MWAGA DAMU YAKO KWA AJILI YA BWANA.

MWAGA DAMU YAKO KWA AJILI YA BWANA.

Nakusalimu katika jina kuu la Bwana wetu Yesu Kristo. Karibu tena tujifunze maneno ya uzima.

Kulikuwa na aina nne za wito ambao Bwana aliwaitwa mitume wake.

  1. Wito wa kawaida: Ambapo Bwana alipowaona mitume aliwaambia nifuate. Lakini hakukuwa na vigezo vyovyote, nyuma yake, au majumu Fulani ya lazima ya kuyafanya.(Yohana 1:35-51)
  2. Wito wa uanafunzi: Baadaye akaja kuwafanya kuwa wanafunzi wake, hapo ndipo aliwakuta na kuwaambia waache vyote kisha wamfuate, na akatoa na vigezo vyake, kwa wale wote waliotaka kuwa wanafunzi wake (Luka 14:25-35), Hivyo Bwana alikuwa nao wengi zaidi ya wale 12
  3. Wito wa kitume: Baadaye akawachagua mitume kati ya wanafunzi wake wengi. Yaani watu ambao atawatuma kwa kazi maalumu. Ndio hapo wakapatikana 12
  4. Wito wa mashahidi: Lakini mwisho akawachagua mashahidi wake, Huu ndio wito wa juu sana na wa mwisho, ambao Bwana aliwakusudia mitume wake, akawapa siku ile aliyokuwa anapaa.

Matendo 1:8  Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi

Sasa nini maana ya kuwa SHAHIDI? Kuwa shahidi maana yake ni kuwa tayari kupitia mateso au kumwaga damu yako kwa ajili ya kumtetea Yule anayekutuma. Hivyo mtu yoyote aliyemwaga damu yake, kwa ajili ya Yesu huyo ni SHAHIDI. Hivyo mitume walijua kabisa hatma yetu ni kumwaga damu tu, huko mbeleni. Na watu kama hawa wanakuwa na nafasi ya juu sana, mbele ya Kristo siku ile watakapofika mbinguni, kwasababu wanakuwa wamepitia sehemu ya mapito yaleyale aliyoyapitia Bwana wao hapa duniani.

Leo tutatazama aina nne(4), za mashahidi wa Kristo. Na wewe pia utajipima upo wapi kati ya hawa na kama haupo popote basi, ufanye bidii uwe katika wingu hili la Mashahidi wa Yesu.

Aina nne (4), za Mashahidi wa Yesu.

1) Wanaoteswa na kupigwa na kuuliwa kwa ajili ya Bwana au injili:

2Wakorintho 11:23  “Wao ni wahudumu wa Kristo? (Nanena kiwazimu), mimi ni zaidi; katika taabu kuzidi sana; katika vifungo kuzidi sana; katika mapigo kupita kiasi; katika mauti mara nyingi. 24  Kwa Wayahudi mara tano nalipata mapigo arobaini kasoro moja. 25  Mara tatu nalipigwa kwa bakora; mara moja nalipigwa kwa mawe; mara tatu nalivunjikiwa jahazi; kuchwa kucha nimepata kukaa kilindini”.

Hata sasa, wapo watu wanateswa kwa namna mbalimbali, wengine wanamwaga damu kwa mapigo, watu kama hawa ni mashahidi wa Bwana. Sawa tu wale mitume wake.

2) Wanaooponza/ wanaohatarisha maisha yao kwa ajili ya Bwana au injili.

Hili ni kundi la pili ambalo linamwaga damu pia. Ijapokuwa haitaonekana kwa nje lakini rohoni Mungu anawaona kama wamemwaga damu kwa ajili ya ushuhuda wake. Kwamfano tukiangazia kile kisa cha Daudi ambapo wakati Fulani alitamani kunywa maji ya kisima kilichokuwa katikati ya maadui zake wafilisti. Lakini tunaona mashujaa wake watatu waliposikia, waliondoka kisirisiri, wakahatarisha maisha yao, kwenda katika marago ya wafilisti, na kuyachukua yale maji na kumletea Daudi, lakini Daudi hakuyanywa alisema ile ni damu yao na sio maji tena.

2Samweli 23:14 Naye Daudi wakati ule alikuwako ngomeni, na jeshi la Wafilisti wakati ule walikuwako Bethlehemu.  15 Daudi akatamani, akasema, Laiti mtu angeninywesha maji ya kisima cha Bethlehemu, kilicho karibu na lango!  16 Basi hao mashujaa watatu wakapenya jeshi la Wafilisti, wakateka maji kutoka kile kisima cha Bethlehemu, kilicho karibu na lango, wakayachukua, wakamletea Daudi; walakini yeye hakukubali kuyanywa, akayamimina mbele za Bwana.  17 Akasema, Hasha, Bwana, nisifanye hivi; je! Si damu hii ya watu hao waliohatirisha nafsi zao? Kwa hiyo hakukubali kuyanywa. Hayo ndiyo waliyoyafanya wale mashujaa watatu.

Umeona? Maji yamekuwa damu kwasababu ya hatari waliyoingia watu wale. Vivyo hivyo na wewe ujitoapo sadaka kwa ajili ya Bwana, unapohatarisha hata kazi yako, muda wako, ujana wako, ili tu umfanyie Mungu jambo. Ndugu hilo linakuwa sio jambo la kawaida bali ni damu yako unayoimwaga kwake.

Kulikuwa na Yule mwanamke alikwenda kumtolea Bwana sadaka ya senti mbili, lakini maandiko yanasema ndio iliyokuwa riziki yake yote, hajui kama kesho ataiona, pengine hata jana yake hakula. Si ajabu kwanini Bwana aliona ametoa zaidi ya wengine wote. Kwasababu kilichokuwa anakitoa ni uhai wake, na sio sadaka ya kawaida.

Jiulize nguvu zako unazozisumbukia daima unazimalizia kwa nani, je! Ni kwenye kujenga tu, ni  kuwekeza, ni kuvaa ni kula? Au ni nini? Vipi kwa Mungu wako, unampa sehemu ndogo tu, ni kweli utapata thawabu? Lakini je! Ulishawahi kufikiria kutenda jambo linalokugharimu wewe kwa Bwana wako? Damu yako unaimwaga wapi?. Watakatifu wa kanisa la kwanza, waliweza kuuza mali zao za thamani na kumtolea Bwana, na sisi tunafanya nini kwa Bwana?.

3) Wanaoondoa viungo vyao vinavyowakosesha kwa ajili ya Kristo.

Hili nalo ni kundi lingine la wanaomwaga damu. Ukisoma Marko 9:43-49, kuna maneno Bwana Yesu alisema, kuhusiana na viungo vyetu. Akasema ikiwa kimojawapo kinakukosesha kikate, ili usikose uzima wa milele. Unajua sikuzote kiungo kikatwapo, ni lazima damu imwagike. Ukiuondoa mguu wako, yapo maumivu, lakini pia ipo damu itakayokutoka.

Viungo vinaweza vikawa ni wazazi, marafiki, ndugu, kazi, mazingira n.k. Ikiwa mzazi anakukosha usisimame vema na Mungu, anakukataza usimwabudu Bwana,au usihubiri huna budi kutomtii kwasababu hiyo, ni kweli utakutana na maumivu, damu itatoka, lakini umemtii Kristo.

Ndicho alichokifanya mfalme mmoja aliyeitwa ASA, yeye alimcha Mungu, na alipoona mama yake anamletea habari za ibada za masanamu, akamwondoa kwenye kiti cha umalkia, japokuwa ni fedheha kubwa alionyesha lakini aliona ni heri kumtii Kristo zaidi ya mwanadamu (1Wafalme 15:11-13)

Hata leo, watu ambao, wameachwa, na viongo vyao vya karibu, au wameviondoa, kwasababu ya Kristo, visiwaghasi, labda ni kazi, ndugu, rohoni wanaonekana kama wamemwaga damu zao kwa ajili ya ushuhuda wa Kristo, na hivyo ni mashahidi wa Bwana. Ndugu usiopoge maumivu, mpende Bwana zaidi ya chochote.

4) Wanaoomboleza kwa ajili ya kanisa, na injili.

Yesu alipokuwa anaomba, kwa maomboleza na dhiki nyingi kwa ajili yetu muda mfupi kabla ya kusulibiwa, maandiko yanasema jasho lake, likageuka kuwa matone ya damu.

Luka 22:41  “Mwenyewe akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti akaomba, 42  akisema, Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke. 43  Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu. 44  Naye kwa vile alivyokuwa katika dhiki, akazidi sana kuomba; hari yake ikawa kama matone ya damu yakidondoka nchini.]

Hivyo na wote, waombolezao kwa ajili ya haki, machozi yao si bure, wanaokesha kuliombea kanisa, na kazi ya Mungu, wanaowaombea wengine kwa machozi na huzuni, wanadumu madhabahuni kwa Bwana muda mwingi mfano wa Ana (Luka 2:36). Rohoni wanamwaga damu, japo wanaweza wasilijue hilo. Na hivyo ni mashahidi wa Kristo duniani. Thawabu yao mbinguni ni sawasawa na wale waliokatwa vichwa kwa ajili ya Bwana.

Swali ni je! Mimi na wewe tunasimama wapi? Paulo anasema ninakufa kila siku, je! Na sisi tunafanya hivyo kwa Bwana wetu? Bwana atusaidie tuwe maaskari wake kwelikweli, ili siku ile ajivunie sisi mbele za Mungu na malaika zake.

Fanyika shahidi mwaminifu wa Bwana.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mada Nyinginezo:

WINGU KUBWA LA MASHAHIDI.

KIFO CHA MTAKATIFU PERPETUA NA FELISTA.

VIFO VYA MITUME WA YESU/ JINSI MITUME WALIVYOKUFA.

KAZI ZA ROHO MTAKATIFU

MAMBO YA KUJIFUNZA KWA KLOPA NA MKE WAKE!

Maana Ya Maneno Katika Biblia.

NAO WAKAMSHINDA KWA DAMU YA MWANA-KONDOO.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments