Mwanazuoni ni mtu gani kibiblia?

Mwanazuoni ni mtu gani kibiblia?

Mwanazuoni ni mtu aliyejikita katika utafiti au usomi wa ndani katika tasnia Fulani, lengo lake likiwa ni kupata uvumbuzi wa yale magumu yenye utata au yaliyojificha.. Hivyo mwanazuoni wa biblia ni mtu anayeingia ndani kujifunza Biblia, ili kuieleza katika urahisi zaidi au katika ufasaha zaidi  kwa jamii au kutoa majibu ya mambo magumu yaliyo ndani ya biblia.

Mwanazuoni anajitofautisha na mwana-theolojia, kwa namna ya kwamba mwanatheolojia yeye yupo kisomi zaidi, kusoma kanuni na taratibu za kidini, hivyo anapohitimu, anakuwa amepata maarifa yale yale yaliyokwisha kuandaliwa. Lakini mwanazuoni, ni mtu ambaye hafungwi na taratibu, anaweza jitenga, kuchunguza, kusoma kwa ndani na kujua maana ya mambo.

Si kila mwanazuoni lazima apitie vyuo vya biblia.. Mtu akijikita katika kusoma biblia kwa undani na kujua siri nyingi zilizo ndani yake, huyo huitwa pia mwanazuoni.

Vilevile si kila mchungaji ni mwanazuoni. Mchungaji kazi yake ni kulichunga kundi la kulilisha, lakini ni vizuri pia mchungaji yeyote awe mwana-zuoni wa biblia. Kwasababu katika siku hizi za hatari zenye mafundisho mengi potofu, na udanganyifu mwingi wa dini za uongo, kila mmoja wetu hana budi kuwa mwanazuoni(mwanafunzi) wa biblia, ili awasaidie na wale ambao, hawajui kweli ya Neno la Mungu.

Lakini..

Kuna aina mbili za wanazuoni;

  1. Wanazuoni ambao hawana msukumo wa Roho Mtakatifu.
  2. Wanazuoni ambao huvuviwa na Roho Mtakatifu.

Mfano wa hilo kundi la kwanza, ndio wale waandishi na mafarisayo, waliokuwa kipindi cha Bwana Yesu, hawa waliipokea torati kama vitabu vya kidini tu, na kuvikariri, na kutunga hata na taratibu zao nyingine ambazo Mungu hakuwaagiza kabisa.

Walikuwa wanayachunguza maandiko, lakini wanamweka Mungu nyuma, Matokeo yake wakashindwa hata  kumwona Kristo katika kila kipengele cha torati walichosoma, badala ya kumpokea wakampinga..Ndipo hapo Yesu akawaambia..

Yohana 5:39  “Mwayachunguza maandiko, kwa sababu mnadhani kwamba ninyi mna uzima wa milele ndani yake; na hayo ndiyo yanayonishuhudia. 40  Wala hamtaki kuja kwangu mpate kuwa na uzima”

Lakini kundi la pili la wanazuoni ni lile ambalo lina nia ya kuujua ukweli, na kiu yao ni wokovu na sio mashindano au usomi, mfano wa hawa ni wale watakatifu wa Beroya, ambao tunawasoma katika..

Matendo 17:10  “Mara hao ndugu wakawapeleka Paulo na Sila usiku hata Beroya. Nao walipofika huko wakaingia katika sinagogi la Wayahudi. 11  Watu hawa walikuwa waungwana kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa walilipokea lile neno kwa uelekevu wa moyo, wakayachunguza maandiko kila siku, waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo. 12  Basi watu wengi miongoni mwao wakaamini, na wanawake wa Kiyunani wenye cheo, na wanaume si wachache”.

Mfano tena wa hawa, ni Nabii Danieli.. ambaye pia biblia inatuonyesha alikuwa ni mtafiti (mwanazuoni) aliyekuwa anasoma sana vitabu, na matokeo yake akagundua hesabu ya miaka ambayo wangekaa Babeli, hivyo akajinyenyekeza mbele za Mungu akaomba dua na rehema, na Mungu akamsikia, na kumfunulia zaidi..

Danieli 9:1 “Katika mwaka wa kwanza wa Dario, mwana wa Ahasuero, wa uzao wa Wamedi, aliyetawazwa kuwa mfalme juu ya milki ya Wakaldayo;  2 katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, mimi Danielii, kwa kuvisoma vitabu, nalifahamu hesabu ya miaka, ambayo neno la Bwana lilimjia Yeremia nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani, miaka sabini”.

Mwingine ni mtume Paulo ambaye mpaka uzee wake alikuwa anasoma vitabu, soma (2Timotheo 4:13), na ndio maana hatushangai  ni kwanini Mungu alimjalia mafunuo mengi namna ile.. mpaka akamuasa na Timotheo naye awe vilevile..

1Timotheo 4:13  “Hata nitakapokuja, ufanye bidii katika kusoma na kuonya na kufundisha”.

Zipo faida nyingi za kila mmoja wetu kuwa mwanazuoni, Kama Apolo asingekuwa mwanafunzi mzuri wa maandiko, asingeweza kuwashinda wayahudi ambao walilisumbua sana kanisa la kwanza kwa imani zao potofu..(Soma Matendo 28:24-28).

Hivyo kuwa mwanazuoni huchangiwa na;  kwanza kwa kuwa na bidii ya kusoma biblia binafsi,  pili kuhudhuria mafundisho ya biblia kanisani, tatu kusoma vitabu mbalimbali vya Kikristo, Nne kusikiliza mafundisho yenye maudhui ya biblia kwenye radio, televisheni na bila shaka, kwenye tovuti kama yetu hii www.wingulamashahidi.org.

Hivi ni baadhi ya vifungu vinavyotuhimiza kuwa wasomi/wanafunzi wa biblia..wenye lengo la kujifunza  kumjua Mungu, (lakini sio mfano wa waandishi na mafarisayo, ambao lengo lao lilikuwa ni vyeo na ukubwa, na heshima waonekane wanayajua maandiko mengi, wasomi, wakubwa waogopwe). Lakini tukiwa na kiu ya kujua mapenzi ya Mungu katika maandiko, ni bora kwetu na kwa wengine..

Wakolosai 4:6  “Maneno yenu yawe na neema siku zote, yakikolea munyu, mpate kujua jinsi iwapasavyo kumjibu kila mtu”.

Mathayo 4: 4  “Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu”.

Yoshua 1:8 “Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana”

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

JINSI YA KUSOMA BIBLIA.

TUNAMHITAJI SANA ROHO MTAKATIFU KATIKA KUYAELEWA MAANDIKO.

Tofauti kati ya maandiko na Neno ni ipi?

UFUNUO NI NINI, NA NITAPOKEAJE UFUNUO KUTOKA KWA MUNGU?

HEKIMA YA KIMUNGU, INAINGIAJE MIOYONI MWETU?

Biblia ni nini?USIACHE KUJIFUNZA NENO LA MUNGU

Gombo ni nini?

Kitabu cha YASHARI kinachozungumziwa katika 2Samweli 1:17-18, ni kitabu gani?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments