Title October 2021

Je! Siku ya unyakuo watoto wachanga watanyakuliwa?

SWALI: Je! Siku ya unyakuo watoto wachanga watanyakuliwa? Na vipi kuhusu walio bado tumboni, na wenyewe watanyakuliwa au wataachwa?


JIBU: Hili ni moja ya swali gumu  kwasababu biblia haijaeleza moja kwa moja ni nini kitawatokea watoto siku ile ya Unyakuo, Hivyo tutajaribu kueleza kwa kadiri ya tunavyoona katika baadhi ya vifungu kwenye maandiko.

Ukitazama katika biblia, utaona, wapo watoto walipata neema kutokana na haki za wazazi wao, mfano wa hawa ni watoto wa Nuhu, na Lutu,  vilevile wapo watoto walioadhibiwa kutokana na makosa ya wazazi wao. Utaliona hilo pia katika vile vizazi vyote vya Sodoma na Gomora, pamoja na gharika  vyote viliteketezwa, hadi watoto walipata adhabu kwa dhambi za wengine. Lakini hiyo haimaanishi kuwa wataadhibiwa tena baada ya kifo.

Pia tukumbuke kuwa hata katikati ya kipindi cha dhiki kuu, bado watu wataendelea kutungishwa mimba na kuzaliwa, hivyo litakuwepo kundi la vichanga ambavyo vitazaliwa katikati ya dhiki kuu na vitakufa katika maangamizi yao..Hilo tunalithibitisha katika andiko hili;

Mathayo 24:19 “Ole wao wenye mimba na wanyonyeshao siku hizo!

20 Ombeni, ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya sabato.

21 Kwa kuwa wakati huo kutakuwapo dhiki kubwa, ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hata sasa, wala haitakuwapo kamwe.

22 Na kama siku hizo zisingalifupizwa, asingeokoka mtu ye yote; lakini kwa ajili ya wateule zitafupizwa siku hizo”.

Unaona? Kwahiyo siku ile ikifika, kuna uwezekano wa watoto wengine kunyakuliwa (hata wale walio tumboni), na vilevile wengine kubaki, japo hatuwezi kusema hivyo ndivyo ilivyo, Yote tunamwachia Mungu. Ikiwa ni wote watanyakuliwa, au ni baadhi, Tunachopaswa kufahamu ni kuwa Mungu ni wa haki, atayaleta yote katika mizani, na yote yatakuwa sawa tu mwisho wa siku, na tutaona kabisa hukumu zake ni za haki. Kama vile Malaika mbinguni wanavyokiri hivyo..

Ufunuo 16:7 “Nikaisikia hiyo madhabahu ikisema, Naam, Bwana Mungu Mwenyezi, ni za kweli, na za haki, hukumu zako”.

Cha muhimu tunachopaswa kujua ni kuwa sisi ambao tayari tumeshafikia kimo cha kuyajua mema na mabaya, Kama hatutayatengeneza mambo yetu sasa, kwa kumpokea Bwana Yesu Kristo kwa kumaanisha kabisa, na kujitwika misalaba yetu na kumfuata, tujue kuwa unyakuo ukipita tutaachwa. Na matokeo yake, yatakuwa ni kuingia katika mateso makali ya dhiki kuu pamoja na Jehanamu ya moto.

Je! Umeokoka? Je! Umebatizwa katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako? Kumbuka Unyakuo ni wakati wowote, tubu umruidie muumba wako. Parapanda ni siku yoyote inalia, hakuna dalili iliyosalia..

Bwana Yesu akubariki.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Rudi nyumbani

Print this post

Mwerezi ni nini?

Mwerezi ni aina ya mti uliokuwa unapatikana maeneno ya nchi ya Lebanoni, Ulikuwa unastawi pia sehemu mbalimbali za dunia, lakini ulistawi zaidi katika nchi ya Lebanoni, iliyopo kaskazini mwa nchi ya Israeli.

Aina hii ya mti ilitumika kwa matumizi mengi, kutokakana ubora wake na uimara wake ukulinganisha na aina nyingine ya miti. Mti huu wa Mwerezi  ulikuwa ni mgumu na usiooza kirahisi.

Nchi ya Lebanoni, ilijipatia utajiri kutokana na biashara ya miti hii, ambapo Mataifa mengi duniani kama Misri, Ashuru, Babeli na Israeli ilinunua miti hii kutoka huko Lebanoni, kwaajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo ya ujenzi.

Mfalme Daudi alitumia miti hii ya Mierezi kutoka Lebanoni kuijenga nyumba yake.

2Samweli 5:11 “Kisha Hiramu, mfalme wa Tiro, akatuma wajumbe kwa Daudi, AKAMPELEKEA NA MIEREZI, NA MASEREMALA, NA WAASHI; NAO WAKAMJENGEA DAUDI NYUMBA”.

2Samweli 7:2 “mfalme akamwambia Nathani, nabii, Angalia sasa, mimi ninakaa katika NYUMBA YA MIEREZI, bali sanduku la Mungu linakaa ndani ya mapazia.”

Lakini pia Nyumba ya Mungu ambayo ilikuja kujengwa na Sulemani, Mwana wa Daudi, ilitengenezwa pia kwa Mierezi mingi kutoka Lebanoni.

1Wafalme 5:5 “Nami, tazama, nakusudia kujenga nyumba kwa jina la Bwana, Mungu wangu, kama Bwana alivyomwambia Daudi baba yangu, akisema, Mwana wako, nitakayemweka katika kiti chake cha enzi mahali pako, ndiye atakayeijenga nyumba kwa jina langu.

6 BASI UAMURU WANIKATIE MIEREZI YA LEBANONI; na watumishi wangu watafuatana na watumishi wako; na ujira wa watumishi wako nitakupa kama utakavyosema; kwa kuwa wajua ya kwamba hakuna kwetu mtu ajuaye kukata miti kama Wasidoni”.

Na hata baada ya Mfalme Nebukadneza kuliharibu hekalu hilo la Sulemani, hekalu la pili lilipokuja kujengwa na wakina Zerubabeli, lilijengwa sehemu kwa miti hiyo ya Mierezi.

Ezra 3:6 “Tangu siku ya kwanza ya mwezi wa saba walianza kumtolea Bwana sadaka za kuteketezwa, lakini msingi wa hekalu la Bwana ulikuwa haujawekwa bado.

7 Tena waliwapa waashi na maseremala fedha; wakawapa watu wa Sidoni, na watu wa Tiro, chakula, na vinywaji, na mafuta, ili walete MIEREZI KUTOKA LEBANONI mpaka Yafa kwa njia ya bahari, kwa kadiri walivyopewa ruhusa na Koreshi, mfalme wa Uajemi”.

Hivyo Mwerezi katika biblia imetumika kama ishara ya UTAJIRI. Kama vile DHAHABU.

Tunaona vitu vikuu viwili vilivyotajwa sana katika ujenzi wa nyumba ya Mungu ni MWEREZI pamoja na DHAHABU.  Kutokana na uthamani wa vitu hivyo.

Na kama Mti wa Mwerezi ulivyojipatia sifa hivyo, Bwana Mungu anasema walio Haki wote watasitawi kama Mwerezi.

Zaburi 92:12 “Mwenye haki atasitawi kama mtende, Atakua kama MWEREZI WA LEBANONI.

13 Waliopandwa katika nyumba ya Bwana Watasitawi katika nyua za Mungu wetu.

14 Watazaa matunda hadi wakati wa uzee, Watajaa utomvu, watakuwa na ubichi.

15 Watangaze ya kuwa Bwana ni mwenye adili, Mwamba wangu, ndani yake hamna udhalimu”.

Je! Wewe ni mwenye HAKI?

Kumbuka mwenye haki sio mtu anayesema anafanya mema huku yupo nje ya Kristo, hiyo sio tafsiri ya mwenye haki. Bali tafsiri ya mwenye haki ni mtu Yule, aliyempokea Yesu, na kubatizwa na kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu, huyo ndiye anayehesabiwa haki kwa IMANI HIYO ya kumwamini Yesu. Mwingine yeyote ambaye hamwamini Bwana Yesu, na kujitumainia katika mambo yake anayoyafanya anayoamini kuwa ni mema, anakuwa bado si mwenye haki mbele za Mungu.

Lakini wote waliompokea Yesu, watasitawi na kuwa na heshima kama miti ya Mierezi.

Bwana atubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

WALA MSIUANGALIE MWILI, HATA KUWASHA TAMAA ZAKE.

Biblia inamaanisha nini inaposema “Mwenye haki huufikiri uhai wa mnyama wake”?

HUYU MELKIZEDEKI NI NANI?

Kwanini Bwana alirejea Tiro na Sidoni kwa mfano wa Sodoma?

Rudi nyumbani

Print this post

Shilo ni wapi?

Shilo ni nini?

Katika biblia Shilo ulikuwa mji mtakatifu, ambapo Kabla ya Mungu kupachagua Yerusalemu kama mji atakaoweka jina lake milele, hapo kabla wana wa Israeli walikuwa wanakusanyiko huko Shilo, kama sehemu takatifu ya kufanyia ibada na kutolea dhabihu.

Na hata sanduku la agano mara tu baada ya wana wa Israeli kuingia nchi ya ahadi, mji uliotueuliwa kwaajili ya kuliweka sanduku hilo la agano la Mungu..ulikuwa ndio huo wa mji wa Shilo, ambapo sanduku hilo lilikaa mjini huko bila kutoka kwa miaka mingi mpaka  Wafilisti walipokuja kulichukua kutoka huko sababu ya makosa ya wana wa Israeli (1Samweli 10-11).

Huko Shilo pia ndiko Nabii Samweli alikolelewa maisha yake yote (1Samweli 1:24 )

Mji huu wa Shilo ulikuwa unapatikana kaskazini mji mwa mji wa Betheli, karibu na Samaria.

Unaweza kusoma zaidi kuhusu mji huo kupitia mistari ifuatayo > Yoshua 18:8-10, Yoshua 19:51, Yoshua 21:2, Waamuzi 18:31, Waamuzi 21:19, 1Samweli 1:9, Zaburi 78:60.

Lakini swali ni je! Hii Shilo mpaka leo ni sehemu takatifu?.

Jibu ni la!

Shilo ya Leo sio tena huko Israeli, bali ni katika Neno la Mungu.

Katika Kweli ya Neno la Mungu na katika Roho Mtakatifu..tunamwabudu Baba..kama Bwana Yesu alivyosema..

Yohana 4:21

“Yesu akamwambia, Mama, unisadiki, saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala kule Yerusalemu.

22 Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi.

23 Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu”

Je umempokea Roho Mtakatifu, je unaliishi Neno?.

Bwana akubariki.

Maran atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Nini maana ya Dirii, Chepeo na Utayari?

Raheli aliwalilia vipi watoto wake?

Nini maana ya “Ulipo mzoga, ndipo watakapokutanika tai?

Kisima cha joka na lango la jaa ni nini?(Nehemia 2:13)

Rudi nyumbani

Print this post

Kwanini Herode aliwakasirikia watu wa Tiro na Sidoni? (Matendo 12:20)

Jibu: Tusome,

Matendo 12:20 “Naye Herode ALIKUWA AMEWAKASIRIKIA SANA WATU WA TIRO NA SIDONI; wakamwendea kwa nia moja, na wakiisha kufanya urafiki na Blasto, mwenye kukitunza chumba cha mfalme cha kulalia, wakataka amani; kwa maana nchi yao ilipata riziki kwa nchi ya mfalme.

21 Basi siku moja iliyoazimiwa, Herode akajivika mavazi ya kifalme, akaketi katika kiti cha enzi, akatoa hotuba mbele yao.

22 Watu wakapiga kelele, wakisema, Ni sauti ya Mungu, si sauti ya mwanadamu.

23 Mara malaika wa Bwana akampiga, kwa sababu hakumpa Mungu utukufu; akaliwa na chango, akatokwa na roho”.

Tiro na Sidoni ni miji iliyokuwepo kaskazini mwa mji wa Galilaya, miji hiyo kwasasa ni sehemu za Lebanoni.

Zamani za biblia Herodi ndiye alikuwa anatawala Yudea, na watu wa miji ya Tiro na Sidoni, walikuwa wanaitegemea Yudea kwa chakula. Lakini ulifika wakati Herode alichukizwa nao (biblia haijataja sababu ni nini), lakini alichukizwa nao, na akakatisha kuwauzia chakula hao watu wa Sidoni na Tiro.

Watu wa Tiro na Sidoni, walipokaa muda mrefu bila chakula, ikawabidi wakatafute amani na Herode huko Yudea, lakini njia waliyoitumia ni kumtafuta mtu aliyeitwa Blasto, ili amshawishi Herode waweze kuwa na mdahalo wa wazi na Hao watu wa Sidoni, kwasababu haikuwa rahisi Herode, kumfikia.

Huyu Blasto ambaye alikuwa anafanya kazi katika nyumba ya Mfalme Herode, na ambaye ndiye aliyekuwa mtu wake karibu kuliko wengine wote, alifanikiwa kumshawishi Herode azungumze na watu wa Tiro na Sidoni kwa wazi.

Hivyo siku ilipofika Herode alijitokeza kuzungumza na watu hao. Lakini kama inavyojulikana Herode alikuwa ni mtu wa kupenda utukufu, alikuwa anajitukuza yeye kama Mungu hapo Yudea. Alikuwa anapenda  kuabudiwa kama Mungu. Alimuua Yakobo ndugu yake Yohana kwa upanga, na mwisho alimfunga Petro ili amuue kama alivyomuua Yakobo,  lakini Malaika wa Bwana alimwokoa na mauti yake. Na hapa anasimama ili ajitukuze, awaonyeshe watu wa Sidoni na Tiro kwamba yeye ndiye anayetoa chakula!, pasipo yeye wao hawawezi kuishi.

Na watu wa Sidoni kwasababu ni watu wa kipagani waliozoea kuabudu miungu, na kumtukuza mtu yeyote ambaye wanamwona ni wa tofauti, kama wale watu wa Athene waliotaka kumtukuza Paulo na Barnaba..

Matendo 14:11 “Na makutano walipoona aliyoyafanya Paulo wakapaza sauti zao, wakisema kwa Kilikaonia, Miungu wametushukia kwa mifano ya wanadamu.

12 Wakamwita Barnaba, Zeu, na Paulo, Herme, kwa sababu ndiye aliyekuwa mnenaji”.

 Kadhalika na hawa watu wa Tiro na Sidoni walipomwona tu Herode kasimama anahutubia kimajivuno na kimajigambo kiasi kile, wote kwa pamoja wakaanza kupaza sauti zao na kusema “Hii ni sauti ya Mungu na si mtu..hii ni sauti ya Mungu na si mtu”

Tofauti na akina Paulo na Barnaba ambao wao walipoona watu wanawageuza miungu-watu walizirarua nguo zao na kuwaeleza kuwa wao ni watu tu kama wao, na sio Mungu. Kinyume chake Herode yeye hakufanya hivyo, bali moja kwa moja alizidi kujitukuza na kutaka kuchukua utukufu zaidi.

Na kwasababu Mungu hashiriki utukufu wake na wanadamu, pale pale Malaika wa Bwana alishuka akampiga Herode kwa change, Chango ni ugonjwa mbaya wa kuliwa na minyoo.. kwa maelezo marefu juu ya ugonjwa huu fungua hapa >>>>>> CHANGO KIBIBLIA

Lakini ni nini tunajifunza katika habari hiyo?

Tunachoweza kujifunza kikubwa ni kuwa Mungu hashirikiani utukufu na mwanadamu yeyote…Na ni jambo la hatari sana kutafuta ufukufu, jambo lililombadilisha shetani kutoka kuwa Kerubi na kuwa Ibilisi ni hilo hilo, la kutafuta kuabudiwa.

Na jambo lingine pia linalomhuzunisha Mungu sio sisi tu kutafuta kuabudiwa bali hata sisi tunapotafuta kuabudu watu au kitu kingine chochote.

Tunapoabudu sanamu, au watu, au fedha au kingine chotechote kile kuna hatari kubwa sana ya kuadhibiwa na Mungu.

Bwana atusaidie na kutubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

TUJIFUNZE JAMBO KWA WANAWAKE HAWA WAWILI:

HERODE NA PILATO, MAADUI WAWILI WAPATANA.

TABIA ZA WATAKAOMKARIBIA SANA MUNGU SIKU ILE.

CHACHU YA MAFARISAYO NA CHACHU YA HERODE.

Rudi nyumbani

Print this post

Ni SIRI gani Paulo aliyokuwa anaimaanisha katika Waefeso 5:32?

Jibu: Labda tuanze kusoma kuanzia juu kidogo..

Waefeso 5:31 “Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja.

32 SIRI HIYO NI KUBWA; ILA MIMI NANENA HABARI YA KRISTO NA KANISA.

33 Lakini kila mtu ampende mke wake kama nafsi yake mwenyewe; wala mke asikose kumstahi mumewe”

Siri Paulo aliyoimaanisha hapo, sio nyingine Zaidi ya hiyo aliyoitaja hapo kwamba “WAWILI WATAKUWA MWILI MMOJA”. Hiyo ndiyo SIRI yenyewe.. Na kwanini iwe siri?, ni kwasababu ni jambo gumu kueleweka au kufafanulika kwamba watu wawili tofauti wenye miili miwili tofauti wamekutana halafu wanakuwa mwili mmoja, na ilihali ni watu wawili tofauti wenye miili miwili tofauti.. afadhali angesema “watakuwa nafsi moja au watakuwa wamoja”.. kidogo ingeweza kuwa rahisi kueleweka, lakini kuwa mwili mmoja? Hapo ni lazima kuna siri katikati yake.

Tunaona pia Bwana Yesu alilisisitiza tena jambo hilo hilo katika injili ya Marko.

Marko 10:7 “Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe;

8 NA HAO WAWILI WATAKUWA MWILI MMOJA; HATA WAMEKUWA SI WAWILI TENA, BALI MWILI MMOJA”

Kwahiyo hiyo ni SIRI kubwa sana.

Lakini biblia imetupa uvumbuzi wa siri hiyo, ni kwa jinsi gani, wawili wanakuwa mwili mmoja na si roho moja.

Na uvumbuzi huo tunaupata pale Mwanzo, Mungu alipowaumba Adamu na Hawa.. Biblia inasema

Mwanzo 2:21 “Bwana Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akalala; kisha akatwaa ubavu wake mmoja, akafunika nyama mahali pake,

22 na ule ubavu alioutwaa katika Adamu Bwana Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu.

23 Adamu akasema, SASA HUYU NI MFUPA KATIKA MIFUPA YANGU, na NYAMA KATIKA NYAMA YANGU, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume.

24 Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja”.

 Hapo katika mstari wa 23, tunaona Adamu hakusema huyu ni “roho katika roho yangu” wala “nafsi katika nafsi yangu”..bali alisema huyu “ni nyama katika nyama yake”.. akimaanisha mwili wa mwanamke yule ni mwili wake…kwasababu katwaliwa kutoka kwake.

Kwahiyo mtu yeyote anayekwenda kuoa au kuolewa, yule aliyejiungamanisha naye, tayari wanakuwa mwili mmoja, kwasababu wote asili yetu ni Adamu. Na kama wanakuwa mwili mmoja maana yake, Baraka zote wanashiriki pamoja, na vile vile laana zote wanashiriki pamoja na mambo yote mazuri au mabaya, ya mwilini au rohoni wanakuwa wanashiriki pamoja.

Ndio maana kuna hatari kubwa sana ya kutoka nje ya ndoa na kuzini, au kufanya uasherati.. kwasababu yule unayezini naye, au unayefanya naye uasherati, kiroho unajiunganisha naye na kuwa mwili mmoja bila wewe kujijua, maandiko yanasema hivyo..

1Wakorintho 6:13 “…………….Lakini mwili si kwa zinaa, bali ni kwa Bwana, naye Bwana ni kwa mwili………………….

15 Je! Hamjui ya kuwa miili yenu ni viungo vya Kristo? Basi nivitwae viungo vya Kristo na kuvifanya viungo vya kahaba? Hasha!

16 Au hamjui ya kuwa YEYE ALIYEUNGWA NA KAHABA NI MWILI MMOJA NAYE? MAANA ASEMA, WALE WAWILI WATAKUWA MWILI MMOJA”

Hivyo kahaba au mtu yeyote unayefanya naye uasherati, kama kuna Laana amezibeba katika maisha yake, wewe unayeshiriki naye, nawe pia unazibeba, kama ana roho na mapepo unaposhiriki naye uzinzi huo, yale mapepo nawe pia yanapata hifadhi ndani yako, (mnayashiriki pamoja) kwasababu tayari mmekuwa mwili mmoja.

Ndio maana moja ya amri za Mungu ni USIZINI! Kwasababu uzinzi una madhara makubwa sana kiroho na kimwili.

Wagalatia 5:19 “ Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, UASHERATI, uchafu, ufisadi,

 20 ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi

21 husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu”.

Bwana azidi atubariki.

Marna tha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

WALIPO WAWILI AU WATATU KWA JINA LANGU

WALIPO WAWILI AU WATATU KWA JINA LANGU

Noeli ni nini, na je! Neno hili linapatikana katika biblia?

JISHUSHE ILI MUNGU AKUHUDUMIE.

Tofauti kati ya uchafu wa mwilini na rohoni ni  ipi?

Rudi nyumbani

Print this post

Ni kweli hakuna mtu aliyewahi kuuona uso wa Mungu Zaidi ya Bwana Yesu?

SWALI: Musa alikuwa na mawasiliano ya ana kwa ana na Mungu, hata kuuona uso wake lakini katika Yohana 1:18, inaonekana Yohana anakanusha kuwa hakuna mtu aliyewahi kumwona Mungu isipokuwa Kristo pekee.


Jibu: Kumwona Mungu kunakozungumziwa hapo sio KUMTAZAMA USONI, kwamba anaonekanaje, mwonekano wake ukoje, uso wake unafananaje fananaje n.k. La! Sio kwa namna hiyo. Bali kumwona kunakozungumziwa hapo ni kwa ufahamu.

Kwamfano tunaposema TUMEUONA MKONO WA BWANA, haimaanishi tumeenda mbinguni tukauona mkono wake jinsi ulivyo, au umeshuka chini tukauona jinsi ulivyo, rangi yake na idadi ya vidole alivyo navyo! N.k. La! Bali tunamaanisha tumeona uweza wake mkuu!. Vile vile tunaposema tumemwona Bwana katika maisha yetu, haimaanishi ameshuka mbele yetu na tukamwona sura yake, bali tunamaanisha tumeona uwepo wake na kuutambua.

Kadhalika maandiko hapo yanaposema hakuna aliyemwona Mungu haimaanishi “aliyemwona Uso wake jinsi ulivyo” bali inamaanisha “hakuna aliyemjua Mungu na kumfahamu, kiuweza na kimamlaka kikamilifu” isipokuwa Kristo peke yake. Wengine wamemwona na kumwelewa lakini si kwa kiwango ambacho Mungu mwenyewe, alikuwa anataka watu wamwelewe.. Hivyo ni sawa na hawakumwona kabisa! Au kumwelewa. Ni Bwana Yesu pekee ndiye aliyemwelewa na kumfunua Baba, kikamilifu…

Luka 10:22 “Akasema, Nimekabidhiwa vyote na Baba yangu, wala hakuna amjuaye Mwana ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana, na ye yote ambaye Mwana apenda kumfunulia”.

Umeona? Kristo pekee ndiye aliyemjua Mungu, jinsi inavyopaswa kumjua.. Musa hakumjua Mungu, ndio maana torati ya Musa havikuweza kumkamilisha mwanadamu!.. Kristo ndiye aliyekuja kumfunua Mungu kwetu jinsi inavyopaswa, na kutuonyesha mapenzi yake kamili..

Yohana 1:17 “Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo”.

Kwamfano Wanafunzi wa Yesu walikuwa wanamwona Bwana Yesu kila siku, lakini walikuwa hawamjui, macho ya mioyo yao yalikuwa yamefumbwa. Ndio maana alipowauliza Yeye ni nani, wakawa wanakosa jibu sahihi, mpaka Petro ambaye alifunuliwa na Baba, aliposema yeye ni Mwana wa Mungu, ili litimie hilo neno “WALA HAKUNA AMJUAYE MWANA ILA BABA”; WALA HAKUNA AMJUAYE BABA ILA MWANA, na ye yote ambaye Mwana apenda kumfunulia”.

Hivyo Bwana Yesu(Mwana wa Mungu).. ndio kila kitu katika haya maisha. Hakuna mtu mwingine yeyote, au nabii mwingine yeyote ambaye tunaweza kumfuata au kumtegemea maneno yake tukafika mbinguni. Injili ya Musa haikumhaidia mtu kufika kule Baba aliko, wala ya Nabii mwingine yeyote.. Ni Yesu pekee ndiye aliyetoa njia ya Watu kumfikia Baba Mbinguni!!..kwasababu yeye ndiye anayemjua.. Na njia hiyo ya kumfikia Baba ni YEYE MWENYEWE, yaani maisha yake na Neno lake.

Yohana 14:5 “Tomaso akamwambia, Bwana, sisi hatujui uendako; nasi twaijuaje njia?

6 Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi”

Je! Unataka kwenda mbinguni kwa Baba?

Kama ni ndio!, basi tambua NJIA NI YESU. Hakuna elimu nyingine yeyote, wala dini nyingine yeyote, wala maarifa mengine yeyote, ambayo yataweza kukufikisha mbinguni.. isipokuwa ni YESU TU!. Huyo ndiye aliyemwona Baba na Baba mwenyewe akamthibitisha.. hivyo hakuna njia ya mkato ya kufika mbinguni.

Hivyo kama hujampokea, mpokee leo na utubu na kubatizwa, ili aingia maishani mwako na kukuongoza katika njia ya uzima wa milele.

Maran atha!

[embedyt] https://www.youtube.com/embed?listType=playlist&list=PLIIhnDzXkeEcXSNPlq09Q5yonU3MOLI0h&v=kuCSAZcnM80&layout=gallery[/embedyt]

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Mlima Gerizimu na Ebali ni ipi, na umuhimu wao rohoni ni upi?

MJUE SANA YESU KRISTO.

Kama Mungu ndiye kaumba kila kitu, je ni yeye huyo huyo ndiye aliyeumba dhambi pia?

TUMEFANYIKA KUWA WANA WA MUNGU!

KWANINI TUNAPASWA TUJIZUIE?

Rudi nyumbani

Print this post

Je! Karamu za ‘Idi’ ndio zipo hizo tunazozisoma katika Hosea (12:9)

Hosea 12:9 Lakini mimi ni Bwana, Mungu wako tangu ulipotoka katika nchi ya Misri; nitakukalisha tena katika hema, kama siku za KARAMU YA IDI.


JIBU: Tofauti na inavyodhaniwa hapo, na watu wa dini tofauti, kwamba Biblia inazitambua sherehe za kiislamu!. Jambo ambalo si kweli.

Ni vizuri kufahamu kuwa lugha yetu ya Kiswahili imetohoa maneno mengi sana kutoka katika lugha ya kiharabu, hata wakati ambapo biblia inatafsiriwa katika Kiswahili ilifuata mkondo huo huo. Kwamfano Sehemu nyingine utaona neno “shehe” likitajwa (1Samweli 5:8), na hapa unaona pia Neno “Idi” .

Kulingana na lugha ya  kiharabu neno IDI, linamaanisha “Sherehe”. Haijalishi ni sherehe ya aina gani, inaweza ikawa ni ya kidini au ya kitaifa, au ya kitamaduni, au ya kimuungano..

Hivyo imezoeleka na watu wengi wasioilewa lugha ya kiharabu kudhani kuwa Idi ni neno la sikukuu ya kiislamu, kumbe sio.

Katika biblia ya kiharabu, mahali popote, kulipotajwa sherehe ya kiyahudi, Neno Idi liliandikwa pale. Mfano, palipoandikwa sikukuu ya pasaka, iliandikwa “idi ya pasaka” n.k..

Hivyo, hatushangai na Neno hilo kuonekana katika baadhi ya vifungu kwenye biblia. Hiyo yote ni kwasababu lugha yetu ya Kiswahili, imeundwa kutoka katika lugha nyingi mbalimbali. Kwahiyo inayozungumziwa hapo sio sikukuu ya kiislamu, bali ni sikukuu ya vibanda, ambayo wana wa Israeli walikuwa wakiisheherekea kwa katika vibanda pindi walipokuwa jangwani.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

SIKUKUU 7 ZA KIYAHUDI ZINAFUNUA NINI KWETU?

UFUNUO: Mlango wa 19

ESTA: Mlango wa 5, 6 & 7

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

Je kunena kwa Lugha mpya kukoje?.Na hizi lugha ni zipi, na je! ni lazima kila mkristo aliyepokea Roho Mtakatifu anene kwa lugha mpya?

Rudi nyumbani

Print this post

MWANAMKE, BINTI, MAMA. (Sehemu ya 2)

Hii ni sehemu ya pili ya mfululizo wa masomo kwa wanawake, katika sehemu ya kwanza tumeona, ni kwanini Bwana alipokutana na yule mwanamke mwenye dhambi, alimtambua kwa jinsia yake (Yaani “mwanamke”) na sio kwa mwonekano wake wa kike pengine wa kiumri au  wa kimaumbile. Hiyo ni kufunua kuwa ujumbe alioubeba yule mwanamke ulikuwa ni wa kijinsia.. yaani maalumu kwa wanawake. Hivyo kama hukupata maelezo yake, unaweza kunitumia ujumbe inbox nikakutumia.

Leo tutaenda katika sehemu ya pili: ya BINTI.

Mahali pengine, Bwana Yesu, aliwatambua wanawake wengine kama, binti zake.. Na cha ajabu ni kuwa, wengine walikuwa pengine wana umri mkubwa kuliko yeye, lakini bado aliwaita BINTI zake, akifunua kuwa kutazama kwake hakukuwa katika jicho la kimwili bali la rohoni. Embu tusome, kisa hiki kimoja..kisha tuone ni ujumbe gani Bwana alitaka kuupitisha kwa ulimwengu kupitia mwanamke huyu.

Mathayo 9:20 “Na tazama, mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, alikuja kwa nyuma, akaugusa upindo wa vazi lake.

21 Kwa maana alisema moyoni mwake, Nikigusa tu upindo wa vazi lake nitapona.

22 Yesu akageuka, akamwona, akamwambia, Jipe moyo mkuu, BINTI YANGU; imani yako imekuponya. Yule mwanamke akapona tangu saa ile.”.

Swali la kujiuliza ni kwanini alimtambua mwanamke huyu kama binti na sio pengine kama Mama, au bibi?

Ni kwasababu ya Imani yake ya kipekee aliyokuwa nayo kwake..Ambayo hakuiona kwa watu wengine wote waliomfuata, ijapokuwa alihangaika kwa miaka 12 kutafuta suluhu la matatizo yake asipate, lakini alipofika kwa Yesu kwa mara ya kwanza tu hakumuhesabia kama mmojawapo wa wale matapeli aliokutana nao, huko nyuma, waliomchukulia fedha zake.

Bali alimwamini moja kwa moja kwa asilimia 100, akasema, nitakapoligusa tu pindo la vazi lake, muda huo huo nitakuwa mzima, kumbuka hakusema sio “naamini nitapona, au pengine nitapona” hapana, bali alisema “NITAPONA” kuonyesha kuwa alikuwa na uhakika wa yule aliyekutana naye sio mbabaishaji au tapeli…. Na ndio maana akaona hata hakuna sababu ya kwenda kumsumbua kuzungumza naye, au kumwomba aje kumtembelea, Bali aliona pindo la vazi lake, tu linatosha yeye kuwa mzima..

Na Yesu alipoiona Imani yake saa ile ile akamgeukia na kumwita “Binti yangu”.. Akampa nafasi ya kipekee sana Kama Mtoto wa kike aliyemzaa yeye mwenyewe, ambaye ana haki zote za kupokea mema yote ya Baba yake.

Tujiulize ni wanawake wangapi leo Bwana anaweza kuwaita binti zangu? Usidhani Kristo kukuita binti yake, kwasababu ya umri wako mdogo, au mrembo wako, au utanashati wako, hilo halipo, yeye hana jicho la mwilini, kama sisi tulilonalo, haangalii umri wala umbile.

Kama wewe ni mwanamke lakini unafika kwa Kristo ili kujaribu jaribu tu, uone kama Bwana atakujibu au la!,atakusaidia au la! unamlinganisha na wale waganga wa kienyeji uliowahi kuwatembelea huko nyuma.. uone kama atajibu au la!. Ujue kuwa wewe sio binti wa Yesu.

Mabinti wa Yesu, tangu walipokutana na Yesu utawakuta wametulia kwa Bwana hadi sasa, wanaouhakika na waliyemwendea, hawahitaji kusaidiwa na mtu, kuelewa kuwa Yesu ni muweza, wanafanya mambo yao wakiwa wame-relax, huwezi kuwakuta leo kanisani Kesho, disco,  leo wamevaa magauni, Kesho wanakatiza barabarani na visuruali na vikaptura, leo kwa nabii huyu Kesho kwa yule..huwezi kuwakuta wapo namna hiyo.

Hao ndio binti za Mungu. Na faida yao ni kuwa kwasababu wameshaitwa binti za Mungu, tayari wanaourithi kutoka mbinguni. Jambo ambalo wengi hawajui wakidhani kila mtu atakuwa mrithi wa kila baraka ya Mungu mbinguni.

Dada/mama/bibi tambua ni nini Kristo anatamani kuona kwako, acha kutangatanga na huu ulimwengu, Acha kujaribu jaribu, maanisha kumfuata Kristo.. Yeye mwenyewe anasema.

2Wakorintho 6:17 “Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha.

18 Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu WANANGU WA KIUME NA WA KIKE”,

Kumbuka hizi ni siku za mwisho, Kristo anarudi siku yoyote. Bado tu hujatulia kwa Bwana? Injili tuliyobakiwa nayo sasa hivi sio ya kubembelezewa tena wokovu, ni wewe mwenyewe aumke usingizini, umtafute Mungu wako. Kwasababu muda umeshaisha.

Maran atha..

Usikose sehemu ya tatu na ya mwisho ya Makala hii, ambayo, tutaona pia ni kwanini Bwana Yesu aliwatambua wanawake wengine kama MAMA.

Bwana akubariki..

Maran atha

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Rudi nyumbani

Print this post

Biblia inasema tusiwe kwazo kwa yeyote, je! inawezekanikaje kwa dunia hii ya sasa?(2Wakorintho 6:3).

Jibu; Tusome,

2 Wakorintho 6:3 “Tusiwe kwazo la namna yo yote katika jambo lo lote, ili utumishi wetu usilaumiwe”

Leo hii ukizungumzia neno “kukwaza” moja kwa moja akili za wengi zinalenga katika “kuudhi au kumuudhi mtu”.

Hivyo andiko hilo ni rahisi kulitafsiri, kuwa tusiwakwaze watu (yaani tusiwaudhi) kwa namna yoyote ile.

Lakini kiuhalisia andiko hilo halimaanishi hivyo.

Tafsiri ya neno kikwazo/kwazo ni kitu chochote ambacho kinaweza kumzui mtu asisonge mbele, kwamfano mtu anayesafiri kwa gari na akakuta jiwe kubwa katikati ya barabara, limezuia barabara jiwe lile ni kikwazo kikwazo kwake kwa safar yake.

Sasa kibiblia KWAZO ni kitu chochote kinachomzuia mtu kuingia katika Imani au kusonga mbele katika imani..

Hivyo hapo biblia inaposema kwamba tusiwe KWAZO la namna yoyote..imemaanisha kuwa TUSIWE KIKWAZO KWA MTU YEYOTE KUINGIA KATIKA IMANI.

Vipo vitu vingi ambavyo vinaweza kuwa kikwazo kwa watu wengine kuvutiwa na imani ya kikristo. Na mfano wa vitu hivyo ni maisha ya kianasa na kiulimwengu watu wanayoishi.

Kwamfano uvaaji wako unaweza kuwa kwazo kwa mwingine kumpokea Yesu, huwezi kwenda kumhubiria mtu ampokee Yesu na huku akikuangalia wewe unavaa vimini, Unatembea nusu uchi, au unajiuza, au ni mtukanaji, au mlevi.. Hapo ni lazima utakuwa KWAZO tu la yeye kuingia katika Imani na hata wakati mwingine kusababisha jina la Mungu kutukanwa.

Warumi 2:21 “basi wewe umfundishaye mwingine, je! Hujifundishi mwenyewe? Wewe uhubiriye kwamba mtu asiibe, waiba mwenyewe?

22 Wewe usemaye kwamba mtu asizini, wazini mwenyewe? Wewe uchukiaye sanamu, wateka mahekalu?

23 Wewe ujisifuye katika torati, wamvunjia Mungu heshima kwa kuiasi torati?

24 Kwa maana jina la Mungu latukanwa katika Mataifa kwa ajili yenu, kama ilivyoandikwa”.

Katika hali kama hiyo biblia ndio inatuonya tusiwe Kwazo la namna yoyote ile kwa watu, ili utumishi wetu pia usilaumiwe.
Lakini haimaanishi kuwa tusiwaudhi watu kwa namna yoyote ile!.

Katika haya maisha haiwezekani kuishi maisha ambayo hutawaudhi watu kabisa..kwasababu hata ukitenda mema yote bado utawaudhi tu baadhi ya watu..hivyo hilo ni jambo lisiloepukika.

Lakini kuishi maisha ambayo hatutakuwa KWAZO la mtu kuingia katika ufalme inawezekana kwa asilimia zote, endapo tukijikana nafsi kweli kweli, na tukimtegemea Roho Mtakatifu.

Bwana azidi kutusaidia katika hilo ili tusiwe kwazo kwa yeyote!

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

USIMLAANI KIZIWI, WALA USITIE KWAZO MBELE YA KIPOFU.

INJILI YA MANENO LAINI ITAKUGHARIMU.

 

ZIKIMBIE TAMAA ZA UJANANI! NA MTU YEYOTE ASIUDHARAU UJANA WAKO.

KUSAMBAA KWA ROHO YA MPINGA-KRISTO.

 

Rudi nyumbani

Print this post

Misukule ni nini? ni kweli ipo? Na je! inaweza kurudishwa?

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe.

Misukule kwa tafsiri inayojulikana na wengi, ni watu waliotekwa kichawi, kwa lengo la kutumikishwa..ambapo kabla ya kutekwa huko, mtu yule anakuwa anatengenezewa kifo bandia, na kuonekana kama amekufa, na hata kuzikwa kabisa..lakini anakuwa hajafa, na kile kilichozikwa kinakuwa si yeye, bali ni kipande kidogo cha gogo, au mgomba.

Ambapo kipande hicho kinageuzwa kimazingara na kuchukua taswira ya yule mtu aliyetekwa. Na hivyo ndugu wa huyu aliyechukuliwa wanakuwa wanadhani wamemzika mpendwa wao kumbe sio.

Sasa swali ni Je! Ni kweli hiyo aina ya ushirikina ipo?.

Jibu ni ndio ipo!. Shetani anao uwezo wa kufanya jambo hilo na mengine Zaidi ya hayo, aliweza kugeuza fimbo kuwa nyoka aliye hai mbele ya Farao, si zaidi fimbo kuwa nyoka aliyekufa?, au fimbo kuwa maiti ya mtu aliyekufa!!..hivyo hilo ni jambo ambalo linawezekana.

Lakini pamoja na kwamba anaweza kufanya hayo,  lakini si rahisi kwake yeye kufanya hivyo, kuna ugumu mkubwa sana kwake….tofauti na wengi tunavyodhani kuwa shetani mambo yote kwake ni mteremko, kwamba lolote atakalojiamulia kwake ni rahisi kulifanya. Nataka nikuambie hata kwa shetani mambo mengine si rahisi kwake bali anapambana sana ili afanikiwe.

Ingekuwa kila kitu kwake ni mteremko, sidhani mpaka leo dunia ingekuwepo..vile vile angewafanya watu wote leo kuwa wabaya kupindukia, lakini utaona ijapokuwa kuna watu wengi walio waovu na ambao hawajampokea Yesu, LAKINI BADO SI WABAYA KUPINDUKIA!!. Si kwamba shetani hapendi kuwafanya wawe wabaya sana!.. anatamani kuwafanya kuwa wabaya kupindukia..Lakini anashindwa na kukwama kwa wengi.. Kwasababu si kila mlango ni mrahisi kwake kuuingia.

Ndio maana utaona ataweza kumshawishi na kumfanya mtu kuwa mwasherati, na mlevi lakini kumshawishi kuwa mkatili na gaidi inakuwa ni ngumu!.. Hiyo ni kwasababu kuna milango ambayo si mirahisi kwa shetani kuiingia kwa mwanadamu.. ataweza kumshawishi mtu kuwa mwongo na mtukanaji na mzinzi wa kupindukia lakini akashindwa kumfanya awe Jambazi linaloua watu kikatili!..utaona ni watu baadhi tu miongoni mwa watu wake anaofanikiwa kufawanya magaidi.

Vivyo hivyo ni watu baadhi tu ndio ataweza kuwateka na kuwageuza kuwa Misukule, na kuwatumikisha, lakini si jambo rahisi kwake, ambalo linaweza kufanyika kwa jinsi anavyotaka yeye au kwa mtu yeyote.

Jambo la mtu kuchukuliwa msukule, ni gumu sana kutokea kwa mtu, kama vile, ilivyo ngumu kwa kahaba, au mlevi kuwa gaidi yule wa kuchinja watu!.. Mtu anaweza asiwe hata ndani ya imani ya kikristo na ikawa ngumu kwa shetani kumchukua msukule. Ni kwasababu kuna ulinzi Fulani ambao upo duniani wa Roho Mtakatifu.

Ni watu wachache sana ambao ndio wanaweza kuchukulika msukule na kutekwa kwa namna hiyo.. (tutakuja kuliona hilo kundi mbele kidogo)..Kama tu vile ilivyo ni watu wachache sana walio katika ufalme wa giza wanaoweza kufanywa kuwa magaidi na shetani…

Wapo wengi walio waovu duniani, wazinzi, waongo, lakini bado isiwe rahisi kwao kuchukuliwa msukule..

Hivyo msukule sio jambo kubwa na linalofanyika kirahisi kama linavyotukuzwa leo. Kiasi kwamba leo hii kati ya misiba 10 inayotokea kiajabu ajabu.. basi 2 au 3 katika hiyo, utasikia watu wakisema huyo mtu kachukuliwa msukule, hajafa!.

Jambo ambalo si kweli!.. ambalo lengo lake ni kuukuza ufalme wa giza na kupachika hofu..

Ingekuwa hivyo ndivyo nadhani shetani angeshamaliza watu wote duniani, kuwachukua misukule..Maana walio nje ya Imani, ni wengi kuliko walio ndani ya Imani. Nchi ya  India na China tu zina mabilioni ya watu wanaoabudu miungu, ambao hata hawamjui Mungu wa kweli, hao nadhani angeshawamaliza wote.. Lakini wengi wa hao wapo salama tu!.

Nchi za Ulaya na Marekani, zina idadi kubwa  ya watu wasioamini kama Mungu yupo, lakini wengi wao wapo huru, hawajachukuliwa misukule. Hata katika jamii zetu, wapo wengi walio waovu lakini wapo wanaishi.. Je! Unadhani shetani hawaoni na kuwatamani??.. anawaona na kuwatamani sana… lakini si rahisi kwake, kwasababu yupo Roho Mtakatifu duniani ambaye anamzuia shetani kujiamulia kufanya baadhi ya mambo.. Maandiko yanasema baada ya huyo kuondolewa duniani ndipo mambo yatabadilika ulimwenguni (2Wathesalonike 2:7).

Sasa wengi wa wanaochukuliwa Msukule, wanakuwa ni watu wanaoangukia katika mojawapo ya makundi haya matatu

1. Wachawi na Washirikina.

Hili ni kundi la kwanza, ambalo ni rahisi sana kuchukuliwa msukule. Wengi wa wanaochukuliwa msukule ni aidha wao wenyewe walikuwa wachawi, au washirikina. Hivyo kama ni mshirikina au mchawi basi, ni rahisi kwako kutekwa na adui.

2. Watu wanaohudhiria kwa waganga wa kienyeji.

Mtu yeyote ambaye anakwenda kwa mganga wa kienyeji, maana yake kamsogelewa shetani kwa hiari yake mwenyewe, hivyo kajiuza kwa shetani na shetani anaweza kumfanya lolote, ikiwemo kumchukua msukule.

3. Watu wanaoyadharau Maneno ya Mungu kwa makusudi.

Hili ni kundi lingine ambao li karibu sana na kuchukuliwa msukule. Mtu yeyote anayeidharau injili kwa muda mrefu, na makusudi, huyo anajiondolea ulinzi wa kiMungu kwa haraka sana pasipo yeye kujijua..na anakuwa amejiuza kwa shetani bila yeye kujua.

Utauliza kivipi?

Kuna mfano mmoja wa mtu aliyechukuliwa Msukule na shetani mwenyewe kwenye biblia..huyo alikuwa ni mtu wa kuyadharau maneno ya Mungu, alipoonywa mara nyingi atubu alishupaza shingo..na ndipo walinzi wa mbinguni ambao kazi yao ni kuwalinda wanadamu, waliopoondoa ulinzi juu yake.. na kumruhusu shetani amchukue. Na huyo si mwingine zaid ya Mfalme Nebukadneza..

Danieli 4:23 “Tena, kwa kuwa mfalme alimwona mlinzi, naye ni mtakatifu, akishuka kutoka mbinguni, akisema, Ukateni mti huu, mkauangamize; ila kiacheni kisiki cha shina lake katika ardhi, pamoja na pingu ya chuma na shaba, katika majani mororo ya kondeni; kikatiwe maji kwa umande wa mbinguni, na sehemu yake iwe pamoja na wanyama wa kondeni, hata nyakati saba zipite juu yake;

24 tafsiri yake ni hii, Ee mfalme, nayo ni amri yake Aliye juu, iliyomjia bwana wangu, mfalme

25 ya kuwa utafukuzwa mbali na wanadamu, na makao yako yatakuwa pamoja na wanyama wa kondeni, nawe utalazimishwa kula majani kama ng’ombe, nawe utatiwa maji kwa umande wa mbinguni, na nyakati saba zitapita juu yako; hata utakapojua ya kuwa Aliye juu ndiye anayemiliki katika ufalme wa wanadamu, naye humpa yeye amtakaye, awaye yote.

26 Na kwa kuwa waliamuru kukiacha kisiki cha shina lake; ufalme wako utakuwa imara kwako, baada ya wewe kujua ya kuwa mbingu ndizo zinazotawala.

27 Kwa sababu hiyo, Ee mfalme, shauri langu lipate kibali kwako; ukaache dhambi zako kwa kutenda haki, ukaache maovu yako kwa kuwahurumia maskini; huenda ukapata kuzidishiwa siku zako za kukaa raha.

28 Hayo yote yakampata mfalme Nebukadreza.

29 Baada ya miezi kumi na miwili, alikuwa akitembea ndani ya jumba la kifalme katika Babeli.

30 Mfalme akanena, akasema, Mji huu sio Babeli mkubwa nilioujenga mimi, uwe kao langu la kifalme, kwa uwezo wa nguvu zangu, ili uwe utukufu wa enzi yangu?

31 Hata neno lile lilipokuwa katika kinywa cha mfalme, sauti ilikuja kutoka mbinguni, ikisema, Ee mfalme Nebukadreza, maneno haya unaambiwa wewe; Ufalme huu umeondoka kwako.

32 Nawe utafukuzwa mbali na wanadamu, na makao yako yatakuwa pamoja na wanyama wa kondeni; utalishwa majani kama ng’ombe, na nyakati saba zitapita juu yako, hata utakapojua ya kuwa Aliye juu ndiye anayemiliki katika ufalme wa wanadamu, naye humpa amtakaye, awaye yote.

33 Saa iyo hiyo jambo hilo likatimizwa, likampata Nebukadreza; alifukuzwa mbali na wanadamu, akala majani kama ng’ombe, na mwili wake ulilowa maji kwa umande wa mbinguni, hata nywele zake zikakua, zikawa kama manyoya ya tai, na kucha zake kama kucha za ndege”

Umeona?.. huyu alitekwa na shetani mwenyewe kwa ruhusa ya Mungu.. kwasababu alikuwa anayadharau wazi maneno ya Mungu, akachukuliwa msukule, maandiko yanasema akalishwa majani kama ng’ombe. Misukule ya siku hizi inalishwa pumba, na vitu visivyofaa..

Hiyo inatufundisha na sisi kutoyadharau maneno ya Mungu na kutokuwa na kiburi. Mungu akitukataa hakuna atakayetukubali.. Na Mungu akiondoa ulinzi wake juu yetu, kama alivyoondoa kwa Nebukadneza, unadhani ni nini shetani atakachokuwa amebakiwa nacho kwetu, Zaidi ya kutuchukua mateka?.

Na Mwisho, je! mtu anatokaje kama tayari kashachukuliwa Msukule?

Mtu anapokuwa katika kutekwa huko, akili zake zinakuwa zimefungwa anakuwa kama kichaa.. Hivyo kama hatakutana na mtu atakayemwombea huko basi atabaki katika hali hiyo hiyo mpaka Bwana atakapomfungua mwenyewe, kama alivyomfungua Nebukadneza..

Na kumbuka watu hawa(Misukule) wanakuwa wapo katika mwili, na si katika roho, kwasababu hawajafa.. Ni ngumu kuwaona kwasababu waliowashika wanawaficha katika nyumba zao..kama mtu anayeficha almasi ndani kwake….hivyo ni ngumu kujua, lakini wapo katika mwili na wanaonekana kwa macho kabisa.. hivyo wanapoonekana ni kama vile kichaa aliyeonekana barabarani.. hivyo anaweza kuchukuliwa na kufanyiwa maombezi, ili akili zake zimrudie..na anapofunguka anarudia hali yake ya kawaida, kama mtu aliyepona ukichaa. kwasababu alikuwa hajafa. (lakini kumbuka si kila kichaa ni msukule)… Na si kila misiba ni misukule.

Na vile vile hakunaga huduma ya kwenda kutafauta misukule, au kuichimbua..au kuiita huko iliko na kuirudisha.. kwasababu hujui ni nani na nani ndio kachukuliwa. Roho Mtakatifu ndiye anayefunua kwamba mahali Fulani katika nyumba Fulani kuna mtu kafungwa, anahitaji kuombewa afunguliwe..Hivyo!, na si kwenda kuzunguka na kutafuta msukule!.

Na Ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko ufalme wa giza. Roho ya Mungu duniani ni KUU kuliko roho ya shetani.

Hivyo hatuhitaji kuishi kwa hofu ya kuchukuliwa msukule, wala watoto wetu kuchukuliwa msukule, wala hatuhitaji kufuatilia sana habari za kichawi, kama tayari tupo ndani ya Kristo. Tunapokuwa ndani ya Kristo, tunapaswa tuongeze bidii katika kumjua sana Mungu Zaidi ya shetani.. Tukimjua sana Yesu na neema yake na utukufu wake..maarifa hayo yanatosha kutulinda na kutuhifadhi, hata kama hatujawahi kusikia neno uchawi katika maisha yetu.

Jambo la hatari shetani analolifanya katika siku hizi za mwisho, ni kuhakikisha anaupandisha hadhi ufalme wake, ambao tayari upo chini. Ndio hapo atanyanyua hata watu wahubiri ili kusifia kazi za shetani, na uchawi wake. Wakati kiuhalisia uchawi, si kitu kwa walio ndani ya Kristo, na wala Bwana Yesu hajawahi kutupa maagizo tukajifunze juu ya uchawi, ili tumwelewe yeye, au tumpendeze yeye. Anachotaka kwetu ni SISI tumjue yeye, na si tujue majina ya mapepo na elimu ya kuzimu.

Hivyo kama umempokea Yesu, tafuta kumjua Zaidi Yesu, na kama bado basi mpokee leo. Na tafuta kumjua.

Bwana akubariki.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Jiunge na Group letu ya whatsapp, la masomo ya kila siku kwa kubofya hapa > Group-whatsapp


Mada Nyinginezo:

KUOTA NYOKA.

EDENI YA SHETANI:

EDENI YA SHETANI:

Kwa maana kahaba ni shimo refu; Na malaya ni rima jembamba.

Kwanini Mungu awachome watu kwenye ziwa la moto na hali yeye ndiye aliyewaumba?

Rudi nyumbani

Print this post

UTAPENDA KUCHANGIA HUDUMA HII?

Tutamshukuru Mungu kwa ajili yako, kwa mchango wako, ili kuifanya injili hii isonge mbele Tuma sadaka yako kwa namba hizi:
Airtel:+255789001312 -Devis Magembe
Mpesa: +255767992434-Denis Magembe


This will close in 315 seconds