KUOTA UMECHELEWA MAHALI FULANI.

KUOTA UMECHELEWA MAHALI FULANI.

Ndoto kama hizi ambazo unajiona umechelewa mahali fulani, aidha  kuota umechelewa kufanya mtihani, au kuota umechelewa kusafiri, au kuota umechelewa kwenda kazini, au kuota umechelewa kwenye appointment fulani, au kuota umechelewa airport au kuota umechelewa interview, au umechelewa mahakamani n.k. huwa zinatoka kwa Mungu na Na kama zinajirudia mara kwa mara basi zidi kuzitilia maanani kwasababu bado hujavuka hapo.

Biblia inasema, Katika Ayubu 33:14-18

“Kwa kuwa Mungu hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali. 

15 Katika ndoto, katika maono ya usiku, Usingizi mzito uwajiliapo watu, Katika usingizi kitandani; 

16 Ndipo huyafunua masikio ya watu, Na kuyatia muhuri mafundisho yao, 

17 Ili amwondoe mtu katika makusudio yake, Na kumfichia mtu kiburi; 

18 Yeye huizuia nafsi yake isiende shimoni, Na uhai wake usiangamie kwa upanga.

Unaona Mungu huwa anasema na mtu hata Zaidi ya mara moja katika ndoto ile ile, na hiyo ni kumtilia msisitizo kuwa anapaswa aizingatie kugeuka.

Kuota umechelewa mahali fulani muhimu, ni ishara kuwa kuna mahali unalegalega kufanya uamuzi wa kuokoka, au kama umeokoka basi unazembea wokovu wako,  na hiyo itayagharimu Maisha yako ya milele kama usipokuwa makini, ukisoma katika kile kitabu cha Mathayo sura ya 25, utaona habari ya wale wanawali 10 ambao walikuwa wanamngojea Bwana wao aje kuwachukua  waingie karamuni, biblia inatuambia watano wao walikuwa ni werevu na watano wao walikuwa wapumbavu…Wale werevu walibeba taa zao pamoja na Mafuta ya ziada katika vyombo vyao, lakini wale wengine wapumbavu, waliliona hilo halina maana sana, wakapuuzia, wakaenda hivyo hivyo na taa zao, lakini Bwana wao alipokuwia kidogo na usiku wa manane, ulipofika wakasikia kelele kwa mbali za shangwe kwamba Bwana wao anakuja, sasa wale ambao walikuwa na Mafuta ya ziada wakazitengeneza taa zao, kwenda kumlaki Bwana, lakini wale wengine baada ya kujiona taa zao zinazima, ndio wakaanza kupata akili kumbe tulipaswa kuwa na Mafuta ya ziada kwenye chupa zetu, na walipowaomba wenzao wawagawie kidogo, wale wengine wakasema hayawezi kututosha sisi na nyinyi, ni heri mwende sokoni mkanunue haraka mrudi labda mtamuwahi…

Lakini biblia inatuambia walipokwenda na kurudi walikuwa tayari wameshachelewa, wakakuta mlango umeshafungwa..kilichoendelea huko nje ni kilio na kusaga meno.

Sasa ndoto yako inaendana kabisa na mfano huu Bwana Yesu alioutoa isipokuwa tu imekuja katika taswira nyingine..Na mara nyingi katika ndoto hiyo wakati umeshachelewa utajiona jinsi unavyopambana ili uwahi lakini inashindikana kama tu vile ilivyowatokea wale wanawali watano wapumbavu, walikuwa wanafanya harakaharaka mambo ambayo wangepaswa wawe wameshayafanya tangu zamani lakini ilishindikana.

Hivyo nawe pia kama upo nje ya Kristo, nakushauri, mgekie muumba wako leo, kabla hazijakaribia siku za hatari ambazo utatamani kweli umjue Mungu wako, lakini hutaweza tena, na siku hiyo ikifika wewe mwenyewe utajisikia  hali ya kujiona umepoteza jambo la msingi katika Maisha yako hapo ndipo majuto yatakapoanza…Je! Ni kitu gani kinachokuchelewesha sasa? Je ni utafutaji mali? Je Ni ndugu, Je, ni kazi yako?..Kama ndivyo basi biblia inasema ni heri kiungo chako kimoja kipotee kuliko mwili mzima ukatupwe katika Jehanamu ya moto, hivyo ni heri hiyo kazi ukaipoteza lakini umpate Yesu, Hizi ni nyakati za mwisho, Parapanda inakaribia kulia, watakatifu kwenda mbinguni usisibirie mpaka hayo yakukute, Tubu sasa mpe Kristo maisha yako ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO sawasawa na Matendo 2:38 upate ondoleo la Dhambi zako, ili Bwana akupe kipawa cha Roho wake Mtakatifu, kukusaidia kukulinda katika siku hizi mbaya.

Halikadhalika ikiwa wewe tayari upo katika wokovu, Jiangalie vizuri kwasababu kuna mahali unarudi nyuma, kuna vitu ambavyo unavifanya, au pengine unataka kwenda kuvifanya vinakucheleweshea taji lako, hivyo nawe pia, uimarishe wokovu wako, uisafishe njia yako, acha kuwa vuguvugu, Bwana anakuonya kwasababu hataki mwisho wa siku uangamie, kuota umechelewa kufanya mtihani au umechelewa kwenda kazini, au umechelewa kwenye interview, au umechelewa stendi ni dalili kuwa unachelewa katika safari yako ya mbinguni..Hivyo jirekebishe na Bwana atakusaidia.

Ubarikiwe sana.

Group la whatsappjiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

Tofauti kati ya ndoto na Maono ni ipi?

Nitajuaje kama ndoto ni ya Mungu au ya Shetani?

UNATAKA KUBARIKIWA? BASI USIKWEPE GHARAMA ZAKE.

JISHUSHE ILI MUNGU AKUHUDUMIE.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments