Nini maana ya kukunguwazwa (Marko 14:27)

Nini maana ya kukunguwazwa (Marko 14:27)

Jibu: Tusome,

Marko 14:27  “Yesu akawaambia, Mtakunguwazwa ninyi nyote kwa ajili yangu usiku huu; kwa kuwa imeandikwa, Nitampiga mchungaji, na kondoo watatawanyika”.

Kukunguwazwa maana yake ni “kuchukizwa”.. Mtu anapokufanya ukasirike au uchukie maana yake amekukunguwaza, biblia imetoa tafsiri ya neno hilo vizuri katika Mathayo 26:30.

Mathayo 26:30  “Nao walipokwisha kuimba, wakatoka nje kwenda mlima wa Mizeituni.

31  Ndipo Yesu akawaambia, Ninyi nyote MTACHUKIZWA kwa ajili yangu usiku huu kwa kuwa imeandikwa, Nitampiga mchungaji, na kondoo wa kundi watatawanyika”.

Unabii huo alioutoa Bwana ulitimia masaa machache tu mbeleni, pale ambapo kikosi cha Askari wa kirumi kilitokea na kumkamata Bwana Yesu.

Na tunasoma Mitume hawakukifurahia kile kitendo, “WALICHUKIZWA SANA”, hata Petro kufikia hatua ya kutoa upanga na kumkata sikio mtumwa wa kuhani mkuu. Hicho ni kiwango kikubwa sana cha hasira.

Yohana 18:7  “Basi akawauliza tena, Mnamtafuta nani? Wakasema, Yesu Mnazareti.

8  Yesu akajibu, Nimekwisha kuwaambieni ya kwamba ni mimi; basi ikiwa mnanitafuta mimi, waacheni hawa waende zao.

9  Ili litimizwe lile neno alilolisema, Wale ulionipa sikumpoteza hata mmoja wao.

10  Basi Simoni Petro alikuwa na upanga, akaufuta, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio la kuume. Na yule mtumwa jina lake ni Malko”.

Vile vile na sisi tuliompokea Yesu ni lazima tutapitia tu vipindi vya kuchukizwa kwaajili ya Yesu.

Unapofika mahali na kukuta watu wanalikufuru jina la Yesu ni lazima utachukizwa tu!, unapofika mahali na kukuta watu kwa makusudi kabisa wanahubiri injili nyingine tofauti na ile ya kimaandiko ni lazima utachukizwa tu!.

Unapofika mahali na kukuta unatolewa unabii wa uongo, au kweli ya Mungu inapotoshwa kwa makusudi, ni lazima utachukizwa tu!, Unapofikia hatua ya kusumbuliwa kiimani na watu wengine kwasababu tu umeokoka, au umeamua kwenda katika njia sahihi ni lazima tu utakunguwazwa! hata wakati mwingine kufikia kiwango kama kile cha Petro cha kutamani kumdhuru mtu kabisa.

Lakini sisi hatujapewa ruhusa wala amri ya kumdhuru wengine, hata kama ni waovu au wanatutendea maovu, au hata kama wanamtukana Mungu mbele yetu, kazi tuliyopewa ni kuziokoa roho, na si kuziangamiza, kwasababu kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama bali juu ya majeshi ya mapepo wabaya katika ulimwengu wa roho.

Lakini siku zote fahamu kuwa, ni lazima tu tutapitia vipindi vya kuchukizwa kwaajili ya Yesu, hilo haliepukiki kwa kila aliyezaliwa mara ya pili.

Yohana 15:20 “Likumbukeni lile neno nililowaambia, Mtumwa si mkubwa kuliko bwana wake. Ikiwa WALINIUDHI MIMI, WATAWAUDHI NINYI; ikiwa walilishika neno langu watalishika na lenu”.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa >> WHATSAPP-GROUP

Mada Nyinginezo:

Nini tofauti ya Mtumwa, Mjakazi na kijakazi?

JINSI MUNGU ATAKAVYOTOA THAWABU ZAKE, NA VIGEZO ATAKAVYOTUMIA. (Sehemu ya 5)

JINSI YA KUEPUKA KUUMIZWA MOYO KUSIKOKUWA NA SABABU.

Je ni lazima kushiriki Meza ya Bwana?

YEYE ATAWABATIZA KWA ROHO MTAKATIFU NA KWA MOTO.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments