JE BADO UNASUBIRIA MAJI YACHEMKE?

JE BADO UNASUBIRIA MAJI YACHEMKE?

Lipo la kujifunza juu ya Yule mtu aliyepooza kwa miaka 38,  na jinsi alivyopokea uponyaji wake katika siku moja.

Maandiko yanasema mtu huyu pamoja na wenzake walikuwa wakingojea muujiza katika birikia (au bwawa) moja lililoitwa bwawa/birika la Bethzatha, kwamaana kuna wakati malaika alishuka na kuyatibua maji ya bwawa hilo, na alipoyatibua yalikuwa yanaonekana mfano wa kuchemka.. (Siku zote Maji yaliyotibuliwa kimwonekano ni kama yanayochemka).

Kwahiyo wote walimtegemea huyu malaika ashuke, labda pengine alishuka kila baada ya miaka 2 au mitatu… Na cha ajabu ni kwamba pindi anaposhuka na kuyatibua maji, anayeponywa ni mtu mmoja tu!, (Yule aliyeingia wa kwanza) wengine mtasubiri mzunguko mwingine ambao haujulikani tena utakuwa ni lini.

Kwahiyo hawa wagonjwa walikuwa wanaishi kwa mashindano, kila mmoja akipambana kuingia wa kwanza.

Lakini siku moja Bwana Yesu alipita maeneo yale, na kuona hilo jopo la wagonjwa! Likisubiri Maji yachemke, likisubiri MAJI HAYO YA UPAKO, yavuviwe.. Na hapa anakutana na mmoja wa wagonjwa ambaye angalau alikuwa na imani ya kuponywa. Na swali la kwanza alilomwuliza “ni kama anataka kupona”..kama hataki maana yake asingemlazimisha..(siku zote Bwana huwa hatulazimishi kupona, ndio maana alisema tuombe!, maana yake tusipoomba hawezi kutulazimisha kupata)..

Tusome…

Yohana 5:1  “Baada ya hayo palikuwa na sikukuu ya Wayahudi; naye Yesu akakwea kwenda Yerusalemu.

2  Na huko Yerusalemu penye mlango wa kondoo pana birika, iitwayo kwa Kiebrania Bethzatha, nayo ina matao matano.

3  Ndani ya hayo jamii kubwa ya wagonjwa walikuwa wamelala, vipofu, viwete, nao waliopooza, [WAKINGOJA MAJI YACHEMKE.

4  Kwa maana kuna wakati ambapo malaika hushuka, akaingia katika ile birika, akayatibua maji. Basi yeye aliyeingia wa kwanza baada ya maji kutibuliwa, akapona ugonjwa wote uliokuwa umempata.]

5  Na hapa palikuwa na mtu, ambaye amekuwa hawezi muda wa miaka thelathini na minane

6  Yesu alipomwona huyu amelala, naye akijua ya kuwa amekuwa hali hiyo siku nyingi, ALIMWAMBIA, WATAKA KUWA MZIMA?

7  Yule mgonjwa akamjibu, Bwana, mimi sina mtu wa kunitia birikani, maji yanapotibuliwa; ila wakati ninapokuja mimi, mtu mwingine hushuka mbele yangu.

8  Yesu akamwambia, Simama, jitwike godoro lako, uende.

9  Mara yule mtu akawa mzima, akajitwika godoro lake, akaenda. Nayo ilikuwa ni sabato siku hiyo”.

Ni somo gani tunajifunza hapo?

1.MAJI YA UPAKO HAYANA MATUMAINI YOYOTE.

Hebu tafakari huyu mtu ametumaini juu ya maji hayo ya upako kwa miaka 38, na hajaambulia chochote..Na ndicho kinachoendelea sasa, Idadi kubwa ya watu wamemwacha Yesu na kujitumainisha na Maji ya upako, chumvi za upako, na mafuta ya upako.. Pasipo kujua kuwa Mungu hajawahi kuvitukuza vitu hivyo… Mungu kamtuza tu Mwanae kupitia jina lake (jina la Yesu).

Ni mara chache chache sana Bwana Mungu anaruhusu watu wapokee uponyaji kupitia maji, au mafuta au leso kama Paulo. (Matendo 19:11-12)., lakini hiyo ni mara moja sana tena baada ya miaka mingi.. sio jambo la desturi kama linavyohubiriwa leo na manabii wengi wa uongo, ndio maana huoni mahali popote Paulo akiitumia hiyo kama staili ya kuombea watu wapone.

Hakuna mahali Petro katuma katengeneza mafuta yenye lebo yake na kuyapeleka Makedonia na Antiokia ili watu wafunguliwe.

Sasa kwanini Mitume pamoja na wakristo wote wa kanisa la kwanza hawakufanya hiyo aina ya uganga?? Ni kwasababu waliielewa hiyo habari ya huyo mtu aliyeponywa na Bwana pale kwenye birika la Bethzatha.

Jambo la Pili tunaloweza kujifunza ni kuwa Bwana Yesu baada ya kumponya huyo mgonjwa, hakumwambia jitiwike godoro lako ubaki hapo birikani, badala yake alimwambia aondoke hapo birikani… Hiyo ikifunua kuwa Kristo hakuwa anapendezwa na watu kudumu birikani, vile vile Leo hii Kristo ni Yule Yule hajabadilika.. hata leo hapendezwi na watu wanaodanganywa katika visima vijulikanavyo kama visima vya upako.

2. BWANA ALIKUWA ANAPITA KATIKATI YA WAGONJWA.

Jambo lingine tunaloweza kujifunza ni ziara ya Bwana kando kando ya lile birika..Utaona Bwana Yesu aliye mponyaji mkuu hakuwemo kwenye lile birika, wala hakuyagusa yale maji..bali alikuwa nje anapita pita akitafuta mtu wa kumponya, na huenda aliwajaribu wengi lakini walimdharau na kuendelea kujitumainisha katika kisima cha upako!.

Na Kristo ni Yule Yule, hata leo hayupo ndani ya kisima chochote kile kijulikanacho kama kisima cha upako, haijalishi hicho kisima kina sifa au historia ya kutendeka miujiza mikubwa kiasi gani, bado Kristo hayupo hapo!!!, hata kisima cha Bethzatha kilikuwa na historia ya miujiza mikubwa lakini KRISTO hakuyagusa hata maji yake..

Ndugu acha kujitumainisha katika maji, chumvi, mafuta, udongo au visima vijulikanavyo kama vya upako.. HUKO KRISTO HAYUPO!!! Na unadanganywa kuwa utapokea uponyaji, huo uponyaji utaungoja karne na karne hutaupata kwasababu Mungu Baba hajatukuza visima, wala michikichi, wala alizeti, wala mapeasi ya upako wala mchanga..Mungu Baba kamtukuza Mwanae  mmoja tu!!!… ambaye ni YESU KRISTO!!!.. Ukijaribu kutafuta faida nje ya huyo Mmoja YESU, unapoteza muda, na unaelekea njia ya kuchanganyikiwa kama usipofunguka macho mapema…

Wafilipi 2:9 “Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina;

10  ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi;

11  na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba”.

3. BWANA AMTOA YULE MTU PALE BIRIKANI.

Jambo la tatu na la mwisho tunaloweza kujifunza ni kuwa Bwana Yesu baada ya kumponya huyo mgonjwa, hakumwambia jitiwike godoro lako ubaki hapo birikani, badala yake alimwambia aondoke pale birikani… Hiyo ikifunua kuwa Kristo hakuwa anapendezwa na watu kudumu birikani, vile vile Leo hii Kristo ni Yule Yule hajabadilika.. hata leo hapendezwi na watu wanaodanganywa katika visima vijulikanavyo kama visima vya upako.

Yesu Kristo, kupitia jina lake ndiye chemchemi ya upako, ndiye kisima cha upako, yeye ndiye mafuta ya upako, yeye ndiye udongo wa upako, tukimpata huyo na kuyashika maneno yake, basi hakuna kifungo chochote kitakachodumu katika maisha yetu.. Yule mgonjwa alimpata Yesu akafunguliwa magonjwa yake ambayo kisima cha upako kilishindwa kumfungua, sasa tunahitaji fundisho gani tena tuelewe, na ilihali biblia imeshatupa hili funzo la huyu mgonjwa?

Je umemwamini Yesu?, je umefungwa na nguvu za giza?.. usikimbilie maji, wala mafuta bali kimbilia toba!, omba rehema na toba mbele zake kwa kumaanisha kabisa na atakusamehe na kukupa Roho wake mtakatifu na zaidi sana kukuponya tena bure!

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

 Je! Ni sahihi kutumia maji ya upako,katika kufanya maombezi?

NITAUVUTAJE UWEPO WA ROHO MTAKATIFU KARIBU NAMI?

OLE WAKO KORAZINI NA BETHSAIDA.

BIRIKA LA SILOAMU.

JINSI YA KUPOKEA UPONYAJI, TUNAPOMWOMBA BWANA ATUGUSE MARA YA PILI.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments