Category Archive Uncategorized @sw-tz

WAPENZI, MSIIAMINI KILA ROHO.

Wakati tunaoishi ni wakati ambao kuna machafuko mkubwa sana ya rohoni kuliko hata nyakati nyingine zilizowahi kupita huko nyuma,. Na muasisi wa hayo  ni shetani kwasababu anajua katika agano letu jipya kiini cha Kanisa ni ROHO MTAKATIFU. Hivyo anajua akiruhusu Roho wa Mungu peke yake alitawale kanisa, atawakosa watu wengi sana.

Hivyo tangu ule wakati wa mitume, alibadilisha mbinu zake za kivita, akitaka kulishambulia kanisa, haji tena mwilini, bali, ni anakuja na roho za udanganyifu zinazofanana sana na Roho Mtakatifu wa kweli kumbe sio.

Hivyo kuanzia ule wakati alianza kutoa matoleo mengi sana ya roho hizo. Mpaka sasa matoleo aliyonayo ni ya hali ya juu sana, kiasi kwamba usipokuwa makini utaweza ukavamiwa na roho za udanganyifu ukadhani ni Roho Mtakatifu kumbe ni uongo. Tupo katika wakati ambao si wa kiziamini kila roho zinazohubiriwa na watu.

Na ndio maana mitume walituonya na kusema..

1 Yohana 4:1 “Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani”.

Sasa ili tuwe salama ni vizuri tukajua tabia za kweli za  Roho Mtakatifu zipoje, ili tuwe na amani na tulichokipokea.

  1. Tabia ya kwanza ni kuwa Atakufanya uwe Mtakatifu: 

Kama jina lake lilivyo, “Roho Mtakatifu”, ndicho anachokifanya ndani ya mtu pale anapokuja juu yake rasmi, Atamfanya awe mtakatifu. Kama alivyosema katika 1Wakorintho 3:16, kuwa miili yetu ni lazima iwe mitakatifu kwasababu huyo Roho anayekaa ndani yetu ni Mtakatifu. Hivyo Ni lazima ahakikishe kuwa yale matunda yote ya roho yapo ndani yako sawasawa (Wagalatia 5:22-23)

Hivyo ukiona umepokea Roho, ambayo ndani yako haikupi kiu ya kuwa mtakatifu, yaani kuacha anasa, kuacha uvaaji mbovu, kuacha, miziki ya kidunia, kuacha vimini, na milegezo, kuwa na upendo, na kiasi, basi ujue hiyo sio Roho ya Mungu, haijalishi utanena kwa lugha muda mrefu kiasi gani.. Kimbia hapo, haraka sana.

2) Atakuongoza katika kuijua kweli yote(Yohana 16:13): 

Kazi nyingine ya Roho wa kweli wa Mungu, ni kuwa hatakuacha katika hali hiyo hiyo,ya ujinga wa kiroho uliokuwa nao sikuzote, ni lazima akupigishe hatua za kiufahamu mpaka kufikia kusimama imara katika maandiko. Lakini ukiona umeokoka na miaka nenda rudi, hujui chochote kuhusiana na Neno la Mungu, wewe unachojua ni habari za wachawi na mapepo, ujue kuwa Huyo sio Roho Mtakatifu uliyempokea bali ni roho nyingine ya adui ipo ndani yako.

3) Atamshuhudia Kristo ndani yako : 

Roho Mtakatifu kazi yake ni kutoa ushuhuda wa Kristo katikati ya kanisa lake, na sio wa mwanadamu yoyote. Ikiwa na maana kiini cha kanisa ulilopo, au huduma, unayoitumikia msingi wa hapo ni lazima awe Bwana Yesu Kristo. Na sio mwanadamu Fulani, au mtakatifu Fulani. Ukiona Kristo hapewi kipaumbele chochote, au anachukuliwa kama mtu wa ziada tu, ujue roho ya mpingakristo ipo hapo.

1Yohana 4:2 “Katika hili mwamjua Roho wa Mungu; kila roho ikiriyo kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili yatokana na Mungu.

3 Na kila roho isiyomkiri Yesu haitokani na Mungu. Na hii ndiyo roho ya mpinga Kristo ambayo mmesikia kwamba yaja; na sasa imekwisha kuwako duniani”.

4) Ataweka karama au huduma ndani yako (1Wakorintho 12):

Karama hiyo/ huduma hiyo Roho Mtakatifu anaiweka kwa lengo la kulijenga kanisa la Mungu. Haiwezekani, ukawa umeokoka muda mrefu na miaka mingi, na umesema umepokea Roho Mtakatifu lakini kazi yako katika ufalme wa mbinguni haionekani. Wakati mojawapo ya kazi ya Roho Mtakatifu ni kuweka vipawa ndani yetu.

Hivyo kama hutakuwa mchungaji, au nabii, au mwinjilisti, au shemasi, au mwenye karama ya lugha, n.k basi utakuwa ni nyingine yenye faida katika kanisa kama kukirimu, kuimba, kufadhili n.k. Lakini haiwezekani kiungo kikawa hakina kazi kabisa katika mwili wa Kristo, kama mshirika anayekuja na kuondoka, miaka yote, ukiona hivyo ujue kuwa Roho uliyempokea si wa Mungu, bali ni wa adui.

5) Atachochea kuomba ndani yako. (Warumi 8:26)

Maandiko yanasema Roho Mtakatifu anaugua ndani yetu, kwa namna isiyoweza kutamkwa. Ikiwa na maana Mkristo wa kweli aliyepokea Roho, hataona amani kukaa wiki, miezi, miaka bila kuomba. Ile furaha ya wokovu itaondoka tu ndani yake, Hivyo atalazimika, kuwa mwombaji mzuri, kuhudhuria mikesha, na kufunga wakati mwingine.

Lakini ukiona unayo amani, kukaa mwezi mzima bila kuomba, na ndani yako husikii chochote, au mzigo wowote, hapo umepokea Roho nyingine ya adui. Jitathimini tena.

Tabia hizi tano (5), ukiziona ndani yako. Basi ujue Roho uliyempokea ni kweli Roho Mtakatifu, uwe na amani. Lakini kama hivyo vyote havipo ndani yako, Roho uliyepokea ni ya adui ibilisi. Unachopaswa ufanye ni umaanishe kuokoka katika maisha yako.

Maana yake, utubu dhambi zako kweli kweli, kisha ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO (Matendo 2:38). Kisha baada ya hapo, Roho wa kweli ataingia ndani yako, kuanza kukupigisha hizo hatua.

Kumbuka hizi ni siku za mwisho, na tumeaswa sana tuzijaribu hizo roho, usiridhike, na tabia mojawapo tu, jiulize je! Zote hizo zinaonekana ndani yako?

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

TUJIFUNZE JAMBO KWA WANAWAKE HAWA WAWILI.

Je aliyezungumza na Musa kule jangwani ni Mungu mwenyewe au malaika wake?

ZIFAHAMU KAZI TATU ZA ROHO MTAKATIFU KATIKA ULIMWENGU.

AHADI YA ROHO ILIYOSALIA SASA KWA KIPINDI CHETU.

Rudi nyumbani

Print this post

Nini maana ya “Torati na manabii”?

SWALI: Tukisoma katika maandiko tunaona sehemu kadha wa kadha likitajwa neno “Torati na manabii”. Sasa hii torati na manabii maana yake ni nini? Kwamfano  Mathayo 7:12  inasema

“Basi yo yote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo torati na manabii”.

JIBU: Bwana Yesu aliposema Torati na manabii, alimaanisha Agano la kale, ambalo ndio limeundwa na vitabu vya Musa (Torati), ambavyo ni vitano (5), Mwanzo, Kutoka, Mambo ya Walawi, Hesabu na Kumbukumbu la Torati.  Pamoja na vitabu vyote vya manabii, kama vile, Yeremia, Isaya, Danieli, Ezekieli, Hababuki, Amosi, n.k. hapa ikijumuisha pia, vile vingine kama  Waamuzi, Zaburi, Ayubu, Wafalme,  Mithali, Ruthu n.k. Ambavyo sio moja kwa moja vya manabii, lakini vimebeba nabii za Mungu ndani yake.

Kwahiyo torati na manabii kwa ufupi ni lile agano lote la kale. Hivyo Pale Bwana Yesu alipokuwa anawafundisha juu ya kanuni za kufuata, alirejea biblia yao, akiwaambia kuwa kiini cha biblia hiyo ni UPENDO. Wala hakuna siri nyingine nyuma yake, Torati yote, pamoja manabii wote, walichokuwa wanahubiri ni Upendo, (Ambao umegawanyika, wa Mungu na wanadamu)

Hata sisi wa leo tulio katika agano jipya, tunaposoma biblia yote tujue Ujumbe mkuu tunaoupata katika agano letu ni ule ule UPENDO. Na ndio maana Mtume Paulo alisema.

1Wakorintho 13:1 “Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao.

2 Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi.

3 Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu”.

Hivyo na sisi, tunapaswa tuutafute huu, kwa bidii zote, ili tuonekane kuwa wakamilifu mbele za Mungu.

Shalom

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo. Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group

Mada Nyinginezo:

Rudi nyumbani

Print this post

Kwanini Yesu aliwaambia wale wakoma wakajionyeshe kwa makuhani?

SWALI: Kwanini Bwana Yesu aliwaambia wale watu wenye ukoma waende kujionyesha kwa makuhani?, kwanini asiwaponye tu hivyo hivyo na kuwaacha mpaka awaambie waende kwa makuhani.

Luka 17:12 “Na alipoingia katika kijiji kimoja, alikutana na watu kumi wenye ukoma; wakasimama mbali,13 wakapaza sauti wakisema, Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu!

14 Alipowaona aliwaambia, Enendeni, mkajionyeshe kwa makuhani. Ikawa walipokuwa wakienda walitakasika”.


JIBU: Kama vile Injili ya Kristo inavyowafikia watu katika namna mbili, wengine kuwaokoa na wengine kama ushuhuda kwao (Mathayo 24:14)

Vivyo hivyo na uponyaji wake alivyouachia, alikusudia uwafikie watu kwa namna mbili. Kuokoa na wakati huo huo kuwa Ushuhuda.Si kila uponyaji au muujiza Yesu aliokuwa anaufanya ulikuwa ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu. Hapana, bali ponyaji nyingine aliziruhusu mahususi kwa lengo la kuwa ushuhuda kwa wengine, ili siku ile ya hukumu wasije wakasema hatukuona, au hatukusikia.

Tunasoma jambo kama  hilo katika..

Mathayo 8:1 “Naye aliposhuka mlimani, makutano mengi walimfuata.

2 Na tazama, akaja mtu mwenye ukoma akamsujudia, akisema, Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa.

3 Yesu akanyosha mkono, akamgusa, akisema Nataka; takasika. Na mara ukoma wake ukatakasika.

4 Yesu akamwambia, Angalia, usimwambie mtu; ila enenda zako, ukajionyeshe kwa kuhani, ukaitoe sadaka kama alivyoamuru Musa, IWE USHUHUDA KWAO”.

Ndicho kilichowakuta Makuhani, pamoja na mafarisayo na waandishi. Ni watu ambao walikuwa hawataki kusikia wala kuamini, Hivyo Bwana Yesu, alipowaponya baadhi ya watu hakuwaacha tu hivi hivi waende,kama alivyofanya sehemu nyingine, bali aliwaagiza waende kuwaeleza makuhani miujiza iliyowakuta,. Hivyo walikuwa wanapokea shuhuda nyingi sana kutoka kwa watu  mbalimbali walioponywa.. Pengine kwa siku  hata watu 100. Na kila walipoulizwa ni nani kawaponya wanasema YESU.

Hivyo hata sasa na sisi, tusifurahie tu miujiza ya Mungu anatuletea miujiza mingi, watu wanaponywa, wanafunguliwa, na huku maisha yetu yapo nje ya Kristo. tusifurahie kwasababu tujue ni hukumu tu tunajiandikia. Na ndio maana Bwana alisema maneno haya sehemu fulani;

Mathayo 11:21 “Ole wako, Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu zamani kwa kuvaa magunia na majivu.

22 Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi Tiro na Sidoni kustahimili adhabu zao siku ya hukumu kuliko ninyi.

23 Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa mpaka mbinguni? Utashushwa mpaka kuzimu; kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika katika Sodoma, ungalikuwapo mji huo hata leo.

24 Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma kustahimili adhabu yake siku ya hukumu kuliko wewe”.

Hivyo hiyo ndio iliyokuwa sababu kwanini aliwaambia wakajionyeshe kwa makuhani, kwasababu wao ndio waliokuwa hawamwamini wala kuziamini kazi zake.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312 Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

Ukoma wa nyumba ulifunua nini zamani?

Nini maana ya msiwe waalimu wengi (Yakobo 1:3)?

Kwanini Bwana Yesu alitokea katika ukoo wa Yuda?

MIUJIZA YA KRISTO, HAITEGEMEI KANUNI ZA KIBINADAMU.

Rudi nyumbani

Print this post

Kwanini Bwana Yesu alitokea katika ukoo wa Yuda?

SWALI: Kwanini Bwana Yesu alitokea katika ukoo wa Yuda na sio kwenye koo nyingine kama vile  Yusufu?


JIBU: Hatma ya yale makabila 12, na tabia zao tunaona kwa mara ya kwanza zikifunuliwa na Yakobo Baba yao siku ile alipokuwa anakaribia kufa, alipowaita na kuwabariki. ukisoma pale utaona kila mtoto alinenewa habari zake. Kwasasa hatuwezi kuziandika zote hapa lakini kwa muda wako soma Mwanzo 49:1-28. Utaona.

Sasa,  kulingana na tabiri zile ni kabila moja  la Yuda, ndio lilibeba, vimelea vikuu sana, vimstahili Kristo.

Kwamfano pale makabila hayo yalipofananishwa na Wanyama, utaona Ni Yuda peke yake ndiye aliyefananishwa na SIMBA. Wakati wengine kama vile Naflati lilifananishwa na Ayala, Isakari  kama na Punda, Dani kama na nyoka aumaye, Benyamini kama mbwa-mwitu mkali. Yusufu kama mti mchanga uzaao. Lakini Yuda ni kama SIMBA .

Na sikuzote simba anajulikana kama ni mfalme wa pori, tena jasiri.

Mwanzo 49:8 “Yuda, ndugu zako watakusifu, Mkono wako utakuwa shingoni mwa adui zako. Wana wa baba yako watakuinamia.

9 Yuda ni mwana-simba, Kutoka katika mawindo, mwanangu, umepanda; Aliinama akajilaza kama simba, Na kama simba mke; ni nani atakaye mwamsha?

10 Fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda, Wala mfanya sheria kati ya miguu yake, Hata atakapokuja Yeye, mwenye milki, Ambaye mataifa watamtii.

11 Atafunga punda wake katika mzabibu, Na mwana-punda wake katika mzabibu mzuri. Amefua nguo zake kwa mvinyo, Na mavazi yake kwa damu ya zabibu.

12 Macho yake yatakuwa mekundu kwa mvinyo, Na meno yake yatakuwa meupe kwa maziwa”.

Vilevile kama tunavyosoma utabiri wake, utaona anaambiwa, FIMBO YA ENZI, haitaondoka kwake, ikimaanisha  kuwa fimbo ya kifalme, itakuwa katika uzao wake daima. Yaani kabila hili la Yuda litakuwa ni kabila la kifalme.

Mambo ambayo yanabeba kabisa tabia zote za masihi atakayekuja. Kwamba ni lazima AWE simba, jasiri, mwenye nguvu, na hodari.. Na ndio maana hatushangai kwanini  Bwana Yesu alijiita Simba wa Yuda (Ufunuo 5:5).

Vilevile ni lazima awe Mfalme mkuu sana mwenye nguvu sawasawa na unabii wa (Isaya 9:6). Hivyo kabila lenye enzi za kifalme lilikuwa ni hili na tunathibitisha hilo tangu enzi wa Daudi.

Hivyo hiyo ndio sababu kwanini Bwana Yesu hakutokea kabila lingine lolote Zaidi ya kabila la Yuda, Kwasababu, ilimpasa awe juu ya yote..Lakini kama angetokea kabila ya Yusufu ambalo limetajwa kama kabila lenye mafanikio makubwa, ni wazi kuwa kusingekuwa na vimelea vyovyote vya kifalme kwake.. Jambo ambalo haliwezekani kwa Kristo. Yeye ni lazima awe juu, atawale kama Mfalme wa wafalme, na Bwana wa mabwana. Hivyo ni lazima tabia hizo zianze kuonekana tokea mbali sana, kwenye vizazi vya vya nyuma, hadi kumfikia yeye.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Makanwa ni nini katika biblia? (Danieli 6:22)

FUNGUO WALIZOKUWA NAZO MABINTI WATANO WA SELOFEHADI!

KITABU CHA YUDA: SEHEMU YA 3

KITABU CHA YUDA: SEHEMU YA 1

Rudi nyumbani

Print this post

YANAYOENDELEA SASA KATIKA MADHABAHU YA MUNGU ROHONI.

Madhabahuni ni mahali ambapo Mungu amepachagua kukutana na mwanadamu. Hivyo palipo na madhabahu ya Mungu mtu anaweza kuwasilisha dua zake, ibada yake, na shukrani zake, na Mungu akazipokea. Mahali pasipo na madhabahu haiwezekani kukutana na Mungu, na kama ikitokea hivyo basi ujue ni kwa neema zake tu, kakujibu pengine kwasababu hukuujua ukweli. Lakini hakuna njia mtu anaweza kuwasiliana na Mungu pasipo madhabahu.

Sasa tunapozungumzia madhabahu hatumaanishi lile eneo la mbele kanisani linalopambwa, hapana, hicho ni kivuli tu cha madhabahu, madhabahu halisi kwasasa ipo rohoni kule mbinguni, kiti cha enzi cha Mungu kilipo. Na Yesu mwenyewe ndio nyenzo ya kutufikisha hapo, Ikiwa na maana ili uweze kumfikia Mungu ni sharti DAMU ya Yesu ikutangulie kwanza kuzifunika dhambi zako. Hapo ndipo utajua ni kwanini alisema yeye ndio njia kweli na uzima, mtu hafiki kwa Baba isipokuwa kwa njia yake yeye.(Yohana 14:6) .Watu wengi wanadhani wanaweza kumkaribia Mungu kwa matendo yao wenyewe au dini zao. Hilo halipo kabisaa.

Sasa turudi kwenye kiini cha somo. Ni nini kinaendelea sasahivi  katika madhabahu ya Mungu rohoni. Kama tulivyotangulia kusema madhabahuni ni mahali ambapo watakatifu wanafikisha Maombi yao au  haja zao kwa Bwana.

Na ni vizuri kufahamu watakatifu wamegawanyika katika makundi mawili. Kundi la kwanza ni watakatifu walio hai duniani, na kundi la pili ni watakatifu waliokufa. Na wote hawa wanawasilisha mahitaji yao mbele ya madhabahu ya Mungu mbinguni. Na leo kwa ufupi tutajifunza ni mahitaji gani wanayawasilisha mbele za Mungu.

Utakumbuka Bwana Yesu alitufundisha kuomba, na katika kuomba kule alisema tutamke neno hili..

Mathayo 6:9 “Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, UFALME WAKO UJE,…

Hii ikiwa na maana kuwa kila mtakatifu aliyepo duniani, kumwomba Mungu ufalme wake uje, ni sehemu ya maisha yake ya kila siku. Hivyo mbele ya madhabahu ya Mungu iliyopo mbinguni, maombi haya yanafikishwa na malaika na kuwekwa mbele ya madhabahu ya Mungu,..Na hivyo Mungu anachofanya ni kuiharakisha ile siku ya kurudi kwake, ifike upesi.

Ufunuo 8:3 “Na malaika mwingine akaja akasimama mbele ya madhabahu, mwenye chetezo cha dhahabu, akapewa uvumba mwingi, ili autie pamoja na maombi ya watakatifu wote juu ya madhabahu ya dhahabu, iliyo mbele ya kiti cha enzi”.

Unaona? Lakini si hilo tu, bado upande wa pili wa watakatifu nao waliokufa katika dhiki, wanayo maombi yao wanayoyapeleka..embu tusome..

Ufunuo 6:9 “Na alipoifungua muhuri ya tano, NIKAONA CHINI YA MADHABAHU ROHO ZAO WALIOCHINJWA KWA AJILI YA NENO LA MUNGU, na kwa ajili ya ushuhuda waliokuwa nao.

10 Wakalia kwa sauti kuu, wakisema, Ee Mola, Mtakatifu, Mwenye kweli, hata lini kutokuhukumu, wala kuipatia haki damu yetu kwa hao wakaao juu ya nchi?

11 Nao wakapewa kila mmoja nguo ndefu, nyeupe, wakaambiwa wastarehe bado muda mchache, hata itakapotimia hesabu ya wajoli wao na ndugu zao, watakaouawa vile vile kama wao”.

Unaona, hawa nao wanaonekana wapo chini ya madhabahu, wakiomba.. Hivyo wakati watakatifu wa duniani wanaomba ufalme wake uje..Watakatifu walio ardhini wanaomba mwisho wa waovu ufike.

Walio mbele ya madhabahu wanalia Unyakuo ufike upesi, utawala wa amani wa miaka 1000 uje haraka, karamu ya mwanakondoo ianze upesi.. wakati huo huo waliochini ya madhabahu wanaomba, waovu walipizwe kisasi, wauaji, wafikishwe katika kiama chao, mbingu zikunjwe kunjwe kama ukurusa, mapigo ya vitasa saba yamiminwe juu ya nchi, ili isafishwe, waje wastarehe na Bwana ulimwenguni milele.

Haya ni maombi mazito sana, na yanausumbua moyo wa Mungu, usiku na mchana, vilio vyao na vyetu vinamfikia kila dakika kila sekunde, kutoka huku duniani na kule peponi walipo watakatifu waliokufa.

Na tunasoma majibu Bwana aliyowapa wale waliolala yalikuwa ni haya..”WASTAREHE KIPINDI KIFUPI SANA”.. Kumbe kimebaki kipindi kifupi, majibu ya maombi yote yajibiwe, ndugu yangu, siku isiyokuwa na jina Yesu atarudi, Kama tunavyoona dalili zote, jinsi zinavyotimia kwa kasi sasa, mfano wa gonjwa hili la Corona (Luka 21:11). Hii ni kuonyesha kuwa siku yoyote tutashuhudia tukio la UNYAKUO.

Siku hiyo pengine ni leo usiku, tutashangaa ghafla kundi fulani dogo sana la watu halipo. Ukiona hivyo basi ujue umebaki, na utakachokuwa unasubiria ni kisasi cha Mungu mwenyewe duniani.  Ambacho kitatanguliwa kwanza na ile dhiki kuu ya mpinga-kristo (666), ile ambayo Bwana Yesu alisema haijawahi kutokea wala haitakaa itokee . Na baada ya hapo ndipo mapigo ya vitasa saba yafuate (Ufunuo 16), Kisha, ulimwengu wote kumalizwa. Watu watatamani mauti lakini itawakimbia, ni kilio na kusaga meno.

Usifikiri tuna muda mrefu tena kama zamani, injili ya sasa sio ya kubembelezewa wokovu. Ni wewe mwenyewe ushtuke utoke usingizini, utengeneze mambo yako na Mungu wako. Ukipumbazwa na injili za manabii wa uongo, wanaokufundisha, ustarehe hapa duniani, kana kwamba hii dunia ni urithi wako utaishi hapa milele. Jihadhari sana, kwasababu Yesu alishatuonya juu yao kwamba watawadaganya hata yamkini walio wateule(Marko 13:22).

Hivyo tubu dhambi zako kwa kumaanisha kabisa kugeuka, kisha ukabatizwe katika ubatizo sahihi, wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo. Na Bwana atakupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu. Hapo ndipo utakuwa umezaliwa mara pili. Na ukiendelea kudumu katika wokovu na utakatifu basi hata Kristo akirudi usiku wa leo, unakwenda naye mbinguni.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Kwanini madhabahu zilitengenezwa kwa mawe yasiyochongwa?

Mahali pa juu palikuwa ni wapi kama tunavyosoma katika biblia?

TUFANANE NA WATAKATIFU WA MAKEDONIA.

Je! Mwandishi wa kitabu cha Warumi alikuwa ni Paulo au Tertio?

Ni nani aliyesema “Nitume mimi”? katika (Isaya 6:8)

Rudi nyumbani

Print this post

Kwanini iwe ni nchi ibubujikayo maziwa na asali?

SWALI: Kwanini Mungu aliufananisha uzuri wa Kaanani na kama nchi ibubujikayo maziwa na asali? Kwanini isiwe kitu kingine chochote, labda dhahabu na nafaka?

Kutoka 3:8 “nami nimeshuka ili niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hata nchi njema, kisha pana; nchi ijaayo maziwa na asali; hata mahali pa Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi”.


JIBU: Mungu aliposema Kaanani ni nchi ibubujikayo maziwa na asali, hakumaanisha kuwa kuna mito ya maziwa, au mabomba ya asali, kila mahali hapana. Bali alitumia lugha hiyo ya picha kuonyesha uzuri wa nchi ile jinsi ulivyo.

Kama tunavyojua maziwa yanatolewa na mifugo, kama ng’ombe,. Na ng’ombe ili atoe maziwa mengi na ya kutosha, anategemea sana mazingira yenye malisho mazuri ya kijani na chemchemi nzuri za  maji. Hivyo Hapo ni Mungu alikuwa anawaonyesha wana wa Israeli kuwa nchi waiendeayo si nchi kame, bali ni nchi yenye rutuba nyingi sana, ambayo mboga mboga na malisho mazuri vinastawi, kiasi kwamba tukisema  ni maziwa basi mifugo yao itamwaga maziwa mengi sana, hadi yasiwatoshe kwa wingi wa malisho yaliyopo huko.

Vilevile aliposema asali, aliwalenga nyuki. Na nyuki ni wadudu wanaotegemea sana, aina mbalimbali za mimea na maua ili kutengeneza asali yao, Kama tunavyojua mahali ambapo pana jamii chache za miti na mimea, inawachukua muda mrefu sana kuunda asali kidogo, kwani inawagharimu kutembea umbali mrefu sana, kutafuta virutubisho hivyo.

Lakini kama wapo eneo lenye misitu, na jamii tofauti tofauti za miti na mimea, huwa inawachukua muda mfupi sana. Hivyo Mungu aliposema hiyo nchi ibubujikayo asali, alimaanisha kuwa ni nchi yenye aina mbalimbali ya miti ya vyakula na matunda, Kama tukisema ni nyuki watengeneze asali, basi asali itakuwa ni ya kumwagika sana.tofauti na hiyo nchi ya ukame waliyotoka.

Na ndio maana wale wapepelezi waliotumwa na Musa kwenda kuipeleleza Kaanani, aliporudi na  kichala kikubwa cha mzabibu na tini na mkomamanga,  waliwaambia wana wa Israeli maneno haya;

Hesabu 13:27 “Wakamwambia wakasema, Tulifika nchi ile uliyotutuma, na hakika yake, ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali, na haya ndiyo matunda yake”

Unaona, kwa yale waliyoyakutana nayo huko walithibitisha maneno ya Mungu kuwa ni kweli, kuwa nchi hiyo ni ya maziwa na asali.

Hata sasa, Mungu ana mpango huo kwa watoto wake , kuwafikisha katika nchi hii, lakini ni lazima kwanza, awafundishe kanuni zake, na jinsi ya kuishi ndani yake. Vinginevyo wakiifikia na huku maisha yao bado hajabadilishwa, nchi hiyo itawatapika kama ilivyowatapika wenyeji wa Kaanani. Na kanuni zenyewe ni kuishi sawasawa na amri za Mungu (Neno lake).

Walawi 18:26 “Kwa hiyo mtazishika amri zangu na hukumu zangu, wala msifanye machukizo hayo mojawapo; yeye aliye mzalia, wala mgeni aketiye kati yenu;

27 (kwa kuwa hao watu wa nchi wameyafanya machukizo haya yote, hao waliotangulia mbele zenu, na hiyo nchi imekuwa najisi;)

28 ILI KWAMBA HIYO NCHI ISIWATAPIKE NA NINYI PIA, hapo mtakapoitia unajisi, kama ilivyoitapika hiyo taifa iliyotangulia mbele yenu”.

Lakini tukiishi sawasawa na Neno lake, wakati huo utafika na Bwana atatuingiza katika nchi hiyo kama alivyofanya kwa wana wa Israeli walipozitii amri zake.

Hesabu 14:8 “Ikiwa Bwana anatufurahia, atatuingiza katika nchi hii atupe iwe yetu, nayo ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali”.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

UNYAKUO.

Maziwa yasiyoghoshiwa ni nini? Kwanini biblia inatumia mfano huo?

UFUNUO: Mlango wa 18

Kuota upo nchi nyingine.

ESTA: Mlango wa 4

Rudi nyumbani

Print this post

KUNA NGUVU YA ZIADA KATIKA KULING’ANG’ANIA KUSUDI LA MUNGU.

Daudi ni mfalme ambaye alikuwa amezungukwa na mashujaa hodari sana, na mashujaa hao aliowachagua walikuwa wamegawanyika katika makundi makuu matatu, Kundi la kwanza kabisa ambalo lilikuwa ndio la juu kabisa zaidi ya yote liliundwa na maaskari watatu, na lile pili yake liliunda na wawili, na lile la tatu liliundwa na mashujaa 37.

Sasa ukitaka kujua kwa urefu ushujaa wao, na mashujaa wenyewe walikuwa ni wakina nani fungua link hii usome zaidi…

Lakini leo tutaona kwa ufupi, ni nini kilimtokea  mmojawapo kati ya wale mashujaa watatu wa kwanza, Na ni ujumbe gani Kristo anataka tuupate kupitia ushujaa wake.

shujaa huyu aliitwa Eleazari, yeye kuna wakati walikutana na jeshi kubwa la wafilisti, wakati huo alikuwa peke yake tu, Israeli yote ilikuwa imeondoka, hata wale mashujaa wenzake hawakuwepo.. Lakini hakuogopa vita bali alinyanyuka na kuushikilia upanga wake mmoja.. akaanza kupigana na wafilisti yeye peke yake kama vile Samsoni, aliushikilia upanga wake kwa nguvu sana kiasi kwamba haikuwa rahisi kuuondoa mkononi mwake.

Lakini kwasababu maadui walikuwa wengi,kuna muda ulifika alilemewa sana, na ile nguvu ya kuendelea kuushikilia upanga ikamwishia, akataka kuuachilia ule upanga kwasababu alichoka sana, lakini biblia inatuambia upanga ule hakuwezi kutoka katika mkono wake, ikiwa na maana ulijiganda kama gundi katika mkono wake. Pale alipojaribu kurusha mkono, upanga haukuchomoka mkononi mwake, bali ulikwenda naye Hivyo akaendelea kupigana na wafilisti mpaka akawamaliza wote. Baadaye Israeli walipokuja kazi yao ikawa ni kuteka nyara tu huko nyuma, kwa kipigo cha jeshi la mtu mmoja.

2Samweli 23:9 “Na baada yake kulikuwa na Eleazari, mwana wa Dodai, Mwahohi, mmojawapo wa wale mashujaa watatu waliokuwa pamoja na Daudi; walipowatukana Wafilisti waliokuwa wamekusanyika huko ili kupigana, na watu wa Israeli walikuwa wamekwenda zao;

10 huyo aliinuka, akawapiga Wafilisti hata mkono wake ukachoka, na mkono wake ukaambatana na upanga; naye Bwana akafanya wokovu mkuu siku ile; nao watu wakarudi nyuma yake ili kuteka nyara tu”.

Hiyo ni kuonyesha jinsi gani, mtu anapotaka kung’ang’ana na kusudi la Mungu, kusudi nalo litang’ang’ana naye, ili kutimiza lile lengo.

Leo hii ukiling’ang’ania kusudi la Bwana kwa moyo wako wote na kwa bidii, lile kusudi nalo litang’ang’ana na wewe tu, hamna namna, kwasababu hiyo ni kanuni ya ki-Mungu, hata kama utafikia wakati umechoka, bado litaendelea kukung’ang’ania tu. Na ndio maana unaona ni kwanini watumishi wa Mungu wa kweli, hawachoki kumtumikia Mungu, japokuwa hawafanyi kazi ya mshahara, sio kwamba hawachoki, au hawapitii magumu, au hawapungukiwi nguvu..wanachoka, lakini wakati wanakaribia kuanguka, lile kusudi la Mungu linang’ang’ana nao, hivyo wanajikuta bado wanaendelea mbele na safari.

Isaya 40:29 “Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo.

30 Hata vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka;

31 bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia”.

Hata sisi sote, tunapodhamiria kweli kwa mioyo yetu yote, kutembea na Mungu, kamwe Mungu hawezi kutuachia katikati tuaibishwe na shetani, tunakuwa mfano wa Eleazari, nguvu za Mungu zitaambatana na sisi kuhakikisha kuwa lile kusudi la Mungu linatimia kwa gharama zozote zile.

Lakini tukiwa watu vuguvugu, leo tupo na Mungu kesho shetani, hatujajikana nafsi zetu na kusema kuanzia leo mambo ya ulimwengu basi, tunakwenda na Kristo. Kamwe nguvu ya Mungu haiwezi kushikamana na sisi kama alivyokusudia, pale tunapoishiwa nguvu au tunapokumbana na majaribu. Na ndio hapo utaona mkristo anakuwa moto na Mungu siku za mwanzoni mwanzoni, tu ikifika baadaye, anapoa, mpaka anauacha wokovu kabisa..ukimuuliza ni kwanini atasema, hali ya maisha ilikuwa ngumu, mwingine nilipitiwa na ujana, mwingine nilikuwa katika mazingira yasiyo rafiki,..Sasa tatizo halipo kwa Mungu bali kwa huyu mtu.

Kwasababu Mungu akishaianzisha safari ndani ya maisha ya mtu  huwa haikatishi katikati, Kwasababu Mungu huwa hashindwi , anaelewa kabisa kuwa yapo majira mbalimbali tutapitia hapa duniani kama wakristo, hivyo anatuhakikishia nguvu ya ziada kutoka kwake,  lakini hiyo inakuja  endapo tu tutakuwa na nia ile ile ya kutembea naye.

Paulo alisema

Wafilipi 1:6 “Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu;”

Hivyo ishi maisha ya kumaanisha mbele zake, ishi ndani ya kusudi la Mungu, ili Mungu awe nawe nyakati za taabu. Swali ni Je umemaanisha kweli kumfuata Kristo? Kama bado basi leo ndio wakati wako wa kudhamiria kutoka katika moyo wako kutubu na kuacha dhambi zako zote, Fanya hivyo kisha baada ya hapo nenda kabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO ikiwa hukubatizwa hapo kabla, Na Mungu mwenyewe atakupa Roho wake Mtakatifu, akutie nguvu hadi siku ukombozi wako.

Zingatia: Waliokombolewa na Mungu hawashindwi na ulimwengu.

Ikiwa utapenda upate huduma ya ubatizo sahihi, basi utawasiliana na sisi kwa namba hizi 0693036618, tukusaidie.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo .jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

LIPO LA KUJIFUNZA KWA WALE MASHUJAA 37 WA DAUDI.

NA VIUNGO VYETU VISIVYO NA UZURI VINA UZURI ZAIDI SANA.

Tofauti kati ya ufalme wa mbinguni na ufalme wa Mungu ni ipi?

LISHIKILIE SANA LILE AGIZO LA KWANZA.

WALA MSIUANGALIE MWILI, HATA KUWASHA TAMAA ZAKE.

Rudi nyumbani

Print this post

TUFANANE NA WATAKATIFU WA MAKEDONIA.

Nakusalimu katika jina kuu sana la Bwana wetu Yesu Kristo. Karibu tuyatafakari maandiko. Sisi kama wakristo, ili tuweze kukua kutoka utukufu hadi utukufu, na imani hadi imani, hatuna budi kuyatafakari maneno ya Mungu sana kwa kadiri tuwezavyo.

Leo tutajifunza tabia za kipekee walizokuwa nazo watu wa Makedonia nyakati zile za mitume.

Makedonia iliundwa na makanisa makuu matatu, (Kanisa la Wathesalonike, Wafilipi, na Waberoya). Hawa watu walikuwa ni wa kipekee sana, Kwamfano watu wa Beroya, tabia yao ya kupenda kuchunguza maandiko pengine iliwasaidia kutambua jukumu kubwa sana ambalo walipaswa walitimize katika utakatifu wao. Na jukumu lenyewe lilikuwa ni katika suala la UTOAJI.

Sasa kwa ufupi tutatazama waliwezaje kulitimiza hilo jukumu katika mazingira magumu waliyokuwa nayo. Naamini na sisi lipo la kujifunza kwa watu hawa, ili tusijikute tunakwamishwa na jambo lolote katika kuuelekea ukamilifu wetu. Embu tuzisome tabia zao ambao zinazungumziwa katika kitabu cha 2Wakorintho 8:1-15

  1. Tabia ya kwanza ni kuwa Wamakedonia ni watu waliokuwa katika dhiki nyingi na umaskini mkubwa.

Lakini hawakusahau kumtolea Mungu, katika umaskini wao, kiasi kwamba wao ndio wakaongoza katika kuitimiza huduma hiyo kuliko makanisa mengine yote .

2Wakorintho 8:1 “Tena ndugu zetu, twawaarifu habari ya neema ya Mungu, waliyopewa makanisa ya Makedonia;

2 maana walipokuwa wakijaribiwa kwa dhiki nyingi, wingi wa furaha yao na umaskini wao uliokuwa mwingi uliwaongezea utajiri wa ukarimu wao.

Mfano mzuri wa kuiga, kumbe umaskini wetu, hauwezi kuwa kikwazo katika  kumtolea Mungu.. Mtume Paulo anatuthibitishia kuwa maskini ndio walioongoza kumtolea Mungu miongoni mwa makanisa yote aliyoyahudumu mataifa mbalimbali.

       2) Licha ya kuwa katika umaskini mwingi, lakini bado walikuwa tayari kutoa hata zaidi ya uwezo wao.

2Wakor 8:3 “Maana nawashuhudia kwamba, kwa uwezo wao, na zaidi ya uwezo wao, kwa hiari yao wenyewe walitoa vitu vyao;”

Embu tutengeneze picha, maskini pengine anayo sh.100 tu lakini anaona hiyo bado haistahili kuipeleka kwa Mungu, anakwenda kuuza hata ile baiskeli yake, anayoitegemea kwenda nayo shambani kila siku, ili tu apate kiasi kingi kidogo  cha pesa akamtolee Mungu, awe radhi kutumia miguu yake kwenda shambani, kuliko kupeleka kiwango kidogo kwa Mungu wake. Unadhani huko tukuiteje, kama sio kutoa zaidi ya uwezo wako.

Sasa mambo kama haya, yalikuwa ni kawaida kwa watakatifu wa Makedonia.

Tujipime na sisi wakristo wa leo hii, pengine Mungu amekubariki gari, tuachilie mbali kwenda kuliuza na kumletea Mungu thamani yake je! Tunaweza kupanda daladala wiki 2 mfululizo, halafu hiyo pesa ambayo tungetumia katika kununua mafuta kila siku  tukaipeleka kanisani? Je hilo linawezakana? Au utampelekea Mungu elfu 1, na huku wiki nzima umetumia elfu 50 ya mafuta?. Je tunaweza kuwafikia watakatifu hawa, ambao walijitoa kwa Mungu zaidi ya uwezo wao?

      3) Walifurahia kumtolea Mungu, kwa moyo wa furaha, licha ya kuwa walikuwa ni maskini, na walitoa zaidi.. 2Wakor 8:3

Tabia nyingine ni hii, walifurahia kufanya hivyo. Hawakuwa wanung’unikaji, walipomtolea Mungu, ndivyo walivyopata amani mioyoni mwao, lakini ni rahisi sana kuona mtakatifu wa leo anatoa malalamiko kwa kila anachokitoa, utasikia, Yule mchungaji anakula sadaka zetu, mbona hatuoni matumizi ya pesa zetu kanisani. Na kwa kawaida ukiangalia hao wanaonung’unika hivyo, asilimia kubwa huwa si watoaji.

       4) Wao wenyewe waliomba na kusihi katika kutoa.

8:4 “Wakituomba sana pamoja na kutusihi kwa habari ya neema hii, na shirika hili la kuwahudumia watakatifu”.

Unaona? Waliwasihi mitume, waitimize huduma hiyo, kana kwamba wanachokifanya ni kwa faida yao,. Embu fikiria wewe leo, mtu anakuja kukuomba akupe pesa tena kwa kukusihi, Unaweza kudhani ni tajiri sana, au ana pesa za mchezo, lakini kumbe sio, hawa watu walikuwa maskini kama tunavyosoma, lakini walijua wajibu wao kwa Bwana.

Na sisi je! Tutamsubiri mpaka mchungaji wetu atukumbushe, kwa habari za zaka? Atukumbushe kuwa kuna kazi ya injili inahitaji fedha? Hapana, ni wajibu wetu kukumbuka, na kumtolea Bwana, pale anapotuamrisha.

       5) Pia Utoaji wao ulianza kwanza na kujitoa kwa Bwana.

2Wakor 8:5 “Tena walitenda hivi si kama tulivyotumaini tu, bali kwanza walijitoa nafsi zao kwa Bwana; na kwetu pia, kwa mapenzi ya Mungu”.

Kuonyesha kuwa, tabia ya utoaji, huwa chanzo chake ni kujitoa kwanza kwa Bwana.. Hawa watu walikubali kujibidiisha na mambo yote ya Mungu. Na ndio maana hawakuona ugumu wowote na kutoa hata zaidi ya uwezo wao kwa Mungu.

Hivyo mwisho kabisa mtume Paulo alipoona mwenendo wa watakatifu hawa wa Makedonia alitaka na makanisa mengine yote yaige mfano wao, hususani kanisa la Korintho, litimize karama hiyo pia, “ili auone unyofu wa upendo wao”.

2Wakor 8:8 “Sineni ili kuwaamuru, bali kwa bidii ya watu wengine nijaribu unyofu wa upendo wenu”.

Hata leo, wapo watakatifu ambao katika roho wapo Makedonia, watu kama hao utawaona tu, kazi ya Mungu, hawaichukulii kama kazi-baki, bali kama ni kazi ya kuthaminiwa sana, wanaelewa kuwa ina gharama zake na mahitaji yake, Hivyo hata kama wapo katika umaskini, hawana kazi, au wana kazi, wanakuwa na moyo kweli kwa kuijali kazi ya Mungu kwa vyovyote vile Mungu anavyowabariki, na wengine wanajitoa hata zaidi ya uwezo wao, ukidhania kuwa ni matajiri sana kumbe, hata kesho hawajui watakula nini, ni moyo wao tu wa upendo kwa Mungu.. Mungu azidi kuwabariki sana watu kama hawa.

Lakini wapo watakatifu wengine ambao kiroho wapo Korintho, ambao utoaji kwao ni jambo lisilo la umuhimu sana. Watakuwa tayari kusikiliza injili, na kulishwa vya rohoni kanisani, kufundishwa miaka nenda rudi, lakini wasijitoe hata kwa lolote kwa Mungu. Kisingizio chao kikubwa ni sina kazi, au ninapitia shida hii au ile, au nina madeni, nina mikopo nahitaji kurejesha..Ni kweli kama utakuwa unafikiria hilo, basi usiwasahau pia na watu wa Makedonia. Ambao walikuwa katika majaribu makubwa na umaskini wa kupindukia, pengine kuliko wewe, lakini hawakuzihusisha shida zao na kumtolea Mungu wao aliyewaumba.

Kumtolea Bwana, si kuchangia mabilioni, lakini kumtolea kinono kwa kile anachokujalia ndicho anachothamini, mfano wa Yule mwanamke mjane aliyemtolea Bwana senti mbili. Unaona> Kama Mungu anakujalia sh. 100 kwa siku, ukimtolea Mungu hata 50, Mungu anathamini sana. Kushinda Yule anayejaliwa bilioni 1 halafu anamtolea Mungu milioni 1 tu..

Hivyo tujitahidi sana, tufanane na watakatifu wa Makedonia.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Rudi nyumbani

Print this post

Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa watoto wake wote.

SWALI: Kwanini Bwana Yesu alisema watu wa kizazi kile wamefanana na watoto walioketi masokoni na kuitana,? Mfano huo unaelewekaje?

Na pia alikuwa na maana gani kusema maneno haya?

Luka 7:35 “Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa watoto wake wote”


JIBU: Habari hizo utazisoma katika sehemu kuu mbili, ya kwanza ni Mathayo 11:16-20 na ya pili ni  Luka 7:31-35

Sasa tuisome hiyo ya Luka ndio yenye vifungu vya moja kwa moja vya swali lenyewe;

Luka  7:31 “Bwana akasema, Niwafananishe na nini watu wa kizazi hiki? Nao wamefanana na nini?

32 Wamefanana na watoto walioketi sokoni na kuitana, wakisema, Tuliwapigia filimbi wala hamkucheza; tuliomboleza, wala hamkulia.

33 Kwa kuwa Yohana Mbatizaji alikuja, hali mkate wala hanywi divai, nanyi mwasema, Ana pepo.

34 Mwana wa Adamu amekuja, anakula na kunywa; nanyi mwasema, Tazama, mlafi huyu, na mnywaji wa divai, rafiki wao watoza ushuru na wenye dhambi.

35 Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa watoto wake wote”.

Shalom.

Bwana Yesu alitoa mfano ambao ulikuwa ni wa kawaida na uliojulikana kwa wagalilaya wakati ule. Kwani ilikuwa ni desturi watoto wa aina mbalimbali  kukutana masokoni kwa ajili ya michezo kulingana na desturi zao, na walipokutana walikuwa wanaunda makundi mawili makubwa, lengo lao likiwa ni kuigiza mambo ambayo waliona watu wazima wakiyafanya aidha katika misiba au sherehe.

Sasa kundi la kwanza lilikuwa linaanza kwa kupiga filimbi za kwenye masherehe walizowahi kuzisikia mahali fulani zikipigwa huko nyuma, na lile kundi lingine kazi yake ilikuwa ni kuitikia kwa kucheza, kama watu wazima walivyofanya. ( Soma Luka 15:25)

Baadaye tena vivyo hivyo, wanarudia  kuigiza  nyimbo za misibani, wale wengine wanajifanya kama wanalia kwa kupiga piga vifua vyao. (Soma Mathayo 9:23).  Hivyo hata watu wazima walipowaona hawakuwazuia bali waliwaacha, kwani walikuwa wanaamini vitendo vile vinawajengea uzalendo wa kutambua tamaduni zao za kiyahudi.

Sasa kulingana na maneno ya Bwana Yesu ni kuwa, watoto hawa walipokusanyika, kundi lile la kwanza lilipopiga filimbi za masherehe, wale wengine hawakuonyesha mwitikio wowote walizira, pengine wakadhani wanataka za msiba, na walipowapigia wenzao za msiba, bado pia hawakujifanya kama wanaomboleza. Kitendo ambacho  pengine kiliwakasirisha wale waliojitoa.

Akifunua kuwa, Yohana alikuja kwa njia ya kujitenga sana na ulimwengu, hivyo pengine wangemwamini kwa maisha yake ya majangwani, na kutokula kula au kunywa, kama vile mtoto aliyewapigia filimbi za maombolezo, lakini hawakulia..Yaani mafarisayo na waandishi hawakuonyesha mwitikio wowote. Kinyume chake wakasema watu wenye mapepo, ndio wanaishi maisha ya namna hiyo, hakuna mtumishi mwenye akili timamu, akawa mchafu na mtu asiyejijali namna ile.

Labda hiyo ikaonekana kama ni njia ngumu kwao kuamini manabii wa Mungu, Hivyo Mungu akawapelekea mkuu wa uzima mwenyewe, Yesu Kristo, Bwana wetu, ambaye yeye alikuja kwa njia ya kula na kunywa, mtu wa watu, aketiye katikati ya wenye dhambi, hivyo mbele yao akafanana na wale watoto waliopiga filimbi, ili wenzao wacheze.. Lakini bado hawakuonyesha mwitikio wowote kwa injili ya Bwana, kinyume chake, wakamwita mlevi na mlafu. Hakuna mtumishi wa Mungu kweli anaweza kushinda bar muda wote na walevu kuwahubiria.

Kuonyesha kuwa hata sasa, Bado Mungu anaweza kutuma watumishi wake, katika wito tofauti tofauti, lakini bado watu wasiompenda Mungu wakapinga tu, wakadhihaki, wakakejeli, wakadharau. Akitumwa nabii wa Mungu anayehubiri injili ya kweli, ambaye pengine ni tajiri, na ana mali, watasema, tapeli huyu, anakula sadaka za waumini, wakipelekewa nabii ambaye muda wake wote anashinda sehemu za ibada, au milimani, mwenye nguo moja, asiye smati, hafanyi kazi yoyote isipokuwa kushinda uweponi mwa Mungu, watasema huyu mlokole maskini hatumtaki, kama Mungu wake ameshindwa kumfanya hata asivae viatu vilivyotoboka, atawezaji kunisaidia mimi?

Unaona?

Lakini sasa ukiendelea mistari inayofuata, Bwana Yesu ndio anasema..

Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa watoto wake wote”.. Ukisoma kwenye Mathayo 11:19 inasema “Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa kazi zake”. Hii ikiwa na maana Hekima ya Mungu ya kuokoa watu, imejulikana kuwa ni ya kweli kwa watoto wake ambao ni (Yohana na Yesu Kristo mwenyewe).. Kwamba kwa vyovyote vile, iwe ni katika utajiri au katika umaskini, au katika kujichanganya au kutojichanganya..kama ni ya Mungu, basi itathibitika tu kwa kazi zake,(matunda yake).

Hata leo hii, usimuhukumu mtumishi wa Mungu kisa ni tajiri, au ni maskini, au anakula au hali, vilevile usihukumu huduma yoyote kisa ni kubwa, au ni ndogo, au inamfumo huu au ule.. kwasababu Hekima ya Mungu haichagui mfumo wa kutembelea. Bali ihukumu hiyo huduma kwa kazi zake baada ya hapo.

Ikiwa matunda yake, ni yale ya Kristo, basi muheshimu mtumishi huyo au huduma hiyo, ikiwa watu wake, wanauelekea wokovu wa kweli na wanaishi maisha ya kumpendeza Mungu basi heshimu hata kama ipo kinyume na matazamio yako.

Vilevile ukiona mtumishi ni tajiri, au ni Yule maskini anayeishi milimani, na anachokifanya hakina matunda Kristo anayoyataka sawasawa na Neno lake. Yaani watu wake ndio wanakwenda mbali na wokovu na utakatifu, maisha yako ni ya kidunia, wanafuata tu kuponywa, basi lakini upendo na Kristo hawana.. achana naye, hata kama atajiona ni wa rohoni kiasi gani..au ni mtu wa kijamii namna gani, au mwenye ushawishi namna gani, achana naye. Hekima ya Mungu haipo hapo.

Kwasababu hekima ya kweli ya Mungu inathibitika kwa kazi zake. Kama ilivyothibitika kwa Bwana Yesu na kwa Yohana, japokuwa mapito yao yalikuwa ni tofauti lakini matunda yao yalikuwa ni thabiti.

Hiyo ndio sababu Bwana Yesu aliwaambia wale mafarisayo maneno hayo..

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Au bofya chini kujiunga na group la whatsapp moja kwa moja;

https://chat.whatsapp.com/GBX2lWIcoCq8zmlnXJgaWQ

https://chat.whatsapp.com/GBX2lWIcoCq8zmlnXJgaWQ

Mada Nyinginezo:

Hamjui ya kuwa mtawahukumu malaika? Ina maana gani?

MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA WARAKA WA PILI WA YOHANA.

USIRUDI NYUMA KWA KUITUMAINIA HAKI YAKO.

MZAZI, JALI MAISHA YA KIROHO YA MTOTO WAKO.

SINA PESA SASA, YESU ATANISAIDIA NINI?

Rudi nyumbani

Print this post

Ni kweli Paulo alipuuzia maonyo aliyopewa ya kwenda Yerusalemu?

SWALI: Je Ni kweli Mtume Paulo alipuuzia, maonyo aliyoonyeshwa na Roho Mtakatifu kwa kinywa cha Agabo juu ya kwenda  Yerusalemu?


JIBU: Tusome habari yenyewe kwa faida ya watu wote;

Matendo 21:10 “Basi tulipokuwa tukikaa huko siku nyingi, nabii mmoja jina lake Agabo akashuka kutoka Uyahudi.

11 Alipotufikia akautwaa mshipi wa Paulo, akajifunga miguu na mikono, akasema, Roho Mtakatifu asema hivi, Hivyo ndivyo Wayahudi wa Yerusalemu watakavyomfunga mtu mwenye mshipi huu, nao watamtia katika mikono ya watu wa Mataifa.

12 Basi tuliposikia haya, sisi na watu wa mahali pale, tukamsihi asipande kwenda Yerusalemu.

13 Ndipo Paulo alipojibu, Mnafanya nini, kulia na kunivunja moyo? Kwa maana mimi, licha ya kufungwa, ni tayari hata kuuawa katika Yerusalemu kwa ajili ya jina lake Bwana Yesu.

14 Alipokataa shauri letu, tukanyamaza tukisema, Mapenzi ya Bwana na yatendeke.

15 Baada ya siku zile tukachukua vyombo vyetu tukapanda kwenda Yerusalemu.

Tofauti na wengi tunavyodhani kwamba mtume Paulo alipuuzia maono ya Mungu, na ndio maana akaenda kukumbana na matatizo makubwa kule Yerusalemu alipokwenda mambo ambayo hayakuwa na ulazima wa yeye kukutana nayo. Lakini si kweli, kama Paulo angekuwa ni mtu wa kupuuzia maono ya Mungu, asingeandika katika waraka wake mmoja “Msitweze unabii” (1Wathesalonike 5:20). Akimaanisha msipuuzie unabii.

Paulo alikuwa ni mtu aliyethamini sana maagizo ya Roho Mtakatifu, na kuyatekeleza wa wakati. Kuna wakati Mungu alimkataza asihubiri Neno Galatia na sehemu nyingine na akatii(mdo 16:6-9). Na wakati huo huo Mungu anamwonyesha maono avuke bahari aende Makedonia kuhubiri mahali ambapo hajawahi kufika hata siku moja. Na akatii

Hivyo kitendo cha kusema Paulo hakutii maagizo ya Roho Mtakatifu, ni kukosa shabaha.

Lakini swali linakuja kama sio kutii basi  ni kwanini aamue vile?

Jibu ni kuwa, ipo tofauti ya “mtu kupewa agizo” na “mtu kuelezwa uhalisia wa mambo / kupashwa habari”. Paulo hakupewa agizo na Roho Mtakatifu kuwa asipande Yerusalemu, kama alivyopewa maagizo sehemu nyingine. Hapana, bali alielezwa uhalisia wa mambo atakayokutana nayo huko mbeleni. Na ndio maana utaona kabla hata ya Agabo kumpa unabii ule, tayari Roho Mtakatifu alikuwa ameshamshuhudia mambo hayo kuwa atakutana nayo mbeleni. Soma.

Matendo 20:22 “Basi sasa, angalieni, nashika njia kwenda Yerusalemu hali nimefungwa rohoni, nisiyajue mambo yatakayonikuta huko;

23 isipokuwa Roho Mtakatifu mji kwa mji hunishuhudia akisema, ya kwamba vifungo na dhiki vyaningoja”.

Hivyo Paulo kwa kulitambua hilo, bado hakusita kukumbana na changamoto hizo, kwa ajili ya injili. Alifikiria sana akaona dhiki haziwezi kumfanya kondoo wa Mungu wasifikiwe na injili. Hivyo akajitia moyo na kwenda kama shujaa.

Jambo kama hilo utaona pia kwa mtume Petro, kipindi kile Bwana Yesu alimwambia wewe ni kijana, lakini ukiwa mzee watu watakuja kukufunga mikono yako na kukuchukua usipotaka, (Yohana 21:18). Kuonyesha kuwa vifungo na dhiki na vifo vinamsubiria mbeleni. Lakini lile halikuwa ni agizo kwamba Petro sasa akatafute namna ya kukwepa, dhiki hizo. Hapana.

Hata sasa ni kawaida ya Roho Mtakatifu kuzungumza nasi kwa namna zote mbili. Kuna wakati atatupa maagizo, na kuna wakati atatueleza uhalisia wa mambo. Sasa pale tunapopewa maagizo au tunapoonywa, ni sharti tutii, Mungu anapokuambia usihubiri mahali Fulani, ni kweli usiende kuhubiri, anapokuambia kahubiri mahali Fulani ni kweli nenda kahubiri.

Lakini kuna wakati utakuwa katika safari yako ya kumtumikia Mungu, na akakuonyesha, matunda, na changamoto zake, akakuonyesha hata, unapigwa mawe, au unafukuzwa, au unafungwa, au unazungumziwa vibaya. Moja kwa moja usikimbilie kusema Roho Mtakatifu ananionya nisiende kuhubiri, hapana, bali tazama pia upande wa pili wa matunda, Kwasababu dhiki kama hizo haziletwi na Mungu, bali ni shetani, ambaye anafanya hivyo ili akuzuie, usifanye kazi yake hilo tu. Lakini kumbe Mungu anatamani sana, ufike kule.

Kwahiyo usitafsiri kila ono, ni agizo ,  mengine Mungu anatuonyesha tu ili yatakapotokea tusifadhaike sana, kwasababu alishatutaarifu mapema.

Yohana 16:1 “Maneno hayo nimewaambia, msije mkachukizwa.

2 Watawatenga na masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada.

3 Na hayo watawatenda kwa sababu hawakumjua Baba wala mimi.

4 LAKINI NIMEWAAMBIA HAYO, ILI MAKUSUDI SAA ILE ITAKAPOKUJA MYAKUMBUKE YA KUWA MIMI NALIWAAMBIA. Sikuwaambia hayo tangu mwanzo, kwa sababu nalikuwapo pamoja nanyi”.

Hivyo Bwana atusaidie na sisi tujifunze kuyapambanua maono ya Mungu.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

VIFO VYA MITUME WA YESU/ JINSI MITUME WALIVYOKUFA.

Tofauti kati ya ufunuo, unabii na maono ni ipi?

PINDO LA VAZI LAKE SASA LIMEREFUSHWA.

BADO UPO YERUSALEMU TU..GALILAYA HUTAKI KWENDA?

LIPI TUNAJIFUNZA KWA WALIOMWONA YESU ALIYEFUFUKA?

Rudi nyumbani

Print this post