwasi wala hofu!…kwasababu utakuwa hufuatilii mambo ya wengine, na wala hushirikiani nao, hivyo hutakuwa na mtu wa kushindana naye wala kujilinganisha naye..Kwahiyo utaishi maisha ya uhuru sana..
Lakini pamoja na hayo kuna hatari kubwa sana ya kuishi maisha ya namna hiyo, Maana yake yanapozidi sana, kiasi kwamba unakuwa umefunga milango yote, umejitenga na hutaki kufuatilia chochote cha nje! Ipo hatari!!
Leo tutajifunza kupitia biblia, mojawapo ya hatari ya maisha ya namna hiyo..
Katika maandiko tunausoma mji mmoja ulioitwa Laisha, mji huu ulikuwepo kaskazini mwa Taifa la Israeli, kabla haujatwaliwa na Israeli, ulikuwa unaitwa hivyo Laisha, lakini mji huu ulikuwa ni wa kipekee sana, kwanza ulikuwa ni mji ambao umejitenga, upo mbali sana na miji mingine, na pili ulikuwa ni mji ambao haukushirikiana na miji mingine, hivyo watu wake walikuwa wanafuata mambo yao tu!, wanafanya kazi kwaajili ya kuuendeleza mji wao, na wala hawakuwa na shughuli na mataifa mengine.. Hiyo ikawafanya wafanikiwe sana, kwasababu mambo yao yote hawakuyaendesha kwa hofu wala kwa mashindano.. Na zaidi ya yote, wakajiwekea utaratibu kuwa watu wote ni sawa katika ile jamii, hakuna wa kumtawala mwenzake wala kunyanyasana..
Lakini biblia inatuambia uharibifu wake ulikuja ghafla bila wao kutegemea..na mji mzima uliangamizwa pasipo msaada, kwasababu walikuwa mbali na miji mingine ambayo pengine ingewasaidia, na vile vile haikuwa na mahusiano na mji wowote ule.. ni wao kama wao..
Tusome habari hiyo kidogo katika maandiko.. (Zingatia vipengele vilivyoainishwa kwa herufi kubwa)
Waamuzi 18:7 “Ndipo hao watu watano wakaenda zao, WAKAFIKA LAISHA, wakawaona wale watu waliokuwamo ndani yake, jinsi walivyokaa salama salimini kwa mfano wa walivyokaa hao Wasidoni, WENYE STAREHE NA HIFADHI, kwa maana hapakuwa na mtu katika nchi hiyo aliyekuwa na amri, aliyeweza kuwatweza katika neno lo lote, nao walikuwa wa mbali na hao Wasidoni, WALA HAWAKUWA NA SHUGHULI NA MTU YE YOTE.
8 Kisha wakawarudia ndugu zao huko Sora na Eshtaoli; ndugu zao wakawauliza; Haya, mna habari gani?
9 Wakasema, Haya, inukeni, twende tukapigane nao; KWA MAANA TUMEIONA HIYO NCHI NAYO NI NCHI NZURI sana; nanyi, je! Mwanyamaa tu? Msiwe wavivu kwenda, na kuingia, ili mpate kuimiliki nchi hiyo.
10 Hapo mtakapokwenda mtawafikilia WATU WAKAAO SALAMA SALIMINI, na hiyo nchi nayo ni kubwa; kwa kuwa Mungu ameitia mikononi mwenu; ni mahali ambapo hapana kupungukiwa na kitu cho chote kilicho duniani.
11 Basi wakatoka hapo watu mia sita waliovaa silaha za vita, wa jamaa ya Wadani, kutoka Sora, na kutoka Eshtaoli……………………………………
27 Nao wakakitwaa hicho alichokuwa amekifanya Mika, na kuhani aliyekuwa naye nao wakafikilia Laisha, KWENYE WATU WALIOKUWA WENYE STAREHE NA HIFADHI, wakawapiga kwa makali ya upanga; wakaupiga moto mji wao.
28 WALA HAKUWAKO MWOKOZI, KWA SABABU HUO MJI ULIKUWA NI MBALI SANA NA SIDONI, NAO HAWAKUWA NA SHUGHULI NA MTU AWAYE YOTE; na mji huo ulikuwa katika hilo bonde lililo karibu na Bethrehobu. Nao wakaujenga huo mji na kukaa humo.
29 Wakauita mji jina lake Dani, kwa kuliandama jina la baba yao Dani, aliyezaliwa kwake Israeli; lakini jina la mji huo HAPO KWANZA ULIKUWA UKIITWA LAISHA”.
Umeona?.. Laiti mji huo ungekuwa na mahusiano na miji mingine, labda wangepata mwokozi, na wangeokoka na maangamizi hayo, kwani ingekuwa ni rahisi wao kusaidiwa na majirani zao, lakini maadui zao walipowasoma udhaifu wao kuwa ni watu wanaojiona kuwa hawawezi kuhitaji msaada kutoka kwa mwingine yeyote, ni watu ambao wapo wenyewe wenyewe, ndipo wakapata nguvu!, kwani walitambua hata watakapowavamia hakuna atakayekuja kuwasaidia. Na siku ya maangamizi yao ilipofika, wakaangamia wote!, pamoja na utajiri wao, na fedha zao, na mali zao na kila kitu chao, waliopotea wote.
Hiyo inatufundisha nini?
Umoja ni ulinzi, biblia inasema katika Mhubiri….
Mhubiri 4:12 “ Hata ikiwa mtu aweza kumshinda yule aliye peke yake, wawili watampinga; wala kamba ya nyuzi tatu haikatiki upesi.”
Wakati mwingine unaweza kufikiri kuwa peke yako ndio afya, lakini kinyume chake ndivyo unavyodhoofisha ulinzi wako! Na usalama wako!.. Ni vizuri kutojishughulisha na mambo ya wengine na kufuata mambo yako!.. lakini isizidi sana, kiasi kwamba hata hutaki kuwa na mahusiano na wengine!, hutaki kujifunza kutoka kwao, hutaki kusaidiwa na wao, hutaki kuwasaidia, hutaki kujinyenyekeza kwao, ni wewe kama wewe tu! n.k
Kwasababu huo ubinafsi wako ambao unadhani ni ulinzi kumbe ndio nguvu ya adui yako shetani. Yeye anatamani uendelee kukaa hivyo hivyo bila kuwa na shughuli na mtu mwingine yeyote ili siku atakapokuletea madhara!, ukose msaada. Ni kweli ubinafsi wako utakupa uhuru!, hata unaweza kukupa utajiri, lakini siku ya hautakusaidia siku ya maangamizi..
Hata katika kanisa kitu cha kwanza shetani anachokiua ni Umoja!.. kwasababu anajua ni ngumu kulishambulia kundi kubwa kuliko mtu mmoja mmoja!.. hivyo anachokifanya kwanza ni kuhakikisha analitenganisha kundi, na kutenga mtu mmoja mmoja, hivyo anahakikisha anaweza roho ya kila mtu kufuata mambo yako, na kutojishughulisha na mambo ya wengine.. Na akishafanikiwa hilo, ndipo anaanza kuwamaliza mmoja mmoja.
Ndugu! Usikimbie vikundi vya maombi, na kutafuta kuomba mwenyewe mwenyewe kila mara, ukidhani ndio salama!… Tenga muda wako mwingi wa kusali mwenyewe lakini usiache kukusanyika na wengine katika maombi.
Vile vile usijione kuwa una hekima kwa wewe kutokwenda kanisani kukusanyika na wengine!, kwasababu tu ya vikasoro vidogo vidogo unavyoviona pale!..na huku ukijitumainisha katika kusali mwenyewe ! Bali kinyume chake uogope!… kwasababu upo katika rada ya shetani!!.. Hutadumu muda mrefu, utapotea kabisa..
Yohana 17: 21 “WOTE WAWE NA UMOJA; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma.
22 Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ILI WAWE NA UMOJA KAMA SISI TULIVYO UMOJA.
23 Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ILI WAWE WAMEKAMILIKA KATIKA UMOJA; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi”.
Bwana atubariki.
Kama hujampokea Yesu, mlango wa neema bado upo wazi!.. ila hautakuwa hivyo siku zote, hivyo mpokee Yesu leo akuoshe dhambi zako na kukupa uzima wa milele.
Maran atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?
UNYAKUO.
Unyakuo ni kitendo ambacho Bwana Yesu atawahamisha watakatifu wake, kutoka katika huu ulimwengu na kuwapeleka mbinguni yeye alipo. Kwa mujibu wa biblia Tendo hilo litakuwa ni la ghafla sana, kama vile mtu anafumba macho na kufungua.
Siku hiyo paraparanda ya Mungu italia, ulimwenguni kote, lakini haitasikiwa na watu wote, bali wale watu waliomwamini Yesu hapa duniani, na wale watakatifu waliokufa katika yeye.
1Wakorintho 15:51 “Angalieni, nawaambia ninyi siri; hatutalala sote, lakini sote tutabadilika,
52 kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika”.
Unaona? Siku hiyo, itakuwa ya kipekee sana, Bwana Yesu aliendelea kusema..
Mathayo 24:40 “Wakati ule watu wawili watakuwako kondeni; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa;
41 wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa.
42 Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu”.
Sasa kulingana na majira tuliyopo sasa, dalili zote zinaonyesha Yesu yupo karibu sana kurudi, hatujui pengine ni leo usiku, au kesho au mwezi ujao, lakini kulingana na tabiri zote za kimaandiko, inatuonyesha kuwa siku yoyote Kristo anarudi. Haleluya.
Na kama ikitokea amerudi leo, wewe uliyempokea Yesu, Utaisikia paraparanda hiyo ya Mungu, ikilia. Na ghafla utayaona makaburi ya watakatifu yanafunguka, na wao wakitoka makaburini (Mathayo 27:51-53), kisha baada ya hapo mtakuwa kitu kimoja, na kwa pamoja, mtanyakuliwa mawinguni kumlaki Bwana Yesu ,.
Tendo hilo litakuwa ni la kufumba na kufumbua, na moja kwa moja mtaelekea mbinguni, kule ambapo Yesu alisema amekwenda kutuandalia makao (Yohana 14:1-3). Huko tutakutana na mambo ambayo jicho halijawahi kuona wala sikio kusikia, kutakuwa na furaha isiyo na kifani, tutakapoingia katika hiyo karamu ya mwanakondoo. Ni mahali ambapo hata mmoja wetu hapaswi kukosa.
Ufu 19:9 “Naye akaniambia, Andika, Heri walioalikwa karamu ya arusi ya Mwana-Kondoo. Akaniambia, Maneno haya ni maneno ya kweli ya Mungu”.
Lakini ikiwa wewe hujaokoka, parapanda hiyo ikilia, siku hiyo hutafahamu au kusikia chochote, kinyume chake, utashangaa tu, fulani ambaye aliyempokea Yesu ulikuwa naye sekunde chache tu nyuma, ametoweka, uliyekuwa unalima naye shambani humuoni, mume/mke uliyekuwa umelala naye ameondoka na milango imefungwa. Hapo ndipo utakapojua Kristo amesharudi na kulinyakua kanisa lake.
Vilevile ikiwa utakufa leo katika hali ya dhambi na bado Bwana hajarudi. Siku ya unyakuo ikifika, hautafufuliwa badala yake utaendelea kubaki hapo makaburini mpaka siku ya hukumu ya mwisho ambayo utafufuliwa na kuhukumiwa kisha kutupwa katika lile ziwa la moto (Ufu 20:11-15).
Ndugu yangu, Ipo sababu kwanini leo umekutana na ujumbe huu, wakati tunaoishi ni wakati wa nyongeza tu, Yesu hajarudi bado ni kusudi kwamba wewe ambaye hujampokea, umpokee sasa, vinginevyo angekuwa amesharudi siku nyingi sana. Anakusubiria wewe ambaye pengine ni mmoja wa wale kondoo wa mwisho mwisho, utubu dhambi zako uokoke.
Hataki hata mmoja wetu aikose hiyo karamu aliyokwenda kutuandalia mbinguni kwa miaka 2000 sasa. Haijalishi wewe ni dini gani au dhehebu gani, Yesu anawapokea watu wote, anawapa tumaini jipya, kisha anawaandaa kwa ajili ya kuwakaribisha nyumbani kwake mbinguni.
Hivyo tubu leo, kisha uwe tayari kubatizwa kwa ajili ya kuukamilisha wokovu wako, Na baada ya hapo yeye mwenyewe atakupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu. Hivyo kama utahitaji msaada wa kuokoka/kubatizwa, basi wasiliana nasi kwa namba hizo mwishoni mwa kipeperushi hichi, au tafuta kanisa la kiroho lililo hai, wakusaidie.
Bwana akubariki.
Neno Ahera limeonekana mara tatu tu katika biblia, limeonekana katika kitabu cha 1Wafalme 2:6 na 9 na katika kitabu cha Wimbo ulio bora 8:6, mara zote hizi Neno hilo limetumika likimaanisha “kaburi”. Hivyo Ahera maana yake ni kaburi.
1Wafalme 2:5 “Na zaidi ya hayo, umejua alivyonitenda Yoabu, mwana wa Seruya, yaani, alivyowatenda majemadari wawili wa majeshi ya Israeli, Abneri, mwana wa Neri, na Amasa, mwana wa Yetheri, ambao aliwaua, na kuimwaga damu ya vita wakati wa amani, akautia damu ya vita mshipi uliokuwa viunoni mwake, na viatu vilivyokuwa miguuni mwake.
6 Kwa hiyo ufanye kama ilivyo hekima yako, wala usimwachie mvi zake kushukia AHERA KWA AMANI”.
Ahera inatukumbusha kuwa kuna mwisho wa maisha haya… hivyo hatuna budi kutengeneza maisha yetu, kabla hatujaingia kaburini… Kwasababu baada ya kifo kitakachokuwa kimebakia kwetu ni hukumu..
Waebrania 9:27 “Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu”.
Bwana atujalie tuishi maisha yanayompendeza yeye, angali bado tunaishi.
Maran atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Mahali pa juu palikuwa ni wapi kama tunavyosoma katika biblia?
Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe, karibu katika kuyatafakari maandiko.
Je! Umewahi kujiuliza kwanini biblia inasema upendo una nguvu kama mauti?.
Wimbo ulio bora 8:6 “Nitie kama muhuri moyoni mwako, Kama muhuri juu ya mkono wako; Kwa maana UPENDO UNA NGUVU KAMA MAUTI, Na wivu ni mkali kama ahera. Mwako wake ni mwako wa moto, Na miali yake ni miali ya Yahu”
Upendo wa Mungu kwetu! Unafananishwa na upendo wa Mtu kwa mpenzi wake. Jinsi mwanaume anavyompenda mke wake ndivyo Kristo anavyotupenda sisi. Na mtu anapozama sana katika upendo huwa anakitu kingine kinachofuatana na huo mpendo, na hicho si kingine zaidi ya Wivu!.. hivi vitu viwili ni Pacha!.. vinakwenda pamoja..
Kadhalika Kristo naye analipenda kanisa na sio tu analipenda bali pia analionea wivu. Endapo watu wake aliowapenda wakikengueka na kujitenga naye, basi wivu wake unawaka!, na kuweza kufanya lolote, kama vile mtu aliyesalitiwa na mke wake.
Lakini leo tutajifunza ni kwa namna gani upendo wa Kristo ulivyo na nguvu!.
Hapo biblia inasema “Upendo una nguvu kama mauti”. Maana yake tukiielewa nguvu ya mauti, basi tutaielewa nguvu ya upendo wa Kristo kwetu.
Kama tunavyojua Mtu anayekumbwa na Mauti, anakuwa haishi tena, anakuwa amepotea moja kwa moja, kumbukumbu lake linapotea duniani, hawezi kutenda jambo lolote wala shughuli yoyote ya huu ulimwengu.
Kadhalika mtu anayeingia na kuzama katika pendo la Kristo, ule upendo wa Kristo unamuua na mambo yote ya kidunia.. unamfanya anakufa kwa habari ya dhambi, anapotea kabisa kwenye dira ya mambo ya ulimwengu huu, anakuwa katika umoja na Kristo, ambao hakuna mtu anayeweza kuukaribia.. na hakuna kitu chochote kinachoweza kumtenga yeye na Kristo..
Warumi 8:33 “Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki.
34 Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea.
35 Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga?”
Je na wewe leo umeingia katika pendo la Mwana wa Mungu??..
Kumbuka huwezi kuushinda ulimwengu kama hutakufa kwa habari za uliwengu.
Yohana 15:9 “Kama vile Baba alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi, kaeni katika pendo langu.
10 Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake.
11 Hayo nimewaambia, ili furaha yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu itimizwe”.
Ni kwanini leo hii huwezi kushinda ulevi?, ni kwasababu pendo la Kristo halijaingia ndani yako, ambalo lingeweza kuua nguvu yote ya ulevi, vile vile kwanini leo huwezi kuacha uzinzi, ukahaba, wizi, uuaji n.k?.. ni kwasababu bado Pendo la Kristo halijamiminwa ndani yako, ambalo lingekufanya ufe kwa habari ya dhambi ndio maana bado ulimwengu una nguvu juu yako.
Lakini habari njema ni kwamba, Kristo mpaka sasa yupo hai na anaokoa!.. utakapompokea kwa kumaanisha kutubu na kuacha dhambi, basi ataingia moyoni mwako, na lile pendo lake litaua kazi zote za ibilisi ndani yako, na kukuacha huru, na hutaona uzito wala ugumu katika kuishi maisha yanayompendeza Mungu. Kumbuka “UPENDO UNA NGUVU KAMA MAUTI”.
Hivyo ukitaka mauti katika kazi zote za ibilisi juu ya maisha yako, zama katika pendo la Kristo. Kwasababu Kristo mwenyewe hawezi kuruhusu wewe usumbuliwe na mambo ya ulimwengu huu!, hivyo lazima aue kazi zote za ibilisi ndani yako..
Kama hujaingia katika pendo hili, basi tubu leo kwa kumaanisha kuziacha dhambi zako zote, na kisha tafuta ubatizo sahihi, ambao ni ule wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo. Na kwasababu Kristo ni mwenye upendo, atakuingiza katika pendo lake na kukupa uzima wa milele.
Maran atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp
Mada Nyinginezo:
Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo, Karibu tena tuyatafakari maneno ya uzima.
Kuna wakati Mtume Paulo alifunuliwa siri nyingi sana zimuhusuzo Bwana wetu Yesu Kristo, hususani zile zinazomlinganisha yeye na Melkizedeki. Na hamu yake ilikuwa ni kanisa zima lifahamu siri hizo, lakini alikumbana na kipingamizi kikubwa, ambacho kilimfanya asiweze kuzieleza zote, na kipingamizi chenyewe ni ule UVIVU WA WATU KUSIKIA.
Waebrania 5:10 “kisha ametajwa na Mungu kuwa kuhani mkuu kwa mfano wa Melkizedeki.
11 Ambaye tuna maneno mengi ya kunena katika habari zake; na ni shida kuyaeleza kwa kuwa mmekuwa wavivu wa kusikia”.
Embu tengeneza picha kama Paulo angeendelea, kumwelezea Melkizedeki kama alivyokuwa anamwelezea katika sura hizo chache za kitabu cha waebrania, ungefahamu mangapi ya ziada yamuhusuyo Bwana Yesu, kuliko hayo unayoyajua sasa hivi, Lakini asingeweza kuwaeleza kwasababu hata yale ya mwanzo machache tu, bado watu walikuwa ni wavivu wa kufuatilia..Hivyo kama mwalimu asingeweza kufundisha hesabu za maumbo wakati hesabu kujumlisha na kutoa bado watu hawazijui.
Hata sasa tabia hii, ipo miongoni mwa watakatifu. Ni rahisi kusikia mkristo fulani akisema tena kwa ujasiri, “Aah huu ujumbe ni mrefu siwezi kusoma” lakini wakati huo huo anaweza kumaliza vitabu vitatu vya hadithi, na asione shida. Anaweza kusikiliza mahubiri dakika 10, lakini muvi za kidunia, akakesha nazo usiku kucha.. Anaweza akatumia dakika 2 kutazama video ya ki-Mungu, lakini akatumia saa 6 kuchat Instagramu, na Facebook. Huyo ni mkristo, hatuzungumzii mpagani. Na bado atagemea Mungu atajidhihirisha kwake zaidi ya hicho kiwango anachomjua.
Ndugu, kila siku Bwana anataka tujae maarifa, ili tuweze kuishi kulingana na viwango anavyovitaka yeye kwetu. Mtume Paulo japokuwa alipewa mafunuo makubwa sana yamuhusuyo Mungu, na kule mbinguni, mpaka Mungu akamwekea mwiba maishani mwake ili asijisifu kupita kiasi kwa wingi wa mafunuo hayo (2Wakorintho 12:7).. Lakini bado hakuwa mvivu wa kusoma Neno la Mungu, na kutaka kujua habari za Mungu, Na ndio maana utaona mpaka dakika yake ya mwisho anamwagiza Timotheo ambebee vile vitabu vya ngozi (torati na manabii) ampelekee.
2Timotheo 4:12 “Lakini Tikiko nalimpeleka Efeso.
13 Lile joho nililoliacha kwa Karpo huko Troa, ujapo ulilete, na vile vitabu, hasa vile vya ngozi”.
Sisi tumekuwa kikwazo cha Mungu kujifunua kwetu katika utimilifu wote, Kwasababu ya uvivu wetu wa kusikia/kusoma. Leo hii Bwana atusaidie tuzidishe bidii, kumtafuta Mungu. Ili Bwana ajifunue kwetu zaidi. Bwana Yesu alisema..
Yohana 3:12 “Ikiwa nimewaambia mambo ya duniani, wala hamsadiki, mtasadiki wapi niwaambiapo mambo ya mbinguni”?
Kumbe alitamani pia kuwaeleza watakatifu wa kipindi kile mambo ya mbinguni, lakini kwa ajili ya uvivu wao wa kutamani kujifunza, hawakuambiwa. Ndugu yangu Leo hii ua TV unazoangalia muda wote, ua huo muda unaokesha Instagramu, na facebook, kutazama video ambazo hazikujengi. Usipokuwa na instagramu, hupungukiwi chochote, si lazima uwe nayo, Muda utakuwa nao mwingi sana na wa kutosha,wa kusikiliza habari za Mungu, na kusoma, kama utaacha mitandao ya kijamii ikupite.
Kumbuka, Mungu anatazamia kile mkristo akue siku baada ya siku.
Shalom.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Naomba kufahamu maana ya “sura ya kijiti” katika Marko 12:26.
Jibu: Tusome kuanzia juu kidogo.
Mwanzo 19:4 “ Hata kabla hawajalala, watu wa mji, wenyeji wa Sodoma, wakaizunguka nyumba, vijana kwa wazee, watu wote waliotoka pande zote.
5 Wakamwita Lutu, wakamwambia, Wa wapi wale watu waliokuja kwako usiku huu? Uwatoe kwetu, tupate kuwajua.
6 Lutu akawatokea mlangoni, akafunga mlango nyuma yake.
7 Akasema, Basi, nawasihi, ndugu zangu, msitende vibaya hivi.
8 Tazama, ninao binti wawili ambao hawajajua mtu mume, nawasihi nitawatolea kwenu mkawafanyie vilivyo vyema machoni penu, ila watu hawa msiwatende neno, kwa kuwa wamekuja chini ya dari yangu”
9 Wakasema Ondoka hapa! Kisha wakanena, Mtu huyu mmoja amekuja kwetu kuketi hali ya ugeni; naye kumbe, ANATAKA KUHUKUMU! Basi tutakutenda wewe vibaya kuliko hawa. Wakamsonga sana huyo mtu, huyo Lutu, wakakaribia wauvunje mlango.”
Kuhukumu kunakozungumziwa hapo sio kutoa hukumu ya adhabu.. hapana! Bali kunamaanisha “kutoa maamuzi” au “kuamua”.. Mtu anayetoa maamuzi kwa lugha ya kibiblia ni mhukumu. Watu wawili wanapopigana na akatokea mtu akawasuluhisha huyo mtu aliyewasuluhisha ni mhukumu wao, kadhalika mtawala wowote wa nchi mhukumu wa hiyo nchi.
Mfano mzuri wa kujifunza katika biblia ni Sulemani… Mfalme Sulemani aliomba kutoka kwa Mungu moyo wa kuweza kuwahukumu/kuwaamua watu kwa adili.
1 Wafalme 3:7 “Na sasa, Ee Bwana, Mungu wangu, umenitawaza niwe mfalme mimi mtumwa wako badala ya Daudi baba yangu; nami ni mtoto mdogo tu; sijui jinsi inipasavyo kutoka wala kuingia.
8 Na mtumwa wako yu katikati ya watu wako uliowachagua, watu wengi wasioweza kuhesabiwa, wala kufahamiwa idadi yao, kwa kuwa ni wengi.
9 Kwa hiyo nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili NIWAHUKUMU WATU WAKO, na kupambanua mema na mabaya; maana ni nani awezaye kuwahukumu hawa watu wako walio wengi?
10 Neno hili likawa jema machoni pa Bwana, ya kuwa Sulemani ameomba neno hili.
11 Mungu akamwambia, Kwa kuwa umeomba neno hili, wala hukujitakia maisha ya siku nyingi; wala hukutaka utajiri kwa nafsi yako; wala hukutaka roho za adui zako; BALI UMEJITAKIA AKILI ZA KUJUA KUHUKUMU;
12 basi, tazama, nimefanya kama ulivyosema. Tazama, nimekupa moyo wa hekima na wa akili; hata kabla yako hapakuwa na mtu kama wewe, wala baada yako hatainuka mtu kama wewe”.
Tukiendelea mbele kidogo.. tunaona uwezo wa kuhukumu wa Sulemani, ukidhihirika..
“22 Ndipo yule mwanamke wa pili akasema, Sivyo hivyo; bali mtoto wangu ndiye aliye hai, na mtoto wako ndiye aliyekufa. Na mwenzake akasema, Sivyo hivyo; bali mtoto wako ndiye aliyekufa, na mtoto wangu ndiye aliye hai. Ndivyo walivyosema mbele ya mfalme.
23 Ndipo mfalme akasema, Huyu anasema, Mtoto wangu yu hai, na mtoto wako amekufa. Na huyu anasema, Sivyo hivyo; bali mtoto aliyekufa ni wako, na mtoto aliye hai ni wangu.
24 Mfalme akasema, Nileteeni upanga. Wakaleta upanga mbele ya mfalme.
25 Mfalme akasema, Mkate mtoto aliye hai vipande viwili, kampe huyu nusu, na huyu nusu.
26 Ndipo mwanamke yule, ambaye mtoto aliye hai ni wake, akamwambia mfalme kwa maana moyoni mwake alimwonea mtoto wake huruma, akasema, Ee bwana wangu, mpe huyu mtoto aliye hai, wala usimwue kamwe. Lakini yule mwingine akasema, Asiwe wangu wala wako; na akatwe.
27 Ndipo mfalme akajibu, akasema, Mpe huyu wa kwanza mtoto aliye hai, maana yeye ndiye mama yake.
28 Na Israeli wote wakapata HABARI ZA HUKUMU ILE ALIYOIHUKUMU mfalme wakamwogopa mfalme; maana waliona ya kuwa hekima ya Mungu ilikuwa ndani yake, ILI AFANYE HUKUMU”
Umeona?…maana ya hukumu ni pana, sio tu kutoa adhabu, au kauli ya kuadhibu…kama inavyoaminika sasa…
Kwahiyo hapo, hao watu wa Sodoma walitaka Luthu asitoe maamuzi yoyote juu ya shauri lao hilo, walilokusudia kulitenda.. Kwani walitaka watolewe wale malaika waliofika kwa Luthu ili walale nao. Na hawakutaka shauri lolote juu ya hilo, walichokisema wamekisema, na walichokiamua wamekiamua…
Sasa anatokea huyu Luthu ambaye kwanza ni mgeni tu katika hiyo nchi wa Sodoma, halafu anataka kuwapangia cha kufanya, “kwamba awape binti zake wawili walale nao badala ya wale malaika”…Jambo ambalo wao hawakulitaka.. Ndio maana wakasema maneno hayo.. “Mtu huyu mmoja amekuja kwetu kuketi hali ya ugeni; naye kumbe, ANATAKA KUHUKUMU! Basi tutakutenda wewe vibaya kuliko hawa”
Na sisi katika maisha yetu tuna mambo mengi ya kuhukumu, katika imani yapo mengi ya kuhukumu, katika familia zetu, katika shughuli zetu n.k kuna mambo mengi ya kuhukumu.. Na hivyo inahitajika siku zote hekima ya kiMungu ili kuhukumu kwa adili. Si lazima wakati wote tuombe tu mali na mafanikio ya kidunia kutoka kwa Mungu. Ni vizuri tukamwomba hekima ya kuhukumu kwa Adili kama Sulemani alivyoomba, na kwasababu Mungu anajua pia hayo mengine tuna haja nayo, hivyo atatuzidishia sawasawa na Neno lake, kama alivyomzidishia Sulemani.
Bwana atubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Biblia inamaanisha nini iliposema “wakidhania kuwa ulevi wakati wa mchana ni anasa;?
Siku moja nikiwa njiani nilikutana na mama mmoja mwenye mtoto, akaniomba shilingi elfu moja apande gari aelekee nyumbani kwake chanika, basi kwa kuwa hiyo pesa nilikuwa nayo nikampa, lakini baadaye kidogo, nilipanda gari, nikasahau kuwa sikuwa na hela nyingine yoyote ya cash mfukoni, tukiwa safarini kondakta, akaniomba nauli, nikajisachi sina pesa, ila ninayo kwenye simu, nikamwambia kondakta sina pesa hapa, naomba tukifika kituoni, nikatoe nikupe, lakini kondakta akaonekana kama sio mwelewa akadhani kama natumia ujanja tu ili nisimpe nauli yake..
Wakati naendelea kufikiria, na huku nikiangalia safari yangu haiishii mwisho wa kituo, nitashukia njiani hata nikienda kutoa atakuwa radhi kunisubiri?,.kulikuwa ni kijana mmoja anaonekana kama maskini, akatoa shilingi elfu moja akanipa, akaniambia chukua hii kondakta atakusumbua, nikamwambia ninayo nauli wacha tu tufike kituoni nitampa, lakini alinishurutisha kuichukua ile hela.
Nikakaa nayo kwa muda, nikitafakari, nikawa sina jinsi baadaye kidogo nikampa yule konda na yule kijana akashuka kwenye gari. Nikapata somo, wakati nadhani wenye shida ndio wanahitaji msaada, kumbe hata wewe usiye na shida utahitaji msaada ule ule kama wa yule mwenye shida.
Mama yule alikuwa na haja ya sh. Elfu moja, muda mchache baadaye uhitaji huo huo ulinigeukia mimi, japokuwa nilikuwa nayo. Ndugu yangu, utatembea, na gari lako, utatembea na mabilioni yako benki, utatembea na afya yako nzuri, lakini kamwe usiache kuwasaidia wenye uhitaji, kwasababu uhitahitaji ule ule wakati Fulani utaupitia hata wewe isipokuwa tu katika maumbile mengine.
Katika utajiri wako huo huo, unaweza ukafa njaa, kama tu vile yule mtu asiye na chakula kabisa, katika afya yako hiyo hiyo unaweza ukasumbuliwa na magonjwa kama tu mtu yule aliyelazwa pale muhimbili, katika nyumba yako nzuri, unaweza kulala nje kama tu yule mtu alalaye mabarazani, Vilevile katika elimu yako kubwa, hiyo hiyo unaweza kuwa mjinga sawa tu na yule ambaye hajasoma kabisa. Kamwe usifikirie kwasababu umeshapata kitu Fulani, ndio tayari umeepukana na tatizo hilo, ambalo watu wengine wanalipitia kwa kukikosa hicho. Lipindue hilo wazo kuanzia sasa.
Bwana atusaidie tujifunze unyenyekevu kwa watu wote, na kusaidiana sisi kwa sisi, kwasababu biblia inasema.
Mhubiri 1:6 “Upepo huvuma kusi, hugeuka kuwa kaskazi; hugeuka daima katika mwendo wake, na upepo huyarudia mazunguko yake.
7 Mito yote huingia baharini, walakini bahari haijai; huko iendako mito, ndiko irudiko tena”.
Shalom.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Mhubiri mmoja maarufu huko India, siku moja alionyeshwa maono, anasema alipokuwa anakwenda katika ziara zake za kuhubiri katika kijiji kimoja, ilikuwa ni desturi yake kukutana na baadhi ya wenyewe wa maeneo hayo nyumbani kwao na kuzungumza nao, Sasa anasema alipokuwa anakaribia nyumbani kwa mwanamke mmoja aliyemfahamu, yule mwanamke alipomwona anaingia uwani mwake, akatoka jikoni moja kwa moja kwenda kukutana naye, na kabla hata hajamuamkia vizuri, muda huo huo alimwangukia magotini kwake, akaanza kulia. Wakati muhubiri huyu anafanya jitahada za kumwinua, amuulize shida yake, muda huo huo anasema alimwona Bwana Yesu amesimama pembeni yake, akimwangalia, kisha kitambo kidogo akamwona anamkaribia huyu mwanamke aliyekuwa Analia, akaenda kwenye shavu lake la kushoto, na kuweka mikono yake, na kukinga machozi yake, mpaka yalipojitengeneza kama kibwawa.
Na ghafla akamwona Bwana Yesu akipaa mbinguni, na yeye yupo naye, akafika sehemu nzuri sana, ambapo kwa mbele aliona kitu kama sanduku la agano limewekwa, kisha akamwona Bwana Yesu akiyamimina machozi ya yule mama juu ya sanduku lile la agano. Kisha akaanza kumwombea kwa Baba, kwa kuuugua sana na kwa machozi mengi.. Aliomba pale kwa kitambo, mpaka ikasikika sauti kama ya radi ikisema, AMESIKIWA. Anasema Hapo ndipo Bwana Yesu alipoacha kuomba. Akageuka akamwangalia huyu mhubiri, akamwambia mwambie binti yangu, maombi yake manne aliyokuwa anamwomba Mungu yamesikiwa.
Na dakika hiyo hiyo alijikuta amesimama karibu na yule mwanamke, kisha akamwinua na kumweleza alichoonyeshwa, yule mwanamke akaruka ruka kwa kuraha na kicheko kwa kujibiwa kule.
Kwanini, nimeandika ushuhuda huo, nikwasababu, biblia inasema machozi ya watakatifu yanathaminiwa sana na Mungu, jambo ambalo watakatifu wengi, pengine hawalijui, wanadhani kulia kwao ni bure, Si kweli, Mungu anayakusanya machozi yetu na kuyahifadhi katika chupa, biblia inasema hivyo;
Zaburi 56:8 “Umehesabu kutanga-tanga kwangu; Uyatie machozi yangu katika chupa yako; (Je! Hayamo katika kitabu chako?)
Umeona Machozi yetu kwa Bwana, yanatiwa katika chupa, kama vile divai nzuri inavyotunzwa katika viriba vipya. Na wakati huo huo bado yanaandikwa katika kitabu cha Mungu cha ukumbusho. Kaka/Dada Umekuwa ukilia kwasababu ya dhiki unazopitia kutokana na Imani yako, kumbuka kuwa Mungu anasikia, umekuwa ukilia kwasababu ya misiba iliyokukuta hivi karibuni Mungu anasikia, kwasababu ya magonjwa yasiyotibika, Mungu anasikia, Kwasababu ya injili Mungu anasikia na kuyatunza hayo machozi kama vile alivyoyatunza ya akina Paulo.
Matendo 20:19 “nikimtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote, na kwa machozi, na majaribu yaliyonipata kwa hila za Wayahudi;
20 ya kuwa sikujiepusha katika kuwatangazia neno lo lote liwezalo kuwafaa bali naliwafundisha waziwazi, na nyumba kwa nyumba”,
Unapaswa ukumbuke kuwa huduma ya Bwana wetu Yesu Kristo ya kutuombea haikuishia tu alipokuwa duniani, hapana, bali bado inaendelea hadi leo hii mbinguni, biblia inasema hivyo;
Waebrania 7:25 “Naye, kwa sababu hii, aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu hai sikuzote ili awaombee”.
Hivyo usiogope ni nini unapitia leo, wala usikate tamaa, kumbuka Yesu, faraja yetu yupo. zidi kumtumaini yeye na kumtegemea yeye, kwasababu daima yupo na wewe, kukusaidia, mkono wake hautakuacha kamwe.
Hakika sifa na heshima, na utukufu, ni kwa Bwana wetu YESU KRISTO milele na milele,
Amen.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?
SWALI: Naomba kujua tofauti kati ya uchafu wa mwilini na rohoni ni ipi ?, kama tunavyosoma katika 2Wakorintho 7:1
2Wakorintho 7:1 “Basi, wapenzi wangu, kwa kuwa tuna ahadi hizo, na tujitakase nafsi zetu na UCHAFU WOTE WA MWILI NA ROHO, huku tukitimiza utakatifu katika kumcha Mungu”.
JIBU: Ili tuwe wakamilifu kwa kiwango cha kuweza kuzikaribia ahadi za Mungu, Tujue kuwa Mungu anataka tuwe watakatifu kote kote yaani Mwilini na rohoni.
Sasa hapo anaposema tujitakase na Uchafu wote wa mwilini. Anamaanisha kuwa tujiweke mbali na dhambi zote zinazozalika katika miili yetu. Mfano wa dhambi hizi ni kama vile, uzinzi, ulevi, wizi, uvutaji sigara, utukanaji, uvaaji mbovu, kama vile vimini na suruali kwa wanawake, kujichubua, kujipaka make-up, kutoa mimba, kuvaa milegezo, kujichoraji tattoo, na ushoga, utumiaji wa madawa ya kulevya na mambo mengine yote yanayofanana na hayo, ambayo asili yake ni mwilini.
Na pale aliposema tuweke kando Uchafu wa rohoni, Anamaanisha dhambi zote zinazotoka ndani ya mtu, ambazo hazihusiani na mwili moja kwa moja, mfano wa dhambi hizi ni kama vile, wivu, hasira, tamaa, mawazo mabaya, unafki, uchoyo, husuda, fitna, majigambo, kiburi, ibada za sanamu, uongo. Hizi ni dhambi ambazo zinazalika ndani, na Mungu anazichukia sana, kama vile tu anavyozichukia zile zinazozalika katika mwili.
Hivyo tujue kuwa Mungu anaangalia kote kote, Kuna watu wanadhani kuwa Mungu anaangalia roho tu, hatazami mwili. Ndugu, mwili wako unathamani sawa na roho yako mbele za Mungu, kwasababu siku ile ya mwisho si roho yako tu itaokolewa, bali hata na mwili wako pia (kasome biblia utalithibitisha hilo). Hivyo mtukuze Mungu katika mwili wako, usidanganywe na mafundisho ya manabii wa Uongo, wanaokuambia Mungu anatazama roho haangalii mwili. Hizi ni nyakati za mwisho, Tii Neno la Mungu Zaidi ya maneno ya mwanadamu. Kwasababu hilo ndilo litakalokutetea siku ile, na hilo ndilo litakalokuhumu siku ile. Neno la Mungu ni upanga. Liogope sana.
Waebrania 4:12 “Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.
13 Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu”.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Nini maana ya “mkilichukia hata vazi lililotiwa uchafu na mwili”?