KUOTA UPO GEREZANI.

KUOTA UPO GEREZANI.

Kuota upo gerezani kunamaanisha nini?


Ndoto ya namna hii inaanguka katika makundi makuu matatu (3) ya watu.

  1. Mtu aliyeokoka
  2. Mtu aliye vuguvugu (Nusu kaokoka nusu dhambini)
  3. Mtu mwenye dhambi

Sasa ni vizuri ukajitathmini kwanza wewe mwenyewe na ukajijua upo katika kundi lipi kati ya hayo, ili upate tafsiri sahihi ya ndoto yako. Sasa tukianzana na kundi la kwanza.

1. Mtu aliyeokoka.(kuota upo gerezani)

Ikiwa wewe unajijua kabisa umeokoka, na umesimama katika Imani na hakuna chochote kinachokuyumbisha, Lakini cha kushangaza umejikuta katika ndoto upo gerezani, au kifungoni na hujui utatokaje. Nataka nikumbie hupaswi kuwa na hofu,.Shetani anaona Imani yako, na bidii yako kwa Mungu, na hivyo atafanya kila njia kukuzuia, au pengine ameshaanza kufanya hivyo katika Imani yako, wewe kusonga mbele, atajaribu kukusonga usifike mahali Fulani, lakini hawezi kufanikiwa.

Ipo mifano kadha wa kadha katika biblia, utaona magwiji wote wa Imani walipokuwa wanafanikiwa katika kumcha Mungu shetani hakutulia tu hivi hivi, badala yake alinyanyua vikwazo vya vifungo. Kwamfano utamwona Yusufu, wakati alipokataa kulala na mke wa Boss wake (Potifa), alisingiziwa na kutupwa gerezani na akakaa kule kwa muda wa karibu miaka 2..Lakini Yusufu hakuacha kumcha Mungu, kwasasababu, vifungo haviwezi kumshika mteule wa Mungu daima,  Na sote tunajua ni nini kilikuja kumpata Yusufu baada ya lile jaribu, ilikuwa ni kufanyika kuwa waziri mkuu wa Misri,

Vilevile utamwona Yeremia naye, alifungwa gerezani kwasababu alikuwa anawatabiria Israeli Habari za kweli za Mungu,(Soma vitabu vya Wafalme na Yeremia chote)

Utamwona tena Yohana Mbatizaji, yeye naye walimshika na kumtupa gerezani kisa tu, alimweleza mfalme Herode kosa lake la kuzini na mke wa ndugu yake, (Marko 6:17)

Halikadhalika utawaona mitume wa Kristo, akina Petro na Yohana vifungo viliwakuta, Paulo alipokuwa kuwa anasafiri katika ziara zake za kuhubiri injili Roho Mtakatifu alimshuhudia kabisa na kumwambia;

Matendo 20:23 “ isipokuwa Roho Mtakatifu mji kwa mji hunishuhudia akisema, ya kwamba vifungo na dhiki vyaningoja.24  Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa kitu cha thamani kwangu kama kuumaliza mwendo”.

Wakati mwingine alipokuwa na Sila, walimkamata na kumtupa gerezani, lakini wakiwa kule gerezani, hawakufadhaika, bali walimwimbia Mungu na kumsifu,

Matendo 16:25  “Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza”.

Vivyo hivyo na wewe, ikiwa ni mkristo ambaye unajijua umesimama kikamilifu katika Imani, unaweza ukawa unapitia sasahivi vipingamizi  vya kiimani, au vitakuja mbele yako kipindi sio kirefu, utakutana na shetani kutaka kukuzuia usisonge mbele na hicho unachomfanyia Mungu, basi usiogope, wewe fanya kama Paulo na Sila, zidi kumwimbia Mungu na kumsifu, na kuomba kwa bidii, kwasababu ipo hatua nzuri Zaidi Mungu anataka kukuvukisha.

Na ndio maana umeoteshwa ndoto kama hiyo upo gerezani, kifungoni. Usiogope, zidisha matendo yako kwa Mungu, wewe ni shujaa..

2. Mtu aliye vuguvugu.

Lakini kama wewe ni mkristo ambaye ni vuguvugu au ulishaanza kupoa, hapo mwanzo ulikuwa umesimama lakini sasahivi ni kama vile umerudi nyuma, na umeota ndoto kama hii upo gerezani, Hiyo ni tahadhari kubwa sana kwako.

Kumbuka shetani anakuwinda usiku na mchana,..Kwenye biblia alikuwepo mtu mmoja aliyeitwa Samsoni, yeye ni mfano wa wakristo vuguvugu wa leo, alilaghaiwa na uongo wa shetani mpaka akatoa siri ya nguvu zake. Na wote tunajua kilichomkuta baada ya pale ni nini?.

Alitobolewa macho, akatupwa gerezani na kufanyishwa kazi hata Zaidi ya punda..

Waamuzi 16:21 “Wafilisti wakamkamata, wakamng’oa macho; wakatelemka naye mpaka Gaza, wakamfunga kwa vifungo vya shaba; naye alikuwa akisaga ngano katika gereza”

Ndivyo ilivyo hata na wewe, Mungu amekuotesha upo gerezani, ni kwamba upo karibuni kutekwa na ibilisi au pengine tayari ameshakuteka kabisa..Biblia inasema kurudi kwake nyuma mpumbavu kutamwangamiza.

Hivyo unachopaswa kufanya ni kutubu na kumgeukia Mungu haraka sana, kama unafanya mambo ambayo hayampendezi heri uache mara moja, Kwasababu Mungu hataki uangamie. Na ndio maana kakupa tahadhari hiyo.

3. Mtu mwenye dhambi.(kuota upo gerezani)

Lakini sasa kama wewe, upo dhambini tangu zamani, hujawahi kuwa na Habari na Mungu, kisha  umeota upo gerezani,..Ni Mungu anazungumza na wewe, na kukuonyesha hali yako ilivyo rohoni. Kwamba upo vifungoni, shetani amekunasa, shetani anaitesa roho yako.

Lakini habari njema ni kuwa lengo kuu mojawapo la Yesu kutumwa duniani ilikuwa ni kuwafungua na kuwaacha huru waliofungwa na ibilisi..

Hivyo ikiwa wewe ni mkristo jina tu, au mwislamu, au muhindu, au mpagani,.. Sikiliza unabii Mungu aliompa Yesu zamani..alisema.

Isaya 42:6 “Mimi, Bwana, nimekuita katika haki, nami nitakushika mkono, na kukulinda, na kukutoa uwe agano la watu, na nuru ya mataifa; 

7 kuyafunua macho ya vipofu, KUWATOA GEREZANI WALIOFUNGWA, kuwatoa wale walioketi gizani katika nyumba ya kufungwa. 

8 Mimi ni Bwana; ndilo jina langu; na utukufu wangu sitampa mwingine, wala sitawapa sanamu sifa zangu”

Na ndio maana Yesu alisema..

Zaburi 61:1 “Roho ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu Bwana amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, KUWATANGAZIA MATEKA UHURU WAO, NA HAO WALIOFUNGWA HABARI ZA KUFUNGULIWA KWAO”.

Hivyo leo umejiona upo vifungoni, pengine unateseka kutafuta njia ya kutoka huwezi, Yesu anakuita leo akuokoe,.

Zaburi 69:33 “Kwa kuwa Bwana huwasikia wahitaji, Wala hawadharau wafungwa wake”.

Ukimpokea Yesu, atafanya mabadiliko makubwa katika Maisha yako, atakufungua katika laana nyingi ambazo hata wewe mwenyewe hukuwahi kuzijua, laana za ukoo, na laana za mapepo na majini, ikiwa utakuwa tu tayari leo kusema Bwana Yesu njoo niokoe yote hayo yatafanyika kwako.

Kwahiyo Ikiwa upo tayari kufanya hivyo leo, basi fungua hapa  kwa ajili ya kuongozwa sala ya toba >>> KUONGOZWA SALA YA TOBA

Na ukimaliza kufanya hivyo basi Kristo anaanza sasa kuyafanya mabadiliko hayo moyoni mwako, na utaona jinsi anavyokufungua kifungo kimoja mpaka kingine. Kama alitufanyia sisi hivyo, atakufanyia na wewe, Hivyo amini tu na fungua moyo wako!

Bwana akubariki.

Pia tazama mafundisho mengine chini tayakusaidia kiroho sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au kwa namba hii +255 789001312

Group la whatsapp  Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

Mada Nyinginezo:

RABI, UNAKAA WAPI?

TAZAMA, MWISRAELI KWELI KWELI, HAMNA HILA NDANI YAKE!

TOBA IGUSAYO MOYO WA BWANA.

MTETEZI WAKO NI NANI?

KIFO CHA REINHARD BONKEY KINAACHA UJUMBE GANI KWETU?

KIAMA KINATISHA.

CHUKIZO LA UHARIBIFU

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments