KWANINI TUNAPASWA KWENDA KUIHUBIRI INJILI KWA UJASIRI WOTE?

KWANINI TUNAPASWA KWENDA KUIHUBIRI INJILI KWA UJASIRI WOTE?

Karibu tujifunze biblia, Neno la Mungu wetu, lililo taa na mwanga wa njia zetu.

Je unajua ni kwanini tunapaswa kwenda kuihubiri injili kwa ujasiri wote, tena pasipo woga wowote?.. na tena sio kwa watu baadhi tu, bali kwa watu wote wa dunia yote na katika kila mtaa, na wilaya, na mkoa, na Taifa, na kila bara?.. Ni lazima tukijue kitu kinachotupa ujasiri wa sisi kufanya hivyo!, tusipokujua hicho tutakuwa waoga wa kuhubiri.

Sasa hebu tusome maandiko yafuatayo..

Mathayo 28:18  “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, NIMEPEWA MAMLAKA YOTE MBINGUNI NA DUNIANI.

19  Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu;

20  na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari”

Hicho ni kipindi ambacho Bwana Yesu aliwatokea wanafunzi wake baada ya kufufuka kwake.. Na siku hiyo alipowatokea alikuja na agizo maalumu kwao!.. Na agizo lenyewe ni hilo la “KWENDA KUHUBIRI INJILI DUNIANI KOTE”.

Lakini agizo hilo ni gumu na zito!.. Yaani kwenda ulimwenguni kote kusema habari za Masihi, kwenda katika jamii za watu wabaya, na wakatili na wauaji, kwenda katika jamii za wasomi na watawala, na tena ulimwenguni kote?, hilo jambo si jepesi hata kidogo!.

Sasa Bwana Yesu alijua hilo jambo sio dogo wala sio lepesi, hivyo akatanguliza kwanza SABABU za kwanini awaagize kwenda duniani kote, katika mitaa yote, na miji yote na vijiji vyote na kwa watu wote wakawahubirie watu..

Na sababu yenyewe ndio tunayoisoma katika mwanzoni mwa mistari hiyo.. hebu tusome tena mstari wa 18..

Mathayo 28:18  “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, NIMEPEWA MAMLAKA YOTE MBINGUNI NA DUNIANI.

19  Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu”

Hiyo sentensi ya kwanza kwamba “amekabidhiwa mamlaka yote mbinguni na duniani” ndio iliyowapa ujasiri Mitume wake kwenda kuhubiri injili kila mahali.

Hebu tafakari leo hii umetumwa kupeleka ujumbe kwa watu Fulani katika mkoa Fulani, halafu aliyekupa huo ujumbe ni mtu tu wakawaida..bila shaka itakuwa ni ngumu kwako kupeleka ujumbe kwa jamii ya hao watu kwasababu kwanza huenda wana nguvu kuliko wewe, hivyo ukiwapelekea vitu tofauti na itikadi zao au jamii zao ni rahisi kujitafutia madhara.. lakini hebu tengeneza picha ni Raisi ndio anakupa ujumbe uwapelekee watu Fulani, ni dhahiri kuwa mashaka yatapungua na ujasiri utaongezeka…kwanini?.. Kwasababu unajua kuwa Raisi amepewa mamlaka yote juu ya hii nchi!..

Vivyo hivyo na kwa mitume…waliposikia tu hayo maneno ya kwanza ya Bwana Yesu kwamba “amepewa mamlaka yote ya mbinguni na duniani” ikawa ni sababu tosha ya wao kuwa na ujasiri wa kwenda kila mahali, kwasababu wanajua kila mahali waendapo tayari ni milki ya Kristo, kwamba Kristo ana nguvu juu ya hilo eneo… na maana akawaambia waende kwasababu yeye atakuwa pamoja nao hata mwisho wa Dahari (yaani mwisho wa Nyakati). Na sasa tupo karibia na Mwisho wa Nyakati, Kwahiyo Kristo yupo na sisi pale tunapokwenda kuieneza injili.

Ndugu usisubiri Bwana Yesu akutokee na kukuambia nenda kahubiri!.. Tayari agizo lilishatoka miaka zaidi ya elfu 2 iliyopita… kwamba nenda kahubiri injili.

Wengi leo hii wanaogopa kwenda kuhubiri injili, kwasababu hawana vitu vya kuhubiri.. Bwana Yesu hakuwaambia wanafunzi wake wakanunue vyombo vya miziki kwanza, au spika au wapate nguo nzuri ndipo wakahubiri injili..hapana! kinyume chake aliwaambia wasibebe chochote kwasababu huko waendako watavipata vyote.

Na wewe unasubiri nini usiende kuhubiri injili? Ni wito gani unaoungoja?, ni sauti gani unayoingoja?.. na upako gani unaoungoja?…ni ujuzi gani unaousubiri?.. ukisubiri ufikie ujuzi Fulani au maarifa Fulani hutayafikia kwasababu kila siku tunakua kutoka utukufu hadi utukufu, hakuna siku tutasema tumeshajua!!.. kila siku tunajifunza..hivyo usiseme ngoja nifikia levo Fulani ndipo nikahubiri, hizo ni akili za kichanga!.. Nenda kahubiri injili..

Sasa unaanzia wapi kuhubiri injili?

Kabla ya kwenda mbali anza kuhubiri injili hapo hapo ulipo, kabla ya kufikiri kwenda nje ya mtaa anza katika mtaa wako, anza katika nyumba yako, anza katika ofisi yako, anza katika shule yako.. hakikisha hapo umemaliza kwanza na watu wameitii injili ndipo uende nje!.. na katika hatua hiyo ya awali kumbuka kuwa Kristo yupo na wewe, na kumbuka kuwa yeye amekabidhiwa mamlaka yote ya mbinguni na duniani, kwahiyo hakuna nguvu zozote wala mamlaka yoyote unayoweza kushindana na hilo agizo la Bwana Yesu.

Bwana Yesu akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

ENZI NA MAMLAKA AMEZIFANYA KUWA MKOGO

NI KWA NAMNA GANI SHETANI ANAIZUIA INJILI?

Ni kweli Paulo alipuuzia maonyo aliyopewa ya kwenda Yerusalemu?

Ni sahihi kusema sikuitiwa kuhubiri ubatizo kama Paulo alivyosema (1Wakorintho 1:17)?.

TUNALINDWA NA NGUVU ZA MUNGU.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments