Title July 2021

Kwanini iwe ni nchi ibubujikayo maziwa na asali?

SWALI: Kwanini Mungu aliufananisha uzuri wa Kaanani na kama nchi ibubujikayo maziwa na asali? Kwanini isiwe kitu kingine chochote, labda dhahabu na nafaka?

Kutoka 3:8 “nami nimeshuka ili niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hata nchi njema, kisha pana; nchi ijaayo maziwa na asali; hata mahali pa Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi”.


JIBU: Mungu aliposema Kaanani ni nchi ibubujikayo maziwa na asali, hakumaanisha kuwa kuna mito ya maziwa, au mabomba ya asali, kila mahali hapana. Bali alitumia lugha hiyo ya picha kuonyesha uzuri wa nchi ile jinsi ulivyo.

Kama tunavyojua maziwa yanatolewa na mifugo, kama ng’ombe,. Na ng’ombe ili atoe maziwa mengi na ya kutosha, anategemea sana mazingira yenye malisho mazuri ya kijani na chemchemi nzuri za  maji. Hivyo Hapo ni Mungu alikuwa anawaonyesha wana wa Israeli kuwa nchi waiendeayo si nchi kame, bali ni nchi yenye rutuba nyingi sana, ambayo mboga mboga na malisho mazuri vinastawi, kiasi kwamba tukisema  ni maziwa basi mifugo yao itamwaga maziwa mengi sana, hadi yasiwatoshe kwa wingi wa malisho yaliyopo huko.

Vilevile aliposema asali, aliwalenga nyuki. Na nyuki ni wadudu wanaotegemea sana, aina mbalimbali za mimea na maua ili kutengeneza asali yao, Kama tunavyojua mahali ambapo pana jamii chache za miti na mimea, inawachukua muda mrefu sana kuunda asali kidogo, kwani inawagharimu kutembea umbali mrefu sana, kutafuta virutubisho hivyo.

Lakini kama wapo eneo lenye misitu, na jamii tofauti tofauti za miti na mimea, huwa inawachukua muda mfupi sana. Hivyo Mungu aliposema hiyo nchi ibubujikayo asali, alimaanisha kuwa ni nchi yenye aina mbalimbali ya miti ya vyakula na matunda, Kama tukisema ni nyuki watengeneze asali, basi asali itakuwa ni ya kumwagika sana.tofauti na hiyo nchi ya ukame waliyotoka.

Na ndio maana wale wapepelezi waliotumwa na Musa kwenda kuipeleleza Kaanani, aliporudi na  kichala kikubwa cha mzabibu na tini na mkomamanga,  waliwaambia wana wa Israeli maneno haya;

Hesabu 13:27 “Wakamwambia wakasema, Tulifika nchi ile uliyotutuma, na hakika yake, ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali, na haya ndiyo matunda yake”

Unaona, kwa yale waliyoyakutana nayo huko walithibitisha maneno ya Mungu kuwa ni kweli, kuwa nchi hiyo ni ya maziwa na asali.

Hata sasa, Mungu ana mpango huo kwa watoto wake , kuwafikisha katika nchi hii, lakini ni lazima kwanza, awafundishe kanuni zake, na jinsi ya kuishi ndani yake. Vinginevyo wakiifikia na huku maisha yao bado hajabadilishwa, nchi hiyo itawatapika kama ilivyowatapika wenyeji wa Kaanani. Na kanuni zenyewe ni kuishi sawasawa na amri za Mungu (Neno lake).

Walawi 18:26 “Kwa hiyo mtazishika amri zangu na hukumu zangu, wala msifanye machukizo hayo mojawapo; yeye aliye mzalia, wala mgeni aketiye kati yenu;

27 (kwa kuwa hao watu wa nchi wameyafanya machukizo haya yote, hao waliotangulia mbele zenu, na hiyo nchi imekuwa najisi;)

28 ILI KWAMBA HIYO NCHI ISIWATAPIKE NA NINYI PIA, hapo mtakapoitia unajisi, kama ilivyoitapika hiyo taifa iliyotangulia mbele yenu”.

Lakini tukiishi sawasawa na Neno lake, wakati huo utafika na Bwana atatuingiza katika nchi hiyo kama alivyofanya kwa wana wa Israeli walipozitii amri zake.

Hesabu 14:8 “Ikiwa Bwana anatufurahia, atatuingiza katika nchi hii atupe iwe yetu, nayo ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali”.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

UNYAKUO.

Maziwa yasiyoghoshiwa ni nini? Kwanini biblia inatumia mfano huo?

UFUNUO: Mlango wa 18

Kuota upo nchi nyingine.

ESTA: Mlango wa 4

Rudi nyumbani

Print this post

KUNA NGUVU YA ZIADA KATIKA KULING’ANG’ANIA KUSUDI LA MUNGU.

Daudi ni mfalme ambaye alikuwa amezungukwa na mashujaa hodari sana, na mashujaa hao aliowachagua walikuwa wamegawanyika katika makundi makuu matatu, Kundi la kwanza kabisa ambalo lilikuwa ndio la juu kabisa zaidi ya yote liliundwa na maaskari watatu, na lile pili yake liliunda na wawili, na lile la tatu liliundwa na mashujaa 37.

Sasa ukitaka kujua kwa urefu ushujaa wao, na mashujaa wenyewe walikuwa ni wakina nani fungua link hii usome zaidi…

Lakini leo tutaona kwa ufupi, ni nini kilimtokea  mmojawapo kati ya wale mashujaa watatu wa kwanza, Na ni ujumbe gani Kristo anataka tuupate kupitia ushujaa wake.

shujaa huyu aliitwa Eleazari, yeye kuna wakati walikutana na jeshi kubwa la wafilisti, wakati huo alikuwa peke yake tu, Israeli yote ilikuwa imeondoka, hata wale mashujaa wenzake hawakuwepo.. Lakini hakuogopa vita bali alinyanyuka na kuushikilia upanga wake mmoja.. akaanza kupigana na wafilisti yeye peke yake kama vile Samsoni, aliushikilia upanga wake kwa nguvu sana kiasi kwamba haikuwa rahisi kuuondoa mkononi mwake.

Lakini kwasababu maadui walikuwa wengi,kuna muda ulifika alilemewa sana, na ile nguvu ya kuendelea kuushikilia upanga ikamwishia, akataka kuuachilia ule upanga kwasababu alichoka sana, lakini biblia inatuambia upanga ule hakuwezi kutoka katika mkono wake, ikiwa na maana ulijiganda kama gundi katika mkono wake. Pale alipojaribu kurusha mkono, upanga haukuchomoka mkononi mwake, bali ulikwenda naye Hivyo akaendelea kupigana na wafilisti mpaka akawamaliza wote. Baadaye Israeli walipokuja kazi yao ikawa ni kuteka nyara tu huko nyuma, kwa kipigo cha jeshi la mtu mmoja.

2Samweli 23:9 “Na baada yake kulikuwa na Eleazari, mwana wa Dodai, Mwahohi, mmojawapo wa wale mashujaa watatu waliokuwa pamoja na Daudi; walipowatukana Wafilisti waliokuwa wamekusanyika huko ili kupigana, na watu wa Israeli walikuwa wamekwenda zao;

10 huyo aliinuka, akawapiga Wafilisti hata mkono wake ukachoka, na mkono wake ukaambatana na upanga; naye Bwana akafanya wokovu mkuu siku ile; nao watu wakarudi nyuma yake ili kuteka nyara tu”.

Hiyo ni kuonyesha jinsi gani, mtu anapotaka kung’ang’ana na kusudi la Mungu, kusudi nalo litang’ang’ana naye, ili kutimiza lile lengo.

Leo hii ukiling’ang’ania kusudi la Bwana kwa moyo wako wote na kwa bidii, lile kusudi nalo litang’ang’ana na wewe tu, hamna namna, kwasababu hiyo ni kanuni ya ki-Mungu, hata kama utafikia wakati umechoka, bado litaendelea kukung’ang’ania tu. Na ndio maana unaona ni kwanini watumishi wa Mungu wa kweli, hawachoki kumtumikia Mungu, japokuwa hawafanyi kazi ya mshahara, sio kwamba hawachoki, au hawapitii magumu, au hawapungukiwi nguvu..wanachoka, lakini wakati wanakaribia kuanguka, lile kusudi la Mungu linang’ang’ana nao, hivyo wanajikuta bado wanaendelea mbele na safari.

Isaya 40:29 “Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo.

30 Hata vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka;

31 bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia”.

Hata sisi sote, tunapodhamiria kweli kwa mioyo yetu yote, kutembea na Mungu, kamwe Mungu hawezi kutuachia katikati tuaibishwe na shetani, tunakuwa mfano wa Eleazari, nguvu za Mungu zitaambatana na sisi kuhakikisha kuwa lile kusudi la Mungu linatimia kwa gharama zozote zile.

Lakini tukiwa watu vuguvugu, leo tupo na Mungu kesho shetani, hatujajikana nafsi zetu na kusema kuanzia leo mambo ya ulimwengu basi, tunakwenda na Kristo. Kamwe nguvu ya Mungu haiwezi kushikamana na sisi kama alivyokusudia, pale tunapoishiwa nguvu au tunapokumbana na majaribu. Na ndio hapo utaona mkristo anakuwa moto na Mungu siku za mwanzoni mwanzoni, tu ikifika baadaye, anapoa, mpaka anauacha wokovu kabisa..ukimuuliza ni kwanini atasema, hali ya maisha ilikuwa ngumu, mwingine nilipitiwa na ujana, mwingine nilikuwa katika mazingira yasiyo rafiki,..Sasa tatizo halipo kwa Mungu bali kwa huyu mtu.

Kwasababu Mungu akishaianzisha safari ndani ya maisha ya mtu  huwa haikatishi katikati, Kwasababu Mungu huwa hashindwi , anaelewa kabisa kuwa yapo majira mbalimbali tutapitia hapa duniani kama wakristo, hivyo anatuhakikishia nguvu ya ziada kutoka kwake,  lakini hiyo inakuja  endapo tu tutakuwa na nia ile ile ya kutembea naye.

Paulo alisema

Wafilipi 1:6 “Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu;”

Hivyo ishi maisha ya kumaanisha mbele zake, ishi ndani ya kusudi la Mungu, ili Mungu awe nawe nyakati za taabu. Swali ni Je umemaanisha kweli kumfuata Kristo? Kama bado basi leo ndio wakati wako wa kudhamiria kutoka katika moyo wako kutubu na kuacha dhambi zako zote, Fanya hivyo kisha baada ya hapo nenda kabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO ikiwa hukubatizwa hapo kabla, Na Mungu mwenyewe atakupa Roho wake Mtakatifu, akutie nguvu hadi siku ukombozi wako.

Zingatia: Waliokombolewa na Mungu hawashindwi na ulimwengu.

Ikiwa utapenda upate huduma ya ubatizo sahihi, basi utawasiliana na sisi kwa namba hizi 0693036618, tukusaidie.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo .jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

LIPO LA KUJIFUNZA KWA WALE MASHUJAA 37 WA DAUDI.

NA VIUNGO VYETU VISIVYO NA UZURI VINA UZURI ZAIDI SANA.

Tofauti kati ya ufalme wa mbinguni na ufalme wa Mungu ni ipi?

LISHIKILIE SANA LILE AGIZO LA KWANZA.

WALA MSIUANGALIE MWILI, HATA KUWASHA TAMAA ZAKE.

Rudi nyumbani

Print this post

TUFANANE NA WATAKATIFU WA MAKEDONIA.

Nakusalimu katika jina kuu sana la Bwana wetu Yesu Kristo. Karibu tuyatafakari maandiko. Sisi kama wakristo, ili tuweze kukua kutoka utukufu hadi utukufu, na imani hadi imani, hatuna budi kuyatafakari maneno ya Mungu sana kwa kadiri tuwezavyo.

Leo tutajifunza tabia za kipekee walizokuwa nazo watu wa Makedonia nyakati zile za mitume.

Makedonia iliundwa na makanisa makuu matatu, (Kanisa la Wathesalonike, Wafilipi, na Waberoya). Hawa watu walikuwa ni wa kipekee sana, Kwamfano watu wa Beroya, tabia yao ya kupenda kuchunguza maandiko pengine iliwasaidia kutambua jukumu kubwa sana ambalo walipaswa walitimize katika utakatifu wao. Na jukumu lenyewe lilikuwa ni katika suala la UTOAJI.

Sasa kwa ufupi tutatazama waliwezaje kulitimiza hilo jukumu katika mazingira magumu waliyokuwa nayo. Naamini na sisi lipo la kujifunza kwa watu hawa, ili tusijikute tunakwamishwa na jambo lolote katika kuuelekea ukamilifu wetu. Embu tuzisome tabia zao ambao zinazungumziwa katika kitabu cha 2Wakorintho 8:1-15

  1. Tabia ya kwanza ni kuwa Wamakedonia ni watu waliokuwa katika dhiki nyingi na umaskini mkubwa.

Lakini hawakusahau kumtolea Mungu, katika umaskini wao, kiasi kwamba wao ndio wakaongoza katika kuitimiza huduma hiyo kuliko makanisa mengine yote .

2Wakorintho 8:1 “Tena ndugu zetu, twawaarifu habari ya neema ya Mungu, waliyopewa makanisa ya Makedonia;

2 maana walipokuwa wakijaribiwa kwa dhiki nyingi, wingi wa furaha yao na umaskini wao uliokuwa mwingi uliwaongezea utajiri wa ukarimu wao.

Mfano mzuri wa kuiga, kumbe umaskini wetu, hauwezi kuwa kikwazo katika  kumtolea Mungu.. Mtume Paulo anatuthibitishia kuwa maskini ndio walioongoza kumtolea Mungu miongoni mwa makanisa yote aliyoyahudumu mataifa mbalimbali.

       2) Licha ya kuwa katika umaskini mwingi, lakini bado walikuwa tayari kutoa hata zaidi ya uwezo wao.

2Wakor 8:3 “Maana nawashuhudia kwamba, kwa uwezo wao, na zaidi ya uwezo wao, kwa hiari yao wenyewe walitoa vitu vyao;”

Embu tutengeneze picha, maskini pengine anayo sh.100 tu lakini anaona hiyo bado haistahili kuipeleka kwa Mungu, anakwenda kuuza hata ile baiskeli yake, anayoitegemea kwenda nayo shambani kila siku, ili tu apate kiasi kingi kidogo  cha pesa akamtolee Mungu, awe radhi kutumia miguu yake kwenda shambani, kuliko kupeleka kiwango kidogo kwa Mungu wake. Unadhani huko tukuiteje, kama sio kutoa zaidi ya uwezo wako.

Sasa mambo kama haya, yalikuwa ni kawaida kwa watakatifu wa Makedonia.

Tujipime na sisi wakristo wa leo hii, pengine Mungu amekubariki gari, tuachilie mbali kwenda kuliuza na kumletea Mungu thamani yake je! Tunaweza kupanda daladala wiki 2 mfululizo, halafu hiyo pesa ambayo tungetumia katika kununua mafuta kila siku  tukaipeleka kanisani? Je hilo linawezakana? Au utampelekea Mungu elfu 1, na huku wiki nzima umetumia elfu 50 ya mafuta?. Je tunaweza kuwafikia watakatifu hawa, ambao walijitoa kwa Mungu zaidi ya uwezo wao?

      3) Walifurahia kumtolea Mungu, kwa moyo wa furaha, licha ya kuwa walikuwa ni maskini, na walitoa zaidi.. 2Wakor 8:3

Tabia nyingine ni hii, walifurahia kufanya hivyo. Hawakuwa wanung’unikaji, walipomtolea Mungu, ndivyo walivyopata amani mioyoni mwao, lakini ni rahisi sana kuona mtakatifu wa leo anatoa malalamiko kwa kila anachokitoa, utasikia, Yule mchungaji anakula sadaka zetu, mbona hatuoni matumizi ya pesa zetu kanisani. Na kwa kawaida ukiangalia hao wanaonung’unika hivyo, asilimia kubwa huwa si watoaji.

       4) Wao wenyewe waliomba na kusihi katika kutoa.

8:4 “Wakituomba sana pamoja na kutusihi kwa habari ya neema hii, na shirika hili la kuwahudumia watakatifu”.

Unaona? Waliwasihi mitume, waitimize huduma hiyo, kana kwamba wanachokifanya ni kwa faida yao,. Embu fikiria wewe leo, mtu anakuja kukuomba akupe pesa tena kwa kukusihi, Unaweza kudhani ni tajiri sana, au ana pesa za mchezo, lakini kumbe sio, hawa watu walikuwa maskini kama tunavyosoma, lakini walijua wajibu wao kwa Bwana.

Na sisi je! Tutamsubiri mpaka mchungaji wetu atukumbushe, kwa habari za zaka? Atukumbushe kuwa kuna kazi ya injili inahitaji fedha? Hapana, ni wajibu wetu kukumbuka, na kumtolea Bwana, pale anapotuamrisha.

       5) Pia Utoaji wao ulianza kwanza na kujitoa kwa Bwana.

2Wakor 8:5 “Tena walitenda hivi si kama tulivyotumaini tu, bali kwanza walijitoa nafsi zao kwa Bwana; na kwetu pia, kwa mapenzi ya Mungu”.

Kuonyesha kuwa, tabia ya utoaji, huwa chanzo chake ni kujitoa kwanza kwa Bwana.. Hawa watu walikubali kujibidiisha na mambo yote ya Mungu. Na ndio maana hawakuona ugumu wowote na kutoa hata zaidi ya uwezo wao kwa Mungu.

Hivyo mwisho kabisa mtume Paulo alipoona mwenendo wa watakatifu hawa wa Makedonia alitaka na makanisa mengine yote yaige mfano wao, hususani kanisa la Korintho, litimize karama hiyo pia, “ili auone unyofu wa upendo wao”.

2Wakor 8:8 “Sineni ili kuwaamuru, bali kwa bidii ya watu wengine nijaribu unyofu wa upendo wenu”.

Hata leo, wapo watakatifu ambao katika roho wapo Makedonia, watu kama hao utawaona tu, kazi ya Mungu, hawaichukulii kama kazi-baki, bali kama ni kazi ya kuthaminiwa sana, wanaelewa kuwa ina gharama zake na mahitaji yake, Hivyo hata kama wapo katika umaskini, hawana kazi, au wana kazi, wanakuwa na moyo kweli kwa kuijali kazi ya Mungu kwa vyovyote vile Mungu anavyowabariki, na wengine wanajitoa hata zaidi ya uwezo wao, ukidhania kuwa ni matajiri sana kumbe, hata kesho hawajui watakula nini, ni moyo wao tu wa upendo kwa Mungu.. Mungu azidi kuwabariki sana watu kama hawa.

Lakini wapo watakatifu wengine ambao kiroho wapo Korintho, ambao utoaji kwao ni jambo lisilo la umuhimu sana. Watakuwa tayari kusikiliza injili, na kulishwa vya rohoni kanisani, kufundishwa miaka nenda rudi, lakini wasijitoe hata kwa lolote kwa Mungu. Kisingizio chao kikubwa ni sina kazi, au ninapitia shida hii au ile, au nina madeni, nina mikopo nahitaji kurejesha..Ni kweli kama utakuwa unafikiria hilo, basi usiwasahau pia na watu wa Makedonia. Ambao walikuwa katika majaribu makubwa na umaskini wa kupindukia, pengine kuliko wewe, lakini hawakuzihusisha shida zao na kumtolea Mungu wao aliyewaumba.

Kumtolea Bwana, si kuchangia mabilioni, lakini kumtolea kinono kwa kile anachokujalia ndicho anachothamini, mfano wa Yule mwanamke mjane aliyemtolea Bwana senti mbili. Unaona> Kama Mungu anakujalia sh. 100 kwa siku, ukimtolea Mungu hata 50, Mungu anathamini sana. Kushinda Yule anayejaliwa bilioni 1 halafu anamtolea Mungu milioni 1 tu..

Hivyo tujitahidi sana, tufanane na watakatifu wa Makedonia.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Rudi nyumbani

Print this post

Naomba kujua maana ya haya maneno katika biblia..“Siti Msharifu”, “Mitalawanda” na “kulalama”

Jibu: Tukianza na Neno “Siti Msharifu”. Neno hili tunalipata mara moja tu! Katika biblia nzima katika kitabu cha Wimbo ulio bora 7:1.

Wimbo ulio bora 7:1 “SITI MSHARIFU, jinsi zilivyo nzuri Hatua zako katika MITALAWANDA. Mapaja yako ya mviringo ni kama johari, Kazi ya mikono ya fundi mstadi”

Maana ya neno hilo ni “binti wa Mfalme”.. Kiswahili cha zamani cha binti wa Mfalme ni “siti-msharifu”.. Kwahiyo katika mstari huo unaweza kusomeka kama “Binti wa mfalme, jinsi zilivyo nzuri hatua zako katika Mitalawanda”.

Na neno “Mitalawanda” linapatikana mara moja tu katika biblia yote, na tunalisoma katika kitabu hicho hicho cha Wimbo ulio bora 7:1.. Na maana ya neno hilo ni “Viatu vilivyotengenezwa kwa kamba”…kwa kiingereza sandals au sendoz.

Maeneo ya mashariki ya kati, watu hawakuwa wanavaa viatu kama hivi vyetu, bali vile vilivyotengenezwa kwa kamba, Kwahiyo Kiswahili cha zamani cha sendoz, ndio hiyo Mitalawanda.

Hivyo Mstari huo wa wimbo uliobora 7:1, unaweza kusomeka hivi.. “Binti wa mfalme, jinsi zilivyo nzuri hatua zako katika sendozi”.

Kwaujumla kitabu cha Wimbo ulio bora, kinahusu mazungumzo ya kimahusiano kati ya  mtu na mke wake katika hatua tofauti tofauti, kikifunua uhusiano wetu sisi na Kristo katika hatua tofauti tofauti (yaani wakati tunampokea Yesu na baada ya kumpokea Yesu), kwasababu kimaandiko, Kristo ndiye Bwana na sisi ni bibi-arusi wake.

Na neno la mwisho ni “Kulalama”. Neno hili limeonekana sehemu kadhaa katika biblia, na maana ya Neno hili ni “kuugua rohoni au moyoni, hususani kwa kuomba”.. Mtu anayeomba kwa kuugua sana, mtu huyo ni ANALALAMA!

Na ni wajibu wa kila Mkristo kuomba kwa kulalama kila wakati, kwasababu kama jambo una mzigo nalo huwezi kuliombea juu juu tu!, bali utaomba kwa kuugua sana. Na jambo linaloombewa kwa mzigo mzito ni rahisi kuleta matokeo haraka sana zaidi ya lile linaloombewa juu juu tu!

Baadhi ya mistari inayolitaja neno ni pamoja na.

Zaburi 55: 1 “Ee Mungu, uisikilize sala yangu, Wala usijifiche nikuombapo rehema.

2 Unisikilize na kunijibu, Nimetanga-tanga NIKILALAMA na kuugua”.

Na mingine ni Zaburi 55:17 na Yeremia 9:10.

Je umempokea Yesu??…Kumbuka Bwana yu karibu na siku zote yakumbuke maneno yake haya..

Marko 8:36  “Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake? 37 Ama mtu atoe nini badala ya nafsi yake?”

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

SOMO no.02 (BINTI WA YEFTHA).

KAMA MKRISTO FAHAMU ZIPO HATUA UTAPIGISHWA NA MUNGU.

Pambaja ni nini katika Biblia kama tunavyosoma katika kitabu cha Wimbo ulio bora 1:2?

FUNGUO WALIZOKUWA NAZO MABINTI WATANO WA SELOFEHADI!

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 11 (Mithali, Wimbo ulio bora, Mhubiri)

Rudi nyumbani

Print this post

Kwa maana kahaba ni shimo refu; Na malaya ni rima jembamba.

SWALI: Nini maana ya huu mstari?

Mithali 23:27 “Kwa maana kahaba ni shimo refu; Na malaya ni rima jembamba.

28 Naam, huotea kama mnyang’anyi; Huwaongeza wenye hila katika wanadamu”.

JIBU: Kahaba ni mwanamke anayezini na mtu ambaye si mume wake, ni mwanamke mwenye mahusiano na wanaume wengi, akiwa na lengo la aidha kujiburudisha au kuharibu maisha ya wengine, huyu huwa hatafutwi bali yeye ndio anatafuta, kutimiza makusudi yake maalumu.

Lakini Malaya kibiblia ni mwanamke anayefanya uasherati kwa lengo la kujipatia fedha , au kupata upendeleo fulani, au kukubaliwa, mara nyingi huwa hajaolewa. Vilevile mwanamke yeyote anayejiamulia tu kufanya uasherati na mtu yeyote pale anapofuatwa, bila kujali chochote huyo pia ni Malaya.

Sasa Biblia inatuambia wote, ni hatari hakuna hata mmoja mwenye afadhali, ikiwa umenaswa nao.  Kwamfano ukizini na kahaba, rohoni ni kama unazama kwenye shimo. Na heri lingekuwa ni shimo tu, bali biblia inasema ni shimo refu, ikiwa na maana mtu akizama, hana matumaini tena ya kutoka huko. Ndio milele anapotea.

Vilevile anasema Malaya ni Rima jembamba. Rima ni shimo maalumu ambalo linachimbwa kwa ajili ya kunasa kitu, hususani wanyama. Zamani watu walipotaka kuwakamata wanyama wakali kama vile simba au dumu, walikuwa hawawapigi sindano za usingizi kama wanavyofanya sasa hivi,hapana, bali walikuwa wanachimba mashimo marefu sana, na membamba kisha, kwa juu wanayafunika na majani, kiasi kwamba mnyama akipita pale hawezi jua kama chini kuna shimo. Na akishasogea tu pale anatumbukia na kwenda chini sana, baadaye wanakuja kumkamata na kumtoa kirahisi.

Hivyo Malaya naye ndio vivyo hivyo, ukijiingiza kwenye mitego yao, unanasika na kutoka kamwe hutaweza. Soma.

Mithali 22: 14 “Kinywa cha malaya ni shimo refu; Anayechukiwa na Bwana atatumbukia ndani yake”.

Sasa tahadhari hii hawapewi wanaume tu, bali pia na wanawake..Kibiblia, kahaba na Malaya inamaanisha jinsia zote. Wewe ni kijana au binti, ikimbie zinaa kama vile biblia inavyosema katika 1Wakorintho 6:18… Kwasababu dhambi nyingine zote mtu unatenda nje ya mwili wako, lakini zinaa ni juu ya mwili wako mwenyewe.

Na ni dhambi inayowaangusha wengi sana, na inayoshusha viwango vya kiroho kwa kasi sana. Kiasi kwamba kitendo kimoja tu kama hicho kinaweza kukufanya uachwe na Mungu milele. Licha tu ya kuachwa na Mungu, pia yapo magonjwa hatari kama vile Ukimwi, jambo ambalo wengi hawafahamu, ni kuwa ukimwi ni PEPO, kwamfano inawezekana kabisa watu wawili wakakutana   wasiwe na maambukizi, lakini kwasababu kile kitendo kinahasisiwa na pepo la uzinzi, moja kwa moja linawavaa wote, na saa hiyo kila mmoja anapata UKIMWI, baadaye wakijiuliza  wametolea wapi, hawajui. Ndivyo ilivyokuwa kwa watu wa kwanza walioupata huo ugonjwa, hawakuambukizwa na mtu bali lilikuwa ni PEPO liliowavaa.

Hivyo kuwa makini sana, biblia inaposema ni Shimo refu na rima jembamba, inamaanisha kweli. Ukinasika usidhani ni rahisi kutoka. Hizo ni tahadhari kwetu. Lakini ukimpa Yesu maisha yako, atakupa uwezo wa kipekee wa kuweza kuvishinda vishawishi hivyo vyote. Uwezo huo hawezi kutoa mtu yeyote, zaidi ya Yesu Kristo tu peke yake. Watu wa ushauri nasaha, hawawezi kukufanya uushinde uzinzi, Madkatari hawawezi, Bali Yesu tu peke yake. Hivyo ukimwamini, utakusaidia.

Na kumwamini kunakuja kwa kutubu dhambi zako zote, kwa kumaanisha kabisa kuziacha, kisha kukubali kubatizwa katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa na kwa maji mengi, na yeye mwenyewe kuanzia huo wakati atakushushia kipawa chake cha Roho wake Mtakatifu kukusaidia kuweza kuyashinda majaribu yote, kama yeye alivyoweza kuyashinda.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

“Shinikizo” ni nini kibiblia, Na maana yake rohoni ni ipi?

Je! Daudi hakuwa mtoto wa ndoa wa Yese? (Zab 51:5)

Kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?

Kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?

Maana Ya Maneno Katika Biblia.

Rudi nyumbani

Print this post

Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa watoto wake wote.

SWALI: Kwanini Bwana Yesu alisema watu wa kizazi kile wamefanana na watoto walioketi masokoni na kuitana,? Mfano huo unaelewekaje?

Na pia alikuwa na maana gani kusema maneno haya?

Luka 7:35 “Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa watoto wake wote”


JIBU: Habari hizo utazisoma katika sehemu kuu mbili, ya kwanza ni Mathayo 11:16-20 na ya pili ni  Luka 7:31-35

Sasa tuisome hiyo ya Luka ndio yenye vifungu vya moja kwa moja vya swali lenyewe;

Luka  7:31 “Bwana akasema, Niwafananishe na nini watu wa kizazi hiki? Nao wamefanana na nini?

32 Wamefanana na watoto walioketi sokoni na kuitana, wakisema, Tuliwapigia filimbi wala hamkucheza; tuliomboleza, wala hamkulia.

33 Kwa kuwa Yohana Mbatizaji alikuja, hali mkate wala hanywi divai, nanyi mwasema, Ana pepo.

34 Mwana wa Adamu amekuja, anakula na kunywa; nanyi mwasema, Tazama, mlafi huyu, na mnywaji wa divai, rafiki wao watoza ushuru na wenye dhambi.

35 Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa watoto wake wote”.

Shalom.

Bwana Yesu alitoa mfano ambao ulikuwa ni wa kawaida na uliojulikana kwa wagalilaya wakati ule. Kwani ilikuwa ni desturi watoto wa aina mbalimbali  kukutana masokoni kwa ajili ya michezo kulingana na desturi zao, na walipokutana walikuwa wanaunda makundi mawili makubwa, lengo lao likiwa ni kuigiza mambo ambayo waliona watu wazima wakiyafanya aidha katika misiba au sherehe.

Sasa kundi la kwanza lilikuwa linaanza kwa kupiga filimbi za kwenye masherehe walizowahi kuzisikia mahali fulani zikipigwa huko nyuma, na lile kundi lingine kazi yake ilikuwa ni kuitikia kwa kucheza, kama watu wazima walivyofanya. ( Soma Luka 15:25)

Baadaye tena vivyo hivyo, wanarudia  kuigiza  nyimbo za misibani, wale wengine wanajifanya kama wanalia kwa kupiga piga vifua vyao. (Soma Mathayo 9:23).  Hivyo hata watu wazima walipowaona hawakuwazuia bali waliwaacha, kwani walikuwa wanaamini vitendo vile vinawajengea uzalendo wa kutambua tamaduni zao za kiyahudi.

Sasa kulingana na maneno ya Bwana Yesu ni kuwa, watoto hawa walipokusanyika, kundi lile la kwanza lilipopiga filimbi za masherehe, wale wengine hawakuonyesha mwitikio wowote walizira, pengine wakadhani wanataka za msiba, na walipowapigia wenzao za msiba, bado pia hawakujifanya kama wanaomboleza. Kitendo ambacho  pengine kiliwakasirisha wale waliojitoa.

Akifunua kuwa, Yohana alikuja kwa njia ya kujitenga sana na ulimwengu, hivyo pengine wangemwamini kwa maisha yake ya majangwani, na kutokula kula au kunywa, kama vile mtoto aliyewapigia filimbi za maombolezo, lakini hawakulia..Yaani mafarisayo na waandishi hawakuonyesha mwitikio wowote. Kinyume chake wakasema watu wenye mapepo, ndio wanaishi maisha ya namna hiyo, hakuna mtumishi mwenye akili timamu, akawa mchafu na mtu asiyejijali namna ile.

Labda hiyo ikaonekana kama ni njia ngumu kwao kuamini manabii wa Mungu, Hivyo Mungu akawapelekea mkuu wa uzima mwenyewe, Yesu Kristo, Bwana wetu, ambaye yeye alikuja kwa njia ya kula na kunywa, mtu wa watu, aketiye katikati ya wenye dhambi, hivyo mbele yao akafanana na wale watoto waliopiga filimbi, ili wenzao wacheze.. Lakini bado hawakuonyesha mwitikio wowote kwa injili ya Bwana, kinyume chake, wakamwita mlevi na mlafu. Hakuna mtumishi wa Mungu kweli anaweza kushinda bar muda wote na walevu kuwahubiria.

Kuonyesha kuwa hata sasa, Bado Mungu anaweza kutuma watumishi wake, katika wito tofauti tofauti, lakini bado watu wasiompenda Mungu wakapinga tu, wakadhihaki, wakakejeli, wakadharau. Akitumwa nabii wa Mungu anayehubiri injili ya kweli, ambaye pengine ni tajiri, na ana mali, watasema, tapeli huyu, anakula sadaka za waumini, wakipelekewa nabii ambaye muda wake wote anashinda sehemu za ibada, au milimani, mwenye nguo moja, asiye smati, hafanyi kazi yoyote isipokuwa kushinda uweponi mwa Mungu, watasema huyu mlokole maskini hatumtaki, kama Mungu wake ameshindwa kumfanya hata asivae viatu vilivyotoboka, atawezaji kunisaidia mimi?

Unaona?

Lakini sasa ukiendelea mistari inayofuata, Bwana Yesu ndio anasema..

Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa watoto wake wote”.. Ukisoma kwenye Mathayo 11:19 inasema “Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa kazi zake”. Hii ikiwa na maana Hekima ya Mungu ya kuokoa watu, imejulikana kuwa ni ya kweli kwa watoto wake ambao ni (Yohana na Yesu Kristo mwenyewe).. Kwamba kwa vyovyote vile, iwe ni katika utajiri au katika umaskini, au katika kujichanganya au kutojichanganya..kama ni ya Mungu, basi itathibitika tu kwa kazi zake,(matunda yake).

Hata leo hii, usimuhukumu mtumishi wa Mungu kisa ni tajiri, au ni maskini, au anakula au hali, vilevile usihukumu huduma yoyote kisa ni kubwa, au ni ndogo, au inamfumo huu au ule.. kwasababu Hekima ya Mungu haichagui mfumo wa kutembelea. Bali ihukumu hiyo huduma kwa kazi zake baada ya hapo.

Ikiwa matunda yake, ni yale ya Kristo, basi muheshimu mtumishi huyo au huduma hiyo, ikiwa watu wake, wanauelekea wokovu wa kweli na wanaishi maisha ya kumpendeza Mungu basi heshimu hata kama ipo kinyume na matazamio yako.

Vilevile ukiona mtumishi ni tajiri, au ni Yule maskini anayeishi milimani, na anachokifanya hakina matunda Kristo anayoyataka sawasawa na Neno lake. Yaani watu wake ndio wanakwenda mbali na wokovu na utakatifu, maisha yako ni ya kidunia, wanafuata tu kuponywa, basi lakini upendo na Kristo hawana.. achana naye, hata kama atajiona ni wa rohoni kiasi gani..au ni mtu wa kijamii namna gani, au mwenye ushawishi namna gani, achana naye. Hekima ya Mungu haipo hapo.

Kwasababu hekima ya kweli ya Mungu inathibitika kwa kazi zake. Kama ilivyothibitika kwa Bwana Yesu na kwa Yohana, japokuwa mapito yao yalikuwa ni tofauti lakini matunda yao yalikuwa ni thabiti.

Hiyo ndio sababu Bwana Yesu aliwaambia wale mafarisayo maneno hayo..

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Au bofya chini kujiunga na group la whatsapp moja kwa moja;

https://chat.whatsapp.com/GBX2lWIcoCq8zmlnXJgaWQ

https://chat.whatsapp.com/GBX2lWIcoCq8zmlnXJgaWQ

Mada Nyinginezo:

Hamjui ya kuwa mtawahukumu malaika? Ina maana gani?

MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA WARAKA WA PILI WA YOHANA.

USIRUDI NYUMA KWA KUITUMAINIA HAKI YAKO.

MZAZI, JALI MAISHA YA KIROHO YA MTOTO WAKO.

SINA PESA SASA, YESU ATANISAIDIA NINI?

Rudi nyumbani

Print this post

PONGEZI NA MAONYO YA BWANA KWA WATAKATIFU.

Kama wewe ni mtoto wa Mungu kweli kweli na sio mwana-haramu, ni vema ukafahamu tabia za Mungu kwako zinavyokuwa hususani katika eneo la pongezi na maonyo, ili usije ukaishi maisha ya wasiwasi au maisha ya kujivuna sana.

Unapaswa ufahamu kuwa Mungu akikuonya haimaanishi kuwa wakati wote unamchukiza, na vilevile Mungu akikusifia haimaanishi kuwa wakati wote unampendeza.

Kwamfano embu tafakari ile habari tunayoisoma katika Mathayo 16 ambayo Bwana Yesu aliwauliza mitume wake, kwa habari yake, kuwa wao wanasema yeye ni nani? Utaona Petro alipotoa jibu fasaha wakati ule ule Bwana alimsifia kweli kweli, kwa jinsi alivyoupokea ufunuo mkubwa namna ile,mpaka akaambiwa kuwa juu ya ufunuo ule Kristo atalijenga kanisa lake na milango ya kuzimu haitalishinda,.Na pia atampa funguo za ufalme wa mbinguni..na lo lote atakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote atakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni..(Mathayo 16:13-20)

Ukiambiwa maneno kama haya, unaweza kujiona wewe ni spesheli sana, hakuna mtume mwingine zaidi yako wewe, wewe ni bora, wewe ni mwamba, Mungu amependezwa na wewe kuliko wengine wote, na ndio maana amekufunulia maono makubwa kama hiyo. Si ni kweli?

Lakini wakati Petro anafikiria vile, dakika chache mbeleni, wakati Bwana Yesu anawaeleza juu ya kifo chake, jinsi kitakavyokuwa, Petro huyo huyo akajitokeza tena na kuanza kumkemea Bwana na kumwambia kuwa hayatampata mabaya hayo mabaya yote. Akidhania kuwa na ufunuo wa namna hiyo amefunuliwa tena na Mungu mbinguni. Lakini majibu ya Bwana Yesu, yalikuwa ni ya tofauti kabisa, tusome..

Mathayo 16:21 “Tangu wakati huo Yesu alianza kuwaonya wanafunzi wake ya kwamba imempasa kwenda Yerusalemu, na kupata mateso mengi kwa wazee na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na siku ya tatu kufufuka.

22 Petro akamchukua, akaanza kumkemea, akisema, Hasha, Bwana, hayo hayatakupata.

23 Akageuka, akamwambia Petro, Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu”.

Tafakari, muda mfupi nyuma ameambiwa ufunuo ule wa kumjua Yesu ni nani alipewa na Mungu mwenyewe..Na muda huu tena Yesu haumwona kama ni Petro anayezungumza, ni heri ingekuwa hivyo, lakini anamwona Shetani kabisa, akizungumza kwenye kinywa cha Petro akinena.

Unaweza kujiuliza, Je!, Bwana hakuona, ni kitu gani Petro atakisema  mbele kidogo? Alijua vizuri lakini hilo halibatilishi kusifiwa kwa lile zuri alilolifikiri.

Ikiwa leo hii Mungu atakuambia habari zako njema, akakusifia, au akakupongeza, au akakuthaminisha, usidhani kuwa kwa kila kitu unachokifanya kwake ni sawa,..hapana usijipumbaze kwa namna hiyo bali zaidi jitahidi kumpendeza na kusimama katika njia zake..Vilevile Mungu akikuonya leo, kwa njia zako, haimaanishi kuwa anachukizwa na wewe kwa kila kitu unachokifanya, hapana, usifikirie hivyo utavunjika moyo hata kwa vile vizuri unavyovifanya, bali rekebisha hapo unapoonyewa, kwasababu, ndicho kikwazo anachokiona ndani yako kwa muda huo. Kwasababu vipo pia vizuri unavyomfanyia na anapendezwa na wewe.

Na wakati mwingine vyote viwili vinaweza kwenda sambamba, maonyo na pongezi.  Hivyo bado usichanganyikiwe, na kudhani kuwa moja ni la Mungu na lingine ni la shetani, hapana, bali vyote vinaweza vikawa ni vya Mungu. Vichukue vitendee kazi, kwasababu anayo mawazo mazuri na wewe.Ndicho alichokuwa anakifanya hata kwa yale makanisa 7 tunayoyasoma katika Ufunuo sura ya 2 & 3

Nikutakie maisha ya heri na ya Baraka tele katika safari yako ya kuelekea mbinguni.

SHALOM.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

HAKUNA MTU ANIONDOLEAYE, BALI MIMI NAUTOA MWENYEWE

NI VIZURI SISI KUWAPO HAPA.

Ni kweli Paulo alipuuzia maonyo aliyopewa ya kwenda Yerusalemu?

KUWA MAKINI NA MITANDAO, NI SHIMO REFU.

MILANGO YA KUZIMU.

KUSAMBAA KWA ROHO YA MPINGA-KRISTO.

Rudi nyumbani

Print this post

Ni kweli Paulo alipuuzia maonyo aliyopewa ya kwenda Yerusalemu?

SWALI: Je Ni kweli Mtume Paulo alipuuzia, maonyo aliyoonyeshwa na Roho Mtakatifu kwa kinywa cha Agabo juu ya kwenda  Yerusalemu?


JIBU: Tusome habari yenyewe kwa faida ya watu wote;

Matendo 21:10 “Basi tulipokuwa tukikaa huko siku nyingi, nabii mmoja jina lake Agabo akashuka kutoka Uyahudi.

11 Alipotufikia akautwaa mshipi wa Paulo, akajifunga miguu na mikono, akasema, Roho Mtakatifu asema hivi, Hivyo ndivyo Wayahudi wa Yerusalemu watakavyomfunga mtu mwenye mshipi huu, nao watamtia katika mikono ya watu wa Mataifa.

12 Basi tuliposikia haya, sisi na watu wa mahali pale, tukamsihi asipande kwenda Yerusalemu.

13 Ndipo Paulo alipojibu, Mnafanya nini, kulia na kunivunja moyo? Kwa maana mimi, licha ya kufungwa, ni tayari hata kuuawa katika Yerusalemu kwa ajili ya jina lake Bwana Yesu.

14 Alipokataa shauri letu, tukanyamaza tukisema, Mapenzi ya Bwana na yatendeke.

15 Baada ya siku zile tukachukua vyombo vyetu tukapanda kwenda Yerusalemu.

Tofauti na wengi tunavyodhani kwamba mtume Paulo alipuuzia maono ya Mungu, na ndio maana akaenda kukumbana na matatizo makubwa kule Yerusalemu alipokwenda mambo ambayo hayakuwa na ulazima wa yeye kukutana nayo. Lakini si kweli, kama Paulo angekuwa ni mtu wa kupuuzia maono ya Mungu, asingeandika katika waraka wake mmoja “Msitweze unabii” (1Wathesalonike 5:20). Akimaanisha msipuuzie unabii.

Paulo alikuwa ni mtu aliyethamini sana maagizo ya Roho Mtakatifu, na kuyatekeleza wa wakati. Kuna wakati Mungu alimkataza asihubiri Neno Galatia na sehemu nyingine na akatii(mdo 16:6-9). Na wakati huo huo Mungu anamwonyesha maono avuke bahari aende Makedonia kuhubiri mahali ambapo hajawahi kufika hata siku moja. Na akatii

Hivyo kitendo cha kusema Paulo hakutii maagizo ya Roho Mtakatifu, ni kukosa shabaha.

Lakini swali linakuja kama sio kutii basi  ni kwanini aamue vile?

Jibu ni kuwa, ipo tofauti ya “mtu kupewa agizo” na “mtu kuelezwa uhalisia wa mambo / kupashwa habari”. Paulo hakupewa agizo na Roho Mtakatifu kuwa asipande Yerusalemu, kama alivyopewa maagizo sehemu nyingine. Hapana, bali alielezwa uhalisia wa mambo atakayokutana nayo huko mbeleni. Na ndio maana utaona kabla hata ya Agabo kumpa unabii ule, tayari Roho Mtakatifu alikuwa ameshamshuhudia mambo hayo kuwa atakutana nayo mbeleni. Soma.

Matendo 20:22 “Basi sasa, angalieni, nashika njia kwenda Yerusalemu hali nimefungwa rohoni, nisiyajue mambo yatakayonikuta huko;

23 isipokuwa Roho Mtakatifu mji kwa mji hunishuhudia akisema, ya kwamba vifungo na dhiki vyaningoja”.

Hivyo Paulo kwa kulitambua hilo, bado hakusita kukumbana na changamoto hizo, kwa ajili ya injili. Alifikiria sana akaona dhiki haziwezi kumfanya kondoo wa Mungu wasifikiwe na injili. Hivyo akajitia moyo na kwenda kama shujaa.

Jambo kama hilo utaona pia kwa mtume Petro, kipindi kile Bwana Yesu alimwambia wewe ni kijana, lakini ukiwa mzee watu watakuja kukufunga mikono yako na kukuchukua usipotaka, (Yohana 21:18). Kuonyesha kuwa vifungo na dhiki na vifo vinamsubiria mbeleni. Lakini lile halikuwa ni agizo kwamba Petro sasa akatafute namna ya kukwepa, dhiki hizo. Hapana.

Hata sasa ni kawaida ya Roho Mtakatifu kuzungumza nasi kwa namna zote mbili. Kuna wakati atatupa maagizo, na kuna wakati atatueleza uhalisia wa mambo. Sasa pale tunapopewa maagizo au tunapoonywa, ni sharti tutii, Mungu anapokuambia usihubiri mahali Fulani, ni kweli usiende kuhubiri, anapokuambia kahubiri mahali Fulani ni kweli nenda kahubiri.

Lakini kuna wakati utakuwa katika safari yako ya kumtumikia Mungu, na akakuonyesha, matunda, na changamoto zake, akakuonyesha hata, unapigwa mawe, au unafukuzwa, au unafungwa, au unazungumziwa vibaya. Moja kwa moja usikimbilie kusema Roho Mtakatifu ananionya nisiende kuhubiri, hapana, bali tazama pia upande wa pili wa matunda, Kwasababu dhiki kama hizo haziletwi na Mungu, bali ni shetani, ambaye anafanya hivyo ili akuzuie, usifanye kazi yake hilo tu. Lakini kumbe Mungu anatamani sana, ufike kule.

Kwahiyo usitafsiri kila ono, ni agizo ,  mengine Mungu anatuonyesha tu ili yatakapotokea tusifadhaike sana, kwasababu alishatutaarifu mapema.

Yohana 16:1 “Maneno hayo nimewaambia, msije mkachukizwa.

2 Watawatenga na masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada.

3 Na hayo watawatenda kwa sababu hawakumjua Baba wala mimi.

4 LAKINI NIMEWAAMBIA HAYO, ILI MAKUSUDI SAA ILE ITAKAPOKUJA MYAKUMBUKE YA KUWA MIMI NALIWAAMBIA. Sikuwaambia hayo tangu mwanzo, kwa sababu nalikuwapo pamoja nanyi”.

Hivyo Bwana atusaidie na sisi tujifunze kuyapambanua maono ya Mungu.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

VIFO VYA MITUME WA YESU/ JINSI MITUME WALIVYOKUFA.

Tofauti kati ya ufunuo, unabii na maono ni ipi?

PINDO LA VAZI LAKE SASA LIMEREFUSHWA.

BADO UPO YERUSALEMU TU..GALILAYA HUTAKI KWENDA?

LIPI TUNAJIFUNZA KWA WALIOMWONA YESU ALIYEFUFUKA?

Rudi nyumbani

Print this post

Ni kama machungwa katika vyano vya fedha.

SWALI: Nini maana ya huu mstari?

Mithali 25: 11 “Neno linenwalo wakati wa kufaa, Ni kama machungwa katika vyano vya fedha”.


JIBU: Vyano ni wingi wa neno “Chano”, lenye maana ya sinia. Hivyo hapo anaposema Neno linenwalo wakati wa kufaa, ni kama machungwa katika vyano vya fedha, anamaanisha kuwa ni kama machungwa katika masinia ya fedha.

Sasa kwanini afananishe Neno linalofaa na machungwa katika masinia ya fedha?. Si rahisi kuelewa kwa sisi watu ambao utamaduni wetu ni tofauti na ule wa watu wa mashariki. Kwasababu machungwa yanayozungumziwa hapo si kama ya jamii yetu hii tuliyonayo. Kule kuna aina ya machungwa, ambayo wanasema ni matamu kuliko jamii zote za machungwa duniani, juisi yake ina harufu nzuri sana, machungwa hayo huwezi kuyasafirisha nje ya nchi, kwasababu hayakai muda mrefu yanaharibika ni ya kule kule tu. Na kwa kawaida wanapoyachuma huwa wanayaweka kwenye vyombo vya masinia, na sio kwenye majaba au magunia.

Sasa machungwa haya yalikuwa ni mahususi, kwa ajili ya kupewa watu waliochoka, pale wanapokula, au wanapoinywa juisi yake, basi wanaburudika na kupunguza uchovu wao kwa sehemu kubwa sana. Ni sawa na leo hii labda mtu unapopewa soda ya baridi (Labda tuseme fanta orange) wakati jua kali na kiu. Itakuburudisha si ndio.. Na ndivyo ilivyokuwa kipindi hicho kwa watu wanaishi mashariki ya kati na baadhi ya sehemu za Asia.

Kufunua kuwa ni jinsi gani Neno zuri la kufajiri lilivyo na maana sana kwa mtu aliyekatika hali ya uchungu, au msiba, au Neno la kutia moyo lilivyo na thamani sana kwa aliyevunjika moyo, au Neno la kuhamasisha lilivyo na nguvu sana kwa walioishiwa nguvu, ni kama machungwa yaliyo kwenye masinia ya fedha, tayari kwa ajili ya waliochoka.

Na habari nzuri za kufajiri, za kujenga, za kuponya, za kuimarisha, hazitoki kwa mwingine zaidi ya Yesu Kristo pekee. Hivyo tunapowahubiria watu habari hizi njema za wokovu wa Yesu Kristo, zinaponya zaidi kuliko habari nyingine zozote tuzifahamuzo. Kwasababu yeye mwenyewe alisema alikuja kwa kazi hiyo..

Isaya 61:1 “Roho ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu Bwana amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao.

2 Kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa, na siku ya kisasi cha Mungu wetu; kuwafariji wote waliao;

3 kuwaagizia hao waliao katika Sayuni, wapewe taji ya maua badala ya majivu, mafuta ya furaha badala ya maombolezo, vazi la sifa badala ya roho nzito; wapate kuitwa miti ya haki, iliyopandwa na Bwana, ili atukuzwe”.

Umeona, hivyo tuwahubiri watu habari za Kristo, hizo zinatosha kutibu makundi yote ya watu. Ukimsaidia mtu kumpata Kristo, umemsaidia kutatua matatizo yake yote. Kwasababu ndani yake sio tu atapata wokovu bali, na furaha ya kweli na amani ya kweli.  Na kwa kufanya hivyo rohoni na sisi Mungu anatuona  kama wahudumu wake wa machungwa katika vyombo vya fedha.

Bwana atupe na sisi macho ya kuyatendea hayo kazi.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

ONDOA TAKATAKA KATIKA FEDHA, NA CHOMBO KITATOKEA KWA MTAKASAJI.

Naye aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjika-vunjika..

APENDAYE FEDHA HASHIBI FEDHA.

Naomba kufahamu maana ya “sura ya kijiti” katika Marko 12:26.

Rudi nyumbani

Print this post